Makwazo ni nini kibiblia? Na madhara yake ni yapi?

Makwazo ni nini kibiblia? Na madhara yake ni yapi?

Makwazo ni  mambo yanayozuia mwendelezo wa jambo Fulani lililokuwa limekwisha anza, au linalotaka kuanza. Kwamfano ulikuwa unasafiri lakini ghafla kwenye safari yako unakutana na mto mpana, unaokufanya ushindwe kuvuka, hicho kinaitwa kikwazo. Au ulikuwa unapika chakula chako, halafu ghafla gesi ikaishia katikati na chakula bado hakijaiva, hicho kinatiwa kikwazo.

Na rohoni pia vivyo hivyo yapo makwazo ambayo yanamzuia mtu asimalize mwendo wake wa imani, au asiendelee mbele tena katika kumtafuta Mungu. Na muhimu sana kuyajua na kujiepusha nayo.

Kibiblia makwazo yamegawanyika katika sehemu kuu tatu.

  1. Makwazo yanayowakumba watu wa Mungu kutoka kwa wapendwa wenzao
  2. Makwazo yanayowakumba watu wa Mungu kutoka kwa wapagani
  3. Makwazo yanayowakumba wapagani kutoka kwa watu wa Mungu.

1) Makwazo yanayowakumba watu wa Mungu kutoka kwa wapendwa wenzao

Tukianzana  na hilo kundi la kwanza, wapendwa tunaowazungumzia hapa ni wale ambao hawajasimama vema katika kweli. Ndio hawa ambayo Bwana Yesu anawazungumzia katika vifungu hivi;

Luka 17:1  Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake! 2  Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa. 3  Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. 4  Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe.

Kwa namna gani hawa wanaweza kumkosesha ndugu. Kwamfano ni pale, Mpendwa mwezako anaposikia umemsengenya, Sasa Kama ni mdhaifu kiimani Hili linaweza kuwa ni kwazo kubwa sana kwake ambalo likamfanya hata nguvu yake ya kuendelea kudumu katika kusanyiko ikapoa. Zipo shuhuda nyingi sana za wapendwa ambao wamerudi nyuma kiwokovu kwasababu ya maisha haya. Hivyo kama mwanaminio hakikisha, kinywa chako, unakichunga. Jifunze kuwa na kiasi na uvumilivu. Jifunze kujiepusha na mambo mabaya Kwa wapendwa wenzio.

Kwazo hili linaweza pia kuwa katika ufahamu wa kiroho .

Utakumbuka Ayubu, alipopitia majaribu yake mazito, hakuna mahali popote alinena maneno yasiyo faa, lakini wale marafiki zake watatu, yaani Sofari, Elifazi na Bildadi, (ambao wanawawakilisha watumishi wa Mungu), walipofika, walitumia ujuzi wao wa kibinadamu kumuhukumu Ayubu, kwamba ni kwasababu alitenda dhambi,  hiyo ikampelekea Ayubu kunena hata maneno yasiyofaa.

Kama mtumishi wa Mungu, epuka hukumu ya macho,ukiletewa tatizo la mtu/ watu, usiangalie kwa jicho la nje, mwingine ni Mungu mwenyewe anampitisha katika madarasa yake, ukajikuta badala ya kutatua tatizo ndio unaongeza tatizo juu yake. Usianze kuhukumu matukio, bali kuwa katika Roho, tegemea zaidi uongozo wa Roho Mtakatifu. Hekima itakusaidia.

Pia lipo katika ujuzi.

Ukisoma Warumi 14, maandiko yanaeleza kwa upana jinsi ujuzi wetu unaweza kuwa kwazo kwa wengine wadhaifu was imani, kwamfano wewe ukipewa chakula ambacho umesikia kimepitishwa kwenye matambiko, ukashukuru, ukakila, ukijua kabisa chakula hakiwezi kukuondoa kwenye mpango wa Mungu. Lakini kwa ujuzi huo mwingine mwenye imani haba akakuona, na yeye akaanza kula vyakula vya kimatambiko na mila, akajikuta anashirikiana na uganga na mizimu, utakuwa umemsababishia kwazo kubwa kwa Mungu.

Lolote tunalolifanya, lazima tuangalie wengine wanaiga nini kwetu sisi wenye ujuzi. Uvaaji wako, wewe kama mkristo, unaweza ukajiona hauna shida kwako, lakini wengine wakaona ni sawa, hata kuvaa mavazi hayo ambayo hayana utukufu mbele za Mungu, utakuwa umefanyika kwazo kwao

2) Makwazo yanayowakumba watu wa Mungu kutoka kwa wapagani

Wapagani wanaweza kuzuia injili, isihubiriwe mahali, wakawapiga au wakawafunga watu wa Mungu n.k. Utaona Herode alimpinga Yohana akamweka gerezani hakuweza tena kuhubiri injili, wapagani waliwapinga watakatifu wengi. Hata mitume katika ziara zao walikutana na vikwazo vingi kutoka kwa watu wa mataifa, mahali pengine hawakuweza kuhubiri kwa utulivu (1Wakorintho 15:32, 1Wathesalonike 2:2).

3) Makwazo yanayowakumba wapagani kutoka kwa watu wa Mungu.

Watu ambao hawajakamilika katika imani. Kwamfano ni mpendwa lakini mzinzi, sasa wale watu wa nje, ambao walikuwa wanakaribia kuvutwa katika imani, wanapoona matendo ya watu kama hawa, wanasema kama ukristo wenyewe ndio huu ni heri niendelee kuwa mpagani. Hayo ni makwazo. Au unakuta mwingine ni tapeli, mwingine ni mtukanaji, mambo kama haya hufanyika kwazo kubwa sana kwa wapagani kuihubiri injili.

2Wakorintho 6:3  Tusiwe kwazo la namna yo yote katika jambo lo lote, ili utumishi wetu usilaumiwe; 4  bali katika kila neno tujipatie sifa njema, kama watumishi wa Mungu; katika saburi nyingi, katika dhiki, katika misiba, katika shida;

Hitimisho:

 Hivyo wewe kama ni mkristo jitahidi sana kuyaepuka makwazo kwa waaminio wenzako au kwa wapagani. Lakini pia kama ulikwazwa na ndugu yako, basi,  suluhisho sio kuvunjika moyo au kuuacha wokovu, bali ni kunyanyuka tena na kuendelea mbele. Biblia inasema;

Mithali 24:16 Kwa maana mwenye haki huanguka mara saba akaondoka tena; Bali wasio haki hukwazwa na mabaya.

Amka tena, mtumikie Bwana, kwasababu alishatujuza tangu mwanzo kwamba hayana budi kuja, hivyo hilo liwe ni jambo la kawaida kwako, jitie nguvu uendelee mbele.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mafundisho mengine:

Mpagani ni nani?

USIMLAANI KIZIWI, WALA USITIE KWAZO MBELE YA KIPOFU.

Kutoka 21:10 ina maana gani?

Biblia inasema tusiwe kwazo kwa yeyote, je! inawezekanikaje kwa dunia hii ya sasa?(2Wakorintho 6:3).

MIMI SIOMBI KWAMBA UWATOE KATIKA ULIMWENGU.

HISIA YA MUNGU ILIYO MBAYA KULIKO ZOTE.

KIKWAZO CHA EUODIA NA SINTIKE.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments