JILINDE NA UNAJISI, UNA MADHARA MAKUBWA.

JILINDE NA UNAJISI, UNA MADHARA MAKUBWA.

Najisi ni kitu gani?


“Najisi” ni kitu chochote kinachokwamisha na kuundoa usafi wako wote, heshima yako yote au hadhi yako yote uliyokuwa nayo ..Kwamfano unaweza ukawa na nguo yako nyeupe, lakini kawino kadogo tu cheusi kakapita kwenye mfuko wa shati hilo, kakakufanya usilavae tena shati hilo kwa doa lile ..Sasa kale kadoa cha wino ndio najisi hivyo kameitia unajisi nguo nzima isifae tena..

Vivyo hivyo kwa watakatifu, yapo mambo mengi unaweza kweli ukayadhibiti na ukawa safi lakini mambo madogo madogo yakakuharibia ukaonekana sio safi tena mbele za Mungu haijalishi umejitahidi kuyazuia hayo mengine kiasi gani..

Ukisoma katika agano la Kale Mungu aliwaorodheshea wana wa Israeli mambo ambayo yatawafanya kuwa najisi..Na mojawapo ni kuigusa maiti, ya mtu aliyekufa au mnyama..Hata kama wewe ni kuhani ilikuwa ukigusa tu maiti basi hutaruhusiwa kufanya chochote hadi siku ya tatu ambapo utajiosha na kujitakasa kwa maji safi..Ukishamaliza kujisafisha hiyo peke yake haitoshi kuundoa unajisi kabisa, itakupasa usubiri hadi siku ya saba bila kwenda popote ndipo utakaporuhusiwa kuingia katika kusanyiko la Mungu.(Soma Hesabu 19:12).

 Kadhalika na baadhi ya wanyama kama vile nguruwe, na wengine wasioweza kucheua walikuwa ni najisi, ukiwala tu tayari umeshajitia unajisi.

Halikadhalika ilikuwa ukitokwa na uchafu sehemu zako za siri iwe ni mwanaume au mwanamke tayari umeshajitia unajisi, hivyo kama wewe ni mwanaume ulikuwa unaoga kwa maji safi, kisha unausubiri mpaka jioni hufanyi chochote ndipo ikishafika jioni utaruhusiwa kuingia kwenye kusanyiko la Mungu (Walawi 15:16), Lakini kama wewe ni mwanamke labda upo katika siku zako basi utasubiri siku 7, ndipo uruhusiwe kuingia katika kusanyiko(Walawi 12:4).

Vilevile kwa mwanamke aliyezaa, tayari ametiwa unajisi kwa tendo lile, hivyo kama amezaa mtoto mwanaume basi atasubiri siku 33 pamoja na siku 14 za uchafu wa siku zake, lakini kama amezaa mtoto wa kike atasubiria siku 66 pamoja na siku nyingine 14 pia..

Hivyo siku zote hizo za unajisi mtu haruhusiwi kuingia katika kusanyiko lolote la Mungu wala kutoa kafara yoyote kwa Mungu, japokuwa tayari ulishajisafisha na unaonekana upo safi lakini inakugharimu usibirie, kinyume chake ukifanya hivyo adhabu yake ilikuwa ni kifo..

Sasa tukirudi katika agano jipya..Unajisi wetu sio wa mwilini tena bali wa rohoni, yote hayo yalikuwa yanafunua unajisi wa Rohoni ambao ndio mkuu, Bwana Yesu alisema..

Mathayo 15:18 ‘Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi.

19 Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano;

20 hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi; lakini kula kabla hajanawa mikono hakumtii mtu unajisi’.

Kama vile tulivyoona unajisi wa mwilini, unaweza ukawa kweli umeshaoga na kusafishika lakini ulikuwa bado huruhusiwi kuingia uweponi mwa Bwana kwa kitambo Fulani, aidha kwa siku moja, au kwa wiki, au kwa mwezi, au kwa miezi miwili inategemea na aina ya unajisi uliokuwa nao..Vivyo hivyo na unajisi wa rohoni, mtu unaweza kweli ukasemehewa kwa alilolifanya lakini hilo bado lisimfanye arudi uweponi mwa Bwana muda huo huo..bali kinaweza kupita kitambo kirefu sana..

Kama Bwana Yesu alivyosema, mawazo mabaya ni moja ya mambo yanayomtia mtu unajisi, unaweza ukawa wewe sio mzinzi lakini ndani yako muda wote unawaza uzinzi, sasa hapo tayari jambo hilo limeshautia doa utakatifu wako, umejitia unajisi.. Utakwenda kutubu kweli na pengine Mungu atakusamehe, lakini kurudi kule uweponi mwa Bwana, ambapo ulikuwa nako mwanzoni kunaweza kukuchukua muda sana..ndio maana tunapaswa tuwe makini sana..

Mawazo kama haya yanapokujia ndani yako hupaswi kuyapa nafasi hata kidogo, unayakataa na kuyakemea, na hapo hapo kupeleka mawazo yako katika Neno la Mungu na ahadi zake. Hiyo ndiyo njia pekee ya kutokujitia unajisi na mawazo ya namna hiyo..Vilevile unaacha kutazama au kuangalia vitu ambavyo vinachochea unajisi huo..Kama utakuwa mtazamaji wa movie za kidunia muda wote ambazo hizo ndani yake huwezi kosa maudhui ya uasherati unategemea mawazo hayo yasikutawale? Yatakutawala tu, unasikiliza miziki ya kidunia yatakutawala tu, unachati kwenye magroup yao, unasikiliza mazungumzo yao, unasoma visa vya hadithi za kiasherati, unafuatilia magazeti ya kiasherati…mawazo kama hayo yatakuteka, na itakuwa nguvu kujitawala..matokeo yake unajitia unajisi, na kuifanya bidii yako kuwa sio kitu mbele za Mungu..

Kama wewe ni mtukanaji au unazungumza maneno yasiyofaa, au msengenyaji…tayari unajitia mwenyewe unajisi, haijalishi unafunga, saumu yako ni bure tu..kwasababu doa tayari limeshaingia,..unapaswa ujifunze kukizuia kinywa chako.

Na ndio maana ukitoka tu kuwaza mambo kama hayo maovu, au ukitoka tu kuzungumza maneno hayo, unaona ndani yako ukame mkubwa, ile nguvu labda ya kusali imepungua ghafla, au ule uwepo wa Mungu ghafla umepotea ndani yako..Sasa ukishaona hivyo basi ujue tayari ulishajitia unajisi..Unapaswa ukatubu na uache kivitendo..na hiyo inaweza kuchukua muda kidogo mpaka kuurudisha tena uwepo wa Mungu karibu na wewe…Hayo ndiyo madhara ya kujitia unajisi…inasababisha uwepo wa Mungu kukaa mbali na wewe kwa muda.

Hivyo biblia ilishatuonya tuilinde mioyo yetu, kuliko kitu kingine chochote,(Mithali 4:23) kwasababu humo ndimo zitokazo chemchemi za maji ya uzima. Hivyo Bwana atusaidie sote tukae mbali na unajisi wa aina yoyote, ili safari yetu isiwe na vikwanzo visivyokuwa na lazima.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Akawaambia Enendeni ulimwenguni mwote,MKAIHUBIRI INJILI KWA KILA KIUMBE.(Marko16:15.) Yesu Anamaanisha nini kusema MKAIHUBIRI INJILI KWA KILA KIUMBE?

Sabato halisi ni lini, Je! ni Jumapili au Jumamosi?, Ni siku gani itupasayo kuabudu?

Inaruhusiwa Kula nyama ya Nguruwe kwa Mkristo wa Kweli?

ZIKUMBUKE FADHILI ZA MUNGU

UNYAKUO.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

MJUMBE WA AGANO.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments