Biblia inapozungumza juu ya fadhili za Mungu, ni zaidi ya zile fadhili ambazo tunazojua ambazo mtu anaweza kuzifanya kwa mtu mwingine, yaani kumuonyesha ukarimu na wema..
Kibiblia Fadhili za Mungu ni Neno pana sana, kwa kiebrania linatamkwa “Hesed”, ambalo tafsiri yake huwezi kuelezea kwa neno moja, au kwa maneno machache.
Fadhili za Mungu sio tu wema na ukarimu Mungu anaotufanyia sisi, bali linamaanisha pia Upendo wa Mungu usioelezeka, upendo wa kusaidia, upendo wa kuvumilia, Upendo wa kuokoa upendo wa kutoa,..
Ni wema usio na masharti, kwamba hatutendei fadhili zake kisa sisi tumemfanyia kitu kwanza, au tumekuwa marafiki zake, Hapana. Anatenda kama vile ni wajibu wake kufanya, Wema huo hauwezi kuelezeka, kwasababu unagusa kila Nyanja, ambazo haziwezi kufikiwa na mwanadamu yoyote Yule, au kiumbe chochote kile mbinguni au duniani., umeingia ndani kabisa.
Na ndio maana Neno hili utalisoma sehemu nyingi sana katika biblia, Na pia utaona Daudi kila alichokiona au alichokitaja alihitimisha na neno “kwa maana fadhili zake ni za milele”..
ZABURI 136
1 Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
2 Mshukuruni Mungu wa miungu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
3 Mshukuruni Bwana wa mabwana; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
4 Yeye peke yake afanya maajabu makuu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
5 Yeye aliyefanya mbingu kwa fahamu zake; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
6 Yeye aliyeitandaza nchi juu ya maji; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
7 Yeye aliyefanya mianga mikubwa; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
8 Jua litawale mchana; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
9 Mwezi na nyota zitawale usiku; Kwa maana fadhili zake ni za milele. 10 Yeye aliyewapiga Wamisri kwa kuwaua wazaliwa wa kwanza wao; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
11 Akawatoa Waisraeli katikati yao; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
12 Kwa mkono hodari na mkono ulionyoshwa; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
13 Yeye aliyeigawa Bahari ya Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
14 Akawavusha Israeli katikati yake; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
15 Akamwangusha Farao na jeshi lake katika Bahari ya Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
16 Yeye aliyewaongoza watu wake jangwani; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Vipo vifungu vingi sana Soma pia.. 1Nyakati 16:34, Zaburi 106:1 n.k.
Utaona pia Musa alipofumbuliwa macho yake na kumwona Mungu kwa sehemu, alipokuwa kule mlima alitangaza na kusema;
Kutoka 34:6 “Bwana akapita mbele yake, akatangaza, Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, MWENYE FADHILI, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli;
Vivyo hivyo kilichomchea Mungu kumtuma mwanawe duniani kuja kutuokoa, hakikuwa kingine zaidi ya Fadhili zake za milele zinazodumu kwetu daima..
Alikuwa tayari kumtoa mwanawe wa pekee kafara ili sisi tupate wokovu, Jiulize wewe unaweza kumtoa mwanao, tena yule unayempenda kuliko wote awe sadaka ili jirani yako ambaye hakusaidii chochote apone au afaidike? Unaweza kufanya hilo? Huwezi kwasababu hujafikia kiwango hicho cha fadhili za Yehova.
Hivyo kama tukiyajua hayo ni wajibu wetu kumwimbia usiku na mchana, kumshukuru juu ya wema wake aliotuonyesha na anaotufanyia kila siku. Na Tunampa Mungu sifa za vinywa vyetu, pamoja na kwa MATOLEO YETU.
Jina la Yesu Kristo libarikiwe daima.
Haleluya.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Vikuku ni vitu mfano wa bangili ambavyo vinavaliwa aidha mikononi au miguuni, kwa lengo la urembo. Tazama picha juu. Katika enzi za zamani vikuku vilivaliwa na jinsia zote, yaani wanaume na wanawake.
Katika biblia tunaona neno hilo likitokea mara kadhaa..
2 Samweli 1:10 “Basi, nikasimama karibu naye, nikamwua, kwa sababu nalijua hakika ya kuwa hawezi kupona baada ya kuanguka; kisha nikaitwaa ile taji iliyokuwa kichwani mwake, na kikuku kilichokuwa mkononi mwake, nami nimevileta hapa kwa bwana wangu”.
Na pia unaweza kusoma mistari ifuatayo binafsi iliyozungumzia juu ya vikuku Mwanzo 24:47, Isaya 3:19, Ezekieli 16:11 na Ezekieli 23:42.
Lakini sio hilo tu, vikuku pia vilitumika katika kutengenezea mishikio ya masanduku. Kwa mfano utaona sanduku la Agano lilitengenezwa kwa vikuku katika pande zake za chini ili kuwezesha upitishaji wa zile fimbo zake, na kufanya ubebaji wake uwe mrahisi… Tazama picha chini.
Kutoka 25: 14 “Nawe tia hiyo miti katika vile vikuku vilivyo katika pande mbili za sanduku ili kulichukua hilo sanduku.
15 Hiyo miti itakaa katika vile vikuku vya sanduku; haitaondolewa.
16 Kisha tia ndani ya sanduku huo ushuhuda nitakaokupa”.
Lakini je! Katika agano tunaruhusiwa kuvaa vikuku?
Jibu ni la!. Mwanaume au mwanamke wa kikristo hapaswi kutoboa pua na kuweka hazama, hapaswi kujiharibu ngozi kwa kujichubua, hapaswi kuvaa vikuku katika mikono yake au miguu yake..Kwasababu miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu.
1Petro 3:3 “Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi;
4 bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.
5 Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao”
Mwanamke anayevaa kikuku mguuni, anakuwa hana tofauti na kahaba. Matumizi ya vikuku yabaki katika kutengenezea masanduku na bidhaa nyingine lakini si kuivalisha miili yetu.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Hazama ni nini katika biblia?(Ezekieli 16:12, Kutoka 24:47)
KUJIPAMBA NI DHAMBI?
UUMBAJI BORA WA MUNGU, UPO NDANI YA MWANADAMU.
UFUNUO NI NINI, NA NITAPOKEAJE UFUNUO KUTOKA KWA MUNGU?
UFUNUO: Mlango wa 3 part 3
Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, Ni neema tumeiona tena siku ya leo, hivyo nakukaribisha katika kuyatafakari Maneno ya uzima wa roho zetu.
Leo tutajifunza jinsi wokovu unavyopatikana.. Tunapozungumzia wokovu maana yake ni tunazungumzia Uponyaji wa Roho zetu. Upo uponyaji wa mwili na uponyaji wa roho. Sasa njia ya uponyaji wa mwili ni tofauti na ile ya roho.
Sasa kama utakumbuka katika hatua za mwanzo kabisa za wana wa Israeli kutolewa Misri, utaona Farao alikuwa akipigwa kwa mapigo kadha wa kadha…Utaona alikuwa analetewa makundi ya nzige, mara nzi, mara Vyura na chawa n.k. Na kila walipomlilia Bwana awaondolee hayo mapigo Mungu alikuwa anayaondoa katikati yao..
Kutoka 8: 8 “Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni na kuwaambia, Mwombeni Bwana, ili awaondoe vyura hawa kwangu mimi na kwa watu wangu; nami nitawapa watu ruhusa waende zao, ili wamtolee Bwana dhabihu.
9 Musa akamwambia Farao, Haya, ujitukuze juu yangu katika jambo hili; sema ni lini unapotaka nikuombee wewe, na watumishi wako, na watu wako, ili hao vyura waangamizwe watoke kwako wewe na nyumba zako, wakae ndani ya mto tu.
10 Akamwambia, Kesho, Akasema, Na yawe kama neno lako; ili upate kujua ya kwamba hapana mwingine mfano wa Bwana, Mungu wetu.
11 Hao vyura wataondoka kutoka kwako wewe na nyumba zako, na watumishi wako, na watu wako; watasalia mtoni tu.
12 Basi Musa na Haruni wakatoka kwa Farao; Musa akamlilia Bwana katika jambo la hao vyura aliokuwa amewaleta juu ya Farao.
13 Bwana akafanya sawasawa na neno la Musa; na hao vyura wakafa kutoka katika zile nyumba, na katika viwanja, na katika mashamba”
Na Mainzi ni hivyo hivyo na mapigo mengine yote… Wamisri walipomwomba Mungu awaondolee, Mungu aliwasikia na kuliondoa lile tatizo…soma Kutoka 8:29-30.
Lakini tunakuja kuona mbele kidogo tu, wakati wana wa Israeli tayari wameshavuka bahari ya Shamu, walipomuudhi Mungu, na Mungu alipowaletea zile nyoka za moto…Walimlilia Mungu aziondoe lakini hakuziondoa…badala yake aliwatafutia dawa ili kila aliyeumwa, wanapoitazama ile nyoka ya shaba wapate kupona.
Hesabu 21: 5 “Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu.
6 Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa.
7 Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu.
8 Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi.
9 Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi”.
Hapo Bwana hakuwaondoa hao nyoka, kama alivyoondoa wale vyura, au nzige, au chawa wakati wa Farao. Badala yake aliwaacha nyoka waendelee kuwepo (maana yake waendelee kuuma watu)..Na mtu mwenyewe achague aidha UZIMA au MAUTI. Kama atachagua uzima basi atajinyenyekeza na kwenda kuitazama ile nyoka wa shaba, lakini kama hatataka na kuamua kutafuta njia zake yeye mwenyewe anazozijua za kujitibu, basi atakufa.
Sasa Jambo hilo ufunuo wake ni upi?
Bwana Yesu mwenyewe alitufumbua macho na kutupa ufunuo wa tukio hilo katika kitabu cha Yohana. Anasema;
Yohana 3:14 “Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa;
15 ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye”
Umeona?.. Yule nyoka wa shaba ni mfano wa Yesu Kristo pale msalabani, na wale nyoka ni dhambi iletayo mauti. Hivyo kila mtu anayetumikishwa na dhambi ambayo mshahara wake ni mauti, Akitaka tiba ya hiyo dhambi ni kumtazama Kristo tu.
Kristo kazi yake hakuja kuiondoa dhambi katikati ya jamii yetu, hapana, dhambi ipo ndio maana unaona mpaka leo watu wanaitenda. Alichokuja kukileta ni dawa ya hiyo dhambi. Na sio lazima mtu kupokea uponyaji, ni uchaguzi wa mtu, kuchagua uzima au kifo. Kwa namna ile ile, jinsi wale nyoka walivyoendelea kuachwa katikati ya wana wa Israeli, hawakuondolewa..ili kila mtu ajue kifo kipo na hivyo achague uzima au kifo.
Ndugu usomaye ujumbe huu. Kama hujayakabidhi maisha yako kwa Yesu, biblia inasema..
Kumbukumbu 30:15 “Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya”
Wokovu sio wa kuchaguliwa na mtu, au kuletewa na mtu, ni jukumu la wewe binafsi kuchagua.. Mungu hawezi kulazimisha wokovu uingie ndani yako kama wewe hutaki. Hivyo ni jukumu lako aidha kuchagua kuishi katika dhambi siku zote ambapo mshahara wake ni mauti ya mwilini na rohoni, au umtazame Kristo pale msalabani upate uzima wa milele. Uchaguzi ni wako.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Ashera au kwa jina lingine anajulikana kama Ashtorethi, Ni mungu-mke wa kipagani ambaye alikuwa anabudiwa katika nchi ya wakaanani, Waashuru na mataifa mengine ya kando kando pale mashariki ya kati..
Ashera pamoja na Baali ni moja ya miungu ambayo ilikuwa ni maarufu sana duniani kwa wakati huo.
Katika nchi ya Kaanani walikuwa wanamwabudu katika mfumo wa mti, ambao ulipandwa chini, na kuchongwa katika maumbile ya mwanamke, kumwakilisha yeye. Wakimwona kama ndiye mti wa uzima.
Sasa tunaona katika maandiko, Wana wa Israeli wakiwa bado jangwani Mungu aliwaonya sana, juu ya miungu ya nchi hiyo ya Kaanani wanayoiendea, kwamba wasijichanganye nayo, badala yake wakifika huko waivunje vunje, na kuiondoa, kwasababu yeye ni Mungu mwenye wivu;
Kutoka 34:12 “Ujihadhari nafsi yako, usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi ile unayoiendea, lisiwe mtego katikati yako.
13 Bali utabomoa madhabahu zao, na kuvunja-vunja nguzo zao, na kuyakata-kata maashera yao.
14 Maana hutamwabudu mungu mwingine, kwa kuwa Bwana, ambaye jina lake ni mwenye wivu, ni Mungu mwenye wivu”.
Lakini tunaona walipofika nchi ya ahadi hilo hawakulizingatia badala yake, nao wao pia wakaanza kuiga desturi za wale wafiisti ambao hawakuwamaliza wote, wakaanza na wao kuabudu Maashera..
2Wafalme 17:9 “Tena, wana wa Israeli wakafanya kwa siri mambo yasiyokuwa mema juu ya Bwana, Mungu wao, wakajijengea mahali pa juu katika miji yao yote, kutoka mnara wa walinzi hata katika miji yenye boma.
10 Wakajisimamishia nguzo na maashera juu ya kila mlima mrefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi”;
Ikafikia hatua mpaka wafalme wengine wakawa sio tu wanaibudia nje kwa siri, bali waliichukua kabisa nguzo zake na kuipeleka katika hekalu la Mungu, mahali ambapo Mungu ameliweka jina lake, watu wamwabudu na kumfanyia dua, wao wanaingiza miungu migeni, Matokeo yake wakamtia Mungu wivu mkubwa zaidi, wakapewa adhabu ambayo isiyosameheka, na adhabu yenyewe ilikuwa kuuliwa, mji kuteketezwa na kuchukuliwa utumwani Babeli.
Mfalme ambaye alifanya kitendo hicho aliitwa Manase;
2Wafalme 21:7 “Akaiweka sanamu ya kuchongwa ya Ashera aliyoifanya ndani ya nyumba, ambayo Bwana alimwambia Daudi, na Sulemani mwanawe, Katika nyumba hii, na katika Yerusalemu, niliouchagua miongoni mwa kabila zote za Israeli, nitaliweka jina langu milele”;
Utasoma habari za maashera katika vifungu hivi;
2Nyakati 14:2,17:6, 19:3, 24:18, 23:14
Je hadi leo kuna maashera yanayoabudiwa?
Hata sasa Mambo hayo yanatendeka katika Kanisa la Kristo hata leo, na cha kusikitisha zaidi ni kuwa wanajua kabisa Mungu amekataza lakini wao wanafanya.
Unapoliweka sanamu la mtakatifu fulani (tuseme bikira Mariamu), na kuanza kulihusianisha na ibada, unaomba kwa kupitia hilo, unaeleza shida zao kwa kutazama sanamu hilo, ujue kuwa unamwabudu Ashera moja kwa moja.
Na tendo hilo linamtia wivu Mungu sana, wivu ambao unaweza kukusababishia mauti. Ni heri ukutane na hasira ya Mungu kuliko Wivu wake..Kwasababu wivu unakula na hivyo mapigo yake ni makali zaidi.
Wimbo 8:6b..Kwa maana upendo una nguvu kama mauti, Na wivu ni mkali kama ahera.
Biblia inasema tena…
Mithali 27:4 “Ghadhabu ni kali, na hasira ni gharika; Lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu”.
Unaona?, shida inakuja ni pale mtu anapoelezwa ukweli kama huu, anadhani dini yake inashutumiwa..Nakwambia ni heri dini ishutumiwe roho yako ipone, kuliko roho iangamie dini yako iendelee kumtia Mungu wivu, faida yake itakuwa ni nini sasa? Tubu mgeukie Kristo, uokoke. Hizi ni nyakati za mwisho.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Shalom, karibu tujifunze maneno ya uzima.. Lipo swali ambalo linaulizwa na watu wengi, kwamba kama Mungu anajua kuna jambo litakwenda kutokea mbeleni ambalo litanisababishia mauti, kwanini basi asinizuie kwenda kulifanya badala yake ananiacha mpaka naingia, na mwisho wa siku napotea na kwenda kuzimu? Mbona kama vile atakuwa sio Mungu wa upendo?
Kama na wewe swali hili lipo ndani yako basi tuzidi kutafakari pamoja somo letu la leo,
Kitabu cha Mithali kinasema..
“Kwa kuwa mtego hutegwa BURE, Mbele ya macho ya ndege ye yote”.( Mithali 1:17).
Embu jiulize, mtu anayetega mtego wa kumshika ndege kwa ajili ya kitoweo chake, Je! Unadhani Mungu hampendi ndege yule? Au unadhani Mungu hajampa uwezo wa kuwakimbia maadui zake kiwepesi?
Au mtu anayetega mtego wa kunasa panya, unadhani Mungu anawachukia panya, na hivyo kawaondolea uwezo wa kuwakimbia adui zao?
Au mtu anayetega ndoano kuvua samaki, unadhani Mungu hawapendi samaki wake,?
Sikuzote mpaka umeona kitu fulani kinaundiwa mitego, basi ujue kuwa kitu hicho kilishashindikana kukamatika kwa njia rahisi, au ya kawaida, hivyo kimetafutiwa njia mbadala, kwamfano leo hii unaweza kumuona ndege katua hapo pembeni yako, hatua kadhaa tu pembeni, lakini embu kajaribu kwenda kumkamata kwa mikono yako kama utaweza,? Au umwone panya anakatiza kwenye kona ya nyumba, au store, halafu fanya mazoezi ya kwenda kumkata kwa mikono kama vile unavyokamata chura uone kama itakuwa ni kazi rahisi kwako.
Au umwone samaki anaelea juu ya maji, hivyo unatakwenda kwenda kumchota haraka kwa mikono yako, jaribu zoezi hilo kama litakuwa rahisi. Huwezi kuwapata kwasababu Mungu tayari kashawekea uwezo ndani yao wa kujiangua kutoka kwa maadui zao kivyepesi sana.. na wenyewe wanajua kabisa maadui zetu ni ngumu kutushika kwasababu hawana wepesi tulionao sisi, au hawana uhodari tulionao sisi wenyewe.. Na sisi tunaowawinda tunajua kuwa ili waendelee kuwa salama ni wajibu wao, kutotuamini sisi kwa kitu chochote siku zote za maisha yao hapa duniani, haijalishi tutawavutia kwa vitu vingi kiasi gani wanavyovipenda.
Vivyo hivyo na sisi wanadamu, Mungu ameshatupa uwezo mkubwa sana ndani yetu wa kumshinda adui yetu shetani, na yeye analijua hilo, hawezi kuja na kukukamata hivi hivi kama anavyotaka, hana uwezo huo, anajua kabisa hawezi kukupata, lakini anachokifanya ni kijiundia mitego yake mbalimbali, ambayo hiyo ikishakunasa, basi hapo ndipo anakuwa na uwezo wa kukufanya chochote anachotaka ikiwemo hata kukuua.
Kwamfano mtego mmojawapo maarufu , ni uasherati, shetani anaweza kukuletea kahaba, ili mkazini, lengo lake sio ukutane na kahaba au uzini tu halafu basi, hapana, bali ni ukosane na Mungu wako kwa kitendo hicho, ili apate nafasi ya kuyaachilia mapepo yake yaingie katika maisha yako kukuharibu kirahisi katika kila nyanja, ikiwemo upate na magonjwa ya zinaa kama vile ukimwi ili ufe kabla ya wakati wako.
Lakini hayo anajua hayawezi kuja hivi hivi, ni mpaka akuwekee mtego, ndipo hapo anakuletea kahaba mzuri, au mwanaume mwenye pesa, anakulaghai na wewe bila kufikiri kuwa ule ni mtego umewekwa mbele yako unakwenda kuuva, ukidhani kuwa Mungu atakuepusha nao.. Hilo Mungu hawezi kulifanya ndugu yangu.
Kwa nafasi yako soma kitabu cha Mithali sura ya 7 yote, uone jinsi, kijana mpumbavu aliyetegwa na mwanamke mzinzi, na hatma yake inavyokuwa; hatuwezi kusoma vyote lakini vile vifungu vya mwisho mwisho vinasema..
Mithali 7:21 “Kwa maneno yake mengi na ulaini akamshawishi, Kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda.
22 Huyo akafuatana naye mara hiyo, KAMA VILE NG’OMBE AENDAVYO MACHINJONI; Au mpumbavu kuadhibiwa katika pingu;
23 Hata mshale umchome maini; KAMA NDEGE AENDAYE HARAKA MTEGONI; Wala hajui ya kuwa ni hasara ya nafsi yake.
24 Basi, wanangu, nisikilizeni sasa, Mkayaangalie maneno ya kinywa changu.
25 Moyo wako usizielekee njia zake, Wala usipotee katika mapito yake.
26 Maana amewaangusha wengi waliojeruhi, Naam, JUMLA YA WALIOUAWA NAYE NI JESHI KUBWA.
27 Nyumba yake ni njia ya kwenda kuzimu, Hushuka mpaka vyumba vya mauti.
Ndege anayenaswa kwenye mtego ni kajitakia mwenyewe na sio kwamba alikuwa ni dhaifu, tamaa zake ndizo zilizompeleka pale,. Leo hii, unapojikuta kwenye matatizo mazito, ambayo unajua kabisa ni kwasababu ya dhambi Fulani uliyoifanya ndio yakakukuta, usianze kumlaumu Mungu ni kwanini hakukuepusha nayo hapo kabla. Mungu alishakupa uwezo huo tangu zamani, Na Mungu naye hawezi kumlaumu shetani, kwasababu shetani naye analo la kujitetea, anasema mimi sikumuita mtu aje kwenye mtego wangu, wala sikumlazimisha mtu, kufuata kile nilichokiweka kwenye mtego, ni yeye mwenyewe alinifuata, ni ndio hapo akanasikia akaangamia, ilikuwa ni wajibu wake kuchukua tahadhari anapoishi duniani.
Na ndio maana biblia inasema..
Hosea 4: 6 “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa;..”
Tukikosa maarifa ya kuzijua njama za shetani, au kuyajua mafumbo ya shetani, tutajikuta tunaingia katika matatizo ambayo tutajiuliza ilikuwaje kuwaje tumejikuta hapa,
Ufunuo 2:24 “Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wo wote wasio na mafundisho hayo, WASIOZIJUA FUMBO ZA SHETANI, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine.
25 Ila mlicho nacho kishikeni sana, hata nitakapokuja”.
Hivyo kila mmoja anao wajibu wa kupata maarifa sahihi ya kuitambua mitego ya adui. Na maarifa hayo utayapata kutoka katika Neno la Mungu tu basi, biblia imejaa siri za kuepukana na hila za adui. Na ndio maana shetani hapendi watu waisome.
Kuwa msomaji wa biblia kila siku, tafakari , usiisome kama gazeti, hiyo tu ndio itakayokuwa nuru yako katika zama hizi za kumalizia, kumbuka mitego ni mingi, vishawishi ni vingi, na ipo ya aina tofauti toauti, uwezo umepewa, pengine umepungukiwa tu na maarifa. Hivyo ni wajibu wako kuyatafuta maarifa hayo, ambayo utayapata katika Neno la Mungu. Yaani BIBLIA.
Hakuna jaribu lolote linalotendeka leo hii, ambalo halijawahi kuandikwa katika biblia na njia ya kuepukana nalo., Hivyo jijengee desturi ya kusoma Neno la Mungu. Ili usiwe wa kumlaumu Mungu, kwanini hiki, kwanini kile, wakati ni wewe mwenyewe uliyakataa maarifa, hivyo ukanasika kirahisi.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Kwanini Mungu awachome watu kwenye ziwa la moto na hali yeye ndiye aliyewaumba?
JINA LAKE KWA KIEBRANIA NI ABADONI, NA KWA KIYUNANI NI APOLIONI.
Ufunuo ni kitu kilichofunuliwa.. Maana yake ni kwamba kilikuwa kimefichika/kimefichwa sasa kimefunuliwa.
Tunaposoma maandiko na kupata kitu kipya ambacho hatukuwa tunakijua hapo kwanza, hapo ni sawa na hicho kitu kimefunuliwa kwetu.
Kwamfano unaposoma biblia kuhusu damu ya Yesu, na ukagundua kitu kipya kuhusu damu hiyo, hicho ulichokipata ndio ufunuo. Sasa hicho ndicho kinachoelezea ukubwa wa Imani yako, Ukipata kujua/kugundua kitu kikubwa zaidi kuhusu damu ya Yesu, ndivyo Imani yako inavyozidi kuwa kubwa. Maana yake ni kwamba kwa ufunuo huo unaweza kutatua matatizo makubwa ya kiroho, au kufanya mambo makubwa, tofauti na yule mtu ambaye bado hajapata ufunuo wowote kuhusu damu ya Yesu.
Na maneno mengine yote ya Mungu ni hivyo hivyo, Ukipata kugundua kitu cha kipekee kumhusu Yesu, ambacho hapo kwanza ulikuwa hukijui.. Hicho ulichokigundua ndicho shetani kinachomwogopesha na ndicho hicho kinachoweza kukupa matokeo makubwa ya rohoni.Na kugundua huko kunaletwa na Roho Mtakatifu mwenyewe ndani ya mtu.
Sasa Ufunuo upo wa uongo, na Pia upo wa ukweli.
Unaweza kusoma neno ukapata kitu au ukagundua kitu ambacho ulikuwa hujakijua hapo kwanza.. Sasa hicho kitu ulichokigundua kama ni cha ukweli (maana yake kama kimetokana na Mungu kupitia Roho wake Mtakatifu) basi kitakubaliana na mistari mingine au habari nyingine za kwenye biblia.
Lakini kama si cha ukweli basi kitakinzana na mistari mingine ya biblia. Maana yake si cha kukipokea wala kukiamini.
Sasa ni kwa namna gani tutapokea Ufunuo?. Zipo njia kuu Mbili.
Wengi hawapendi kulisoma Neno la Mungu wao binafsi, na badala yake wanapenda kufundishwa, au kutazama filamu fulani tu za kikristo, Lakini pasipo kujua kuwa kuna hatari kubwa sana ya kudanganywa kama usipojijengea tabia ya kulisoma mwenyewe Neno.
Kwasababu wanaofundisha uongo ni wengi kuliko wanaofundisha ukweli. Bwana Yesu alisema Njia ni nyembamba, maana yake mimi na wewe hakuna namna tunaweza kuifanya iwe nene, na alisema Manabii wengi wa uongo watatokea watawadanganya hata yamkini walio wateule, hakuna namna tunaweza kuwafanya wawe wachache hawa manabii wa uongo. Kwahiyo Njia itakayobakia kuwa bora siku zote ni ile ya mtu binafsi kutafuta kulisoma Neno yeye binafsi maadamu anao uwezo wa kusoma na kuandika. Na hapo hapo Roho Mtakatifu anapata nafasi ya kumfunulia maandiko.
Na kumbuka tunapozungumzia kusoma Neno hatumaanishi kwenda kuchukua mstari mmoja hapa kwenye Mathayo na kisha kwenda kuruka kutafuta mstari mwingine wa faraja kwenye Isaya, Na kurudi kuunganisha mwingine kwenye Yeremia..na hivyo kujikuta kwa siku umesoma mistari mia, tofauti tofuati kwa masaa mawili na kujipongeza kuwa umelisoma Neno..Nataka nikuambia hapo utakuwa hujasoma biblia bali umeiperuzi biblia, wanaoiperuzi biblia ni wahubiri, na wanafanya hivyo kwa lengo la kufundisha, somo lipate kueleweka kwa muda mfupi. Hivyo wewe usiiperuzi biblia, hutaelewa chochote na wala hutapata kitu cha kudumu cha kukusaidia roho yako.
Kusoma Neno kunakofaa ni huku, kushika kitabu kimoja kimoja…kukisoma chote pasipo kuruka…sio lazima ukisome chote kwa siku moja hapana, Mfano unaweza kuanza kusoma kitabu cha Mwanzo, sura 10 za kwanza na kisha kupata muda mrefu wa kuzitafakari, na hata kuzirudia tena hizo mpaka utakapoona umeelewa vya kutosha kusonga mbele.. lakini ukisoma sura 4, 5 ukafika sehemu inazungumzia vizazi ukaboreka na kisha ukarukia kitabu cha kutoka hutakaa uielewe biblia..
Soma kitabu cha Mwanzo chote kimalize, haijalishi itakuchukua wiki au mwezi, kisha nenda kitabu kinachofuata… Ukifanya hivyo utaielewa biblia sana, na Ndio chanzo kikubwa cha KUPATA UFUNUO WA KWELI wa Neno . Na pia unaposoma biblia, hakikisha unafungua kule nyuma kwenye ramani, uielewe pia ramani kama biblia yako inayo ramani..fuatilia kwenye ramani zile hatua Ibrahimu alizopita, Wana wa Israeli walizopita, miji Bwana Yesu aliyokuwa anatembea n.k.
Sasa kama tulivyotangulia kusema, Kuna hatari kubwa sana katika kutegemea njia hii kupata ufunuo wa Neno la Mungu. Lakini njia hii ikitumika sahihi pia ni rahisi kupata mengi.
Sasa njia bora sio kufungulia redio au internet na kwenda kusoma au kusikiliza mahubiri yanayoendelea kila siku, na huku huna habari kabisa na biblia yako, hapo nakuambia utakwenda na maji, haijalishi mhubiri huyo umemwamini kiasi gani.
Njia bora ni ya kupata ufunuo wa Neno la Mungu kupitia watumishi wa Mungu, ni wewe kwenda kusoma Neno kwanza, labda mada fulani katika biblia.. Na kisha ukishaisoma hiyo mada na ukaielewa, isipokuwa kuna vipengele vichache ambavyo hukuvielewa na ungehitaji kuviongezea maarifa, ndipo unamtafuta Mtumishi na kumuuliza kulingana na ile mada uliyoisoma, au unakwenda katika internet na kukitafuta kitu kile, uone maoni ya watumishi mbali mbali kuhusu jambo hilo.
Hiyo ni njia bora ambayo itakusaidia kutokudanganywa kirahisi, kwasababu utakuwa unakwenda kutafuta kujua kitu ambacho tayari una ufahamu nacho angalau kidogo, hivyo ni ngumu kudanganyika…Kamwe usiende kutafuta kuuliza kitu ambacho hata wewe mwenyewe hujui kinapatikana wapi kwenye biblia.
Ni sawa umekwenda kwenye mji uliochanganyikana kama Kariakoo, na kuanza kuuliza uliza, bila ya wewe kuwa na angalau taarifa ndogo ya kile unachokitafuta au unakokwenda, kwasababu kama hujui kabisa ni rahisi kutapeliwa na kupoteza kila kitu ulichonacho..Unaweza kuomba kuelekezwa benki ukaelekezwa kichochoro cha vibaka, ukaibiwa kila kitu hata nauli uliyokuwa umebakiwa nayo.
Ndio maana Bwana Yesu alisema katika Luka..
Luka 8:8 “Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang’anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho.”
Bwana anatuonya tujiangalie jinsi TUNAVYOSIKIA. Maana yake ukienda kutafuta kusimuliwa vitu bila wewe mwenyewe kutafuta kusoma kile kitu kwanza, angalau kidogo, kuna hatari kubwa ya wewe kupoteza kila kitu hata kile kidogo kizuri ulichokuwa nacho moyoni mwako. Ni rahisi hata kama kulikuwa na kitu cha ukweli moyoni mwako, ni rahisi kukipoteza hicho, Kwasababu utakayekutana naye kama atakuwa ni mwalimu au nabii wa uongo, atakutoa kabisa kwenye mstari (huko ndio kunyang’anywa hata kile kidogo ulicho nacho).
Kwamfano unakwenda kumuuliza Mwalimu/Nabii (wa uongo) kuhusu habari fulani kwenye biblia ambayo ulisikia tu watu mtaani wakisimuliana, ili hali wewe hujawahi hata kwenda kuifuatilia kwenye biblia inasemaje, yule nabii atakudanganya, na wewe utamwamini..na zaidi ya hayo, kama pia kama ulikuwa unaamini kuwa si sahihi kuoa wake wengi, huyo nabii atakupa maandiko na maandiko pia ya kukuambia ni ruksa kuoa wake wengi, na wewe utamwamini. Pasipo kujua kuwa tayari umeshanyang’anywa hata kile kidogo ulicho nacho.
Roho Mtakatifu anataka kutufundisha mengi, lakini sisi ndio hatutaki kumpa nafasi ya yeye kutufundisha, kwasababu tunakuwa wavivu wa kusoma (Waebrania 5:11). Tujitahidi kumpa nafasi.
Bwana atubariki.
Kama hujampokea Yesu, Basi fahamu kuwa ANARUDI.
Waebrania 10:37 “Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia”.
Hivyo mkaribie leo naye atakukaribia.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
JIFUNZE NENO LA MUNGU KWA BIDII ZOTE.
Uga ni nini? Na kazi yake ni ipi kibiblia?
MWILI NA DAMU YA YESU KRISTO.
VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 10 (Kitabu cha Zaburi).
CHUKIZO LA UHARIBIFU
Uga ni sakafu ya kupuria/kupepetea nafaka iliyotumika zamani.
Ikumbukwe kuwa zamani, hawakuwa na mashine za kupuria kama tulizonazo sasahivi baadhi ya sehemu, ilikuwa nafaka ikishatolea shambani, na majani yake, ilipelekwa moja kwa moja kwenye sakafu hii maalumu iliyonyooka ambayo ilijengwa kwa mawe, au juu ya ardhi ngumu,..Karibu kila shamba lilikuwa ni lazima liwe na sakafu yake maalumu kama hii, na kama shamba ni dogo, basi waliungana wawili au watatu kushea Uga mmoja.
Tazama picha juu,
Sasa nafaka ilipokuwa ikipelekwa pale, hatua ya kwanza, ilimwagwa kwenye Uga huo, kisha wanyama, kama Ng’ombe, au Punda, au Farasi, walipitishwa juu ya nafaka hiyo kuikanyanga kanyaga..Na lengo la kufanya hivyo ni kuyalegeza magamba magumu yaliyoishikilia nafaka.
Sehemu nyingine walitumia fimbo badala ya wanyama, na kuzichapa kama vile wanavyochapa maharage au mbaazi, katika baadhi ya sehemu tunazoishi, vivyo hivyo katika enzi za biblia hususani kipindi kile cha Ruthu.
Sasa baada ya hatua hiyo, kilichofuata, ilikuwa ni kupepeta ili kuondoa hayo makapi yaliyochanganyikana na nafaka.. Hivyo walitumia kifaa maalumu kilichoitwa pepeto.. pepeto lililotumika wakati ule, halikuwa kama hili la kwetu, la chekecheke, hapana, bali lilikuwa ni beleshi fulani ambalo mbeleni lina mdomo kama wa uma, au rato.
Hivyo walichokifanya ni kupitisha pepeto hilo katikati ya mchanganyiko huo wa nafaka na makapi, na kurusha juu, waliporusha juu, yale makapi yalichukuliwa na upepo na nafaka kurudi chini, na hivyo, wanairudia hatua hiyo, tena na tena na tena..mpaka nafaka peke yake ibaki chini kwenye ile sakafu. (Uga)
Kisha inaichotwa na kwenda kusagwa ajali ya matumizi ya nyumbani.. Hayo ndiyo yalikuwa matumizi ya Uga.
Unaweza kulisoma neno hilo katika vifungu hivi baadhi;
Ruthu 3:1 “Kisha Naomi akamwambia mkwewe, Je! Mwanangu, si vizuri nikutafutie raha, ili upate mema?
2 Basi na huyu Boazi, je! Siye wa mbari yetu, ambaye ulikuwapo pamoja na wasichana wake? Tazama, usiku wa leo atakuwa akipepeta shayiri pale ugani.
3 Basi wewe oga, ujipake mafuta ujivike mavazi yako, kisha uende kwenye uga; walakini usijionyeshe kwake mtu yule, ila atakapokwisha kula na kunywa”.
Soma pia kwa wakati wako, Ruthu 3:6,14, 1Nyakati 13:9, Yoeli 2:24, 1Samweli 14: 2 , Hosea 13:3, Yeremia 51:33
Je kuna umuhimu wowote wa sisi kufahamu juu ya Uga?
Jibu ni ndio, kwa kujua hilo itatusaidia kufahamu, Yohana alimaanisha nini pale inaposema juu ya habari za Yesu kuwa pepeto lake lipo mkononi mwake, kuusafisha uwanda wake..
Tusome;
Mathayo 3:11 “Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.
12 Ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake; na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika”.
Anachofanya Kristo leo hii ulimwenguni, ni kuusafisha uwanda wake(sakafu yake ya kupepetea ambalo ndio kanisa lake), na anaisafisha kwa pepeto, (uma) ulio mkononi mwake, Hivyo sote ni kama tunarushwa rushwa juu, na kama wewe utakuwa ngano halisi utashuka chini, lakini ukiwa kapi jepesi, utapeperushwa na upepo. Na baadaye utakusanywa na kwenda kuchomwa moto usiozimika.
Zipo pepo za aina nyingi leo hii ndugu yangu, Upepo wa mafundisho ya uongo, upepo wa unasa, upepo wa uzinzi, upepo wa fedha n.k..vyote hivi vinawapeperusha watu, Hizi ni nyakati za mwisho. Injili tuliyonayo sasa hivi sio injili ya kupembelezwa tena, ni injili ya kujichunguza umesimama wapi. Na unakwenda wapi. Hakuna mtu ambaye hajawahi kusikia injili, hivyo ni wajibu wako wewe mwenyewe kuhakikisha Kristo yupo ndani yako. Ili uwe mahali salama.
Shalom.
Tazama maana ya maneno mengine ya biblia chini.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
USIPIGE MATEKE MCHOKOO!
Hisopu/ Hisopo ni nini katika biblia?(Zaburi 51:7)
Bwana Yesu alikufa akiwa na umri gani?
Duara ya Ahazi ni ipi? Na je! Kivuli cha Hezekia kilirudije nyuma?
Mungu anaposema “nitaliweka jina langu” ana maana gani?
Rudi nyumbani
Biblia inatuonyesha Bwana Yesu alianza huduma yake akiwa na umri wa miaka kama 30. Luka 3:23.
Sasa ili tujue alikufa na umri gani, ni vizuri kwanza tukajua urefu wa huduma yake ulikuwa ni miaka mingapi, na hiyo ndio itakayotusaidia kujua alikufa na umri gani.
Tukisoma kitabu cha Yohana kinatuonyesha Bwana alihudhuria sikukuu za Pasaka zisizopungua tatu.
Ya kwanza tunaisoma katika Yohana 2:13, Ya pili katika 6:4, Na ya tatu tunaisoma katika 11:55-57
Kama tunavyojua pasaka hizi zilikuwa ni mwaka kwa mwaka, hivyo tukijumlisha hapo, tunaweza kupata hesabu ya miaka miwili (2).Ili kuelewa vizuri, chukulia mfano sikukuu ya kwanza ilikuwa ni mwezi april mwaka huu, sikukuu ya pili itakuwa ni mwezi April mwaka kesho, na sikukuu ya tatu itakuwa ni mwezi April mwaka kesho kutwa,. Hivyo ukianza kujumlisha tangu april mwaka huu, hadi April mwaka kesho kutwa utaona ni jumla ya miaka miwili mizima.
Lakini kutokana na kurekodiwa kwa matukio mengi ambayo aliyafanya Yesu, pamoja safari zake nyingi, wanazuoni walihitimisha kuwa kulikuwa na pasaka nyingine ambayo haijaandikwa katika biblia ilipita hapo katikati.
Na pasaka yenyewe iliangukia kati ya ile pasaka ya kwanza (Yohana 2:13) na ile ya pili (Yohana 6:4)..Kufanya muda wa huduma ya Yesu Kristo kuwa ni miaka 3.
Lakini, pia yapo matukio mengine ambayo yalitendekea kabla ya ile pasaka ya kwanza kufika, tunaona tangu Bwana Yesu abatizwe pale Yordani na Yohana, kulikuwa ni kipindi ambacho alifunga siku 40 kule jangwani, kulikuwa na wakati alisafiri kutoka Yordani, kwenda Kana, na baadaye kwenda Yerusalemu, kulikuwa na kipindi aliwaita wanafunzi wake na kuanza huduma ya kuhubiri, yote hayo yalichukua kipindi cha miezi kadhaa,kabla ya kuifikia ile pasaka ya kwanza. Na pia baada ya kufa na kufufuka kulikuwa na siku 40 ambazo aliwatokea watu wengi, kabla ya kupaa.
Hivyo tunaweza kusema, huduma ya Yesu Kristo, inakadiriwa kwenda kwa miaka mitatu na nusu.
Tukijumlisha na ile miaka 30 ya mwanzo, tunapata miaka thelathini na tatu na nusu. Hivyo Bwana Yesu alikufa akiwa na umri wa miaka hiyo (Thelathini na tatu na Nusu).
Lakini ni nini tunajifunza katika maisha ya Kristo?
Kristo Yesu Bwana wetu alikufa akiwa bado na umri mdogo sana, kwa dunia ya sasa watu watasema amekufa kabla ya wakati. Lakini tunaona katika umri huo mdogo aliimaliza kazi ile aliyoitwa duniani, na hivyo mbinguni akaonekana ndiye aliyefanya kubwa na yenye faida kuliko wanadamu wote waliowahi kuishi duniani, sio wale waliokufa wakiwa na miaka 900, wala wale waliokuwa na miaka 120, hakuna hata mmoja aliyefanya kazi kubwa yenye matunda mengi kama Kristo hapa duniani.
Siri ilikuwa ni nini?
Embu tafakari kwa maneno yake mwenyewe aliyoyasema katika vifungu hivi;
Yohana 9:4 “Imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi”.
Yohana 11:9 “Yesu akajibu, Je! Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu akienda mchana hajikwai; kwa sababu aiona nuru ya ulimwengu huu”.
Yohana 4:33 “Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula?
34 Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake”.
Mpaka hapo tunaweza kuona Bwana wetu alikuwa ni mtu wa namna gani.. Ni mtu ambaye aliuthamini muda wake akiwa hapa duniani, alijua kuwa muda hautakuwepo wakati wote, kuna siku giza litakuja na mtu asiweze kufanya kazi tena, aliichukulia kazi ya Mungu kama ndio chakula chake, kinachomfanya aishi hapa duniani, kwamba bila hicho atakufa, na kama tunavyojua mtu kula ni lazima kila siku.Hivyo yeye kuifanya kazi ya Mungu ilikuwa ni desturi yake kila siku na kila wakati..
Na ndio maana haikumchukua hata muda mrefu kumaliza huduma yake, hakusongwa na kitu chochote katika huu ulimwengu..
Je! Na sisi tunaweza kufanana naye?. Bwana atutie nguvu tuwe kama yeye.. Kwa nguvu zake tu peke yake ndio tutaweza.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Hisopo au Hisopu ni jamii ya mmea, ambao ulitumiwa zamani na wana wa Israeli kwa matumizi mbalimbali. Tazama picha ya mmea wenyewe juu.
Lakini mmea huu sana sana ulitumiwa kwa kwaajili ya shughuli za utakaso wa kimaagano, Kwamfano Hisopo ilitumika kuwatakasa watu waliokuwa na ukoma na nyumba zote zilizoathiriwa na ugonjwa huu,
Walawi 14:4 “ndipo huyo kuhani ataagiza kwamba watwae kwa ajili yake atakayetakaswa ndege wawili walio hai, ambao ni safi, na mti wa mwerezi, na sufu nyekundu, na hisopo;
5 kisha kuhani ataagiza ndege mmoja achinjwe katika chombo cha udongo kilicho juu ya maji ya mtoni;
6 kisha huyo ndege aliye hai atamshika, na huo mti wa mwerezi, na hiyo sufu nyekundu, na hisopo, naye atavichovya hivyo, pamoja na yule ndege aliye hai, katika damu ya huyo ndege aliyechinjwa juu ya maji ya mtoni;
7 kisha atamnyunyizia huyo atakayetakaswa na ukoma mara saba, naye atasema kwamba yu safi, kisha atamwacha yule ndege aliye hai aende zake nyikani”.
Soma pia Walawi 14:51
Waebrania 9:19 “Maana kila amri ilipokwisha kunenwa na Musa kwa hao watu wote, kama ilivyoamuru sheria, aliitwaa damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji na sufu nyekundu na hisopo, akakinyunyizia kitabu chenyewe, na watu wote”,
Brashi la kupakia damu, wakati ule Mungu anawapiga wamisri kwa pigo la mwisho, la kuwaua wazaliwa wa kwanza wa kimisri aliwaambia wana wa Israeli, watwae damu ya kondoo, kisha watumie tawi la hisopo kama brash la kuipaka damu hiyo, kiashirio cha kutakaswa kwao.
Kutoka 12:22 “Nanyi twaeni tawi la hisopu, mkalichovye katika ile damu iliyo bakulini na kukipiga kizingiti cha juu, na miimo miwili ya mlango, kwa hiyo damu iliyo katika bakuli; tena mtu ye yote miongoni mwenu asitoke mlangoni mwa nyumba yake hata asubuhi”.
Zaburi 51:7 “Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi, Unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji”
Wale askari walitumia ufito wa mmea huu, kushikilizia ile sifongo(sponji), ili kumnywesha Bwana Yesu siki,.
Yohana 19:29 “Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani”.
Kama tunavyojua mmea huu ni mmea wa utakaso, ulitumika kusafishia, hatushangai, kuona kwanini Kristo alipelekewa siki kwa mmea huu. Ni kuonyesha kuwa tayari alikuwa ni dhabihu safi iliyotakaswa, iliyowekwa tayari kwa ajili ya kutundolea sisi dhambi zetu.
Hivyo, mimi na wewe, tutatakaswa kwa hisopo ya rohoni si kwa kitu kingine zaidi ya damu ya Yesu Kristo tu. Kama hatutaoshwa kwa damu hii, kamwe tusitazamie ukoma wetu wa rohoni utaondoka, kamwe tusitazamia unajisi wetu utaondoka, kamwe tusitazamie tutamshinda shetani, na kamwe tusitazamie tutampendeza Mungu.
Swali ni Je! Umesafishwa kwa damu ya Yesu? Kama bado unasubiri nini mpendwa. Mkaribishe moyoni mwako akuokoe hizi ni siku za mwisho. Kuwa serious na maisha yako ya rohoni. Tubu dhambi zako, ufanywe mwana wa Mungu.
Maran Atha.
Tazama maana ya maneno mengine ya biblia chini,
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 693036618 / +255789001312
Mada Nyinginezo:
Kumlingana Mungu ni Kiswahili cha zamani chenye maana ya “kumwita Mungu”. Pale mtu anapopitia jaribu, au tatizo, anapomwita au kumlilia Mungu wake kwaajili ya kupata msaada, maana yake mtu huyo “amemlingana” Mungu.
Tunaweza kuona mifano michache katika biblia ya watu waliomlingana Mungu.
Wana wa Israeli:
Hawa walimwacha Bwana, na Bwana akawatia chini ya utumwa mkali kwa maadui zao.
Waamuzi 3: 8 “Kwa hiyo hasira za Bwana ziliwaka juu ya Israeli, naye akawauza na kuwatia mikononi mwa Kushanrishathaimu mfalme wa Mesopotamia; na wana wa Israeli wakamtumikia huyo Kushan-rishathaimu muda wa miaka minane.
9 Kisha wana wa Israeli walipomlingana Bwana, Bwana akawainulia wana wa Israeli mwokozi, aliyewaokoa, yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu”.
Yabesi:
1 Nyakati 4: 10 “Huyo Yabesi akamlingana Mungu wa Israeli, akisema, Lau kwamba ungenibarikia kweli kweli, na kunizidishia hozi yangu, na mkono wako ungekuwa pamoja nami, nawe ungenilinda na uovu, ili usiwe kwa huzuni yangu! Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba”.
Kwa Habari ndefu kuhusu huyu Yabesi na maisha yake unaweza kufungua hapa >> MAISHA YA YABESI.
Pia Neno hilo limetumika katika mistari mingine michache ifuatayo..1Nyakati 5:20, na 1Nyakati 21:26.
Jambo tunalojifunza ni kwamba hata sisi tunapoadhibiwa na Mungu, kutokana na makosa yetu tunapomgeukia Bwana na kumlilia (kumlingana), yeye ni mwenye rehema na huruma, anaghairi mabaya.
Na kama tupo kwenye dhambi, yaani hatumkabidhi Yesu Maisha yetu, basi ghadhabu ya Mungu ipo juu yetu, na kila tunapoisikia injili inayohubiriwa na watumishi wa Mungu, na kuidharau, Mabaya yanatuandama…
Yeremia 26:2 “Bwana asema hivi, Simama katika uwanja wa nyumba ya Bwana, useme na miji yote ya Yuda, wajao ili kuabudu katika nyumba ya Bwana; sema nao maneno yote ninayokuamuru kuwaambia, usizuie hata neno moja.
3 Labda watasikia, na kughairi na kuacha kila mtu njia yake mbaya; ili niyaghairi mabaya niliyokusudia kuwatenda, kwa sababu ya uovu wa matendo yao”.
Bwana yupo tayari kughairi mabaya aliyokuwa ameyapanga kuyaleta juu yako kwasababu ya uzinzi wako, au kwasababa ya utoaji wako mimba, au ulevi wako, au yoyote yale mabaya unayoyafanya. Endapo ukiamua kutubu na kumgeukia yeye.
Kama upo tayari leo kutubu na kumwita yeye (kumlingana), kama alighairi mabaya kwa wana wa Israeli, na kwa watu wengine wengi, ikiwemo mimi hatashindwa na wewe basi kama upo tayari leo kuanza maisha mapya fungua hapa kwa msaada Zaidi >> SALA YA TOBA.
Na kama tayari umeshaokoka, basi usiache kumwita (kumlingana) Mungu wako kila wakati, kwasababu yeye anajishughulisha sana na mambo yako.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo: