Je sisi wakristo tunaruhusiwa kufanya 40 za marehemu?

Je sisi wakristo tunaruhusiwa kufanya 40 za marehemu?

Je sisi wakristo tunaruhusiwa kufanya 40 za marehemu, au kufanya maziara ya makaburi baada ya mazishi?

Historia ya sherehe ya 40 ni ya kipagani na si ya kikristo. Asili yake ni katika Taifa la Misri, ambapo Watu waliokuwa mashuhuri (yaani wafalme au watu maarufu), baada ya kufa walikuwa wanapakwa dawa maalumu kwa muda wa siku 40, (Kila siku unapakwa mara moja na kisha unaachwa!, na kesho tena kurudiwa, na kesho kutwa mpaka siku 40 zitimie).

Na baada ya siku hizo kuisha ndipo mwili wa marehemu unafungwa katika sanda, na kisha kuwekwa kwenye sanduku Fulani maalumu, ambapo mwili ule utakaa mamia ya miaka bila kupotea kabisa kwa kuoza!. Ndicho Yusufu alichomfanyia baba yake Yakobo..

Mwanzo 50:1 “Yusufu akamwangukia babaye usoni, akamlilila, akambusu.

2 Yusufu akawaagiza watumishi wake waganga, kwamba wampake baba yake dawa asioze. Waganga wakampaka dawa Israeli.

3 SIKU ZAKE AROBAINI ZIKAISHA, maana hivyo hutimizwa siku za kupaka dawa. Wamisri wakamlilia siku sabini”.

Sasa hizo zilikuwa ni desturi za wamisri, na si waIsraeli, Yusufu alitumia desturi hiyo ya wamisri kwasababu sehemu kubwa ya Maisha yake aliishi Misri, hata mke wake alikuwa Mmisri, na hata jina lake alibadilisha na Farao na kuwa la KiMisri. Lakini baada ya sheria kuja kwa mkono wa Musa, hizo taratibu zilikufa!!!..na wala hakuna mahali popote Mungu aliwaagiza Israeli wazipake maiti dawa kwa siku 40 baada ya hapo!..

Kulikuwa na taratibu za kupata Mwili wa marehemu Marhamu (yaani Perfume), lakini si kwa kipindi cha siku 40 mfululizo!, na ni Marhamu iliyokuwa inapakwa na si Dawa!

Lakini swali ni kwanini leo katika Ukristo, sherehe hii imeingizwa kana kwamba ni sherehe ya kiimani?

Sherehe hii ya 40, ilikuja kubadilika kutoka katika kupaka dawa mwili wa marehemu mpaka kuadhimisha marehemu. ilikuja kuingizwa baada ya kundi dogo la watu ambao si wakristo, walipolilinganisha tukio la Bwana Yesu kuwatokea watu kwa siku 40, baada ya kufufuka kwake, na jinsi alivyopaa baada ya siku hizo 40.

Hivyo kwa kulinganisha huko wakazalisha hoja kwamba, mtu anapokufa roho yake kabla haijakwenda kuzimu au paradiso, inakuwa inazunguka na kuwatokea wengi kwa siku 40, na baada ya siku 40, ndipo aidha inapaa kwenda juu au inapelekwa chini kuzimu.

Hivyo kulingana na baadhi ya madhehebu wanaamini kuwa ndani ya hizo siku 40 baada ya kifo ndio wakati sahihi wa kuwaombea marehemu, ili waishie katika hatima nzuri, maana yake wasipoombewa katika hizo siku 40, basi kama marehemu alikufa katika dhambi basi hatakwenda mbinguni, bali motoni, na ndugu zake walio hai watakuwa hawajamfanyia wema.

Lakini je jambo hilo lina uhalisia wowote kibiblia?

Jibu ni la! Halina uhalisia wowote kibiblia, maandiko yanathibitisha kuwa mtu anapokufa, saa ile ile anashuka kuzimu kama amekufa katika dhambi, au anaingia paradiso kama amekufa katika haki (Soma Luka 16:22-23 na Waebrania 9:27). Hakuna siku 40 za mangojeo..Na Zaidi ya yote!, Bwana Yesu hakuwa Marehemu kipindi anawatokea watu kwa siku 40!, alikuwa tayari ameshafufuka na kuwa hai, wala hakuwa “Mzimu”.. Mizimu inabakisha mifupa yao makaburini, lakini Bwana Yesu hakukuwa na kitu kilichobaki katika kaburi lake Zaidi ya zile “SANDA!”.

Kwahiyo sherehe ya 40, ni ya kipagani!, wakristo hatupaswi kuiadhimisha, kwasababu Kristo hayupo katika hizo sherehe.

Sasa unaweza kuuliza, ikitokea umealikwa na ndugu wanaofanya sherehe hizo na wewe uhudhurie!..

Kama umealikwa na ndugu zako, ambao bado macho yao hayajafumbuliwa kulitambua hilo, unaweza kuhudhuria ila usishiriki hata kidogo ibada zao! (Kwasababu ni ibada za wafu), Na lengo la wewe kwenda kule isiwe kula!, bali liwe kuwahubiria na kuwaonesha pendo la Kristo! Katika hekima yote!!. Ili wanapotoka pale wamjue Kristo na uweza wake na ukweli kuhusu yatakayojiri baada ya kifo!..

Na vile vile wakristo hatuna ruhusa ya kufanya maziara katika makaburi ya Marehemu kwa lengo la kuwafanyia Ibada, kwamba kubadilisha hatima yao kule walipo!, au kupata baraka kutoka kwao!.. Hapana!. Tunapaswa kufanya maziara katika makaburi kwa lengo tu! La usafi!, na heshima yetu sisi tuliosalia, kuonesha ustaarabu wetu!, mbele za watu walio nje!.. Sawasawa tu na unavyofanya usafi katika viunga vyako na bustani zako, au uwanja wako.

Kwa maelezo marefu kuhusu nini kitatokea baada ya kifo, unaweza kufungua hapa >> Nini kitatokea baada ya kifo!

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Je! Karamu za ‘Idi’ ndio zipo hizo tunazozisoma katika Hosea (12:9)

CHAPA YA MNYAMA

LIPI TUNAJIFUNZA KWA WALIOMWONA YESU ALIYEFUFUKA?

Zeri ya Gileadi ni nini?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments