UNAFAHAMU KUWA YESU HUWA ANAJITENGA NA BAADHI YA WATU?

UNAFAHAMU KUWA YESU HUWA ANAJITENGA NA BAADHI YA WATU?

Nakusalimu katika jina la mwokozi wetu Yesu Kristo, utukufu na heshima vina yeye milele na milele amina.

Zipo tabia kadhaa za Yesu ambazo watu wengi huwa hatuzitambui. Kwamfano utakumbuka wakati ule, anakwenda Yerusalemu kwenye sikukuu, biblia inasema alipita mahali penye birika Fulani iliyojulikana kama Bethzatha, Birika hii kuna kipindi ilitoa uponyaji, hivyo, watu wengi maelfu kwa maelfu walikuwa wakikusanyika, kungojea bahati zao, ambayo ilitokea kwa nadra sana pengine mara moja kwa mwaka.

Lakini hapa tunamwona Bwana Yesu, akiingia katikati ya mkusanyiko huo, na kumponya Yule mtu aliyekuwa amepooza, Cha kushangaza ni kwamba Yesu hakuendelea kubaki mule mule kuwaponya watu wengine kama ilivyo desturi yake, bali aliondoka mara moja, kwa haraka ambayo hata aliyeponywa hakuweza kumkariri.

Hata baadaye makuhani walipomuuliza, ni nani kakupa amri hiyo ya kujitwika godoro lako uende, Yule aliyepooza hakuweza kumtambua,.

Lakini ni nini kilichompelekea Yesu aondoke pale?

Tusome kidogo;

Yohana 5:12  “Basi wakamwuliza, Yule aliyekuambia, Jitwike, uende, ni nani?

13  Lakini yule mtu aliyeponywa hakumjua ni nani; MAANA YESU ALIKUWA AMEJITENGA, KWA SABABU PALIKUWA NA WATU WENGI MAHALI PALE.

14  Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya HEKALU, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi.

15  Yule mtu akaenda zake, akawapasha habari Wayahudi ya kwamba ni Yesu aliyemfanya kuwa mzima.

Sababu ya kujitenga maandiko yanasema ni kwamba palikuwa na watu wengi.. Watu wengi ambao wanatafuta miujiza na uponyaji wa miili yao, na sio roho zao. Na ndio maana Yesu hakuweza kustahimili kuendelea kuwepo pale muda mrefu, akaondoa mara..

Mpaka Yule mtu alipopata akili, akaona pale sio sehemu yake, akaenda zake HEKALUNI kutulia uweponi mwa Bwana, kukaa kusali na kujifunza sheria za Mungu, Ndipo Yesu akajidhihirisha kwake alipokuwa kule hekaluni,..akamwambia “usitende dhambi tena!”, “usitende dhambi tena!”, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi”. Akampa siri ya matatizo yake, na suluhisho la kudumu.

Lakini kama mtu Yule asingekwenda hekaluni, badala yake akaendelea kumtafuta  Yesu kila siku pale birikani, kamwe asingekaa amwone, na ugonjwa wake ungemrudia muda si mrefu, kwasababu, angeenda kurudia dhambi yake ile ile aliyoitenda.

Ni nini Bwana anataka tufahamu.

Hii ni picha kamili ya kinachoendelea sasa katika ulimwengu wa wakristo. Kinachowakimbiza kwa Mungu ni ishara na miujiza, na uponyaji, Hivyo wanayaacha makanisa yanayowafundisha Njia za wokovu, na kujitenga na dhambi, wanakimbilia kwenye vituo vya maombi na maombezi, huko ndipo walipojazana, wakisikia kuna mafuta ya upako, wanamiminika mpaka wanakanyagana, Lakini ukweli ni kwamba sio wote wanaopokea uponyaji, bali ni wachache sana..na tena hao wachache ni Yesu ndiye anayewafuata huko kwa huruma zake, na kuwadhihirishia uponyaji wake.. Lakini huko hayupo..Utasubiri sana, na kulia sana, na kungoja sana.

Huwezi kuliacha Hekalu lake, ukakimbilia mikusanyiko ya miujiza na uponyaji, ambayo hukemewi dhambi, hufundishwi kusali, hufundishwi habari za kwenda mbinguni, hufundishwi utakatifu, ukadhani utamwona Yesu..Ataendelea tu kujitenga nawe kwasababu yeye hakai katika mikusanyiko ya watu wa namna hiyo.

Wanaoponywa wanakuwa wanarudiwa matatizo yaleyale, baada ya muda, kwasababu hawafundishwi chanzo cha matatizo yao, kwamba ni dhambi, Bali wanamgeuza Mungu mganga wa kienyeji, anayetoa tu dawa, hajali kujua machafu yako.

Embu leo tubu na ugeuke, ondoka huko, Usikae mahali ambapo Yesu hayupo, hata kama kuna utiriri wa watu, Yesu hapokei umati wa watu,kama tulivyoona hapo anapokea watu waliotayari kumwabudu katika roho na kweli haijalishi watakuwa wawili au watatu.

Epuka upepo wa watu, asilimia kubwa Yesu hayupo huko.

Tubu dhambi zako, maanisha kwa moyo wako wote, kumfuata Yesu. Kumbuka hizi ni siku za mwisho,  majira yale ya  makristo na manabii wa uongo ndio haya Yesu aliyoyatabiri, Kaa katika Kristo Yesu, hakikisha umejitwika msalaba wako na kumfuata Yeye. Parapanda inakaribia kulia, Hukumu ipo karibu, umejiwekaje na Kristo wako?.

Bwana akubariki

Amen.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

KUNA WAKATI YESU ATAPITA NA WATU HAWATAJUA.

JINSI YA KUPOKEA UPONYAJI, TUNAPOMWOMBA BWANA ATUGUSE MARA YA PILI.

USIJARIBU KUMGEUZA MUNGU MGANGA WA KIENYEJI,UTAKUFA.

Kwanini wanawake wengi huwa wanalipuka mapepo?

Nini maana ya msiwe waalimu wengi (Yakobo 1:3)

Usimwache mwanamke mchawi kuishi! Biblia ilimaanisha nini?

Afadhali mtu akutwe na dubu aliyenyang’anywa watoto wake.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments