JE UMEJIFUNZA ULE WIMBO MPYA?

JE UMEJIFUNZA ULE WIMBO MPYA?

Nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo, Tukijua kuwa ule mwisho unakaribia, hatuna budi siku baada ya siku tujichunguze je! Tumekamilika vema? ili siku ile tusionekane na mawaa mbele zake. Tulipokee taji timilifu tuliloandaliwa mbinguni na mwokozi wetu Yesu Kristo kwa neema zake.

Leo, napenda tufahamu juu ya wimbo mpya. Kama wewe ni msomaji mzuri wa kitabu cha Ufunuo. Utagundua zimetajwa nyimbo kuu tatu.

  1. Wimbo wa Musa
  2. Wimbo wa Mwanakondoo
  3. Wimbo mpya

Swali ni je! Hizi nyimbo ni zipi na zinatimiaje?

Wimbo wa Musa na wa mwanakondoo tunazisoma, katika Ufunuo 15:2-3

Ufunuo 15:2  Tena nikaona kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto, na wale wenye kushinda, watokao kwa yule mnyama, na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake, walikuwa wamesimama kando-kando ya hiyo bahari ya kioo, wenye vinubi vya Mungu.

3  Nao WAUIMBA WIMBO WA MUSA, MTUMWA WA MUNGU, NA WIMBO WA MWANA-KONDOO, wakisema, Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa

Wimbo wa Musa, ni injili ya Musa, ambayo iliwafanya watu wa kale, kutembea katika hiyo ili wamkaribie Mungu, ndiyo ile torati, ambayo wale waliokuwa katika agano la Ibrahimu kwa uzao, walirithi neema hiyo. Hivyo wana wa Israeli wote walikuwa wanauimba wimbo wa Musa. Yoyote ambaye hakuwa hana wimbo huo, basi wokovu au kumkaribia Mungu hakukuwezekana kwake.

Lakini wimbo wa Musa haukuwa na ukamilifu wote kwasababu ulikuwa ni wa mwilini, na wa kutarajia ahadi ya mwokozi mbeleni. Hivyo Mungu akaleta wimbo mwingine mpya kwa wanadamu wote. Ndio huo wimbo wa mwana-kondoo.

Ambayo ni injili ya neema iliyoletwa na Bwana wetu Yesu Kristo na kuhubiriwa na mitume wake. Kwa ufupi sisi wote tuliomwamini Yesu Kristo katika agano hili jipya, kwa pamoja tunauimba wimbo wa mwana-kondoo. Ndio maana kiini cha imani, na wokovu wetu ni Yesu Kristo. Mtu yeyote ambaye hajaoshwa dhambi zake kwa damu ya Yesu, hawezi kumwona Mungu, wala kamwe hataweza kumwelewa, haijalishi ataonyesha bidii zake nyingi kiasi gani. Kwasababu ndio utimilifu wote.

Lakini upo wimbo mwingine wa Tatu ndio huo wimbo mpya.

Wimbo huu, si wote watakaoweza kuuimba, lakini watakaoweza kuuimba watakuwa karibu sana na mwana-kondoo (Yesu Kristo), baada ya maisha haya. Ndio wale washindao, Ndio wale Yesu aliosema atawakiri mbele ya Baba na malaika zake, ndio wale watakaoketi pamoja naye katika viti vya enzi, ndio wale watakaotoka mashariki, magharibi, kaskazini na kusini, kula mkate naye mezani pake. Na vigezo amevianisha pale. Anasema..

Ufunuo 14:1  Kisha nikaona, na tazama, huyo Mwana-Kondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, na watu mia na arobaini na nne elfu pamoja naye, wenye jina lake na jina la Baba yake limeandikwa katika vipaji vya nyuso zao.

2  Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni, kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi kuu. Na hiyo sauti niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi, wakivipiga vinubi vyao;

3  na KUIMBA WIMBO MPYA mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele ya wale wenye uhai wanne, na wale wazee; WALA HAPANA MTU ALIYEWEZA KUJIFUNZA WIMBO ULE, ila wale mia na arobaini na nne elfu, WALIONUNULIWA KATIKA NCHI.

4  HAWA NDIO WASIOTIWA UNAJISI PAMOJA NA WANAWAKE, KWA MAANA NI BIKIRA. Hawa ndio wamfuatao Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo.

5  NA KATIKA VINYWA VYAO HAUKUONEKANA UONGO. MAANA HAWANA MAWAA

Kama tunavyoweza kuona hapo tabia za wale walioweza kuuimba wimbo huo ni mbili;

  1. Hawakutiwa unajisi na wanawake.

Hapo hamaanishi kuwa hawakuwa wazinzi, hapana, (ni kweli uzinzi sio jambo lao) bali anamaanisha hasaa uzinzi wa rohoni, yaani Kumwabudu Mungu pamoja na sanamu. Na sanamu kwa wakati wetu si tu vile vinyago vya kuchonga tu, bali pia ni kitu chochote kinachochukua nafasi ya Mungu wako moyoni. Wengine mali, wengine tv,  wengine mipira, wengine elimu, wengine ma-magemu, wengine ushirikina, wengine udhehebu. Hizo ni sanamu, unapozidhibiti wewe kama mkristo hiyo ni hatua mojawapo ya kuweza kuuimba wimbo huo mpya.

Lakini anasema..

  1. Katika vinywa vyao haukuonekana uongo, maana hawana mawaa.

Ni watu walionena kweli yote ya  Mungu (injili ya Kristo), wala hawakuibatilisha kwa ajili ya fedha, au maslahi, au cheo, au unafki au wafuasi. Bali waliitetea kweli yote ya Mungu na kuiishi pia, . Maana yake mimi na wewe tukiinena kweli ya Kristo na kuiishi, basi vinywani mwetu tunakuwa hatuna uongo.

Na matokeo ya mtu wa jinsi hii, ni kwamba anakuwa nafasi maalumu sana mbinguni(Ufunuo 5:8-9), Ni sawa na leo unajisikiaje unapoitwa uishi ikulu na raisi wako? Unajisikiaje kila mahali aendapo na msafara wake wewe upo pamoja naye. Anapopokea heshimu, na wewe unapokea naye.

Hivyo bidii ina malipo. Nyakati tulizonazo sio kusema nimeokoka hiyo inatosha!.. Ni nyakati za kujifunza wimbo huu mpya kwa bidii. Kutijahidi kumpendeza Bwana. Na yeye mwenyewe ameahidi neema yake itatusaidia.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

KARAMU YA MWANA-KONDOO.

JE! NI DHAMBI KUIMBA WIMBO WA TAIFA?

Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule(Kutoka 12:4)

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments