NI WAPI PA KUONGOZWA NA ROHO, NA WAPI NI WAJIBU WANGU?

NI WAPI PA KUONGOZWA NA ROHO, NA WAPI NI WAJIBU WANGU?

Fahamu mambo ambayo ni wajibu wako kufanya, na yale ambayo unapaswa umsubiri kwanza Roho Mtakatifu akuongoze.

Kama mkristo ni vizuri kuweza kutofautisha mambo ambayo ni wajibu wako kuyafanya, na mambo ambayo utahitaji kwanza uongozwe na Roho Mtakatifu kuyafanya. Ukishindwa kutambua yaliyo wajibu wako, kisha ukasubiri Roho akuongoze, utapotea, halikadhalika ukishindwa kutambua yale ambayo utapaswa usubiri Roho akuongozwe ukayafanya kwa matakwa yako,vilevile utajikuta unapata hasara.

Hivyo haya ni baadhi ya mambo ambayo Mungu anaona ni wajibu wako, na unapaswa uyafanye, na haya usitazamie Bwana atakufunulia uyafanye.  Ni mfano tu wa baadhi ya mambo ya mwilini, kwa mfano hakuna mtu anayeweza kusubiri afuatwe na Mungu na kuambiwa ale chakula ndio ale, au anywe maji ndipo anywe, hapana, ni wewe tu mwenyewe utaona unahisi njaa, na hivyo utatafuta kila namna ya kupata chakula na utakula, wala hutamlaumu Mungu kwanini hakumfunulia juu ya chakula . Vivyo hivyo na baadhi ya mambo ya kiroho.

Haya ni mambo ya kuzingatia kuyafanya pindi tu uokokapo kwa maendeleo yako bora ya kiroho.

Kuomba: Maombi hayaepukiki kwa mwamini yoyote, wapo watu wanasema siwezi kuomba bila kuongozwa na Mungu. Ndugu Maombi hayahitaji kuongozwa, yanahitaji kujiongoza kwanza. Kuomba ni lazima iwe desturi yako kila siku, na kiwango cha chini Bwana alichotoa kwa kila mwaminio ni SAA 1.

Mathayo 26:40  Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? 41  Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.

Hivyo tangu sasa zingatia kujiwekea utaratibu huu, vinginevyo maisha yako ya wokovu yatakuwa ni mazito sana kuyaishi.

1) Kusoma Neno: Neno ndio chakula chetu cha rohoni, kwasababu Bwana alisema, mtu hataishi kwa mkate tu, bali kwa Neno lake. Kama hutajiwekea ustaarabu ya kutenga muda wako kila siku wa kuyatafakari maandiko, ukasubiri ipo siku Bwana ataanza kukufunulia uanze kusoma kitabu gani, na gani..Utapotea ndugu yangu. Hii njaa ya kiroho tuliyonayo siku hizi za mwisho, tutasubiri kweli, tuletewe chakula mdomoni?. Ni sisi wenyewe kuchangamka kusoma biblia daima, haijalishi wewe ni mchungaji umesoma biblia yote mara saba, au umeokoka leo,wote tunapaswa tuwe watu wa kusoma na kujifunza Biblia.

2) Mifungo ya mara kwa mara: Tunaposema mifungo ya mara kwa mara tunamaanisha ile mifungo ambayo, kila mmoja anaweza kuistahimili, ya saa 24, au siku mbili, au tatu, bila kula. Mifungo inakurahisishia wigo wako wa kimaombi, na kuivuta roho yako juu, ili iweze kukutana na uso wa Mungu kirahisi. Kwahiyo usingoje, kusikia sauti Fulani ikuambie anza kufunga. Anza kujijengea utaratibu huo wewe mwenyewe, walau kila mwezi uhesabu kuna siku kadhaa umefunga.

3) Ibada: Halikadhalika ukikoka, usisubiri Bwana akuambie nenda kanisani ukaniabudu. Au anza kuniimbia sifa. Ni wajibu wako, ‘kumvukizia’ Mungu wako uvumba wa shukrani, sifa, matoleo, nyimbo, ushirika wa  meza yake n.k. mara nyingi kwa jinsi uwezavyo. Wengine watasema ipo changamoto ya makanisa, ndio hiyo isiwe sababu ya kutulia tu nyumbani, nenda kwingine, pakiwa pabaya tafuta kwingine, hatimaye Mungu ataiona nia yako, na kukupa mahali sahihi pa kutuliza moyo wako. Maana kila atafutaye huona.

4) Kushuhudia habari za Yesu kwa wengine: Kuwaeleza wengine Habari za Yesu, ni wajibu wetu sote, aidha umeokoka leo, au umekomaa kiroho.  Kushuhudia haihitaji ujuzi mwingi wa kimaandiko kama wengi wanavyodhani, hata kueleza uzuri wa Kristo na ushuhuda wako kwa mwingine tayari ni injili hiyo.. Paulo alipookoka, tu baada ya kubatizwa hapo hapo akaanza kuwaeleza wengine habari za Yesu na uchanga wake wote.

Matendo 9:18 “ Mara vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama, akabatizwa;19  akala chakula, na kupata nguvu. Akawa huko siku kadha wa kadha pamoja na wanafunzi walioko Dameski.20  Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu.21  Na wote waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu aliyewaharibu walioliitia Jina hili huko Yerusalemu? Na hapa alikuwa amekuja kwa kusudi hilo, awafunge na kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani?”

HAYA NI MAMBO AMBAYO UNAPASWA USUBIRI, UONGOZWE NA ROHO

1) Kuanza huduma: Huduma ni kama kituo rasmi cha kuwasaidia watu kiroho, kwa ule wito uliowekewa na Mungu ndani yako. Na hapa, ni kuwa makini sana, kwasababu mtu akishaona amekoka, au anayo-karama Fulani, anachowaza ni kwenda kuanza kanisa, au akishajiona anao-ushawishi Fulani wa kuwakusanya watu anakwenda kuanza huduma. Ndugu hiyo ni hatari. Chukua mfano rahisi, leo hii wapo watu ambao wanaujuzi Fulani, labda tuseme wajenzi, lakini kama hawana elimu ya shuleni iliyothibitishwa hawawezi kupewa usimamizi wa majengo makubwa wayasimamie, kwasababu wanajua hata kama watakuwa wanaelewa aina nyingi za michanga na matofali, lakini bado kuna mambo watayakosa tu, ya ndani yahusuyo ujenzi, ambayo yanapatikana darasani tu, na hivyo kuna hatari ya kupata hasara kubwa mbeleni kwa mtu kama huyo kupewa usimamizi.

Halikadhalika, Mungu kumuita mtu katika huduma, si jambo atakalolikurupukia, bali atakuandaa, kwa kipindi Fulani katika shule yake ya Roho Mtakatifu (hatulengi shule ya vyuo vya biblia). Na hivyo, mwishoni kabisa ndio atakuita ufanye jambo ili isiwe hasara kwa watu wake.  Kwahiyo usiwe mwepesi wa kutaka kuanza jambo, kuwa mshuhudiaji, huku ukiwa chini ya uangalizi . Mtume Paulo japokuwa alikuwa anashuhudia habari za Kristo kwa ushujaa mwingi lakini alisubiri kwanza mpaka wakati wa Bwana.

Matendo 13:2  “Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. 3  Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao. 4  Basi watu hao, wakiisha kupelekwa na Roho Mtakatifu wakatelemkia Seleukia, na kutoka huko wakasafiri baharini hata Kipro”

2) Mifungo mirefu: Ipo mifungo ya kutokula na kunywa kwa kipindi kirefu kama wiki 2, mwezi, siku 40 n.k. Katika hali kama hizi, usijiamulie tu mwenyewe kwa akili yako kuiingia. Unawezi  kupata matatizo au kifo kabisa. Kwasababu hiyo inahitaji ROHO wa Mungu kukuongoza. Ndivyo ilivyokuwa kwa Bwana Yesu.. aliongozwa na Roho, hakujiamulia tu kuanza mifungo hiyo.

Luka 4:1  “Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, 2  akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa”

Hivyo zingatia haya, na Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

3) Unayefanya naye mapatano, au maagano: Maagano/mapatano yapo ya namna mbalimbali, yapo ya kipindi kifupi na mengine ya maisha, mfano, unapotaka kuingia katika ndoa, huna budi kumshirikisha Roho Mtakatifu, akupe mwongozo wake, ndio hapo inakugharimu utangulize maombi. Unapochagua viongozi wa kusimamia kundi, hupaswi kuwaza kwa akili zako, bali jipe muda wa Roho Mtakatifu kukufunulia. Ilimpasa Bwana afunge usiku kucha kuomba mwongozo wa wanafunzi wa kutembea nao. Unapotaka kutumika na mtu, usiyemjua chukua muda wa kumuuliza Roho Mtakatifu. kwasababu yapo makosa mengi ambayo hata katika maandiko yalitokea kwa kukosa kumshirikisha Mungu kwanza. Wakati fulani mfalme Yehoshafati alitaka kutumika na mfalme Ahabu, na ilikuwa nusu afe, kwasababu alifanya mapatano na mfalme mwovu.(2Nyakati 18:1-25)

Yoshua aliingia katika mapatano na maadui zake, ambao Bwana alimwambia awaangamize, na ndio hao wakaja kuwa mwiba kwa wayahudi baadaye. Hiyo yote ni kwasababu hawakuwa tayari kumsikiliza kwanza Roho Mtakatifu. Hivyo jambo lolote la kiroho, ambao unaona linahitaji umakini mkubwa, subiri kwanza uongozo wa Roho Mtakatifu. Usiangalie, zawadi, uzuri, utajiri, au chochote. (Yoshua 9:1-27)

Bwana akubariki.

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mada Nyinginezo:

ANDALIZI LA MWISHO LA UJIO WA MPINGA KRISTO.

Pale mwanandoa mmoja anaposhindwa kutimiza wajibu wake ufanyaje?

Aina za dhambi

AMEFANYIKA BORA KUPITA MALAIKA!

REKEBISHA YAFUATAYO ILI UCHUMI WAKO UKAE SAWA.

Roho Mtakatifu ni nani?.

IMESALIA RAHA YA SABATO KWA WATU WA MUNGU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments