Tujifunze siri mojawapo iliyopelekea habari za Bwana wetu Yesu Kristo kuenea kwa mafanikio makubwa sana ndani ya kipindi kifupi. Tunaweza kudhani kujisifia kwetu mbele za watu, au kuonyesha wema wetu mbele ya macho ya watu wengi kutatusaidia kuongeza umaarufu wetu, Utamwona mtu mfano ametoa msaada kidogo tu, au kamsaidia mtu kwa kitu kidogo,atatangaza kila mahali, na watu wote watajua kuwa yeye ndiye aliyefanya lile jambo.
Lakini embu tuangalie mbinu Yesu aliyoitumia. Nasi tupate kitu hapo kitakachotusaidia katika huduma zetu , na shughuli zetu tuzifanyazo kila siku, na mambo mengine yote.
Marko 1:40 “Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa.
41 Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika.
42 Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika.
43 AKAMKATAZA KWA NGUVU, akamwondoa mara,
44 akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao.
45 LAKINI AKATOKA, AKAANZA KUHUBIRI MANENO MENGI, NA KULITANGAZA LILE NENO, HATA YESU ASIWEZE TENA KUINGIA MJINI KWA WAZI; bali alikuwako nje mahali pasipokuwana watu, wakamwendea kutoka kila mahali”.
Unaona, sio kwenye habari hiyo tu peke yake alimzuia yule mtu asimtangaze, lakini kila mahali alipofanya miujiza yake alitumia kanuni hiyo hiyo, sio kana kwamba hakutaka UTUKUFU au habari zake zisienee kila mahali hapana! badala yake alifahamu kuwa “kumbe kumzuia mtu asikutangaze ndio kumruhusu atangaze”..
Marko 7:34 “akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka. Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri. AKAWAONYA WASIMWAMBIE MTU; LAKINI KADIRI YA ALIVYOZIDI KUWAAGIZA, NDIVYO WALIVYOZIDI KUTANGAZA HABARI; wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme”
Tukitaka sifa zetu zienee katika nyanja yoyote ile maishani iwe ni katika Utumishi, au shughuli zetu, au chochote kile tukifanyacho, tuhakikishe tunatoa kilicho bora kwanza, kisha tukae kimya, tusijikweze, tukatae kutukuzwa tukuzwa na watu, Kwa kufanya hivyo ndio tutasifiwa, yule yule aliyekipokea ndiye atakayekisambaza kwa nguvu kuliko hata wewe unavyodhani..Hiyo ndio ilikuwa kanuni ya Bwana..alisema “ajikwezaye atashushwa na ajishushaye atakwezwa”…Kwahiyo yeye mwenyewe alijishusha ili akwezwe.
Hali kadhalika mara nyingine Tunamwomba Mungu jambo kubwa, na huku tunatazamia jibu kubwa kutoka kwake. Tunamwomba Mungu atupe labda tuchukue mfano wa Gari, tunamwomba atupe gari, lakini kwa bahati mbaya haliji gari inakuja baiskeli tunaweza tukasema sio Mungu lakini tusipojifunza kanuni za Mungu kibiblia tunaweza tukakosa shabaha ya kupokea majibu yetu.
Embu mtafakari Eliya jinsi alivyofanya alimwomba Mungu mvua kubwa ya kutosha itakayoinyeshea nchi kame ya Israeli iliyokaa zaidi ya miaka 3 bila kupata hata tone moja la maji, lakini alipoomba kwa nguvu nyingi na kwa bidii mara 7 huku akitazamia kuona wingu zito jeusi, likitokea mashariki, lakini badala yake kilizuka kiwingu kidogo kama mkono wa mtoto mchanga. Lakini Kwa imani yeye alipoona vile hakushtuka kusema kuwa Mungu hajanisikia, kiwingu kile sio cha mvua, bali kijiupepo tu kimeuvumisha, badala yake alipokea vile vile katika udogo ule kwa Imani, na kuondoka mahali pale, lakini biblia inasema ghafla wingu zito likatanda juu ya nchi,na mvua kubwa sana ikanyesha.
Usidharau udogo wa majibu utokao Kwa Bwana juu yako, “usiidharau siku ya mambo madogo”…Ulimwomba nyumba kwa muda mrefu lakini umejikuta unapata pikipiki kwa sasa, usiseme Mungu hajakusikia pokea hiyo kwa Imani na kwa shukrani ukijua kuwa Mungu alishakusikia ulichomwomba na ghafla hiyo pikipiki moja itazaa nyumba 5 kwa muda mfupi sana usioutazamia…
Lakini pia usisahau, duniani sisi ni wapitaji tu! Hatujaitiwa kupata majumba, wala magari, wala mashamba…hayo ni ya muda tu! Pindi tukiwapo hapa duniani na yote yanapita…lakini tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya kama maandiko yanavyosema (2 Petro 3:13), mbinguni ndio kwetu, Hivyo Kila siku ni wajibu wetu, kutazama usalama wa roho zetu zaidi ya vitu vyetu tunavyomiliki. Kwasababu Biblia inasema
“ Uzima wa Mtu haupo katika wingi wa vitu tulivyonavyo Luka 12:15” na tena inasema “itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake Marko 8:36”
Bwana akubariki sana. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
About the author