BASI, JIANGALIENI MIOYO YENU ISIJE IKALEMEWA NA ULAFI, NA ULEVI.

BASI, JIANGALIENI MIOYO YENU ISIJE IKALEMEWA NA ULAFI, NA ULEVI.

Luka 21:34 “Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo;

35 kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima”

Shalom, Jina kuu la mwokozi wetu Yesu libarikiwe daima.

Wengi tunayafahamu maneno hayo ya Bwana, lakini hatujui ni ulevi na ulafi wa namna gani unaozungumziwa katika Habari hiyo mpaka siku hiyo iwajilie ghafla, kama mtego unasavyo..

Ili kupata picha embu tutazame mfano mmoja halisi kabisa wa kwenye biblia na jinsi walivyolemewa na ulafi na ulevi wa kipekee mpaka, mwisho wao ulipowakuta kwa ghafla..

Sasa kama tukisoma kile kitabu cha Danieli sura ya 5, tunamwona mfalme mmoja aliyejulikana kwa jina la Belshaza, huyu alikuwa ni mtoto wa Nebukadreza, kama wengi tunavyoifahamu Habari, ni mtu ambaye alibahatika kuona mambo yote ambayo Baba yake aliyoyapita na jinsi alivyoadhibiwa kutokana kiburi chake na ukatili wa kutesa watu wasiokuwa na hatia na wengine kuwatupa katika matanuru ya moto, kama sio kuwachinja, lakini baadaye Mungu alikikomesha kiburi chake, kwa kumng’oa katika ufalme wake, akawa anaishi misituni kama sokwe Fulani tu, mpaka miaka 7 ilipoisha, na pale alipogundua kuwa Mungu ndiye anayetawala dunia nzima, na kwamba yeye ndio anatakiwa aogopwe ndipo akatubu na kumgeukia Mungu na Mungu akamrehemu na akamrejeshea enzi yake kupita kiasi hata kuliko pale alipokuwepo mwanzo.

Sasa huyu mtoto wake aliyeitwa Belshaza, alikuwa anayaona hayo yote, na alikuwa ameshapata somo kamili ambalo haikumpasa yeye tena alipitie kwasababu babayake tayari ameshafanyika mfano..Kama tu vile sisi, watu wa kizazi hiki, tayari mifano mingi ilishatangulia mbele yetu huko nyuma, mfano ile ya watu wa Nuhu, na Watu wa sodoma na Gomora, jinsi walivyoangamizwa kwa maovu yao, lakini sasa tunaona na kuzipuuzia, na kuzichukulia tu kama Habari zilizopitwa na wakati kama tu huyu mtoto wa Nebukadreza.

Yeye alipuuzia yale yote ambayo Baba yake aliyotendewa na Mungu.. Na kibaya Zaidi akaamua kuchukua hatua nyingine mbaya kuliko zote, ambayo ndiyo iliyompelekea hata Mungu kumwangamiza kwa ghafla na kwa haraka sana..Na hicho ndicho wote tunachopaswa tujifunze leo hii.

Alichofanya ni kuchukua vile vyombo vya hekaluni, ambavyo baba yake alivichukua kutoka Yerusalemu, alipouteketeza mji na hekalu, na kuvihifadhi asivitumie kwa kitu chochote kwasababu vilikuwa ni vitakatifu, lakini yeye (huyu Belshaza), akawa mlevi, na mlafi wa kupindukia, akawa anafanya karamu, akaona kuwa haitoshi kunywea vyombo vyake mwenyewe, chupa zake za vilabu vyake, na kutumia visu vyake vya kifalme kuchinjia nyama zake, na hata sahani zake akaona hazitoshi kuzitumia kuwekea vyakula vyake haramu…

hivyo akaenda kwenye hazina ya baba yake, na kupekua pekua na kuvikuta vile vyombo vya hekaluni ambavyo vilikuwa vimefunga na kuhifadhiwa visitumike, yeye akavichukua vile vyombo vitakatifu vya Mungu, akaanza kuvinywea na kuvilia yeye Pamoja na wakuu wake, na makahaba wake..Unaweza kuona Ni uvunjifu wa heshima kiasi gani.?? Hayo ndio mambo yanayoendelea katika roho sasa hivi..

Na alipomaliza kufanya vile tu, saa hiyo hiyo kiganja cha mkono kikatokea, kikasogea mpaka ukutani mahali ambapo mwanga ulikuwa unapiga, akaona kikiandika maneno yale, MENE, MENE, TEKELI NA PERESI.. Kama tunavyoijua habari maneno yale yalikuwa ni Hukumu, kwamba mwisho wake umeshafika, ufalme wake ndio umeishia pale..

Sasa huyu Belshaza, utaona tena aliposikia vile badala atubu, ndio kwanza anafikiria kumpandisha Danieli cheo, na kumfanya awe mkuu, unajua ni kwanini?.. Ni kwasababu alidhani, jambo hilo haliwezekani kutokea kwake, na hata kama likiwezekana basi litakuwa ni jambo la baadaye sana, kwasababu mji wake wote ameshauzungushiwa kuta kubwa sana pande zote, ambazo juu yake wapo walinzi wamekaa wakiangalia malango yake usiku na mchana yenye askari waliobebea wenye sifa dunia nzima, (kwasababu kipindi hicho Babeli ndio iliyokuwa inatawala dunia nzima)..

Hivyo Habari hizo za Danieli hazikumwogopesha hata kidogo, akiangalia kuwa hayo mataifa ambayo ameambiwa yatakuja kuuchukua ufalme wake, yaani umedi na uajemi ni vitaifa vidogo, visivyokuwa na nguvu, hivyo akawa hana hofu tena..

Lakini ndivyo alivyojidanganya..Biblia inasema usiku ule ule, alivamiwa na kuuliwa, na ufalme wake kuchukuliwa kirahisi na Wamedi na Waajemi, ni jambo la ghafla sana..utajiuliza wale watu walitokea wapi asipate Habari siku zote..

Ili kufahamu ukirudi katika historia inasema, ule mji wa Babeli ulikuwa na mto mkubwa ambao ulikuwa unaingiza maji katika mji, sasa kwa namna ya kawaida, maji yanayoingia katika mji hayawezi kuwekewa kuta, hivyo pale pale kwenye maingilio ya mto ule ndipo hapo hapo Wamedi walipokuja kuingilia usiku ule, walichokifanya ni kuupindisha ule mto mbali sana hivyo maji yakapungua ndipo walipopatia nafasi ya kuuingia mji, na kuwaua watu wale kwa ghafla sana na haraka usiku ule..wakati walinzi wa mji wanaendelea kulinda mageti makubwa kule..kumbe huku kwa njia ya chini ya watu wameshaingia mjini na kuanza kuangamiza watu.

Hata leo, Kanisa la sasa limeshalemewa na ulafi na ULEVI WA ROHONI, ni heri ungekuwa ni ulevi wa kawaida, lakini ni ulevi unaotumia vyombo vya hekaluni mwa Bwana na hiyo ndiyo inayoleta ghadhabu.. Yaani watu wanapomchanganya MUNGU NA DUNIA..leo wapo kanisani, kesho disko, leo wanamwimbia Mungu, kesho shetani, leo wanashiriki meza ya Bwana, kesho wanakwenda kuzini, yaani hayo yamekuwa mambo ya kawaida kabisa, mtu kusema ameokoka, na huku, anakunywa pombe kisirisiri, anazini nje ya ndoa, anajichua, anatazama picha za ngono ni mambo ya kawaida, anakula rushwa, ana honga..

Huo ndio ulevi na ulafi Bwana Yesu aliokuwa anauzungumzia pale..

Luka 21:34 “Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo;

35 kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima”

Moja ya hizi siku, dunia nzima itaingia katika mtego huo, wakati watu wakiwa katika vilele vya amani, katika furaha, ndipo mambo yatakapobadilika kwa ghafla. Hivyo ndugu, huu ni wakati wa kutengeneza uhusiano binafsi na Mungu..Dunia hii imeshaandikiwa MENE, MENE, TEKELI na PERESI..Ukizidi kung’ang’ania kwenda nao, mwisho wa siku itakuchukua kama ilivyomchukua Belshaza, Leo hii tubu itii injili, uokolewa, Usafishwa Maisha yako, Na Bwana atakusaidia kwa yale yaliyobakia.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

VIUNO VYENU VIWE VIMEFUNGWA NA TAA ZENU ZIWE ZINAWAKA

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

RABI, UNAKAA WAPI?

KUSUDI LA MIMI KUWEPO DUNIANI NI LIPI?

ANGALIA USIJE UKANG’OA NGANO KATIKATI YA MAGUGU.

MUNGU AKIKUPITA LEO, HAIMAANISHI KUWA HAJAKUCHAGUA.

HATA NA BARNABA PIA AKACHUKULIWA NA UNAFIKI WAO!!

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
4 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
2 years ago

Amen

grasiano mlelwa
grasiano mlelwa
3 years ago

Naomba kutumiwa masomo zaidi…