Agano jipya ni nini?

Agano jipya ni nini?

Agano jipya ni nini?


Tukitamka neno “agano jipya”  tunathibitisha kuwa lilishawahi kuwepo agano la zamani (La kale) hapo kabla.

Hivyo ili kufahamu agano jipya ni nini, ni vizuri kwanza ukapata msingi wa agano la Kale, lilikuwaje.

Kama tunavyojua Biblia imeundwa na maagano makuu wawili, yaani jipya na la kale.

  1. Agano la Kale:

Sasa msingi wa agano la kale ulitoka kwa mtu mmoja aliyeitwa Ibrahimu. Mungu alipomuita hakumuita ilimradi tu, bali aliingia agano naye akamwambia atambariki na kumfanya kuwa baba wa mataifa mengi, ikiwa tu atakuwa mkamilifu na atakwenda  katika njia zake..Tusome.

Mwanzo 17:1 “Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, Bwana akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu. 

2 Nami nitafanya agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana sana. 

3 Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema, 

4 Mimi, agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi, 

5 wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi. 

6 Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako. 

7 Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako. 

8 Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao. 

9 Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada. yako. 

10 Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa. 

11 Mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na ninyi”.

Unaona, Jinsi Mungu alivyokuwa mwaminifu, baadaye Mungu akaja kumtimizia kweli agano aliliomuahidia, kwa jinsi uzao wake ulivyokuwa unaongezeka duniani kwa kasi, Lakini wakati huo wote uzao wake ulikuwa haumjui Mungu vizuri, ulikuwa bado haujajua kanuni za agano hilo ambalo Mungu aliloingia na Ibrahimu baba yao linavyopaswa liwe..

Ndio hapo wakiwa kule jangwani sasa Mungu anamtumia Musa kusema nao na kuwapa sheria na amri za kuzishika ili wafanikiwe..

Sheria hizo ndizo zilizoandikwa katika vitabu vya Torati: yaani

  • Mwanzo
  • Kutoka
  • Hesabu
  • Mambo ya Walawi
  • Kumbukumbu la Torati.

Hivyo vitabu hivyo vitano vilikamilisha Sheria yote ya Agano hilo ambalo Mungu aliingia na Ibrahimu.

Lakini hiyo peke yake haikuwa inatosha wana wa Israeli kumfahamu Mungu katika ukamilifu wote, Hivyo ilipasa  Mungu azungumze nao mara kwa mara kupitia watu mbalimbali wakamilifu na manabii wake.. Mfano tunamwona mtu kama Ayubu, Esta, Ruthu, kwa kupitia maisha ya hawa Mungu aliwafundisha wana wa Israeli jinsi ya kuishi katika njia zake. Vilevile akawa anasema nao mara kwa mara kupitia manabii wake wengi na waamuzi na mfano Samweli, Isaya, Yeremia, Danieli, Yona,Malaki N.k.

Hivyo kwa kupitia hao pia, na vitabu vyao walivyoviandika, iliwasaidia wana wa Israeli walishike na kulikumbuka agano ambalo aliingia nao zamani.

Kwahiyo tunapovisoma vitabu 39 vya Agano la Kale,.. tunafahamu kuwa ni jumuisho la sheria zote na kanuni zote za Mungu kwa wale alioingia nao agano kupitia Ibrahimu.

Sasa mpaka hapo umeshapata msingi wa Agano la kale kwa ufupi lilipoanzia..


      2.  Tukirudi kwenye agano jipya..

Hilo ni agano lingine lili bora zaidi kuliko lile la Ibrahimu.,

Hili nalo  Mungu aliingia katika agano na mtu mmoja tu, kama vile alivyoingia na Ibrahimu.. Na mtu huyo si mwingine zaidi ya YESU KRISTO.

Ibrahimu alipewa tu uzao wake wa kimwili, lakini huyu alipewa uzao wa wote wenye mwili wakimwamini tu kwa kuzaliwa mara ya pili.

Na ndio maana kuna umuhimu wa kila mmoja wetu kuzaliwa mara ya pili ili tufanyike kuwa uzao wake. yeye mwenyewe alisema..

Yohana 3:3  “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu”.

Na kubatizwa kwetu ndio ishara ya tohara yenyewe ya rohoni kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu na watoto wake wote walipotahiriwa kwa kutolewa magovi. Vivyo hivyo na sisi tunapaswa tukabatizwe kama ishara ya kutahiriwa mioyo yetu.

Lakini tukishazaliwa mara ya pili, hilo tu peke yake haitoshi, ni sharti pia tujue kanuni, na amri Mungu anazozitaka za agano hili ili tuweze kudumu ndani yake. Kama Uzao wa Ibrahimu ulivyopewa.

Hapo ndipo vitabu vya Injili ya Yesu Kristo, na vile  vya mitume, viliandikwa kwa ajili yetu ili sisi sote tutakapovisoma na kuvishika basi tuweze kudumu na kuimarika katika hilo agano jipya la Damu ya Yesu Kristo.

Ndipo hapo tunakutana na vitabu 27 vya agano jipya.

Hivyo kwa kwa hitimisho fupi.. Agano jipya ni agano Mungu aliloingia na Yesu pamoja na uzao wake wote. Ambao mimi na wewe tunahesabiwa katika uzao huo  kwa kumwamini Yesu na kubatizwa.

Tukifanikiwa kufanya hivyo basi na baraka zote, Mungu alizomuahidia Yesu Kristo, na sisi sote pia tunazishiriki na kuzirithi, ikiwemo uzima wa milele.

Bwana akubariki.

Je! Na wewe upo ndani ya agano jipya? Kama bado basi fanya hima ukaribishe Yesu leo ndani ya maisha yako akuokoe ufanyike uzao wa kifalme. Kumbuka hii ni neema ambayo sisi watu wa mataifa hatukustahili, hivyo uiichezee hata kidogo..

1Petro 2:9  “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; 10  ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema”.

Haleluya.

Mada Nyinginezo:

TOBA IGUSAYO MOYO WA BWANA.

Je! habari ya Yusufu, inabeba ujumbe gani kwa agano jipya?

Bwana aliposema “sikuja kutangua torati bali kuitimiliza” alikuwa anamaanisha nini?

UTIMILIFU WA TORATI.

TAZAMA, MWISRAELI KWELI KWELI, HAMNA HILA NDANI YAKE!

Sanduku la Agano lilikuwa linawakilisha nini katika Agano jipya?

KUTAHIRIWA KIBIBLIA

MWAKA WA BWANA ULIOKUBALIWA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments