USICHOKE KUNGOJEA, WALA USIKATISHWE TAMAA.

USICHOKE KUNGOJEA, WALA USIKATISHWE TAMAA.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima, Nakukaribisha tena tuyatafakari maneno ya uzima.

Leo tutatazama kwa ufupi Habari ya watu wawili. Wakwanza ni mtu mmoja anayeitwa Yairo mkuu wa sinagogi, na wa pili ni mwanamke mmoja aliyekuwa anatokwa na damu kwa muda mrefu lakini baadaye alikuja kuponywa na Bwana Yesu kwa kulishika tu pindo la vazi lake.

Sasa lipo jambo moja la kusisimua nataka ulione kwa hawa watu wawili ambalo kila mmoja lilikuwa kichwani mwake. Embu tusome kidogo;

Luka 8:40 “Basi Yesu aliporudi mkutano ulimkaribisha kwa furaha, maana walikuwa wakimngojea wote.

41 Na tazama, mtu mmoja akaja, jina lake Yairo, naye ni mtu mkuu wa sinagogi, akaanguka miguuni pa Yesu, akamsihi aingie nyumbani kwake;

42 kwa kuwa binti yake yu katika kufa, ambaye ni mwana pekee, umri wake amepata miaka kumi na miwili. Na alipokuwa akienda makutano walimsonga.

43 Na mwanamke mmoja, ambaye ametokwa na damu muda wa miaka kumi na miwili, [aliyekuwa amegharimiwa mali zake zote kwa kuwapa waganga] asipate kuponywa na mtu ye yote,

44 alikwenda nyuma yake, akaugusa upindo wa vazi lake; na mara hiyo kutoka damu kwake kulikoma”.

Sasa ukiangalia hapo, utaona huyu Yairo, alikuwa na binti yake aliyepatwa na matatizo katika umri wake wa miaka kumi na miwili (12), Na wakati huo huo alikuwepo yule mwanamke alitokwa na damu kwa muda wa miaka kumi na miwili (12). Ipo sababu kwanini biblia imeutaja umri wa mtoto na muda wa mwanamke kutokwa damu.

Kwamfano biblia inatuambia huyu Yairo hakuwa na mwana mwingine isipokuwa yule binti tu, pengine alimlea kwa taabu na shida, akiwa na matumaini kuwa huyu ndiye atakayekuja kuwa heshima yake ukubwani, pengine aliona mwelekeo mzuri wa binti yake, kama vile Yokebedi(mama yake Musa) alivyoona uzuri wa Musa tangu akiwa mdogo, akaamua kumficha ambapo kweli baadaye tunaona akaja kuwa nyota ya Israeli mwokozi wa Israeli,

Vivyo hivyo pengine huyu Yairo naye alimwona binti yake kuwa ni mzuri atakuja kuwa mcha Mungu kama Hana, au Sara, na kumletea fahari kwake, hivyo pengine akajitahidi kumlea katika maadili tangu anapozaliwa, mpaka anafikisha umri wa miaka 11, lakini alipofikisha umri wa miaka 12, ghafla akaanza kuona mabadiliko katika afya ya mtoto wake, miezi ya kwanza kwanza, hali inaanza kuwa mbaya mpaka inakaribia miezi ya katikati mtoto ndio yupo mauti uti kabisa,..katika hali kama hiyo anawaza afanyaje mtoto wake anakwenda kufa?

Je! Aruhusu maono yake yafe katika umri wa miaka 12,akizingatia kuwa ndio mwana pekee aliye naye? au afanye nini?. Lakini kama tunavyosoma habari, hakuruhusu jambo hilo litokee, hakuruhusu ndoto zake alizozihangaikia tangu zamani zizimwe na shetani katika mwaka wake wa 12 wa Maisha ya mwanawe, hapo ndipo akaanza safari ya kumtafuta Yesu.

Lakini huku nako upande wa pili, kulikuwa na mwanamke aliyetokwa na damu naye kwa muda mrefu, ambaye pia harakati zake za kutafuta uponyaji, zilianza tangu kipindi yule binti anazaliwa, tangu mwaka wa kwanza, akaendelea hivyo hivyo mpaka mwaka wa 2,..3…4, bila mafanikio mpaka mwaka wa 11, (Biblia inasema alikuwa ameshapoteza pesa zake nyingi kwa madaktari bila mafanikio) na ulipofika mwaka wa 12 bado hajapata alichokuwa anakitafuta, lakini naye siku moja akasikia Yesu yupo mjini..akasema sitakubali uponyaji wangu niliokuwa ninautafuta kwa miaka yote hii 12, leo hii ukatishwe na kukata tamaa, nitakwenda kukutana na Yesu.

Hivyo wote hawa wawili kila mmoja akaanza safari yake kivyake, na kama tunavyoisoma Habari Kristo aliwaponya wote, na wakapata walichokuwa wanakihangaikia, na kukiongojea.

Hata leo, tunapaswa tujifunze kuwa upo wakati wa kuyashindania yale maono ya kumtumikia Mungu ambayo tulikuwa tumeshaanza kuyafanya tangu zamani,haijalishi leo hii ni kipingamizi kikubwa kiasi gani kimesimama mbele yako, tunapaswa tuyashindanie…

Kwa kumkabidhisha Yesu hayo matatizo bila kuruhusu yaangamie kabisa..

Wapo watumishi ambao walishaanza kumtumikia Mungu,na walishapiga hatua fulani lakini pengine wakapitia vitisho Fulani vya ibilisi wakaacha kuhubiri, au kutumika. Ndugu usiruhusu taabu yako uliyoisumbukia iwe bure.

Kumbuka wapo wengine wamekuwa wakimwomba Mungu wapate kama tu hicho ulichonacho kwa muda mrefu, pengine tangu ulipoanza wewe kutumika, lakini bado hawajakipata, na hawakati tamaa kumwomba Yesu, na atawapa, kwanini wewe uruhusu kukata tamaa?

Mwaka wa 12 wa mtoto ya Yairo, Sio sawa na miaka 12 yule mwanamke aliyokuwa anangojea uponyaji wake..Hivyo na wewe, tatizo lako mpito lisikwamishe katika kazi yako ya utumishi Mungu aliyoiweka ndani yako.

Ili tushinde, ni lazima tushindane, Hivyo songa mbele.

Na sio tu kwenye kuifanya kazi ya Mungu, bali pia katika vitu vingine vyote unavyovitafuta vilivyo mapenzi ya Mungu, hupaswi kukata tamaa kabisa.

Bwana akubariki sana.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

MWAKA WA BWANA ULIOKUBALIWA.

NAMNA YA KUITAMBUA SAUTI YA MUNGU INAPOZUNGUMZA NA WEWE

KUOTA UMEFUNGA NDOA.

NENO LA MUNGU NI DAWA ILIYO TOFAUTI NA DAWA NYINGINE.

FUKUZA TAI WOTE JUU YA SADAKA YAKO.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
JOSHUA MUINDI JUMA
JOSHUA MUINDI JUMA
3 years ago

Need to be receiving messages