SWALI: Kwanini wale wayunani, walimfuata Filipo na kumwambia tunataka kumwona Yesu, maudhui ya tukio lile ni nini, mpaka lirekodiwe?
JIBU: Kipindi cha Bwana Yesu hadi kipindi chote cha mitume, yalikuwepo makundi mawili ya watu ambayo yalijikita kwa umakini sana katika kutafuta uhalisia na ukweli wote kuhusu masuala ya Mungu.
kundi la kwanza lilikuwa ni wayahudi, na kundi la pili ni wayunani. Tofauti ya wayahudi na wayunani ni kwamba. Wayahudi walijikita kuthibitisha kwa njia ya ishara. Lakini wayunani kwa hekima.
1 Wakorintho 1:22-23
[22]Kwa sababu Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima; [23]bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi;
Hivyo Yesu ambaye ni jibu lao wote alipokuja, baadhi ya hawa wayahudi walipomwona Kristo wakaanza kumthibitisha kwa ishara kwa walivyotarajia, kwamba ndiye masihi na mkombozi waliyemtarajia la!.(wakitaka wafanyiwe matendo fulani ya ajabu mbele ya macho yao, waamini)
Ijapokuwa Mungu hathibitishwi kwa ishara, bado Kristo aliwapa ishara.. Na ishara hiyo ilikuwa ni ile ya Yona. kukaa katika moyo wa nchi siku tatu, usiku na mchana na hatimaye kutoka mzima.
Mathayo 12:38 Hapo baadhi ya waandishi na Mafarisayo wakamjibu, wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako.
39 Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona.
40 Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi.
Hilo lilipokuja kutimia…tunaona wayahudi wengi waliamini, ikiwemo mitume (akina Tomaso). Na ndio ukawa mwanzo wa kumuhubiri Yesu aliyefufuka.
Lakini wale waliotazamia ishara walizoziwaza kwa akili zao, mfano za kushusha moto, kama Eliya, na kusahau ile ya kufufuka ambayo imezidi zote, bado Kristo akabakia kikwazo kwao.
Halikadhalika na kwa wayunani. Walimtafuta Mungu kwa njia ya hekima, ya elimu, ya maarifa, walimtafuta Mungu mwenye siri zote za uumbaji, na ujuzi, na utashi zaidi ya wanadamu wote na viumbe vyote.Ambaye atawazidi wanafalsa wao kama Plato, Socrates, Aristotle.
Kwa muda mrefu hawakufanikiwa mpaka baadhi yao, wakaishia kumwabudu tu, huku wakikiri hawamjui.
Matendo 17:22-23
[22]Paulo akasimama katikati ya Areopago, akasema, Enyi watu wa Athene, katika mambo yote naona ya kuwa ninyi ni watu wa kutafakari sana mambo ya dini.
[23]Kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua.
Yaani wakiwa na maana tunasikia miungu mingi,.lakini katika hiyo yote bado hatujaona mwenye hekima ya kuitwa Mungu wa ulimwengu. Wote akili zao ni kama za kibinadamu tu.
Sasa tukirudi kipindi cha Yesu, tunaona tukio jipya linajitokeza,
sio tu wayahudi walimwamini, bali hadi hawa wayunani watafuta-hekima wengi wao waliposikiliza maneno ya Yesu, na kupima kwa jicho la hekima, wakaona hakika hajawahi tokea anayeweza kuelezea ukweli wote wa uumbaji kama Yesu.
Hilo liliwashawishi na kuwafanya kukiri kuwa huyu ndiye suluhisho la utata wetu kuhusu Mungu na elimu.
Hivyo wakaamini, ndio sababu ya wao kumfata Filipo kumwomba wamwone Yesu. Hiyo ilikiwa ni heshima kubwa sana kwa Yesu (kidini) mbele ya macho makuhani na mafarisayo wote, kwamba Mungu kathibitishwa kifalsafa. Kumbuka wayunani hawa waliokwenda hawakuwa watu tu wa kawaida. Bali ni watu wenye heshima ya juu sana na hadhi.
Hiyo ndio sababu Bwana Yesu kusema saa imefika mwana wa Adamu atukuzwe.
Yohana 12:20-26
[20]Palikuwa na Wayunani kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu.
[21]Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu.
[22]Filipo akaenda, akamwambia Andrea; kisha Andrea na Filipo wakamwambia Yesu.
[23]Naye Yesu akawajibu, akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu.
[24]Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.
[25]Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.
[26]Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.
Hata leo, Yesu anathibitika katika mambo yote endapo tu tutamaanisha kumwona katika namna hizo. Ndio maana katika makundi yote ya watu ni lazima utakuta waamini.
Katika ya wanasayansi utawaona, katikati ya wanajeshi utawaona, katikati ya watawala utawaona,katikati ya mamajusi utawaona, katikati ya matajiri utawaona, katikati ya maskini utawaona, kati ya wanazuoni utawaona, kati ya madaktari utawaona,
Ukiuliza imekuwaje katika hali zao/ nafasi zao ambazo ni mbaya, na nyingine zenye majaribu, au zenye kumkana Mungu waziwazi, lakini wao wamemwamini Mungu?.
Ni kwasababu YESU anathibitika kila mahali.
Mtu kutokuamini ni yeye mwenyewe kataka. Hakuna atakayekuwa na udhuru siku ya mwisho, kwasababu Yesu amefunuliwa kila mahali.
Swali ni je! umemwamini Kristo? kama ni la! unasubiri nini. Mwamini leo kwa kuikubali kazi aliyoikamilisha juu yako ya kuondoa dhambi kwa kifo na kufufuka kwake. Ambayo hiyo huambatana na toba ya kweli na ubatizo.
Baada ya hapo utakuwa umepokea ondoleo la dhambi zako bure, mpokee Yesu sasa
Mungu akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Rudi Nyumbani
About the author