(Ukarimu na maziwa)
Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo mwokozi wetu. Karibu tujifunze maneno ya uzima. Haya ni mafunzo maalumu kwa ajili ya wanawake. Ikiwa utatamani kupata mengine mengi basi fungua link hii.. uweze yasoma..
https://wingulamashahidi.org/2021/07/21/masomo-maalumu-kwa-wanawake/
Kama wewe ni msomaji mzuri wa biblia, utakumbuka ile habari ya Debora na Baraka katika kitabu cha waamuzi.
Habari ile inaeleza jinsi Israeli ilivyo nyanyaswa na kutumikishwa na maadui zao wakaanani kwa muda wa miaka ishirini, chini ya mfalme mmoja aliyeitwa Yabini, na jemedari wake mkali aliyeitwa Sisera.(Waamuzi 4)
Watu hawa walikuwa wameendelea sana kivita, hivyo Israeli hawakuweza kufanya lolote isipokuwa kukubali mateso, ndipo wakamlilia Bwana sana. Naye akawasikia akawainulia mtetezi. Ndio huyu Debora nabii pamoja na baraka shujaa wa Israeli.
Sasa huyu Sisera alikuwa ni jemedari kwelikweli, hata Neno la Mungu lilipomjilia Debora, kumwagiza Baraka jemedari wa Israeli, akapange vita nao, bado alisita, na alichofanya ni kuomba Debora aende naye vitani..
Ni jambo ambalo ni kinyume na asili, wanawake kuhusishwa kwenye vita, kwasababu hiyo Debora akapewa Neno na Bwana kwa Baraka..kufuatana na wazo lake la kutaka.mwanamke aende naye vitani..kuwa ushindi huo hautakuwa mkononi mwake bali mkononi mwa mwanamke.
Waamuzi 4:8-9
[8]Baraka akamwambia, Kama utakwenda pamoja nami ndipo nitakwenda; bali kama huendi pamoja nami, mimi siendi.
[9]Basi akasema, Hakika nitakwenda pamoja nawe, lakini safari utakayoiendea haitakupatia heshima wewe; maana BWANA atamwuza Sisera katika mkono wa mwanamke. Debora akainuka, akaenda pamoja na Baraka mpaka Kedeshi.
Na kweli tunaona walipokwenda vitani kupigana nao. Yule Sisera jemedari wao, alifanikiwa kutoroka..Alipokuwa anakimbia alimwona mwanamke mmoja aliyeitwa Yaeli. Mwanamke huyo alimkaribisha kwake kwa ukarimu wa hali ya juu sana. Akampeleka sehemu ya maficho kabisa mahali ambapo si rahisi kugundulika, tena akamfunika ili kumuhakikishia ulinzi wote,
Jambo lile la ukarimu usio wa kawaida lilimtuliza moyo Sisera, akajihisi kama amepona, ndipo akamwomba yule mwanamke maji kidogo anywe. Lakini yule mwanamke bado akaendelea kuonyesha ukarimu wa hali wa juu sana, akaenda kumletea MAZIWA badala ya MAJI.. Pengine akamwambia aah! bwana wangu, maji si mazuri ukiwa umefunguka tangu asubuhi, tena kwenye mbio na pilika pilika za vita, kutumia maji si vizuri kiafya, kunywa kwanza maziwa haya, mwili uchangamke, upate nguvu, ndipo baadaye nitakupa maji unywe.
Sisera kuona vile akaendelea ku-relax, zaidi kuona ukarimu wa ajabu wa yule mwanamke, akafanya kosa akanywa yale maziwa, yakamlewesha kwa haraka mpaka akapotelea usingizini akasahau kabisa kwamba yupo vitani anatafutwa.
Lakini mwanamke Yaeli alipoona shujaa Sisera amelala fofofo, akasema nimempata adui yetu, sasa ninakwenda kumuua kirahisi kabisa.Akaenda kuchukua msumari mrefu, na nyundo. akavielekezea kichwani, akaupigilia ukaingia wote kichwani. Na mwisho wake ukawa umefikia pale pale.
Hata baadaye Baraka anakuja akakuta tayari mtu ameshakuwa marehemu.
Waamuzi 4:17-21
[17]Lakini Sisera akakimbia kwa miguu, akaifikilia hema ya Yaeli mkewe Heberi, Mkeni; kwa maana palikuwa na amani kati ya Yabini, mfalme wa Hazori, na nyumba ya Heberi, Mkeni.
[18]Yaeli akatoka kwenda kumlaki Sisera, akamwambia, Karibu Bwana wangu, karibu kwangu; usiogope. Akakaribia kwake hemani, naye akamfunika kwa bushuti.
[19]Akamwambia, Tafadhali nipe maji kidogo ninywe; maana nina kiu. Akafungua chupa ya maziwa, akampa kunywa, akamfunika.
[20]Naye akamwambia, Simama mlangoni pa hema; kisha itakuwa mtu awaye yote akija na kukuuliza, akisema, Je! Yupo mtu hapa, basi, mjibu, La, hapana.
[21]Ndipo Yaeli, mkewe Heberi, akatwaa kigingi cha hema, akashika nyundo mkononi mwake, akamwendea polepole, akamtia kile kigingi katika kipaji chake, nacho kikapenya, hata kuingia mchangani; kwa maana usingizi mzito ulikuwa umemshika; basi akazimia, akafa.
Ni nini Kristo anataka wanawake wafahamu kwa ushujaa wa Yaeli? (Ni ukarimu na Maziwa)
Kumbuka vita vyetu sisi si juu ya damu na nyama, bali dhidi ya wakuu wa giza hili na ibilisi. Na mtu yeyote ambaye anahubiri injili, mtu huyo ni askari wa Bwana. Mfano wa akina Debora, na Baraka. Haijalishi jinsia yake ni ipi, wote ni watendakazi katika shamba la Bwana.
Lakini kama tunavyojua Mungu ameweka majukumu mbalimbali ndani ya mwili wa Kristo, wewe kama mwanamke hujaitwa kuwa mchungaji, au askofu, lakini umeitwa kuwa shujaa wa kumwangamiza adui kwa karama uliyopewa. Debora na Yaeli hakuwa kama Baraka, maumbile yao hayakuumbwa kusimama na mikuki na ngao, na kukimbizana maporini usiku na mchana na maadui. Hapana.. bali ni kuwa katika utulivu. Na utulivu ukitumiwa vizuri huleta mlipuko mkubwa kuliko wingi wa makombora ya vita.
Aliyemuua shujaa Sisera alikuwa mwanamke, aliyekuwa nabii wa Israeli alikuwa mwanamke. Ushindi ulipatikana kwa mikono ya wanawake. Lakini bila kuvaa suruali, na mitutu vya vita.
Hata leo, ikiwa mwanamke ataitambua vema kazi ya injili kwa kufuata kanuni za kibiblia anaouwezo wa kuwavua watu wengi kwa Kristo zaidi hata ya mhubiri wa kusimama kwenye majukwaa makubwa.
Ukarimu, kwa wenye dhambi, upendo wa waliotekwa na mwovu, pamoja na maziwa (Ndio Neno la Mungu) ni Njia hii ya YAELI, ukiitumia itakufanya uwavute wale watu kwa Kristo wengi, na hatimaye kanisa la Kristo kukua na kuongezeka.
Ni watu wangapi unaweza wafadhili kichakula huku unawahubiria injili, unaweza wapelekea mavazi huku unawafundisha habari za Kristo, unaweza wafadhili kwa chochote huku unawaalika kanisani..kidogo.kidogo, upo kazini kwako, unazungumza nao kwa ukarimu, unawasaidia majukumu ambayo wangepaswa wayafanye wao wenyewe lakini wewe unawasaidia, lengo lako ni uwavute katika imani, huku ukihakikisha unawapa na maziwa, yaani maneno ya faraja ya Mungu,(1Wakorintho 3:2, 1Petro 2:2).
Wewe ni mamantilie, wateja wako, unawapa zaidi ya huduma, huku unawafundisha habari za Kristo, unawaeleza uzuri wa kukusanyika kanisani, n.k.
Ukiendelea hivyo baada ya kipindi fulani utashangaa watu hao wanavutika kwako, na kwa Kristo. Hata yule mpinga-kristo aliyekuwa na moyo mgumu kuliko wote anaokoka, yule boss wako ambaye alikuwa hataki kusikia masuala ya Mungu anaokoka. Wale ambao walirudi nyuma, wanaamka tena.
Onyesha tu ukarimu, lakini usiwe ukarimu wa bure, huo hautazaa chochote bali wenye injili nyuma yake.
Hivyo wewe kama mwanamke/binti wa kikristo simama katika eneo la utulivu, kiasi, kujisitiri, ni ukweli utaziangusha ngome sugu za adui.
1 Petro 3:1-5
[1]Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno;
[2]wakiutazama mwenendo wenu safi, na wa hofu.
[3]Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi;
[4]bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.
[5]Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
KWANINI DANI ALIKAA KATIKA MERIKEBU.
Maziwa yasiyoghoshiwa ni nini? Kwanini biblia inatumia mfano huo?
Maana ya Mithali 30:33 Kwa maana kupiga maziwa huleta siagi
Rudi Nyumbani
About the author