UWEZO WA KIPEKEE.

UWEZO WA KIPEKEE.

Kuna kipindi tuliishi bila kutegemea pua zetu kupumua, kuna kipindi tuliishi bila kutegemea midomo yetu kulia chakula…Na kipindi hicho si kingine zaidi ya kile kipindi ambacho tuliishi tumboni mwa mama zetu, kwa miezi 9 tuliishi maisha ya kimiujiza ujiza.. Hakuna mwanadamu yoyote anayeishi sasa ambaye hajapitia kuishi maisha hayo ya kimiujiza.

Hivyo si ajabu Bwana alisema… “….Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu (Mathayo 4:4).

Kama kuna wakati maisha hayo yaliwezekana…hata sasa kuna mambo yanaonekana kama hayawezekani lakini yanawezekana.

Inaweza kuonekana haiwezekani kabisa leo kuishi maisha makamilifu yanayompendeza Mungu…lakini nataka nikuambie hilo linawezekana kabisa..kwasababu Bwana mwenyewe alisema tutakuwa wakamilifu kama Baba yetu alivyo mkamilifu…(Mathayo 5:48). Hivyo Mungu asiyeweza kusema uongo, hawezi kuumba kiumbe ambacho anajua atakipa jukumu kubwa zaidi ya uwezo wake…Kwasababu hiyo basi jinsi alivyotuumba sisi, anajua kabisa kuna namna au mazingira ambayo tukijiweka tutakuwa wakamilifu kama yeye anavyotaka sisi tuwe.

Na ukamilifu na utakatifu tunaouzungumzia sio ule wa kujisifu na kujibeza kwamba ni mkamilifu au mtakatifu mbele za Mungu, wala sio ule wa kujihesabia haki kwamba sifanyi hichi wala kile kama mtu Fulani au watu Fulani wanavyofanya…bali ukamilifu na utakatifu unaozungumziwa ni ule wa roho ya unyenyekevu, na ya kumwogopa Mungu, ambao huo unaleta moyo wa toba siku zote mbele za Mungu na hofu ya Mungu…ambapo hofu hiyo itakuzuia wewe kutokufanya mambo yote yasiyompendeza Mungu, hofu hiyo itakufanya usidhubutu kwenda kuzini, mawazo ya uzinzi yanapokujia unayashinda ndani ya sekunde chache sana, pia hofu hiyo inakuzuia kwenda kuiba, kwenda kutoa mimba, kwenda kula rushwa, n.k..Na haikufanyi wewe kujilinganisha na wengine au kufurahia wengine wanapofanya mambo ambayo wewe huyafanyi na kujifanya bora kupita hao…Yaani unapomwona mwingine anajiuza, unapata hisia kama ni dada yako au ndugu yako wa damu ndio yupo vile, lakini sio kufurahia kana kwamba umemzidi utakatifu, na hivyo wewe ni heri kuliko yeye…Huo sio utakatifu bali ni kujibeza, ambako hakumpendezi Mungu.

Hivyo..huo uwezo wa kuwa mkamilifu kwa namna hiyo ya kumpendeza Baba…Tumeahidiwa kwenye Neno la Mungu kwamba “Unaweza ukashuka juu yetu na ni ahadi”..Tunauita ni uwezo kwasababu katika hali ya kawaida, ni ngumu kumpenda Yule mtu anayekuchukia, ni ngumu kumsamehe Yule mtu ambaye amekutendea ubaya mkubwa sana, ni ngumu kurudisha mali ya Yule mtu aliyekuibia, ni ngumu kuacha uasherati au ukahaba unaokuingizia kipato kizuri n.k…Hivyo inahitajika uwezo mwingine kushuka juu yetu. Na huo uwezo ukishuka ndio unatufanya tuishi kimiujiza kama tulivyokuwa tunaishi kipindi Fulani huko nyuma tulivyokuwa tumboni mwa mama zetu…

Tulikuwa na pua lakini tulikuwa huituitumii tumboni, tulikuwa na midomo lakini tulikuwa huutumii kula..lakini bado tulikuwa tunaishi na kukua…Hali kadhalika ukiupokea huu uwezo leo, watu watashangaa unawezaje kuishi bila kufanya uzinzi na hali una uwezo wa kufanya hayo yote, na mazingira yanakuruhusu…wewe mwenyewe utajishangaa umewezaje kuishi bila kulewa tena pombe na ilihali una fedha za kukutosha kufanya hayo yote n.k.

Sasa uwezo huo utashuka juu yako endapo tu, utakubali tu kuviacha hivyo vitu…Kitu kimoja ambacho unahitaji kufahamu wewe ambaye bado hujampokea Yesu, ni kwamba Nguvu ya Roho Mtakatifu haiwezi kuzidi nguvu ya maamuzi yetu…maana yake ni kwamba Mungu hatulazimishi kama ma-robot kufanya mapenzi yake ingawa anao uwezo wa kufanya hivyo, ila hajachagua kufanya hivyo…anachokifanya ni kutuwekea chaguzi mbili mbele yetu…tuchague UZIMA au MAUTI. Tunapochagua uzima basi ndipo anatupa Baraka zote za Uzima ikiwemo UWEZO wa kuwa kama yeye.. Lakini tukichagua mauti hatatulazimisha kutupa uzima…Hivyo uchaguzi ni wetu.

Sasa hatuchagui kwa midomo…bali kwa vitendo..Maana yake ni kwamba kama ulikuwa unafanya kazi ya Bar, unaiacha mara moja, kama ulikuwa ni msikilizaji wa miziki ya kidunia kupitia simu yako unaifuta hiyo miziki na hizo video za kidunia zote pasipo kubakiza hata moja..kama ulikuwa ni mwizi na umeiba, unamrudishia Yule mtu mali yake uliyomuibia kama bado unayo na unakusudia kuacha wizi..kama ulikuwa unajiuza unaiacha hiyo biashara, kama ulikuwa ni mlevi hivyo hivyo unaacha kwenda ile Bar, na vitu vingine vyote visivyompendeza Mungu unajilazimisha kuviacha katika maisha yako Sasa Baba wa mbinguni akiona kwamba kwa vitendo umeacha mambo hayo…Ule uwezo unaushusha juu yako wakati huo huo ulipoamua kuyaweka chini maisha ya kale…

Kwasababu umeingia gharama ya kuyavua maisha yako ya kale, na yeye Baba wa mbinguni anaingia gharama ya kukutuza wewe usirudi tena nyuma..na anakutunza kwa njia gani?..kwa njia hiyo ya kukupa UWEZO wa kushinda Dhambi, na kuwa mkamilifu.

Sasa ndani ya kipindi kifupi baada ya wewe kuamua kuacha maisha ya dhambi kwa vitendo, utaona ile kiu ya pombe inakata ghafla, ile kiu ya kufanya ukahaba inakata ghafla, hupambani vita vikali kuukataa uasherati tofauti na hapo kwanza…mpaka wewe mwenyewe utajishangaa umekuwaje?..zamani ulikuwa ukipitisha siku mbili bila kunywa pombe unasikia kuumwa, lakini utashangaa inapita wiki, mara mwezi, mara mwaka hata ile hamu haipo..ulikuwa haipiti siku bila kujichua lakini utajikuta imepita wiki, mwezi na mwaka bila hata kukikumbuka hicho kitendo…sasa ukishafikia hatua kama hiyo basi ule uwezo umeshamiminwa ndani yako…na uwezo huo utaambatana na mambo mengine ya muhimu kama tuliyoyataja hapo juu..utajikuta unakuwa na hofu ya Mungu, na mtu wa kumpenda Mungu na kuzidi kujitenga na ulimwengu, pamoja na kuwa msaada kwa wengine ambao hawajaingia ndani ya Neema hiyo.

Kwahiyo kama wewe bado hujamwamini Yesu Kristo na bado hujapokea huo uwezo, tambua kwamba bado nafasi unayo…nguvu hiyo ni kutubadilisha ni zawadi kwetu sote kutoka kwa Baba, endapo tu tukimwamini Yesu..Hivyo basi popote pale ulipo tenga muda kadhaa peke yako binafsi, mwombe Mungu rehema..kisha kusudia kuacha yale yote uliomwomba akurehemu…Kumbuka kutubu maana yake ni kugeuka!..Hivyo matendo yako yana maana sana mbele za Mungu Baba zaidi ya maneno yako..

Pia inawezekana umeshamwamini Yesu, lakini umeomba muda mrefu uwezo huu ushuke juu yako, lakini bado huoni chochote, bado unajikuta unafanya punyeto, bado unajikuta unarudi kwenye ulevi, uasherati na ushirikina…kama unapitia hali kama hiyo basi fahamu kuwa hukutubu vizuri…Uliomba tu rehema..kwamba Bwana akusamehe tu hiki na kile..lakini hukukusudia kuviacha vile vitu kwa vitendo..bado ulikuwa ni miziki kwenye simu yako, bado ulikuwa unatembelea zile site za pornograph bado ulikuwa umejiungamanisha na makundi yale ya ulevi na walevi, na ndani kwako kulikuwa na chupa za bia, bado ulikuwa unarudi kwenye kazi yako ya Bar n.k..Hiyo ndio maana ule uwezo haukushuka ndani yako..lakini leo bado unayo nafasi..Tubu tu kwa kuacha hayo mambo na Bwana atakushushia uwezo huo wa kuishi kimiujiza kama aliokupa wakati ule ulipokuwa tumboni mwa mama yako.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

MUUNGANIKO WA MADHEHEBU NI MPANGO WA MPINGA-KRISTO.

NAMI NINAZO FUNGUO ZA MAUTI, NA ZA KUZIMU.

JE MOYO WAKO NI MNYOFU MBELE ZA MUNGU

Je ni sahihi kumtenga mtu anapofanya dhambi kanisani?

Mbona Mungu anaruhusu watu wapate shida, ilhali ana uwezo wa kutuepusha?

Kwanini Mungu alisema hakuna mtu awazaye kuuona uso wake akaishi?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments