Title July 2020

VUKA UJE MAKEDONIA UTUSAIDIE.

Shalom,

Nakukaribisha tutafakari pamoja vifungu vifuatavyo vya maandiko, naamini lipo jambo utajifunza mwishoni mwa somo..

Matendo 16:6 “Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia.

7 Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa,

8 wakapita Misia wakatelemkia Troa.

9 Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie”.

Wengi wetu tunafahamu vipingamizi pekee mtume Paulo alivyokuwa anapitia vya kuhubiri injili vilitoka kwa shetani, lakini hatujui kuwa kuna wakati mwingine Mungu mwenyewe alikuwa anamzuia Paulo asihubiri injili japokuwa alitamani kufanya hivyo,.

Mungu anafanya hivyo sio kwamba hataki watu wahubiriwe injili kama ilivyo kwa shetani, hapana, bali ni kawaida yake kuwapa vipaumbele vya kwanza wale ambao wanaonyesha kiu ya kutaka kumjua yeye.

Ili kutimiza haya maandiko.

Mathayo 5:6 “Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa”.

Na haya..

Mathayo 5:3 “Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao”.

Kama ukichunguza hiyo mistari utaona, Mungu hakumkataza Paulo kufika kabisa katika hiyo miji iliyotajwa hapo juu, lakini aliifikia na kuipita, kuonyesha kuwa kama kungekuwa na utayari wa wenyeji wa pale kutamani kumjua Mungu basi wangeanzwa kwanza wao, kisha ndio wafuate wale wengine..

Jaribu kufikiria anafika pale Frigia, anataka tu kuanza kuhubiri Mungu anamzuia, anaondoka anaenda mji unaofuata Galatia huko nako Mungu anamzuia anaondoka tena anafikiria labda ashuke kwenye miji mingine ya Asia (ambayo ndio kama Efeso, Smirna, Pergamo, Laodikia n.k. ) lakini huko nako Mungu anamwambia asihubiri chochote aondoke…

Haishii hapo anaondoka tena Asia anafika mji ulioitwa Misia ili aanze kuhubiri bado Mungu anamkataza, anafika Troa bado Mungu hampi kibali, wakati sasa akiwa hapo Troa ukingoni kabisa mwa mji ndipo Mungu anamwonyesha maono ambayo yalikuwa yanaonyesha jinsi watu wa kule Ng’ambo ya bahari Makedonia walivyokuwa wanahitaji msaada mkubwa sana wa kiroho..

Ndipo hapo utaona inamgharimu Paulo kuvuka bahari sasa asafiri, mpaka kwenye hiyo miji ya Makedonia ambayo, ilikuwa ni Filipi, Thesalonike, na Beroya.. Ili kuihubiri injili.. Si jambo rahisi

Ili kuelewa vizuri jaribu kutengeneza picha labda mtumishi wa Mungu anatoka nchi ya mbali Afrika Magharibi labda tuseme Ghana, anafika nchi za Afrika ya kati kama vile Congo n.k., Mungu anamwambia pita usihubiri, anafika mpaka nchi zetu za Afrika mashariki, Anaanzia Uganda anaambiwa pita, anafika Kenya anaambiwa pita, anafika hapa Tanzania, bado Mungu anamwambia usihubiri hapo, sasa akiwa ameshavuka kote toka kigoma, akiwa pale Daresalaam, Mungu anamwambia panda Meli nenda taifa la India wapo watu wangu kule wanahitaji msaada wa kunijua mimi..

Ndivyo ilivyokuwa kwa Mtume Paulo na wenzake, walienda Makedonia na kweli kule walikutana na watu ambao kwanza walikuwa ni maskini, lakini walikuwa tayari kumtolea Mungu kwa moyo wao wote..na zaidi ya yote walikuwa tayari kulipokea Neno la Mungu, mfano watu wa Beroya ndio wale ambao walikuwa wapo tayari kuchunguza maandiko ya kujua ufasaha wa yote,

2Wakorintho 8:1 “Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia;

2 maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na UMASKINI WAO uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao.

3 Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao;

Hivyo mimi na wewe tunajifunza nini?

Mungu ni yeye ule jana na leo na hata milele, kama mengi ya makanisa ya Asia hayakustahili kupewa neema ya wokovu kwanza, atafanya na kwetu vivyo hivyo kama hatutakuwa tayari kuipokea.

Tupaswa tujiulize je! mioyo yetu ni kweli ina kiu ya kumjua Mungu, kiasi kwamba mpaka rohoni Mungu anatufananisha na watu wa Makedonia?.. Vuka, uje Makedonia utusaidie?. Je! ni kweli tunaonyesha tunahitaji msaada kutoka kwa Mungu? Je tunastahili msaada?.. Kama ni kweli tunaonyesha tunahitaji msaada, basi hapo ndipo Mungu atakapofungua njia ya kutusaidia, kwa namna ya ajabu.

Na tunaonyesha tunahitaji msaada kwa namna gani?.. Tunaonyesha kwa bidii yetu sisi ya kutafuta yeye kwa nguvu zetu zote, kwa akili zetu zote, kwa mioyo yetu yote na kwa Roho zetu zote.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

SAYUNI ni nini?

Mitume wote waliopita walikuwa ni watu weupe hata manabii wote waliopita hadi Ma-papa ni ngozi nyeupe. ni kweli ngozi nyeusi ililaaniwa ?

USIPOKUWA MWAMINIFU, NAFASI YAKO ITACHUKULIWA.

TABIA YA KIPEKEE USIYOIJUA KUHUSU NENO LA MUNGU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

USIISHI BILA KUIFANYA KAZI YA MUNGU KABISA..

Shalom mtu wa Mungu, karibu tuyatafakari maandiko…leo ni siku nzuri Bwana aliyotupa..hivyo ni vyema tukachukua nafasi hii kulitafakari Neno lake kwa ufupi..

Kumbuka siku zote kuwa baada ya kumpokea Kristo, kila mmoja wetu anawajibu wa kuifanya kazi ya Mungu kupitia karama Mungu aliyoiweka ndani yake. Kuna hatari kubwa sana ya kutoitumia karama Mungu aliyoiweka ndani yako kabisa….Na madhara makubwa yapo baada ya maisha haya…wakati ule ambapo watakatifu watapewa thawabu zao wewe hutakuwa na chochote…

Katika siku ile waliokuwa waaminifu kwa karama zao watapewa thawabu kubwa zaidi..na wale waliokuwa walegevu na kuleta faida ndogo katika ufalme wa mbinguni watalipwa kidogo, na wale ambao hawajafanya kitu kabisa hawatapewa chochote…

Lakini ni heri kufanya hata kama ni KIDOGO sana ukapata kitu kule kuliko kutofanya kabisa…

Hebu naomba usome mfano huu Bwana alioutoa…inawezekana ulishawahi kuusoma hapo kabla mara nyingi, na kuurudia rudia…. lakini hebu chukua muda tena sasa hivi kuusoma hadi mwisho taratibu, pasipo kuruka kipengele hata kimoja, kuna kitu cha kipekee sana nataka tujifunze leo.

Luka 19:11 “Waliposikia hayo, aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara.

12 Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi.

13 Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, FANYENI BIASHARA HATA NITAKAPOKUJA.

14 Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale.

15 Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake.

16 Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi.

17 Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi.

18 Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida.

19 Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano.

20 Akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso.

21 Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda.

22 Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda;

23 BASI, MBONA HUKUIWEKA FEDHA YANGU KWA WATOAO RIBA, ili nijapo niipate pamoja na faida yake?

24 Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang’anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi.

25 Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi.

26 Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang’anywa hata alicho nacho”.

Mfano huo unamhusu Bwana Yesu mwenyewe, yeye ndio mfano wa huyo mtu kabaila..ambaye aliondoka na kwenda nchi ya mbali(mbinguni) kutuandalia ufalme…na alipoondoka alitupatia vipawa (karama) akatuambia tukawafanye watu wote kuwa wanafunzi (maana yake kuwahubiria na kuwageuza wamwamini yeye kila mmoja kwa kipawa alichopewa)…Na siku moja atarudi kutoka huko nchi ya mbali(mbinguni)…alipokwenda kututengenezea ufalme…atarudi duniani kwaajili ya utawala wa miaka 1,000 (Ufunuo 20).. Na siku atakaporudi atawaangamiza wale wote ambao hawakumkubali (yaani watu waovu)..Na baada ya kuwaangamiza waovu wote ndipo atakapowakusanya watumishi wake waliompokea…na hapo kila mmoja ataketi na kutoa hesabu ya faida aliyoileta katika ufalme wa mbinguni..

Watasimama wachungaji, watasimama waimbaji, watasimama mitume, watasimama mashemasi, waalimu, manabii, maaskofu, wazee wa kanisa, waumini wote na kila mmoja atatoa hesabu jinsi alivyoitumia karama yake…waliofanya vizuri watapewa mamlaka makubwa na waliokuwa wavivu watakosa vyote…

Sasa katika kisa hicho tunasoma kuna mmoja alifukia talanta yake chini…kwa uvivu akijitumainisha kwamba Bwana huwa hasaidiwagi kazi…yeye anang’oa pando asilolipanda, kazi ambayo hajaifanya yeye anaiharibu!…kwahiyo akajifariji kwamba Mungu huwa hasaidiwi kazi…hatutegemei hata tusipokwenda kuhubiri walio wake watakuja tu!.. kwanza unaweza kwenda kuhubiri ukakosea kosea maneno ndio ukawa umemuudhi badala ya kumfurahisha……pia sio lazima sana kumtolea kwani hata tusipochangia chochote kwenye kazi yake yeye ni tajiri na sisi ni mavumbi hivyo atafanya njia tu kwa vyovyote vile(hasaidiwi kazi)……pia yeye hahitaji sana sifa zetu, tayari anao malaika wengi wanaomwimbia….. n.k

Kwahiyo kwa kujitumainisha huko na visingizio hivyo… mtu wa namna hii akawa hafanyi kazi ya Mungu akafananishwa na mtu aliyefukia fedha yak echini ya shimo…siku ile ikafika na Bwana akamhukumu kwa kinywa chake…

Ndugu mpendwa baada ya kuokoka…usikae ufikiri kwasababu Mungu ni mkuu basi hatutegemei sisi….Ni kweli hatutegemei anaweza kufanya asilimia mia pasipo sisi…lakini hataki tuwe wajinga!…Sio kwasababu kasema maneno haya…

Matendo 7:49 “Mbingu ni kiti changu cha enzi, Na nchi ni pa kuwekea miguu yangu; Ni nyumba gani mtakayonijengea? Asema Bwana,

50 Au ni mahali gani nitakapostarehe? Si mkono wangu uliofanya haya yote?”

Basi na sisi ndio tubweteke tusimjengee nyumba…kwasababu amesema yeye hakai kwenye nyumba zilizofanywa na mikono yetu…Ndugu Usikae ufikiri hivyo kamwe!.. Daudi aliujua vizuri huo mstari pamoja na Sulemani mwanawe lakini walimjengewa Bwana nyumba hivyo hivyo…na Mungu akapendezwa nao..Sikia maneno Sulemani aliyoyasema..

1Wafalme 8: 26 “Sasa, Ee Mungu wa Israeli, nakusihi, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako, Daudi, baba yangu.

27 LAKINI MUNGU JE? ATAKAA KWELI KWELI JUU YA NCHI? TAZAMA, MBINGU HAZIKUTOSHI, WALA MBINGU ZA MBINGU; SEMBUSE NYUMBA HII NILIYOIJENGA!

28 Walakini uyaelekee maombi ya mtumwa wako, na dua yake, Ee Bwana, Mungu wangu, uisikilize sauti na maombi ya mtumwa wako, aombayo mbele zako leo.

29 Macho yako yafumbuke na kuielekea NYUMBA HII usiku na mchana, mahali hapa ulipopataja, ukasema, Hapa ndipo litakapokuwapo jina langu; ili uyasikie maombi ya mtumwa wako aombapo akikabili mahali hapa”.

Walijua Mungu mbingu hazimtoshi na huku duniani ni mahali pa kuwekea miguu yake..lakini walilazimisha kumjengea Mungu duniani japokuwa waliyajua hayo maandiko…na mpaka leo Hekalu la Sulemani linajulikana.

Vivyo hivyo na wewe..usiseme Bwana ana malaika wengi…usiseme Bwana hahitaji fedha yangu kwani dhahabu zote na fedha zote ni za kwake… Usiseme sio lazima kujisumbua kuhubiri kwani Bwana anao watumishi wengi…usiseme sio lazima kujisumbua kuimarisha kazi ya Mungu kwasababu Mungu hahitaji msaada kutoka kwetu..ukifanya hivyo utakuwa umefukia talanta yako chini uliyopewa…

Na Mwisho kabisa Bwana alimwambia Yule mtu aliyefukia ile fedha chini maneno haya…” BASI, MBONA HUKUIWEKA FEDHA YANGU KWA WATOAO RIBA”… Mtu anayeweka fedha kwa watoa riba…maana yake haendi kuifanyia shughuli yoyote ile hela..ni kuiweka tu baada ya wakati Fulani inajizalisha…ni kama vile umemkopesha mtu hela…Sasa kazi ya kukopesha haitumii jasho lolote…ni kuwekeza tu hela na kusubiria faida basi!….Hata hiyo kazi nyepesi ambayo haihitaji jasho! Bwana angetegemea aione kwa huyu mtu lakini hakuiona..

Kadhalika na wewe…inawezekana huwezi kabisa kusimama mimbarani, au kwenda mitaani kuhubiri… basi angalau wekeza kwenye kazi ya Mungu kwa fedha zako au mali zako kwa uaminifu, nunua kinanda, nunua mifuko kadhaa ya cement, au nunua chochote kile uwezacho kipeleke nyumbani kwa Mungu…kwasababu unapomtolea Mungu, fedha au mali zile zinakwenda kutumika katika kuifanya kazi ya Mungu na hivyo unaleta faida katika ufalme wa Mbinguni… ukifanya hivyo angalau Bwana atakuheshimu siku ile utakuwa umeiweka talanta yako kwa watoa riba…

Bwana atusaidie sana katika hayo..

Kama bado hujampa Yesu maisha yako…tunaishi katika siku za mwisho, Kristo yupo mlangoni kurudi…hivyo tubu leo kwa kumaanisha kuacha dhambi zote unazozifanya kama ulevi, rushwa, anasa, uasherati, uuaji, ufiraji, ulawiti,ushoga, usagaji, utazamaji wa picha za ngono, kujichua na nyingine zinazofanana na hizo…Tubu leo kwa dhati na amua kuziacha…na baada ya kuomba rehema Bwana atukusamehe kama alivyoahidi…Na amini kashakusamehe kama umetubu kwa dhati!..Na baada ya hapo tafuta ubatizo sahihi ambao ni wa maji tele na kwa jina la Yesu ambalo ndio jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu…na baada ya hapo Roho Mtakatifu ambaye tayari atakuwa ameshafika karibu yako atakupa uwezo wa kuzishinda hizo dhambi ulizoziacha..ili usizirudie tena…na mengine yaliyosalia atakuongoza kuyafanya.

Maran atha

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

USITUPE LULU ZAKO MBELE YA NGURUWE.

Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu ya sindano.

MAOMBI YA VITA

FAIDA ZA MAOMBI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

NI KITU GANI PETRO NA YOHANA WALIKIGUNDUA KABURINI?

Shalom..

Asubuhi ile Mariamu Magdalene alipokwenda kaburini na kukuta jiwe limeondolewa na mwili wa Yesu haupo, aliondoka ghafla na kwenda kuwapa taarifa wanafunzi wa Yesu, na kuwaambia Bwana hayupo kaburini wamemwiba na hatujui ni wapi walipompeleka..

Taarifa hiyo ya kushtusha iliwafanya watu wawili waondoke mahali pale kwa kasi sana, mmoja alikuwa ni Yohana na mwingine alikuwa ni Petro ili kwenda kuthibitisha kama waliyoelezwa ni kweli au La..

Yohana 20:2 “Basi akaenda mbio, akafika kwa Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, Wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka.

3 Basi Petro akatoka, na yule mwanafunzi mwingine, wakashika njia kwenda kaburini.

4 Wakaenda mbio wote wawili; na yule mwanafunzi mwingine akaenda mbio upesi kuliko Petro, akawa wa kwanza kufika kaburini.

5 Akainama na kuchungulia, akaona vitambaa vya sanda vimelala; lakini hakuingia.

6 Basi akaja na Simoni Petro, akaingia ndani ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala,

7 na ile leso iliyokuwako kichwani pake; haikulala pamoja na vitambaa, bali imezongwa-zongwa mbali mahali pa peke yake.

8 Basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza wa kufika kaburini, akaona na kuamini.

9 Kwa maana hawajalifahamu bado andiko, ya kwamba imempasa kufufuka”.

Sasa ukiangalia hapo, utagundua Yohana alipofika pale kaburini na kuchungulia kwa mbali, aliona kweli Bwana hayupo na vitambaa vya sanda vimelala pale chini, pengine hilo lilimpa uhakika kuwa kweli mwili wa Bwana uliibiwa usiku na kuhamishwa pale na kupelekwa mafichoni sawasawa na maneno ya Mariam Magdalene..

Lakini tunaona Petro alipokuja baadaye kidogo, yeye kuishia pale mlangoni tu, bali alipitiliza moja kwa moja mpaka ndani kabisa mwa kaburi pale Bwana alipokuwa amelazwa ili kuthibitisha jambo hilo, Lakini alipofika karibu aliona jambo lingine la kushangaza kidogo, ambalo ndio lililowapa uhakika kuwa Bwana hakuibiwa bali ni kweli alifufuka..

Jambo hilo pengine hata wewe hukuwahi kulifahamu, ukisoma huo mstari wa 7 utaona vitambaa vya sanda vilikuwepo kweli pale chini sawasawa na Yohana alivyoona kule nje, lakini ile LESO ya kichwani biblia inasema haikuwa Pamoja na vitambaa bali ilizongwa zongwa mbali kabisa mahali pake yenyewe.. Sasa hilo neno kuzongwa zongwa biblia inamaanisha KUKUNJWA VIZURI, yaani hiyo leso ya kichwani ilikunjwa vizuri kwa utashi na Bwana mwenyewe kisha akaenda kuiweka kwa mbali kidogo na vile vitambaa vilivyokuwa vimefungwa mwilini mwake, pengine kwenye mwamba wa juu kidogo, mbali na pale alipokuwa amelala..

Hilo ni jambo la kufikirisha sana… Kama kweli wezi walikuja kumuiba wasingekuwa na muda wa kuikunja leso na kuiweka sehemu yake yenyewe mfano wa mtu anayekunja shati lake na kuliweka kabatini.. mwizi hawezi kufanya kazi kama hiyo..

Hilo ni tendo linaloonyesha kuwa Bwana hakuibiwa, bali alifufuka, na alipofufuka alianza kujifungua yeye mwenye taratibu, alipoliza, akaichukua ile leso ya kichwa akaanza kuikunja bila haraka yoyote akaenda kuiweka ndipo akaondoka..

Hilo ndilo lililowafanya Petro na Yohana biblia iseme katika mstari wa nane, wakaamini..

Habari hiyo inatufundisha nini?

Hatuwezi tukaufahamu ukweli wa Kristo kwa kuambiwa ambiwa tu, vilevile bado hatuwezi kuelewa siri ya kufufuka kwake kwa kusimama mlangoni mwa kaburi lake, Tutaelewa siri za Kufufuka kwa Kristo kwa kuzama kabisa mule kaburini alipokuwepo kama Petro, yaani kuwa tayari kufa na Kristo na kufufuka Pamoja naye kwa Habari ya dhambi, ndipo tutakapoelewa siri za kufufuka kwake kwa mapana na marefu..

Tukubali tu tusipotaka kuzama ndani katika wokovu, kamwe hatutakaa tuelewe maana ya ufufuo maishani mwetu, tukiwa wakristo vuguvugu, au wakristo jina, au wakristo wa kusita sita, wakristo wa kuvutwa vutwa tujue kuwa wapo tuliowaacha nyuma mfano wa Petro watatutangulia siku moja kuzijua siri za Kristo kuliko sisi ambao tunajiona tumeshajua kila kitu, na huku bado tupo mguu mmoja nje mwingine ndani.

Naamini hatutakuwa wasikiaji tu wa hadithi, bali tutayatendea kazi, tutazama kaburini kuuthibitisha ufufuo,…hicho ndicho Bwana anachokitaka maishani mwetu.

Bwana atubariki sote.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

SHETANI ANAITHAMINI HATA MAITI YAKO.

JE! PAKA KULIA USIKU NI ISHARA YA UCHAWI?

ZIKIMBIE TAMAA ZA UJANANI! NA MTU YEYOTE ASIUDHARAU UJANA WAKO.

Nitaitofautishaje sauti ya Malaika na ya Roho Mtakatifu?

HAPO NDIPO WATU WALIPOANZA KULIITIA JINA LA BWANA.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi Nyumbani:

Print this post

TUNA JUKUMU LA KWENDA KUTEKA MATEKA.

Shalom, mtu wa Mungu..karibu tuyatafakari maandiko pamoja,

Biblia inasema…

2Wakorintho 10:3 “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili;

4 (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)”

Kazi ya kwenda kuvua watu inafananishwa na shughuli za wanajeshi vitani…Wanajeshi wanapotaka kushambulia mahali huwa hawampi adui taarifa…na wanafanya hivyo, wanashtukiza tu…na wakisha angamiza wote wanateka mateka na kuchukua nyara vitu vyao..

Na katika kazi ya uvuvi wa watu ni hivyo hivyo…Hatupaswi kuingia mkataba na adui, wala kushauriana naye…tunachopaswa kufanya ni kila mara kuvamia kambi ya adui na kuteka mateka..

Unaposikia msukumo wa kuhubiri, sio suala la kusema hapa panafaa au hapafai..unachopaswa kufanya ni unavamia!…kwasababu katikati ya kambi ya Adui kuna mateka…na mateka unawaweka huru kwa kuwavamia..Ingawa vita utakutana navyo hiyo ni kawaida hata kambi ya adui akivamiwa ghafla ni lazima ijibu mashambulizi kidogo hata kama inajua itakwenda kushindwa..

Ukiwa shuleni, hata mwanya mdogo unaoupata, usipoteze muda…hubiri Habari njema, ukiona mgonjwa mahali mwanya huo ulioupata mnyang’anye shetani hilo teka…Mwombee apone na mhubirie, Ukikutana na mtu mwenye mapepo..itumie hiyo fursa vizuri, ya kuyakemea hayo mapepo yamwondoke na kumweka huru huyo mtu, na kisha Mweleze Habari za Yesu…

Usitazame huyu ni mkubwa kuliko mimi hawezi kunisikiliza, huyu ana elimu kuliko mimi, huyu ana heshima kuliko mimi, anavaa vizuri kuliko mimi, ni mwalimu wangu, ni kiongozi wangu, au nimekutana naye tu siku ya kwanza usiyaangalie hayo hata kidogo.. Kwasababu silaha ulizo nazo zina NGUVU! Kuifanya kila Fikra imtii Kristo. Wapo maprofesa waliobadilishwa fikra zao wakamtii Kristo na watu ambao hawajasoma hata darasa moja..Wapo maraisi waliowekwa huru na injili ya watu ambao hawajasoma hata darasa moja. Wapo waliokuwepo sugu lakini leo hii ni watumishi wa Mungu. Kwahiyo vaa silaha na ingia kazini..

Nguvu ile ile iliyokubadilisha wewe ndiyo hiyo hiyo itakayowabadilisha na wengine..wewe mpaka umemtii Kristo ni kwasababu Kristo alimtumia Mtumishi wake kuja kumnyang’anya shetani wewe ambaye ulikuwa mtumwa wake…Na baada ya kumpokonya shetani ndipo akakufanya wewe kuwa TEKA lake. Na hakuishia hapo akakupa na wewe Kipawa (yaani karama)..ambayo ni silaha na kazi yake mojawapo ni kwenda na wewe kuteka mateka mengine na kuyaleta kwa Kristo.

Waefeso 4:7 “Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo.

8 Hivyo husema, Alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa”.

Hivyo kama umempa Kristo Maisha yako…ni jukumu lako kwenda kuteka mateka…kwasababu tayari silaha unayo…kama ni mtaani ingia anza kuhubiri, na utaona matokeo, kama ni shuleni ni hivyo hivyo, kama ni kusafiri huko na huko fanya hivyo kwa nguvu zote kwa karama Mungu aliyoiweka ndani yako, kama ni katika mahospitali na magereza..usikawie kawie..Nenda kwasababu Mungu atakuwa Pamoja nawe siku zote kukuongoza… yakumbuke haya maneno ya Yesu mwenyewe Bwana wetu aliyoyasema..

Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.

19 Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;

20 na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; NA TAZAMA, MIMI NIPO PAMOJA NANYI SIKU ZOTE, HATA UKAMILIFU WA DAHARI”

Atakuwa Pamoja na wewe hata ukamilifu wa dahari!…dahari maana yake ni nyakati/wakati….Hivyo hapo maana yake ni kwamba ameahidi kuwa “Pamoja nasi mpaka mwisho wa nyakati”…Lakini hiyo ni kama tutaondoka na kwenda kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi…na kuwafanya kuwa mateka wa Kristo.

Bwana atusaidie kumuamini..

Kumbuka pia katika kwenda kuhubiri kuwa mwaminifu na kuwa na nia ya Kristo, sio nia ya kuwa maarufu au kutafuta fedha, bali ya kutafuta roho za watu…huku ukijua kuwa una thawabu yako mbinguni na Kristo anakuja upesi..

Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.

13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

MKUU WA UZIMA AKUWEKE HURU.

Kuungama ni nini?

UTASIMAMA PEKE YAKO SIKU ILE.

Katika biblia Neno “Mshenzi” linatajwa.Kwanini liwekwe?

KUTAKUWA NA MATETEMEKO YA NCHI, NJAA NA TAUNI.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

USIPUNGUZE MAOMBI.

Rudi Nyumbani:

Print this post