JIFUNZE KUDUMU UWEPONI MWA MUNGU.

JIFUNZE KUDUMU UWEPONI MWA MUNGU.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tena tuyatafakari maneno matukufu ya mola wetu. Leo napenda tuutafakari huu mstari kwa ukaribu sana, kwasababu una maana kubwa nyuma yake huwenda tofauti na vile tunavyoufahamu.

Biblia inasema..

Mithali 23:29 “Ni nani apigaye, Yowe? Ni nani aliaye, Ole? Ni nani mwenye ugomvi? Ni nani mwenye mguno? Ni nani aliye na jeraha zisizo na sababu? Ni nani aliye na macho mekundu?

30 NI WALE WAKAAO SANA KWENYE MVINYO; Waendao kutafuta divai iliyochanganyika”.

Mwandishi anaeleza matokeo, ya mtu kufikiwa na hayo mambo yote sita(6) mabaya kwa mpigo ni nini.. Yaani Yowe, ole, ugomvi, mguno, jeraha zisizo na sababu, na macho mekundu.. ni nini..

> Anaposema Yowe, sote tunafahamu, mpaka mtu apige yowe, ni matokeo ya kakumbwa na jambo baya sana, ambalo linamfanya ahitaji msaada wa haraka sana, pengine labda anafukuzwa auawe,  au anapigwa vikali , au amekumbwa na taarifa za kushtusha sana..Hivyo kwa kawaida hakuna yowe inayotokana na mema.

> Vilevile anaposema ni nani aliaye ole..Tunafahamu ole ni baada ya kutahadharishwa kwa mabaya. Lakini mpaka mtu analia ole, “kusema ole wangu mimi,” ni mtu ambaye tayari ameshakumbwa na mabaya hayo,aidha vifungo, magonjwa, taabu, mateso n.k.

> Halikadhalika anaposema, ni nani mwenye mguno; Anamaanisha mtu mwenye malalamiko, mwenye maneno yasiyofaa, au kueleweka, mtukanaji, mtu wa kashfa. Jambo hili nalo haliji kutoka katika mema.

> Vilevile aliye na jeraha zisizo na sababu, ni mtu aliyejiingiza katika matatizo ambayo hakustahili au hakupaswa kukumbwa nayo. Pengine amrukwa na akili, au uzembe uliopitiliza usio wa kibinadamu.

> Anaposema tena ni “nani mwenye ugomvi”..Yaani mtu anayezua ugomvi, malumbano, yasiyo na maana au sababu, kufoka, na ukorofi.

> Na pia mwenye macho mekundu, .Yaani macho yaliyolegezwa na pombe.

Sasa ukisoma kwa makini, vyote hivyo sita (6), haviji hivi hivi kwa wanywaji pombe kidogo, wanaweza wakafikia kiwango Fulani..Lakini mpaka tabia hizo zitokee kwa mlevi ni lazima awe ni mtu wa “KUKAA SANA KWENYE MVINYO” kama maandiko yanavyosema..Walevi waliopitiliza, ndio huwa wanaanguka mitaroni na kujiumiza miza wenyewe ovyo bila sababu, ndio wenye macho yaliyolegea mpaka kuwa mekundu, ndio wanaopiga piga makelele njiani na majumbani, ndio wanaopata hasara ya mali zao, na kupiga mayowe, anayetapika ovyo n.k… Hii hali mpaka afikie mtu, ni lazima atukuwa mule mlevi wa kishinda kilabuni usiku kucha.

Hii inafunua nini?

Ni kutuonyesha jinsi kitu chenye ulevi kinapotumiwa kwa muda mrefu na sanaa, kinavyoweza kuleta matokeo yakubwa Zaidi..

Lakini biblia inatuambia kuwa  ipo DIVAI MPYA. Ambayo sisi wakristo, tunakunywa na katika hiyo, tunalewa. Lakini kanuni ni ileile hatutaweza kulewa vema na kutoa matokeo yake, kama hatutakaa sana katika kuinywa..

Na divai yenyewe si mwingine Zaidi ya ROHO MTAKATIFU.

Siku ile ya Pentekoste mitume walipojazwa Roho Mtakatifu, walionekana kama walevi, waliolewa kwa mvinyo mpya..Kumbe hawakujua kuwa alikuwa ni Roho Mtakatifu kawafanya vile. Kuonyesha kuwa Roho naye huwa anawalewesha watu wake pia katika roho.

Matendo 2:12 “Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?

13 Wengine walidhihaki, wakisema, wamelewa kwa mvinyo mpya.

14 Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu.

15 Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana;

16 lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli,

17 Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto”.

Na matokeo ya kuleweshwa kisawasawa na Roho Mtakatifu, ni kutoa matunda yake.. ambayo tunayasoma katika, Wagalatia 5:22 na pia kufanya kazi kama za mitume, walizofanya baada ya kupokea Roho..

Wagalatia 5:22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”.

Hivyo hatuwezi kuwa na Upendo, kama hatutakaa sana uweponi mwa Mungu tulewe mema yake kisawasawa, hatutakaa tufikie furaha timilifu, kama tutakuwa tunamtafuta Mungu jumapili kwa jumapili, na sio muda wote.. Hatutakaa tuwe na kiasi, na upole na amani, kama hatujibidiishi, kuutafuta uso wa Mungu, kwa wakati mrefu. Hatuwezi kuzidhihirisha karama za Roho kama hatutampa muda wa kutosha mioyoni mwetu.

Tukae sana kwenye mvinyo wetu (Roho Mtakatifu), ili tumzalie Bwana matunda ya haki.

Hivyo, tukiwa na bidii katika Mungu, kusali, kufunga, kutafakari sana, maneno ya Mungu Pamoja na wapendwa wenzetu, Kidogo kidogo tunakuwa walevi, na kwa jinsi tunavyozidisha ndivyo tutakavyoyatoa hayo matunda ya Roho kirahisi sana ndani yetu.

Hivyo sote kwa Pamoja tuanze kuzidisha bidi zetu kwa Bwana. Ili Bwana naye apate nafasi ya kutuponya

Bwana akubariki.

Ikiwa hujaokoka, kumbuka kuwa hizi ni siku za mwisho, siku yoyote Yesu anarudi kulinyakua kanisa lake. Kumbuka injili iliyobakia sasa sio ya kubembelezewa wokovu, ni wewe mwenyewe kuona hali halisi na kujiokoa nafsi yako. Ikiwa upo tayari kutubu leo na kumpa Yesu Maisha yako, basi utakuwa umefanya uamuzi wa busara, katika dakika hizi za majeruhi tulizopo.

Hivyo kama utapenda kupata msaada huo. Basi wasiliana nasi kwa namba zetu hizi, ili tuweze kuomba na wewe na pia kukuongoza sala ya Toba (Bure). >>> +255693036618/  +255789001312 .

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Nini maana ya “Siku moja nyuani mwa Bwana ni bora kuliko siku elfu”?

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Mapooza ni nini? Na je! Twawezaje kuepukana nayo?

Kwanini Bwana Yesu alisema “Msimwamkie mtu njiani”?

Roho Mtakatifu ni nani?

Bwana alimaanisha nini kusema “kila mtu atatiwa chumvi kwa moto”

Je! Bwana Yesu alikunywa kileo mpaka watu wakasema ni mlafi na mlevi? Kulingana na Mathayo 11:19?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Daudi Sagara
Daudi Sagara
2 years ago

kazi yenu ni njema sana watumishi wa Mungu

Anonymous
Anonymous
2 years ago

Mungu awabariki sana nimepokea kitu