USIISHIE TU KUPATA HAKI, BALI PATA NA WOKOVU.

USIISHIE TU KUPATA HAKI, BALI PATA NA WOKOVU.

Jina kuu la Bwana na Mwokozi wetu, Yesu Kristo libarikiwe!. Karibu tuyatafakari maandiko,

Neno la Bwana wetu, lililo chakula cha roho zetu linasema hivi..

Warumi 10:10 “Kwa maana KWA MOYO mtu huamini HATA KUPATA HAKI, na KWA KINYWA hukiri HATA KUPATA WOKOVU”.

Ipo sababu kwanini Biblia imetenganisha hayo mambo mawili, HAKI na WOKOVU. Watu wengi leo wameishia kupata HAKI tu, lakini si WOKOVU.. Wapo wengi leo waliomwamini Bwana Yesu mioyoni mwao na kuishia kupata haki sawasawa na Warumi 5:1 na Wagalatia 2:16, lakini hawana WOKOVU, maishani mwao, Na Wokovu unakuja kwa kumkiri Yesu na maneno yake kwa kinywa!.

Wakati Bwana Yesu akiwa duniani, walikuwepo Mafarisayo na wakubwa wengi waliomwamini mioyoni mwao, lakini katika Vinywa vyao, hawakumkiri..na hivyo Imani yao ikahesabika si kitu!.

Yohana 12:42 “Walakini hata katika wakuu WALIKUWAMO WENGI WALIOMWAMINI; lakini kwa sababu ya Mafarisayo HAWAKUMKIRI, wasije wakatengwa na sinagogi”.

Umeona?. walivifunga vinywa vyao, kuhofia kutengwa na dini zao, au madhehebu yao, au wakubwa wenzao, au kuonekana washamba na waliorukwa na akili!!..

Ndugu unapomwamini Bwana Yesu na maneno yake, ndani ya moyo wako, hiyo bado haitoshi kukupa wewe wokovu.. Huna budi kumkiri kwa kinywa chako kila siku katika Maisha yako..  Wokovu wa siri siri, na wakujificha ficha huo sio wokovu kibiblia!!.. Bwana Yesu alisema mtu yeyote akimwonea yeye na maneno yake, yeye naye atamwonea haya mtu huyo mbele za baba yake na malaika zake.

Luka 9:26 “Kwa sababu kila ATAKAYENIONEA HAYA MIMI NA MANENO YANGU, Mwana wa Adamu ATAMWONEA HAYA MTU HUYO, atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu”.

Soma tena..

Mathayo 10:32 “Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, NAMI NITAMKIRI MBELE ZA BABA YANGU ALIYE MBINGUNI”.

Umeona?..kumbe unaweza kuwa umemwamini Bwana Yesu moyoni mwako, lakini kwasababu tu! Humkiri maishani mwako, siku ile naye akakukana!!..kumbe wokovu wetu unakamilika pia kwa kumkiri Bwana Yesu.

Wakati Fulani, Bwana Yesu alimponya kipofu mmoja, ambaye alizaliwa katika hali hiyo ya upofu.. Na baada ya kumponya..Wazazi wake yule kipofu, walimwamini Bwana Yesu kuwa ni Kristo, lakini kwa hofu ya kutengwa hawakumkiri kwa vinywa vyao, lakini mwanao ambaye alikuwa kipofu, alimwamini Bwana Yesu na kumkiri..

Yohana 9:18 “Basi Wayahudi hawakusadiki habari zake, ya kuwa alikuwa kipofu, kisha akapata kuona; hata walipowaita wazazi wake yule aliyepata kuona.

19 Wakawauliza wakisema, Huyu ndiye mwana wenu, ambaye mnasema kwamba alizaliwa kipofu? Amepataje, basi, kuona sasa?

20 Wazazi wake wakawajibu, wakasema, Tunajua ya kuwa huyu ndiye mwana wetu, tena ya kuwa alizaliwa kipofu;

21 lakini jinsi aonavyo sasa hatujui; wala hatujui ni nani aliyemfumbua macho. Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima; atajisemea mwenyewe.

22 Wazazi wake waliyasema hayo kwa sababu WALIWAOGOPA WAYAHUDI; kwa maana Wayahudi walikuwa wamekwisha kuafikiana kwamba MTU AKIMKIRI KUWA NI KRISTO, ATATENGWA NA SINAGOGI.

23 Ndiyo sababu wale wazazi wake walisema, Ni mtu mzima, mwulizeni yeye”.

Umeona hawa wazazi, walikuwa na Imani mioyoni mwao, lakini Imani yao haikuwasaidia..Bwana Yesu hakuwafuata…lakini mbele kidogo, utaona Bwana anamfuata yule kipofu, na kujidhihirisha kwake kwasababu alimkiri..

Yohana 9:33 “Kama huyo asingalitoka kwa Mungu, asingeweza kutenda neno lo lote.

34 Wakajibu, wakamwambia, Ama! Wewe ulizaliwa katika dhambi tupu, nawe unatufundisha sisi? Wakamtoa nje.

35 YESU AKASIKIA KWAMBA WAMEMTOA NJE; NAYE ALIPOMWONA ALISEMA, WEWE WAMWAMINI MWANA WA MUNGU?

36 NAYE AKAJIBU AKASEMA, NI NANI, BWANA, NIPATE KUMWAMINI?

37 YESU AKAMWAMBIA, UMEMWONA, NAYE ANAYESEMA NAWE NDIYE.

38 AKASEMA, NAAMINI, BWANA. AKAMSUJUDIA”.

Leo Bwana Yesu ajidhihirishi kwa wengi, kwasababu hiyo moja tu!.. ya KUTOMKIRI YEYE!!.. Tunampenda na kumwamini kweli Yesu, lakini hatuwezi kumkiri mbele ya mabosi zetu, hatuwezi kumkiri mbele ya wanafunzi wenzetu, hatuwezi kumkiri mbele ya wafanyakazi wenzetu, hatuwezi kumkiri mbele ya ndugu zetu…huku tukidhani kuwa ndio tunao wokovu..kumbe bado hatuna wokovu!!!.

Vile vile ukiyaonea haya maneno yake yote ya kwenye biblia..bado hauna wokovu!!.. Haijalishi unalijua Neno kiasi gani, au unaijua biblia kiasi gani…

Siku zote kumbuka hilo, Wokovu wetu unakamilika na KUMKIRI BWANA YESU NA MANENO YAKE!!!!..(Usilisahau hilo kamwe).

Warumi 10:8 “Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, KATIKA KINYWA CHAKO, na katika MOYO WAKO; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo.

9 Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka

10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu”

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

HIZO NDIZO ROHO ZA MASHETANI.

USIMLAANI KIZIWI, WALA USITIE KWAZO MBELE YA KIPOFU.

Kama tunaokolewa kwa neema kwanini wokovu tuupate kwa nguvu?

Ni nani aliye kipofu, ila mtumishi wangu?

NJIA YA KUPATA WOKOVU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Gloire bahati
Gloire bahati
1 year ago

Nafaidika sana mungu awabariki

Raphael Biachu
Raphael Biachu
1 year ago

I’m very much inspired by the deep revelation of God’s Word, be blessed men of servants of God. Kindly if you still have copies of the book of Revelation. Uchambuzi wa kitabu cha Ufunuo mwanzo hadi mwisho kwa email yangu nitashukuru sana. Nilihifadhi japo ilipotea, naomba huo msaada tafadhali. Nko Dubai kikazi, Shalom