Nakusalimu katika jina kuu lenye uweza la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tujifunze maneno ya Mungu ambayo ndio uzima wetu.
Mungu ana njia nyingi za kuzungumza, anaweza kutumia ufunuo wa roho, anaweza kutumia Neno, anaweza kutumia maono anaweza kutumia mambo ya asili au matukio. Lakini si wakati wote Mungu ataleta majibu kwa kupitia njia hizo. Haijalishi utakuwa ni wa kiroho kiasi gani. Ipo njia nyingine ambayo Mungu huitumia na hiyo tusipoifahamu vema, tutapata hasara ya mambo mengi kama sio kupotea kabisa. Na njia yenyewe ni kupitia mashauri yetu sisi wenyewe tunapokuwa wengi pamoja..
Kwamfano embu tafakari hivi vifungu;
Mithali 11: 14 “Pasipo mashauri taifa huanguka; Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu”
Maana yake ni nini? Kwamba taifa linapokataa maoni, mapendekezo, mawazo mbalimbali, kutoka kwa wananchi wake, kamwe taifa hilo haliwezi kufanikiwa,
Maandiko bado yanasema..
Mithali 15: 22 “Pasipo mashauri makusudi hubatilika; Bali kwa wingi wa washauri huthibithika”.
Mithali 24:6 “Maana kwa mashauri ya akili utafanya vita; Na kwa wingi wa washauri huja wokovu”.
Maana yake ni nini? Kwamba palipo na vita, ni lazima yawepo maono ya askari wengi, ni jinsi gani watapambana na adui yao, huyu anasema hivi, Yule vile, na mwisho wa siku linatoka jawabu moja madhubuti ambalo litaleta mafanikio makubwa, lakini ikiwa pendekezo linatoka kwa mmoja tu yaani yule mkuu wa kikosi, ni dhahiri kuwa jeshi, litakuwa dhaifu, na matokeo yake ni kupigwa..
Amen.
Hili ni jambo la muhimu sana kwa sisi tulio wakristo. Bwana Yesu aliposema tuwe na umoja, tunie mamoja, alijua kabisa atatumia njia hiyo kuleta majibu ya mambo mengi pasipo hata kusubiria mafunuo au maono.
Utauliza jambo hili lilifanyika wapi katika kanisa kwenye agano jipya.
Utakumbuka, Paulo na Barnaba walipokwenda kuhubiri injili kwa watu wa mataifa, walitokea wayahudi kadha wa kadha, wakaanza kuwaambia mataifa kuwa msipotahiriwa ninyi hamwezi kuokoka()..Hivyo jambo hilo likaleta mkanganyiko mkubwa sana, ikawabidi hadi Paulo na Barnaba warudi Yerusalemu wakasikilize mitume na wazee wanasema nini juu ya hilo.
Hivyo walipofika Yerusalemu, akina Petro na wazee, waliitisha baraza, na kuanza kulitathimini jambo hilo. Je ni sawa watahiriwe na kuishika torati ya Musa au sio sawa.. Sasa maandiko yanatuambia walihojiana sana, huyu anasema hivi, yule vile (Lakini katika amani na upendo, na sio katika mashindano).. na matokeo yake Roho wa hekima akaingia ndani yao, likapatikana shauri moja thabiti. Na kwa kupitia hilo kanisa la mataifa likathibitika sana kwa waraka waliowaandikia, likaenenda katika furaha ya Roho Mtakatifu daima.
Embu tusome pale kidogo, litusaidie…
Matendo 15:7 “NA BAADA YA HOJA nyingi Petro akasimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu, na kuliamini.
8 Na Mungu, ajuaye mioyo ya watu, akawashuhudia, akiwapa Roho Mtakatifu vile vile kama alivyotupa sisi;
9 wala hakufanya tofauti kati yetu sisi na wao, akiwasafisha mioyo yao kwa imani…..
13 Na hao walipokwisha kunyamaza Yakobo akajibu, akisema, Ndugu zangu, nisikilizeni.
14 Simeoni ametueleza jinsi Mungu hapo kwanza alivyowaangalia Mataifa ili achague watu katika hao kwa ajili ya jina lake.
15 Na maneno ya manabii yapatana na hayo, kama ilivyoandikwa, 16 Baada ya mambo haya nitarejea, Nami nitaijenga tena nyumba ya Daudi iliyoanguka. Nitajenga tena maanguko yake, Nami nitaisimamisha;”
Kwa muda wako isome habari yote katika kitabu hicho cha Matendo ya mitume sura ya kumi na tano (15),
NINI BWANA ANATAKA SISI TUJUE KAMA KANISA?
Lazima tujifunze wakati mwingine tuwe watu wa Hoja nyingi, mapendekezo mengi, (lakini katika upendo na amani), ili kanisa lijengwe, ili injili ihubiriwe katika ufasaha wote. Kama tulivyosoma hapo juu inavyosema.. “kwa mashauri ya akili utafanya vita; Na kwa wingi wa washauri huja wokovu.” Hatutaweza kushindana na shetani kama tutakuwa hatuna mikakati, na mipango ya mara kwa mara,.
Kila kiungo katika mwili wa Kristo, kina nafasi ya kuchagia mashauri mema. Hivyo tujifunze njia hii, ili Mungu azungumze na sisi. Lakini tukikosa mapatano, “Taifa huangamia”..Sisi hatutaangamia kwa kutii agizo hili.
Bwana alibariki kanisa lake.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Kuwaogopa wanadamu huleta mtego,(Mithali 29:25)
Ni kwa namna gani, upendo husitiri wingi wa dhambi? (1Petro 4:8)
Na ulimi laini huvunja mfupa.(Mithali 25:15)
JE! NINAWEZA KUPOTEZA FURAHA YA WOKOVU?
Kama tunaokolewa kwa neema kwanini wokovu tuupate kwa nguvu?
About the author