Wanefili walikuwa ni watu gani?

Wanefili walikuwa ni watu gani?

Wanefili tunawasoma kwa mara ya kwanza katika kitabu cha Mwanzo 6:4, Tusome..

Mwanzo 6:4 “Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile; tena ,baada ya hayo ,wana wa Mungu walipoingia kwa binti za binadamu,wakazaa nao wana; HAO NDIYO WALIOKUWA WATU HODARI ZAMANI ,WATU WENYE SIFA.

5 Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.”

Sasa tafsiri ya wanefili ni “watu wakubwa”.. yaani watu wenye maumbo makubwa. Hivyo wanefili walikuwa ni watu wenye miili makubwa sana.. Na biblia inaendelea kusema kuwa walikuwa ni WATU HODARI na WENYE SIFA. Maana yake walikuwa ni watu wenye uwezo mkubwa wa kiakili na vile vile walikuwa ni watu wenye sifa (maaana yake maarufu na wanaojulikana sana). Hivyo hawakuwa tu wakubwa kama tembo halafu hawana akili, hapana! Walikuwa wakubwa na vile vile walikuwa na uwezo mkubwa wa kiakili, ambao uliwafanya wawe maarufu.

Sasa asili ya hawa wanefili ilianzia kwa Kaini. Ikumbukwe kuwa Kaini baada ya kumuua ndugu yake, alilaaniwa na Mungu, na baada ya ile laana, Mungu alimtia alama Kaini ili yeyote atakayemwona asimuue.

Mwanzo 4: 13 “Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki.

  14 Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua.

 15 Bwana akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. BWANA AKAMTIA KAINI ALAMA, MTU AMWONAYE ASIJE AKAMPIGA.

 16 Kaini akatoka mbele za uso wa Bwana, akakaa katika nchi ya Nodi, mbele ya Edeni”

Umeona hapo? Kaini anatiwa alama na Mungu, ili kila atakayemwona asimpige!.. Sasa alama hiyo aliyotiwa na Mungu sio mchoro Fulani katika mwili, hapana bali ni UKUBWA WA MWILI NA AKILI, hiyo ndiyo alama aliyowekewa Kaini na Mungu, ambayo itakuwa kwake kama ulinzi, kila atakayemwona na kujaribu kumdhuru aogope!..  kwa kawaida ni ngumu kujaribu kupambana na mtu aliyekuzidi ukubwa!

Kwahiyo Uzao wa Kaini, Mungu aliupa akili na ukubwa, ingawa ulikuwa umelaaniwa..Laana ile ilimfanya Kaini na uzao wake kuacha kazi zao za ukulima, kwasababu walishalaaniwa, na kuanza kufanya kazi nyingine za ufugaji na utengenenezaji wa bidhaa..Ndio maana ukiendelea mbele kidogo kusoma utaona wana wa Kaini wanajishughulisha na utengenezaji wa vyuma na shaba na bidhaa nyingine, kama vifaa vya muziki n.k. (Mwanzo 4:22)

Hivyo kwa shughuli hizo zikawafanya wawe watu maarufu sana duniani na hodari, wakajenga miji mikubwa, na wakawa na ustaarabu wao, wakazaliana wao kwa wao, na wakafanyiana biashara wao kwa wao kwa hizo bidhaa zao na hivyo wakawa na ngome kubwa duniani…

Kutokana na ngome yao kuwa kubwa, na ukubwa wa teknolojia yao, maana ndio watu wa kwanza kugunudua vyuma, shaba na madini mengine yote,  na zana zote za kazi, ni wazi kuwa jamii nyingine za watu ziliwaogopa.. (ili litimie neno la Bwana kwamba kila atakayemwona Kaini asimuue) na pengine walijiwekea sheria ya kwamba yeyote atakayemuua mtu yeyote wa jamii ya uzao wa Kaini adhabu yake ni “kulipiziwa kisasi mara saba”, kwasababu wao ndio walikuwa hodari na wenye nguvu kuliko wengine wote. Ni sawa na wakati wana wa Israeli wapo Misri utumwani, ni wazi kuwa ilikuwa ni kosa kubwa sana kwa mwisraeli aliye mtumwa kumuua Mmisri, pengine adhabu yake ilikuwa ni kubwa sana!. Au wakati wa kipindi cha ukoloni,barani Afrika, inawezekana ilikuwa ni adhabu kubwa sana, mtu mweusi kumuu mtu mweupe!, kutokana na nguvu walizokuwa nazo watu weupe!.. Ndicho kilichokuwa kinaendelea katika dunia ya wakati wa Nuhu.

Lakini wakati huo huo uzao wa Sethi ambao Mungu aliuweka ili kuziba pengo la Habili, ulikuwa ni wa watu wakawaida wakulima na vile vile wafugaji. Uzao huu haukulaaniwa, ndio WANA WA MUNGU tunaowasoma katika Mwanzo 6:2. Na walikuwa ni watu wenye Miili ya wastani, (kwaufupi ni watu wa kawaida tu), na hawakuwa hodari kama hawa Wana wa Kaini (Wanefili).. uzao wa Kaini ndio ulioitwa WANA WA WANADAMU na wanawake wao Binti za Wanadamu (Mwanzo 6:2)

Hivyo wana wa Mungu walipowatamani hao binti za wanadamu na kuwaoa, jambo hilo likamchukiza Mungu, kwasababu ni dhahiri kuwa waliwageuza mioyo, wakapunguza au wakaacha kabisa kumtumainia Mungu wa mbingu na nchi. Hivyo dunia ikajaa dhuluma, kukawa hakuna tena watu wanaomcha Mungu..

Kwahiyo wanefili walikuwa ni wanadamu, ambao ni uzao wa Kaini, na si (mchanganyiko wa wanadamu na malaika), biblia inasema Malaika hawaoi wala hawaolewi (Marko 12:25).

Lakini hata leo hawa wanefili wapo!. Wanaweza wasiwe wakubwa kimwili lakini ni wakubwa kiulimwengu!. Watu wenye sifa na hodari, ambao wanaweza kutengeneza ala za miziki ambazo zinaweza kuiteka dunia nzima, ambao wanaweza kutengeneza filamu na ikakomba watu wengi, ambao wanaweza kutunga mitindo wa mavazi ikaharibu mamilioni ya wanawake, ambao wanaushawishi mkubwa wa kimawazo ambayo ni kinyume na mapenzi ya Mungu, hao ndio wanefili wa kipindi hichi…

Na biblia inasema kama zilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa siku za kuja kwake mwana wa Adamu (Luka 17:26). Siku za Nuhu wana wa Mungu waliwatamani binti za wanadamu.. kadhalika siku hizi wana wa Mungu (wakristo) wanawatamani binti za wanadamu (wanawake wa kiulimwengu), na wanawake wa kikristo wanawatamani wana wa ulimwengu huu, na kujitafutia wanaume wanaowataka!, pasipo hata kujali vigezo vya kibiblia. Jambo ambalo ni machukizo mbele za Mungu kwasababu watawageuza mioyo na kuwafanya wamwache Mungu. Ndicho kilichotokea wakati wa Nuhu.

Binti wa Mungu, jiepushe na tamaa za ulimwengu huu.. Furaha pekee ya maisha utaipata kwa Yesu na si kutafuta kuoelewa na mtu asiyemcha Mungu, huyo atakugeuza moyo wako umwache Mungu, maandiko yanasema hivyo. (1Wafalme 11:2-4)

Kijana uliyemwamini Yesu, jiepushe na wanawake wa kidunia, usiitamani mitindo yao, wala mionekano yao…hao watakugeuza moyo, kama walimgeuza Sulemani aliyekuwa na Hekima kuliko watu wote, hawatakushindwa wewe!!. Hivyo Kabla ya kukimbilia kuoa, ni heri ukambadilisha kwanza ampokee Yesu Yule Yule uliyempokea wewe, na awe na imani ile ile uliyonayo wewe, na ubatizo ule ule ulionao wewe, na Roho Mtakatifu Yule Yule uliyenaye wewe (Waefeso 4:5). Vinginevyo utakuwa unajiharibia mwenyewe.

Hivyo kwa hitimisho ni kwamba wanefili walikuwa ni majitu, hawakuwa na habari na Mungu isipokuwa mambo ya ulimwengu huu!. Walikuwepo wakati wa Nuhu, na baada ya Nuhu walikuwepo na hata leo wapo!

Bwana atubariki na kutulinda.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

WANA WA MUNGU, NA BINTI ZA WANADAMU.

MWANZO WA INJILI YA YESU KRISTO.

MUNGU HAONI SHIDA KUMUHAKIKISHIA MWOVU ULINZI.

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
AMOS PAUL
AMOS PAUL
2 years ago

Barikiwa sana kwa ufafanuzi. Nimebarikiwa.