CHUKUA MZIGO WA MWINGINE.

CHUKUA MZIGO WA MWINGINE.

Katika Biblia kuna mahali panasema… “Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo (Wagalatia 6:2)”.

Lakini Biblia hiyo hiyo mbele kidogo katika mstari wa 6 inasema “Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe (Wagalatia 6: 5)”.

Ni rahisi kuona kama biblia inajichanganya lakini sio kweli, biblia sikuzote ipo sawa,.Isipokuwa tu Mungu anahitaji tupate msaada wake katika kuyatafakari maandiko yake.

Biblia iliposema kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe…Ilikuwa inalenga juu ya matendo ya mtu..Kwamba kila mtu matendo yake yatamfuata mpaka siku ile ya hukumu..Na hayo anakuwa ni kama ameyabeba…atayabeba yeye peke yake na atasimama nayo mbele ya kiti cha Hukumu siku ile akiwa peke yake. Hivyo matendo ya mtu yanafananishwa na FURUSHI!.

Kadhalika Biblia iliposema tuchukuliane mizigo ilimaanisha tusaidiane sisi kwa sisi..Maana yake tukiwa na nguvu tunapaswa tuwasaidie wale wasio na nguvu..Ili tuwe wenye haki mbele za Mungu..na kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeitimiza sheria ya Kristo ambayo ni UPENDO.(Yohana 13:34, 1Yohana 3:17-18).

Katika siku hizi za mwisho Biblia imetabiri kwamba upendo wa wengi utapoa!…Upendo wa watu kumpenda Mungu utapoa, kadhalika na upendo wa watu kupendana wao kwa wao utapoa. Na hivyo kuifanya dunia kuikosa hii sheria ya Kristo ambayo ni UPENDO.

Na biblia imetuasa kuwa kuna upendo wa Ulimi na upendo wa tendo.

1Yohana 3: 17 “Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?

18 Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli”

Kwahiyo kama tumeokoka ni lazima tuitimize hiyo sheria ya Kristo. Tupendane kama matendo kama yeye alivyotupenda sisi. Sio tu kumuombea au kumuhurumia bali pia kutenda.

Na pendo hilo pia ni pamoja na KUCHUKULIANA MIZIGO.

Unaposikia mpendwa mwenzako ana tatizo hili au lile na unajua kabisa yupo katika shida ambayo hawezi kuzungumza..Usisubiri yeye akuambie wewe chukua hatua ya kwenda kumsaidia tatizo lake. Ukiona ndugu yako ni mgonjwa pamoja na kumwombea chukua hatua ya kwenda kumtazama, kumfariji na hata kumhudumia. Usiangalia wewe ulipokuwa na matatizo alikuja kukutafuta au la!..kuwa kama kipofu kwa mabaya uliyofanyiwa na uwe mkumbukaji wa mazuri aliyowahi kukufanyia…

Wengi wetu hatujui kuwa Neema ya Mungu juu ya Maisha yetu inaongezeka juu yetu siku baada ya siku, na pia inaweza ikapungua juu yetu endapo tukiipuuzia…Unapomsaidia mtu hususani mkristo mwenzako..na ukamsaidia kwa moyo kabisa…

Kuna Neema fulani inakuwa inaongezeka juu yako kiasi kwamba utakavyokuja tena kumsaidia mwingine hutasikia uzito kama ulivyosikia kwa yule wa kwanza…na hivyo hivyo watatu utakuwa mwepesi Zaidi…na kwajinsi unavyoendelea hivyo hivyo ile Neema ya utakatifu inaongezeka juu yako mpaka unafikia hatua kusaidia mtu kwako si jambo kubwa wala kukuwazisha kichwa, linakuwa linatoka lenyewe kama vile pumzi…Na Neema hiyo ya utakatifu inavyoongezeka juu yako inaambatana na Milango mikubwa sana ya Baraka…Kwasababu unakuwa umeshaaminiwa na Mungu sana…

Kwasababu Bwana anajua hata akishusha kwako kiasi fulani cha mali, asilimia 90 ya ile itakwenda kuwasaidia watu wake walioko katika shida..walioko katika uhitaji, anajua kiasi kikubwa cha ile fedha au mali itaenda katika kuiendeleza kazi ya yake…hivyo yule mtu anakuwa kama Bomba la Mungu la kupitishia baraka kwa watu wake…Hivyo na lenyewe haliwezi likakauka maji. Lakini mtu anayejizuia kuchukua mizigo ya wengine mtu huyo anakuwa kama ni bomba lililofungwa…Bomba lililofungwa haliwezi kupokea maji kutoka kwenye chanzo kadhalika haliwezi kujaza ndoo za maji zilizopo chini yake kwenye foleni..lakini lililofunguliwa kwa jinsi linavyotoa ndivyo linavyopokea.

Tenga muda nenda kajaribu kuwatafuta watu waliojizoeza kusaidia watu sana kiasi kwamba hata kutoa chochote kwao si shida..tenga muda wahoji waulize kama walishawahi kupungukiwa..watakupa shuhuda za ajabu sana…

Hivyo hatuna budi leo kujikumbusha jambo hili..ili tuzidi kuielewa Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo inavyofanya kazi.

Warumi 15:1 “Basi imetupasa sisi tulio na nguvu kuuchukua udhaifu wao wasio na nguvu, wala haitupasi kujipendeza wenyewe.

2 Kila mtu miongoni mwetu na ampendeze jirani yake, apate wema, akajengwe.

3 Kwa maana Kristo naye hakujipendeza mwenyewe; bali kama ilivyoandikwa, Malaumu yao waliokulaumu wewe yalinipata mimi”.

Kuwahubiria pia wengine habari za Mungu ni kuwachukulia mizigo yao…Bwana akikupa kitu na kile kitu hutaki kuwashirikisha wengine ukidhani kwamba watajua Zaidi kuliko wewe, au hawatakutaja wewe uliyewashirikisha hapo unajifungia mwenyewe bomba lako la neema. Mungu hawezi kukupa jambo jipya kama lile la zamani hujalitoa..Toa lile la zamani katika hazina yako washirikishe wengine bure! Ili Uweze kupokea lingine lakini ukiwa na moyo wa uchoyo na wivu na hutaki kutoa hazina Mungu aliyoiweka ndani yako kwa muda mrefu, ukisema ufunuo huu ni wangu tu…kamwe usitegemee kubarikiwa kwa vyovyote vile..

Bwana Yesu alisema katika Mathayo 13:52 “Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale”.

Hivyo jizoeze kuwashirikisha wengine habari za Uzima..Umepata kitu fulani ambacho kimekusaidia wewe na umeona kuna wengine kama wewe wengi kinaweza kuwasaidia…huo ndio wakati wa KUWACHUKULIA MIZIGO YAO!..Na watakutaja mbele za Mungu katika maombi yao kwamba uliwasaidia na Mungu atakukumbuka na wewe na kukubariki.

Unaona mpendwa mwenzako anafanya kitu fulani cha kujiendeleza na anahangaika mno na wewe una ujuzi wa kutosha wa namna ya kumsaidia, usingoje akutafute, wala usimwonee wivu..wewe huo ndio wakati wa kumchukulia MZIGO!..Kama umekutana na nafasi za kazi na unaona pengine zitamfaa mtakatifu mwenzako Msaidie hata kama hapo alipo tayari kaendelea kuliko wewe. Wewe timiza wajibu wako kwasababu yupo Mungu juu anayetazama..Na mambo mengine yote ya kimaisha na ya ki-roho…SHERIA YA KRISTO NI ILE ILE UPENDO!! Na KUCHULULIANA MIZIGO.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine:

Mada Nyinginezo:

KWANINI WENGINE WANYAKULIWE,NA WENGINE WAACHWE?

USIMPE NGUVU SHETANI.

INJILI YA KRISTO HAITANGAZWI KWA HATI MILIKI.

IVUMBUE INJILI YA KRISTO KUTOKA KATIKA KILA JAMBO.

KWA KUWA NGUVU ZA MBINGUNI ZITATIKISIKA.

TUUTAZAME PIA MWISHO WA UJENZI WETU.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 7 (Yeremia na Maombolezo)

Je! Ni kweli ubatizo wa maji hatuuhitaji tena?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments