Title 2021

Nini maana ya “Nitaomba kwa roho, tena nitaomba kwa akili pia?

SWALI: Paulo alimaanisha nini kusema…”Nitaomba kwa roho, tena nitaomba kwa akili pia;?

1Wakorintho 14:14 “Maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda.

15 Imekuwaje, basi? Nitaomba kwa roho, tena nitaomba kwa akili pia; mtaimba kwa roho, tena nitaimba kwa akili pia”.


JIBU: Hapa mtume Paulo alikuwa anaondoa mkanganyiko uliokuwa unaendelea katika kanisa kuhusiana na karama za rohoni, hususani karama ya lugha. Na mkanganyiko huu unaendelea hata sasa katika kanisa la Mungu.

Lakini kabla ya  kufahamu mtume Paulo alikuwa anamaanisha nini hasaa hapo, ni vizuri tukajua jinsi hii karama inavyofanya kazi. Lugha zinazozungumziwa katika maandiko, ambazo Roho Mtakatifu anazishusha juu ya mtu kwa jinsi apendavyo yeye, zimegawanyika katika makundi mawili.

Kundi la kwanza: Ni lugha za kibinadamu. Mfano kichini, Kiswahili, kimasai n.k.

Kundi la Pili: Ni Lugha za malaika. Hizi hazijulikani na wanadamu,.

Sasa lengo kuu la hizi  lugha ni kama zifuatavyo:

  1. kulijenga kanisa la Mungu (waliookoka),
  2. kuwavuta watu wengine katika wokovu(ambao hawajaokoka).
  3. Na pia kuwasiliana na Mungu katika roho.

Mtu yeyote akimwomba Mungu ampe kunena kwa lugha, atapewa, (1Wakorintho 14:5)..  Lakini pia haiwezi kuwa wakati wote, au ikaja kwa wepesi kama vile mtu yule aliyejaliwa karama hii na Mungu. Mtu aliyepewa karama hii, inakuwa ni rahisi sana kwake kunena, hususani pale anapoanza tu kuomba, hatumii nguvu nyingi, anashangaa ulimi wenyewe unaanza kuzungumza lugha nyingine gheni. Sasa kwa mtu kama huyu anapaswa kujua hiyo ni sehemu ya karama yake, na hivyo anapaswa aelewe ni nini anatakiwa afanye baada ya pale ili karama hiyo iwe ina manufaa kwa ajili ya kanisa la Mungu.

Sasa, jambo ambalo watu wengi hawajui ni kuwa hizi lugha zinaposhushwa ndani ya mtu, kwa kipindi cha mwanzoni, huwa haziji na tafsiri yoyote, zinakuwa ni kwa ajili ya yule mtu tu husika (mnenaji), na sio kwa kanisa, hapo ndipo utaona mtu anaweza kunena kwa lugha usiku kucha. Lakini kusiwe na kitu chochote unachokielewa yeye, au yule mwingine anayesikia.

Lakini baadaye kama ataichochea karama yake, kwa kumwomba Mungu, amjalie na tafsiri, ndio inapokuja na tafsiri ndani yake. Na hiyo inakuwa ni kwa faida ya kanisa la Kristo. Hivyo mtu ambaye karama yake inatenda kazi ni yule ambaye akinena katika kanisa, basi na Mungu anamfunulia tafsiri ya maneno yale aliyoyanena, kisha analiambia kanisa.. Na kanisa linajengwa, kwasababu hiyo.

Sasa tukirudi katika jambo ambalo Paulo alilisema.. kuhusiana na upungufu wa maarifa kuhusu karama hizi, ni kwamba watu walikuwa wananena kwa lugha mbele ya kanisa, lakini hakuna tafsiri yoyote ile. Ndipo hapo mtume Paulo akasema, Je! Yule anayesikia, ataelewaje?si atakuona wewe ni mwendawazimu? Akaongezea kusema, kama hutakuwa na tafsiri ya lugha hiyo, basi ni heri ukae kimya uombe kivyako vyako. Kuliko kusimama mbele ya kanisa na huku unatoa lugha ambazo hazieleweki kwa wasikiaji.

Ndipo hapo akasema..

Imekuwaje, basi? Nitaomba kwa roho, tena nitaomba kwa akili pia; mtaimba kwa roho, tena nitaimba kwa akili pia..

Yaani, nitaomba kwa lugha, halafu wakati huo huo ninaomba kwa akili zangu, na sio tena tafsiri ya ile lugha niliyoizungumza bali maneno yangu mengine ya sikuzote.. kwamfano, mtu aanze kuzungumza  kiharabu katikati ya mahubiri, bila kutolea tafsiri yoyote halafu anaendelea kuzungumza Kiswahili chake..wewe kama msikiaji utaelewa nini hapo?..

Ndicho kinachoendelea leo hii, mtu atasema ananena kwa lugha, anapohubiri, lakini hatoi tafsiri ya kile anachokisema, anaendelea na maneno yake ya Kiswahili. Katika mazingira kama hayo, wewe msikiaje unajengekaje?

Vilevile Roho Mtakatifu atakujalia kuimba hata wimbo katika lugha nyingine ya rohoni, halafu hutoi tafsiri yake, Je! Msikaji atajengekaje?

Naamini, kama na wewe ni mmojawapo mwenye karama hii, utafanya marekebisho katika hilo. Na kama umekuwa ukinena tu, huoni tafsiri, basi unawajibu wa kumwomba Mungu kwa bidi akupe na tafsiri, pindi uwapo mbele ya kanisa lake. Kwa msingi huu sasa, naomba upitie vifungu hivi hapa chini, ili uelewe Zaidi.

1Wakorintho 14:10 “Yamkini ziko sauti za namna nyingi duniani, wala hakuna moja isiyo na maana.

11 Basi nisipoijua maana ya ile sauti nitakuwa kama mjinga kwake yeye anenaye; naye anenaye atakuwa mjinga kwangu.

12 Vivyo hivyo na ninyi, kwa kuwa mnatamani sana kuwa watu wenye karama za roho, takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa.

13 KWA SABABU HIYO YEYE ANENAYE KWA LUGHA NA AOMBE APEWE KUFASIRI.

14 Maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda.

15 Imekuwaje, basi? NITAOMBA KWA ROHO, TENA NITAOMBA KWA AKILI PIA; MTAIMBA KWA ROHO, TENA NITAIMBA KWA AKILI PIA.

16 Kwa maana wewe ukibariki kwa roho, yeye aketiye katika mahali pa mjinga ataitikaje, Amina, baada ya kushukuru kwako, akiwa hayajui usemayo?

17 Maana ni kweli, wewe washukuru vema, bali yule mwingine hajengwi.

18 Namshukuru Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote;

19 lakini katika kanisa napenda kunena maneno matano kwa akili zangu, nipate kuwafundisha wengine, zaidi ya kunena maneno kumi elfu kwa lugha.

20 Ndugu zangu, msiwe watoto katika akili zenu; lakini katika uovu mgeuzwe watoto wachanga, bali katika akili zenu mkawe watu wazima.

21 Imeandikwa katika torati, Nitasema na watu hawa kwa watu wa lugha nyingine, na kwa midomo ya wageni, wala hata hivyo hawatanisikia, asema Bwana.

22 Basi, hizi lugha ni ishara, si kwao waaminio, bali kwao wasioamini lakini kuhutubu si kwa ajili yao wasioamini, bali kwa ajili yao waaminio”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

FAHAMU TAFSIRI ZA NDOTO MBALIMBALI.

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Nini maana ya “wazimu” katika biblia?

NA VIUNGO VYETU VISIVYO NA UZURI VINA UZURI ZAIDI SANA.

USINIE MAKUU.

Rudi nyumbani

Print this post

JE UNA MATUMAINI YA KUPATA TENA KILE ULICHOPOTEZA?

Jina kuu la Bwana na Mwokozi wetu na wa ulimwengu, Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze Neno la Mungu ambalo ndio taa iongozayo miguu yetu na mwanga wa njia yetu. (Zab 119:105).

Je unafanya kazi yoyote ya mikono?, ya kujiajiri au kuajiriwa?.. labda una shamba, au mifugo, au biashara, ambayo katika hiyo unategemea kukuingizia kipato?…

Je unayo shughuli ambayo ghafla umeshangaa mambo yameharibika!, yameenda kombo!..wakati mwingine unaweza kujiuliza ni nini chanzo, na ukashinda kujua..Leo nataka uone sababu ya mambo hayo kupitia maandiko?

Kama upo ndani ya Kristo, umesimama vizuri na ni mwaminifu kwa Bwana na mambo yamekuharibikia ghafla!, tambua kuwa chanzo ni kama kile kile cha  Ayubu na wala si kingine..

Kwamba Shetani amekwenda kukushitaki mbele za Bwana, kwasababu ya haki yako, na hivyo Bwana akamruhusu aiharibu kazi yako,.. Na majaribu hayo mwisho wake ni mzuri, kwasababu ukiisha kuyashinda basi Bwana atakunyanyua mara dufu.. Ni majaribu ya kuwavusha watu wa Mungu kutoka hatua moja hadi nyingine.

Lakini kama upo nje ya Kristo (Yaani hujampokea Yesu na kumwamini, na kubatizwa, na kuishi maisha ya utakatifu yanayompendeza yeye), na ghafla umeona mambo yako yameharibika, kwa uharibifu usio wa kawaida..nataka nikuambie kuwa jambo ni lile lile lililomtokea Ayubu limekutokea na wewe, isipokuwa katika pande tofauti.

Ni kwamba shetani, au mapepo yake yamekwenda mbele za Mungu na kukushitaki na hivyo kupewa ruhusa ya kuja kuharibu kazi yako, au biashara yako au mifugo yako..na mwisho wa uharibifu huo ni mbaya kwasababu hauna tumaini la kuvipata  tena vile ulivyopoteza.

Sasa hebu tusome habari moja katika biblia ambayo hiyo itatusaidia kuelewa vizuri.. tumsome mtu mmoja tajiri, ambaye alikuwa na biashara yake kubwa ya mifugo lakini iliharibika ghafla na wala hakupata kurejeshewa..

Marko 5:6 “Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia;

7 akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese.

8 Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu.

9 Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi.

10 Akamsihi sana asiwapeleke nje ya nchi ile.

11 NA HAPO MILIMANI PALIKUWA NA KUNDI KUBWA LA NGURUWE, WAKILISHA.

12 PEPO WOTE WAKAMSIHI, WAKISEMA, TUPELEKE KATIKA NGURUWE, TUPATE KUWAINGIA WAO.

13 AKAWAPA RUHUSA. WALE PEPO WACHAFU WAKATOKA, WAKAINGIA KATIKA WALE NGURUWE; NALO KUNDI LOTE LIKATELEMKA KWA KASI GENGENI, WAKAINGIA BAHARINI, WAPATA ELFU MBILI; WAKAFA BAHARINI.

14 Wachungaji wao wakakimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka walione lililotokea”.

Umeona hapo?.. huyu mtu pengine alikuwa tajiri sana mwenye nguruwe wengi (biblia inasema walikuwa nguruwe elfu 2), na akaajiri wachungaji wakawachunge kondoo wale milimani.. Na siku hiyo ghafla anakuja kuletewa taarifa kuwa nguruwe wake wote elfu mbili wamekimbilia baharini na wamekufa huko.

Bila shaka kwa haraka haraka  angeweza kusema ni uchawi, au ana gundu!.. Lakini kumbe kuna jambo lililokuwa linaendelea katika roho juu yake na mali zake bila yeye kujua. Kwamba mapepo yalikwenda kwanza mbele za Bwana Yesu kuomba ruhusa yaingie kwenye kitega uchumi chake, ili yaiharibu kazi yake! Na Bwana Yesu akayapa ruhusa na wala hakuyakataza..

Kama  vile tu!, shetani alivyokwenda mbele za Bwana kuomba ruhusa aharibu mifugo ya Ayubu, na Mungu akampa ruhusa wala hakumkataza.(Ayubu 1:9-12). Ndicho kilichomtokea huyu mtu mwenye nguruwe Elfu 2.

Lakini cha ajabu ni kwamba hatusomi tena habari za huyo tajiri aliyepoteza nguruwe wake, (hao elfu mbili kwa siku moja) kwamba alikuja kuwapata tena.. maana yake ni kwamba hakuja kuwapata tena.. kama ilivyokuwa kwa Ayubu.. Ayubu yeye alipopoteza mifugo yake maandiko yanasema alikuja kupata mara dufu.. Lakini huyu tajiri wa nguruwe hakuna chochote alichoambulia..zaidi ya kupata hasara tu!

Na kinachoshangaza zaidi ni kwamba hata Bwana hakumhurumia wala hakusikitika, yeye kupoteza nguruwe wote wali, Zaidi ya yote aliruhusu mapepo yaingie nguruwe wake.

Sasa ni kwasababu gani hatusomi ushuhuda wowote wa huyu tajiri kuja kupata tena alichokipoteza kama Ayubu?.. Jibu ni rahisi, ni kwasababu hakuwa ndani ya wokovu kama aliokuwa nao Ayubu.. hakutubu!, wala hakumwamini Yesu kabla wala baada ya hapo.. Zaidi ya yote maandiko yanasema wakuu wa miji pengine na yeye akiwemo miongoni mwao, walimfukuza Bwana Yesu atoke katika mipaka yao.

Ndugu unayesoma ujumbe huu, jitafakari je!, hiyo kazi unayoifanya ina usalama kiasi gani?..je upo ndani ya Kristo au nje!.. Unaweza kufikiri mali zako zitakusaidia, au mifugo yako..lakini nataka nikuambie mapepo kila siku yanazitaja hizo mali zako mbele za Mungu.. Na cha kuogopesha ni kwamba Mungu anaweza kuyaruhusu yazichukue au waziue ndani ya siku moja..

Kwasababu kama aliruhusu kwa mtumishi wake Ayubu, ambaye alikuwa mkamilifu mbele zake, wewe na mimi ambaye pengine si wakamilifu mbele zake ni wakina nani, Mungu asiruhusu mabaya hayo?

Jiulize je!, siku ya uharibifu itakapokuja ghafla kama ilivyokuja kwa huyu Tajiri wa nguruwe na Ayubu, utakuwa wapi?.. utakuwa na tumaini kama Ayubu au utapotea moja kwa moja kama huyu Tajiri.

Kama bado hujampokea Yesu, ni vyema ukampokea sasahivi, kwa usalama wa Roho yako na watoto wako, na mali zako na mifugo yako. Kwani usipofanya hivyo kuna hatari ya kukosa tumaini katika siku za kujaribiwa.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Kwanini Bwana aliwalenga mbwa na nguruwe tu katika Mathayo 7:6?

Nini maana ya “kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi?”

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).

KWANINI MIMI?

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

Rudi nyumbani

Print this post

Je ni sahihi kumwita mtu “Mkuu”?

Katika Mathayo 9:2 tunasoma Bwana anamwita “Mkuu” Yule mtu aliyepooza ?.. Je ni sahihi na sisi kuitana wakuu?


Jibu: Tusome,

Mathayo 9:2 “Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye Yesu, alipoiona imani yao, ALIMWAMBIA YULE MWENYE KUPOOZA, JIPE MOYO MKUU, MWANANGU, umesamehewa dhambi zako”.

Hapo ukisoma vizuri utaona Bwana hakumwita Yule mtu “Mkuu”.. Bali alimaanisha “ajipe Moyo Mkuu” yaani “moyo ulio mkuu”. Kwahiyo ni moyo mkuu ndio uliotajwa hapo, na si Mkuu kama mtu. Kristo hana Mkuu juu yake zaidi ya Baba, hivyo hawezi kumwita mtu yeyote  duniani Mkuu,  zaidi sana anatuita sisi WANAWE,  kama mwishoni hapo alipomalizia.. “jipe moyo mkuu, MWANANGU, umesamehewa dhambi zako”

Kadhalika biblia haijaruhusu sisi kwa sisi kuitana “Wakuu”, kwasababu aliye Mkuu wetu sisi sote ni mmoja tu naye ni Kristo, (Soma Matendo 3:15 na Ufunuo 1:5). Sisi tukiitana majina yetu kama ndugu inatosha!..Vyeo vingine vya juu zaidi ya hivyo vinamhusu Bwana wetu Yesu peke yake (Mathayo 23:8-11).

Sasa hivi upo mtindo wa sisi kwa sisi kuitana “wakuu”, utaona mtu atazungumza maneno mawili matatu na mwenzie na katikati atataja neno “mkuu” kama kionjo cha kumpandisha hadhi Yule anayezungumza naye. Si sawa kufanya hivyo!.. Ni mtindo ambao chanzo chake ni kutoka kwa Yule adui yetu shetani.

Lakini pamoja na hayo, tunaweza kujifunza kitu kupitia hiyo habari!.. Bwana alimwambia Yule aliyepooza kwamba “jipe moyo mkuu ” na si “ajipe tu moyo”..bali “moyo mkuu”.. Maana yake tunapokuwa katika dhiki fulani, au tatizo fulani, au ugonjwa fulani.. Hatuna budi kujipa moyo mkuu wenyewe!.. Maana yake hatupaswi kukata tamaa.. Tunapaswa kuamini mpaka mwisho, ili tupokee uponyaji wetu, au Baraka zetu. Kama ni kuomba tunapaswa tuendelee kuomba kwa Moyo Mkuu, kama kutafuta tunapaswa tuendelee kutafuta kwa Moyo Mkuu, mpaka tukipate. Lakini tunapokata tamaa kirahisi ni ngumu kupokea au kupata kile tulichokuwa tunakitafuta.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Kwanini ndugu wanaokaa pamoja wawe kama mafuta ya Haruni?

Nini tofauti kati ya moyo na roho?

SHETANI ANAPOKUINGIA, ANATIA MOYO MGENI NDANI YAKO.

 Je kualikwa kwenye sherehe za watu ambao si wakristo ni dhambi?

JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.

MPAKA UTIMILIFU WA MATAIFA UTAKAPOWASILI.

Rudi nyumbani

Print this post

Je Mungu anaweza kumdanganya mtu?

Tukisoma katika kitabu cha Ezekieli 14:9 tunasoma Mungu anaweza kumdanganya Nabii, sasa swali ni je Mungu anadanganya?

Jibu: Tusome

Ezekieli 14:9 “Na nabii akidanganyika, na kusema neno, MIMI, BWANA, NIMEMDANGANYA NABII YULE, nami nitaunyosha mkono wangu juu yake, na kumwangamiza, asiwe kati ya watu wangu Israeli.

10 Nao watauchukua uovu wao; uovu wa nabii utakuwa sawasawa na uovu wake yule amwendeaye aulize neno”

Kufuatia mstari huo ni rahisi kuamini kuwa Mungu anadanganya… lakini kiuhalisia ni kwaba, Mungu kamwe hawezi kudanganya na wala hasemi uongo!.. Yeye ni mtakatifu siku zote.. Isipokuwa Mungu anaweza kuruhusu roho ya upotevu kutoka kwa adui imwingine mtu,  endapo mtu huyo atayakataa mema na kulazimisha mabaya katika maisha yake, ndivyo maandiko yanavyosema katika 2Wathesalonike 2

2Wathesalonike 2:10 “na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.

11 Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo;

12 ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu”.

Sasa ili tuelewe vizuri Mungu anaiachiaje nguvu ya upotevu juu ya mtu, hebu tusome kisa kimoja cha Mfalme Ahabu katika maandiko..

1Wafalme 22:16 “Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la Bwana?

17 Akasema, Naliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji. Bwana akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.

18 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya?

19 Mikaya akasema, Sikia basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kuume na wa kushoto.

20 Bwana akasema, NI NANI ATAKAYEMDANGANYA AHABU, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.

21 Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya.

22 Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo.

23 Basi angalia, BWANA AMETIA PEPO WA UONGO KINYWANI MWA MANABII WAKO HAWA WOTE; NAYE BWANA AMENENA MABAYA JUU YAKO”.

Umeona hapo?..Mfalme Ahabu alikuwa amemwacha Mungu na alikuwa anaabudu miungu na wala alikuwa hana mpango wa kubadili njia yake, na wakati huo huo anakwenda kumwuliza Mungu kwa habari ya vita iliyo mbele yake, huku moyoni amemwacha Bwana, yaani kwaufupi alikuwa anamgeuza Mungu kama mganga wa kienyeji kumtabiria mambo yake ya vita tu!

Lakini hapo tunasoma Mungu yeye mwenyewe hakumdanganya Ahabu, kwasababu yeye hasemi uongo, lakini aliiachia roho ya upotevu imfuate mfalme Ahabu.. Maana yake Mungu aliruhusu pepo liwaingie manabii wake 400, na kuwapa maono ya uongo, na kufikiri ni maono ya Mungu… Na hivyo Mfalme akadanganyika na maono yale na akaenda kufa katika vita badala ya kupona. Hivyo ni pepo ndilo lililomdanganya Ahabu na si Mungu, ingawa Mungu ndiye aliyeruhusu..hivyo ni sawa na kusema ni Mungu kamdanganya Ahabu..

Kama vile maandiko  yanavyosema kuwa Mungu alimpiga Ayubu.. lakini kiuhalisia si Mungu aliyempiga bali ni shetani, isipokuwa kwa ruhusa ya Mungu..

Ndicho biblia pia ilichomaanisha hapo katika  Ezekieli 14:9 “Na nabii akidanganyika, na kusema neno, MIMI, BWANA, NIMEMDANGANYA NABII YULE”.

Maana yake ni kwamba kama Nabii kamwacha Bwana moyoni mwake, Mungu anaweza kuruhusu pepo la uongo limwingie na kumpa maono ya uongo.. Sasa kitendo hicho cha Bwana kuruhusu upotevu umwingie mtu, ndio unaweza kutafsirika kama Bwana kamdanganya mtu huyo!.. Lakini kiuhalisia si Bwana aliyemdanganya bali ni mapepo ambayo yameruhusiwa na Mungu yamwingie na kumdanganya huyo mtu.

Sio jambo la ajabu pia Mungu anaweza kumuua mtu kwa kumweka mikononi mwa shetani..

Hivyo tunachoweza kujifunza ni kwamba hatuna budi kuwa makini sana na kutomgeuza Mungu kama waganga wa miungu ya kidunia, ambao unaweza kuwafuata wakutatulie matatizo yako,  na kuondoka kuendelea kuishi maisha yako ya ulevi, ya uzinzi, au mengine yoyote.

Kwa Mungu wa mbingu na nchi sio hivyo, tunapomwendea hatuna budi kumkubali kwanza, na kujinyenyekeza chini yake na kufuata kile anachokitaka yeye katika maisha yetu, na si kile tunachokitaka sisi.. Maana yake ni kwamba tunapomwendea Mungu kumuuliza jambo na huku mioyoni mwetu bado tunapenda ulevi, na hatutaki kuacha, bado tunaabudu sanamu, bado ni wachawi, bado ni wazinzi n.k Bwana ataachia nguvu ya upotevu, kwasababu yeye hadhihakiwi alisema hivyo katika neno lake..

Ezekieli 14:1 “Ndipo baadhi ya wazee wa Israeli wakanijia, wakaketi mbele yangu.

2 Ndipo neno la Bwana likanijia, kusema,

3 Mwanadamu, watu hawa wametwaa vinyago vyao na kuvitia mioyoni mwao, nao wameweka kwazo la uovu wao mbele ya nyuso zao. Je! Ni laiki yangu niulizwe na wao katika neno lo lote?

4 Basi sema nao, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Kila mtu wa nyumba ya Israeli atwaaye vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, na kumwendea nabii; mimi, Bwana, nitamjibu neno lake sawasawa na wingi wa sanamu zake;

5 ili niwakamate nyumba ya Israeli kwa mioyo yao wenyewe, kwa sababu wamefarakana nami kwa vinyago vyao”.

Kama hujaokoka!, kumbuka kuwa Kristo ndiye njia kweli na Uzima, na hakuna njia nyingine ya kumfikia Baba zaidi yake yeye. Hivyo wote hatuna budi kumwamini na kumpokea ili tupate wokovu na ondoleo la dhambi zetu, na tunapata wokovu kwa kumwamini, na kutubu na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji tele na kwa jina la Bwana Yesu Kristo. Na Roho Mtakatifu atayakeyeingia ndani yetu atatuongoza katika kweli yote.

Marana tha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

KUMBE MUNGU ANAWEZA KUKULIPA KWA USICHOSTAHILI!

MUNGU ATAKUUA UKIWA MBAYA MACHONI PAKE.

NI WAPI MAHALI SAHIHI PA KULIPA ZAKA?

Kwanini Yakobo alimshinda Mungu, Je! Mungu huwa anashindwa na wanadamu?

Je! Ni kweli ubatizo wa maji hatuuhitaji tena?

USITUPE LULU ZAKO MBELE YA NGURUWE.

Rudi nyumbani

Print this post

Kwanini Paulo aungane na wale watu wanne wenye nadhiri?

SWALI: Naomba kuelewa kitendo cha Paulo, kuungana na wale watu wanne wenye nadhiri, alipoenda Yerusalemu kilimaanisha nini?. Au kinaelewekaje?


JIBU: Kama tunavyosoma katika maandiko tunaona ziara ya mwisho ya mtume Paulo kwenda Yerusalemu baada ya miaka mingi sana, kwa mara ya kwanza alikutana na Yakobo pamoja na wazee baadhi watakatifu wa Yerusalemu, na moja kwa moja alianza kuwasimulia mafanikio ya huduma yake, na jinsi alivyofanikiwa kuwavua watu wengi kwa Kristo na kuihubiri injili.

Yakobo na wazee wa kiyahudi waliposikia vile, walifurahi sana na kumtukuza Mungu, lakini walimpa taarifa nyingine ambazo, zilikuwa ni ngeni masikioni  mwa Paulo. Kwamba, habari zake zimevuma kwa wayahudi wote wa kikristo waliokaa Yerusalemu kuwa yeye amekuwa akiwafudisha watu waipuuzie torati ya Musa, sio tu kwa watu wa mataifa bali pia kwa wayahudi waliokoka, wasishike sheria  kama vile wasitahiriwe n.k.

Hivyo hiyo imemfanya Paulo aonekane kuwa ni mpingamizi mkubwa sana wa Torati kwa wayahudi, jambo ambalo sio kweli. Paulo aliwafundisha watu kwamba torati sio kipimo cha wokovu, bali neema inayotokana na kumwamini Kristo. Lakini hakuwa mpingamizi wa Torati kwa namna yoyote ile. Na ndio maana kuna wakati alimlazimisha hata Timotheo atahiriwe kwa ajili ya wayahudi. Kama angekuwa mpingamizi asingeruhusu hata kitendo cha kutahiriwa kufanyika(Matendo 16:1).

Hivyo, Yakobo, pamoja na wazee, walijua ukweli kuwa Paulo hawezi kufanya vile, ndipo hapo wakamashauri, kwamba ili kuondoa dukuduku hilo, hana budi kuwaonyesha wayahudi wote kuwa, yeye ahialifu torati hata kidogo. Ndipo wakamwambia, wapo watu wanne ambao wanakaribia kumaliza nadhiri zao (nadhiri ya mnadhiri), na kwamba aungane nao kuwahudumia, katika siku hizo, ili wayahudi watakapoona wajue kuwa Paulo, aihalifu torati.

Matendo 21:17 “Tulipofika Yerusalemu wale ndugu wakatukaribisha kwa furaha.

18 Hata siku ya pili yake Paulo akaingia kwa Yakobo pamoja nasi, na wazee wote walikuwako.

19 Na baada ya kuwaamkua, akawaeleza mambo yote moja moja Mungu aliyoyatenda katika Mataifa kwa huduma yake.

20 Nao waliposikia wakamtukuza Mungu, wakamwambia, Ndugu yetu, unaona jinsi Wayahudi walioamini walivyo elfu nyingi, nao wote wana wivu sana kwa ajili ya torati.

21 Nao wameambiwa habari zako, ya kwamba unawafundisha Wayahudi wote wakaao katika Mataifa kumwacha Musa, ukiwaambia wasiwatahiri watoto wao, wala wasizifuate desturi.

22 Basi, ni nini? Bila shaka watasikia kwamba umekuja.

23 Basi fanya neno hili tunalokuambia. Wako kwetu watu wanne waliofungwa na nadhiri.

24 Wachukue watu hao, ujitakase pamoja nao, na kuwagharimia ili wanyoe vichwa vyao, watu wote wapate kujua ya kuwa habari zile walizoambiwa juu yako si kitu, bali wewe mwenyewe unaenenda vizuri na kuishika torati”.

Sasa kwa kawaida, Mnadhiri kulingana na kitabu cha Hesabu 6, alikuwa haruhusiwi kuonyoa kichwa chake, wala kunywa divai, au mzabibu wa aina yoyote, wala kugusa maiti, mpaka siku zake zote zitakapotimia, Hivyo siku ya mwisho alikuwa anachukua, kondoo madume wawili na jike mmoja pamoja na vikapu vya unga, kwa ajili ya upatanisho.

Hivyo, kwa kuwa Paulo alilazimika kuungana nao katika nadhiri zao, basi, ilikuwa ni desturi uwahudumie kwa kuzichukua zao gharama zote za kinadhiri zilizohitajika. Hivyo Kwa kitendo hicho Paulo alionekana kuwa nay eye ni mtunzaji mzuri wa torati. Japo hilo pekee halikutosha kujiaminisha kwao kwa wayahudi, utaona walikuja kutaka kumkamata na kumuua.

Lakini Hiyo ndio sababu ya Paulo kuungana na wale watu wanne waliokuwa na nadhiri, ilikuwa ni ili kuwaonyesha wayahudi kuwa yeye haivunji torati.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Nini maana ya “Torati na manabii”?

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

Tofauti ya kazi ya Damu ya Yesu na Jina la Yesu ni ipi?

Ni kweli Paulo alipuuzia maonyo aliyopewa ya kwenda Yerusalemu?

Rudi nyumbani

Print this post

Je tutakaa mbinguni milele?

 Maandiko yanasema katika 1Wathesalonike 4:17 tutakaa na Bwana milele mbinguni, sasa iweje tushuke tena kutawala na Yesu duniani kwa miaka 1000?.. Au tutarudi tena mbinguni, baada ya utawala huo kuisha?

Jibu: Tusome..

1Wathesalonike 4:16 “Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza.

17 Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; NA HIVYO TUTAKUWA PAMOJA NA BWANA MILELE.

18 Basi, farijianeni kwa maneno hayo.

Kama ukitafakari maandiko hayo kwa makini yanasema “Tutakuwa pamoja na Bwana milele”. Na sio “tutaishi na Bwana mbinguni milele”.. 

Kuna tofauti ya kuwa na mtu milele na kuishi na mtu mahali fulani milele.
Kuwa na Yesu milele maana yake ni kwamba popote atakapokuwepo tutakuwepo naye, popote atakapokwenda tutakwenda naye..hatutamwacha wala yeye hatatuacha, kama alivyotuacha sasa na kwenda mbinguni.

Lakini baada ya sisi kwenda mbinguni huko alipo ,tutakuwa naye milele, hata wakati atakaporudi kwaajili ya hukumu ya vita vya harmagedon tutakuwa naye hatatuacha mbinguni..maandiko yanasema hivyo..

Yuda 1:14 “Na Henoko, mtu wa saba baada ya Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu”.

Umeona hapo?..

Kwahiyo mbinguni tutakwenda na vile vile tutarudi kutawala na Kristo kwa miaka elfu hapa duniani..

Kulingana na maandiko mbinguni tutakaa kwa kipindi cha miaka saba tu!..baada ya hapo tutarudi kutawala na Kristo hapa duniani kwa miaka elfu, na hatitarudi tena mbinguni..Kwani Mji wa kimbinguni Yesrusalemu mpya utashuka hapa, na hapa patageuzwa kuwa mbingu mpya na nchi mpya.

Kwa maelezo marefu kuhusu mbingu mpya na nchi mpya unaweza kufungua hapa >> Mbingu mpya na nchi mpya

Hivyo hatuna budi kupiga mbio ili tuweze kuwa miongoni mwa watakaokuwa na Bwana milele.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.

Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Je mbinguni itakuwa ni kuimba tu wakati wote?.

Tofauti kati ya ufalme wa mbinguni na ufalme wa Mungu ni ipi?

KUJIFUNUA KWA YESU KWA PILI.

Je! Kuna malaika wangapi mbinguni?

Jeshi la Mbinguni wana wa Israeli waliloliabudu ni lipi?

Rudi nyumbani

Print this post

Kwanini Bwana Yesu aliwaagiza wanafunzi wake wakanunue upanga?

Naomba kufahamu Kwanini Bwana Yesu aliwaagiza wanafunzi wake wakanunue upanga?. Na tunafahamu kazi ya upanga si njema?

Tusome

Luka 22:35 “Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La!

36 Akawaambia, Lakini sasa mwenye mfuko na auchukue, na mkoba vivyo hivyo; naye asiye na upanga, na auze joho yake akanunue”.

Maneno haya aliwaambia wanafunzi wake, alipokaribia mwishoni kabisa mwa huduma yake, akimaanisha kuwa majira yamebadilika, sasa sitawatuma, na kama siwatumi basi na faida zile zinazombatana na wito wangu mtazikosa, hivyo kama ulikuwa huna tabia ya kutunza pesa zako, basi sasa anza kuzitunza, maana yake jiwekee akiba kwenye mfuko wako, jihifadhie vitu vyako, kwa matumizi ya baadaye kwasababu kuna kupungukiwa huko mbele, vivyo hivyo na kama huna upanga, ukauze joho lako ukaununue!

Lakini swali linakuja kwanini uwe ni Upanga tena, wakati upanga ni wa kuulia?. Hata mitume nao walifikiri Bwana anamaanisha hivyo hivyo, kwamba wakanunue upanga kwa ajili ya kujilinda, au kuwapiga maadui zao pale wanapotaka kuwadhuru.. Na ndio maana muda huo huo wakamwambia Bwana maneno haya;

Luka 22:38 “Wakasema, Bwana, tazama, hapa pana panga mbili. Akawaambia, Basi”.

Wakidhani, kuwa Kristo alimaanisha wazitumie hizo kujilindia au kuwapiga maadui zao.. Utaona mawazo hayo bado yalikuwa vichwani mwao, hata baadaye kidogo, majeshi ya makuhani yalipokuja kumkamata Yesu, yakiwa na marungu na mapanga, utaona Petro alichukua upanga wake, na kwenda kumpiga na kumata sikio mtumwa wa kuhani Mkuu. Kitendo ambacho kilimuudhi sana Bwana, akawakemea, na kuwaambia auye kwa kwa upanga atauawa kwa upanga(Mathayo 26:52),.

Luka 22:49 “Na wale waliokuwa karibu naye walipoona yatakayotukia, walisema, Bwana, tuwapige kwa upanga?

50 Mmoja wao akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume.

51 Yesu akajibu akasema, Mwe radhi kwa hili. Akamgusa sikio, akamponya”.

Hapo ndipo wakagundua kuwa Panga walizoambiwa wakanunue si kwa lengo la kujihami au kuwadhuru wengine.

Bali Bwana alichomaanisha, aliposema mkanunue Panga, ni kwa lengo la kujipatia rizki, panga hapo linawakilisha vitu vyote vikali aidha vya kukatia, kuulia, kuchinjia, au kupasua. Kama vile kisu, shoka, mkuki, n.k. Kwamfano katika kupika utahitaji kisu tu mahali Fulani, kama huna kisu huwezi kukata nyama, au kitunguu, nyanya n.k. hivyo hapo mwanzo ulikuwa huna vitu hivi nyumbani kwako nenda kanunue kwasababu vitakufaa sana wakati huu.

Vilevile kama wewe ni mvuvi kama Petro utahitaji tu Kisu cha kuparulia samaki, hakuna namna utakikwepa. Kama wewe ni mwindaji, utahitaji mkuki au upanga, kama wewe ni mkulima utahitaji shoka, au rato n.k.

Hicho ndicho Bwana alichokimaanisha, kwamba wakajitafutie kitu chochote, kinachoweza kuwafaa kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao ya mwilini, lakini sio upanga wa kuulia watu.

Ni nini Bwana anatufundisha katika kauli hiyo? Ni kuwa anapotuita katika utumishi wake tusiwe na wasiwasi tutakula nini, au tutakunywa nini, yeye mwenyewe atahakikisha anatuhudumia kwa kila kitu, kama alivyowahudumia mitume wake mpaka dakika ya mwisho, kwasababu anajua muda wote tunaupoteza kwake, hivyo yeye mwenyewe atahakikisha tunaishi kwa namna yoyote ile, Lakini kama hatupo katika utumishi wake, hatuna budi kuitunza mifuko yetu, kujiwekea akiba zetu, na kujitafutia mawindo yetu, na yeye atatubariki kwa njia hiyo.

Lakini baada ya pale, mtume walifurahia kuendelea na utume wa Bwana, hata siku ya pentekoste ilipofika, na kazi ya utume ulipoanza, Kristo alikuwa nao wakati wote akiwahudumia kama alivyowahidia katika Mathayo 28:20

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

NA VIUNGO VYETU VISIVYO NA UZURI VINA UZURI ZAIDI SANA.

KUNA NGUVU YA ZIADA KATIKA KULING’ANG’ANIA KUSUDI LA MUNGU.

Kwanini Bwana Yesu alitokea katika ukoo wa Yuda?

Kwanini Yesu aliwaambia wale wakoma wakajionyeshe kwa makuhani?

Rudi nyumbani

Print this post

KWANINI NI NUHU, AYUBU NA DANIELI?

Jina la Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia.. Maandiko yanasema..

Ezekieli 14:13 “Mwanadamu, nchi itakapofanya dhambi na kuniasi, kwa kukosa, nikaunyosha mkono wangu juu yake, na kulivunja tegemeo la chakula chake, na kuipelekea njaa, na kukatilia mbali mwanadamu na mnyama;

14 WAJAPOKUWA WATU HAWA WATATU, NUHU, NA DANIELI, NA AYUBU, kuwamo ndani yake, WANGEJIOKOA NAFSI ZAO WENYEWE TU KWA HAKI YAO, asema Bwana MUNGU”.

Hapo maandiko yamewataja watu watatu tu! Nuhu, Danieli pamoja na Ayubu. Unaweza kujiuliza ina maana ni hao tu ndio waliokuwa na haki kuliko manabii wengine wote na watakatifu wengine wote walioandikwa kwenye biblia (Agano la kale)?. Jibu ni la!..

Watakatifu wote wa kwenye biblia walikuwa na haki mbele za Mungu, na walimpendeza Mungu katika nafasi zao.. Lakini kulikuwa na jambo la kipekee katika hawa watu watatu, lililowafanya mpaka Bwana Mungu awataje hapa.. tutaenda kulitazama jambo hilo, ambapo litatusaidia na sisi kuenenda vyema katika ukristo wetu.

Sasa ili tuweze kuweka msingi wa kuelewa tabia waliyokuwa nayo hawa watu watatu, hebu tusome tena, maandiko mistari inayofuata ya mbele kidogo..

Ezekieli 14:19 “Au nikipeleka tauni katika nchi ile, na kumwaga ghadhabu yangu juu yake, kwa damu; ili kuwakatilia mbali nayo wanadamu na wanyama;

20 wajapokuwamo ndani yake Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, HAWATAOKOA WANA WALA BINTI; watajiokoa nafsi zao tu kwa haki yao”.

Nataka tuone huo mstari wa 20, unaosema.. “Hawataokoa wana wala binti”. Maana yake ni kwamba watu hawa walikuwa wana tabia ya KUWAOKOA WATU NA GHADHABU YA MUNGU,  yaani Mungu alipotaka kuwaadhibu watu wote, hawa walisimama kuwaombea watu wao, au familia zao au wana wao, kitu kilichomfanya Mungu aghairi hasira yake kwa wale waliowaombea.

Kwa mfano utaona Nuhu, Mungu alipotaka kuigharikisha dunia, maandiko yanasema alionekana Nuhu peke yake ndiye mwenye haki,  wengine wote ikiwemo familia yake walikuwa miongoni mwa watu waliostahili adhabu ya gharika…. Lakini Nuhu alimwomba kwa ajili ya familia yake, na Mungu akamwambia atengeneze safina, sasa lengo la kutengeneza ile safina sio kujiokoa yeye peke yake bali yeye na nyumba yake, maandiko yanasema hivyo..

Waebrania 11:7 “Kwa imani Nuhu akiisha kuonywa na Mungu katika habari za mambo yasiyoonekana bado, kwa jinsi alivyomcha Mungu, ALIUNDA SAFINA, APATE KUOKOA NYUMBA YAKE. Na hivyo akauhukumu makosa ulimwengu, akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani”.

Hapo biblia inasema aliunda safina “APATE KUIOKOA NYUMBA YAKE”.. maana yake apate kuwaokoa wana wake na mke wake!.. Hivyo kitendo cha watoto wake kupata neema ya kuokoka ilikuwa ni kwasababu ya Nuhu Baba yao.

Vile vile tunamwona mtu kama Ayubu. Huyu naye alikuwa ni mtu wa kipekee sana, kwani kabla ya mambo yote alikuwa akiwaombea rehema watoto wake kwa Mungu kila siku.

Ayubu 1:4 “Nao wanawe huenda na kufanya karamu katika nyumba ya kila mmoja wao kwa siku yake; nao wakatuma na kuwaita maumbu yao watatu ili waje kula na kunywa pamoja nao.

5 Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, YUMKINI KWAMBA HAWA WANANGU WAMEFANYA DHAMBI, NA KUMKUFURU MUNGU MIOYONI MWAO. NDIVYO ALIVYOFANYA AYUBU SIKUZOTE”.

Umeona tabia ya Ayubu?.. alikuwa ni mtu wa kuiombea nyumba yake rehema.. Inapokuja hatari hakutaka aokoke peke yake..alitaka kuokoka na familia yake..

Na mtu wa mwisho tunayeweza kumtazama ni Nabii Danieli, huyu maandiko hayajasema kama alioa au hakuoa!.. Lakini tabia ile ile ya kuwajali watu wa jamii yake, hata kuwaombea kwa Mungu, ndiyo iliyokuwa ndani yake..mpaka Mungu akaghairi mabaya juu ya watu wake Israeli kutokana na maombi ya Danieli. Na maandiko yanamtaja Danieli kama mtu aliyependwa sana na Mungu!..

Danieli 9:20 “Basi hapo nilipokuwa nikisema, na kuomba, na kuiungama dhambi yangu, NA DHAMBI YA WATU WANGU ISRAELI, na kuomba dua yangu mbele za Bwana, Mungu wangu, kwa ajili ya mlima mtakatifu wa Mungu wangu;

21 naam, nilipokuwa nikinena katika kuomba, mtu yule, Gabrieli, niliyemwona katika njozi hapo kwanza, akirushwa upesi, alinigusa panapo wakati wa dhabihu ya jioni.

22 Akaniagiza, akaongea nami, akasema, Ee Danielii, nimetokea sasa, ili nikupe akili upate kufahamu.

23 Mwanzo wa maombi yako ilitolewa amri, nami nimekuja kukupasha habari; maana wewe UNAPENDWA SANA; basi itafakari habari hii, na kuyafahamu maono haya.

24 Muda wa majuma sabini UMEAMRIWA JUU YA WATU WAKO, na juu ya mji wako mtakatifu, ili kukomesha makosa, na kuishiliza dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, na kuleta haki ya milele, na kutia muhuri maono na unabii, na kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu”.

Kama ukisoma sala hiyo kuanzia juu kidogo (mstari wa kwanza), utaona jinsi Danieli alivyokuwa akiomba dua kwaajili ya watu wake(Yaani waisraeli wenzake walio katika hali ya utumwa huko Babeli). Na alipomaliza kuomba kwaajili yake na Watu wake, hapo katika mstari wa 24, maandiko yanasema Malaika Gabrieli alimjia na kumpa maneno ya faraja juu ya WATU WAKE ANAOWAOMBEA , ili kukomesha makosa, kuishiliza dhambi na kufanya upatatisho n.k

Ni jambo gani tunajifunza kwa watu hawa watatu?

Jambo kuu tunaloweza kujifunza kutoka kwa hawa watatu ni ile hali ya kujali wengine!… Wanaona itawafaidia nini wao kupata raha na kuokoka, na ilihali familia zao zinapotea?, ndugu zao wanapotea?..!.. wakaona hawana budi kutafuta njia yoyote ya watu wao kuwaokoa ndugu zao, haijalishi wanaonekana bado ni waovu mbele za Mungu!.. Ndio maana unaona Nuhu alijenga safina na akapona na wanawe watatu!, kadhalika Ayubu alikuwa anawaombea wanawe kila siku kwa kuwatolea dhabihu, kwasababu alihisi pengine wanawe wanaweza kuwa wamemuudhi Bwana mahali fulani katika maisha yao, hivyo aliuchukua mzigo wao.

Na wa mwisho ni Danieli, aliona hana sababu ya yeye kujifurahisha kwenye nyumba ya kifalme na ilihali watu wake wapo katika hali ya kukataliwa na Mungu, hivyo akachukua jukumu la kufunga na kuomba kwaajili ya watu wake.

Ndugu tabia ya kujali uzima wa wengine, inaweza kudharaulika leo lakini ni jambo la heshima kubwa sana mbele za Mungu, Mungu ameweka kumbumbu la hawa watatu zaidi ya manabii wengine wote kutokana na tabia yao hiyo, kwa tabia hiyo ndio iliyomfanya Bwana awatukuze watu hawa watatu zaidi ya wengine wote.

Inawezekana leo umempokea Yesu, lakini ndani ya moyo wako, huna mzigo wa wengine kuwa kama wewe!.. Ni jambo baya sana…Inawezekana umeokoka, lakini moyoni mwako huna mzigo na Baba yako au mama yako ambaye bado hajaokoka kama wewe, Au huna mzigo na rafiki yako au ndugu yako ambaye bado yupo katika ulimwengu, au unaserebuka mtu fulani anapokufa bila kuokoka!

Fahamu kuwa tuna wajibu wa kuokoka sisi na vile vile kuwafikishia wengine wokovu.. kama sisi tulivyoupokea..ni lazima tuwe sababu ya wokovu kwa watu wengine..Ndivyo tutakavyompendeza Bwana na kukaa katika kumbukumbu lake daima.

Bwana atujalie tuweze kuyatenda mapenzi yake.

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).

HUTATAMBUA LOLOTE, SIKU YA UNYAKUO IKIFIKA.

NI LIPI KATI YA MAKUNDI HAYA, WEWE UPO?

KWANINI MIMI?

Neno “Via” linamaanisha nini katika biblia?

Nyumbani:

Print this post

IEPUKE GHADHABU YA MUNGU.

Tofauti na inavyoaminika na wengi kuwa hasira ya Mungu au ghadhabu ya Mungu, inakuja au inachochewa sana na watu waliomwacha Mungu, wa ulimwengu huu, yaani watu ambao hawajamwamini Mwokozi Yesu.

Hiyo ni kweli kabisa, lakini nataka nikuambia kuwa hiyo haichangii pakubwa kuimwaga ghadhabu ya Mungu ulimwenguni.

Jambo kubwa linaloleta ghadhabu ya Mungu ulimwenguni ni maovu katikati ya watu wa Mungu, pamoja na ndani ya nyumba ya Mungu. Kikawaida mtu asiyekujua akikutusi, au akikudhalilisha jambo lile haliwezi kuugusa moyo wako sana, kama ukitukanwa au kudhalilishwa na mtu unayemjua, au uliye na mahusiano naye ya karibu sana.

Yule uliye na mahusiano naye ya karibu ndiye anayeweza kukuudhi sana na kukufurahisha sana, tofauti na mtu mwingine ambaye hamna mahusiano yoyote au hata hamjuani.

Ndivyo hivyo hivyo na Mungu wetu, watu wanaompendeza sana ni watu wale alio na mahusiani nao maana yake watu waliookoka, na wala si watu wa ulimwengu huu ambao hawamjui Mungu.. kadhalika watu wanaomuudhi sana, ni watu waliookoka ambao hawajasimama sawasawa. Hao ndio wanaomhuzunisha sana na wanaougusa moyo wake kwa maovu yao zaidi ya watu wale ambao hawajaokoka kabisa na wanatenda mabaya.

Maana yake ni kwamba mtu anayesema ameokoka na huku ni mzinzi, au mtukanaji, au muuaji.. Huyo anamhuzunisha Mungu na kumuudhi mara nyingi zaidi ya Yule ambaye hamjui Mungu kabisa na ambaye hajaokoka. Mtu ambaye hajaokoka kabisa na yupo katika ulimwengu, na anafanya maasi, ni kweli anamhuzunisha Mungu lakini si kwa kiwango kile cha mtu aliye katika mahusiano na Mungu, na wakati huo huo anafanya maasi.

Ni muhimu sana kulijua hili ili tuweze kuchukua tahadhari, na kuacha kunyoosha vidole kwa watu waovu wasiomjua Mungu, ilihali sisi wenyewe tuliomjua Mungu hatujajiweka sawa ipasavyo.

Wewe uliyeokoka utasema unazini mara moja tu kwa mwezi au kwa mwaka, na kufikiri moyoni mwako kuwa una heri sana kuliko Yule kahaba unayeona anajiuza kila siku ambaye hamtaki Mungu na hajaokoka kabisa.

Nataka nikuambie wewe uliyeokoka unayezini mara moja kwa mwezi au mara moja kwa mwaka ndiye mwenye dhambi kubwa kuliko Yule kahaba anayezini kila siku ambaye hajaokoka!.. Wewe ndiye unayemhuzunisha Mungu sana kuliko Yule kahaba..

Wewe unayesema umeokoka na kulewa mara moja kwa mwezi, ndiye unayeichochea ghadhabu ya Mungu kuja ulimwenguni zaidi hata ya Yule mlevi, anayeshinda bar kila siku na huku hajaokoka kabisa.

Wewe unayejiita umeokoka na huku unatazama picha za utupu mitandaoni na unajichua, mara moja kwa mwezi ndiye unayefanya dhambi kubwa kuliko Yule ambaye hajamjui Mungu kabisa na anafanya mambo hayo kila siku.

Sasa hivi utatazama mataifa mengine, watu wanatembea uchi barabarani, watu wanamtukana Mungu.. na moyoni ukadhani una heri wewe ambaye humtukani Mungu lakini unatukana mara moja moja.. Nataka nikuambie ndugu, hao wamemkataa Mungu tangu zamani, na Mungu alishawaacha sawasawa na (wafuate tamaa zao), hivyo wanayo hukumu yao inayokuja kama hawatatubu..Lakini wewe unayejua kila kitu, ambaye umeshaanza mahusiano na Mungu, na unafanya mambo kama hayo, hata kama ni siku moja moja.. jua kuwa wewe ndiye unayeichochoa hasira ya Mungu.

Hivyo ndugu kumbuka siku zote, Maasi katikati ya  watu wa Mungu ndio yanayoleta ghadhabu ya Mungu zaidi ya wale walio nje ya Imani.

Hivyo ni wajibu wetu, kujitakasa zaidi, nyakati hizi za siku za mwisho.. wala tusijilinganishe na watu walio nje!.. na kufikiri kuwa makosa yao Mungu anayafananisha na yetu. Ni wakati wa kuukataa uvuguvugu wote na kutafuta kuwa moto katika Imani.

Ufunuo 3:14 “Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.

15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu”.

Bwana akubariki.

Kumbuka pia ule mwisho umekaribia sana, na parapanda ya mwisho ipo karibuni kulia.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

“Shinikizo” ni nini kibiblia, Na maana yake rohoni ni ipi?

Je watu ambao hawajasikia kabisa injili watahukumiwa?

MATARAJIO YA KILA MWANADAMU DUNIANI NI YAPI?

INJILI YA MANENO LAINI ITAKUGHARIMU.

Rudi nyumbani

Print this post

KIFAHAMU KIGEZO  CHA KUSAMEHEWA NA MUNGU.

Shalom nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo. Leo nataka tujifunze jambo la muhimu sana ambalo Bwana anataka tufahamu tunapokwenda mbele zake hususani katika kumwomba msamaha au rehema..hili ni jambo la muhimu sana..naomba usome hadi mwisho.

Kwa kawaida hakuna mtu asiyemkosea Mungu..hata kama hutamkosea kwa dhambi ya moja kwa moja zipo dhambi nyingine ndogo ndogo  ambazo si rahisi kuzitambua kwa haraka..kwamfano unaweza kumkwaza jirani yako kwa kauli fulani.ambayo pengine wewe uliiona ni sawa tu, lakini kumbe hujui tayari ulishatenda dhambi mbele za Mungu, kumfanya mwenzako ajisikie vibaya…na ndio maana maisha ya toba ni ya muhimu sana kwa mkristo yeyote..

Sasa jambo ambalo wengi hatujui ni kuwa msamaha wa Mungu unayo masharti yake..huwa hauji hivi hivi tu kama unavyodhani..Na leo tutaona ni kwanini..

Embu kaa chini uitafakari kwa makini ile sala ya Bwana..ukisoma pale vizuri utaona wanafunzi wake walipomwomba awafundishe kuomba hakusita kuwafundisha, mwanzoni alianza kwa kuwaambia vipengele vya kuombea, bila masharti au vigezo vyovyote ..kwamfano aliposema “utupe leo riziki zetu hakutoa” sababu yake mbele kwanini iwe hivyo..hakusema kwa kuwa na sisi tunawapa wengine riziki zetu..hapana..bali alisema tuombe tu hivyo hivyo na Mungu atatugawia..vilevile aliposema “usitutie majaribu” hakusema kwasababu na sisi hatuwatii watu wengine majaribuni hapana..alisema tuombe tu hivyo hivyo inatosha na yeye mwenyewe atatuepusha na majaribu yote…

Lakini alipofikia kipengele cha Utusamehe makosa yetu..utaona hapo hapo alitoa na sababu ya kwanini sisi tusamehewe..na sababu yenyewe ni kwasababu na sisi tunawasamehe waliotukosea makosa yetu..

Hapo ndipo Mungu anapataka kila mmoja wetu ajue na aliweke hilo akilini kwamba hayo mawili yanakwenda sambamba..hapo hamvumilii mtu yeyote..na ndio maana kayaambatanisha yote mawili  kwa pamoja.

Tusome..

Mathayo 6:9 “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje,

10 Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.

11 Utupe leo riziki yetu.

12 Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu.

13 Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.]

14 Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi.

15 Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu”.

Umeona bado huko mwishoni kabisa Kristo analiwekea tena msisitizo neno lile lile alilolisema katika hiyo sala..kwamba Mungu anasamehe tu pale tunaposamehe..ndugu Mungu anaweza kukupa kila kitu unachomwomba hata kama wewe huwapi  wengine hivyo vitu…anaweza kukufanyia jambo lolote lile utakalo hata kama huwafanyii wengine hayo..unaweza ukawa mchoyo wa kupindukia na mbinafsi kwelikweli hutaki kuwapa watu vyakula vyako vinaozea huko ghalani..lakini ukamwomba Mungu akupe nafaka nyingi zaidi na akakupa tena tele mpaka ukakosa pa kuweka.

Lakini kwenye suala la kumwomba msamaha kama hutamsamehe ndugu yako aliyekukosea..hutamsamehe mke wako/mume wako aliyekuvunja moyo au kukusaliti ..sahau Mungu kukusamehe na wewe makosa yako..hiyo ondoa akilini kumbuka Mungu yupo makini (STRICT) sana na neno lake…akisema amesema..usijidanganye wala usidanganywe na mtu..huna msamaha wowote wa dhambi zako zote zilizokutangulia wala unazozitenda leo hii..

Ukifa leo ni moja kwa moja kuzimu..hakuna mzaha hapo..Na ndio maana jambo la KUSAMEHE linapaswa liwe ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Haijalishi amekuudhi kiasi gani, amekutukana mara ngapi..kama bado una vinyongo vya tokea mwaka juzi, hutaki kuachilia na bado unaona okay..utakufa vibaya sana Ndugu ukiendelea hivyo, haijalishi utasema umeokoka. Dhambi hii imewashusha wengi kuzimu. Ni wengi kweli kweli kwasababu neno msahama kwao ni gumu lakini bado wanawataka na wenyewe wasamehewe na Mungu.

Bwana atutie nguvu. Tujifunze kusamehe Tutembee katika kanuni zake.Ili tuishi kwa amani hapa duniani, tuikwepe hukumu ya Mungu.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

SAMEHE KUTOKA NDANI YA MOYO WAKO.

Je! Kuna dhambi kubwa na ndogo, na kama hakuna je! Mtu aliyeua na aliyetukana je watapata adhabu sawa?

NI KIPI KINAMZUIA MUNGU KUZUNGUMZA NA SISI?

SISI NI WINDO BORA SANA, LA DHAMBI.

Kama Mungu ndiye kaumba kila kitu, je ni yeye huyo huyo ndiye aliyeumba dhambi pia?

Rudi nyumbani

Print this post