Karibu tujikumbushe machache juu ya ujio wa Bwana Yesu, jinsi utakavyokuwa.
Bwana Yesu alikuja mara ya kwanza miaka ile 2,000 iliyopita…Alizaliwa na Bikira Mariamu, akasulubiwa na wayahudi, akazikwa, akafufuka baada ya siku tatu, na akapaa juu mbinguni kwa Baba…Mpaka muda huu tunapozungumza yupo mbingu za mbingu, amepokea Enzi na mamlaka yote ya mbinguni na duniani(1Timotheo 6:16). Lakini huko amekwenda kutuandalia makao (yaani nafasi zetu).
Baada ya muda mfupi atarudi tena kutuchukua tuende naye kwake, ili alipo nasi pia tuwepo..(Yohana 14:3).
Sasa siku ya kuja kutuchukua itakapofika, siku hiyo ndiyo inayoitwa SIKU YA UNYAKUO, Hatashuka duniani, bali atabaki pale mawinguni na atatuita sisi juu tupae kumfuata kule aliko..Siku hiyo tutaisikia sauti ya parapanda na muda huo huo uweza wa ajabu utashuka juu yetu ambapo kufumba na kufumbua tutajikuta miili hii yetu ya udhaifu imebadilika na kuwa kama wa kwake Bwana wetu Yesu. Na tutapaa juu, tutaicha hii ardhi kwa mara ya kwanza na kwenda juu sana…
Watu wa ulimwengu waliomkataa hawatamwona atakapotuita juu…watakaomwona ni wale tu ambao watanyakuliwa…kama vile alivyofufuka mara ya kwanza ni mitume wake tu na wafuasi wake wachache ndio waliomwona na wengine wote Mafarisayo na masadukayo hawakumwona, wala Pilato aliyemsulubisha hakujua chochote..ndivyo siku hiyo itakavyokuwa, wale wakristo ambao wameishikilia Imani mpaka siku hiyo itakapofika ndio watakaomwona Bwana mawinguni, na ndio watakaoisikia parapanda siku hiyo..
Sasa wafu ambao walitangulia kufa katika Kristo hawatasahaulika nao pia, kwasababu wao ndio watakaokuwa wa kwanza kuona tukio zima jinsi litakavyoendelea kwasababu watufufuliwa kwanza, kisha baadaye wataungana na sisi tulio hai na wote kwa pamoja tutavikwa miili ya utukufu. (kasome 1Wathesalonike 4:15)..
Na hali kadhalika wafu hao ambao watafufuka sio watu wote watawaona..hapana, watu wengine wakidunia watahisi tu labda kumetokea tetemeko la ardhi kama ilivyotokea siku ile Bwana aliyofufuka, lakini hawatamwona mtu yoyote….Watakaowaona wafu waliofufuliwa ni wale tu ambao wataungana nao kwenda kumlaki Bwana mawinguni.
Sasa Mbinguni, kutakuwa na karamu inaendelea kwa muda wa miaka saba, kutakuwa na raha isiyo na kifani..ambapo wakati huo duniani itakuwa inapitia kipindi cha dhiki kuu, na udhihirisho wa Mpinga-Kristo kwa watu waliosalia bila kwenda kwenye unyakuo, wachache watagundua Kristo amesharudi na wameachwa, wengi hawataamini na kuhisi ni uzushi tu umezuka..na hivyo watadanganyika kwa uongo wa mpinga-kristo na kuipokea chapa, na hatimaye kufa katika siku ya hasira ya Bwana ambapo Mungu mwenyewe ataiadhibu dunia kwa maovu yake kwa kupitia mapigo yale ya vitasa saba (Ufunuo 16).
Baada ya mambo hayo kuisha, Bwana kujilipizia kisasi kwa watenda maovu… Kristo pamoja na wale watakatifu wake ambao walikuwa wapo mbinguni katika karamu, watakuja duniani kwaajili ya ile vita ya Harmagedoni na kwa ajili ya kuanza utawala wa miaka 1,000..Wakati huo atakapokuja..wale watu wachache sana ambao wamebaki duniani ndio watakaomwona akija mawinguni kwa nguvu na utukufu mwingi.… atashuka na kulimalizia kundi dogo lililosalia katika vita vile vya Harmagedoni.. Hapo ndipo lile neno litakapotimia kwamba “kila jicho litamwona”…wataomboleza na kulia na kushikwa na hofu kuu, watakapomwona Kristo sio yule waliokuwa wanamwona kwenye picha au waliokuwa wanamsoma kwenye kitabu akija kwa upole na unyonge, wakati huu watamwona akija kwa utukufu mwingi kama umeme na ghadhabu nyingi.
Mathayo 24:30 “ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi”.
Baada ya hapo utawala wa miaka 1,000 utaanza…na baada ya utawala huo itakuja mbingu mpya na nchi mpya, ambapo huko kutakuwa hakuna kufa, wala kuzeeka, wala kujaribiwa, wala kuteswa…Mambo ya kwanza yamekwisha kupita, atayafanya yote kuwa mapya..watakatifu wataishi na Bwana milele, katika utukufu usio na mwisho..Muda utasimama kutakuwa hakuna kuhesabu miaka, kwasababu maisha yatakuwa ni ya umilele.
Ufunuo 21:4 “Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”
Bwana atausaidie tuwe miongoni mwa wale watakaokuwa wamealikwa katika karamu ya mwanakondoo mbinguni..
Ufunuo 19:9 “Naye akaniambia, Andika, Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo…”.
Wafu wafao sasa katika dhambi, hawatafufuliwa siku ya unyakuo itakapofika..watabaki kuzimu sehemu ya mateso..na siku moja watakuja kufufuliwa na kuhukumiwa kila mmoja kulingana na matendo yake(Ufunuo 20:13)..na baada ya kuhukumiwa watahamishwa kutoka kuzimu walipokuwepo na watakwenda kutupwa katika ziwa la moto lenye mateso makali Zaidi kuliko kule kuzimu walipokuwepo. Na huo ndio utakuwa mwisho wao.
Sio hilo tu, kwa wale waliokutwa wakiwa hai na wameachwa kwenye unyakuo na kuipokea chapa ya mpinga-kristo, hatapona hata mmoja wote baada ya kipindi kifupi watapitia mapigo makali ambayo yataletwa na Mungu mwenyewe kupitia vile vitasa 7..wakati wenzao waliokufa katika dhambi wakiwa jehanamu wanateseka wao watakuwa wanapitia mateso ya ghadhabu ya Mungu huku duniani, maji yote ya duniani yatageuzwa kuwa damu watu watasikia kiu mpaka kufikia hatua ya kuyanywa maji ya damu na kufa,(ili Mungu kuwalipizia kisasi kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu wake hivyo Mungu amewarushia hiyo damu wainywe), siku hizo jua litashushwa na kuwa kama moto juu ya wanadamu, mvua zitasimama kunyesha, na badala yake vitu vya ajabu vitaanza kuanguka kutoka mbinguni, na Bwana atawafanya watu wawe hawaelewani wao kwa wao hivyo kutakuwa na mapambano na vita vikuu,
Na katikati ya mateso hayo ya jua hilo kali, na kukosekana kwa maji na chakula duniani, Bwana ataleta magonjwa ya ajabu ya majipu ya ajabu juu ya wanadamu wote waliopokea chapa ya mnyama..kwahiyo mtu atakayeukosa unyakuo atakuwa hatna tofauti sana na mtu aliyekufa na kwenda kuzimu kutokana na mateso atakayoyapata akiwa hapa duniani.
Ufunuo 16:1 “Nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni, ikiwaambia wale malaika saba, Enendeni, mkavimimine vile vitasa saba vya ghadhabu ya Mungu juu ya nchi.
2 Akaenda huyo wa kwanza, akakimimina kitasa chake juu ya nchi; pakawa na jipu baya, bovu, JUU YA WALE WATU WENYE CHAPA YA HUYO MNYAMA, NA WALE WENYE KUISUJUDIA SANAMU YAKE.
3 Na huyo wa pili akakimimina kitasa chake juu ya bahari, ikawa damu kama damu ya mfu, na vitu vyote vyenye roho ya uhai katika bahari vikafa.
Na baada ya kupitia mapigo hayo yote pamoja na kuuawa na mwanakondoo watakufa wote na kuungana na wenzao walioko jehanamu..wote kwa pamoja wakisubiria hukumu ya kutupwa katika ziwa la moto.
Hivyo unyakuo sio wa kukosa hata kidogo, Ni heri tukose hayo mengine yote lakini si unyakuo…Bwana atusaidie atukute tukiwa tunakesha katika roho kama alivyosema…
Marko 13:32 “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba.
33 Angalieni, kesheni, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo.
34 Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe.
35 Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jimbi, au asubuhi;
36 asije akawasili ghafula akawakuta mmelala.
37 Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni”
Ulevi ni usingizi, uasherati ni usingizi, wizi ni usingizi, usengenyaji ni usingizi, kiburi, hasira, matukano,rushwa, utapeli,uongo, uuaji, moyo unaowaza mabaya, na mambo yanayofanana na hayo.
Bwana atubariki.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Kwanini Mungu aliikubali sadaka ya Yeftha ya kumtoa binti yake kafara?
About the author