BIDII YA MFALME YOSIA.

BIDII YA MFALME YOSIA.

Moja ya Wafalme 19 waliopitia Yuda, na Wafalme 20 waliopita Israeli, enzi zile wafalme, tukiachilia wale wafalme watatu ambao waliitawala Israeli kabla ya kugawanyika yaani (Sauli, Daudi, na Sulemani)..Ni mfalme mmoja tu ambaye kuzaliwa kwakwe kulitabiriwa kwa namna ya ajabu sana, na mfalme huyu alijulikana kama mfalme Yosia,.

Mwanzoni kabisa wa ufalme kugawanyika, ambao tunajua ulisababishwa na kosa la Sulemani, la kuweka miungu migeni Israeli, Mungu alikasirishwa hadi kufikia hatua ya kutaka kumnyang’anya ufalme wote lakini kwasababu ya viapo ambavyo Mungu alimwahidia Daudi baba yake kuwa hatakosa mtu wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli milele(2Nyakati 6:16),hivyo Mungu akambakishia Daudi kabila moja , yaani kabila la Yuda, na la Benyamini kama msindikizaji wake.

Lakini mengine yote kumi, alimgawia mtu mwingine ambaye alikuwa ni mtumwa wa Sulemani aliyeitwa Yeroboamu, ikiwa hujapata uchambizi wa vitabu vya wafalme, bofya hapa..⏩Vitabu vya biblia

Sasa siku ile Yeroboamu anaahidiwa ufalme huo Mungu alimwambia maneno haya:

1Wafalme 11:38 “Tena itakuwa, ukiyasikia yote nitakayokuamuru, na kuenda katika njia zangu, na kutenda yaliyo mema machoni pangu, ili kuzishika amri zangu na hukumu zangu kama Daudi mtumishi wangu alivyotenda, basi, nitakuwa pamoja nawe, nitakujengea nyumba iliyo imara, kama nilivyomjengea Daudi, nami nitakupa wewe Israeli.

39 Tena nitawatesa wazao wa Daudi kwa sababu hii, lakini si daima”.

Lakini kama tunavyosoma, huyu mfalme japo alijua kuwa ufalme umekuja kwake kwa kosa la Sanamu za Sulemani, yeye hakulitia hilo moyoni mwake badala yake, akawa mbaya kuliko hata Sulemani, na kiongozi yoyote ambaye alishawahi kutokea Israeli, alileta giza kubwa Israeli ambalo kuondoka kwake iligharimu miaka zaidi ya 400, ni huyu Yeroboamu…yeye alijenga madhabahu za ng’ombe kaskazini na kusini mwa ufalme wake, ili kuzuia watu wasiende kuabudu Yerusalemu kwenye Hekalu la Sulemani, mahali ambapo Mungu alipachagua mambo ya ibada yafanyike, hakuishia kuwazuia tu watu wasiende kuabudu bali akatunga mpaka na sikukuu zake mwenyewe za miezi yake mwenyewe ya kuabudu, hivyo kwasababu yeye ndiye aliyekuwa mfalme basi watu wote walimtii na kumfuata..

Sasa sikumoja wakati amekaa katika dhabihu ya jioni, anaifukuzia uvumba miungu yake, Nabii wa Mungu alitokea palepale kama tunavyosoma katika kitabu cha 1 Wafalme..

1 WAFALME: MLANGO 13

1 “Na tazama, akatoka mtu wa Mungu katika Yuda kwa neno la Bwana, akafika Betheli. Naye Yeroboamu alikuwa akisimama penye madhabahu, afukize uvumba.

2 Basi mtu huyo akapiga kelele juu ya madhabahu, kwa neno la Bwana akasema, Ee madhabahu, madhabahu, Bwana asema hivi, Angalia, mtoto atazaliwa katika nyumba ya Daudi, JINA LAKE YOSIA; na juu yako atawachinja makuhani wa mahali pa juu, wanaofukiza uvumba juu yako, na mifupa ya watu itateketezwa juu yako.

3 Akatoa ishara siku ile ile, akasema, Hii ndiyo ishara aliyoinena Bwana, Tazama, madhabahu itapasuka, na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.

4 Ikawa, mfalme Yeroboamu alipoyasikia maneno ya yule mtu wa Mungu, alipopiga kelele juu ya madhabahu huko Betheli, alinyosha mkono wake pale madhabahuni, akasema, Mkamateni. Basi ule mkono wake aliounyosha ukakatika, wala hakuweza kuurudisha kwake tena.

5 Madhabahu ikapasuka, majivu ya madhabahuni yakamwagika, sawasawa na ishara aliyoitoa mtu wa Mungu kwa neno la Bwana”.

Huyu nabii alipomaliza kutoa Ishara ile akaondoka zake,..Lakini maneno yale yalisikiwa sio tu na wale waliokuwa pale, bali pia habari ile ilivuma Israeli yote, kwamba kuna mtoto atazaliwa naye ataitwa YOSIA ndiye atakayekuwa na ujasiri wa kuja kuibomoa madhabahu hiyo ya ndama iliyopo Betheli karibu na Yerusalemu, na nyingine zote, ziliyosimamishwa na Yeroboamu,..Na hatazaliwa katika Israeli ufalme wake, bali atazaliwa katika YUDA ufalme wa Daudi..

Basi pengine ilidhaniwa jambo hilo lingetokea kwa mzao aliyefuata wa mfalme wa Yuda aliyekuwa anatawala kipindi hicho, aliyeitwa Rehoboamu, lakini hakuwa huyo, wakatazamia pengine mjukuu wake, bado hakuwa huyo, wakatazamia pengine atakayefuata baada ya huyo bado haikuwa hivyo. Leo hii tukiona unabii wa Mungu unachelewa ni rahisi kusema mtu huyu si wa Mungu, hata kama Mungu alilithibitisha hilo kwa ishara kubwa kiasi gani, kitendo tu cha unabii kuchelewa basi tayari tunahitimisha kuwa yule ni nabii wa uongo….

Siku zikapita hivyo hivyo mpaka kikanyanyuka kizazi kingine kisichowajua manabii hao, Na siku zilivyokuwa zinazidi kwenda ndivyo uovu ulivyokuwa unashamiri katika Taifa ya Israeli na Yuda, mpaka enzi za mfalme Ahabu, lakini bado huyo Yosia hajulikani,..Watu wa kejeli walikuwepo, kama tu walivyo wengi sasa hivi, wanaosema huyo YESU aliyesema anarudi yupo wapi?. Wafalme 20 ishirini walipita juu ya Israeli, Yosia bado hajazaliwa…Mpaka taifa nzima linaondolewa na kuchukuliwa utumwani Ashuru, bado Yosia hajazaliwa, hapo ndipo unabii wa namna hiyo unathibitika kuwa ni batili, kwani mpaka taifa halipo tena hakuna chochote kinachoweza kutokea, hata akizaliwa leo atakuwa na faida gani…Lakini siku zilizidi kuendelea..

Miaka kama 300 baadaye tangu unabii ulipotolewa, wakati taifa la Yuda peke ndio liliobakia Israeli, mfalme mmoja aliyejulikana kama mfalme Amoni, akamzaa mtoto akamwita jina lake Yosia, mtoto huyu katika umri wa miaka 15 alianza kuutafuta uso wa Mungu kwa bidii sana, na alipofika umri wa miaka 19, alianza kusafisha, madhabahu zote za mabaali na maashera na mahali pa juu, ambazo baba zake walishindwa kufanya,.kwa muda miaka yote hiyo, alizifanya kuwa vumbi, yaani hakuacha sanamu yoyote katika Yuda, isitoshe hakuishia hapo alipanda mpaka kule Israeli ambapo sio hiyama yake, akasafisha kila madhabahu ya mabaali aliyokutana nayo njiani, aliipondoponda na kuiichoma, na alikuwa haondoki mpaka ahakikishe imekuwa jivu, akawaua wapunga pepo wote, na makuhani wao, vile vile akafukua makaburi ya makuhani wao waliokuwa wanaifukizia uvumba zamani, moja baada ya lingine, na kutoa mifupa yao, na kuisagasaga

Mpaka alipofikia kwenye kaburi moja lililokuwa kando-kando ya madhabahu zile, akaliona limekewa kumbukumbu juu yake, akaisoma, akasema hii ni kumbukumbu ya nani?..ndipo akaambiwa, hebu tusome ili tuelewe vizuri..

2 Wafalme 23:17 “Kisha akasema, Ni kumbukumbu la nani, hili ninaloliona? Na watu wa mji wakamwambia, Ni kaburi la yule mtu wa Mungu, aliyetoka Yuda, akayanena mambo hayo uliyoyatenda wewe juu ya madhabahu ya Betheli.

18 Akasema, Mwacheni; mtu awaye yote asiiondoe mifupa yake. Basi wakaiacha mifupa yake, pamoja na mifupa ya yule nabii aliyetoka Samaria.”

Ndipo hapo Israeli yote ikajua kumbe huyu ndiye aliyetabiriwa vile vile zamani, na Yosia akagundua kumbe Mungu alishauona wema wake tangu zamani, na kumwekea kumbukumbuku lake. Haleluya. Maandiko yanatuambia hakukuwa na mfalme aliyemwelekea Mungu kwa moyo wake wote kama ilivyokuwa kwa Yosia, Alimfanyia Mungu sherehe kubwa ambayo haikuwahi kufanywa Israeli tangu enzi za wafalme, isitoshe alikwenda kulikarabati hekalu la Mungu ambalo lilikuwa limechakazwa na wafalme waliotangulia.

2Wafalme 23:25 “Kabla ya huyo hapakuwa na mfalme mfano wake, aliyemwelekea Bwana kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kwa nguvu zake zote, sawasawa na sheria zote za Musa; wala baada yake hakuinuka mmoja mfano wake yeye.”

Ndugu kanuni ya Mungu ni ile ile wala hana upendeleo biblia inasema, Mungu huwapa thawabu wale wote wamtafutao kwa bidii,(Waebrania 11:6), Na wewe pia unaweza ukawa YOSIA ya KRISTO leo, ikiwa tu utataka kumwelekea Mungu kwa moyo wako wote, kwa nguvu zako zote na kwa akili zako zote bila kujali dini yako inaamini hiki au uamini hiki, ndugu zako wanasema hivi au hawasemi hivi. Ukianza leo hakika kumbukumbu lako Bwana alishaliweka, kama hutalifahamu leo hii basi utafahamu siku ile unayomalizia mwendo kama vile YOSIA. Utakuja kugundua kuwa Mungu alishaziandika thawabu zako kabla hata hujazaliwa, kama ilivyo kwa Yosia, Hivyo habari ya Yosia ni habari ya kutupa moyo kukaza mwendo kwasababu Mungu anaijua hatima yetu na kazi zetu na bidi zetu kabla hata hatujazaliwa..

Na pia habari hii inatufundisha kuwa unabii wa Mungu alioutoa ni lazima uje kutimia haijalishi utachukua miaka mingapi, lakini ni lazima uje kutimia, hapa ulitolewa lakini ulikuja kutimia baada ya miaka 300, wakati ambao watu hawatazamii kama ungekuja kutimia, kadhalika Yesu alisema atarudi…hakika atarudi, na wala hadanganyi…Unabii huo upo karibuni sana kutimia, inaweza ikawa ni leo. Je! Umeokolewa? Wewe utakuwa ni miongoni mwa watakaoenda naye?

Bwana akubariki sana.

Kwa Maombezi, Ushauri, au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/+225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

LAANA YA YERIKO.

MFALME ANAKUJA.

NEHUSHTANI (NYOKA WA SHABA).

NGUVU ZA ZAMANI ZIJAZO:


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Eng.Azza Msuya
Eng.Azza Msuya
1 year ago

Amen Mungu AWABARIKI SANA