BADO KITAMBO KIDOGO HAMNIONI

BADO KITAMBO KIDOGO HAMNIONI

Bwana Yesu alisema, ilimpasa yeye aondoke ili Roho Mtakatifu aje, hata hivyo Roho Mtakatifu sio kitu kingine tofauti na Yesu, bali ni yeye yeye Bwana Yesu katika mfumo wa Roho,

Kwamfano Mchawi anapotaka kukiloga kikundi cha watu Fulani au kijiji, hawezi kufanya uchawi wake kwa namna ya kimwili bali atakiendea kijiji kile au watu wale kwa namna ya Roho isiyoweza kuonekana kwa macho na kuleta madhara makubwa sana katika kile kijiji. Atakuwa ana uwezo wa kudhuru watu hata 100 kwa mda mfupi kuliko kuwa katika mwili. Sasa ni Yule Yule mchawi ila anatenda kazi katika namna ya roho.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ili kwamba ajipatie matokeo makubwa zaidi ilimpasa aondoke katika namna ya kimwili, ili aje tena katika namna ya roho ili alete matokeo makubwa zaidi katika ulimwengu.

Na ndio maana Bwana Yesu kabla ya kuondoka aliwaambia wanafunzi wake, kwamba bado kitambo hawamwoni na tena bado kidogo watamwona tena, akimaanisha kuwa muda mfupi baadaye atakwenda kusulibiwa na atachukuliwa juu mbinguni nao hawatamwona tena, lakini baada ya kusulibiwa na kupaa muda mfupi baadaye watamwona tena (atakuja kwao) kwa namna ya Roho katika siku ile ya Pentekoste..

Tunasoma ;

Yohana 16:12 “Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa.

13 Lakini yeye atakapokuja, HUYO ROHO WA KWELI, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.

14 Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.

15 Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari.

16 BADO KITAMBO KIDOGO NANYI HAMNIONI; NA TENA BADO KITAMBO KIDOGO NANYI MTANIONA.

17 Basi baadhi ya wanafunzi wake wakasemezana, Neno gani hilo asemalo, BADO KITAMBO KIDOGO NANYI HAMNIONI, NA TENA BADO KITAMBO KIDOGO NANYI MTANIONA? NA HILO, KWA SABABU NAENDA ZANGU KWA BABA?

18 Basi walisema, Neno gani hilo asemalo; hilo, Bado kitambo kidogo? Hatujui asemalo.

19 Yesu alifahamu ya kwamba wanataka kumwuliza, akawaambia, Ndilo hilo mnaloulizana, ya kuwa nalisema, BADO KITAMBO KIDOGO NANYI HAMNIONI, NA TENA BADO KITAMBO KIDOGO NANYI MTANIONA?”

Kwahiyo ili Bwana Yesu aweze kuhudumia mamilioni ya watu waliopo duniani asingeweza kubaki katika ile hali ya mwili, ilimpasa aje kwa namna ya Roho, ili aweze kuwaganga moyo wengi waliovunjika moyo, ili aweze kuwafundisha watu wengi wa ulimwengu mzima, ili aweze kuwatembelea majumbani mwao, mtu mmoja mmoja, lakini katika ile hali ya mwili aliyokuwepo ingekuwa ni ngumu, ingechukua mamilioni ya miaka kutimiza kusudi lake, hivyo ilimpasa abadili njia ya kuwafikia wanadamu, kwa sababu hiyo basi akawaambia wanafunzi wake bado kitambo kidogo nanyi hamnioni na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona, na kweli siku ile Bwana Yesu alipoondoka wanafunzi wake walihuzunika sana, wakajihisi kuwa mayatima, wakajifungia ndani kwa hofu ya wayahudi, mioyo yao ilikuwa mizito kwasababu Bwana ameondoka, lakini tunasoma katika siku ile ya Pentekoste Roho Mtakatifu alipowashukia mioyo yao ilihuishwa tena, wakapata ujasiri wa hali ya juu, wakamwona Kristo tena, wakamuhisi wapo karibu naye kuliko hata hapo kabla walipokuwa naye. Walipokea nguvu ya ajabu, Huyo alikuwa ni Yule Yule Kristo katika Roho. Na baada ya hapo ndio tunaona injili ikaenda duniani kote.

Injili ilianza kuenea kwa kasi duniani kote nguvu sana, kwasababu Kristo hatendi kazi tena katika mwili mmoja bali katika Roho, hivyo matokeo yake yanakuwa ni makubwa zaidi, ni Kristo Yule Yule hajabadilika lakini sasa hatumii tena njia ile aliyokuwa anaitumia, bali anatumia njia iliyobora zaidi kuufikishia ulimwengu wokovu.

Ni sawa na mtu aliyekuwa anatangaza biashara yake kwa mabango barabarani kwenye hari za jua kali, lakini baadaye akabadilisha mbinu na kuanza kutumia mitandao kutangaza matangazo yake ili kupata matokeo makubwa zaidi, sasa huyo mtu hajabadilika ni yeye Yule Yule isipokuwa tu amebadilisha njia ya kuwafikia watu. Badala ya yeye kwenda kugonga nyumba moja moja kutangaza biashara yake, ambapo pengine kwa siku angewafikia watu 100 tu! sasa anatumia mitandao ya kijamii ambapo kwa siku anaweza kuwafikia hata watu laki moja na zaidi, pasipo hata yeye kuwepo maeneo yao. Kwa kupitia mitandao anakuwa anatimiza kusudi lile lile kama tu angetumia miguu yake..tena zaidi ya yote anapata matokeo bora zaidi.

Kadhalika Bwana Yesu alisema.. “Walipo wawili au watatu wamekusanyika kwa jina langu, MIMI NIPO PAPO HAPO KATIKATI YAO”

Unaona hapo? Hayupo kwa namna ya kimwili lakini yupo kwa namna ya Roho, kwahiyo kama wakikusanyika wawili au watatu kwa jina lake, hasemi uongo ni kweli yupo katakati yao, sawa tu na kama angekuwepo kwa namna ya kimwili.

Kaka/ Dada unayesoma ujumbe huu, ni muhimu kujua kwamba Kristo yupo leo anatembea ulimwenguni, anafanya kazi zile zile, isipokuwa tu haonekani kwa macho, ni Kristo Yule Yule aliyekuwa anatembea na wakina Petro, ni Yule Yule aliyekuwa anagonga kwenye jumba za watu, na kwenye miji ili aingie aihubiri injili. Na wale waliomkubali aliwapa uzima wa Milele na wale waliomkataa aliwaacha na kwenda kwa wengine, Na leo ndio Yule Yule anagonga katika mioyo ya watu kwa namna ya Roho akitaka aingie ayabadilishe maisha ya watu na kuwaletea wokovu. Aliwaambia wanafunzi wake maneno haya wakati anawatuma kwenda kuhubiri injili…

Luka 10:10 “Na mji wo wote mtakaouingia, NAO HAWAWAKARIBISHI, TOKENI HUMO, nanyi mkipita katika njia zake semeni,

11 HATA MAVUMBI YA MJI WENU YALIYOGANDAMANA NA MIGUU YETU TUNAYAKUNG’UTA JUU YENU. Lakini jueni hili, ya kuwa Ufalme wa Mungu umekaribia.

12 Nawaambia ya kwamba SIKU ILE ITAKUWA RAHISI ZAIDI SODOMA KUISTAHIMILI ADHABU YAKE KULIKO MJI HUO”.

Umeona ndugu?, hakuna nafasi ya pili kama ukimkataa Kristo kwa makusudi sasa, unapohubiriwa injili yake kwa Roho wake, anaondoka na kwenda kwa mwingine? Na kwako inabakia kuwa hukumu. Biblia inasema waasherati wote, wasengenyaji, walafi, walawiti, walevi,wachafu,watukanaji, wala rushwa, waabudu, sanamu sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti, HAIDANGANYI!! Ni kweli itakuwa hivyo, mtu yeyote anayekuambia kwamba walevi wataokolewa anakudanganya, yeyote anayekuambia kwamba wanaopaka wanja na lipstiki na kuvaa wigi na suruali na herein wataokolewa kwamba Mungu haangalii Roho anaangalia mwili, nataka nikuambia jambo hili moja Roho Mtakatifu anasema sehemu yao itakuwa ni KATIKA LILE ZIWA LA MOTO!!. Anayekuambia kwamba kuwa kuishi na mwanamume au mwanamke ambaye hamjafunga ndoa au ambaye ameachana na mke/mume wake sio dhambi, anakudanganya Yesu Kristo anazungumza na wewe leo kwa namna ya Roho, kwamba “AMWACHAYE MKE WAKE NA KUOA MWINGINE AZINI, NAYE ALIYEMUOA YULE ALIYEACHWA AZINI” Mtii Yesu Kristo leo na maneno yake, Usiusikilize uongo wa shetani ambao baadaye utakufanya ujute milele.

Bwana alisema..UFUNUO 3: 20 “TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI, NABISHA; MTU AKIISIKIA SAUTI YANGU, NA KUUFUNGUA MLANGO, NITAINGIA KWAKE, NAMI NITAKULA PAMOJA NAYE, NA YEYE PAMOJA NAME”.

Tubu leo kama hujafanya hivyo, mpe Bwana maisha yako ayabadilishe, kabla hajaacha kugonga ndani ya moyo wako na kuhamia kwa mwingine, ukishatubu fanya hima ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwenye maji mengi na kwa Jina la Yesu Kristo, kwa ajili ya ondoleo la dhambi, uwe na uhakika wa wokovu wako na BWANA mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake, ndipo utakapokuwa na uhakika wa kuzaliwa mara ya pili.

Bwana akubariki.

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments