Title January 2019

KUNDI LA MALAIKA WALETAO MABAYA.

Pale tu mtu anapogeuka na kuacha maisha yake ya dhambi, na kukusudia kutoka rohoni kumfuata Kristo siku zote za maisha yake, kisha akabatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kama biblia iagizwavyo kwa ajili ya ondoleo la dhambi zake (Matendo 2:38), basi kuanzia huo wakati na kuendelea Mungu humpa kipawa cha Roho Mtakatifu, kama msaidizi na kumwongoza katika kuijua kweli yote. Na zaidi ya hayo mtu huyo hupewa zawadi nyingine nayo ni kuhudumiwa na malaika watakatifu wa Bwana, anakuwa anatembea na malaika wa Bwana.

Waebrania 1:14 “Je! Hao wote [malaika] si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?”

Sasa malaika hawa hutumwa kuhakikisha usalama wa huyu mtu kwa kila namna, kuhakikisha uzima wa huyu mtu, kuhakikisha mapenzi yote ya Mungu yanatendekea kwa huyu mtu bila ya kuongezwa au kupunguzwa. Ikiwa Mungu amependa mwanawe kwa kipindi fulani apitie katika bonde la uvuli wa mauti kwa muda, lakini asidhuriwe wala asife, basi malaika hawa wanaotembea naye ndio watakao hakikisha kuwa hadhuriki kwa namna yoyote ile katika majaribu yoyote atakayokumbana nayo, anaweza kukutana na hatari hata ya kufa lakini wengine wote wanaweza wakafa yeye akabaki mzima. Sasa hii kazi inafanywa na hawa malaika watakatifu wa Mungu.

Tunamwona mfano Daudi, ulifika wakati Mungu aliruhusu, awindwe na maadui zake, mpaka wakati mwingine anaona hakuna mlango wa kumkwepa Sauli, lakini mara zote hizo alizokuwa katika shida na hatari za kufa hakuwahi kudhuriwa na lolote.

Kadhalika Ikiwa ni mapenzi ya Mungu kumbariki mwanawe na kumfanikisha katika jambo aliloikusudia au aliloombwa na mwanawe kwa wakati huo basi wale malaika watahakikisha njia zote za mafanikio zinamfikia yule mtu kwa wakati husika, watatengeneza mifereji yote ya mafanikio ili tu kufanikisha lile kusudi waliloitiwa kulifanya, ambalo ni kuwahudumia watakatifu. Hivyo tunaona faida ni nyingi sana kwa mtu yule aliyezaliwa mara ya pili na kumfanya Mungu kuwa tegemeo lake.

Na ndio maana Mungu anaitwa BWANA WA MAJESHI,.Analo jeshi kubwa sana la malaika wa kila namna, na wote hao ni kwa kusudi la kuwahudumia tu watakatifu. Lakini kama hujawa mtakatifu kwa kuzaliwa mara ya pili basi ni kinyume chake, ufalme mwingine utakuwa unakuongoza na huo si mwingine zaidi ya ufalme wa giza, na kundi la roho chafu litakuwa ndio limekuzunguza muda wote, hilo ndilo linalolokuhudumia wewe, ili kukupa nguvu ya kuendelea kutamani mabaya, kuendelea kuzini, kuendelea kukupa kiu ya pombe na sigara, kutazama pornography, kufanya mustabation, kuendelea kuwa shoga, kuendelea na usagaji,kuendelea kula, kuendelea kuiba, kutukana,kula rushwa..n.k.. Unaweza ukawa unatamani kuacha hayo mambo lakini huwezi kwa nguvu zako kwasababu ufalme wenye nguvu zaidi yako upo juu yako na MKUU WA ANGA hili amekufanya kuwa mfu kwa habari ya mambo mema..

Waefeso 2: 1 “Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu;

2 ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata MFALME WA UWEZO WA ANGA, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;

3 ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine.”

Lakini leo tutaona malaika watakatifu jinsi wanavyotenda kazi kwa wale watu wanaojiona kuwa ni wakristo lakini ni vuguvugu, wale ambao Mungu alishawakomboa, wale ambao wameshaonja vipawa vyote vya Mungu lakini bado hawataki kusimama imara, wale ambao wameshadumu katika imani kwa muda mrefu lakini ukitazama maisha yao ni mguu mmoja ndani, mguu mmoja nje, leo wapo kwa Mungu kesho wapo kwa shetani, ni mkristo anaye itangaza injili kwa njia ya uimbaji lakini ni mwasherati, kwa siri na anakunywa pombe, na huyo huyo bado anashiriki meza ya Bwana na kutawadhana miguu, anahudhuria ibadani, anajisitiri lakini kwasiri ni mtukanaji na anakwenda kwa waganga wa kienyeji. Yani kwa ufupi mtu ambaye ni vuguvugu.

Sasa kumbuka watu wa namna hiyo mwanzoni walianza vizuri, na kwa jinsi Mungu alivyomwaminifu wa ahadi zake, siku ile walipokata shauri kuokoka Bwana alilituma jeshi la malaika zake watakatifu watembee nao. Hivyo siku zile za kwanza ukiwauliza wokovu kwako ulikuwaje watasema nilikuwa namwona Mungu sana katika maisha yangu akinipigania. Ni kweli ni lazima uone hivyo kwasababu jeshi la Mungu aliye mkuu sana linatembea na wewe. Lakini baadaye kidogo alipoanza kukengeuka kumchanganya Mungu na dunia, mguu mmoja huku na mwingine kule ndipo hali yake ikaanza kuwa mbaya sana, anaona hasongi tena mbele kwa habari ya wokovu, anaenda mbele anarudi nyuma, magonjwa sasa yanamwandama, taabu na masumbufu asiyoelewa chanzo chake ni nini!. Hajui kuwa ni wale wale malaika watakatifu ambao walitumwa na Bwana kumuhudimia wamegeuka sasa na kuwa KUNDI LA MALAIKA WALETAO MABAYA.

Wana wa Israeli walipokuwa Misri Mungu aliwatumia malaika zake, kuwapigania, unaona yale mapigo yote yaliyokuwa yanatokea Misri, maji kuwa damu, nzige, giza, mvua ya mawe, pigo la mzaliwa wa kwanza n.k. Ilikuwa ni kazi ya malaika waliotumwa kutekeleza maagizo ya Mungu kwa ajili ya kuwakomboa watoto wake.

Zaburi 78: 45 “Aliwapelekea mainzi wakawala, Na vyura wakawaharibu.

46 Akawapa tunutu mazao yao, Na nzige kazi yao.

47 Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, Na mikuyu yao kwa mawe ya barafu.

48 Akaacha ng’ombe zao wapigwe kwa mvua ya mawe, Na makundi yao kwa umeme.

49 Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, KUNDI LA MALAIKA WALETAO MABAYA.

50 Akiifanyizia njia hasira yake; Wala hakuziepusha roho zao na mauti, Bali aliiachia tauni uhai wao;

51 Akampiga kila mzaliwa wa kwanza wa Misri, Malimbuko ya nguvu katika hema za Hamu.”

Lakini pindi tu walipovuka bahari ya Shamu, baada ya kubatizwa kwao, Mungu aliwaonya mapema kabisa na kuwaambia maneno haya.

Kutoka 23: 20 “Tazama, mimi namtuma MALAIKA AENDE MBELE YAKO, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea.

21 Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; WALA MSIMTIE KASIRANI; maana, hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake.”

Unaona hapo?, wana wa Israeli walionywa mapema sasa mmeokoka, na mimi nawatumia malaika wangu kuwahudumia mbele yenu, kuweni makini kwasababu mkifanya makosa hatawasamehe kwasababu maagizo yangu yapo ndani yake. Lakini wana wa Israeli hawakulitilia hilo maanani kama walivyo wakristo wengi leo hii, wanakwenda kubatizwa, wakidhani lile ni jambo la kimasihara tu, isitoshe wanakwenda kushiriki meza ya Bwana, lakini wakitoka hapo wanarudia mambo yale yale waliyoyaacha huko nyuma..Sasa unadhani ni jambo gani litamkuta mtu wa namna hiyo? Wale malaika waliokuwa wanatembea naye watampinga..Na ndio maana hata siku za Mwisho Mungu atakapoikuhumu dunia nzima, atatumia malaika zake, kuleta mapigo juu ya nchi, wataipiga bahari na kuwa damu, milima na visiwa vitahamishwa, watalitia jua giza wakati wa adhuhuri, Na hao hao ndio watakaowakusanya waovu wote pamoja na shetani na kuwatupa katika lile ziwa la Moto.

Kama vile wana wa Israeli walivyotumiwa lile jeshi la malaika waletao mabaya, ndivyo itakavyokuwa kwa mtu yule asiyemama imara mbele za Mungu. Wana wa Israeli mapigo ambayo yangewapasa yawakute adui zao ndio yaliyowakuta wao, kwa manung’uniko yao, kwa zinaa zao, kwa anasa zako, kwa kuabudu kwao sanamu, kwa ulevi wao, ndipo walipokuta na wale nyoka wa moto kule jangwani, tauni, ardhi kupasuka na kuwameza, n.k. Hivyo ndivyo kizazi kile chote kilichomchukiza Mungu jangwani kilivyoishia, hakuna hata mmoja aliiona nchi ambayo Mungu aliyokuwa amewaahidia. Isipokuwa Yoshua na Kelebu miongoni mwa wale wote waliotoka Misri.

Na ndivyo ilivyo hata kwetu sisi tutakaposhindwa kuupambanua mwili wa Kristo, na kujiaumulia kufanya tunayotaka kwa kivuli cha wokovu, na ndio maana biblia inasisitiza NI HERI KUWA MOTO AU BARIDI KULIKO KUWA VUGUVUGU. Wakati mwingine maisha ya mtu yanaweza kukatizwa, anaweza kukumbwa na magonjwa yasiyoponyeka, anaweza kukutana na mikosi ya ajabu akidhani ni shetani kamletea, kumbe hajui ni mwenendo wake wa uvuguvugu, ndio unaomtia Mungu wivu.(Soma 1Wakorintho11:17-14 utathibitisha jambo hilo ).

Lakini Wale wa nje hawawezi kumtia Mungu wivu kwasababu hawajakombolewa hivyo si wa Mungu, hawajanunuliwa kwa damu ya Kristo. Ni sawa sawa na wale wamisri, Mungu hakushughulika baada ya Wana wa Israeli kutoka Misri, waliendelea na miungu yao wala Mungu hakuizungumzia tena baada ya pale, bali alishughulika zaidi na watu wake (Wana wa Israeli) aliokuwa amekwisha kuwakomboa.

Waebrania 3:16 “Maana ni akina nani waliokasirisha, waliposikia? Si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa?

17 Tena ni akina nani aliochukizwa nao miaka arobaini? Si wale waliokosa, ambao mizoga yao ilianguka katika jangwa?

18 Tena ni akina nani aliowaapia ya kwamba hawataingia katika raha yake, ila wale walioasi?

19 Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.

Waebrania 4 : 1 “Basi, ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa.

2 Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanganyika na imani ndani yao waliosikia.

3 Maana sisi tulioamini tunaingia katika raha ile; kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu:”

Hivyo Kaka/Dada Biblia inatuagiza tuutimize wokovu wetu KWA KUOGOPA NA KUTETEMEKA, kwa maana ni Mungu ndiye atendaye kazi ndani yetu.(wafilipi 2:12), Hivyo Mungu hasemi hivyo kwa kututisha lakini badala yake anataka kutubariki.

Tufurahie wokovu wetu pamoja na lile kundi kubwa la Jeshi la mbinguni linapotembea na sisi kutuhudumia. Tutaishi bila hofu, tutaisha bila wasiwasi tutaishi kwa amani tutaishi kwa furaha tukijua kuwa hakuna nguvu yoyote itakayoweza kushindana nasi kwasababu sisi ni uzao mteule wa kifalme, watu wa milki ya Mungu mwenyewe.

Hivyo nikutie moyo wewe ambaye umeokolewa na unaendelea kumcha Mungu na kutembea katika njia zake, uwe na uhakika kuwa hakuna chochote kitakachoweza kwenda kinyume chako kwasababu jeshi la Mungu wa Miungu YESU KRISTO linatembea na wewe daima, kukiongoza na kukulinda na kukuhudumia.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine na Mungu atakubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Print this post

JE! ULEVI NI DHAMBI?.

Ulevi ni dhambi?…Shalom, mtu wa Mungu, karibu tujifunze Neno la Mungu, ambapo leo tutajifunza kwa ufupi juu ya unywaji wa Pombe (au ULEVI). Kumekuwa na mgawanyiko wa makundi mengi katikati ya Wakristo; ambapo wapo wanaoamini kuwa unywaji wa pombe sio dhambi na wapo wanaoamini kuwa pombe imehalalishwa katika maandiko. Na kila kundi linadai kuwa na maandiko ya kusimamia.

Lakini ni muhimu kufahamu kuwa “kuielewa Biblia sio kusoma kile kilichoandikwa pale na kwenda kukushikilia kama kilivyo”..Hapana bali ni kuelewa “ufunuo wa kile kilichoandikwa pale kwa uongozo wa Roho Mtakatifu na kukifanyia kazi”.. Vinginevyo biblia utaiona kuwa inajichanganya mahali na mahali, na kukiona kama ni kitabu cha Uongo, lakini tunajua Biblia ni Kweli wala hakuna chochote kilichokosewa wala cha uongo.. Kama tunaona kuna mahali inajichanganya basi tujue kwamba si biblia inayojichanganya bali ni ufahamu wetu ndio unaojichanganya juu ya kile tunachokisoma.

ulevi ni dhambi

Biblia Takatifu imegawanyika katika sehemu mbili: AGANO LA KALE na AGANO JIPYA. Utendaji kazi wa Mungu katika Agano la kale ni tofauti kidogo na utendaji wake katika Agano jipya ingawa Mungu ni Yule Yule. Hata katika maisha ya kawaida utendaji kazi wa Serikali iliyokuwa mwaka 1990 ni tofauti na hii iliyopo awamu hii, Ingawa Serikali ni ile ile, isipokuwa tu imerekebisha sera zake, katiba yake, na Huduma zake kwa wananchi. Na madhumuni ya kubadilika utendaji kazi wa serikali ni ile kumfanya mwananchi akae katika hali iliyo bora zaidi kuliko ile aliyokuwa hapo kwanza.

Kadhalika katika Ufalme wa Mbinguni, baada ya Adamu kuasi, Mbingu zilishusha mwongozo wa Kwanza wa namna mwanadamu anavyotakiwa kuishi huo mwongozo ndio unaoitwa Agano la Kale, na Baada ya Muda Fulani, Mbingu zikaleta mwongozo mwingine mpya (katiba mpya )itakayomkamilisha mwanadamu katika ukamilifu wote na hiyo katiba ndio inayoitwa AGANO JIPYA. Kwahiyo Agano jipya ndio utimilifu wa Mwanadamu..Agano la kale halikuweza kumkamilisha mwanadamu..Lakini Mungu ni Yule Yule hajabadilika.

Kwahiyo yapo mambo ambayo Mungu aliyaruhusu katika Agano la Kwanza (yaani Agano la kale) ambayo hayakuwa mapenzi yake kamili, kwamfano Bwana Mungu aliruhusu katika agano la kale, kuwepo na ndoa za mitara (yaani ndoa za mwanaume mmoja kuoa wake wengi)…Lakini katika Agano jipya tunaona Bwana anasema mambo hayo yaliruhusiwa lakii haikuwa hivyo tangu mwanzo (ndoa inapaswa iwe ya mume mmoja na mke mmoja), na hivyo sio sahihi kuwa na mke zaidi ya mmoja.

Kadhalika tunaona pia Katika agano la kale, Bwana aliruhusu Mwanadamu kuua mtu yoyote anayeenda kinyume na maagizo yake aliyoyatoa katika torati, mfano mtu katika Israeli akionekana anaabudu sanamu, au miungu mingine sheria ilikuwa ni kuuawa..Lakini katika agano jipya hilo jambo halipo, tumeambiwa tusiue kabisa, na wala tusilipize kisasa, Mungu mwenyewe ndiye atakayelipa.

Katika agano la kale pia Mungu aliruhusu talaka, yaani aliruhusu Mwanamume kutoa hati ya talaka kwa mkewe endapo wamekosana, lakini katika Agano jipya Hatujapewa ruhusa ya kutoa talaka ya namna yoyote ile, wala kuachana isipokuwa kwa habari ya uasherati tu. Na vivyo hivyo kuna mambo mengine mengi ambayo Agano la kale iliruhusu lakini agano jipya imezuia.

Na pia tunaona katika agano la kale, damu iliyokuwa inatumika kuondoa dhambi ilikuwa ni damu ya wanyama, lakini katika agano jipya lililo bora zaidi ilitumika damu ya mtu mmoja mtakatifu kwa ajili ya ondoleo la dhambi, kwasababu damu za wanyama zisingeweza kuondoa dhambi bali zilifunika tu.

Na leo tutazungumzia jambo moja ambalo Mungu aliliruhusu katika agano la kale na akalizuia katika Agano jipya. Kwasababu halikuweza kumkamilisha mwanadamu.

Hebu tusome mstari ufuatao..

Mithali 31: 1 “Maneno ya mfalme Lemueli; mausia aliyofundishwa na mama yake.

2 Ni nini, mwanangu? Tena ni nini, mwana wa tumbo langu? Tena, ni nini mwana wa nadhiri zangu?

3 Usiwape wanawake nguvu zako; Wala moyo wako usiwape wale wawaharibuo wafalme.

4 Ee Lemueli, kunywa mvinyo hakuwafai wafalme, hakuwafai wafalme; Wala haifai wakuu waseme, Ki wapi kileo?

5 Wasije wakanywa na kuisahau sheria, Na kuipotosha hukumu ya mtu aliye taabuni.

6 Mpe kileo yeye aliye karibu na kupotea;

Kampe divai yeye aliye na UCHUNGU NAFSINI.

7 Anywe akausahau umaskini wake; Asiikumbuke tena taabu yake”

Ukisoma huu mstari kwa haraka pasipo kujua utendaji kazi wa Mungu katika nyakati tofauti tofauti unaweza ukasema “Mungu kahalalisha unywaji wa Pombe”…Na pia ukisoma mstari huu haraka haraka unaweza ukasema Mungu kahalalisha uuaji “Usimwache mwanamke mchawi kuishi (kutoka 22: 18)”., au usomapo mstari huu unaweza ukasema Mungu kahalalisha visasi “Walawi 24: 19 Na mtu akimtia mwenziwe kilema; vile vile kama alivyofanya, naye atafanyiwa vivyo; jeraha kwa jeraha, jicho kwa jicho, jino kwa jino; vile vile kama alivyomtia mtu kilema, naye atalipwa vivyo”

Kwahiyo unaona mistari hiyo Mungu alihalalisha mambo yasiyo sahihi yafanyike miongoni mwa watu wake ili wakae kwa utulivu na ustaarabu, ndio maana unaona alihalalisha visasi, alihalalisha mauaji kwa waabudu sanamu, n.k

Lakini pia aliruhusu UNYWAJI WA DIVAI, (kumbuka, ni divai tu ndiyo iliyohalalishwa sio kilevi chochote nje na hicho) na ilihalalishwa kwa watu walio katika UCHUNGU na walio katika shida, na umaskini mkali, ili wanywapo wakausahau Umaskini wao…Lakini kama tunavyosema agano la kwanza halikumkamilisha mwanadamu..Mtu anaweza kweli kunywa divai, akalewa akausahau umaskini wake kwa wakati ule aliokuwa amelewa tu, lakini akili yake itakaporudi atakuwa bado ana kumbukumbu la umaskini wake na uchungu wake katika maisha yake (shida zake zipo palepale).

kwahiyo kilevi hakingeweza kumweka huru mtu mbali na uchungu nafsini, au hali ya kukosa raha nafsini, kama tu vile damu ya ng\ombe na Mbuzi isivyoweza kuondoa dhambi bali kufunika kwa kipindi kifupi tu, na baada ya muda kunakuwa na kumbukumbu la dhambi ndivyo ilivyo kwa divai. Na tunaona pia mbali na divai kumfanya mtu asahau umaskini wake kwa kitambo, bado pia ilikuwa inamfanya mtu kwa sehemu asahau sheria za Mungu..Kwahiyo haikuwa ni dawa kamili ya makosa. Ni sawa madaktari watoe dawa ya kwanza ya kutibu ugonjwa Fulani, lakini dawa hiyo haitibu bali inapunguza tu makali, na zaidi ya yote inayomadhara ya pembeni lakini baada ya muda wagundue dawa nyingine ambayo haina madhara kabisa ya pembeni na inatibu ugonjwa wote kabisa.

Hivyo agano la kale lilivyokuwa, tunaweza kulifananisha na dawa hiyo yenye kupunguza makali lakini haiondoi ugonjwa, na zaidi ya yote ina madhara ya pembeni kwa mtumiaji,

Lakini lilivyokuja, agano jipya,yaani agano la Yesu Kristo hilo ndilo tunaloweza kulifananisha na dawa mpya yenye uwezo wa kuondoa ugonjwa kabisa kabisa na isiyokuwa na madhara ya pembeni.Agano hili jipya ndilo lililo na uwezo wa kuondoa dhambi kabisa kabisa, na ndilo lenye uwezo wa kumfanya mtu aliye na uchungu nafsini mwake kupata tumaini, furaha na raha isiyoisha kwasababu pombe inampa mtu tu faraja ya kitambo lakini, Yesu akiwa moyoni mwa mtu anampa raha ya milele isiyoisha.Ndio maana Bwana Yesu alisema..

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; NANYI MTAPATA RAHA NAFSINI MWENU;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.

Unaona! Pombe yetu kwasasa ambayo inaweza kutufanya tusahau shida zetu na uchungu wetu, Ni kuwa na Yesu Kristo ndani yetu, na sio ULEVI. Huyo ndiye atakayekata kamba za mateso, shida, ya huzuni, uchungu na umaskini,…Yeye ndiye Maji yaliyo hai ambayo mtu akiyanywa hataona kiu tena. Divai sio maji yaliyo hai kwasababu mtu akiinywa baada ya muda atakwenda kuitafuta tena.

Lakini utasema mbona Mtume Paulo alihalalisha pombe katika agano jipya na kusema..katika 1 Wakorintho 11: 22 “Je! Hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu? La! Siwasifu kwa ajili ya hayo”

Hapo aliposema “hamna nyumba za kulia na kunywea ” hakumaanisha kuhalalisha ulevi,..tafakari mfano huu> umepanda gari la umma labda akaingia mtu na sigara yake mdomoni na kuanza kuivuta ndani ya lile gari, na wewe ukamwambia samahani tunaomba ukavutie sigara zako nje” je! Kwa sentensi hiyo utakuwa umehalalisha sigara?? Ndicho Mtume Paulo alichokuwa anajaribu kuwaambia hapa, watu baadhi walioko kanisa Koritho ambao walikuwa wanaidharau meza ya Bwana, kwa kunywa divai ile pasipo kiasi mpaka kufikia kulewa.

Kadhalika wapo wanaosema Mtume Paulo alimwambia Timotheo anywe pombe 1Timotheo 5: 23 Tokea sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo kidogo, kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa yakupatayo mara kwa mara..

Kumbuka zamani hawakuwa na piriton, au panadol tulizonazo sisi leo, hivyo tiba ya karibu ambayo ilikuwa inaweza kumfanya mtu atulize magonjwa madogo madogo ilikuwa ni divai tena kwa kiwango kidogo sana. Lakini kwasasa mtu huwezi kutumia divai kutuliza homa zipo dawa nyingi hospitalini zilizobora kushinda hizo na zenye uwezo mkubwa.. Kwahiyo utaona hapo haikunywewa kama kitu cha kujiburudisha mpaka kulewa, bali kama dawa.

Kwahiyo kama maandiko pia yanavyotuambia Waefeso 5: 18 “Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho”.

Hivyo ndivyo Mungu anavyotaka, usikubali kwa namna yoyote kushawishika kwamba Mungu kahalalisha unywaji wa pombe katika nyakati hizi, Ulevi ni dhambi inayowapeleka maelfu kuzimu leo, Ulevi na Uasherati. Jiepushe na hivyo vitu ndivyo vinavyouharibu mwili wa Mtu ambao biblia imesema ni hekalu la Roho Mtakatifu..

1 Wakoritho 6: 9 “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,

10 wala wevi, wala watamanio, WALA WALEVI, wala watukanaji, wala wanyang’anyi”.

Kama hujampa Bwana Maisha yako, fanya hivyo sasahivi, tubu kutoka ndani ya moyo wako, na dhamiria kabisa kuacha dhambi na maisha ya kale uliyokuwa unaishi, anza maisha mapya na Kristo kisha, katafute ubatizo sahihi kulingana na maandiko,wa maji mengi na kwa Jina la Yesu Kristo na Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu, atakayekusaidia kushinda dhambi na kukuongoza katika kuijua kweli yote ya Biblia.

Bwana akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

MATUMIZI YA DIVAI.

TUNAJUA KUWA POMBE INATENGENEZWA NA MTAMA JE! NI SAWA KWA MKRISTO WA KWELI KULIMA MTAMA NA KUUZA NA HATA HIYO HELA KUITUMIA KUTOLEA SADAKA?

MWILI NA DAMU YA YESU KRISTO.


Rudi Nyumbani

Print this post

JIANGALIENI BASI JINSI MSIKIAVYO;

Mwalimu mmoja aliwapa wanafunzi wake fumbo hili, akawaambia watu wawili walikuwa wanatembea barabara wakielekea katika shughuli zao, na mvua ilipoanza kunyesha kwa Nguvu mtu mmoja hakunyeshewa na mvua ile..je! mnaweza kunielezea maana ya sentensi hii? ..

Mwanafunzi mmoja mwerevu akajibu Ndio ninaweza kwani ni wazi kuwa mmojawapo alikuwa na mwamvuli na mwingine hakuwa nao.

Mwingine akasimama kwa furaha na kusema hapana mmoja alipita pembezoni mwa majengo na mwingine barabarani, hivyo Yule wa barabarani ni lazima alilowesha na mvua.

Mwingine akasema, inawezekana mmoja alivaa koti la mvua, na mwingine hakuwa nalo hivyo Yule mwenzake ni wazi kuwa alilowanishwa na mvua.

Kila mwanafunzi alisema la kwake, na ndipo mwalimu akasema ninyi wote mmepeleka mawazo yenu, “ kwa wale watu wawili tu kana kwamba ndio hao peke yao waliokuwa kwenye hiyo sentensi”..Lakini sentensi inasema “mtu mmoja hakunyeshewa”..Hivyo inawezekana wote wawili walinyeshewa na mvua lakini kulikuwa na mwingine aliyekuwa anapita katika njia hiyo, au yupo kwenye gari lake hakunyeshewa.

Wanafunzi wote wakaingiwa na aibu kwa kulijibu juu juu tu bila ya kufikiria kwa undani.

Ndio maana Bwana Yesu alisisitiza akituambia “Luka 8: 18 “JIANGALIENI BASI JINSI MSIKIAVYO; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang’anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho.”

Kwani kama tukiwaangalia hao wanafunzi inawezekana kabisa ni kweli majibu yao yalikuwa ni sahihi, lakini kwa mwalimu wao hayakuwa sahihi.

Unaona kauli hiyo ya Bwana anayosema, ‘hata kile ambacho mtu anadhaniwa kuwa anacho, atanyanganywa’, pale mtu anapojihisi anajua kila andiko, hivyo hakuna haja ya kuhubiriwa na huku anaona kabisa maisha yake hayaakisi kwa namna yoyote maisha ya Kristo. Mtu kama huyo atanyang’anywa hata kile anachodhani anakijua.

Tunaona Maneno hayo Bwana Yesu aliyatamka baada ya kutoa ule mfano wa mpanzi, akisema kuwa wale wote ambao mbegu zao ziliangukia katika miiba,na wengine barabarani, na wengine,na kwenye miamba na wengine kwenye udongo mzuri, wote hao WALISIKIA NENO LA MUNGU kwa wakati mmoja, Ni neno lile lile walilisikia la habari ya Yesu mwokozi, wala hakuna aliyehubiriwa zaidi ya mwingine, lakini viwango vya kusikia vilitofautiana kati ya mmoja na mwingine na ndio maana utaona wengine waliishia njiani, wengine, kwenye miamba, na wengine kwenye udongo mzuri..

Lakini tujiulize Yule aliyeishia kwenye udongo mzuri yeye alisikiaje sikiaje tofauti na wengine mpaka kufikia kuzaa hata 60 mpaka 100, sikio lake lilikuwa ni la namna gani?

Embu tusoma kidogo huo kisha tutapata majibu.

Luka 8:10 “Akasema, Ninyi mmepewa kuzijua siri za ufalme wa Mungu; bali wengine kwa mifano, ili

wakiona wasione, na wakisikia wasielewe.

11 Na huo mfano, maana yake ni hii; Mbegu ni neno la Mungu.

12 Wale wa karibu na njia NDIO WASIKIAO, kisha huja

Ibilisi akaliondoa hilo neno mioyoni mwao,wasije wakaamini na kuokoka.

13 Na wale penye mwamba ndio wale ambao WASIKIAPO hulipokea lile neno kwa furaha; nao hawana mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa hujitenga.

14 Na zilizoanguka penye miiba ni WALE WALIOSIKIA, na katika kuenenda kwao husongwa nashughuli na mali, na anasa za maisha haya, wasiivishe lolote.

15 Na zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao KWA UNYOFU NA WEMA WA MIOYO YAO HULISIKIA neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia.

16 Hakuna mtu ambaye akiisha washa taa huifunika kwa chombo, au kuiweka mvunguni, bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuona nuru yake.

17 Kwa maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo halitajulikana na kutokea wazi.

18 JIANGALIENI BASI JINSI MSIKIAVYO; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kituatanyang’anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho.”

Unaona hapo, wale waliofanikiwa kufika kwenye udongo mzuri, Bwana Yesu anasema KWA UNYOFU, na KWA WEMA hulililisikia na KULISHIKA, kwa KUVUMILIA.

Ni kwanini kama tukitazama leo hii mtu anahubiriwa injili kila siku, lakini inaonekana haina manufaa, miaka inapita haonyeshi badiliko lolote, si kwamba Neno alilohubiriwa linatofauti na la Yule aliyempokea Kristo na kusimama katika Imani, hakuna tofauti yoyote, isipokuwa huyu wa pili Aliangalia jinsi asikiavyo, alizingatia kwa unyofu wa moyo, na kwa wema wote kutokulidondosha hilo aliloambiwa, alilishika na kwenda kulitafakari, na hivyo kwa kufanya vile Mungu akamfunulia akili zake za rohoni kujua maana zaidi ya kile alichokisikia..na ndicho hicho kilichompa nguvu ya kuchukua uamuzi wa kumwishia Bwana mpaka sasa.

Na kwa kuwa hakutaka kulichukulia suala hilo juu juu tu, bali kwa hofu akijua kuwa siku moja atasimama hukumuni na kutoa hesabu ya yote aliyoyasikia, alijishusha na kutii, hivyo Mungu akampa neema zaidi ya kumwelewa yeye kama alivyotaka amwelewe, na kwa jinsi alivyozidi kuendelea kulipalilia lile Neno ndani yake, ndivyo kidogo kidogo Mungu akamjalia kuzaa matunda mengi baadaye. Anaongezewa na vya ziada kwasababu alizingatia kuangalia jinsi anavyosikia.

Inawezekana Injili ya Kristo haijawa na manufaa yoyote kwako kwa miaka mingi, ni kwasababu hauyachukulii maneno ya Mungu katika unyofu wote, unayaona kama ni siasa, na maneno ya kawaida tu, umekuwa ukiyachukulia juu juu tu, na hivyo Mungu amekuacha uendelee kuyasikia lakini usiyaelewa, uyaone tu lakini usiyatambue. Lakini leo hii Mungu amekupa neema ya kuliambua hilo ufanye tena upya maisha yako.

Itakufaidia nini uupate ulimwengu mzima kisha upate hasara ya nafsi yako?, Embu chagua jambo la msingi kwanza kumtii Mungu uokolewe na hayo mengi yaje huko mbeleni kama yatakuwa na muhimu, okoa roho yako kwanza, Sikia Neno la Mungu leo na ulipokee kwa weupe wa moyo kwa mara nyingine tena, ili Bwana akapate kukufunua akili yako uanze kuona uzuri wa wokovu, ili baadaye ukamzalie matunda.

Ikiwa utakuwa tayari kutubu, basi fanya hivyo kwa kudhamiria kabisa kutoka moyoni mwako, kwamba kuanzia leo utazingatia kutii kile Mungu anachosema na wewe, kuacha maisha ya dhambi na baada ya kutubu kwako unapaswa ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na uwe kwa jina la YESU KRISTO ili upate ondoleo la dhambi zako(Matendo 2:38),, kumbuka ubatizo wa vichanga sio wa kimaandiko, kadhalika ubatizo wa kwa jina la Baba na Mwana, na Roho Mtakatifu sio sahihi kwani umetafsiriwa isivyopaswa kwasababu walioubatizia huo hawakuzingatia JINSI WASIKIAVYO…Ubatizo wa kwa jina la YESU KRISTO ndio wa kimaandiko, na ndio uliotumiwa na mitume wote katika kubatizia kwenye biblia. Soma (Matendo 2:38, 8:16, 10:48, 19:5) utayathibitisha hayo mwenyewe.

Hivyo ukiyakamilisha hayo, basi Bwana mwenyewe kuanzia huo wakati atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu atakayekuongoza katika kweli yote. Na hapo utakuwa umeshazaliwa mara ya pili. Ni Wengi wanaosema wameokolewa lakini hawazingatii vigezo vya wokovu vilivyotolewa na Bwana Yesu. Ubatizo sahihi ni muhimu kwa mtu yoyote anayedai amemwamini Kristo. Hivyo fanya hima ukabatizwe tena, kama ulibatizwa ukiwa mtoto au kama hukuwahi kubatizwa kabisa.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine. Na Mungu atakubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

JE! UNA MASIKIO YANAYOSIKIA?

ANGALIA JINSI USIKIAVYO

UMESIKIA SAUTI AU NGURUMO?

NAMNA YA KUITAMBUA SAUTI YA MUNGU INAPOZUNGUMZA NA WEWE


Rudi Nyumbani

Print this post

IMANI YENYE MATENDO;

Waebrania 11: 3 “Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri”.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze Neno la Mungu, leo tutajifunza somo fupi linalohusiana na Matendo ya Imani.”

Kama Biblia inavyotafsiri maana ya Imani kuwa “ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Waebrania 11:1”..

Tukitaka kujua kitu kinachoendelea upande wa pili au kinachokuja mbele yetu, au kilichokatika mazingira yetu tutatumia milango yetu ya ufahamu aidha macho, au masikio, au pua, au ngozi zetu, au ulimi..hizo zitatusaidia kujua ni nini kinaendelea upande mwingine au ni nini kinakuja mbele yetu..Kama hatuna hizo basi hatuwezi kujua chochote kinachoendelea,. Kwamfano wewe unaweza ukawa unapika pilau nyumbani kwako, lakini jirani yako aliye nyumba ya nne akajua unachofanya, japo hajakuona wala hajaingia nyumbani kwako,lakini amepata uhakika huo, na ndivyo ilivyo sasa kitu kilichomfanya ajue hayo yote si kingine zaidi ya pua yake. Vivyo hivyo na katika kuona, kuhisi, ulimi. Vyote hivi ni kuthibitisha kitu Fulani au jambo Fulani au mazingira Fulani.

Lakini Biblia haijatuambia kwamba kuona kwa macho au kusikia au kuhisi ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo, vinaweza kutupa uhakika wa mambo yaliyopo sasa yanayotuzunguka lakini sio kwa mambo yatarajiwayo, lakini Biblia inatuambia Imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo, unaweza usione, wala usisikie, wala usihisi chochote na bado ukapata uhakika kwamba kuna gari linakuja mbele yako kwa kutumia Imani na kweli ikawa hivyo..Unaweza usione, wala usihisi, wala usisikie, wala usinuse lakini ukajua mwakani kutakuwa na njaa na kweli ikawa hivyo… Hii ikiwa na maana kuwa imani ni hisia nyingine ya kipekee tofauti na hisia hizi tano tulizonazo..Kama mhubiri mmoja alivyowahi kusema kuwa “IMANI NI HISIA YA SITA TOFAUTI NA ZILE TANO”.

Kwahiyo Mungu hakuimba dunia kwa macho, wala kwa masikio wala kuhisi, wala kwa chochote kile, bali aliimba dunia kwa Imani.

Lakini leo hatutaingia huko sana, bali tutajifunza zaidi juu ya Matendo ya Imani.

Kama Biblia inavyotuambia “imani isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake.”..Ni wazi kuwa Ili imani iwe hai ni lazima iwe na Matendo. Huwezi ukaona kwa macho yako gari linakuja kwa kasi mbele yako na bado ukabakia pale pale, ni ngumu sana..ni lazima utajikuta unalikwepa tu! wakati mwingine hata sio kwa kutaka..utajikuta tu mwili unajitupa upande wa pili, au mtu anapoleta kitu fulani machoni pako utajikuta tu unafumba macho, wakati mwingine sio hata kwa kutaka, unaposikia harufu ya chakula fulani ukipendacho mahali mate ni lazima yatakutoka tu! wakati mwingine sio kwa kupenda inatokea inakuwa hivyo tu…ikifunua kwamba kile unachokiona lazima ukifanyie kazi.

ndivyo inavyokuwa pia kwa Imani, siku zote lazima ifuatane na matendo fulani, kwa sababu na yenyewe ni hisi, Imani ikishahisi kama kuna kitu mbeleni kinakuja ni lazima matendo yafuate, na hayo matendo wakati mwingine sio kwa hiari ya mtu, yanajitengeneza tu yenyewe..kama vile yanavyojitengeneza pale mtu anapofumba macho ghafla kitu kinakuja machoni pake. Ndio maana biblia inasema “imani isipokuwa na matendo imekufa”.

Kadhalika tunaweza kujifunza zaidi katika uumbaji wa Mungu, Tunajua Mungu aliiumba dunia na vitu vyote kwa Imani, Bwana alisema na iwe hivi na ikawa hivyo..Lakini hakuishia kusema na iwe hivi au vile na kuishia pale. Hapana tunaona baada ya kusema na iwe hivi..akaendelea mbele “kufanya kile kitu”… na ndipo kile kitu kikatokea.. Tunasoma.

Mwanzo 1: 6 “Mungu akasema, NA LIWE anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji.

7 Mungu AKALIFANYA ANGA, akayatenga yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo.”

Hapo tunaona Mungu alisema…na bado Mungu akafanya…hakuishia kusema tu, bali pia akafanya. Kudhihirisha “matendo ya ile imani aliyokuwa nayo”..Kadhalika tunasoma pia katika mistari inayofuata.. ..

“14 Mungu akasema, NA IWE MIANGA katika anga la mbingu ili itenge kati ya mchana na usiku; nayo iwe ndiyo dalili na majira na siku na miaka;

15 tena iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya nchi; ikawa hivyo.

16 MUNGU AKAFANYA MIANGA MIWILI MIKUBWA, ule mkubwa utawale mchana, na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia.

17 Mungu akaiweka katika anga la mbingu, itie nuru juu ya nchi”

Na hapa pia tunaona Mungu, alisema na Mungu akafanya.

“20 Mungu akasema, Maji na yajawe kwa wingi na kitu kiendacho chenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu.

21 Mungu akaumba nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho, ambavyo maji yalijawa navyo kwa wingi kwa jinsi zao, na kila ndege arukaye, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema”.

Vivyo hivyo na hapa tunaona jambo lile lile Mungu alisema na Mungu akaumba..Kwahiyo Mungu hakuishia kusema tu, bali pia alitenda..kudhihirisha Matendo ya ile imani.

Kadhalika na mambo yote Mungu aliyoyasema kwa Neno lake aliyatendea kazi, tena kazi kubwa sana…Na ndio maana tunasoma baada ya Mungu kuumba vitu vyote kwa siku sita alipumzika siku ya saba…akaacha kufanya kazi zake zote… Sasa kama ilikuwa ni “kusema tu na kuachia pale” kwanini aseme alipumzika siku ya saba??… kwani kuzungumza tu nako kunahitaji kupumzika??..ni wazi kuwa kwa yale matendo ya Imani aliyokuwa anayafanya ndiyo yaliyomfanya apumzike. Kazi kubwa ndio ilikuwa hapo pa matendo na si pengine.

Vivyo hivyo na sisi Mungu katuumba kwa mfano wake.. Kama yeye aliiumba dunia kwa Imani yenye matendo na sisi vivyo hivyo tukitaka kupata kitu lazima tuenende kwa Imani yenye matendo. Kwanza TUNASEMA katika vinywa vyetu..huku tukiwa na uhakika kwamba kile kitu tulichokisema kitakwenda kutokea…Na moja kwa moja pasipo kulazimishwa wala kusukumwa tunaingia kwenda kuifanyia kazi ile Imani…

Kadhalika tunapohitaji riziki za ulimwengu huu, tunaweka imani yetu katika matendo..Kile tunachoamini Mungu atakwenda kutupa kwa wakati huu, hizi tunaweka katika matendo, tunakwenda kukifanyia kazi kwa bidii ili kutokee, tusipofanya hivyo hakitatokea.

Vivyo hivyo na kama tunaamini tutakwenda mbinguni siku moja, na kwamba Bwana atakuja kutunyakua kwenda naye mawinguni..Ni lazima kuanzia sasa tukifanyie kazi kile tunachokiamini, pasipo kulazimishwa wala kusukumwa, ni lazima ndani ya moyo wetu tujikute tunatendea kazi ile Imani iliyo ndani yetu. Hivyo tunapaswa tujiweke mbali na dhambi, lazima tujiweke mbali na uasherati, uchawi, rushwa, utukanaji, uvaaji mbaya, ulevi, uvutaji sigara,anasa, usengenyaji, usagaji, utoaji mimba,ulawiti,ushoga, utazamaji pornography na ufanyaji masturbation, uuaji, chuki,wivu, majigambo, ibada za sanamu na matendo yote ya giza.

Ni lazima tukeshe katika roho kama Bwana alivyotuagiza, ni lazima tuhakikishe taa zetu zimejaa mafuta mfano wa wale wanawali wenye busara, na mafuta yenyewe ni Roho Mtakatifu,

Vinginevyo mbingu tutaisahau..vinginevyo hatutaingia katika sabato yetu iliyoahidiwa katika biblia (Warumi 4:9), hatutaingia katika pumziko la milele lililoko mbele yetu, Kwasababu Bwana alipomaliza kuitendea kazi imani yake ndipo alipumzika na kuibariki ile siku.

Na sisi tukiitendea kazi vizuri Imani yetu tuliyokabidhiwa mara moja tu, tukiwa wakamilifu na kujitenga mbali na uchafu wote wa dunia hii, na kujiweka katika utakatifu tumeahidiwa kuingia katika sabato yetu ya utawala wa miaka 1000 na umilele, lakini kama hatutaitendea kazi imani hii ya Thamani iliyo katika Yesu Kristo, na kujichanganya na ulimwengu huu, na kuudharau msalaba…Neno la Mungu lisilodanganya linatuonya.

Ufunuo 21: 8 “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, SEHEMU YAO NI KATIKA LILE ZIWA LIWAKALO MOTO NA KIBERITI. Hii ndiyo mauti ya pili”.

Kazi ya matendo ya Imani yako ni ipi ndugu?? Tangu umeanza kusikia Injili mpaka leo ni muda, na umezalisha nini?? matendo ya imani yako ni yapi?? UCHAFU AU UTAKATIFU?. Jibu unalo wewe, lakini kumbuka Neno moja, Bwana anasema hakawii kuja, wala kuzitimiza ahadi zake..na anakuja na ujira wake, kumlipa kila mtu kile anachostahili.. 

Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila MTU KAMA KAZI YAKE ILIVYO.

13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.

14 Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake.

15 Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya.

16 Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi”.

Bwana akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana;

USIISHIE KUTAZAMA JUU, ENDELEA MBELE.

SI SHETANI BALI NI WEWE. (CHAGUA MEMA)

NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?

Print this post

MWAMBA WETU.

Wana wa Israeli walipotoka nchi ya Misri, baada ya miezi kadhaa tu walifika mahali PALIPOITWA KADESH-BARNEA, ilikuwa safari ya mwendo mfupi tu, kabla ya kuingia katika nchi yao ya ahadi. Lakini tunasoma walipofika mahali pale walikutana na kikwazo kikubwa sana. Biblia inaonyesha eneo lile lilikuwa ni eneo kame kuliko maeneo yote, hakukuwa na jani wala mche, wala dalili ya mto kupita maji mahali pale, ni eneo lilokuwa limezungukwa na milima tupu, Na ndipo wana wa Israeli walipofika pale wakaona kuwa hakuna dalili yoyote ya kupata maji mbeleni kwa ajili yao na watoto wao na mifugo yao, wakaona kuwa pengine hawatakuwa na siku 5 za kuishi mbeleni kwa jinsi hali ilivyokuwa mbaya, ndipo wakaanza kumnung’unikia Musa na Mungu kwa nguvu sana, ni kwanini aliwatoa kule Misri katika nchi yenye bustani nzuri na chakula na kuwaleta katika jangwa baya kama lile ili kuwamaliza huko wao na watoto wao?.

Wana wa Israeli walifika mahali wakasahau siku chache tu nyuma Mungu aliwageuzia yale maji yalikuwa machungu kuwa matamu, walisahau miujiza yote waliyofanyiwa na Mungu kule Misri, walisahau nyama zote zilizokuwa zinawafikia za wale kware kutoka mahali wasipopajua, pamoja na Mana iliyoshuka kutoka mbinguni, wakashindwa kumwesabia Mungu kuwa anaweza hata kuwafanyia miujiza ya kuwanyeshea mvua nyingi mahali pale lakini badala yake baada ya kukutana na ukame ule, na kiu kile na mbele yao upo MWAMBA MKUBWA SANA umesisimama ambao kwa kiu kile wasingeweza kuuvuka, ndipo wakaanza kunung’unika kwa nguvu.

Hawakujua kuwa ni Mungu kwa makusudi kabisa aliwaacha waone kiu ili akawanyeshwe maji yaliyo hai, yatakayowafanya wasione kiu tena ya mambo watakayokutana nayo huko mbeleni baada ya pale, lakini wao mawazo yao yalikuwa yanafikiria mambo ya mwilini tu . Huku Wakiutazama huo mwamba mgumu mkubwa uliowafunika mbele yao usio na mahali pa kuzungukia ndio uliwafanya wazidi kujawa na hasira na uchungu, hata kutaka kumpiga Musa kwa mawe.

Hawakujua kuwa ule mwamba ulikuwa ni KRISTO mwenyewe. Hawakujua kuwa Kristo alikuwa amesimama mbele yao kuondoa kiu yao ya mambo maovu, lakini wao kwa kuwa macho yao ya mwilini yalikuwa yanaona ni jiwe tu kubwa sana limewazinga hawana mahali pa kwenda wakawa wanakufuru mbele ya Kristo.

Na ndipo Mungu hakupendezwa nao matokeo yake akamwambia Musa, aupige mwamba ule na utatoa maji. Na kweli Musa alipoupiga ule mwamba ulitoa maji mengi sana, lakini maji yale hayakuwa maji ya rohoni tena, bali yalikuwa ni ya kukata kiu chao tu kwa muda,lakini matatizo yataendelea pale pale.

1 Wakorintho 10 : 1-33

“1 Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari;

2 wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari;

3 wote wakala chakula kile kile cha roho;

4 wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; KWA MAANA WALIUNYWEA MWAMBA WA ROHO ULIOWAFUATA; NA MWAMBA ULE ULIKUWA NI KRISTO.

5 Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani.

6 Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani”.

Na ndio maana tunaona baada ya pale, hata hawakuweza kustahimili zile habari za wapelelezi zilizoletwa na Akina Yoshua matokeo yake Mungu akakasirishwa nao akawarudisha tena kwenye lile jangwa, Biblia inasema wakalizunguka tena kwa muda wa miaka 40 mpaka kile kizazi chote kilichomnung’unikia Mungu kilipopotea na ndio tunakuja kuona tena Mungu akiwarudisha mahali pale pale kwenye ue mwamba wa kwanza,kuwajaribu kwa mara nyingine baada ya muda huo mrefu kupita.

Hakukuwa na njia ya mkato nyingine ya kufika Kaanani, ni Sharti waupitie MWAMBA ULE ULE uliokataliwa. Na kama ilivyo ada eneo lile la Kadesh-barnea ni eneo lisilokuwa na maji, eneo kame kuliko maeneo yote, na mahali ambalo halina kitu chochote, na wana wa Israeli walipofika tena mahali pale, tunaona wakaanza kumnung’unikia tena Musa kama mwanzo na kusema.

“Ingalikuwa heri kama tungalikufa wakati ule ndugu zetu walipokufa mbele za Bwana!

4 Mbona mmewaleta kusanyiko la Bwana hata jangwa hili ili tufe huku, sisi na wanyama wetu?

5 Na mbona mmetupandisha kutoka Misri ili kutuleta hata mahali hapa pabaya? Si mahali pa mbegu, wala tini, wala mizabibu, wala makomamanga; wala hapana maji ya kunywa..”( Hesabu 20: 3-5)

Unaona?. Ni mahali ambapo hata viumbe hai hawakuweza kuishi kwa jinsi palivyokuwa pakame kupindukia na zaidi ya yote upo mwamba mkubwa sana umesimama mbele yao, usiovukika, japo ni mahali palipokuwa karibu sana na nchi yao ya ahadi waliyokuwa wanatazamia kwa muda mrefu.

Hawakujua kuwa kiu chao kitaondolewa na ule mwamba mmoja tu, licha ya kuzunguka huku na huko jangwani kwa muda mrefu lakini hatimaye wanairudia njia ile ile ya mwamba waliokuwa wameukataa. Na safari hii pia tunaona wakinung’unika vile vile, Ndipo Mungu akamwambia Musa nenda kaseme na Mwamba ule. Lakini Musa naye hakuwa makini kwa kuzingatia aliyoambiwa alidhani kuwa anazungumza na jabali hakujua kuwa ni Kristo alikuwa amesimama pale katika Roho kuwaponya watu wake, Lakini yeye akaenda kwa zile desturi za kwanza za kuuchapa mwamba, na huku Mungu alimwambia azungumze na ule Mwamba, akaenda hivyo hivyo kuuchapa maji kweli yalitoka lakini kumbe na yeye alikuwa amejiwekea hukumu mwenyewe.

Hivyo laana ambazo zingepaswa ziwapate wale watu zikamwangukia Musa na Haruni .Hivyo kwa tendo lile tu hawakuweza kuiona nchi ya Ahadi. Hapo ndipo walipojua kuwa ule mwamba haukuwa jabali ni Mungu mwenyewe.

Kristo hadhihakiwi, alikuja Hapa duniani kwa ajili ya kuwaokoa watu wake, yeye kama ule Mwamba imara utoao maji ya uzima wakati wa Kiu lakini mwamba huo huo unaweza kukwamisha wengi na wakati mwingine kuletea mauti kama hatutajua njia ya kuuendea.

Mathayo 21:42 “Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu?

43 Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake.

44 NAYE AANGUKAYE JUU YA JIWE HILO ATAVUNJIKA-VUNJIKA; naye YE YOTE AMBAYE LITAMWANGUKIA, LITAMSAGA TIKITIKI”.

Ule mwamba ndio ulikuwa njia pekee ya wao kuingia katika nchi yao ya ahadi,lakini wengi wao uliwaangamiza. Uliwaangukia na kuwasaga tikitiki, ni wawili tu ndio walifanikiwa kuingia katika nchi ya Ahadi kati ya mamilioni ya watu. Ule Mwamba ndio uliokuwa geti la kuingia Kaanani..Leo hii na sisi tunasema ni wakristo tuliokatika safari ya kwenda mbinguni, jiwe lile (YESU KRISTO), ndio litupalo maji ya uzima katika safari yetu ya wokovu hapa duniani. Yesu ndiye Lango la kuingia Kaanani (mbinguni)

Lakini na sisi tukiwa watu wa kumnung’unikia Mungu tunapopitia shida, au tunapopungukiwa, au tunapougua, ni kweli Mungu alituokoa na sisi tulibatizwa kama wana wa Israeli walivyobatizwa katika bahari ya shamu, lakini tunaweza tukakosa mbingu kwa mambo kama yale yale ya kunung’unika, kusahau kuwa jana yetu na juzi yetu ilikuwa mikononi mwake, yeye ndiye aliyetufanikisha katika hili katika lile kipindi fulani, lakini leo tunapitia haya madogo tu kwa muda tunamnung’unikia. Tena mbele ya ule mwamba wake mteule Yesu Kristo Bwana wetu aliyetuokoa kwa damu yake ya thamani.

Biblia inatuambia mambo hayo yaliandikwa kwa mifano ili kutuonya sisi. Je! leo unaonyeka wewe mkristo? 

Daudi alisema.

Zaburi 18: 1 “Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana;

2 Bwana ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu, MWAMBA WANGU ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu.

3 Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa, Hivyo nitaokoka na adui zangu.”

Zaburi 18: 31 “Maana ni nani aliye Mungu ila Bwana? NI NANI ALIYE MWAMBA ILA MUNGU WETU”.

Tumpende Bwana wetu, tumtii yeye, tuvumilie, tulale juu ya ule mwamba salama, tunywe maji yale kwa utulivu, naye pekee ndiye atakayetuweka mbali na maadui zetu.

Zaburi 40:1 “Nalimngoja Bwana kwa saburi, Akaniinamia akakisikia kilio changu.

2 Akanipandisha toka shimo la uharibifu, Toka udongo wa utelezi; AKAISIMAMISHA MIGUU YANGU MWAMBANI, AKAZIIMARISHA HATUA ZANGU”.

Bwana akabariki sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

MAJI YA UZIMA

MIISHO YA ZAMANI.

YAKUMBUKE YA NYUMA.

ZIKUMBUKE FADHILI ZA MUNGU


Rudi Nyumbani

Print this post

JIFANYIE RAFIKI KWA MALI YA UDHALIMU.

Shalom! Mwana wa Mungu, Karibu tujifunze Neno la Mungu, ambapo leo tutajifunza somo lenye kichwa kinachosema “Tujifanyie rafiki kwa Mali ya udhalimu”. Somo hili linatoka katika kitabu cha Luka 16:1-10, Ni Mfano ambao Bwana aliutoa kwa wanafunzi wake wakati fulani, akifananisha hekima ya wana wa Ulimwengu huu wasiomjua Mungu (walio wadhalimu), wanavyotumia Busara katika kuamua Mambo yao ya kidunia..Na sisi jinsi tunavyopaswa kutumia hekima na Busara katika kuamu hatima yetu ya maisha ya umilele zaidi yao.

Biblia inasema:

Luka16 : 1 “Tena, aliwaambia wanafunzi wake, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyekuwa na wakili wake; huyu alishitakiwa kwake kuwa anatapanya mali zake.

2 Akamwita, akamwambia, Ni habari gani hii ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena.

3 Yule wakili akasema moyoni mwake, Nifanyeje? Maana, bwana wangu ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya.

4 Najua nitakalotenda, ili nitakapotolewa katika uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao.

5 Akawaita wadeni wa bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, Wawiwani na bwana wangu?

6 Akasema, Vipimo mia vya mafuta. Akamwambia, Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini.

7 Kisha akamwambia mwingine, Na wewe wawiwani? Akasema, Makanda mia ya ngano. Akamwambia, Twaa hati yako, andika themanini.

8 Yule bwana akamsifu wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru.

9 Nami nawaambia, Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu, ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele.

10 Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia.

11 Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli?

12 Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?”.

Ili kuufanya mfano huu ueleweke vizuri tunaweza kuufupisha hivi,

“Kulikuwa na mtu mmoja Tajiri, aliyekuwa na meneja wake, wa kusimamia mzunguko wa fedha za biashara yake pamoja na shughuli zake zote alizokuwa nazo, lakini ulifika wakati yule meneja hakuwa mwaminifu, akawa anaanza kutapanya fedha za Yule Tajiri wake (mwajiri wake),anachukua faida iliyopatikana na kutumia kwa anasa zake mwenyewe, Na hivyo ikapalekea kuleta hasara kubwa kutokana na matumizi mabaya ya zile fedha, Lakini siku moja ikafika waajiriwa wengine wakagundua anachokifanya wakampelekea taarifa Yule boss wao mkubwa kwamba Meneja wako ana matumizi mabaya ya fedha., Hivyo Yule tajiri alipochunguza akagundua ni kweli yule mtu alikuwa na matumizi mabaya, akamwita Yule Meneja na kumwoji, ikawa wazi kuwa alikuwa ni mtu ambaye sio mwaminifu hivyo kilichobaki ni kufukuzwa kazi tu, hakuna lingine.

Lakini kwakuwa Yule Meneja alikuwa na Busara hata katika hali yake ya utapanyaji wa fedha, alijua tayari hata iweje kibarua hana tena,na Bosi wake kashamchukia hivyo ikambidi atafute namna ya kujipatanisha na wale Wadaiwa wa Bosi wake,wale matajiri ili siku atakapoishiwa kabisa, wale wadeni wa Bosi wake wasimtupe,wamfadhili, angalau wawe wanamkaribisha majumbani mwao, na hata kama kutatoke fursa yoyote wamkumbuke ili asiwe omba omba huko mtaani, mtu asiyekuwa na msaada, wa kudharauliwa na kila mtu.

Kwahiyo alichokifanya Yule Meneja ni kwenda kuchukua baadhi ya zile mali chache alizobakiwa nazo na alizojilumbukizia na kuwatafuta wale watu wote waliokuwa wanadaiwa na Yule Tajiri wake…Kama kuna aliyekuwa anadaiwa lita 1000 za mafuta , alimlipia lita 500, na kumwachia zile nyingine 500 zilizosalia ajilipie mwenyewe, na Mwingine kama alikuwa anadaiwa magunia 100 ya ngano alimlipia magunia 20 na kuacha yale 80 yaliyosalia ajilipie mwenyewe ”..Hivyo wale watu wote waliopunguziwa mzigo wa Madeni yao walimpenda sana Yule Meneja kwa vile alivyowapunguzia mizigo yao, hata ingekuwa ni wewe unapewa misamaha ya madeni yako usingeacha kumfurahia huyo anayekupa ofa hiyo. kwahiyo alijua hata kama akiondolewa katika Umeneja wake, siku atakapoishiwa kabisa yupo mtaani hawatamtupa kwasababu aliwasaidia katika shida zao.

Na Yule Tajiri alipopata taarifa za busara za Yule Meneja wake dhalimu alimsifu ijapokuwa alimwibia fedha nyingi lakini zile fedha alikwenda kuzitumia kuwapunguzia madeni wale aliokuwa anawadai..Kwahiyo hata kama alikuwa hataki kumsamehe kwa kitendo kile pengine siku hasira yake ikipoa anaweza kumrudisha tena kwenye kazi yake ya Umeneja” Haleluya.

Mfano huo Bwana alioutoa unatufundisha nini? Kwamba Na sisi tuwe na Hekima kuliko hata watu wa ulimwengu huu, ya kufahamu kuwa, tutakachokifanya leo kinachompendeza Yeye tutapata malipo yake baadaye.

Tutakachomfanyia Bwana Yesu leo hii katika dunia hii, kiwe kizuri au kibaya kitakuja kuwa na malipo yake katika ulimwengu ujao,.

Leo hii umepata chochote aidha ni mali, chakula, mavazi, makazi, uzima, uwezo au chochote kile na umepata kwa njia yoyote ile..hiyo ni kama “mali ya udhalimu mbele za Mungu”..Nenda kawatafute wale watu ambao hawanakabisa hivyo vitu (Hususani walio Wakristo) wapatie, wale watumishi wa Mungu unaojua ni waaminifu, sio lazima uwapatie vyote, hapana bali sehemu tu, angalau asilimia 20 au zaidi, Hiyo ni sawa umewalipia madeni wale wanaodaiwa na Mungu..

Kwasababu siku zinatakuja katika Mbingu Mpya na Nchi Mpya, hao waliokuwa na uhitaji leo (wanaomcha yeye), watairithi nchi, watakapopewa ufalme, na mamlaka..Watakukaribisha katika makao ya Milele hata kama haukuwa mkamilifu kwa viwango vile vinavyotakiwa, watakutaja mbele za Bwana na kukukaribisha katika makao ya Milele, kwasababu walipokuwa wapo uchi, uliwavisha nguo,walipokuwa na kiu uliwanywesha maji, walipokuwa na njaa uliwapa chakula, walipokuwa wagonjwa ulikwenda kuwatembele, walipokuwa na uhitaji uliwasaidia..Na kwasababu uliwasaidia hao basi ni sawa na ulimsaidia Kristo Mwenyewe.

Mathayo 25: 31 “Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake;

32 na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi;

33 atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto.

34 Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu;

35 kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha;

36 nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia.

37 Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuonauna njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha?

38 Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika?

39 Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia?

40 Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi”

Je! Na wewe umemtendea Kristo nini?..Kwasasa yupo Mbinguni, hahitaji fedha wala mavazi wala haumwi, wala hayupo kifungoni…Lakini yupo ndani ya watu wengi walio kifungoni, wanaohitaji mavazi, wanaohitaji chakula n.k n.K..Nani atakayekuwa mtetezi wako siku ile??..Kitakapokosekana kila kitu cha kukuvukisha ng’ambo kule?? Ni nini kitakachokutetea basi? Kama leo hii hujifanyii urafiki kwa mali ya udhalimu? Siku ile Utaangukia kwenye hili kundi..

Mathayo 25: 41 “Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake;

42 kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe;

43 nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama.

44 Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe u

na njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie?

45 Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi.

46 Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele”

Mtetezi wako atakuwa ni nani siku ile?

Wakati Fulani vita vilipotokea katika Israeli, na Israeli walipokuwa wanakawia kawia kwenda kupigana na Maadui zao wafilisti,Yonathani aliyekuwa mwana wa Mfalme Sauli, Mungu alimtia Moyo wa Ushujaa na kwenda kuvamia kambi ya wafilisti na kuishinda ile vita, Hivyo Yonathani akawa ameleta wokovu na ushindi katika ile vita siku ile, lakini Baba yake (ambaye ni Mfalme Sauli). Alitoa amri kwa kiapo mbele za Mungu kwamba mtu yoyote asile chochote mpaka jua litakapozama, na yeyote atakayefanya hivyo amri ilitolewa auawe. Na kiapo hicho Mungu akakisikia na akakithibitisha, hivyo Israeli wote hawakula siku hiyo chochote ingawa walikuwa na njaa kali ya kuishiwa nguvu kabisa, lakini wakati anatoa hiyo amri Yonathani mwanawe ambaye ndiye aliyekuwa sababu ya ushindi wa vita hakuwepo muda huo, hivyo hakuisikia hiyo amri, na wakati anapita porini alikutana na sega la asali, akala!. Na baba yake hakujua, na ilipopita muda kidogo Baba yake akaenda kumwuliza Mungu habari za kwenda kuteka nyara za wafilisti Mungu hakumjibu. Ndipo alipogundua kuwa kuna kosa limefanyika mbele zake, ndio maana Mungu hajibu chochote, na wakatumia Urimu kumuuliza Mungu ndipo ikajulikana kuwa na kugundua kuwa ni mwanae Yonathani ndiye aliyevanja kiapo kile kwa kula asali wakati wa vita.

Hivyo Yonathani akawa katika hatari ya Kufa, kwasababu ndiye Mungu aliyemteua afe kutokana na kile kiapo cha Baba yake. Kumbuka Yonathani aliyekuwa sababu ya kushinda vita sasa ndiye anayepaswa kufa, Lakini tunasoma nini??, Kwa wema wake alioutenda hata kuwapa furaha na wokovu Jeshi la Israeli, shauri lake la kufa likabatilishwa, Ile hati ya mashtaka mbele za Mungu ilibadilishwa. Watu wakamwokoa Yonathani mbele ya ghadhabu ya Mungu na ya baba yake.

1 Samweli 14: 42 “Basi Sauli akasema, Sasa piga kati ya mimi na mwanangu Yonathani, [naye awaye yote ambaye Bwana atamtwaa, atakufa. Nao watu wakamwambia Sauli, La! Sivyo hivyo; lakini Sauli akawaweza watu. Nao wakapiga kati ya yeye na mwanawe Yonathani,]

43 Ndipo Sauli akamwambia Yonathani, Niambie ulilolifanya. Basi Yonathani akamwambia, akasema, Nikweli, mimi nalionja asali kidogo kwa ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwangu; na tazama, imenipasa kufa.

44 Naye Sauli akasema, Mungu anifanyie hivi, na kuzidi; kwa kuwa hakika utakufa, Yonathani.

45 Walakini watu wakamwambia SAULI, JE! ATAKUFA YONATHANI, AMBAYE NDIYE ALIYEUFANYA HUO WOKOVU MKUU KATIKA ISRAELI? HASHA! AISHIVYO BWANA, HAUTAANGUKA CHINI HATA UNYWELE MMOJA WA KICHWA CHAKE;

kwa maana ametenda kazipamoja na Mungu leo. HIVYO HAO WATU WAKAMPONYA YONATHANI, ASIFE”

Na ndivyo itakavyokuwa siku ile kwa mema wale wachache watakayowatendea watu wa Mungu, ndio yatakayowaepusha na adhabu ya Milele, watakatifu watakuwa watetezi wao siku ile, lakini kwa wema wao waliowatendea watu wa Mungu (wataokolewa siku ile). Yonathani alijifanyia urafiki kwa mali ya udhalimu ili ilipokosekana hata kama alistahili kufa watu walimponya. Ni matumaini yangu Bwana atazidi kutujalia kuyaona hayo siku zote za maisha yetu.

Mungu akubariki

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

 

 

 


Mada zinazoendana


MWINUE YESU KRISTO KATIKA MAISHA YAKO.

JIANGALIENI BASI JINSI MSIKIAVYO.

TUKAZE MWENDO KWA TULIYOANDALIWA.


Rudi Nyumbani

Print this post

HISIA YA MUNGU ILIYO MBAYA KULIKO ZOTE.

Tabia hizi zote tunazozionyesha zitokazo ndani yetu kwa mfano, furaha, amani, upendo, hasira, ghadhabu, wivu, uchungu, huruma, n.k. asili yake sio sisi bali ni Mungu, kwasababu sisi tumeumbwa kwa mfano wa Mungu kama maandiko yasemavyo, hivyo hizi ni baadhi tu ya tabia ambazo Mungu mwenyewe alikuwa nazo kabla hata ya ulimwengu kuwako.

Sababu ya Mungu kuviruhusu vitu kama hivi vitokee ndani yetu, ni kutufundisha sisi kwa vitendo ili tuyajue mapenzi yake ni nini. Pale tunapoweza kuuhisi upendo au kuutoa upendo kwa wengine, basi tunafahamu kuwa yupo ambaye anayeitwa Upendo mwenyewe, na hivyo hiyo inatufanya sisi kuilewa vizuri asili ya Mungu tofauti na kama tungekuwa tumehadithiwa tu kuwa Mungu anatupenda halafu hatujawahi kuhisi upendo wowote ndani yetu, au hatujui upendo ni kitu gani. Ni wazi kabisa kuwa tusingemwelewa Mungu vizuri, na vivyo hivyo katika mambo mengine mema kama vile huruma, furaha, amani, faraja,fadhili, upole, unyenyekevu n.k. Yote hayo tusingeweza kuyapokea kutoka kwa Mungu kama asingetuonjesha mambo hayo ndani yetu sisi wenyewe pale tunapohudumiana sisi kwa sisi.

Lakini pia upo upande wa pili wa hisia hizo, ambao huo sio mzuri sana, na kila mwanadamu amepewa, kwamfano hasira sio jambo jema, na hasira huja kwa kuudhiwa, na tunajua hakuna mtu hata mmoja anayependa kuudhiwa, lakini hasira hutokea yenyewe ndani pale mambo kama hayo yanapokuja, si kwamba mtu anaitengeneza hapana, bali ni jambo ambalo linatokea lenyewe pale vitu kama maudhi au makwazo vinapozuka kinyume na matarajio yake, kadhalika na mambo mengine kama ghadhabu, uchungu, huzuni, sononeko n.k.

Lakini lipo jambo ambalo linafunika vyote katika hisia mbaya, kama vile UPENDO unavyofunika hisia zote nzuri, kadhalika katika upande wa hisia mbaya lipo jambo linalofunika hisia zote kwa ubaya na hili si lingine zaidi ya WIVU. Wivu nao unaweza kuja kwa sababu nyingi lakini wivu ulio wa kiwango cha juu ni ule wivu unaokuja kwasababu ya mpenzi (mke au mume).

Kwasababu kiwango cha juu kabisa cha hisia nzuri (yaani upendo) huwa kinatoka kwa mpenzi, kadhalika na kiwango cha juu kabisa cha hisia mbaya (yaani wivu), huwa kinatoka kwa huyo huyo mpenzi. Hasira inaweza kuleta madhara ya hasira, ghadhabu inaweza kuletea madhara ya ghadhabu peke yake, uchungu unaweza kuleta madhara ya uchungu pekee yake,lakini kitu kinachoitwa WIVU ni mbali sana na hivi vingine hicho kinajumuisha vyote humo humo, ni kiwango cha juu kabisa cha hisia mbaya kwa mwanadamu, na ndivyo ilivyo hata kwa Mungu, na sababu kubwa ya wivu ni USALITI.

Leo hii ni wazi kabisa kuona watu wakijiua, watu wakiua wengine, watu wakisaliti hata wazazi wao ndugu zao,kwa ajili ya wivu wa mpenzi, watu wakimkosea Mungu wakienda hata kwa waganga, watu wakilipiza visasi vibaya kwa sababu ya jambo dogo tu la wivu wa mapenzi, watu wanapigana kila siku kwa ajili ya jambo hilo, wengine wanafanya uhalifu n.k. Kwa ufupi pale mtu anapofikia kiwango cha juu sana cha wivu basi mtu huyo huwa anaamua kufanya jambo lolote lile bila kujali ni madhara mangapi anaweza kuleta katika jamii yake au kwake mwenyewe kwa tukio hilo. Kwasababu ni jambo ambalo limechanganyikana na hasira humo humo, uchungu humo humo, ghadhabu humo humo, huzuni humo humo na kila kitu, Hivyo ili watu kuepuka na hilo mapema kabisa kabla hawajingia katika vifungo vya ndoa, huwa wanaingia kabisa katika mapatano kuwa huko mbele hawataumizana kwa kusalitiana.

Na ndio maana biblia inasema katika:

Mithali 27: 4 “Ghadhabu ni kali, na hasira ni gharika; LAKINI NI NANI AWEZAYE KUSIMAMA MBELE YA WIVU”.

Mungu ameziweka hizo hisia makusudi ndani ya wanadamu ili waweze nao kumwelewa pale anaposema jambo Fulani ni chukizo kwake, wajue alimaanisha linamchukiza kweli kweli , anaposema MIMI NI MUNGU MWENYE WIVU (Kutoka 20:5). Wajue kuwa kwa jinsi ile ile wivu unavyokula ndani yao ndivyo unavyokula ndani ya moyo wa Mungu, Na hivyo inawapasa wachukue sana tahadhari kujiepusha nayo, kwasababu wasipofanya hivyo basi wao wenyewe watakuwa wamejiweka katika hatari ya kupatwa na madhara makubwa sana yatokanayo na wivu wake.

Katika agano la kale Mungu alikuwa anatiwa wivu pale anapokuwa anaona watu wake wanaacha kumwabudu yeye, wanageukia masanamu na kuyafanya kuwa ndio miungu yao, jambo ambalo alishawaonya tangu zamani kwenye zile amri kuu 10 akisema:

Kutoka 20: 2 “Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.

3 Usiwe na miungu mingine ila mimi.

4 Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini

duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.

5 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, NI MUNGU MWENYE WIVU; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao”,.

Unaona lakini wengi wao hawakuijali hiyo hisia mbaya ya Mungu wakaendelea kufanya hivyo angali wanajua kabisa waliyokuwa wanayafanya sio sahihi. Matokeo yake ikawapelekea Mungu kuwapiga kwa mapigo ya kila namna, wanyama wakali, njaa, upanga,magonjwa ya kila namna, na mwisho wa siku wakaondolewa katika nchi ambayo Mungu aliwaambia itakuwa urithi wao milele, nchi ambayo Mungu aliwaapia itawazaliwa wenyewe, nchi ibubujikayo maziwa na asali. Lakini sasa imebalika na kuwa kinyume chake, kutokana na njia zao mbaya mbele zake.

Vivyo hivyo na katika agano jipya, kumbuka agano la kale ni kivuli cha agano jipya, mambo yale ambayo Mungu alikuwa anayachukia wakati ule ndiyo hayo hayo anaendelea kuyachukia hata wakati huu, na tena sasa hivi tunapaswa tuwe makini zaidi kwasababu Mungu ameuweka wivu wake kwa uwazi zaidi kuliko ilivyokuwa ameuweka katika agano la kale.

Kwani kipindi kile Wivu wale aliufunua tu katika mambo ya nje, kwenye ibada za sanamu za nje, lakini sasa sio tu zile za nje, bali pia na zile zinazotoka rohoni. Embu tuzitamaze kwa ufupi sanamu hizo.

1.SANAMU ZA NJE! ZA SASA.

1Wakorintho 10: 14 “Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu.

15 Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo.

16 Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo?

17Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.

18Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana shirika na madhabahu?

19 Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu?

20 Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani.

21 Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani.

22 AU TWAMTIA BWANA WIVU? Je! Tuna nguvu zaidi ya yeye?”.

Unaona hapo?, matambiko, na mila mtu asizozijua maana yake, unakuta mtu anakwenda kufanya huko kijijini kwake, hajui kuwa unafanya ushirika na mashetani badala ya Mungu, anakwenda kwenye ngoma na hivyo anamtia Mungu wivu kwa ibada hizo za masanamu anazozifanya, anakwenda kwa waganga, anakwenda kwa wasoma nyota. anaabudu sanamu za watakatifu waliokufa zamani (sanamu za bikira Maria, Mt Petro n.k), anafanya kazi katika makampuni ya pombe, au sigara, au ya biashara haramu au anauza hivyo vitu. Hizo zote ni ibada za sanamu na kibaya zaidi bado mtu huyo anajiita mkristo hujui kuwa anamtia Mungu wivu ambao huo hauzimwi kwa namna yoyote ile, isipokuwa mauti, biblia inasema ni NI NANI AWEZAJE KUSIMAMA MBELE YA WIVU?

2. SANAMU ZA NDANI.

Wakolosai 3:5-9

“5 Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, NDIYO IBADA YA SANAMU;

6 kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu.

7 Katika hayo ninyi nanyi mlitembea zamani, mlipoishi katika hayo.

8 Lakini sasa yawekeni mbali nanyi haya yote, hasira, na ghadhabu, na uovu, na matukano, na matusi vinywani mwenu.

9 Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake;”

Unaona hapo?, hata uasherati mtu anaoufanya ni ibada za sanamu, pornography ni ibada za sanamu, ushoga, usagaji, mustarbation, uasherati yote hayo ni ibada za sanamu mbele za Mungu, biblia inaendelea kusema matusi midomoni na lugha chafu, uovu, n.k. yote hayo ni ibada za sanamu na hivyo kwa hayo mtu anamtia wivu Mungu kila siku anavyozidi kuendelea kufanya. Na ghadhabu ya Mungu, inaujilia ulimwengu mzima kwasababu ya hayo.

Hivyo ndugu, tuikwepe ghadhabu ijayo kutokana na wivu wake, Kwasababu wivu huleta visasi hivyo tukae mbali na kisasi cha Mungu kila siku tuishi maisha ya kujitakasa ikiwa sisi ni wakristo.. Lakini kama upo nje ya ukristo (yaani hujampa Bwana maisha yako). Mungu pia hapendezwi na njia zako, ni heri ukageuka sasa, na kutubu angali muda upo, ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa na kwa jina la YESU upate ondoleo la dhambi zako, kisha Bwana atakupa Roho wake mtakatifu kukulinda na kukufundisha. Ni maombi yangu utafanya hivyo na Bwana akuangazie Nuru yake.

“Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu.( 1Yohana 5:21)”

Ubarikiwe.

Print this post

HERI, WALE MUNGU ASIOWAHESABIA MAKOSA YAO.

Shalom! Mtu wa Mungu karibu tujifunze maandiko, kwa pamoja. Maandiko yanatuambia katika kitabu cha Zaburi 32:1-2 kwamba…

Zaburi 32:1 “Heri aliyesamehewa dhambi, Na kusitiriwa makosa yake.

Heri Bwana asiyemhesabia upotovu, Ambaye rohoni mwake hamna hila.”

Mstari huu pasipo ufunuo wa Roho ni mgumu kidogo kueleweka, unaweza ukajiuliza inakuwaje Mungu aliye mkamilifu na asiyechangamana na dhambi kuwa na kikundi cha watu Fulani ambao hata watendeje dhambi yeye hawahesabii makosa, na wakati huo huo pia anacho kikundi cha watu ambao kila dhambi wanayoitenda ina hesabiwa mbele zake. Ni mstari kidogo wenye utata na mgumu kuelewa.

Lakini ashukuriwe Mungu kwa kumpa Mtume Paulo ufunuo wa Neno hilo kwa uweza wa Roho, ambaye alielezea kwa undani kabisa maana ya mstari huu Mfalme Daudi aliouandika katika Zaburi 32. Alisema…

Warumi 4: 6 “Kama vile Daudi aunenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na HAKI PASIPO MATENDO,

7 Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao.

8 HERI MTU YULE AMBAYE BWANA HAMHESABII DHAMBI.”

Unaona hapo! Paulo anaelezea vizuri kuwa uheri ni kwa wale ambao Mungu ANAWAHESABIA HAKI PASIPO MATENDO, yaani wale waliompokea Bwana Yesu Kristo na kuvua utu wa kale na kuvaa upya, hao ndio kundi la watu ambao Mungu hawahesabii makosa yao haleluya!.

Sasa swali lingine linakuja..Je! watu waliompokea Bwana Yesu na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu na kuzaliwa mara ya pili wanakuwa na makosa? Na wakati huo huo maandiko yanasema katika 1 Yohana 3: 9 “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu”.

Maadamu tunaishi katika huu mwili hatuwezi kuwa wakamilifu asilimia 100, tunayo madhaifu mengi na kuna makosa tunayoyafanya mengi pasipo kujua hata kama hatutayaona, hayo ndio makosa ambayo kwa mtu aliyezaliwa mara ya pili, Mungu hayahesabu, Na pia mtu aliyezaliwa mara ya pili hawezi kutenda dhambi kwa makusudi, hawezi kwenda kuzini, au kuiba, au kutukana, au kula rushwa..hizo ni dhambi za dhahiri kabisa na sio za madhaifu, yapo makosa ya udhaifu, kama hasira zinazomjia mtu pasipo kujijua, na ufahamu ukimrudi anajua kosa lake na haraka anakwenda kutubu na kujirekebisha, lakini sio hasira mpaka za kwenda kupiga mtu au kusababisha madhara yoyote. Na madhaifu mengine yote ambayo pengine ulimkosea Mungu au Mtu mwingine pasipo kujijua, mpaka siku alipokuja kukwambia kwamba pale ulinikosea, ndipo unapojua kosa lako. Hayo yote mbele za Mungu hayahesabu kwa wale waliompokea yeye.

Ili kuelewa vizuri maana ya mambo haya hebu tafakari mfano huu.

Mzazi (ambaye hamjui Mungu) ana mtoto wake anayempenda na hapo hapo ana mfanyakazi aliyemwajiri.

Na wote wawili wakafanya makosa kila mtu kwa sehemu yake, unadhani ni atakayepata adhabu kubwa zaidi kuliko mwingine, yupi atafukuzwa ndani ya nyumba na yupi ataachwa…ni wazi kuwa Yule mfanyakazi atafukuzwa kutoka ndani ya ile nyumba na mtoto kuachwa…. Kwahiyo hapo tunaweza kujifunza kuwa kwa namna Fulani makosa ya watoto yanafunikwa na wazazi kuliko makosa ya watu wasio watoto wao, huwezi kukuta mahali popote mzazi ambaye hamjui Mungu anamsema vibaya mwanae mbele ya watu..zaidi ya yote hapendi kusikia mwanawe anasemwa vibaya hata kama ni mwovu kiasi gani.

Na kwa Mungu wetu wa mbinguni ndio ivyo hivyo, watoto wake (yani wale waliomwamini mwanawe mpendwa Yesu Kristo), hawahesabii makosa, hata kama watakuwa na madhaifu mengi kiasi gani, yeye bado atabaki kuwa baba yao tu! Ndio maana biblia inasema WANA HERI HAO HAWAHESABIWI DHAMBI ZAO. Haleluya!.

Lakini kinyume chake ni OLE WAKE YULE AMBAYE BWANA ANAMHESABIA MAKOSA YAKE.

Sasa Mtu anahesabiwaje makosa yake?.

Kwa kutomwamini Yesu Kristo, na kutokuzaliwa mara ya pili, ni sawa na kuwa nje ya familia ya Mungu, hivyo mtu kama huyo akifanya uovu tu wowote ule uwe wa bahati mbaya uwe wa makusudi, kwasababu hana mtetezi juu yake,anakuwa kama yatima, basi huo uovu wake utahesabiwa

Hiyo ndiyo hasara aliyonayo mtu ambaye hajampokea Yesu Kristo katika ulimwengu huu tuliopo wa dhambi, anakuwa anaishi katika dunia ambayo hana kibali chochote mbele za Mungu, anakuwa anaishi katika dunia ambayo maombi yake yanakuwa hayasikilizwi na yanakuwa hayana thamani yoyote, anakuwa anatoa sadaka ambazo hazina thawabu kubwa mbele za Mungu, anakuwa anatenda wema ambao hauhesabiki au kama unahesabika unakuwa na thamani na heshima ndogo sana mbele za Mungu. Kamwe anakuwa hawezi kumpendeza Mungu. Siku zote anakuwa hana amani na maisha yake.

Ndio maana utasikia wengi leo hii wanakwambia “mimi kumfuata Yesu siwezi” lakini natenda mema halafu anaulizwa kwani nitahukumiwa??..Ndugu yangu wema wako nje ya familia ya MUNGU ni kupoteza Muda..Fanya hima uwe kwanza MWANA WA MUNGU ili wema wako uweze kuhesabiwa!. Hata wauzaji wa madawa ya kulevya wapo wakarimu, kuliko wewe, lakini Mungu hawatambui kwasababu sio wake,…Ni sawa na mfanyakazi anayejitahidi kumpendezesha bosi wake kwa kufanya kazi kwa bidii, na kuwa mwaminifu ili mwisho wa siku awe mrithi, hata atende wema mwingi kiasi gani URITHI atapewa Mtoto wa Yule Bosi hata kama Yule mtoto ni mpumbavu kiasi gani.

Na ndicho tunachopaswa kufanya sisi, sio kutafuta kutenda mema kwanza, hapana bali kutafuta kuwa WANA WA MUNGU. Kutafuta kuzaliwa mara ya pili kutoka katika kuwa WATUMWA WA DHAMBI(Wafanya kazi) na KUWA WANA WA MUNGU, Ndipo tutapata kibali mbele za Mungu katika hii dunia tunayoishi na katika ulimwengu ujao.

Kama hujampa Bwana maisha yako, huu ndio wakati, usisubiri kesho kwasababu biblia inasema “usijisifu kwa ajili ya kesho kwasababu hujua yatakayozaliwa katika siku moja”..Kesho huijui, mkabidhi Bwana leo maisha yako, unachotakiwa kufanya ni kutubu kabisa dhambi zako kwa kudhamiria kuziacha kuzifanya kuanzia leo na kuendelea, kisha baada ya hapo haraka sana nenda katafuta mahali wanapobatiza ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kama hujabatizwa bado,(Zipo batizo nyingi, lakini unapaswa uujue ubatizo sahihi wa kimaandiko ni upi kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako).

kisha baada ya kubatizwa Bwana Mwenyewe atafanya yaliyosalia,atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu atakayekuwezesha kushinda dhambi na kukuongoza katika kuijua kweli yote ya Biblia. Na hapo utakuwa umeshazaliwa mara ya pili kulingana viwango vya Baba wa Mbinguni anavyovitaka yeye, lakini ukiendelea kudumu katika UTAKATIFU, basi utakuwa nawe ni mmoja wa wana wa Mungu, wasiohesabiwa makosa yao, na wanaopewa thawabu haraka hata kwa yale madogo wanayoyafanya, utakuwa miongoni mwa waliobarikiwa wazao wateule, ukuhani wa kifalme, watu wa Milki ya Mungu, warithi wa Utajiri wote wa Mungu.

Bwana akubariki sana, Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

UZAO WAKO UTAMILIKI MALANGO YA KUZIMU;

NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?


Rudi Nyumbani

Print this post

IELEWE SAUTI YA MUNGU.

Shalom Mwana wa Mungu, karibu tujifunze kwa pamoja Neno la Mungu, na Leo tutajifunza moja ya njia ya kuielewa sauti ya Mungu inapozungumza nasi.

Kwanza ni muhimu kufahamu kuwa Mungu ni Mkuu, Upeo wake na mawazo yake yapo mbali sana, mahali ambapo hatuwezi kuyafikia…Kwahiyo kwa ukuu wake namna hiyo tunajua kabisa hakuna mwanadamu yoyote atakayeweza kumwelewa kama akitaka kuzungumza na sisi katika ukuu wake wote.

Kwahiyo kwasababu yeye ni mkuu na katuumba sisi watu wake katika hali ya udogo, hawezi akazungumza na sisi kwa lugha zake, bali atazungumza na sisi kwa lugha nyepesi na inayoeleweka, ili tuweze kumwelewa. Hata na sisi pia huwa tunapokuwa na mifugo yetu, hatuwezi kuzungumza nayo kama tunavyozungumza na wanadamu wenzetu, kama tukifanya hivyo ni wazi kuwa mifugo haitatuelewa ni sharti tutumie vitendo au sauti watakazozielewa kama miluzi au kutumia ishara fulani.

Kwasababu hiyo basi Mungu naye anazungumza na sisi kwa lugha za kibinadamu, kwa sauti za kibinadamu, kwa lafudhi za kibinadamu..Kwasababu mfano akizungumza na sisi kwa lugha za malaika hatutamwelewa, kwa lafudhi za kimbinguni hatutamsikia. Na endapo angejishusha zaidi na kuzungumza na sisi kwa ngurumo na radi na umeme, ndio kabisa tusingemwelewa, tungeishia kumwogopa badala ya kumpenda n.k.

Na ndio maana tunasoma Katika kitabu cha 1Samweli 3, Bwana akizungumza na Samweli kwa sauti inayofanana na ya Eli. Tunaona hakumwita kwa sauti ya mawimbi au radi, bali kwa sauti kama ya Baba yake wa kiroho. Mpaka Samweli akadhani ni Eli ndiye anayemwita. Na tunaona hakuishia kumwita mara moja bali alimwita kwa sauti ile ile mara nne.

1 Samweli 3:1-8 “Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya Eli. Na neno la Bwana lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri.

2 Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona),

3 na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu;

4 basi, wakati huo Bwana akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa.

5 Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena.

6 Bwana akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena.

7 Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake.

8 Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto.”

Umeona hapo? Ni mara nyingi tumekuwa tukitafuta kuisikia sauti ya Mungu kwa namna nyingi, lakini ni muhimu kujua kwamba sauti ya Mungu haipo mbinguni, sauti ya Mungu ipo pamoja nawe pale ulipo. Ipo karibu sana na wewe, ipo hapo ulipo moyoni mwako au pembeni kidogo chumba cha pili kinachofuata cha jirani yako aliye mkristo.

Kumbukumbu 30: 11 “Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali.

12 Si mbinguni, hata useme, Ni nani atakayetupandia mbinguni akatuletee, aje atuambie tusikie, tupate kuyafanya?

13 Wala si ng’ambo ya pili ya bahari, hata useme, Ni nani atakayetuvukia bahari, akatuletee, aje atuambie, tusikie, tupate kuyafanya?

14 Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya”.

Sauti ya Mungu haifanani na ya Malaika kwetu sisi, hapana sauti ya Mungu inafanana na sauti zetu sisi wanadamu, kiasi kwamba anapozungumza na sisi tusipokuwa makini tunaweza kudhani kuwa tunazungumza na wanadamu. Samweli pengine alifundishwa kuwa Mungu huwa anazungumza kutoka mbinguni, na akizungumza basi bahari na kuzimu, na mbingu na nchi zinatetemeka..Hiyo ni kweli, lakini hapa tunasoma sauti ya Mungu ilipoita ilisikika kama inatoka chumba kinachofuata, na ilifanana sana na sauti ya Baba yake wa kiroho aliyekuwa anamfundisha njia za wokovu.

Ndugu/Dada unayesoma ujumbe huu, mahali popote ulipo sauti ya Mungu ipo inazungumza na wewe, unaposikiliza Mahubiri au Mafundisho yanayohubiriwa na mtu fulani, yanayohusiana na wokovu wako, hiyo ni sauti ya Mungu inazungumza nawe..usijaribu hata kidogo kufikiri ni yule mtu ndiye anayezungumza na wewe la! Ni Mungu ndiye anayezungumza nawe, katika sauti ya Yule mtu.

Mahali popote usikiapo Mahubiri ya kutubu dhambi, ni sauti ya Mungu ikikukumbusha kile alichokiandika katika Neno lake (Biblia takatifu), kwamba wenye dhambi wote hawataurithi ufalme wa mbinguni, Mahali popote usikiapo habari za maonyo yahusuyo hukumu inayokuja hiyo ni sauti ya Mungu ikikukumbusha kile kilichoandikwa katika Biblia yake takatifu (juu ya hukumu itakayoijia ulimwengu mzima).

Kwahiyo usikiapo hiyo sauti usimkimbilie yule mtu anayekuhubiria na kudhani ni yeye ndiye anayezungumza na wewe kama Samweli alivyomkimbilia Eli, Kwasababu ukifanya hivyo basi anaacha kwanza kuzungumza na wewe, badala yake mkimbilie Mungu anayezungumza nawe moyoni mwako pale ulipo, Itii sauti yake na mgeukie yeye, Na kumwambia Bwana “ Zidi zungumza nami kwa kuwa mtumishi wako anakusikia, mwambie nibadilishe kwa kuwa mtumishi wako anakusikia” acha kuishi maisha ya dhambi kuanzi wakati huo na kuendelea, acha maisha ya ulevi, maisha ya uchawi, ya usengenyaji, ya uasherati,ya utazamaji pornography, ya ufanyaji masturbation, ya wizi,ya kamari, ya utukanaji, ya ulaji rushwa n.k n.K. Mtii Mungu na kuanza kuishi maisha yanayokubalika mbele zake, kwa kuacha kuvaa nguo zisizofaa; kama vimini, suruali,nguo zinazobana na upakaji wanja na lipstick..Jitenge na hivyo vyote kwasababu ndivyo vinavyowapeleka mamilioni ya watu kuzimu. Na sauti ya Bwana inakuonya leo uviache hivyo vyote.

Bwana Yesu alisema katika Yohana 3:3 “…Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.”. Unazaliwa mara ya pili kwa kumwamini Yesu Kristo kwamba alitumwa na Mungu, akaishi duniani maisha matakatifu yanayokubalika na Mungu akampendeza Mungu, akakushuhudiwa kuwa ndiye pekee ampendezaye Mungu, akasulibiwa kwa ajili ya dhambi zetu, akafa, akazikwa na siku ya tatu akafufuka, akapaa mbinguni, naye amewekwa kuwa mpatanishi wa sisi na Mungu na hakuna mwingine, na atarudi tena kuja kulinyakua kanisa lake kwenda nalo mbinguni.

Baada ya kumwamini hivyo..Hatua inayofuata ni kukusudia na kudhamiria kuacha maisha ya dhambi uliyokuwa unaishi huko nyuma maisha yote ya usengenyaji, maisha yote ya ulevi na uvutaji sigara, maisha yote ya kikahaba na utoaji mimba, maisha yote ya ulaji rushwa, utapeli na uwizi, maisha yote ya uashetari na uvaaji mbaya..Unasema kuanzia leo na kuendelea mimi ni hayo maisha ndio basii..!!

Ukishakusudia kufanya hivyo kwa vitendo na sio kwa mdomo tu, moja kwa moja bila kukawia nenda katafute ubatizo sahihi, huo utakuwa ni kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako,kulingana na Matendo 2:38, na kumbuka ubatizo sahihi sio wa kunyunyiziwa, bali ni wa maji mengi, wakuzamishwa mwili wote na ni kwa jina la Yesu Kristo.

Baada ya kufuata hatua hizo mbili rahisi, utakuwa umepiga hatua moja kubwa na ya muhimu katika maisha yako, ambayo hutajutia kamwe. Na baada ya hapo Bwana atayafanya yaliyosalia kwa kukupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu atakayekuwezesha kuishi maisha matakatifu na kukutia katika kuijua na kuielewa kweli yote ya Neno lake (Yaani Biblia takatifu). Nawe utakuwa umezaliwa mara ya pili, Mrithi wa Baraka za Mungu.

Mungu akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

SAUTI NYUMA YA ISHARA.

NAMNA YA KUITAMBUA SAUTI YA MUNGU INAPOZUNGUMZA NA WEWE

ROHO MBAYA KUTOKA KWA BWANA.

Print this post

VITA BADO VINAENDELEA.

Shetani hapo nyuma alikuwa na mamlaka na hii dunia hata kufikia hatua ya kuweza kujiamulia kufanya jambo lolote na kufanikiwa, kiasi cha kuweza hata kuzuia majibu ya maombi ya watu yasiwafikie kwa wakati haijalishi mtu huyo atakuwa ni mcha Mungu kiasi gani, bado atayazuia tu, Tunaona mambo hayo yalitokea kwa Danieli, pale alipokuwa amefunga majuma matatu akiutafuta uso wa Mungu, Na kama tunavyosoma, biblia inasema mkuu wa ufalme wa Uajemi (Pepo la uajemi ), alimzuia malaika wa Bwana kwa muda wa wiki tatu ili tu asifikishe majibu ya maombi ya Danieli, Unaona hapo vita vya kiroho vilikuwa ni vikali sana wakati ule mpaka Danieli kufikia kusema, NI VITA VIKUBWA (Danieli 10:1) haikiwa ni kazi ndogo, aliiona taabu yake.

Zaidi ya hayo Shetani alikuwa na uwezo hata wa kuwaendea watakatifu wa Mungu waliokuwa wamelala, huko sehemu za wafu na kuzungumza nao, alifahamu mahali walipo na kwenda huko,kwani funguo za mauti na kuzimu zilikuwa bado mikononi mwake.

Hivyo Shetani aliendelea, kulitawala hili anga la kiroho kwa muda mrefu sana, vitu vyote vilikuwa mikononi mwake, na ndio maana alimwambia Bwana Yesu kule nyikani “Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo”.

Unaona? Wayahudi waliliona hilo tangu zamani, hivyo walikaa katika matumaini wakingojea siku ambazo ile Nuru kuu, nyota ya Alfajiri itakapozuka Israeli na kuangaza tena katikati yao na katika ulimwengu mzima, Walikuwa wanalisubiria hilo kwa hamu, siku ambazo Mungu atawarejeshea tena lile tumaini lao lililokuwa limepotea tangu Edeni..

Maneno haya yaliwatia faraja walipoyasoma:

Isaya 49: 6 “naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu [Azungumza habari za YESU] ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe NURU YA MATAIFA, UPATE KUWA WOKOVU WANGU HATA MIISHO YA DUNIA”.

Isaya 9:2 “Watu wale waliokwenda katika giza WAMEONA NURU KUU; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza.”

Nuru hiyo kuu, waliitazamia wakimwomba Mungu kila siku bila kukoma.

Na ndio hapo tunakuja kuona miaka 2000 iliyopita Nuru hiyo inakuja kutokea duniani, Nuru ambayo hata wanajimu waliuona utukufu wake kwa jinsi ilivyokuwa inang’aa sana gizani, Siku ambazo alizaliwa mwokozi duniani, ni wakati ambao shetani alipatwa na wakati mgumu sana, kuliko nyakati nyingine zote ambazo alishawahi kuwa nazo. Na tunaona siku ile Bwana alipokufa na kufufuka ndipo hali yake ilipozidi kuwa mbaya zaidi, akiona kuwa ameshanyang’anywa mamlaka yote na nguvu zote, na funguo zote za mauti na kuzimu alizokuwa nazo juu ya huu ulimwengu hapo kabla.

Tunayathibitisha hayo kwa maneno yaliyotoka katika kinywa cha Kristo mwenyewe akisema:

Mathayo 28: 18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.”

Unaona hapo? Kauli hiyo inaonyesha kuwa kumbe hapo kabla mamlaka hayakuwa kwake, bali yalikuwa mikononi mwa mtu mwingine, na huyu si mwingine zaidi ya shetani. Sasa kuanzia huu wakati, na kuendelea vitu vyote, mamlaka yote na chochote kile unachokifahamu kilianza kumilikiwa na YESU KRISTO, Bwana wetu.Haleluya!!…Vita alishavipigana na kushinda, kama kutupwa chini basi shetani alishatupwa chini tangu siku ile pale Kalvari, hana lake tena duniani.

Na kama ni hivyo basi, hapa juu yetu mkuu wa anga anapaswa awe YESU Kristo na si pepo tena, shetani hapaswi kuamua chochote juu ya miili yetu, hapaswi kuzuia maombi yetu, hapaswi kutuamulia mbaraka wetu kutoka kwa Mungu, yeye hana uwezo wa kututajirisha wala kutufukarisha, kwa ufupi hapaswi kuonekana katika dira ya maisha yetu popote pale, kwani alishashindwa vita na anayemiliki sasa ni mwingine, hivyo yeye hastahili kuwepo duniani, atafute sehemu yake nyingine ya kumiliki, lakini si katika dunia hii,

Lakini swali linakuja kama ni hivyo basi, ni kwanini, shetani bado anaendelea kuwatesa watu?, ni kwanini bado kuna vita, ni kwanini bado tunamwona shetani akizurura zurura katikati ya maisha yetu, ni kwanini bado anatuletea matatizo kana kwamba hakuna chochote kilichofanyika pale Kalvari, Na bado Biblia bado inatuambia maneno haya:

Waefeso 6:11-18 “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.

12Kwa maana kushindana kwetusisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.

14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,

15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;

16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye

moto ya yule mwovu.

17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;

18 kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;

Ni kwanini haya yote?. Sasa Kama utakuwa ni mfuatiliaji mzuri wa habari zinazaoendelea duniani, utakuwa umeshawahi kusikia mara nyingi juu vita vinavyoendelea katikati ya mataifa Fulani, mfano jeshi la nchi la husika pamoja na vikosi vya umoja wa mataifa utasikia vimefanikiwa kudhibiti maficho yote, na maeneo yote yaliyokuwa yanamilikiwa na waasi na hivyo waasi wametawanywa na kukimbilia katika mataifa jirani, hivyo nchi sasa ipo katika amani. Lakini utaona taifa litadumu katika amani kwa kipindi kifupi tu, halafu ghafla utasikia mapambano yamezuka tena, waasi wamevamia kambi za wanajeshi na kuwaua, au sehemu nyingine utasikia waasi wamekivamia kijiji Fulani na kukichoma moto.

Na hali hiyo hiyo utaona itaendelea kwa muda mrefu sana, japo hiyo nchi ni kweli imefanikiwa kuwatokomeza waasi wote, lakini ile roho ya uasi bado ipo ndani ya nchi, na ndio hapo utaona leo kumetulia kesho mapambano, hivyo hivyo itaendelea kwa miaka na miaka . Na ndio hapo utaona majeshi yanalazimika kuweka makao ya kudumu katika nchi husika, muda wote yanakuwa macho, yanakesha kulinda usalama wa raia,na mali zao yanazunguka huku na huko, kuangalia kama upo usalama katikati ya vijiji vyake, na kuvuruga vikundi vyote wanavyovihisi vitakuwa vinahusika na shughuli za uasi.

Kwasababu wanajua mfano wakizembea tu, au wakipunguza nguvu kidogo, wanafahamu kabisa wale waasi bado wana hasira na serikali, japo wameshindwa lakini chini kwa chini bado wanaunda mbinu za kuupindua ufalme. Hivyo vile vikosi vya kulinda amani haviwezi kustarehe japo kweli vinaimiliki nchi yote.

Na ndivyo ilivyo kwetu sisi wakristo vita bado vinaendelea. Ni kweli ushindi tuliupata pale Kalvari, Tulifanikiwa kumnyang’anya shetani mamlaka yote kwa Damu ya Yesu Kristo iliyomwagika pale msalabani, shetani hana uwezo tena wa kuzuia maombi yetu, wala kufanya kitu chochote juu ya miili yetu au katika maisha yetu. Lakini kama na sisi hatutakuwa macho, kuilinda enzi yetu tukilala, tuwe na uhakika kuwa kama vile Bwana Yesu alivyosema katika

1Petro 5:8 “mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze”. Basi tujue kuwa yale mambo aliyokuwa anaweza kuyafanya zamani bado ataendelea kuyafanya hata sasa hivi kama hatusimama.

Tusijifariji na kusema sisi ni wakristo maombi yetu hayawezi kuzuiwa kwasababu sisi tupo katika agano lililo bora zaidi ya lile agano la kale, na huku hatuzingatii kusimama kama wanajeshi wa Kristo, hatujajifunga kweli viunoni mwetu, Neno la Mungu hatulijui,halipo ndani yetu, chepeo ya wokovu ipo mbali nasi, habari za wokovu hatutaki kusikia, hatuna Roho ndani yetu, ambaye kwa huyo anatupa uhakika kuwa sisi ni watoto wa Mungu, na kutuongoza katika kweli yote. Dirii ya haki hatujaivaa yaani, mambo maovu ya rushwa, ulaguzi, biashara haramu vimekuwa ni sehemu ya maisha yetu na bado tunajiita wakristo. Hatuna muda wa kusali wala kudumu katika maombi kama biblia inavyotuagiza kila wakati tunawaza mambo ya ulimwengu huu, , unategemea vipi tutayakwepa majaribu ya Yule mwovu?.

Bwana mwenyewe alituambia tukeshe tuombe tusije tukaingia majaribuni, sasa kama sisi hatuna desturi hizo, unategemea vipi tutamkwepa Yule mwovu maishani mwetu? Yeye Bwana Yesu mwenyewe alifunga na kusali, sisi inatupasaje? Na ndio maana wakati mwingine tunaomba tunaona kama hatujibiwa, au majibu yanachukua muda kufika ni kwasababu Yule mkuu ya anga (Pepo) ambaye alishashindwa tangu siku nyingi, sisi tunamrudisha katika nafasi yake ya kale kwa mienendo yetu, na ndio maana matokeo yanakuwa ni hafifu au wakati mwingine kuchukua muda mrefu kujibiwa.

Vita bado vinaendelea. Kazi yako wewe ni kuilinda enzi uliyopewa na YESU, kila wakati kuhakikisha je! Zile silaha zote zinazozungumziwa katika Waefeso 6, umezivaa?. Kama umezivaa basi shetani atabakia kuwa mbali na wewe, na dunia yako itakuwa chini ya milki ya Bwana Yesu na vyote utakavyomwomba utapata, kwasababu shetani hatapata mlango wa kuzua mambo yake kwenye njia zako.

Mpaka siku itakapofika ambayo sasa, UASI wote utaondolewa duniani, Yaani siku ambayo shetani, pamoja na mapepo yake, pamoja na watu wake waovu watakapoondolewa duniani sasa siku hiyo ndiyo, hakutakuwa na haja ya kulinda enzi yoyote ile na siku hiyo haipo mbali ndugu, mwisho wa kila kitu umekaribia. Hakutakuwa na kukesha huko, hakutakuwa kusoma biblia, hakutakuwa na majaribu,ni wakati wa mambo mapya, ni wakati ambao mema yote Mungu aliyokuwa ameyakusudia watu wake kabla hata ya kuwekwa msingi ya ulimwengu ndipo yatakapofunuliwa, mambo ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia. Tusitamani kukosa.

Lakini kwasasa hatuna budi kuyathibishwa mamlaka tuliyopewa, kwa kuzingatia kukesha, kuzivaa SILAHA ZOTE tulizopewa ili tuweze kuyafurahia matunda yote ya Bwana wetu Yesu aliyotushindia siku ile pale Kalvari.

Kama hujampa Bwana maisha yako, huu ndio wakati usingoje kesho, Mwamini kwamba yeye ni Mwana wa Mungu, na alikuja kwa ajili ya kukuosha dhambi zako, na kukupa uzima wa milele. Na kisha utubu dhambi zako zote naye ni mwaminifu atakusamehe na kukupa uzima wa milele.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine, Na Bwana atakubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

TUKAZE MWENDO ILI TUUFIKILIE UTIMILIFU

VITA VYA KIFIKRA BAADA YA KUZALIWA MARA YA PILI

NINI MAANA YA HUU MSTARI “NIMEVIPIGA VITA VILIVYO VIZURI, MWENDO NIMEUMALIZA, IMANI NIMEILINDA”?(2TIMOTHEO 4:7)


Rudi Nyumbani

Print this post