Jina la BWANA wetu YESU KRISTO lihimidiwe daima. Karibu katika uchambuzi wa kitabu cha Ufunuo leo tukianza na ile sura ya kwanza.; Tunasoma…
“1 Ufunuo wa Yesu Kristo, aliopewa na Mungu awaonyeshe watumwa wake mambo ambayo kwamba hayana budi kuwako upesi; naye akatuma kwa mkono wa malaika akamwonyesha mtumwa wake Yohana;
2 aliyelishuhudia Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu Kristo, yaani, mambo yote aliyoyaona.”
Awali ya yote tunaona hapa Yohana akiandika na kusema “Ufunuo wa Yesu Kristo” akimaanisha kuwa alichokipokea sio ufunuo wake bali ni wa Yesu mwenyewe. Kumbuka Yohana ndiye Mtume pekee aliyekuwa karibu sana na Bwana, na aliyependwa na Bwana kuliko mitume wote, Kiasi kwamba hata siri za karibu sana za Bwana alikuwa anazipokea kwanza yeye ndiye ndipo wengine wafuate, ni mtume pekee aliyekuwa akiegema kifuani mwa Bwana muda wote (Yohana 13:23, na Yohana 21:20), Na ndio maana tunaona wakati ule wa jioni wa kuumega mkate, Bwana aliposema mmoja wenu atanisaliti, Petro alimpungia mkono Yohana amuulize Bwana ni nani atakayemsaliti, na Bwana akamfunulia Yohana ni yule atakaye mmegea tonge na kumpa, kwasababu Petro alijua Yohana ndiye kipenzi wa Bwana.
Kwasababu ya uhusiano wake wa kipekee na Bwana, ilimpelekea, mpaka kufikia hatua ya kupewa neema hii ya MAFUNUO na Bwana mwenyewe, mambo ambayo yatakuja kutokea katika siku zake na siku za mwisho. Yohana ni mfano wa Danieli ambaye naye alikuwa ni mtu aliyependwa sana na Mungu, Ikapelekea yeye naye kupewa mafunuo yanayofanana na ya Yohana. Kwahiyo kama ukichunguza utagundua watu wanaofunuliwa Mafunuo makuu kama haya sio tu kila mkristo, au mwamini yoyote bali ni mtu yule anayependezwa na Mungu, Vivyo hivyo na sisi tukimpendeza Bwana atatupa siri zake za ndani zaidi.
Mstari wa 3 unasema; “Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu”. Hapa Biblia inasema heri ikiwa na maana kuwa amebarikiwa mtu yule ASOMAYE, ASIKIAYE, na AYASHIKAYE ..Na kusikiwa kunakozungumziwa hapo ni kusikia kwa masikio ya ndani (yaani kupata Ufunuo ) na sio masikio ya nje, na kuyashika ikimaanisha kuyaishi uliyoyasikia. Hivyo Mtu yeyote afanye hivyo biblia inasema amebarikiwa. Kumbuka Si watu wote wanapata neema hii ya kukielewa kitabu hichi, kwasababu ni kitabu kilichofungwa hivyo kinahitaji kufunguliwa na Roho mwenyewe. Kwahiyo kama wewe umepata neema, jitahidi kuyaishi yaliyoandikwa humo ili na wewe uitwe HERI.
Tukiendelea mistari inayofuata;
“4 Yohana, kwa yale makanisa saba yaliyoko Asia; Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwake yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja; na zitokazo kwa roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi;
5 tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake,
6 na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina”.
Tunasoma hapa Yohana anaanza na salamu kwa yale makanisa 7 aliyopewa kuyaandikia maneno hayo. Anasema neema iwe kwenu na amani zitokazo kwa yeye “aliyekuwako, aliyeko na atakayekuja”, Hii inafunua umilele wa Mungu Elohimu, Yeye pekee ndiye asiyekuwa na mwanzo wala mwisho. Tena zitokazo kwa Roho saba walioko mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Sasa kumbuka Mungu hana Roho 7, Tunajua wote Mungu mwenyewe ni Roho(1),na nafsi moja, hapo anaposema hapa roho 7 haina maana kuwa anazo roho 7, bali anaonyesha jinsi Roho ya Mungu ilivyokuwa inatenda kazi katika yale makanisa 7 ambayo tutasoma habari zake hapo baadaye. Na pia anasema Neema na Amani zitakazo kwa Yesu Kristo aliyeshahidi mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa. Kama tunavyojua Mungu alitoka katika UMILELE akaingia katika MUDA ili kumkomboa mwanadamu. Hivyo akauandaa mwili ili akae ndani yake. Na huo mwili ukawa YESU.
Kwahiyo Mungu alikuwa ndani ya Yesu akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake (2Wakorintho 5:18-19). Kwahiyo hapa haizungumzii UTATU, hapana Mungu ni mmoja anayo nafsi moja, na Roho moja. Kwa mfano mimi ninaweza kuzungumza na wewe kwa kutumia account ya facebook, yenye jina, picha na utambulisho wangu. Ninazungumza, ninaongea na wewe ninajibu maswali, lakini haimaanishi sisi tupo wawili. kwamba wa kwanza ni mimi na wapili yule wa mtandaoni hapana mimi ni yule yule mmoja isipokuwa nimeingia ndani ya facebook ili nikutane na jamii ya watu fulani. vivyo hivyo na Mungu ambaye hana mwanzo wala mwisho aliingia ndani ya mwili wa kibinadamu (1Timotheo 3:16) ili tu kutupata sisi wanadamu..Na kama vile ile account yangu siku moja ilikuwa na mwanzo wake vivyo hivyo Bwana Yesu alikuwa na mwanzo, na ndio maana utakuja kuona kuna mahali anasema yeye ni ALFA NA OMEGA. Lakini haimaanishi kuwa Mungu (ELOHIM) ana mwanzo na mwisho…hapana Yeye hana mwanzo wala mwisho, kwasababu yeye ndio mwanzo na ndio mwisho.
“7 Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake. Naam. Amina.
8 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi”.
Sasa Biblia inasema upo wakati Bwana aliouweka wa yeye kurudi tena ambao kila jicho litamwona na hao waliomchoma mkuki pale Kalvari (yaani wayahudi na watu wa mataifa) watamwombolezea, kumbuka hapa sio ule wakati wa kulichukua kanisa lake, hapana bali utakuwa ni ujio wa Bwana Yesu kuja duniani na watakatifu wake waliokuwa wameshanyakuliwa muda wa miaka 7 iliyopita tangu tukio hilo litokee. Hapo ndipo kila jicho la watu waliosalia ambao majina yao hayakuandikwa katika kitabu cha uzima tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu watamwona na kumuombolezea..
Mathayo 24: 29 “
Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika;
30 ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi. (soma pia Yuda 1:14 na Ufunuo 19:11-21,)
Tukiendelea mistari inayofuata….
” 9 Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika MATESO na UFALME na SUBIRA ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu.
10 Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu,
11 ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba: Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira, na Sardi, na Filadelfia, na Laodikia.”
Yohana anasema “mimi ndugu yenu mwenye kushiriki pamoja nanyi”…Ikiwa na maana kuwa kile alichokuwa anakipitia, ndugu wengine walikuwa wanakipitia pia.mateso, dhiki,vifungo, na subira ya Yesu Kristo. Hii inaonyesha kabisa mojawapo ya utambulisho wa mkristo kwamba yupo katika safari ya Imani ni kupitia hayo kwa ajili ya Bwana.(Kumbuka ni kwa ajili ya Bwana, na si kwasababu nyingine zozote)
Lakini tunapokuwa wakristo lakini hatuna subira, kwa ajili ya Bwana, inaonyesha kabisa hatupo miongoni mwa hao ndugu waaminio.. Yohana anasema alikuwa katika kisiwa kiitwacho PATMO.Hichi ni kisiwa kilichokuwa maeneo ambayo sio mbali sana na yale makanisa 7 yaliyokuwepo Asia ndogo (ambayo kwasasa ni maeneo ya UTURUKI) umbali wa takribani km 60-120.
Ni kisiwa ambacho wafungwa walikuwa wanaenda kuachwa huko wafe, ni kisiwa kilichokuwa na mawe mawe tu, mijusi nyoka na kenge, na nge. Hakuna mimea kumezungukwa na maji kote, hivyo ni mahali pasipokuwa na jinsi yoyote ya kuishi au kutoroka mtu utaishia kufa kwa njaa au kuuawa na wanyama wakali. Hivyo Yohana naye alitupwa kule kama mmojawapo wa wafungwa. Na ndipo huko huko Bwana akamfunulia mambo ya siri kama tunavyoyasoma. Nasi pia tunajifunza wakati mwingine tukitupwa katika majaribu mazito (maadamu ni wakristo) tujue ni Bwana anaruhusu mwenyewe ili kutupa mafunuo zaidi.
Hivyo maono hayo Yohana aliyoonyeshwa hayakuwa ndani ya siku moja yote..Bali ulikuwa ni mfululizo wa maono kwa kipindi cha muda fulani.Ndipo akapewa maagizo kwamba ayaandike mambo yote anayoyaona na ayapeleke kwa yale makanisa saba yaliyopo Asia, yaani Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira, na Sardi, na Filadelfia, na Laodikia.
MTU MFANO WA MWANADAMU.
“12 Nikageuka niione ile sauti iliyosema nami. Na nilipogeuka, niliona vinara vya taa saba vya dhahabu;
13 na katikati ya vile vinara nikaona mtu mfano wa Mwanadamu, amevaa vazi lililofika miguuni, na kufungwa mshipi wa dhahabu matitini.
14 Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe, kama theluji; na macho yake kama mwali wa moto;
15 na miguu yake kama shaba iliyosuguliwa sana, kana kwamba imesafishwa katika tanuru; na sauti yake kama sauti ya maji mengi”.
Tunaona Yohana alipogeuka aisikie ile sauti akaona mtu “MFANO” wa mwanadamu. aliyevaa vazi lililofika miguuni, na kufungwa mshipi wa dhahabu matitini. Kumbuka Yohana kuonyeshwa vile haikuwa na maana kuwa Bwana Yesu anataka kuonyesha mwili wake jinsi ulivyo na utukufu au unavyotisha mbele za wanadamu, hapana, bali kila kitu alichokuwa anakiona katika mwili wake kilikuwa kina maana fulani.. Kumbuka lile lilikuwa ni ONO sio kitu halisi.
Tukisoma tunaona Mtu yule alikuwa na nywele kama sufu nyeupe. Ikiashiria kuwa ni HAKIMU. (Kumbuka mahakimu huwa ni desturi yao kuvaa wigi nyeupe kichwani) Hivyo yule ni Muhukumu wa mambo yote, na weupe wake inaashiria usafi na haki ya hukumu yake. Atakapokuja kuketi katika kiti chake cha enzi cheupe, atawahukumu kwa haki watu wote. Tutakuja kuona vizuri katika sura 20.
Na pia mtu huyu alionekana ana macho kama mwali wa moto, na miguu iliyosuguliwa kama shaba. Ikifunua hukumu yake juu ya waovu katika kanisa na wasiomcha yeye ulimwenguni kote,.Kumbuka na macho kazi yake ni kuona, na miguu ni kukanyaga. Hivyo anapoonekana na macho ya moto inamaanisha kuwa anaona mambo yote yanayopaswa kuhukumiwa kwa moto. Tutakuja kuona pia katika kanisa la tatu la Thiatira (jinsi Bwana alivyojionyesha kwao kama miale ya moto na miguu ya shaba, kutokana na maovu yaliyojificha ndani ya kanisa hilo,).
Na kama miguu yake ilivyokuwa ya SHABA atakanyaga mambo yote maovu ndani ya kanisa lake kwanza kisha baadaye atamalizia na kwa ulimwengu mzima tutakapofika katika sura ya 14 tutaona pia jinsi atakavyokuja kukanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu mwenyezi (Ufunuo 19:15).
Tukizidi kuendelea kusoma mistari inayofuata..;
“16 Naye alikuwa na nyota saba katika mkono wake wa kuume; na upanga mkali, wenye makali kuwili, ukitoka katika kinywa chake; na uso wake kama jua liking’aa kwa nguvu zake.
17 Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho,
18 na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu. 19 Basi, uyaandike mambo hayo uliyoyaona, nayo yaliyopo, na yale yatakayokuwa baada ya hayo.
20 Siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume, na ya vile vinara saba vya dhahabu. Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba; na vile vinara saba ni makanisa saba”.
Tunaona pia mtu huyu anaonekana akiwa na nyota saba katika mkono wake wa kuume. Hizi nyota saba tafsiri yake kama inavyoelezwa ni malaika saba, mkono tunajua kazi yake ni kubeba, na ukiwa wa kuume, inamaana unabeba kitu stahiki, hivyo wale malaika (wajumbe 7) watakuwa wamebeba ujumbe stahiki kwa kanisa husika. na pia alionekana akitembea katikati ya vile vinara 7 vya taa ambavyo ndiyo yale makanisa 7. Jiulize ni kwanini hakuonekana akiwa katikati ya madhabahu, au katika birika ya shaba Katika Hekalu la Mungu?, bali anaonekana katikati ya vile vinara 7 vya Taa akitembea katikati yake?. Inamaana kuwa makao yake ni katikati ya yale makanisa saba. Huko ndipo jicho lake lilipo na Roho yake ilipo.
Mtu huyu pia alionekana na Upanga mkali ukatao kuwili unaotoka kinywani mwake. Kwa kawaida mtu hawezi kutoa upanga mdomoni, Tunafahamu Neno la Mungu ndio upanga wa Roho (soma waefeso 6:17) na pia waebrania 4: 12 inasema …“Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo”.
Hivyo upanga huo ambao ni NENO lake ameuandaa tayari kwa ajili ya vita kwa watu wote wanaokwenda kinyume na mapenzi ya Mungu. Na kama anavyosema ni upanga ukatao kuwili anamaanisha kuwa ni upanga unaokata pande zote yaani watu walioko ndani ya kanisa na watu walioko nje ya Kanisa.
Jambo hili tutakuja kuliona jinsi Bwana alivyojifunua kwao(Kanisa la pili Pergamo) kwamba yeye ndiye mwenye ule upanga mkali ukatao kuwili…aliasema “anayajua matendo yao na kwamba watubu na wasipotubu atakuja kufanya vita nao kwa huo upanga wa kinywa chake.(Ufunuo 2:16).
Kadhalika na kwa watu wa mataifa wasiomjua Mungu wao nao Bwana atakuja kufanya nao vita kwa huo upanga, jambo hili tutakuja kuliona katika ile sura ya 19:15 katika siku ile atakapokuja mara ya pili na watakatifu wake.
Utaona pia baada ya Yohana kuuona muonekana wa nje wa yule mtu alianguka chini kwa hofu na kutetemeka, Tunasoma ” 17 Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho,
18 na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu. “
Ndipo baada ya hayo yule mtu akajitambulisha kwa tabia zake za ndani ambazo Yohana hakuziona kwa macho..nazo ni
1)yeye ni wa kwanza na wa mwisho,
2) aliye hai,aliyekuwa amekufa na sasa yu hai milele na milele na ambaye
3) anazo funguo za Kuzimu.
Sasa kwa tabia hizo TATU Yohana ndipo alipojua kuwa yule MTU ni YESU KRISTO mwenyewe. Hivyo ule muonekano wa Nje ni msingi utakaotusaidi kuelezea ujumbe na kuelewa utendaji kazi wa Yesu katika habari husika zinazofuata. Ni muhimu kuzingatia hivyo vipengele, mfano tunaweza kuona katika kila kanisa anaanza kwa kujitambulisha kwa kipengele kimoja wapo cha mwili wake au tabia zake.
Hivyo kwa ufupi Alichoonyeshwa Yohana ni mfano wa ile sanamu aliyoonyeshwa Nebukadreza juu ya zile Falme 4 zitakazokuja kutawala mpaka mwisho wa dunia. Na kwamba kila sehemu ya ile sanamu (Kichwa cha dhahabu, kifua cha fedha, kiuno cha shaba na miguu ya chuma) ilikuwa na maana, na ndio iliyounda msingi wa kuelewa undani wa kitabu cha Danieli katika sura za mbeleni.Kadhalika na hichi kitabu cha Ufunuo, sura hii ya kwanza (Ambayo Inayoonyesha muonekano na tabia za Yesu Kristo ) ni msingi wa sisi kuelewa ujumbe katika sura zinazofuata za kitabu cha Ufunuo.
Hivyo usikose mwendelezo wa sura zinazofuata..
Ubarikiwe sana
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Washirikishe na wengine habari hizi.
Kwa Mwendelezo >>Ufunuo: Mlango wa 2 Part 1.
Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara, kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.
Mada Zinazoendana:
KWANINI YESU KRISTO ALIKUJA DUNIANI?
JE! HIZI ROHO SABA ZA MUNGU NI ZIPI?
About the author