Category Archive Uncategorized @sw-tz

Ipi Tofauti ya Agano jipya na Agano la Kale?.

Ili tuelewe vizuri utofauti uliopo kati ya Agano jipya na la kale,  tutafakari mifano ya kawaida ya maisha;

Hebu tafakari juu ya Elimu ya Awali (msingi) na Elimu ya Sekondari.. Utaona ulipokuwa shule ya msingi ulijifunza mahesabu ya  kujumlisha na kuzidisha kwa kutumia vitu vya asili kama vijiti au mawe.. Lakini ulipofika sekondari ulitumia kikokotoo (yaani calculator).

Sasa mabadiliko hayo hayaifanyi elimu ya msingi kuwa batili, kwasababu tu vipo vikokotoo..La bali zinaithibitisha zaidi ile elimu ya msingi.. kwasababu kikokotoo (calculator) kinapiga mahesabu yale yale ya kujumlisha na kuzidisha kwa kasi  na ufasaha zaidi.

Ni hivyo hivyo kwa Agano la kale na Agano jipya..

Mambo yaliyopo ndani ya Agano jipya ni mambo yale yale yaliyopo ndani ya agano la kale isipokuwa katika ufunuo bora zaidi na ufasaha mkubwa zaidi..

Tafakari tena mfano huu…

Toleo la kwanza la simu yako miaka 15 iliyopita..bila shaka lilikuwa ni mfano wa  “tochi”, lenye mipaka mingi ya matumizi lakini toleo la pili la sasahivi ni “smart” ambalo unaweza kuingia internet, kupakua applications, kutazama video na hata kusikiliza nyimbo.

Kwahiyo Toleo jipya halijaja kuondoa chochote kilichopokuwepo kwenye toleo la kale, isipokuwa limeboresha zaidi vile vilivyopo na kuongeza vingine vya ziada.. maana yake Kama mtu alikuwa anasikiliza tu sauti pekee, sasa katika toleo jipya atasikika sauti pamoja na picha ya anayeongea..

Hali kadhalika kama toleo la kwanza la simu lilikuwa linachukua muda kuwaka na linahifadhi nambari za simu za watu 100 tu, basi toleo jipya litakuwa linawahi kuwaka na pia kuhifadhi namba za watu hadi 1,000.

Ni hivyo hivyo katika habari ya Agano la kale na Agano Jipya..  

Agano jipya ni toleo bora zaidi la agano la kale,  ni kitu kile kile isipokuwa kimeandikwa na kutendeka katika ubora mkubwa zaidi, na ufunuo mkubwa zaidi..

Kwamfano katika agano la kale, kafara na dhabihu zilikuwa ni za wanyama lakini tunapokuja katika Agano jipya dhabihu zimeboreshwa zaidi,  badala ya kutumika damu za wanyama, inatumika damu ya MTU, YESU KRISTO (Ambayo ni bora zaidi).

Vile vile katika Agano la kale, amri ziliandikwa kwenye mbao za mawe kule mlima Sinai, lakini katika agano jipya amri na sheria za Mungu zinaandikwa katika mioyo yetu kiufunuo zaidi.

Yeremia 31:31  “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.

32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana.

33 Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu”.

Katika Agano la kale Uzinzi ulijulikana katika mwili tu (Kutoka 20:14) lakini katika Agano jipya uzinzi unajulikana katika mwili na roho kwa ufunuo bora zaidi (Soma Mathayo 5:28)

Katika Agano la kale uuaji ulijulikana katika mwili tu (Kutoka 20:13), lakini katika Agano jipya uuaji unajulikana katika mwili na roho kwa ufunuo bora zaidi (Soma Mathayo 5:21-22).

Katika Agano la Kale ni watu wachache tu ndio walishukiwa na Roho wa Mungu, (ambao walikuwa ni Manabii na Waamuzi) lakini katika Agano jipya watu wote wanayo fursa la kushukiwa na Roho Mtakatifu (Matendo 2:17-18).

Kwahiyo Agano  jipya ni mwendelezo wa Agano la kale katika ubora zaidi na utimilifu na ufunuo mkamilifu, ndio maana Bwana YESU alisema hakuja kuitangua torati bali kuitimiliza.

Mathayo 5:17 “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza”.

Na Roho Mtakatifu ndiye Msaidizi wetu tuliyepewa ambaye atatusaidia kulielewa Agano la Kale na Agano jipya, hivyo hatuna budi kumtafuta huyo kwa bidii zote.

Na Roho Mtakatifu ni ahadi ya Bure kwetu kwa watu wote pasipo kujali umri (Matendo 2:37-38), tukimpata Roho Mtakatifu basi tutazidi kuielewa Biblia.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Orodha ya majina ya Miji ya Biblia (Agano la kale) na Sasa

Je! habari ya Yusufu, inabeba ujumbe gani kwa agano jipya?

Neno “Mashehe” tunaliona likitajwa katika biblia(Agano la kale); Hawa mashehe ni wakina nani?

MAWE YALIYOKWISHA KUCHONGWA MACHIMBONI.

NGUVU YA UPENDO WA KRISTO.

Print this post

kila mtu alaye zabibu kali, meno yake yatatiwa ganzi

SWALI: Nini maana ya Yeremia 31:30 “Bali kila mtu atakufa kwa sababu ya uovu wake mwenyewe; kila mtu alaye zabibu kali, meno yake yatatiwa ganzi”.


JIBU: Zamani za agano la kale katika taifa la Israeli, kulikuwa na usemi maarufu, unaosema “Baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi”.

Kikawaida zabibu au matunda mengine yenye asidi nyingi mtu alapo , huwa meno yanatia  ganzi, lakini kamwe haiwezekani mtu mwingine akatiwa ganzi kwa ulaji wa mwingine.

Hapa Waisraeli wakiwa wanamaanisha kuwa adhabu za Mungu huwa zinatembea hata kwa kizazi cha watu,  Lakini Mungu kwa kinywa cha Yeremia anawasahihisha kuwa hilo si jambo lake..Anawaambia kila mtu ataadhibiwa sawasawa na uovu wake, wala watoto hawatauchukua uovu wa wazazi wao..Jambo ambalo alilirudia pia kwa kinywa cha Nabii Ezekieli (Ezekieli 18:20).

Lakini pia ukisoma muktadha wa vifungu hivyo, utaona anatoa unabii wa agano jipya ambalo atalifanya na watu wake kupitia Yesu Kristo, akimaanisha kuwa wokovu wake pia , utakuwa ni wa mtu binafsi, mmoja mmoja. Tusome habari yote tokea juu.

Yeremia 31: 27 Tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapoipanda nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda, mbegu ya mwanadamu na mbegu ya mnyama.
28 Tena itakuwa, kwa kadiri nilivyowaangalia, ili kung’oa, na kubomoa, na kuangusha, na kuangamiza, na kutesa; kwa kadiri iyo hiyo nitawaangalia, ili kujenga, na kupanda, asema Bwana.
29 Siku zile, hawatasema tena, Baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi.
30 Bali kila mtu atakufa kwa sababu ya uovu wake mwenyewe; kila mtu alaye zabibu kali, meno yake yatatiwa ganzi.
31 Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.
32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana.
33 Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.

Hivyo vifungu hivi, vinatupa kutambua kuwa wajibu wa kulitunza  agano la Mungu ni la mtu binafsi, sawasawa na alivyokuja kulifunua katika agano jipya kupitia Yesu Kristo, kwamba ijapokuwa wokovu umeachiliwa kwa wote, lakini haupokelewi kijumuiya, kifamilia, au kikabila, bali kibinafsi.

Kila mtu atalibeba furushi lake mwenyewe. (Wagalatia 6:5)

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Tafsiri ya Yeremia 29:12 Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza.

Yeremia alikuwa na umri gani alipoitwa?

Mti wa MLOZI alioonyeshwa nabii Yeremia 1:12 tafsiri yake ni nini?

 

 

 

Print this post

Je! Ni sahihi kwa mkristo kufundishwa na AI mfano wa Chatgpt, deepseek n.k.

SWALI: Je! Ni sahihi kwa mkristo kujifunza, au kufundishwa na AI (Artificial Inteligence), mfano wa Chatgpt, deepseek n.k.


JIBU: Ili kujibu swali hili ni vema, kutambua mashine hizi za akili bandia (AI), zinafanya kazi gani.

Kwa ufupi ni kuwa AI, inafanya kazi ya kuchakata taarifa nyingi, kutoka katika vyanzo vingi vilivyopo mitandaoni, mfano vitabu, makala, sauti, machapisho n.k, na hivyo inazichanganya taarifa hizo zote kwa kuangalia muktadha unaofanana na kuzifupisha, na kukujibu.

Hivyo kimsingi, ni chombo ambacho kinatoa msaada mkubwa katika ulimwengu wa sasa, na ndio ukweli usiopingika..Kwasababu kinarahisisha utafutaji wa taarifa. Lakini pamoja na hayo haimaanishi kuwa kinatoa kwa ufasaha wote.

Sasa tukija kwenye eneo la kiroho. Je ni vema mkristo kwenda kuuliza AI, au kuandaa maombi au masomo kupitia hiyo, n.k.

Ukweli ni kwamba Imani, sio taarifa, ni zaidi ya taarifa.. Hizi AI, zinatoa tu taarifa lakini hazitoi mafunuo. Hazina pumzi ya Roho Mtakatifu ndani yake.

Ikiwa unataka kuongeza maarifa kwa sehemu fulani zinaweza kukusaidia, lakini sio kukujenga nafsi, kwani inahitaji pumzi ya Mungu na miongozo ya Mungu wewe kujengwa nafsi, na sio taarifa.

Kwamfano ikiwa wewe ni mchungaji halafu, kila inapokaribia jumapili unachowaza ni kwenda chatgpt, kuiambia ikuandalie somo la kufundisha jumapili,  ndugu hapo hesabu kuwa umepotea kama sio kukengeuka… Tumia hiyo kwenye biashara zako, masomo yako,  projekti zao lakini sio kwenye mambo ya kiroho. Hilo liepuke kabisa.

Kufundisha Neno inahitaji ‘Neno’ mwenyewe (Yesu) akae ndani yako, kwasababu ni UHAI sio taarifa (Waebrania 4:12) ndio hapo itakupasa kupiga magoti kwanza uombe, kwa muda mrefu, utafakari moyoni mwako, ukae kwenye utulivu wa kutosha, ndipo Mungu alipande somo lake moyoni mwako. Ambalo yeye mwenyewe anajua litakuwenda kuwagusa vipi watu wake, wenye changamoto mbalimbali, kwamfano, pengine mtu mmoja alikuwa anakaribia kwenda kujinyonga kwasababu ya ugumu wa maisha na mateso fulani, na Mungu kamwona anataka amsaidie, kwa kuliweka somo linalohusiana na mapito ya Ayubu ili ainuliwe imani. Kinyume chake kwasababu ya uvivu wako wewe unakwenda kuiambia chatgpt (akili bandia), ikuandalie somo. Halafu jumapili utakwenda na taarifa zao sio mafunuo. Badala uokoe roho inayokwenda kujinyonga, unaiambia, “leo tunajifunza kanuni kumi za kudumisha ndoa na mahusiano kibiblia”. Hapo unafanya nini sasa?

Au Neno fulani Bwana anataka kukupa la wakati wako, sasa ikiwa unakimbilia AI ikusaidie, hutaki kuchukua muda wako binafsi kutafakari na kuomba ‘jiandae kukutana na ukame wa kiroho.

Visaidizi hivi, hatupaswi kuvifanya ndio sehemu ya imani yetu, kwamba kila kitu tutegemee kule, hivi ni tone dogo sana kati ya bahari kubwa. Roho Mtakatifu alishatuandalia njia zake, kuu za kujengwa na yeye.

Wekeza zaidi, kuomba msaada kwa wakufunzi wako, viongozi wako, ndugu zako katika Kristo, wekeza katika maombi, mifungo, tafakari, na kujisomea mwenyewe Neno.  kwa njia hizi hakika Bwana atasema nawe na kujengwa zaidi kuliko visaidizi. Lakini pia ikiwa pana umuhimu wa kujiongezea taarifa kwa vile unavyovijua, visaidizi hivi vitakufaa (Katika uangalizi maalumu), vinginevyo utajidumaza kiroho.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >>  https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Karismatiki ni nini?

Uinjilisti kama agizo kuu la Bwana.

Vita vya kiroho, na mwamini Mpya.

Print this post

Nyakati za Mwisho na Tumaini la Utukufu kwa Mwamini Mpya

Kama mwamini ni lazima ujue kila kitakachotekea siku za mwisho, na kile Mungu alichokiahidi kuhusu maisha yajayo

Siku za mwisho zilianza wakati ule wa pentekoste Roho alipomiminwa duniani, kwa watu wote, na hizo zinaendelea hadi sasa mpaka wakati ambapo Kristo atatokea ulimwengu kwa mara ya pili kuleta hukumu na ufalme wake mpya.

Ni ukweli usiopingika kwamba tupo ukiongoni kabisa mwa siku za mwisho.Ingawa Biblia haitupi tarehe kamili (Mathayo 24:36), inatupa ishara na maagizo ya kuwa macho na wenye tumaini wa siku hiyo kuu.

1) Baadhi ya Matukio Muhimu ya Nyakati za Mwisho ni kama yafuatayo:

  •  Injili kufikishwa kwa mataifa yote. (Mathayo 24:14).
  • Dhiki kuu — mateso na majaribu makali (Mathayo 24:21; Ufunuo 13)
  • Kuongezeka kwa maovu na maasi (2 Wathesalonike 2:3)
  • Kuibuka kwa Mpinga Kristo (1 Yohana 2:18; 2 Wathesalonike 2:4)
  • Kurudi kwa Yesu katika utukufu (Mathayo 24:30)
  • Ufufuo wa wafu na hukumu ya mwisho (Yohana 5:28-29)

Hii inaonyesha kwamba historia inaelekea kwenye mwisho ulioamriwa na Mungu.

2. Kurudi kwa Yesu Kristo

Yesu aliahidi atarudi tena (Yohana 14:3). Kurudi kwake hakutakuwa kwa siri, bali kutakuwa kwa utukufu, nguvu na hukumu.

[11]Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.
. — Matendo 1:11

Ukweli uhusuo Kurudi Kwake:

  • i) Utaonekana na wote (Ufunuo 1:7)
  • ii) Utakuwa ghafla (Mathayo 24:27)
  • iii) Utakuwa katika utukufu mkubwa (Mathayo 24:30)
  • iv) Yesu atarudi akiwa na malaika na watakatifu wake (1 Wathesalonike 3:13)

Katika siku hiyo:

  • Uovu wote utaangamizwa (2 Wathesalonike 1:7-10)
  • Shetani atahukumiwa (Ufunuo 20:10)
  • Ufalme wa Mungu utaonekana kikamilifu (Ufunuo 11:15)

 3. Tumaini la Utukufu

Hili si tumaini la kubahatisha — ni matumaini ya hakika yaliyowekwa juu ya ahadi za Mungu.

“Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu.” — Wakolosai 1:27

Utukufu” Ni Nini?

Kimaandiko, utukufu humaanisha:

Uwepo wa Mungu unaoonekana (Kutoka 33:18-20)

Utakatifu wake ulio mkuu na mkamilifu (Isaya 6:3)

Hali ya mwisho ya waamini — kufanana na Kristo milele (Warumi 8:17; 2 Wakorintho 3:18)

 4. Nini Kinamngojea Mwamini?

  1. Mwili wa utukufu.

1 Wakorintho 15:52
[52]kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.

Hakutakuwa na ugonjwa, uchovu, wala mauti tena. Tutakuwa na miili kama wa Yesu baada ya kufufuka kwake (Wafilipi 3:20-21).

ii) Makao ya Milele

Yesu amekwenda kutuandalia  makao (Yohana 14:2). Mbingu mpya na dunia mpya hazitakuwa na huzuni, machozi wala laana (Ufunuo 21:1-5).

iv) . Kumwona Mungu Uso kwa Uso

Hatutamtazama tena kwa imani bali tutamwona moja kwa moja (Ufunuo 22:4). Tutamtumikia na kumtukuza milele (Ufunuo 22:5).

 5. Kuishi kwa fikra za Milele

🔸Kuwa Macho

Kanisa la kwanza liliishi kwa umakini mkubwa. Wakijua kuwa Yesu anaweza kurudi wakati wowote (Tito 2:13).

→ Usicheleweshe toba wala kuwa mzembe kiroho.

🔸Ishi Maisha Matakatifu

“Kila mwenye tumaini hilo ndani yake hujitakasa, kama Yeye alivyo mtakatifu.” — 1 Yohana 3:3

Ufahamu wa kurudi kwa Kristo unapaswa kutuchochea kuishi maisha ya utakatifu na utii.

🔸 Kuwa na Tumaini

Tufahamu kuwa Majaribu haya ni ya muda. Tumaini letu ni nanga ya roho zetu (Waebrania 6:19).

🔸 Tembea na Ujumbe kwa wengine.

Milele ni halisi. Ndio maana tunahubiri Injili—kwa sababu maisha ya watu yana hatma ya milele.

 Tafakari ya Mwisho:

“Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo!” — Ufunuo 22:17

 “Amina. Njoo, Bwana Yesu.” — Ufunuo 22:20

Sauti ya kanisa si hofu, bali ni shauku. Nyakati za mwisho si mwisho wa matumaini, bali ni mwanzo wa utukufu wa milele kwa wote waliomo ndani ya Kristo.

Mafundisho ya ziada kuhusu Siku za Mwisho.

KUWA MAKINI, HATUA ZA UNYAKUO ZINAENDELEA.

NYUMBANI MWA BABA YANGU MNA MAKAO MENGI.

SIFA SITA (6), ZINAZOIKAMILISHA ILE SIKU YA BWANA ITISHAYO.

Jehanamu ni nini?

MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 1)

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >>  https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Biblia unapozungumzia kuhusu kupewa jina jipya inamaanisha nini?

MZEITUNI HALISI UTAKAPOPACHIKWA.

Print this post

Vita vya kiroho, na mwamini Mpya.

SEHEMU YA KWANZA: KUELEWA VITA VYA KIROHO

1.1 Vita vya Kiroho ni Nini?

Vita vya kiroho ni mapambano yasiyoonekana kwa macho ya kawaida, yanayofanyika katika ulimwengu wa roho kati ya ufalme wa Mungu na ufalme wa giza (Shetani na mapepo yake).

Ingawa hayaonekani, lakini vita vyao ni vibaya zaidi ya vile vinavyoonekana, kwani vinamuathiri mwanadamu kotekote, mwilini lakini pia rohoni katika mawazo yetu, hisia, tabia, ndoa, huduma, na hata afya.

Biblia inasema:

Waefeso 6:12

Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho

Mfano:

Mtu anayeokoka anaweza ghafla kuanza kupata majaribu makubwa ya kuudhiwa na watenda dhambi, jambo ambalo huko nyuma hakuwahi kuliona, mpaka anawaza kwamba maisha wa wokovu ni magumu. Hili ni shambulio la kiroho, linalolenga kumrudisha nyuma kiroho.

1.2 Kwa Nini Kuna Mapambano?

Ulipompokea Yesu, uliingia katika Ufalme wa Mungu. Na moja kwa moja ulifanyija adui wa Shetani.

Shetani alikupoteza na sasa anafanya kila juhudi kukurudisha, kukuzuia usikue kiroho, au kukushawishi uishi maisha yasiyo ya ushindi.

“Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake.” (Wakolosai 1:13)

 SEHEMU YA PILI: KUMFAHAMU ADUI

2.1 Shetani ni Nani?

Maandiko yanatuambia Shetani alikuwa malaika aliyeasi (Isaya 14:12–15).

Anaendesha vita kwa kutumia uongo, hofu, mashaka, tamaa, magonjwa, migawanyiko, na kushambulia akili zetu.

2.2 Mbinu za Shetani:

Uongo – Anapandikiza mawazo kama: “Hujasamehewa” au “Mungu hajasikia maombi yako.”

Vishawishi – Hutumia tamaa za mwili, pesa, au kiburi kukushawishi.

Kuchosha kiroho – Anakufanya uchoke au kupoteza hamu ya kusoma Biblia au kuomba.

Kuvuruga mahusiano – Kupitia fitina, chuki, au hasira isiyoisha.

“Yeye ni mwongo na baba wa huo.” (Yohana 8:44)

🛡️ SEHEMU YA TATU: SILAHA ZA MUNGU

Waefeso 6:10–18 inatupa silaha saba za kiroho za kujilinda na kushambulia nguvu za giza:

3.1 Kweli kiunoni.

Kuwa na ujuzi wa kweli ya Neno la Mungu na kuiishi.

Hii inasaidia kutambua uongo wa Shetani.

Mfano: Unapofikiri “Mungu hanipendi,” Neno la Mungu linasema “Hakika amekupenda kwa upendo wa milele.” (Yeremia 31:3)

3.2 Dirii ya Haki

Maisha ya uadilifu na kutokubaliana na dhambi.

Haki hii inatoka kwa Yesu, sio kwa matendo yako.

“Yeye asiyemjua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.” (2 Wakorintho 5:21)

3.3 Viatu vya Injili ya Amani (utayari miguuni)

Kuwa tayari kueneza habari njema na kuishi kwa amani.

Mtu aliye tayari kushuhudia haogopi mapambano.

3.4 Ngao ya Imani

Imani huuzima mishale ya hofu, mashaka, na huzuni.

Unaposema, “Mungu atanitetea,” hata wakati hali ni ngumu, hiyo ni imani.

3.5 Chapeo ya Wokovu

Linda mawazo yako kwa kufikiri mambo yanayohusiana na wokovu wako.

Kukumbuka kwamba umeokolewa hukufanya usiyumbishwe na hila za adui.

3.6 Upanga wa Roho (Neno la Mungu)

Neno la Mungu ni silaha ya kushambulia.

Yesu alilitumia aliposhambuliwa na Shetani (Mathayo 4:1–11).

3.7 Maombi

Maombi ni silaha ya nguvu inayoweza kubadilisha hali yoyote.

Omba kwa ajili yako, familia yako, kanisa, na hata waliopotea.

Waefeso 6:18

[18]kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;

🧭 SEHEMU YA NNE: MBINU ZA USHINDI KILA SIKU

Soma Biblia kila siku – Neno la Mungu hukujenga kiroho.

Omba kila siku – Ushindi unapatikana kwa kusali daima.

Kataa dhambi kimaamuzi – Usingojee hisia, fanya uamuzi wa kiroho.

Tembea na Wakristo wengine – Ushirika hukupa nguvu.

Fanya ibada (Sifu na abudu) – Hukuza uwepo wa Mungu na huvunja vifungo vya giza.

Tubu haraka unapokosea – Usimpe shetani nafasi ya kukushitaki.

⚠️ SEHEMU YA TANO: MAMBO YA KUZINGATIA

5.1 Vita vya Kiroho Sio:

Kila shida ni mapepo – Baadhi ya mambo ni matokeo ya maamuzi au mazingira. Hivyo ni wajibu kuchunguza chanzo cha tatizo ni je Adui kweli au!

Kukemea tu– Mamlaka ya kiroho hutegemea maisha ya utii kwa Kristo. Utiifu wako

Kuwa na hofu – Kwamba tuigope, au tuishi kwa mashaka, kana kwamba tuwezekeze nguvu zetu zote kupamba a nayo. Hapana Tuna mamlaka kupitia Yesu.

“Nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge, na kushinda nguvu zote za adui; wala hakuna kitakachowadhuru.” (Luka 10:19)

💬 SEHEMU YA SITA: MANENO YA KUHIMIZA

Ukiwa ndani ya Kristo, huna sababu ya kuogopa. Mapambano yapo, lakini ushindi ni wako kupitia Yesu Kristo.

“Katika mambo haya yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.” (Warumi 8:37)

📖 MISTARI YA KUKARIRI

Waefeso 6:11 – “Vaeni silaha zote za Mungu…”

Yakobo 4:7 – “Mtiini Mungu, mpingeni ibilisi naye atawakimbia.”

2 Wakorintho 10:4 – “Silaha za vita vyetu si za mwili…”

1 Petro 5:8 – “Muwe na kiasi na kukesha… ibilisi yenu… hutafuta mtu wa kummeza.”

Masomo ya ziada kukusaidia kuvishinda vya kiroho

NGUVU YA “KUKATAA” UNAPOPAMBANA VITA VYA KIROHO

Maana ya Mhubiri 9:18 Hekima ndiyo bora kupita silaha za vita;

JINSI YA KUPIGANA MAOMBI YA VITA.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >>

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

BWANA ni mtu wa vita,  BWANA ndilo jina lake.(Kutoka 15:3)

Mishale ya moto ya mwovu inayozungumziwa kwenye Waefeso 6:16 ni ipi?

Nini maana ya huu mstari ” Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda;”?(2Timotheo 4:7)

Print this post

Uinjilisti kama agizo kuu la Bwana.

Kila mwamini ameitwa kuieneza injili ya Yesu Kristo. Ambayo huitwa habari njema.

Mathayo 28:19-20

[19]Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;

[20]na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.

Habari njema ni nini? Ni habari za wokovu kwa mwanadamu, ulioletwa na  kupitia mtu mmoja Yesu Kristo kwa tendo la kufa na kufufuka kwake kaburini.

Kwanini tunapaswa tuwashuhudie wengine habari njema?

1) Ni agizo la Bwana (Mathayo 28:19)

Kama tulivyotangulia kuona hapo juu, kuwa siku Yesu alipoondoka hakutuacha bila wajibu, bali kila mmoja wetu alipewa sehemu ya huduma katika shamba lake. Ya kuenenda ulimwenguni kote kuwafanya watu kuwa wanafunzi wake.

Kazi hii sehemu nyingine anaifananisha na talanta, ambayo amempa kila mwamini na anataka kila mmoja aizalishe (Mathayo 25:14-30), sehemu nyingine anaifananisha na matunda, anasema sisi ni matawi na yeye ni mzabibu  kwamba tumzalie matunda, (Yohana 15:1-7),sehemu nyingine nyingine anaiita posho, huku yeye  akijiita bwana, na sisi mawakili wake, akitutaka tutoe posho kwa wakati kwa watu wake, (Luka 12:42-48)

Sasa ukiangalia utaona sehemu zote hizo tunazofananishwa nazo, kama mtu hajafanya chochote au hajazalisha chochote, haachwi hivi hivi, bali kuna aidha kuondolewa sehemu ya thawabu yake, au kukataliwa kabisa.

Ndio maana ni lazima tujue mwamini yoyote yule, ni lazima aishi maisha ya kuwashuhudia wengine injili.

2) Watu wanapotea bila Kristo.

Warumi 10:14 Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri?

Ni lazima ujue kuwa hukumu ipo na kuzimu pia ipo, na inawameza wengi, Na watu hawawezi kuokoka tu wenyewe hivi hivi bila kusikia injili kama wewe ulivyosikia.  Tengeneza picha unamwona baba yako, au mama yako kwenye ziwa la moto, halafu anakuambia laiti ningelijua ukweli nisingekuwa huku, utajisikiaje? Ukilijua hili basi huruma ya ki-Mungu itakujaa tu ndani yako, na utasukumwa kujitoa kuwaendea wenye dhambi, kama Kristo alivyotujia sisi, kutoka mbinguni, na kama mitume walivyowaendea watu, ili kuhakikisha wanaokoka.

3) Mbingu zinafurahi.

Luka 15:7 Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu

Mungu hufurahi malaika pia hufurahi, wanapoona roho za watu zinaokoka,duniani, Hivyo sisi kama wana wa Mungu ni wajibu wetu kuyatenda yale tu ambayo yanamfanya Baba yetu afurahi, na hilo si lingine zaidi ya kutoka na kwenda kuwashuhudia watu injili.Hapo tunaufanya moyo wa Mungu hufurahi sana.

4) Ushuhuda wa maisha yetu.

Ni ukweli usiopingika kuwa kila mmoja wetu kuna mahali Mungu amemtoa mpaka hapo alipomfikisha, anayo mengi ya kushuhudia kuhusu uzuri wa Kristo.

Wazia yule kichaa ambaye alikuwa katika hali mbaya kule makaburini, uchi, usiku na mchana, ameshindikana kwa vifungo vyote. Lakini Yesu alipokutana naye saa ile ile alipona, akataka kuambatana na Yesu, lakini Yesu akamwambia nenda nyumbani kwa watu wako uwasimulie matendo makuu ambayo Mungu amekutendea, Na tunaona alikwenda kusimulia yote mji ule, na watu wengi wakamwamini Kristo, kwa ushuhuda wake tu.

Marko 5:20 Akaenda zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli, ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu

Hata wewe, wazia uzuri ulioupata pindi ulipompokea Kristo, utamani pia mwingine aupate, na huo ndio upendo, umeonja uzuri wa Kristo unakwenda kuwaambia na wengine mfano tu wa yule mwanamke pale kisimani.

NI Njia zipi za kuhubiri?

i) Kwa kusimulia ushuhuda wa maisha yako, jinsi Yesu alivyokuokoa.

Sawasawa na agizo ambalo Yesu alimwagiza yule mtu ambaye aliteswa Na mapepo akamfungua. (Marko 5:19-20)

ii) Kwa kumkaribisha Kanisani.

Hii ni njia bora, ambayo utapata nguvu ya kikanisa, kwasababu mule akutanapo na vipawa mbalimbali vya Mungu, hurahisisha zaidi moyo wake, kuamini ujumbe uliompelekea.

iii) Kwa Mwenendo mwema wa  rohoni.

Ishi maisha yanayomuhakisi Kristo. Kwasababu matendo yako ni injili kuwa wengine kumgeukia Kristo. (1Petro 3: 1-2)

iv) Kwa kutumia Visaidizi

Hivi Ni kama vitabu, kanda, luninga, na kwa dunia ya sasa, Vitu kama whatsapp, websites,  panaweza pakawa mahali Ambapo injili yetu kupaa sana na kuwavuta wengi ndani ya ufalme. Ulimwengu wa sasa, upo mtandaoni, hivyo tumia fursa hiyo, kushea mafundisho, mahubiri sahihi ya Neno la Mungu kwa marafiki zako, familia, ndugu, majirani, huko huko Mungu ataanza kazi ya wokovu ndani yao.

Namna ya kushinda hofu.

Haya ni mambo ya kukumbuka kila uendapo kushuhudia, ili usishindwe na hofu.

1) Kile uendapo kushuhudia ukumbuke kuwa Roho Mtakatifu ndiye anayetupa nguvu na si kwa uweza wetu tu wenyewe. (Matendo 1:8)

2) Omba kabla ya kwenda kuwashuhudia watu.

3) Anza katika udogo, shuhudia mtu mmoja mmoja, kabla ya kufikia umati wa watu wengi.

4) Pia ukumbuke  jambo la kushawishi ni la Roho Mtakatifu, sisi ni kushuhudia.

Usiwe na hofu ikiwa huoni mwitikio wowote, kwa yule unayemweleza habari ya wokovu, fahamu kuwa ipo mbegu imemwingia ambaye itakuja kumea tu kwa wakati wake.

5)Ongozana na mtendakazi wenzako, au kiongozi wako. 

Uinjilisti wa wawili huwa mrahisi zaidi ya ule wa mmoja (isipokuwa unao uzoefu). Yesu aliwatuma wanafunzi wake wawili wawili, alijua ujasiri utaongezeka lakini wangeweza kufanya zaidi, pale mmoja anapochoka anamtia nguvu mwenzake. Vivyo hivyo na wewe katika hatua za awali ongozana na kiongozi wako, au mshirika mwenza katika kazi ya injili.

Vifungu vya kukariri, ambavyo unapaswa uwe navyo kichwani, katika hatua za kuwashuhudia watu.

Yohana 3:16

Warumi 3:23

Warumi 6:23

Warumi 10:9–10

2 Wakorintho 5:17

Kwa mwongozo wa namna ya kutembea katika baadhi ya vifungu hivyo, pitia hili fundisho >>> NJIA/BARABARA YA WOKOVU NDANI YA KITABU CHA WARUMI.

Mafundisho ya ziada

KWANINI TUNAPASWA KWENDA KUIHUBIRI INJILI KWA UJASIRI WOTE?

IHUBIRI INJILI, KILA MAHALI KWASABABU AKUZAYE NI MUNGU.

HEKIMA NANE(8) ZA KIUINJILISTI, KATIKA KUWAVUA WATU KWA KRISTO.

JE UDHAIFU WANGU UNAWEZA KUZUIA INJILI?

KUTOKUIHUBIRI INJILI,KUNA MADHARA GANI?

KWANINI KILA MWAMINI ANAPASWA AWE MHUBIRI WA INJILI

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Print this post

Baraka ni nini na kuna aina ngapi za baraka?.

Jibu: Baraka ni thawabu ya kipekee itokayo kwa Mungu na kumfikia mtu akiwa hapa duniani.


Baraka yaweza kutokana na matendo mtu aliyoyatenda au maombi aliyoyaomba.

Kwamfano utamwona mtu anayeitwa Yabesi alimwomba Mungu ambariki na Mungu akasikia na kumbariki.

1Nyakati 4:10 “Huyo Yabesi akamlingana Mungu wa Israeli, akisema, Lau kwamba ungenibarikia kweli kweli, na kunizidishia hozi yangu, na mkono wako ungekuwa pamoja nami, nawe ungenilinda na uovu, ili usiwe kwa huzuni yangu! Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba”

Baraka za MUNGU zimegawanyika katika makundi makuu mawili;

  1. BARAKA ZA ROHONI.

Hizi ni baraka zinazoinufaisha roho ya mtu na ndizo zenye umuhimu sana kuliko zile nyingine.

Baraka ya kwanza ya rohoni ni “WOKOVU”. Mtu aliyepata Neema ya kumwamini YESU na kuoshwa dhambi zake huyo amebarikiwa, kwasababu anao uzima wa milele.

Waefeso 1:3 “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa BARAKA ZOTE ZA ROHONI, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo”.

Baraka ya rohoni inazaa Furaha, amani, utulivu na utakatifu kwa ujumla.

Watu waliobarikiwa rohoni hata wakose vyote vya mwilini bado wanaishi maisha ya raha, kwasababu roho zao zimebarikiwa kuwa ndani ya YESU ambaye kila kitu.

  2. BARAKA ZA MWILINI.

Baraka za mwilini ni vyote ambavyo mtu anavipokea kutoka kwa MUNGU vyenye manufaa ya mwili, ikiwemo afya, cheo, uzao au mali.

Mfano wa watu waliobarikiwa kwa baraka za mwilini ni Sulemani, alipewa utajiri mkubwa hata baada yake hakukuwa na mtu kama yeye,

Na wengine kwenye Biblia agano la kale ni Abramu na Ayubu hawa walibarikiwa vingi na MUNGU.

Lea naye alibarikiwa kuwa na watoto wengi, Samsoni alibariwa nguvu za mwilini n.k

Katika Agano jipya walikuwepo akina Yusufu wa Arimathaya, (Mathayo 27:57), na wanawake si haba, akina Yoana, Suzana na wengine wengi (Luka 8:3).

Na waliobarikiwa kwa vyeo, waliomwamini Bwana YESU walikuwa wengi sana wanaume na wanawake (soma Matendo 17:12-14).

Na kubarikiwa mwilini kunaweza kuwa ishara ya kubarikiwa pia rohoni, lakini sio ishara pekee kwasababu wapo matajiri wasiomwamini YESU na walikuwepo matajiri kabla ya Bwana YESU,

Na watakuwepo matajiri wengi katika ziwa la moto (Soma Luka 16:20-34).

Na tena Bwana Yesu alisema itamfaidia nini mtu apate kila kitu halafu apate hasara ya nafsi yake (Marko 8:34).

Na pia wapo maskini ambao hawajabarikiwa baraka za mwilini lakini wamebarikiwa mambo ya rohoni..

Yakobo 2:5 “Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao?”.

Kwahiyo tukiwa wote ndani ya Kristo, hatupaswi kudharauliana kwa hali zetu, bali tunapaswa tuhudumiane kwa viwango vya baraka tulivyobarikiwa..

kwasababu yule unayemwona ni maskini wa vya mwilini huenda ni tajiri wa vya rohoni sana, ndivyo Neno la Mungu linavyosema..

Ufunuo 2:9 “Naijua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri)…”

Na yule unayemwona hana vya rohoni kama ulivyo navyo wewe basi amebarikiwa vya mwilini, ambavyo kupitia hivyo vinahitajika kwaajili ya injili, ili mambo yote yakae katika uwiano na wote tuheshimiane.

Na pia inawezekeana mtu akabarikiwa kwa vyote vya rohoni na mwilini, kwa mapenzi ya MUNGU, lakini haiwezekani mtu aliyemwamini YESU akakosa vyote..

Ikitokea dalili ya kukosa vyote basi kuna kasoro katika imani, hivyo mtu huyo anapaswa aangalie jinsi alivyosikia na anavyoenenda.

Je umempokea YESU?..huo uchungu na hofu na wasiwasi ni ishara ya kupungukiwa baraka za rohoni.

Leo hii mpokee YESU ili uanze kula matunda ya baraka za rohoni.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MAOMBI YA YABESI.

Fahamu maana ya Mithali 28:20 Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele;

KILA MTU NA AMCHE BABA YAKE NA MAMA YAKE.

MUNGU HANA MBARAKA MMOJA TU!..MWAMINI.

TAFUTA UZIMA WA MILELE NA SI UZIMA TU!.

Print this post

Ipi tofuati ya Andiko na Neno.

Swali: Huwa tunasema.. “tusome maandiko” na wakati mwingine “tusome Neno”..ipi tofauti ya maneno haya mawili?.


Jibu: Tuanze na Neno au Neno la Mungu.

“Neno” ni sauti ya MUNGU yenye ujumbe inayokuja kwa mtu kwa  njia ya maono au ndoto au njozi..

Kwamfano katika biblia utaona lugha iliyotumika kwa manabii wote waliojiliwa na sauti ya Mungu iliyobeba ujumbe ni hiyo ya “Neno la Mungu”

Mwanzo 15:1 “Baada ya mambo hayo NENO LA BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.

Soma pia  1Wafalme 17:8, Isaya 38:4, Yeremia 1:11, Ezekieli 1:3, Ezekieli 12:21, Hosea 1:1, Yona 1:1, Mika 1:1, Sefania 1:1 n.k 

Hata sisi wakati mwingine tunapotaka kuzungumza na mtu, tunaweza kutumia lugha hiyo kwa kumwambia “nina neno nataka kusema nawe”… au kama kuna mtu amekuambia jambo unaweza kusema “mtu Fulani kaniambia neno”.. kwahiyo ni hivyo hivyo hata katika biblia, Neno la Mungu ni sauti ya MUNGU.

Sasa kama “Neno” tafsiri yake ndio hiyo, vipi kuhusu “Andiko”?

Andiko ni Neno la Mungu lililo katika maandishi… Kwamfano; hilo Neno lililomjia Abramu, kwake yeye ni Neno la Mungu lakini kwetu sisi ni andiko, ndio maana tunalisoma.. Na Nguvu ya andiko na Neno ni ile ile.

Hivyo maneno ya Mungu yote yaliyoandikwa katika Biblia ni “MAANDIKO”.. Hata wewe maneno yako unayoyasema unaweza kuyaandika katika kitabu, na yakawa ni maandiko kwasababu ni maneno yaliyoandikwa.. Hali kadhalika, kila Neno la Mungu kwenye Biblia ni andiko.

Hivyo mtu anayesema “tusome maandiko” na Yule anayesema “tusome Neno la Mungu” ni kitu kimoja.. na nguvu ni ile ile..

Na kila Andiko lenye pumzi ya Mungu linafaa kwa mafundisho, kuonya, kuongoza na kuadibisha..

2Timotheo 3:16 “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki;

17 ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema”

Kwa urefu kuhusiana na kazi ya MAANDIKO inayofanya kwa mtu fungua hapa >>MAMBO MANNE(4) YAFANYAYO NENO LA MUNGU.

Je umempokea YESU?, Umebatizwa katika ubatizo sahihi?..una uhakika Bwana YESU akirudi unaenda naye?.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

EPUKA KUJIFANYA HUJUI.

MANENO YA MUNGU YANAPINDULIWAJE?

TUUTAZAME PIA MWISHO WA UJENZI WETU.

ZIFAHAMU KARAMA 9 ZA ROHO MTAKATIFU NA UTENDAJI KAZI WAKE.

NI NANI TUNAPASWA TUMWONE ZAIDI KILA TUSOMAPO BIBLIA?

Print this post

Simoni Mkirene aliubeba msalaba wa Bwana Yesu au la?

Swali: Katika  Mathayo 27:31-32 tunasoma kuwa Simoni Mkirene alimsaidia Bwana kuubeba msalaba wakati anaelekea mahali pa kusulibishwa, lakini tukirudi katika Yohana 19:17-18 tunasoma kuwa hakusaidiwa na mtu badala yake aliubeba mwenyewe mpaka Golgotha, je mwandishi yupi yupo sahihi?.

Jibu: Turejee mistari hiyo..

Mathayo 27:31 “Hata walipokuwa wakitoka, wakamwona mtu Mkirene, jina lake Simoni; huyu wakamshurutisha auchukue msalaba wake.

33 Na walipofika mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa”

Hapa ni kweli Simoni Mkirene alimsaidia Bwana kuubeba msalaba..

Lakini hebu tusome tena Yohana 19:17-18..

Yohana 19:16 “Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea Yesu.

17 Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha.

18 Wakamsulibisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati”.

Hapa inaonyesha ni kama hakusaidiwa na mtu mpaka alipofika Golgotha..

Je kwa mantiki hiyo biblia inajichanganya?…

Jibu ni La! Biblia ni kitabu kisicho na makosa wala mkanganyiko mahali popote, isipokuwa fahamu zetu na pambanuzi zetu ndizo zinazojichanganya.

Sasa tukirejea katika habari hizo mbili, ni kwamba Mwandishi wa kitabu cha Yohana (ambaye ni Yohana mwenyewe) alijaribu kueleza safari ya Bwana kwenda Golgotha kwa ujumla, bila kuhusisha matukio madogo madogo yaliyokuwa yanatokea njiani.

Kwamfano utaona yeye kasema tu Bwana alijichukulia msalaba wake mpaka Golgotha, pasipo kutaja matukio kama ya kutemewa mate njiani, au wale wanawake kumlilia na Bwana kuwajibu kwamba wajililie nafsi zao na watoto wao (Luka 13:26-28).. Sasa matukio kama haya Yohana hajayataja lakini haimaanishi kuwa amesema hayapo, la! Bali ni kwamba kafupisha tu habari.. hata wewe/mimi tunaweza kuelezea jambo kwa urefu au ufupi kutegemea na mapenzi yetu.

Lakini sasa tukirudi kwa Mathayo yeye kataja safari ya Bwana kwa urefu kidogo, akihusisha matukio madogo madogo yaliyokuwa yanaendelea njiani katika safari yake..na mojawapo ya tukio ndio hilo la Simoni Mkirene aliyekuwa anatokea shamba na akashurutishwa kuubeba msalaba wa Bwana YESU.

Na utaona pia ijapokuwa Mathayo alirekodi tukio la Simoni Mkirene kumsaidia Bwana msalaba, lakini pia hakutaja tukio la wanawake waliomlilia Bwana njiani, ambapo tukio hilo linakuja kutajwa na mwandishi mwingine wa kitabu kingine ambaye ni Luka..

Luka 23:26 “Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shamba, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu.

27 Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea.

28 Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu.

29 Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha”.

Umeona kwahiyo habari ya Bwana YESU kujichukulia msalaba mpaka Golgotha kama ilivyoandikwa na Yohana haipingani na ile iliyoandikwa na Luka, Mathayo au Marko.. kinachotofautisha habari hizo ni kwamba moja imeandikwa kwa urefu nyingine kwa ufupi.

Je umempokea YESU, je umeubeba msalaba wako na kumfuata?.. Je unajua ni kwanini Simoni Mkirene aliruhusiwa kubeba msalaba nyuma ya YESU?.. ni ufunuo kuwa tukitaka kumfuata YESU ni lazima tubebe msalaba tumfuate YESU nyuma.

Marko 8:34 “Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate.

35 Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha”.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MANENO SABA YA YESU MSALABANI.

YESU MNAZARETI,  ANWANI YA MSALABA.

MSALABA NI ZANA YA UJENZI WA MAISHA YAKO.

Je! Bwana Yesu alisulubiwa juu ya msalaba au juu ya mti uliokuwa wima?

Kwanini Bwana Yesu alisema pale msalabani naona kiu?

Print this post

Chakula kigumu mfano wake ni upi kama tunavyosoma katika Waebrania 5:12?

SWALI: Biblia inasema maziwa ni kwa watoto wachanga, lakini chakula kigumu ni cha watu wazima. Mfano wa chakula hichi kigumu ni kipi?

Waebrania 5:12 Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. 13 Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. 14 Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya

JIBU:

Kabla ya kufahamu hicho chakula kigumu, ni vema kujua kwanza maziwa ni yapi.

Hivyo ukiendelea kusoma  vifungu vinavyofuata anasema..

Waebrania 6:1 Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu, 2 na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele. 3 Na hayo tutafanya Mungu akitujalia.

Sasa hayo mafundisho ya kwanza ya Kristo ndio maziwa. Yaani Mafundisho ya toba, imani kwa Mungu, ubatizo, kuwekewa mikono, kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele ni mafundisho ya watoto wachanga..kiroho hujulikana kama maziwa..

Kimsingi mtoto akiendelea kunywa maziwa tu peke yake daima, kitakachotokea baadaye ni kudumaa kama sio kufa kabisa, hivyo itafika wakati tu atahitaji chakula kingine ili aendelee kuishi. Vivyo hivyo na sisi, vipo vyakula ambavyo tunapaswa tule, kwa jinsi tunavyoendelea kukua kiroho.

Vifuavyo ndio vyakula vigumu vya kiroho vya watu wazima:

1) Upendo kwa maadui

Mathayo 5:44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,

Kwanini ni chakula kigumu?. Kwasababu jambo hilo linaenda kinyume na asili ya mwanadamu, linafunua asili ya ndani kabisa ya Kristo, ambayo si rahisi mtu aliyemchanga kiroho, kuielewa, au kulipokea nyakati za mwanzoni, yaani kumwombea  na kumpenda Yule ambaye anaiwinda roho yake au aliyemjeruhi, ..

2) Makusudi ya Mungu katika mateso

Wafilipi  1:29 Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake;

Kwanini ni chakula kigumu?. Kwasababu mwamini mchanga, mara nyingi atapenda kuambiwa maneno ya faraja, baraka, na mafanikio, awapo kwa Kristo,  lakini mkristo aliyekomaa, anayaona mapenzi ya Mungu pia hata katika majaribu na kuyashangalia.

1Wathesalonike 3:3 mtu asifadhaishwe na dhiki hizi; maana ninyi wenyewe mnajua ya kuwa twawekewa hizo

Soma pia 1Petro 1:6-8, 4:13, Wakolosai 1:24, Luka 6:22-23

3) Upambanuzi wa kiroho

Waebrania 5:14 Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya

Mkristo aliyekomaa kiroho, anafundishwa na Mungu kutambua na kugawanya vema mambo yote, kujua vilivyo najisi na visivyo najisi, mafundisho ya kweli na yale ya uongo, anafundishwa, busara, ujuzi na hekima hata katika kuhubiri injili kwa makundi yote, bila kuanguka na kunajisika, kwasababu amepewa roho ya upambanuzi ambayo huja kwa kuzoeshwa na Mungu kwa kipindi Fulani cha muda kupitia  Neno lake.

1Wakorintho 9:20 Nalikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi; kwa wale walio chini ya sheria, nalikuwa kama chini ya sheria, (ingawa mimi mwenyewe si chini ya sheria), ili niwapate walio chini ya sheria.

21 Kwa wale wasio na sheria nalikuwa kama sina sheria, (si kwamba sina sheria mbele za Mungu, bali mwenye sheria mbele za Kristo), ili niwapate hao wasio na sheria. 22 Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu.

Soma pia, 1Wakorintho 8:6-13, Yohana 2:1-12, Mathayo 11:19.

Kwanini ni chakula kigumu? Kwasababu mtu ambaye ni mchanga kiroho, akijihusisha katika viwango hivyo, hupotea na kunajisika kama sio kupotea kabisa. Ndicho kilichowatokea Adamu na Hawa kuuvamia mtu wa ujuzi wa mema na mabaya nje ya ratiba ya Mungu, matokeo yake wakayavuna mabaya, wala sio mema.

4) Kuikubali Fimbo ya Mungu.

Katika wokovu ipo fimbo ya Mungu; Mzazi yoyote huwa hatoi zawadi tu, sikuzote, hacheki na mwanawe siku zote, lakini pia kuna wakati fimbo hutumika, Vivyo hivyo Mungu ni Baba yetu, huadhibu, pale tunapokosea..

Waebrania 12:11 Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani.

Kwanini ni kigumu? Kukubali marekebisho kwa kuadhibiwa kama sehemu ya kutengenezwa na Mungu, si jambo rahisi mtu kulikubali mkristo ambaye hajakomaa. Yeye atakachojua tu, kuwa Mungu ni upendo.

5) Kujikana na kuubeba msalaba.

Luka 9:23 Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.

Kwanini ni chakula kigumu? Aliye mchanga kiroho kukubali kukataa mapenzi , kuingia gharama kuacha vyote na kuyakubali ya Mungu tu, si jambo rahisi kwa mwanafunzi wa ngazi ya chini.

6) Unyenyekevu na kujitoa kwa wengine.

Wafilipi 2:3 Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.

4 Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.

5 Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;

6 ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;

7 bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;

8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba

Kwanini ni chakula kigumu?.

Mkristo mchanga kiroho, si rahisi kuangalia mambo ya wengine, mfano wa Kristo, si rahisi kujinyenyekeza na kukubali kutembea kama mtumwa ili kuwatumikia wengine.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Print this post