Shalom, karibu tujifunze Biblia.
Katika kitabu cha Mwanzo tunasoma kuhusu uumbaji..Tunasoma Mungu alimwumba Mtu kutoka katika mavumbi ya nchi, lakini Zaidi ya hayo tunaona aliumba na vitu vingine vinavyoonekana kama miti, Wanyama, samaki n.k.
Sasa kama umekisoma vizuri kitabu hicho utagundua kuwa vimetajwa tu vitu na viumbe vinavyoonekana kwa macho, lakini vile visivyoonekana kwa macho havijatajwa. Kwamfano hutaona viumbe kama bakteria wametajwa hapo katika uumbaji..ingawa ni wengi kuliko idadi ya viumbe vyote vinavyoonekana kwa macho, na tena kuna aina nyingi za bakteria na virusi, hutaona pia Mungu kazitaja chembe chembe hai za damu zilizopo ndani ya mwili wa Adamu zinazoishi ndani yake na kumlinda dhidi ya maadui wa mwili wake..hali kadhalika utaona Mungu kataja mavumbi katika kitabu cha mwanzo…lakini hajataja elementi nyingine zilizo ndogo sana na nyingi kuliko mavumbi yote ya dunia na mchanga zinazoitwa protoni na elektoni, zilizopo ndani ya huo mchanga na ndani ya kila kitu.
Kwahiyo hiyo ina maana kuwa Uumbaji wa Mungu sio tu huu wa vitu tunavyoviona kwa macho, bali pia kuna vitu na viumbe vingine vingi visivyoonekana kwa macho ambavyo Mungu kaviumba pia vinavyoishi katikati yetu..Hii tunayoiona ni kama tu “summary” ya vitu vilivyoumbwa.
Na kama umegundua matatizo mengi na mafanikio mengi yanatokana na hivi vitu tusivyoviona…Kwamfano matatizo ya magonjwa yote ni kutokana na hawa bakteria au virusi. Hawaonekani lakini wanaweza kusababisha madhara makubwa, hata kifo, virusi vya korona havionekani kwa macho lakini leo hii vinausumbua ulimwengu.
Vivyo hivyo mafanikio mengi yanatokana na vitu visivyoonekana..kwamfano unaweza kushangaa inawezekanikaje kioo chenye waya waya tu kinaweza kuonyesha sura ya mtu na matukio yake..(kumbe ukifuatilia nyuma yake ni hivyo vitu vidogo sana visivyoonekana protoni na elecroni vinatumika), na umeme ni hivyo hivyo, unajiuliza ule waya mwembamba vile unawezaje kupitisha nguvu kubwa vile ya kuwezesha mashine kusukuma vyuma Na hata kusaga nafaka na kuzifanya unga, au unawezaje kupitisha moto mwingi kiasi kile cha kuchemsha maji kwa dakika tano na yakatokota kabisa. Kumbe nguvu ile inatokana na sayansi ya vitu visivyoonekana (protoni na electroni).
Kwa mantiki hiyo basi, hakuna sababu za kusema kwamba shetani hayupo kwasababu tu hatumwoni, au hakuna sababu ya kusema kwamba mapepo hayapo kwasababu hatuyaoni kwa macho, wala hatuna sababu za kusema kwamba Malaika hawapo..kwasababu tu hatuwaoni.
Matukio mengi yanayoendelea sasa duniani, yanaanzia rohoni. Hata hii dunia tu yenyewe imeumbwa kutoka katika vitu visivyoonekana..kasome Waebrania 11:3.
Kwahiyo vitu vile visivyoonekana ndio vya kuvizingatia Zaidi kuliko vile vinavyoonekana.
2Wakorintho 4:18 “tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele”.
Na pia vipo vitu vingine ambavyo hata kwa kutumia hizo hadubini havionekani lakini vipo..na tunaamini kuwa vipo..Kwamfano Ile “nguvu ya uvutano ya sumaki” haionekani kwa njia yoyote ile. Mpaka leo hakuna mtu wala mwanasayansi aliyegundua kifaa cha kuiona..Imebakia fumbo mpaka leo.
Vivyo hivyo ndugu, ulimwengu wa roho upo, huo hauonekani kwa macho, vipo viumbe vya rohoni pia navyo havionekani kwa macho, lakini madhara yake ni makubwa katika Maisha yetu.
Kama unakiogopa kirusi cha ukimwi usichokiona kisiingie mwilini mwako kwa kujitenga na uasherati.. Basi kuna viumbe vingine vibaya kuliko hivyo virusi ambavyo vinaweza kuingia mwilini mwako kwa njia hiyo hiyo ya uasherati,(mapepo) vitakavyokuletea madhara kwenye Maisha yako moja kwa moja. Pepo mmoja tu anayeweza kuingia katika Maisha yako kwa njia ya tendo moja tu la uasherati na ana uwezo wa kukuharibia Maisha yako moja kwa moja.
Kama unaogopa kupigwa shoti usiyoiona kwa kushika nyaya za umeme bila uangalifu, basi iogope dhambi kwasababu vipo vitu katika ulimwengu wa roho vibaya kuliko kuliko umeme.. ambavyo havionekani, vyenye uwezo wa kukusababishia hata kupoteza Maisha yako ghafla utakapovisogelea tu.
Biblia ndio “hadubini yetu”. Unaposoma Neno ni rahisi kuzigundua roho hizi na jinsi zinavyotenda kazi..na namna ya kujihadhari nazo. Kwamfano biblia inasema katika Mithali…
Mithali 6:32 “Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake”
Hivyo mtu akilijua hili Neno na akaenda kinyume nalo, anakuwa amefungua mlango wa mapepo kuingia katika Maisha yake.. hataona kwa macho, lakini baada ya kipindi Fulani kupita ndipo atakapoona madhara yake. Madhara ya uasherati wengi wanafikiri ni yale ya kupata HIV tu basi!.. lakini hawajui kuwa mtu anaweza kutoka kufanya usherati leo na akaanguka ghafla tu na kupoteza Maisha, au akafa tu ghafla kifo kisichoeleweka, au akapata ajali au akapoteza tu ghafla kitu cha muhimu katika Maisha yake kama kazi, au heshima.
Bwana atusaidie kuyajua Zaidi mambo ya rohoni kuliko ya mwilini, na kutupa Imani Zaidi.. Nasema hivyo kwasababu siku chache tu nyuma nimekutana na pepo, kwa macho haya ya mwilini barabarani, ndipo Mungu akanipa somo kuwa hizi roho zinazurura huku duniani kutafuta watu kwa nguvu kuwaangamiza, na yanaongeza bidii siku hizi za mwisho kwasababu yanajua muda wao ni mchache, hivyo wanawinda watu kwa nguvu, ili kuwaangamiza.
Hivyo kuwa makini sana. Mambo rohoni sio kama unavyoyasikia. Ingia ndani ya Kristo uwe salama.
Maran Atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
KITABU CHA UZIMA
MAFUNDISHO YA MASHETANI
MIHURI SABA
MTUMAINIE YESU ASIYEISHA MATUKIO.
UFUNUO: Mlango wa 6
Rudi Nyumbani:
Print this post