NI SAHIHI KABISA, HUU SI WAKATI WA TINI!

NI SAHIHI KABISA, HUU SI WAKATI WA TINI!

Katika ukristo ogopa sana ile kauli ya kusema “Huu si wakati”… “Bado kidogo”…. “Wakati wake utafika tu siku moja”… Ogopa sana kauli kama hizo, tena ziogope kuliko  ukoma.

Kwanini ninakuambia hivyo? Ni kwasababu wakati ambapo unafikiria majira yake bado, huo ndio wakati Kristo anatazamia kuona matunda kwako. Jambo ambalo ni kinyume kabisa na asili. Hana tabia ya kutafuta matunda wakati wa msimu. Haongozwi na misimu.

Embu kitafakari vizuri kitendo alichokifanya siku ile alipokuwa anakwenda Yerusalemu kutokea Bethania, alipokutana na ule mtini njiani, alifanya nini!. Utaona alikwenda moja kwa moja na kutafuta matunda juu yake, Na alipokosa akaulaani na kunyauka saa ile ile , pasipo kujali kuwa ule haukuwa hata msimu wake wa kuzaa..

Marko 11:12 “Hata asubuhi yake walipotoka Bethania aliona njaa.

13 Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; MAANA SI WAKATI WA TINI.

14 Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia”.

Hili ni jambo ambalo watu wengi hawalifahamu, wanapoangalia mazingira Fulani, wanaona kama vile wakati wake bado, pale mtu unapomuambia biblia inasema “saa ya wokovu ni sasa, na wakati uliokubalika kuokoka ni leo (2Wakorintho 6:2 )” yeye atasema, ngoja kwanza, siku moja nitaokoka tu!, ngoja nimalize chuo, ngoja nioe kwanza, ngoja nipate kazi, ngoja nitoke kwanza kwa wazazi wangu..Ngoja nijenge nyumba yangu kwanza..

Huku akitazamia kweli siku moja akishavipata hivyo vitu  ndio atatulia afikirie sasa kumtumikia Mungu. Lakini hajui wakati amekaa akiungojea huo wakati  ufike Kristo anatokea ghafla kwenye maisha yake, kutafuta matunda, anayakosa, hatua inayofuata kwake ni KULAANIWA MILELE.

Maana yake ni kuwa kamwe asahau WOKOVU katika maisha yako, na ndio maana watu kama hao ambao wana tabia ya kusubiri, subiri, kujivuta vuta, mwisho wa siku unawakuta mpaka wanakufa hawajaokoka haijalishi kuwa wameshapata kila kitu. Sio kwamba kulikuwa na ugumu wowote. Hapana lakini kwasababu walishalaaniwa na Yesu tangu zamani, walipotazamiwa wamzalie Kristo matunda wakashindwa.

Hivyo ndugu, tambua kuwa jicho lako sio jicho la Yesu. Wewe unatazama misimu, Yesu hajui msimu. Wewe unatazama nyakati, Kristo hajui nyakati. Wakati wowote anataka ajapo akukute, ukiwa na matunda. Akukute unamzalia matunda ya Roho. Lakini ukiwa ni mtu wa kusubiria siku Fulani ifike ndio ufanye maamuzi. Upo katika hatari kubwa sana ya kulaaniwa.

Wana wa Israeli, kuna wakati nao pia walijibunia utaratibu kama huo, wakati ambapo Mungu alishawapa tamko la kwenda kumjengea nyumba, Lakini walipopokea vitisho kutoka kwa mfalme aliyefuata kwamba waache ujenzi, wao nao wakasikiliza sauti yake kweli wakaacha. Ukisoma pale utagundua kuwa Kilichofuata ni Mungu kuwalaani, akawapiga kwa umaskini na shida zisizokuwa za kawaida. Mpaka siku walipogundua kosa lao, na kwenda kumjengea tena Mungu nyumba, walijutia mawazo yao.

Hagai 1:2 “Bwana wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Watu hawa husema, Huu sio wakati utupasao kuja, huu sio wakati wa kujenga nyumba ya Bwana.

3 Ndipo neno la Bwana lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema,

4 Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika”?

Leo hii, mtu akishazuiwa na wazazi wake, au boss wake, au mume wake, basi hiyo ndio inakuwa tiketi ya yeye kuukimbia kabisa wokovu au utumishi wa Mungu, akijitetea kuwa pengine haukuwa wakati sahihi na ndio maana vikwazo kama hivyo vimetokea. Nataka nikuambie, ondoa hayo mawazo kuanzia leo, kwasababu hata kwa Yesu hayapo, utalaaniwa.

Upokee wokovu leo, tubu dhambi zako leo, kuwa tayari kubatizwa katika ubatizo sahihi  leo, anza kuishi maisha matakatifu yampendezayo Mungu, bila kujali mazingira, watu, hali, au msimu,..Na baada ya hapo yeye mwenyewe atakupokea na kukujalia kuzaa matunda wakati huu huu, unaoonekana kama haufai kwako.

Kumbuka hizi ni siku za mwisho, wakati wa mavuno umekaribia sana, dalili zote zinaonyesha kizazi chetu tunachoishi kitashuhudia tukio halisi la kurudi kwa Bwana Yesu duniani mara ya pili, kulinyakua kanisa lake. Jiulize Ikiwa atarudi leo usiku utakuwa na lipi la kujitetea, ikiwa hukumpa maisha yako? Au ukifa leo utamweleza nini huko uendako kama Yesu si mwokozi wa maisha yako.

Usizifiche dhambi zako, ikiwa upo tayari kuokoka leo, basi uamuzi huo utakuwa ni wa busara sana kwako. Basi popote pale kama utahitaji msaada huo wasiliana nasi kwa namba hizo hapo chini, au tafuta kanisa la kiroho lililo karibu na wewe, wakusaidie kupokea wokovu.

Kisha hakikisha unatafuta ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwenye maji mengi, na kwa jina la YESU KRISTO (Zingatia sana hilo), kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako. Na yeye mwenyewe atakupa kipawa cha Roho Mtakatifu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita..

AINA TATU ZA WAKRISTO.

UFUNUO: Mlango wa 22

JE UNAYAFANYA MAPENZI YA MUNGU?

Mlima wa Mizeituni  unaumuhimu gani kwetu?

VAZI LA YESU HALIGAWANYWI.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments