Kombeo ni nini? Teo ni nini katika biblia?

Kombeo ni nini? Teo ni nini katika biblia?

Kombeo ndio hiyo hiyo teo,  ni moja ya silaha ya kurusha iliyotumika zamani katika vita.

Kombeo/teo ilitengenezwa kwa Ngozi au Kamba, na jiwe lilikuwa likiwekwa katikati yake na kurushwa kumwelekea adui. Kwa ulimwengu wa sasa Silaha ya manati ndio inayotumika kama mbadala ya teo.

Hivi ni vifungu ambavyo utakutana na neno hilo;

Waamuzi 20:16 “Katika watu hao wote walikuwako watu waume mia saba waliochaguliwa, wenye shoto; kila mmoja alikuwa anaweza kuutupia unywele mawe kwa teo, wala asikose”.

Maana yake ni kuwa jeshi la Benyamini, lilikuwa na watu mia saba ambao wakuwa na shabaha ya hali ya juu sana ya kuweza kurusha mawe kwa kombeo/teo bila kukosea.. Biblia imetumia mfano wa ‘kulengwa kwa unywele’, jinsi ulivyo mdogo, kuonyesha kiwango cha shabaha cha hawa watu kilivyokuwa cha juu sana.

Utasoma pia andiko hilo katika vifungu hivi;

1Nyakati 12:2 “Walikuwa wenye kupinda upinde, nao walikuwa hodari wa kutumia mkono wa kuume na wa kushoto, kwa kutupa mawe ya teo, na kwa kupiga mishale ya upinde; walikuwa wa nduguze Sauli, wa Benyamini”.

2Wafalme 3:25 “Wakaibomoa ile miji; wakatupa katika kila mahali palipo pema kila mtu jiwe lake, wakapajaza; wakaziziba chemchemi zote za maji, wakaikata miti yote iliyo mizuri; mpaka katika Kir-haresethi tu wakayasaza mawe yake; ila wenye kombeo wakauzunguka wakaupiga”.

Kombeo ni nini? Teo ni nini katika biblia?

Lakini pia katika biblia tunaona, hii ilikuwa ni silaha maarufu aliyoitumia Daudi kumwangusha adui yake Goliathi..

1Samweli 17:40 “Akaichukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe laini matano katika kijito cha maji, akayatia katika mfuko wa kichungaji aliokuwa nao, maana ni mkoba wake, na kombeo lake alikuwa nalo mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti…

49 Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi”.

Silaha hii inafunua nini rohoni?

Tunaona Daudi alipopewa, mikuki, na mapanga, na mishale, Silaha zenye ufanisi wa hali ya juu wa kivita, yeye hakutaka, bali alichagua kombeo lake na mawe matano. Alikubali kutumia silaha dhaifu, ili tumaini lake lisiwe katika silaha alizonazo bali katika Bwana ndio maana akasema..

1Samweli 17:45 Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. 46 Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli.

47 Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi mwetu.

48 Ikawa, hapo Mfilisti alipojiinua, akaenda akamkaribia Daudi, ndipo Daudi naye akapiga mbio, akalikimbilia jeshi ili akutane na yule Mfilisti.

Hata sasa, hatupaswi kutegemea nguvu zetu, kushindana au kupambana na hali au majaribu mazito yanayotukabili mbele yetu.. Wengi wakiona hali imekuwa ngumu, wanachowaza ni moja kwa moja kutafuta  fedha nyingi ili waweza kukabiliana na shida zao, ndugu ni heri umtegemee Bwana, amini katika  hicho hicho kidogo ulichonacho, kwamba Bwana anaweza kukitumia hicho kukupa ushindi mkuu.

Mwingine atakuambia ukikosa elimu, hutoweza kufanikiwa, au kumtumikia Mungu. Ni kweli elimu ni nyenzo nzuri ya kukufikisha mahali Fulani pazuri, lakini isipokuwa na Mungu nyuma yake ni bure. Wewe usiyekuwa na elimu ya kutosha ukimtumikia Bwana kwa uaminifu, utafanikiwa hata Zaidi ya wale wenye elimu kubwa.

Kombeo  hilo Bwana alilokupa lielekeze tu kwa Bwana, na yeye mwenyewe atakuonyesha maajabu.

Zaburi 20:7 “Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja jina la Bwana, Mungu wetu”.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Kigao ni nini? Na Je kinafunua nini kwa agano jipya?

Nini maana ya Dirii, Chapeo na Utayari?

Kibanzi na Boriti ni nini kama tunavyosoma kwenye biblia?

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

TUZIDI KUWA HODARI KATIKA BWANA.

SIFONGO NA SIKI NI NINI?

Jehanamu ni nini?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Jacob Kazungu
Jacob Kazungu
1 year ago

Amen hakika nimebarikiwa

Lucas mhula
Lucas mhula
1 year ago

Amina