Waliouawa Shitimu kwa pigo walikuwa ni watu Elfu 23 au elfu 24?.

Waliouawa Shitimu kwa pigo walikuwa ni watu Elfu 23 au elfu 24?.

Swali: Napenda kujua je!, idadi ya Wana wa Israeli waliouawa kwa pigo kule Shitimu ilikuwa ni Elfu 23 au elfu 24?..maana sehemu moja tunaona biblia inataja watu elfu 23 (1Wakorintho 10:8) na sehemu nyingine Elfu 24, (Hesabu 25:9) je biblia inajichanganya?.

Jibu: Biblia haijichanganyi sehemu yoyote kwasababu sio kitabu cha Uongo, bali ni kitabu kilichojaa maneno ya uzima wa Mungu, na ya kweli.

Sasa ili tuielewe vizuri tuisome habari yenyewe kuanzia ule mstari wa kwanza wa kitabu hicho cha Hesabu 25

Hesabu 25:1 “Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu; 2 kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao.

3 Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za Bwana zikawaka juu ya Israeli.

4 Kisha Bwana akamwambia Musa, Watwae wakuu wote wa hao watu, ukamtungikie Bwana watu hao mbele ya jua, ili kwamba hizo hasira kali za Bwana ziwaondokee Israeli.

5 Basi Musa akawaambia waamuzi wa Israeli, Waueni kila mtu watu wake waliojiungamanisha na Baal peori.

6 Na tazama, mtu mmoja miongoni mwa wana wa Israeli akaja na kuwaletea nduguze mwanamke Mmidiani mbele ya macho ya Musa, na mbele ya macho ya mkutano wote wa wana wa Israeli, hapo walipokuwa walia mbele ya mlango wa hema ya kukutania.

7 Naye Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, alipoona jambo hilo, akaondoka hapo katikati ya mkutano, akashika fumo mkononi mwake;

8 akamwandama huyo mtu wa Israeli na kuingia ndani ya hema nyuma yake, naye akawachoma wote wawili kwa fumo lake, yule mume wa Israeli na huyo mwanamke kati ya tumbo lake. Basi pigo likazuiwa kwao wana wa Israeli.

9 Nao waliokufa kwa hilo pigo walikuwa WATU ELFU ISHIRINI NA NNE HESABU YAO

Hapa tunaona ni watu elfu 24 waliokufa kwa pigo hilo… lakini tunaona idadi nyingine tofauti ikitajwa katika kitabu cha Waraka kwa wakorintho.

1Wakorintho 10:8  “Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, WAKAANGUKA SIKU MOJA WATU ISHIRINI NA TATU ELFU”.

Sasa je! Biblia inajichanganya? Jibu ni La!

Ukweli ni kwamba idadi ya waliokufa kwa pigo ni watu elfu 24 na si elfu 23 lakini kwanini Paulo katika hiyo 1Wakorintho 10:8 aseme ni elfu 23?

Ni lazima uangalie ni nini Paulo alichokuwa anajaribu kukupitisha kwa watu wa wakorintho, Lengo na Nia ya Paulo ilikuwa ni kuwaonyesha madhara ya Uasherati, jinsi unavyoweza kuleta madhara makubwa ndani ya kipindi kifupi!.

Sasa hapa Paulo anasema walianguka watu elfu 23 “KATIKA  SIKU MOJA”. Ikiwa na maana kuwa huwenda lile pigo lilienda Zaidi ya “siku moja” . Huwenda lilidumu siku mbili au Zaidi ya hapo! Ndipo likakoma!.. lakini katika ile siku moja tu ya kwanza walianguka watu elfu 23 (hiyo ni idadi kubwa sana)…na idadi ya wote waliokufa mpaka siku ya mwisho pigo lilipokoma ilikuwa ni watu elfu 24.

Sasa Paulo anajaribu kuwaonya Wakorintho jinsi uasherati unavyoweza kuleta madhara makubwa ndani ya kipindi kifupi kuliko wanavyodhania, kama ilivyokuwa kwa hawa wana wa Israeli walivyozini na wanawake wa Moabu..

Ndio maana tukirudi nyuma kidogo kwenye kitabu hicho hicho, mlango ule wa 6 utaona jinsi Paulo anavyoelezea ubaya wa dhambi ya uasherati..kwamba ni mbaya  Zaidi ya dhambi zote mtu anazoweza kuzifanya katika mwili…

1Wakorintho 6:15 “Je! Hamjui ya kuwa MIILI YENU NI VIUNGO VYA KRISTO? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha!

16  Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja.

17  Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye.

18  Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ILA YEYE AFANYAYE ZINAA HUTENDA DHAMBI JUU YA MWILI WAKE MWENYEWE.

19  Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe;

20  maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu”.

Ni nini tunajifunza?

Kikubwa tunachoweza kujifunza ni madhara ya Uasherati, wengi wanasema nikishafanya uasherati nitatubu tu!..pasipo kujua kuwa uasherati wa mara moja unaweza kuleta madhara makubwa ndani ya muda mfupi!ll…Wana wa Israeli walipomaliza kufanya dhambi hiyo ndani ya siku moja walikufa watu elfu23, nafasi ya kutubu hawakuiona..

Vile vile dhambi ya uasherati inaweza kukuharibia mambo yako mengi ndani ya siku moja. Inaweza kukuharibia maisha yako moja kwa moja ndani ya siku moja, inaweza kukupeleka kuzimu ndani ya siku moja, na inaweza kukuletea majuto makubwa ndani ya siku moja, Zaidi sana biblia inasema mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa.

Mithali 6:32 “Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake”.

Itaishindaje dhambi ya Uasherati?.. Je kwa kuomba tu? Jibu ni La!..bali kwa kuikimbia kama Yusufu alivyoikimbia..

1Wakorintho 6:18  “Ikimbieni zinaa..”

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Je! Miaka Israeli waliokaa Utumwani ilikuwa mingapi? (miaka 400 au 430) kulingana na Mwanzo 15:13 na Kutoka 12:40-42?, Je biblia inajichanganya?

Uasherati wa Kiroho maana yake nini?

Nini Tofauti kati ya uzinzi na uasherati ?

Nini maana ya siku moja kwa Bwana ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja? (2Petro 3:8)

Kipaku ni nini kama tunavyosoma katika biblia?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Michael Wanyanga
Michael Wanyanga
1 year ago

Kwa kweli uasherati ni mbaya mno na ndio maana katika Efe.5:3 biblia inaonya kuwa “Lakini uasherati usitajwe kwenu KAMWE, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; haya hayapendezi; bali afadhali kushukuru.”