LIITE JINA LA BWANA KATIKA NYAKATI MBALIMBALI ZA MAISHA.

LIITE JINA LA BWANA KATIKA NYAKATI MBALIMBALI ZA MAISHA.

Upo umuhimu mkubwa wa kuliita Jina la Bwana

Warumi 10:12 “Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao;

13  kwa kuwa, KILA ATAKAYELIITIA JINA LA BWANA ATAOKOKA

Kuna umuhimu mkubwa wa kuliitia jina la Bwana kiusahihi, na kuna hatari kubwa ya kuliita au kulitaja jina la Mungu kimakosa.

Kutoka 20:7 “Usilitaje bure jina la Bwana, Mungu wako, maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure”.

Kwahiyo kama kwa kulitaja jina la Mungu bure ni dhambi, vile vile kinyume chake ni kweli kwamba tukilitaja inavyopaswa na kwasababu muhimu basi ni Faida kubwa kwetu.

Kwanini?, ni kwasababu jina la Mungu lina nguvu kuliko mwonekano wake…amelitukuza jina lake kuliko umbile lake, ndio maana amependa kutujulisha jina lake Zaidi ya sura yake.

Mithali 18:10 “Jina la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama”

Leo kwa neema zake tutatazama njia sahihi ya kulitaja jina la Bwana Mungu kulingana na mazingira tunayopitia ili tupate wokovu, tumaini, faraja, ushindi, Amani na Nguvu!.

  1.Katika kipindi cha mahitaji-Mwite YEHOVA-YIRE.

Yehova-Yire maana yake ni Mungu-Mpaji, (Mungu anayetoa kimiujiza)..Asili ya jina Yehova-Yire, ni kipindi Ibrahimu anakwenda kumtoa Isaka mwanae kama sadaka kwa Mungu, akiwa njiani mwanae Isaka alimwuliza Ibrahimu baba yake kuwa kuni zipo na moto pia upo lakini yupo wapi mwanakondoo?..Ndipo Ibrahimu kwa Imani alimjibu.. “Mungu atajipatia (Mwanzo 22:7-8)”.

Na walipofika katika mlima Moria ndipo wakamkuta kondoo ambaye tayari Bwana alikuwa amewaandalia. Ibrahimu akamwita Bwana YEHOVA-YIRE.

Vile vile na sisi tuwapo katika hali ya kuhitaji jambo Fulani (kama hitaji) tumwite Mungu kama YEHOVA-YIRE, itakuwa na mashiko Zaidi mbele zake kuliko kumwita au kumwomba tu kama MUNGU-MWENYEZI.

    2. Katika nyakati za Magonjwa- Mwite YEHOVA-RAFA

Yehova-Rafa maana yake ni “Mungu-atuponyaye”. Wakati wana wa Israeli wanaelekea Kaanani, Bwana Mungu aliwaahidi “kutowaletea magonjwa yale aliyowapiga nayo wamisri” endapo wakidumu katika sheria zake na amri zake.. Hivyo wana wa Israeli baada ya kusikia hivyo wakawa wanamwita Mungu YEHOVA-RAFA, kipindi walipopitia magonjwa na maradhi, na Mungu alikumbuka ahadi yake hiyo na aliwaponya na magonjwa yao.

Kutoka 15:26 “akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye”.

Vile vile upitiapo magonjwa au maradhi, mwite Mungu kama YEHOVA-RAFA, na utauvuta uponyaji kirahisi Zaidi..ndivyo walivyofanya wana wa Israeli katika nyakati za magonjwa.

     3. Katika Nyakati za vita- Mwite YEHOVA-NISI

Yehova-Nisi maana yake ni “Bwana ni Mungu wa vita”. Kipindi wana wa Israeli wanashambuliwa na Waamaleki, Mungu alimwambi Musa anyanyue mikono yake miwili juu, na aliponyanyua Israeli walishinda na aliposhusha waamaleki walishinda, na mwisho wa vita vile Israeli walishinda kwasababu Haruni aliitegemeza mikono ya Musa kuanzia asubuhi mpaka jioni (Kutoka 17:8-16).

Ndipo wana wa Israeli wakamwita Bwana YEHOVA –NISI, maana yake “Mungu wa Vita” (bendera yao).. Kwahiyo Nyakati za Vita walimwimbia Bwana, na kumsifu kama YEHOVA NISI na si Yehova Yire, na Bwana aliwaonekania.

Na sisi tukutanapo na vita mbele yetu viwe vya kiroho, kiimani au kiuchumi.. basi ni vizuri tukamwita Mungu wetu kama Yehova Nisi, tukamsifu na kumwimbia kwa jina hilo,  na vita mbele yetu atavifanya maji!.. kwasababu yeye anaketi katika sifa.

   4. Katika vipindi vya Hatari- Mwite YEHOVA–ROHI.

Yehova-Rohi maana yake ni “Bwana ndiye mchungaji wangu”. Daudi alipopita vipindi vya hatari, alimwita Bwana kama mchungaji wake, Yehova-Rohi  na kumsifu kwa jina hilo (Zaburi 23). Na Bwana daima alionekana mbele yake alimwokoa na hatari za kifo na dhiki zilizopo mbele yake.

Vile vile na sisi tuonapo hatari, au tuhisipo hatari, jina jema la kumwita Bwana na kumtukuza nalo, na kumsifu nalo ni YEHOVA-ROHI.

  5.Katika kipindi cha mambo yasiyowezekanika –Mwite YEHOVA-EL – SHADAI.

Yehova-Elshadai maana yake “Bwana ni Mungu-Mwenyezi” (anayeweza kufanya mambo yote).

Kipindi ambacho Ibrahimu anaona uwezekano wa kupata mtoto haupo kutokana na umri wa mke wake Sara, Bwana alijidhihirisha kwake kama Mungu mwenye uwezo wote (Mungu mwenyezi), na Sara akapata mimba, Hivyo Ibrahimu na Israeli wote wakaendelea kumwomba BWANA kama YEHOVA-ELSHADAI Katika vipindi vya mahitaji yaliyo magumu, kama utasa, ukame n.k

   6. Katika nyakati za Upweke- Mwite YEHOVA-SHAMA.

Yehova-Shama maaana yake “Mungu yupo hapa” (Ezekieli 48:35). Nyakati ambazo unajiona upo peke yake, mwambie Bwana wewe upo hapa, YEHOVA-SHAMA, na uwepo wa kipekee utakufunika, ndivyo Israeli walivyomwita Bwana nyakati za upweke.

  7. Nyakati za kukosa Amani- Mwite YEHOVA-SHALOM.

Yehova-Shalom, maana yake ni “Mungu Amani yangu”. Gideoni alipotokewa na yule malaika alihisi atakufa, lakini malaika yule alimwambia “hutakufa” na Gideoni akapata “amani”akamwita Mungu Yehova-Shalom.. Mungu ni Amani yangu.

Waamuzi  6:22 “Gideoni akaona ya kuwa ni malaika wa Bwana; Gideoni akasema, Ole wangu, Ee Bwana MUNGU! Kwa kuwa nimemwona Bwana uso kwa uso.

23 Bwana akamwambia Amani iwe pamoja nawe; usiogope; hutakufa.

24 Ndipo Gideoni akamjengea Bwana madhabahu hapo, akaiita jina lake, Yehova-Shalomu; hata hivi leo iko huko katika Ofra ya Waabiezeri”.

Na sisi vitokeapo vipindi vya Amani ya moyo kupotea na hofu kutawala, hususani hofu ya kifo, basi tumwite Mungu kama Yehova-Shalom, na amani yake itatufunika.

  8. Nyakati za kutamfakari Mungu kwa matendo yake- Mwite YEHOVA-ADONAI.

Yehova-Adonai maana yake ni “Mungu mwenye enzi yote(mfalme)” aliyeumba vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Sifa kwa ADONAI zina nguvu kama zikitajwa kwa maarifa hayo..

  9.Katika vipindi vya Kupotea na kuhitaji wokovu- Mwite YEHOVA-MWOKOZI (YESU KRISTO)

Maana ya YEHOVA-MWOKOVU ni YESU,… Tafsiri ya jina YESU ni Yehova-Mwokozi. Hili ndilo jina lenye nguvu katika vipindi karibia vyote. Na ndilo jina la ukombozi, na hakuna jina lingine litupasalo sisi kuokolewa kwalo isipokuwa jina hili la YESU, (Matendo 4:12).

Ikiwa umepotea dhambini, liite jina la YESU naye atakusaidia, ikiwa hutajabatizwa ili ukamilishe wokovu sawasawa na  andiko la Marko 16:16,  na ukabatizwe kwa jina la YESU, (Matendo 2:38, Matendo 19:5 na Matendo 10:48).

Yapo na majina mengine mengi yafaayo kumwita Bwana wetu katika nyakati hizo, lakini hayo yatoshe kusema tu, kuwa Mungu wetu anatupenda na anataka tupate faida, na faida moja wapo ni hiyo ya kulitumia jina lake wakati wa mahitaji.

Lakini katika hayo yote fahamu jambo moja kuwa unapoamua kuanza kulitaja jina la Bwana ili uvute msaada kutoka kwake, hakikisha unaacha UOVU..

2Timotheo 2:19  “Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena, KILA ALITAJAYE JINA LA BWANA NA AUACHE UOVU

Je umempokea Yesu Kristo, na kusafishwa dhambi zako kwa damu yake?

Kumbuka tunaishi majira ya kurudi kwa YESU mara ya pili, na shetani anafanya bidii nyingi kuhakikisha watu wanaenda katika lile ziwa la moto pamoja naye.

Bwana atusaidie.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

ZIFAHAMU NYAKATI SABA ZA KANISA NA WAJUMBE WAKE SABA.

HIZI NI NYAKATI ZA KUFUNGA NA KUOMBA.

Kutazama Nyakati mbaya ni kufanyaje?.

JE UMEJIANDAA KUTIMIZA UNABII UPI?

UMEJIANDAAJE KWA NYAKATI ZA KUWA PEKE YAKO?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Mr RENATUS
Mr RENATUS
3 months ago

Wapendwa ahsanteni mnooo mana Mimi nafaidika Sana Kwa mafundisho haya…..