MKUMBUKE TOMASO.

MKUMBUKE TOMASO.

Nakusalimu katika jina la Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo. Karibu tuzitafakari habari njema.

Tomaso alikuwa ni mtume  wa Bwana. Lakini alikuwa na tabia ya kitofauti na wale mitume wengine 11. Yeye hakuwa msaliti kama Yuda, zaidi sana alikuwa hata radhi kufa na Bwana wake, kipindi Fulani aliposikia anatafutwa ili  auawe (Yohana 11:16), hiyo ni ishara ya upendo wake kwa Yesu.

Lakini alikuwa na tabia nyingine ambayo ilimgharimu kwa sehemu Fulani, Na tabia yenyewe ni mashaka juu ya uweza wa Mungu, ni hiyo ikapelekea hata kuathiri mahudhurio yake, ya kiibada na kiutendaji kazi pale alipolazimika kuwepo na wenzake kama mtume.

Hakutaka kuamini kwamba Yesu anaweza kufufuka, hivyo wakati huo alipoitwa waombe pamoja, hakuwa tayari kukusanyika na wenzake, alipoitwa awafariji watu yeye kama mtume wa Bwana aliyepewa mamlaka hiyo, hakutaka kufanya hivyo kinyume chake akaenda kuendelea na shughuli zake. Walipokuwa wanatafakari maneno ya Yesu, yeye mawazo yake yalikuwa mbali kabisa na wenzake. Ni kama alikuwa amechoka.

Matokeo yake ikawa Yesu alipowatokea mitume wake, walipokuwa wamejifungia kuomba, yeye hakuwepo. Hata walipokuja kumuhadithia bado hakuamini, kwasababu moyo wake ulikuwa umeshahama kabisa.

Yohana 20:24  Walakini mmoja wa wale Thenashara, Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu. 25  Basi wanafunzi wengine wakamwambia, Tumemwona Bwana. Akawaambia, Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo. 26  Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani iwe kwenu 27  Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.

Wewe kama mtumwa wa Yesu usiwe tomaso, wakutanikapo wenzako kamwe kataa kujitenga, hata kama hakuna tumaini, dumu na wenzako, epuka utoro, epuka udhuru, dumu hapo. Zipo nyakati ambazo Bwana hamtokei mtu kivyake-vyake, bali wawapo wote. Zipo Baraka, ipo neema, katika umoja na wenzako, kupo kumwona Mungu unaposhikamana na wenzako kiuaminifu, katika kujengana na kutiana moyo.

Kamwe usifikiri kivyako, kataa hiyo hali, Bwana anasema ajitengaye na wenzake anatafuta matakwa yake mwenyewe, Tomaso alikuwa hivyo. Lakini fikra zake hazikuwa sahihi, aliligundua hilo baadaye aliporudi kujumuika na wenzake, ndipo akamwona Bwana, alidhani angemwonea kule alipokimbilia. Dumu na wenzako maadamu Bwana wenu ni mmoja, Roho wenu ni mmoja, Ubatizo wenu mmoja. Hiyo inatosha. Dumu hapo.

Bwana atusaidie.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Kwanini Tomaso atake kwenda kufa pamoja na Lazaro? (Yohana 11:14-16).

Je! hizi roho saba za Mungu ni zipi? na je zinatofautiana na Roho Mtakatifu?

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

KWANINI MITUME WAMUULIZE BWANA FARAGHANI?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments