Category Archive Home

Je! Ni sahihi kwa mkristo kufundishwa na AI mfano wa Chatgpt, deepseek n.k.

SWALI: Je! Ni sahihi kwa mkristo kujifunza, au kufundishwa na AI (Artificial Inteligence), mfano wa Chatgpt, deepseek n.k.


JIBU: Ili kujibu swali hili ni vema, kutambua mashine hizi za akili bandia (AI), zinafanya kazi gani.

Kwa ufupi ni kuwa AI, inafanya kazi ya kuchakata taarifa nyingi, kutoka katika vyanzo vingi vilivyopo mitandaoni, mfano vitabu, makala, sauti, machapisho n.k, na hivyo inazichanganya taarifa hizo zote kwa kuangalia muktadha unaofanana na kuzifupisha, na kukujibu.

Hivyo kimsingi, ni chombo ambacho kinatoa msaada mkubwa katika ulimwengu wa sasa, na ndio ukweli usiopingika..Kwasababu kinarahisisha utafutaji wa taarifa. Lakini pamoja na hayo haimaanishi kuwa kinatoa kwa ufasaha wote.

Sasa tukija kwenye eneo la kiroho. Je ni vema mkristo kwenda kuuliza AI, au kuandaa maombi au masomo kupitia hiyo, n.k.

Ukweli ni kwamba Imani, sio taarifa, ni zaidi ya taarifa.. Hizi AI, zinatoa tu taarifa lakini hazitoi mafunuo. Hazina pumzi ya Roho Mtakatifu ndani yake.

Ikiwa unataka kuongeza maarifa kwa sehemu fulani zinaweza kukusaidia, lakini sio kukujenga nafsi, kwani inahitaji pumzi ya Mungu na miongozo ya Mungu wewe kujengwa nafsi, na sio taarifa.

Kwamfano ikiwa wewe ni mchungaji halafu, kila inapokaribia jumapili unachowaza ni kwenda chatgpt, kuiambia ikuandalie somo la kufundisha jumapili,  ndugu hapo hesabu kuwa umepotea kama sio kukengeuka… Tumia hiyo kwenye biashara zako, masomo yako,  projekti zao lakini sio kwenye mambo ya kiroho. Hilo liepuke kabisa.

Kufundisha Neno inahitaji ‘Neno’ mwenyewe (Yesu) akae ndani yako, kwasababu ni UHAI sio taarifa (Waebrania 4:12) ndio hapo itakupasa kupiga magoti kwanza uombe, kwa muda mrefu, utafakari moyoni mwako, ukae kwenye utulivu wa kutosha, ndipo Mungu alipande somo lake moyoni mwako. Ambalo yeye mwenyewe anajua litakuwenda kuwagusa vipi watu wake, wenye changamoto mbalimbali, kwamfano, pengine mtu mmoja alikuwa anakaribia kwenda kujinyonga kwasababu ya ugumu wa maisha na mateso fulani, na Mungu kamwona anataka amsaidie, kwa kuliweka somo linalohusiana na mapito ya Ayubu ili ainuliwe imani. Kinyume chake kwasababu ya uvivu wako wewe unakwenda kuiambia chatgpt (akili bandia), ikuandalie somo. Halafu jumapili utakwenda na taarifa zao sio mafunuo. Badala uokoe roho inayokwenda kujinyonga, unaiambia, “leo tunajifunza kanuni kumi za kudumisha ndoa na mahusiano kibiblia”. Hapo unafanya nini sasa?

Au Neno fulani Bwana anataka kukupa la wakati wako, sasa ikiwa unakimbilia AI ikusaidie, hutaki kuchukua muda wako binafsi kutafakari na kuomba ‘jiandae kukutana na ukame wa kiroho.

Visaidizi hivi, hatupaswi kuvifanya ndio sehemu ya imani yetu, kwamba kila kitu tutegemee kule, hivi ni tone dogo sana kati ya bahari kubwa. Roho Mtakatifu alishatuandalia njia zake, kuu za kujengwa na yeye.

Wekeza zaidi, kuomba msaada kwa wakufunzi wako, viongozi wako, ndugu zako katika Kristo, wekeza katika maombi, mifungo, tafakari, na kujisomea mwenyewe Neno.  kwa njia hizi hakika Bwana atasema nawe na kujengwa zaidi kuliko visaidizi. Lakini pia ikiwa pana umuhimu wa kujiongezea taarifa kwa vile unavyovijua, visaidizi hivi vitakufaa (Katika uangalizi maalumu), vinginevyo utajidumaza kiroho.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >>  https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Karismatiki ni nini?

Uinjilisti kama agizo kuu la Bwana.

Vita vya kiroho, na mwamini Mpya.

Print this post

JIHADHARI NA MANENO YASIYO NA  MAANA

Mathayo 12:36 “Basi, nawaambia, KILA NENO LISILO MAANA, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu.

37 Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa”.

Mfano wa maneno yasiyo na maana ni maneno yote ya kukufuru, kulaani, kutukana, mizaha, mashindano, mazungumzo machafu, nyimbo za kidunia na mengine yanayofanana na hayo.

    1.  Mizaha

Unapotumia baadhi ya mistari ya kwenye Biblia au matukio kwaajili ya kufanya utani, au mzaha au vichekesho…maneno hayo utayatolea hesabu siku ile. Biblia sio kitabu cha comedy.

Zaburi 1:1 “Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha”.

    2.  Dhihaka.

Unapotoa dhihaka juu ya Neno la Mungu, au Watumishi wa Mungu ambao unajua kabisa ni wa kweli, siku ya mwisho utatoa hesabu..

    3. Mabishano na Mashindano.

Unapobishana na ukweli, kwasababu tu unataka uonekane unajua au unatafuta ushindi wa maneno.. basi fahamu kuwa siku ya mwisho utatoa hesabu ya maneno yako yote… Biblia inasema mashindano ya dini yote ni maneno yasiyo na maana..

1Timotheo 6:20 “Ee Timotheo, ilinde hiyo amana; ujiepushe na maneno yasiyo ya dini, yasiyo na maana, na mashindano ya elimu iitwayo elimu kwa uongo”

     4. Kufuru

Unapotoa kufuru na kashfa juu ya kazi ya Mungu, na moyoni unajua kabisa ni kazi kamili ya Mungu,  mbeleni kuna kutoa hesabu ya maneno yaliyotoka kinywani.

Mafarisayo walinena maneno ya kumkufuru Roho Mtakatifu katika kitabu hiko cha Mathayo 12, na ndio sababu ya Bwana YESU kusema maneno hayo kuwa “kila neno lisilo maana watu watatoa hesabu yake siku ya mwisho”.

     5. Nyimbo za kidunia.

Maneno yaliyopo kwenye nyimbo za kidunia hayana maana na yanamtukuza shetani, na hivyo hata maneno ya nyimbo hizo yatatolewa hesabu.

Amosi 6:5 “ninyi mnaoimba nyimbo za upuzi pamoja na sauti ya vinanda, na kujifanyizia vinanda vya namna nyingi, kama vile Daudi”.

      6. Mazungumzo machafu.

Mazungumzo machafu ni yale yote ya kijiweni au ya mtu na mtu, ambayo ni mazungumzo ya uasherati, ushabiki, uhuni, na mipango mibaya, matusi na mambo mengine yote mabaya.. yote hayo mtu atayatolea hesabu siku ya mwisho.

Sasa nini maana ya kutoa hesabu?

Kutoa hesabu maana yake ni kutoa “maana au tafsiri ya kina ya kile kilichotoka kinywani”.  Kwamfano kama mtu umemtukana mtu na kumwita yeye ni Mbwa, basi siku ile utaeleza sababu za kumwita vile, na kama kweli yeye ni mbwa kama ulivyosema… kwaufupi maneno ambayo sisi tuliyatamka kwa utani tu na ufupi, kule yatarefushwa na kuwa mada ndefu mno.

Hivyo hatuna budi kuwa makini na yanayotoka kinywani mwetu.. kwamaana yanarekodiwa yote, na pia ni vizuri kama tumekosea kwa vinywa vyetu kuwahi kurudi kutubu kwa tuliyemtolea maneno mabaya, au tuwahi kurudi kwa Mungu kutubu ili tusiangukie hukumu.

Hukumu inakuja, hukumu inakuja, tumwamini YESU na kutubu na tuyashike sana maungamo yetu.

Ubarikiwe.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

KILA MTU ATATOA HABARI ZAKE MWENYEWE.

Je mtu anayeua anabeba dhambi zote za yule aliyemuua?

UTASIMAMA PEKE YAKO SIKU ILE.

USIGEUZE JIWE KUWA MKATE.

USI..USI..USI.

Print this post

Majini wanaotajwa kwenye Walawi 17:7 ni viumbe gani?

Jibu: Turejee kuanzia mstari wa 6..

Walawi 17:6 “Naye kuhani atainyunyiza damu yake juu ya madhabahu ya Bwana, mlangoni pa hema ya kukutania, na kuyateketeza mafuta yake, yawe harufu njema mbele za Bwana.

7 WALA HAWATATOA TENA SADAKA ZAO KWA WALE MAJINI, ambao huwafuata ili wafanye uasherati nao. Sheria hii itakuwa sheria ya milele kwao, kizazi baada ya kizazi”.

“Majini” wanaotajwa hapo ni “mashetani”..

Katika agano la kale sadaka yoyote iliyotolewa nje ya hema  ya Mungu (maana yake katika madhabahu nyingine), sadaka hiyo ilihesabika kuwa imetolewa kwa majini/mashetani, na yeyote aliyetoa sadaka yake huko, akabainika sheria ilikuwa ni kutengwa na watu wake.

Walawi 17:8 “Nawe utawaambia, Mtu awaye yote katika nyumba ya Israeli, au miongoni mwa wageni, wanaokaa nao, atoaye sadaka ya kuteketezwa au dhabihu,

9 wala haileti mlangoni pa hema ya kukutania, ili aisongeze kwa Bwana BASI MTU HUYO ATATENGWA NA WATU WAKE”.

Mahali pekee Bwana Mungu alipopachagua pa kutolea sadaka ni katika “HEMA YA MUNGU”, katika kipindi cha Waamuzi na katika “NYUMBA YA MUNGU” aliyoitengeneza Sulemani katika kipindi cha Wafalme na kuendelea.

Kwahiyo sadaka yoyote inayopelekwa mahali panapoabudiwa ibilisi, basi sadaka hiyo ni imetolewa kwa majini/mashetani..na sadaka inayotolewa kwa mashetani basi mtu huyo au watu hao wanakuwa na ushirika na mashetani, ndivyo Neno la Mungu linavyosema..

1Wakorintho 10:20 “Sivyo, LAKINI VITU VILE WAVITOAVYO SADAKA WAVITOA KWA MASHETANI, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi KUSHIRIKIANA NA MASHETANI. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani”.

Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba “majini” wanaotajwa katika Walawi 17:7 ni mashetani/mapepo ambao pia wanatajwa katika Isaya 13:21 na 2Nyakati 11:15 wakati wa mfalme Yeroboamu.

2Nyakati 11:15 “naye akajiwekea makuhani wa mahali pa juu, na wa WALE MAJINI, na wa zile ndama alizozifanya.”

Na pia zipo sadaka zitolewazo kwa Mungu na pia zitolewazo kwa mashetani, Mtu anayeenda kwa waganga wa kienyeji sadaka yake anaitoa kwa mashetani, na kafara yoyote iwe ya mnyama au kiumbe chochote inayofanyika katika agano jipya ni sadaka kwa mashetani na si kwa Mungu, kwani hatuna tena kafara za wanyama katika agano jipya, wala hakuna kafara za watu kwa Mungu na hazijawahi kuwepo huko kabla, kafara zote za namna hiyo ni za mashetani.

Zaburi 106:37 “Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani.

38 Wakamwaga damu isiyo na hatia, Damu ya wana wao na binti zao, Waliowatoa dhabihu kwa sanamu”

Je umempokea YESU?.. fahamu kuwa hakuna wokovu kwa mwingine yoyote isipokuwa kwake!, na tunaishi majira ya kurudi kwa YESU, huu si wakati wa kucheza na dunia, bali kujitoa kwa MUNGU.

1Petro 4:2 “Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika MAPENZI YA MUNGU, WAKATI WENU ULIOBAKI WA KUKAA HAPA DUNIANI.

3 Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuenenda katika ufisadi, na tamaa, na ulevi, na karamu za ulafi, na vileo, na ibada ya sanamu isiyo halali”.

Bwana atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Je mapepo au majini yanaweza kuviingia vitu visivyo na uhai?

MAJINI WAZURI WAPO?

Tunathibitisha vipi kuwa Yule Malaika wa (Yohana 5:4) ni wa MUNGU?

AINA ZA MAJINI, MAJINA YAO, KAZI ZAO, NA TIBA ZAKE.

Ipi tofauti kati ya Uhai na Uzima kibiblia?

Print this post

Uinjilisti kama agizo kuu la Bwana.

Kila mwamini ameitwa kuieneza injili ya Yesu Kristo. Ambayo huitwa habari njema.

Mathayo 28:19-20

[19]Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;

[20]na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.

Habari njema ni nini? Ni habari za wokovu kwa mwanadamu, ulioletwa na  kupitia mtu mmoja Yesu Kristo kwa tendo la kufa na kufufuka kwake kaburini.

Kwanini tunapaswa tuwashuhudie wengine habari njema?

1) Ni agizo la Bwana (Mathayo 28:19)

Kama tulivyotangulia kuona hapo juu, kuwa siku Yesu alipoondoka hakutuacha bila wajibu, bali kila mmoja wetu alipewa sehemu ya huduma katika shamba lake. Ya kuenenda ulimwenguni kote kuwafanya watu kuwa wanafunzi wake.

Kazi hii sehemu nyingine anaifananisha na talanta, ambayo amempa kila mwamini na anataka kila mmoja aizalishe (Mathayo 25:14-30), sehemu nyingine anaifananisha na matunda, anasema sisi ni matawi na yeye ni mzabibu  kwamba tumzalie matunda, (Yohana 15:1-7),sehemu nyingine nyingine anaiita posho, huku yeye  akijiita bwana, na sisi mawakili wake, akitutaka tutoe posho kwa wakati kwa watu wake, (Luka 12:42-48)

Sasa ukiangalia utaona sehemu zote hizo tunazofananishwa nazo, kama mtu hajafanya chochote au hajazalisha chochote, haachwi hivi hivi, bali kuna aidha kuondolewa sehemu ya thawabu yake, au kukataliwa kabisa.

Ndio maana ni lazima tujue mwamini yoyote yule, ni lazima aishi maisha ya kuwashuhudia wengine injili.

2) Watu wanapotea bila Kristo.

Warumi 10:14 Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri?

Ni lazima ujue kuwa hukumu ipo na kuzimu pia ipo, na inawameza wengi, Na watu hawawezi kuokoka tu wenyewe hivi hivi bila kusikia injili kama wewe ulivyosikia.  Tengeneza picha unamwona baba yako, au mama yako kwenye ziwa la moto, halafu anakuambia laiti ningelijua ukweli nisingekuwa huku, utajisikiaje? Ukilijua hili basi huruma ya ki-Mungu itakujaa tu ndani yako, na utasukumwa kujitoa kuwaendea wenye dhambi, kama Kristo alivyotujia sisi, kutoka mbinguni, na kama mitume walivyowaendea watu, ili kuhakikisha wanaokoka.

3) Mbingu zinafurahi.

Luka 15:7 Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu

Mungu hufurahi malaika pia hufurahi, wanapoona roho za watu zinaokoka,duniani, Hivyo sisi kama wana wa Mungu ni wajibu wetu kuyatenda yale tu ambayo yanamfanya Baba yetu afurahi, na hilo si lingine zaidi ya kutoka na kwenda kuwashuhudia watu injili.Hapo tunaufanya moyo wa Mungu hufurahi sana.

4) Ushuhuda wa maisha yetu.

Ni ukweli usiopingika kuwa kila mmoja wetu kuna mahali Mungu amemtoa mpaka hapo alipomfikisha, anayo mengi ya kushuhudia kuhusu uzuri wa Kristo.

Wazia yule kichaa ambaye alikuwa katika hali mbaya kule makaburini, uchi, usiku na mchana, ameshindikana kwa vifungo vyote. Lakini Yesu alipokutana naye saa ile ile alipona, akataka kuambatana na Yesu, lakini Yesu akamwambia nenda nyumbani kwa watu wako uwasimulie matendo makuu ambayo Mungu amekutendea, Na tunaona alikwenda kusimulia yote mji ule, na watu wengi wakamwamini Kristo, kwa ushuhuda wake tu.

Marko 5:20 Akaenda zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli, ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu

Hata wewe, wazia uzuri ulioupata pindi ulipompokea Kristo, utamani pia mwingine aupate, na huo ndio upendo, umeonja uzuri wa Kristo unakwenda kuwaambia na wengine mfano tu wa yule mwanamke pale kisimani.

NI Njia zipi za kuhubiri?

i) Kwa kusimulia ushuhuda wa maisha yako, jinsi Yesu alivyokuokoa.

Sawasawa na agizo ambalo Yesu alimwagiza yule mtu ambaye aliteswa Na mapepo akamfungua. (Marko 5:19-20)

ii) Kwa kumkaribisha Kanisani.

Hii ni njia bora, ambayo utapata nguvu ya kikanisa, kwasababu mule akutanapo na vipawa mbalimbali vya Mungu, hurahisisha zaidi moyo wake, kuamini ujumbe uliompelekea.

iii) Kwa Mwenendo mwema wa  rohoni.

Ishi maisha yanayomuhakisi Kristo. Kwasababu matendo yako ni injili kuwa wengine kumgeukia Kristo. (1Petro 3: 1-2)

iv) Kwa kutumia Visaidizi

Hivi Ni kama vitabu, kanda, luninga, na kwa dunia ya sasa, Vitu kama whatsapp, websites,  panaweza pakawa mahali Ambapo injili yetu kupaa sana na kuwavuta wengi ndani ya ufalme. Ulimwengu wa sasa, upo mtandaoni, hivyo tumia fursa hiyo, kushea mafundisho, mahubiri sahihi ya Neno la Mungu kwa marafiki zako, familia, ndugu, majirani, huko huko Mungu ataanza kazi ya wokovu ndani yao.

Namna ya kushinda hofu.

Haya ni mambo ya kukumbuka kila uendapo kushuhudia, ili usishindwe na hofu.

1) Kile uendapo kushuhudia ukumbuke kuwa Roho Mtakatifu ndiye anayetupa nguvu na si kwa uweza wetu tu wenyewe. (Matendo 1:8)

2) Omba kabla ya kwenda kuwashuhudia watu.

3) Anza katika udogo, shuhudia mtu mmoja mmoja, kabla ya kufikia umati wa watu wengi.

4) Pia ukumbuke  jambo la kushawishi ni la Roho Mtakatifu, sisi ni kushuhudia.

Usiwe na hofu ikiwa huoni mwitikio wowote, kwa yule unayemweleza habari ya wokovu, fahamu kuwa ipo mbegu imemwingia ambaye itakuja kumea tu kwa wakati wake.

5)Ongozana na mtendakazi wenzako, au kiongozi wako. 

Uinjilisti wa wawili huwa mrahisi zaidi ya ule wa mmoja (isipokuwa unao uzoefu). Yesu aliwatuma wanafunzi wake wawili wawili, alijua ujasiri utaongezeka lakini wangeweza kufanya zaidi, pale mmoja anapochoka anamtia nguvu mwenzake. Vivyo hivyo na wewe katika hatua za awali ongozana na kiongozi wako, au mshirika mwenza katika kazi ya injili.

Vifungu vya kukariri, ambavyo unapaswa uwe navyo kichwani, katika hatua za kuwashuhudia watu.

Yohana 3:16

Warumi 3:23

Warumi 6:23

Warumi 10:9–10

2 Wakorintho 5:17

Kwa mwongozo wa namna ya kutembea katika baadhi ya vifungu hivyo, pitia hili fundisho >>> NJIA/BARABARA YA WOKOVU NDANI YA KITABU CHA WARUMI.

Mafundisho ya ziada

KWANINI TUNAPASWA KWENDA KUIHUBIRI INJILI KWA UJASIRI WOTE?

IHUBIRI INJILI, KILA MAHALI KWASABABU AKUZAYE NI MUNGU.

HEKIMA NANE(8) ZA KIUINJILISTI, KATIKA KUWAVUA WATU KWA KRISTO.

JE UDHAIFU WANGU UNAWEZA KUZUIA INJILI?

KUTOKUIHUBIRI INJILI,KUNA MADHARA GANI?

KWANINI KILA MWAMINI ANAPASWA AWE MHUBIRI WA INJILI

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Print this post

Akaabudu akiegemea kichwa cha fimbo yake

Akaabudu akiegemea kichwa cha fimbo yake.

Waebrania 11:21

[21]Kwa imani Yakobo, alipokuwa katika kufa, akambariki kila mmoja wa wana wa Yusufu, akaabudu akiegemea kichwa cha fimbo yake.

Ulishawahi kujiuliza ni kitu gani Yakobo alikuwa anawaonyesha wana wake siku ile alipokuwa anakaribia kufa.. kitendo cha yeye kusujudu kwa kuegemea kichwa cha fimbo?

Kwanini biblia iseme akaegemea fimbo na sio ukuta, au kitanda au au kiti au isikae tu kimya, bila kueleza chochote?

Yakobo alikuwa na maana kubwa kufanya vile, kwasababu hata alipokuwa akiwabariki watoto wa Yusufu (Efraimu na Manase) alipishanisha mikono..wakidhani kuwa amekosea, akawaambia sijakosea naelewa ninachokifanya, leo ndio tunajua kumbe alikuwa anaunda msalaba, ambao kwa kupitia huo neema inawafikia mataifa kwanza.

Vivyo hivyo na alipokuwa anakufa alisujudu kwa kuegemea kichwa cha fimbo, na huwenda watoto wake walistaajabishwa na kusujudu kule, pengine walijaribu kumwondoa pale ili asujudu vema, lakini akawaambia niacheni naelewa…

Fimbo kibiblia inafunua mamlaka ya mfalme, mchungaji na safari.

Yakobo hakuishi bila tegemeo la mchungaji…udhihirisho Ulikuwa ndio ile fimbo..kwasababu sikuzote alijiona kama kondoo wa Mungu, hakutaka kuiacha fimbo ya mchungaji wake, popote alipokuwepo kwasababu ndio faraja yake.

Daudi alisema…Bwana ndiye mchungaji wangu…gongo lake, na fimbo yake vyanifariji..

Zaburi 23:1-4

[1]BWANA ndiye mchungaji wangu,  Sitapungukiwa na kitu.

[2]Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,  Kando ya maji ya utulivu huniongoza.

[3]Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza  Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.

[4]Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya;  Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. 

Kwa ufupi ni kuwa palipo na fimbo ya mchungaji hapo hapo utaona Na kondoo wamejilaza. Yakobo alitembea na Kristo, Mpaka dakika ya mwisho wa maisha yake.

Lakini pia Fimbo inamfunua msafiri…zamani wasafiri walikuwa wanasafiri na fimbo kuwasaidia kutembea..

Wana wa Israeli walipokuwa wanajiandaa na safari ya kutoka Misri, utakumbuka usiku ule walipewa maagizo kila mmoja kushika fimbo yake.

Kutoka 12:11

[11]Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya BWANA.

Kristo pia alipokuwa anawatuma wanafunzi wake katika ziara za injili aliwaagiza Kubeba fimbo zao..

Marko 6:8

[8]akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni;

Hii ni kutufunulia kuwa Yakobo alikataa kuishi kama mwenyeji duniani.. bali msafiri..

Hivyo alitamani urithi wake ujue jumla ya mwenendo wa maisha yake hapa duniani ulikuwaje..

Hiyo ndio sababu kwanini historia za maisha ya watu kama hawa Mungu kazihifadhi tuzisome hadi leo.

Hata sasa, ujiulize je na Mimi je! fimbo ya mchungaji wangu(YESU KRISTO), ipo pamoja nami? ujiulize je mimi ni msafiri hapa duniani?

Fahamu tu Wazao wote wa Mungu huwakosi na fimbo ya Mungu, hiyo ndio alama yetu.

Shalom

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Yakobo alimaanisha nini kusema ‘ndipo BWANA atakuwa Mungu wangu’ Mwanzo 28:21

Kwanini Yakobo alimshinda Mungu, Je! Mungu huwa anashindwa na wanadamu?

Ni kwanini mifugo ya Yakobo iliongezeka kwa wingi kiasi kile?

Print this post

Biblia inamaana gani inaposema “Mungu wa neema yote” (1Petro 5:10)

Biblia inamaana gani inaposema “Mungu wa neema yote”

1 Petro 5:10

[10]Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu.

Tafsiri ya Neema ni kukubaliwa kusikostahili.. au upendeleo usio na sababu. Kwamfano pale mtu anapomwajiri mtu asiye na ujuzi kisha akampa nafasi au mshahara mkubwa wa kiwango cha sawasawa na yule mwenye elimu nyingi na uzoefu..hiyo tunaiita neema.

Hivyo katika ukristo msingi mkuu wa wokovu wetu unategemea neema ambayo ililetwa na Bwana wetu Yesu Kristo(Yohana 1:17).

Yaani Tunakubaliwa na Mungu kuwa sisi tumestahili kuingia katika ufalme wa Mungu na kuwa watoto wake, kwa kumwamini tu Yesu Kristo bila kutegemea matendo yetu wenyewe kama kigezo cha sisi kufikia kiwango hicho.

Neema hiyo hujulikana kama neema ya wokovu. Ambayo ndio neema kuu, iliyomfanya Kristo aje duniani kufa kwa ajili yetu kama fidia ya dhambi ili sisi tuitwe waliostahili. (Waefeso 2:8-9)

Lakini pamoja na hayo Mungu hana mipaka kwamba anatoa neema ya aina moja tu yaani ya wokovu peke yake…hapana anazo Neema nyingi, ambazo zinaingia katika nyanja mbalimbali za maisha ya mwanadamu.

Sehemu nyingine katika biblia huitwa. Neema juu ya neema..

Yohana 1:16

[16]Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema.

 

Zifuatazo ndio mfano wa neema Mbalimbali ambazo Mungu anatoa.

1) Neema ya kutumika na kibali.

Neema hii unamwezesha mtu, kuwa na matokeo katika Huduma na ustahimilivu wote. Ndiyo ambayo Paulo na Barnaba walipewa, iliyowafanya waweze kukichukua kijiti cha injili na kufanikiwa kukipeleka kwa mataifa.

Matendo ya Mitume 13:2

[2]Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.

Mbeleni utaona maandiko yanasema..

Matendo ya Mitume 14:26

[26]Na kutoka huko wakaabiri kwenda Antiokia. Huko ndiko walikoombewa neema ya Mungu kwa ile kazi waliyokwisha kuitimiza.

Hivyo wewe kama mtakatifu ukitaka mafanikio katika huduma au karama yako. Kujifunza kuomba neema ya Mungu katika huduma ni liwe ni sehemu ya maisha yako. Kwasababu hiyo Ipo kukusaidia…Na utapata matokeo ambayo hayategemei zaidi nguvu zako. Ndicho walichokuwa wanakiomba sana mitume.

Matendo ya Mitume 15:40

[40]Lakini Paulo akamchagua Sila, akaondoka, akiombewa na wale ndugu apewe neema ya Bwana. Neema ya kupokea vitu.

2 Wakorintho 9:8

[8]Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema;

Kumbukumbu la Torati 8:18

[18]Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.

Hata kupata vitu kiwepesi, hasaa hutegemea neema ya Mungu, kama mkristo ni lazima ujifunze kumwomba Mungu neema ya kufanikishwa, katika mambo yako yote ya kimaisha, isizitegemee tu nguvu zako au akili zako, hata kama jambo ni jepesi vipi, ikiwa ni kazi Omba Mungu akupe neema ya mafanikio, ikiwa ni biashara omba Akupe neema ya kupata Faida Zaidi, ikiwa ni elimu omba Mungu akuongezee akili zaidi.

2) Neema ya kuendelea Mbele (nguvu mpya).

Zaburi 68:9

[9]Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema; Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu.

Ni sifa ya Mungu kauchilia neema yake kwa watu wake pale wanapochoka huwatia nguvu mpya, wao wenyewe wanashangaa wanainuka tena na kuendelea mbele.. Ndio maana tunasema Mtu anayedumu katika wokovu maisha yake yote, hata anapopitia katika tufani, Pepo na mawimbi, bado hatetereki.. Ni neema ya Kristo inakuwa imehusika hapo kumvusha, si nguvu Zake.

Jifunze kuiomba hii namna ya neema.

3) Neema ya madhirihisho ya karama za Roho.

Matendo ya Mitume 6:8

[8]Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu.

Karama za Roho, mfano miujiza, uponyaji, lugha, unabii, utume, uchungaji, n.k, ni vipawa ambavyo hutolewa bure na Roho Mtakatifu, Hakuna jitihada Yoyote ambayo mtu atafanya aweze kukunua nguvu za kumfufua mfu, au kuona mambo ya mbeleni Ayatolee unabii, au kuundoa Ukimwi kwenye damu Ya mtu, isipokuwa kwa neema za Mungu, kutembea na yeye.

Ni neema ambayo tunapaswa tuiombe, ambayo inamfanya Mungu aachilie mafuta mengi ndani yako ya kutembea katika vipawa hivyo, ili kulijenga kanisa.

1 Petro 4:10

[10]kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu.

4) Neema ya Kutembea katika utakatifu.

2 Wakorintho 1:12

[12]Kwa maana kujisifu kwetu ni huku, ushuhuda wa dhamiri yetu, ya kwamba kwa utakatifu na weupe wa moyo utokao kwa Mungu; si kwa hekima ya mwili, bali kwa neema ya Mungu; tulienenda katika dunia, na hasa kwenu ninyi.

Inategemea nguvu ya Mungu (neema), kutembea katika hali ya kutimiza mapenzi yote ya Mungu katika utakatifu… maana yake ni kuwa mwanadamu Akijifunza kumpa Nafasi Roho Mtakatifu ndani yake. Atajaliwa kuishi Maisha yote yampendezayo Mungu, sawasawa na Wagalatia 5:16

5) Neema ya kutoa.

2 Wakorintho 8:1-3

[1]Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia;

[2]maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao.

[3]Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao;

Hii ni uwezo wa kutoa vitu/ maisha/ chochote kwa wengine bila kujali nafsi yako mwenyewe.

Jifunze kumwomba Mungu neema ya utoaji. inafaida kubwa sana kwa wengine, kwa binafsi lakini pia katika kukua kwa ufalme wa Mungu.

2 Wakorintho 8:9

[9]Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.

6) Neema ya ulimwengu ujao.

1 Petro 1:13

[13]Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo.

Yapo mambo Mengi mema tusiyoyajua, ambayo tutapewa tukifika kule ng’ambo Kristo atakaporudi.. ni mambo ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia, biblia imehitimisha kwa kuyaita “neema”

Je Umepokea neema zote? Lakini zaidi ya yote neema ya wokovu?. Ikiwa bado hujaokoka na upo tayari leo Yesu akusamehe dhambi zako, basi tawasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya chapisho hili upate msaada huo.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >>https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

NI MAJIRA YAPI YA NEEMA WEWE UPO?

TAHADHARI YA NEEMA YA MUNGU.

UMEIZALIA MATUNDA MIAKA 4 YA NEEMA ULIYOPEWA?

 

Print this post

Mishale ya moto ya mwovu inayozungumziwa kwenye Waefeso 6:16 ni ipi?

Waefeso 6:16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu

Waefeso sura ya 6, inaeleza mapambano ambayo yapo rohoni kati ya sisi na ufalme wa giza, na namna ambavyo tunapaswa tusimame kushinda vita hivyo, kwa kuvaa zile silaha zote za haki zinazotajwa pale. Kama vile chapeo ya wokovu, dirii ya haki, kweli kiunoni, upanga wa Roho,  na ngao ya Imani,.

Lakini pia katika vifungu hivyo tunaelezwa mojawapo ya silaha ya adui, nayo ni “mishale ya moto”. Swali Je hii mishale ya moto ni ipi?

Mishale ni silaha zilizotumika zamani, za kumshambulia adui kwa mbali, na hivyo ili kuziboresha waliweka moto kwa mbele ili zitakapomfikia adui basi zilete madhara zaidi ya yale tu ya  kutoboa, bali kuunguza kama sio kumuharibu kabisa adui.

Tofauti na silaha kama rungu, au upanga ambavyo vinahitaji uso kwa uso kutumika. Kwa mbali havina matokeo.

Tukirudi katika ulimwengu wa sasa mishale ya vita  ni makombora, Kwanini hapo shetani anaonekana akirusha mishale kutokea mbali? Ni kwasababu kwa karibu hamwezi mwamini, kwani nguvu zilizo ndani yake ni nyingi kuliko alizonazo.

Ifuatayo ni mishale ya moto ya adui.

1) Ulimi:

Shetani hutumia sana ulimi kuleta, aidha udanganyifu,  mafarakano, vita n.k. Ndio maana maandiko yanasema;

Yakobo 3:5 Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana.

6 Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum.

7 Maana kila aina ya wanyama, na ya ndege, na ya vitambaavyo, na ya vitu vilivyomo baharini, vinafugika, navyo vimekwisha kufugwa na wanadamu.

8 Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti.

9 Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu.

10 Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo.

Hawa alidanganywa na Nyoka kwa ulimi, Mafundisho ya uongo, huanzia katika maneno. Hivyo sisi kama watoto wa Mungu ni lazima tuijue silaha hii na kuidhibiti kwanza sisi wenyewe ndani yetu, kuhakikisha hatutumiki kama warusha mishale, kwa kusema yasiyopasa, lakini pia kusimama kwa imani kuhakikisha, tunakuwa thabiti kiimani, kwa kupuuzia, au kutokuweka moyoni kila Neno linalosemwa kinyume chetu, sambamba na kuwa makini kwa kupima kila neno tunaloambiwa kama kweli ni la Mungu au la!.

Mkristo usipojua silaha hii ya adui, utajikuta kila kukicha unaishi kwa machungu ya maneno ya watu, huna raha, una mashindano,  au utajikuta unaanguka katika mikono ya manabii wa uongo, na hatimaye shetani anakuwa amekupata.

2) Mshale wa moto pia ni Majaribu.

1Petro 4:12 Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.

13 Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.

14 Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia

Majaribu yote hutoka kwa Yule mwovu, lengo lake ni kumwangusha mwamini ili amwasi Mungu, hata wakati ule Bwana Yesu anakaribia kusulubiwa, alimwombea Petro ili imani yake isitindike, kwasababu alijua wataingia kwenye majaribu makubwa, kwa upungufu wa maombi yao. Vivyo na sisi yatupaswa tuwe waombaji ili tuizime mishale ya majaribu mbalimbali ya adui tusiyojua pembe ipi yanatokea.  Na pia tunapojikuta ndani ya hayo majaribu, yatupasa kuishikilia imani yetu hasaa, kwa kuamini kuwa Bwana yupo pamoja nasi kutengeneza njia ya kutokea.

3) Mishale mingine ni vitisho, hofu , mashaka

Shetani akijua kuwa hana nguvu ya kumshinda mwamini moja kwa moja,  hivyo hupenda kuinua ujasiri wake kama silaha, na akiwa mbali anajua akirusha mishale yake kisha Yule mtu akiiogopa basi anamwangusha. Ndio hapo huleta vitisho, mfano wa kipindi kile cha wana wa Israeli walipopewa agizo la kwenda kumjengea Mungu nyumba Yerusalemu, tunasoma baada ya kipindi kifupi maadui zao wakainuka, na kuwasemelea kwa mfalme, hatimaye marufuku ikatoka, wasiendeleze ujenzi, hivyo mahali pa Mungu pakabaki gofu tu la msingi kwa muda mrefu, kisa hofu ya utalawa mpya. Lakini baada ya muda mwingi sana, tunaona Mungu akawaamsha  mioyo Hagai pamoja na Zekaria, na kuwaambia  Israeli kwanini wameacha kuijenga nyumba ya Bwana.  (Hagai 1:1-9), walipogundua makosa yao, kwa kuruhusu hofu, Ndipo walipoamka kwa ujasiri tena na kuijenga, Mungu akawafanikisha sana.

Vivyo hivyo na sisi, tumepewa agizo la kuhubiri injili, ikiwa itapingwa, au tutatishiwa kuuawa au kufungwa, ikiwa tutapitishwa kwenye miiba au miamba hatupaswi kuogopa mishale hiyo, bali tusimame kwa imani kama akina Shedraki na Danieli, wakiwa katika matanuru ya moto, na matundu ya simba hawakutetereka. Bali walimtumaini Mungu anayewaokoa, na hatimaye kweli ikawa vile.

Hivyo kwa hitimisho ni kwamba ipo kweli mishale mingi ya moto, ya adui lakini hiyo mitatu ndio mikuu. Na tukiweza kusimama kwa imani basi shetani pande zote anakuwa ameshindwa kabisa kabisa, (Akiwa karibu na vilevile akiwa mbali) linda kinywa chako /puuzia/ pima maneno unayoyasikia, vilevile kuwa mwombaji ili usiingie majaribuni/ uyashinde majaribu, Lakini zaidi sana kamwe usiogope vitisho vya adui, kwasababu hawezi kufanya lolote kwa ihari yake mwenyewe.

Mungu akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Silaha za Mkono wa kuume na za mkono wa kushoto ni zipi

Nini maana ya Dirii, Chapeo na Utayari?

TUZIDI KUWA HODARI KATIKA BWANA.

Print this post

FUNDISHA KILE UNACHOKITENDA NA KUKIISHI

Kamwe usifundishe kitu ambacho wewe mwenyewe hukitendi.. Usiwafundishe wengine kumcha MUNGU ilihali wewe mwenyewe uko mbali na MUNGU!.. Usiwafundishe wengine umuhimu wa kuomba ilihali wewe mwenyewe hufanyi hivyo..

Kuna madhara makubwa ya kuwafundisha watu kitu ambacho wewe mwenyewe hukifanyi au hukiwezi.. Katika Biblia walikuwepo Mafarisayo ambao walikuwa wanawatwika watu mizigo ambao wao wenyewe hawakuiweza..

Mathayo 23:2 “Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa;

3 basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi.

4 Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao”.

Na tena kitabu cha Warumi kinazidi kuliweka hilo vizuri zaidi…

Warumi 2:21 “basi wewe umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe?

22 Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu?

23 Wewe ujisifuye katika torati, wamvunjia Mungu heshima kwa kuiasi torati?

24 Kwa maana jina la Mungu latukanwa katika Mataifa kwa ajili yenu, kama ilivyoandikwa”.

Mitume wa Agano jipya pamoja na Manabii wa agano la kale, hawakuwahubiria watu vitu wasivyoviishi wao, bali waliwafundisha watu yale wanayoyaishi ili wawe vielelezo..

Ezra 7:10 “Kwa maana huyo Ezra alikuwa ameuelekeza moyo wake KUITAFUTA sheria ya Bwana, na KUITENDA, na KUFUNDISHA maagizo na hukumu katika Israeli”.

Hapa Ezra kwanza alianza kwa KUITAFUTA sheria ya Bwana, na AKAITENDA na ndipo AKAWAFUNDISHA wengine..  Ni lazima na sisi tupitie hizi hatua tatu; KUTAFUTA, KUTENDA na KUFUNDISHA.

Tukiiruka ile ya kwanza na ya pili na kuifanya hiyo ya Tatu ya kufundisha, hatutakuwa mashahidi wazuri, na wala ushuhuda wetu hautakuwa na nguvu, tutakuwa ni mashabiki wa injili na si wahubiri wa Injili.. Injili inahubiriwa kwanza katika matendo ndipo mafundisho, hatuwezi kufundisha tusichokitenda!, hapo tutakuwa waongo, au watu wa kutafuta faida zetu.

Bwana YESU atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MWOMBENI BWANA WA MAVUNO APELEKE WATENDA KAZI.

TENDA AGIZO LA YESU, HILO NDIO LITAKALOKULINDA.

MATENDO YETU YANAPIMWA KATIKA MIZANI.

Mtande ni nini? Ni funzo gani lipo nyuma yake?

Utakuwa Kichwa na si Mkia maana yake nini? (Kumbukumbu 28:13).

Print this post

Kwanini Roho Mtakatifu amzuie Paulo kuipeleka injili Asia? (Matendo 16:6-7).

Jibu: Turejee Matendo

Matendo 16:6 “Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, WAKIKATAZWA NA ROHO MTAKATIFU, WASILIHUBIRI LILE NENO KATIKA ASIA.

7 Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa,

8 wakapita Misia wakatelemkia Troa”.

Biblia haijataja sababu za moja kwa moja kwanini Roho Mtakatifu awazuie wasiingie Asia kuhubiri injili lakini zifuatazo zinaweza kuwa sababu za Roho Mtakatifu kuwazuia Paulo na wenzake wasiingie hiyo miji kuhubiri injili.

   1. WAKATI WA INJILI KWA HIYO MIJI ULIKUWA HAUJAFIKA.

Kila mahali pana wakati wake wa kuhubiri injili kulingana na mapenzi ya Mungu, kwamfano kuna wakati ambao injili ilikuwa haijaruhusiwa kuhubiriwa kwa watu wa mataifa isipokuwa wayahudi tu peke yao, na kipindi hiko ni kile ambacho Bwana YESU alikuwa yupo bado duniani.

Mathayo 10:5 “Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie.

6 Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.

7 Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia”.

Maneno hayo ya Bwana Yesu yanaonyesha kuwa wakati wa injili kwa watu wa mataifa ulikuwa haujafika, lakini haikumaanisha kuwa Mataifa hawakuwa katika mpango wa Mungu wa kupokea Injili, walikuwepo lakini muda wao ulikuwa bado haujafika.

Na hapa katika Asia ni hivyo hivyo, huwenda muda wao wa kufikishiwa injili ulikuwa bado.

    2. WATUMISHI WENGINE WALIKUWEPO WAKIHUBIRI INJILI.

Kama muda wao wa kupokea Injili ulikuwa umefika na bado Roho Mtakatifu akawazuia akina Paulo kufika miji hiyo, sababu nyingine ni kwamba labda walikuwepo watumishi wengine wakihubiri katika hiyo miji, hivyo hakukuwa na haja ya akina Paulo kwenda huko tena wasije wakajenga juu ya msingi wa wengine kama Neno la Mungu linavyosema katika Warumi 15:20.

Warumi 15:20 “kadhalika nikijitahidi kuihubiri Injili, nisihubiri hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine”

    3. WATUMISHI WENGINE WAMEKUSUDIWA KWENDA KUHUBIRI KATIKA HIYO MIJI.

Na kama hakukuwa na watumishi wengine waliokuwa wanahubiri katika miji hiyo, basi sababu nyingine ya Roho Mtakatifu kumzuia Paulo na wenzake kufika huko Asia huwenda ni kwasababu Roho Mtakatifu alikuwa amepanga/kusudia watumishi wengine ndio wakahubiri kwenye hiyo miji mbali na Paulo na wenzake.

Kikawaida Roho Mtakatifu ndiye anayepanga watu na mahali watakapokwenda..Paulo asingeweza kwenda miji yote peke yake, ni wazi kuwa ipo miji mingine ilikusudiwa kupelekewa injili na watumishi wengine/mitume.

    4. WALIIKATAA INJILI.

Hii yaweza kuwa sababu ya mwisho ya Roho Mtakatifu kuzuia injili isiingie Asia kupitia Paulo na wenzake… Inawezekana Roho Mtakatifu alishatanguliza watu huko waliohubiri Neno la Mungu lakini wakaikataa ile injili.. na matokeo yake ni kufungiwa dhambi sawasawa na  Yohana 20:22-23..

Yohana 20:22 “Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu.

23 Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa”.

Kufungiwa dhambi kunakuja pale ambapo Neno la Mungu linahubiriwa kwa watu na wale watu wanalikataa kwa makusudi na hata kuwaua au kuwafukuza watumishi wa MUNGU, inapotokea wale watumishi wanakung’uta mavumbi kwenye miguu yao na kuondoka hapo wanakuwa wameufungia dhambi ule mji au mtaa, matokeo yake ni kwamba Roho Mtakatifu hawezi tena kupeleka wahubiri hapo mahali, wale watu watabaki vile vile kwasababu walishamkataa Roho Mtakatifu.

Mathayo 10:14 “Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, KUNG’UTENI MAVUMBI YA MIGUUNI MWENU.

15 Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule”.

Tunachoweza kujifunza ni kuwa Injili sio kitu kinachoweza kupatikana kila wakati, upo wakati ambapo Neema ikishaondoka mahali hairudi, au hata ikirudi yaweza kuchukua muda sana, hivyo hatuna budi kuiheshimu sana Neema ya Mungu.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Je Paulo, alihimiza kusikiliza nyimbo za kidunia kulingana na Matendo 17:28

Paulo aliwapaje watu karama ya rohoni?

Je ni sawa kuukubali udhaifu kama mtume Paulo alivyojisifia kwa huo? (2Wakorintho 12:9-10)

Kwanini Paulo, alihukumu wakati hukumu hairuhusiwi?

Paulo alikuwa anamaanisha nini kusema “Mnatenda vema kuvumiliana naye” (2Wakorintho 11:4).

Print this post

Chakula kigumu mfano wake ni upi kama tunavyosoma katika Waebrania 5:12?

SWALI: Biblia inasema maziwa ni kwa watoto wachanga, lakini chakula kigumu ni cha watu wazima. Mfano wa chakula hichi kigumu ni kipi?

Waebrania 5:12 Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. 13 Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. 14 Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya

JIBU:

Kabla ya kufahamu hicho chakula kigumu, ni vema kujua kwanza maziwa ni yapi.

Hivyo ukiendelea kusoma  vifungu vinavyofuata anasema..

Waebrania 6:1 Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu, 2 na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele. 3 Na hayo tutafanya Mungu akitujalia.

Sasa hayo mafundisho ya kwanza ya Kristo ndio maziwa. Yaani Mafundisho ya toba, imani kwa Mungu, ubatizo, kuwekewa mikono, kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele ni mafundisho ya watoto wachanga..kiroho hujulikana kama maziwa..

Kimsingi mtoto akiendelea kunywa maziwa tu peke yake daima, kitakachotokea baadaye ni kudumaa kama sio kufa kabisa, hivyo itafika wakati tu atahitaji chakula kingine ili aendelee kuishi. Vivyo hivyo na sisi, vipo vyakula ambavyo tunapaswa tule, kwa jinsi tunavyoendelea kukua kiroho.

Vifuavyo ndio vyakula vigumu vya kiroho vya watu wazima:

1) Upendo kwa maadui

Mathayo 5:44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,

Kwanini ni chakula kigumu?. Kwasababu jambo hilo linaenda kinyume na asili ya mwanadamu, linafunua asili ya ndani kabisa ya Kristo, ambayo si rahisi mtu aliyemchanga kiroho, kuielewa, au kulipokea nyakati za mwanzoni, yaani kumwombea  na kumpenda Yule ambaye anaiwinda roho yake au aliyemjeruhi, ..

2) Makusudi ya Mungu katika mateso

Wafilipi  1:29 Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake;

Kwanini ni chakula kigumu?. Kwasababu mwamini mchanga, mara nyingi atapenda kuambiwa maneno ya faraja, baraka, na mafanikio, awapo kwa Kristo,  lakini mkristo aliyekomaa, anayaona mapenzi ya Mungu pia hata katika majaribu na kuyashangalia.

1Wathesalonike 3:3 mtu asifadhaishwe na dhiki hizi; maana ninyi wenyewe mnajua ya kuwa twawekewa hizo

Soma pia 1Petro 1:6-8, 4:13, Wakolosai 1:24, Luka 6:22-23

3) Upambanuzi wa kiroho

Waebrania 5:14 Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya

Mkristo aliyekomaa kiroho, anafundishwa na Mungu kutambua na kugawanya vema mambo yote, kujua vilivyo najisi na visivyo najisi, mafundisho ya kweli na yale ya uongo, anafundishwa, busara, ujuzi na hekima hata katika kuhubiri injili kwa makundi yote, bila kuanguka na kunajisika, kwasababu amepewa roho ya upambanuzi ambayo huja kwa kuzoeshwa na Mungu kwa kipindi Fulani cha muda kupitia  Neno lake.

1Wakorintho 9:20 Nalikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi; kwa wale walio chini ya sheria, nalikuwa kama chini ya sheria, (ingawa mimi mwenyewe si chini ya sheria), ili niwapate walio chini ya sheria.

21 Kwa wale wasio na sheria nalikuwa kama sina sheria, (si kwamba sina sheria mbele za Mungu, bali mwenye sheria mbele za Kristo), ili niwapate hao wasio na sheria. 22 Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu.

Soma pia, 1Wakorintho 8:6-13, Yohana 2:1-12, Mathayo 11:19.

Kwanini ni chakula kigumu? Kwasababu mtu ambaye ni mchanga kiroho, akijihusisha katika viwango hivyo, hupotea na kunajisika kama sio kupotea kabisa. Ndicho kilichowatokea Adamu na Hawa kuuvamia mtu wa ujuzi wa mema na mabaya nje ya ratiba ya Mungu, matokeo yake wakayavuna mabaya, wala sio mema.

4) Kuikubali Fimbo ya Mungu.

Katika wokovu ipo fimbo ya Mungu; Mzazi yoyote huwa hatoi zawadi tu, sikuzote, hacheki na mwanawe siku zote, lakini pia kuna wakati fimbo hutumika, Vivyo hivyo Mungu ni Baba yetu, huadhibu, pale tunapokosea..

Waebrania 12:11 Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani.

Kwanini ni kigumu? Kukubali marekebisho kwa kuadhibiwa kama sehemu ya kutengenezwa na Mungu, si jambo rahisi mtu kulikubali mkristo ambaye hajakomaa. Yeye atakachojua tu, kuwa Mungu ni upendo.

5) Kujikana na kuubeba msalaba.

Luka 9:23 Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.

Kwanini ni chakula kigumu? Aliye mchanga kiroho kukubali kukataa mapenzi , kuingia gharama kuacha vyote na kuyakubali ya Mungu tu, si jambo rahisi kwa mwanafunzi wa ngazi ya chini.

6) Unyenyekevu na kujitoa kwa wengine.

Wafilipi 2:3 Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.

4 Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.

5 Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;

6 ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;

7 bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;

8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba

Kwanini ni chakula kigumu?.

Mkristo mchanga kiroho, si rahisi kuangalia mambo ya wengine, mfano wa Kristo, si rahisi kujinyenyekeza na kukubali kutembea kama mtumwa ili kuwatumikia wengine.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Print this post