Category Archive Uncategorized @sw-tz

Maana ya Mithali 25:25 Kama vile maji ya baridi kwa mtu mwenye kiu 

SWALI: Nini maana ya

Mithali 25:25 Kama vile maji ya baridi kwa mtu mwenye kiu, Ndivyo ilivyo habari njema itokayo katika nchi ya mbali.

JIBU: Biblia inalinganisha burudiko kubwa mtu analolipata pale anaposikia habari fulani njema na mfano wa mtu mwenye kiu halafu ghafla akaletewa kikombe cha maji ya baridi, sasa katika mazingira kama hayo ni wazi kuwa maji yale atayafurahia sana kwasababu yupo katika kiu.

lakini kiini cha mstari huo ni hapo anaposema ni habari njema ITOKAYO KATIKA NCHI YA MBALI.

Tukumbuke kuwa zipo habari njema nyingi..kwamfano habari za kupewa tenda fulani ya kibiashara ni habari njema, habari za kufaulu darasani ni habari njema, habari za kuzaliwa mtoto duniani ni habari njema, habari za kupandishwa cheo ni habari njema n.k…lakini zote hizi hazina jipya kwasababu ni za hapa hapa tu duniani.

Bali zipo habari njema zinazotoka katika nchi ya mbali na huko si kwingine zaidi ya MBINGUNI, hizo ndizo watu wana kiu nazo, wakizisikia tu ni lazima mioyo yao ni lazima iburudike sana.

Na habari zenyewe ni zile zinazomuhusu  Yesu Kristo.

Alisema.

Yohana 6:33-35

[33]Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.

[34]Basi wakamwambia, Bwana, sikuzote utupe chakula hiki. 

[35]Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe.

Yesu ndio maji yakatao kiu, alileta habari njema iliyotoka mbinguni, alikuja kutuletea ukombozi na msamaha wa dhambi, alikuja kutufungua katika vifungo vyetu, na shida zetu mbalimbali, na kutumwagia karama za rohoni, mambo ambayo mwingine yoyote hawezi kutoa. Lakini zaidi sana alikuja kutuambia habari za ufalme wake, kwa habari ya mambo yanayokuja, kuhusu mbingu mpya na nchi mpya, na Yerusalemu mpya, na umilele, na uzuri na thawabu alizotuandalia sisi tuliomwamini. Mambo ambayo ukisikia kama wewe unapenda kweli maisha…utayafurahia sana.

hivyo yatupasa mimi na wewe tuwe na mwitikio huu, wa habari hizi njema kwa kuwashuhudia pia na wengine maji haya, kwasababu ni wazi kuwa wengi wana kiu, na hivyo wanahaja ya kuzisikia hizi habari njema zimuhusuyo Yesu Kristo.

Sote kwa pamoja tuamke tukahubiri injili. Tukijua kuwa inahitajiwa sana.

shalom

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

INJILI NI NINI?

Maana ya Mithali 17:22 Moyo uliochangamka ni dawa nzuri;

KAMA UNAPENDA MAISHA, NA KUTAKA SIKU YAKO IWE NJEMA.

Rudi Nyumbani

Print this post

AINA TATU ZA IBADA ZA SANAMU.

Jina la Bwana na Mwokozi wetu YESU KRISTO libarikiwe, karibu tujifunze biblia Neno la Mungu wetu, lililo Taa ya njia zetu na Mwanga wa njia yetu (Zab. 119:105).

Zipo aina tatu (3) za sanamu zinazoabudiwa na watu.

1.Sanamu zenye mfano wa Mtu

2.Sanamu-watu

3.Sanamu-vitu

Tutazame moja baada ya nyingine.

      1.SANAMU ZENYE MFANO WA MTU.

Hivi ni vitu vyote visivyo na uhai vyenye mfano wa mtu, ambavyo vinatengenezwa na watu kwa lengo la kuabudiwa.

Tabia ya hizi sanamu kulingana na biblia ni kwamba zina midomo lakini hazisemi, zina macho lakini hazioni, zina masikio lakini hazisikii, zina pua lakini hazinusi..na wanaoziabudu wanafanana na hizo kiroho.

Zaburi 115:4 “Sanamu zao ni fedha na dhahabu, Kazi ya mikono ya wanadamu.

5 Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni,

6 Zina masikio lakini hazisikii, Zina pua lakini hazisikii harufu,

7 Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, Wala hazitoi sauti kwa koo zake.

8 Wazifanyao watafanana nazo, Kila mmoja anayezitumainia”

Hizi ndio zile zote zinazoabudiwa na wapagani, pamoja na baadhi ya madhehebu yajiitayo ya kikristo. Utakuta sanamu imewekwa ndani ya nyumba ya ibada, na watu wanakwenda kuiangukia na kuisujudia, hata kuitolea sadaka na kuiomba, jambo ambalo ni machukizo makubwa..

Ni dhambi kubwa kusujudia sanamu yoyote ile, Kasome Kutoka 20:1-6.

2. SANAMU-WATU.

Hii ni aina  ya pili ya sanamu ambayo ni tofauti kidogo na ile ya kwanza… ile ya kwanza ina midomo lakini haisemi, ina macho lakini haioni, ina masikio lakini haisikii…. Hii ya pili nayo ni hivyo hivyo, ina macho lakini haioni, ina masikio lakini haisikii, ina macho lakini haioni..tofauti tu ni kwamba ile ya kwanza ile ya kwanza haipumui ila hii ya pili inapumua, ile ya kwanza imetengenezwa kwa miti, udongo, chuma, fedha au dhahabu lakini hii ya pili ni Wanadamu.

Sasa tunaisoma wapi katika biblia…

Ezekieli 12: 1 “Neno la Bwana likanijia tena, kusema,

2 Mwanadamu, wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, WATU AMBAO WANA MACHO YA KUONA, ILA HAWAONI, WANA MASIKIO YA KUSIKIA, ILA HAWASIKII; kwa maana ni nyumba iliyoasi”.

Umeona? Kumbe sanamu sio tu mawe na udongo vinavyoweza kuwa sanamu bali hata watu..

Kama hujamaanisha kumfuata YESU wewe ni SANAMU.. Kwasababu una macho lakini huoni mambo ya rohoni, una masikio lakini husikii sauti ya MUNGU, Una kinywa lakini hakineni mambo ya Mungu, Hivyo wewe ni sanamu pamoja na viungo vyako vyote.

“KICHWA” chako ni sanamu/mungu wako, ndio maana unakitumikia kwa vitu vya kidunia kama YEZEBELI..

“MASIKIO” yako ni sanamu/mungu wako, ndio maana unayatumikia kwa kubadilisha vipuli kila siku.

“MACHO” yako ni sanamu/mungu wako, ndio maana unayatumikia usiku na mchana kupaka uwanja, na kupadilisha kope pamoja na kuchonga nyusi.

“MDOMO” wako ni sanamu/mungu wako, ndio maana unautumika kwa rangi na kila aina ya lipstick

“MIKONO” yako na “MIGUU” ni sanamu/mungu wako, ndio maana unaitumika kwa bangili na kucha za bandia..

“TUMBO” lako ni mungu wako ndio maana unalitumikia kwa kulinywesha pombe na kuliburudisha kwa kila linachohitaji usiku na mchana… Huna muda wa kufunga na kuomba walau kwa wiki mara moja, kwako kufunga ni adhabu kubwa!!..

Wafilipi 3:19  “mwisho wao ni uharibifu, MUNGU WAO NI TUMBO, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani”.

Ikiwa hujamaanisha kumfuata YESU kila kiungo katika mwili wako ni sanamu/mungu.. Ndio maana biblia inasema tuvifishe viungo vyetu vilivyo katika nchi, maana kwa hivyo huzaa dhambi na NDIO ibada ya sanamu.

Wakolosai 3:5 “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu;

6  kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu”.

     3. SANAMU-VITU.

Hizi ni sanamu zote zisizo na mwonekano au maumbile ya mwanadamu lakni zinaabudiwa.

Mfano wa hizi ni kazi, fedha, umaarufu, Elimu, Mali kama nyumba, magari, ardhi n.k. Mtu akiwa na hivi na hana KRISTO maishani mwake ni mwabudu sanamu tu!

KUMBUKA: Usipomwabudu MUNGU  WA KWELI, basi unaabudu sanamu, na usipoabudu sanamu basi unamwabudu MUNGU WA KWELI, Hakunaga hapo katikati! Ni aidha uwe wa shetani au wa Mungu.

Kama kazi yako inaheshima kuliko Mungu kiasi kwamba unakosa hata siku moja ya wiki kumtolea Mungu wako, hiyo kazi ni sanamu/mungu kwako.

Kama elimu yako, au umaarufu wako au cheo chako kina nguvu kuliko Neno la MUNGU, basi hicho ulichonacho tayari ni mungu wako.

Je umeokoka?…Kumbuka wote wanaoabudu sanamu sehemu yao ni katika lilwe ziwa liwakalo moto na kiberiti kulingana na biblia.

Ufunuo 21:8 “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, NA HAO WAABUDUO SANAMU, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.

Biblia inamaanisha nini kusema Yeye aliye na sikio, na asikie?

USIMWABUDU SHETANI!

MAJARIBU MATANO (5) YA MKRISTO.

DANIELI: Mlango wa 3

Rudi Nyumbani

Print this post

Maana ya Mithali 17:22 Moyo uliochangamka ni dawa nzuri;

SWALI: Nini maana ya

Mithali 17:22 Moyo uliochangamka ni dawa nzuri; Bali roho iliyopondeka huikausha mifupa.


JIBU: Mstari huu unatuonyesha jinsi gani hali ya moyo inavyoweza kuathiri hali za nje za mwili. Si kila wakati dawa itatibu, ikiwa moyo umepondeka afya inaweza kuathiriwa pia. Kwamfano labda mtu yupo katika nyumba au makazi ambayo hana amani, anateswa, anaudhiwa, anaabishwa, muda wote anakuwa mnyonge, utaona pia kwa namna Fulani afya yake itaathirika, labda atasumbuliwa na ugonjwa Fulani ambao hauna sababu wala chanzo.

Lakini moyo ukichangamka, hata kama huyo mtu yupo katika hali/mazingira magumu kiasi gani, mwili wake pia baada ya mda utaitikia hali ya roho yake. Na hivyo atakuwa na afya yake.

Sasa Nitaufanyaje moyo wangu uchangamke?

1)    Kwa kutembea ndani ya ahadi za Mungu katika Neno lake. Mara kadhaa katika maandiko Bwana Yesu alisema” jipeni moyo”. Unapojipa moyo katika ahadi za Mungu ukijua kabisa, ni hakika atatenda,hasemi uongo, Fahamu kuwa utakuwa ni mwanzo wa kuchangamka kwako. Kwamfano ukikumbuka kuwa alisema hatatuacha wala kutupungukia, unakuwa na amani wakati wote, nyakati zote, ukiwa na vingi ukiwa umepungukiwa yote yatakuwa sawa tu, kwasababu sikuzote yupo pamoja na wewe. Furaha inakutawala.

Hata upitiapo magonjwa, ukikumbuka ahadi zake kuwa atakuponya, ukaendelea kuzishika kwa imani, afya yako hurejea.

Yeremia 30:17 Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema Bwana, kwa sababu wamekuita, mwenye kutupwa, wakisema, Ni Sayuni, ambao hapana mtu autakaye. 

18 Bwana asema hivi, Tazama, nitarudisha tena hema za Yakobo zilizohamishwa, na kuyahurumia makao yake; nao mji huo utajengwa juu ya magofu yake wenyewe, nalo jumba litakaliwa, kama ilivyokuwa desturi yake. 

19 Tena kwao itasikiwa shukrani, na sauti yao WACHANGAMKAO; nami nitawazidisha, wala hawatakuwa wachache; tena nitawatukuza, wala hawatakuwa wanyonge.

Hivyo ishi kwa kushikilia ahadi za Mungu kwenye Neno lake, zipo nyingi sana, na zimefika katika kila Nyanja ya maisha yetu. Hakuna sababu ya kutochangamka, wakati Neno la ahadi lipo. Aliyekuahidia ni Mungu wa miungu muumba wa mbingu na nchi hakuna lolote linalomshinda, kwanini uogope?

2) Pili, kwa kupenda ushirika na wengine. Kamwe usiishushe wala kuipuuzia  nguvu iliyopo ndani ya ndugu katika Kristo. Zipo nyakati utahitaji kutiwa nguvu na wenzako, hata kukaa pamoja tu, kutafakari Neno la Mungu na kumwimbia Mungu ni tiba nzuri sana, itakayochangamsha moyo wako, tofauti na kama ungekuwa mwenyewe mwenyewe tu wakati wote.

Ndivyo ilivyokuwa hata kwa Paulo, wakati ule..

Matendo 28:15  Na kutoka huko ndugu, waliposikia habari zetu, wakaja kutulaki mpaka Soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, AKACHANGAMKA.

Chuma hunoa chuma, tuwapo pamoja, tunajengana nafsi, na matokeo ya kufanya hivyo yataonekana mpaka nje.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

PALE AHADI ZA MUNGU ZINAPOKUJARIBU.

JE! UNAIONA ILE NCHI NZURI YA KUMETA-META MBELE YAKO?

Je sisi wakristo tunaruhusiwa kufanya 40 za marehemu?

Rudi Nyumbani

Print this post

Maana ya Mithali 10:12 Kuchukiana huondokesha fitina

Elewa maana ya mstari huu;

Mithali 10:12 Kuchukiana huondokesha fitina; Bali kupendana husitiri makosa yote.

Mstari huu unalenga kutufundisha sifa za kipekee sana za upendo. Ambazo zinazungumziwa pia sehemu mbalimbali.

Kwamfano hapo anasema kuchukiana hakuzai kingine zaidi ya fitina,( yaani uchongezi, na kudhuriana), lakini upendano husitiri MAKOSA YOTE.  Anaposema yote. Ni kweli yote. Endapo upendo utatoka kwelikweli katika kilele chake. Hiyo ndio sifa ya ajabu ya upendo ambayo kitu kingine chochote chema hakiwezi kutoa, kwamfano imani, nguvu, mamlaka, uweza n.k. haviwezi kusitiri “makosa yote”. Ni upendo tu peke yake.

Neno hilo hilo pia limerudiwa katika agano jipya.

1Petro 4:8  Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana; kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi

Ndio maana Bwana Yesu alisema Torati yote imelalia hapo, katika kumpenda mwenzako kama nafsi yako, alisema  vile unavyotaka wewe utendewe watendee wenzako. Utashangaa tu, wivu unayeyuka wenyewe, hasira inakufa, vinyongo vinaondoka, mashindano yanapotea, wizi, uzinzi unafutika, kwasababu umegundua kuwa mwenzako ni kama hiyo nafsi yako mwenyewe, kama vile wewe unavyopenda kufanikiwa vivyo hivyo usichukie kuona mwenzako amefanikiwa.

Lakini Jambo hili linaweza kutoka ndani yetu kwa njia tatu. Ya kwanza ni kujazwa Roho Mtakatifu.  Kwasababu tunda mojawapo la Roho Mtakatifu ni upendo (Wagalatia 5:22). Hivyo unapokuwa mwombaji sana, hususani wa “masaa” sio dakika, unajazwa Roho Mtakatifu vema. Na matokeo yake ni kuwa urahisi wa kuudhihirisha upendo unakuja.

Lakini hilo peke yake halitoshi, unapaswa  uambatanishe na usomaji  wa Neno kila siku. Neno ni njia nyingine ya Roho Mtakatifu kukukumbusha, yale unayopaswa kufanya, kwamfano ukidhihirisha hasira ukisoma Neno utajifunza uvumilivu, utajifunza unyenyekevu, kuachia, na madhara ya kutokusamehe. Hivyo litakufanya uweze kurejea  kwenye mstari haraka pale unapokaribia kuteleza. Usipuuzie kusoma Neno kila siku.

Tatu, ni kutendea kazi. Lazima ujiwekee malengo. Kwasababu ukiwa mwombaji tu, na msomaji peke yake bado  haitakusaidia sana , kama huna mikakati ya kukifanyia kazi. Ndio maana hapo anasema iweni na JUHUDI nyingi katika kupendana,.Juhudi ni lazima yaani unaanza kuchukua hatua ya kushindana na vipinga-upendo, na hapo hapo utaanza kuona, wepesi umekuja ndani yako,

Sisi kama watoto wa Mungu, tumeagizwa tukue kila siku kuufikia upendo wa ki-Mungu ndani yetu. Ndio ukomavu wetu na kilele cha imani yetu. Kwasababu hii ndio dawa ya dhambi zote.(2Petro 1:5-11)

Bwana atuongezee neema.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Kuhubiri injili kwa husuda na fitina ndio kupi?

UMETEKWA NA UPENDO WA KRISTO?

UPENDO NI NINI NA JE! KUNA AINA NGAPI ZA UPENDO?

Rudi Nyumbani

Print this post

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA MATHAYO.

(Hotuba za Yesu)

Kitabu cha Mathayo ni moja ya vitabu vinne (4), vya injili. Yapo mambo mengi ya kujifunza ndani yake, lakini katika makala hii, tutaona mambo muhimu ya kufahamu ambayo yatakusaidia katika usomaji wako.

Tukiachia mbali matukio, na huduma mbalimbali ikiwemo za uponyaji alizozifanya Yesu. Tunafahamu kuwa Bwana “ALIFUNDISHA” pia. Na hapa ndipo kiini cha kujifunza kwetu.

Hivyo katika kufundisha kwake, kuligawanyika mara mbili. Kuna taarifa ambazo alizotoa bila kutolea maelezo mengi, lakini pia kuna taarifa alizitoa kama hotuba.

Sasa tutaangazia hizo HOTUBA, ambazo zimerekodiwa kwenye kitabu hichi.

Zipo tano (5), Nazo ni

  1. Hotuba ya Mlimani. (Mathayo 5-7)
  2. Hotuba ya utume (Mathayo 10)
  3. Hotuba ya ufalme wa mbinguni (Mathayo 13)
  4. Hotuba ya kanisa (Mathayo 18)
  5. Hotuba ya siku za mwisho (Mathayo 24)

Kabla ya kuziangalia kwa upana kidogo. Tufahamu kwanza hapo tusemapo “hotuba” tunamaanisha nini.

Hotuba ni mahubiri/mafundisho aliyoyasema Yesu kwa upana, yaliyolenga mada Fulani maalumu.

Ni mazungumzo marefu ya Bwana Yesu. kukazia jambo lile lile moja. Sasa embu Tuangalie kiini cha kila hotuba.

1) Hotuba ya mlimani. (Mwenendo wa Mkristo)

Hii tunaisoma katika sura ile ya 5,6,7. Ni wakati ambapo Bwana Yesu alipanda mlimani, kisha wanafunzi wake wakamfuata, akaanza kuwafundisha mambo mengi. Sasa kiini cha hotuba hii, kilikuwa ni kuwafundisha mwenendo sahihi wa Mkristo, unaokubaliwa na Mungu.

Anaanza kwa kusema HERI, HERI, HERI, maskini wa roho, wapole, wenye rehema, wapatanishi, wenye moyo safi, wenye kiu na njaa ya haki, n.k. anaendelea jinsi tunapavyopaswa tuwapende maadui, tusamehe, tusilipize kisasi, akafundisha usahihi wa kuomba, kufunga, kutoa sadaka, usafi wa moyo, na upendo, na mambo mengine kadha wa kadha.

Ni maneno ambayo kama wewe ni mwamini basi unapaswa uyasome na kuyatafakari kila inapoitwa leo. Kwasababu Huu ndio uliokuwa mwenendo wa Yesu duniani. Akahesabiwa kumpendeza Mungu kabla hata hajaanza huduma yake ya kuhubiri, kwasababu aliishi aliyokuwa anayasema. Hivyo siri iliyopo hapa ni kwamba alikuwa anasema mwenendo wa maisha yake yalivyokuwa.

Na sisi pia tukitaka tufanane, na Kristo kimwenendo na tabia, basi tuzingatie sana, kuyaaishi haya tunayoyasoma katika sura hizi tatu yaani 5,6,7, Ni muhimu sana, sio kuimba “natamani kufanana na wewe”, lakini hatujui tunafananaje na yeye.

2) Hotuba ya Utume (Mathayo 10)

Katika mahubiri haya, Bwana Yesu aliwaita wanafunzi wake na kuanza, kuwapa maelezo ya namna ya kuhubiri kule atakapowatuma. Akawaeleza kwa upana jinsi mazingira ya kuhubiri yalivyo, kwamba kuna mahali pia hawatakubalika, akawafundisha pia jinsi ya kuhubiri, akawaondoa hofu ya wanadamu, na hofu ya kusumbukia mahitaji kwamba huko huko mbele ya safari Bwana atakuwa nao, akawafundisha pia mahali pa kuanzia kuhubiri, akawafundisha hekima ya kuhubiri, na kuponya watu. Na mambo mengine kadha wa kadha.

Kiasi kwamba, wewe kama mtendakazi katika shamba la Bwana ukisoma habari hizi, zitakusaidia katika ustahimilivu wako shambani mwa Bwana, tukikumbuka kuwa kila mmoja wetu ameitwa na Bwana kwenda kuwafanya wengine kuwa wanafunzi. Hivyo, Usomapo habari hii ya kitume, itakusaidia kunoa vema utumishi wako, katika eneo la upelekaji kazi ya Mungu mbali. Pata nafasi pitia wewe mwenyewe kwa utulivu sura yote ya kumi. Bwana atakupa kuelewa mengi ndani yake. Na hivyo utakuwa mtume, kama mitume wako walivyokuwa.

3) Hotuba ya ufalme wa mbinguni (Mathayo 13)

Hii ni hotuba, iliyohusu siri za ufalme wa Mbingu. Ambapo Bwana Yesu alitumia mifano (mafumbo), kuulezea. Biblia inaposema ufalme wa mbinguni, inamlenga YESU mwenyewe, na kazi yake aliyokuja kuifanya duniani (Luka 4:18-19).

Katika sura hii ya 13, alieleza mifano mikuu saba (7), japokuwa kulikuwa na mengine aliyokuwa iliyohusu ufalme wa mbinguni isipokuwa haijarekodiwa katika kitabu hichi. Mfano wa kwanza ulikuwa ni wa mpanzi, kisha magugu na ngano, kisha chembe ya haradali, kisha chachu katika unga, kisha hazina iliyositirika katika shamba, kisha mfano wa mfanyabiashara na lulu, na juya lililotupwa baharini.

Katika mifano hii yote, maudhui ni kuonyesha ukubwa ulio ndani ya Kristo Yesu, pale mtu anapomwamini na kustahimili kumfuata ukweli ni kwamba ataanza kama chenye ya haradali, lakini ataishia mti mkubwa, ni kama aliyepata hazina na lulu kubwa sana, akaenda kuuza akawa tajiri,.

Hivyo usomapo kwa makini mifano hii, utakuwa na kila sababu ya kuutafuta sana ufalme wa Mungu (yaani Kumuhufadhi Kristo sana moyoni mwako). Kwasababu unajua ulichokitapata ni zaidi ya vitu vyote duniani. Ambavyo utakuja kuvifurahia vema uendapo kule ng’ambo mbinguni.

4) Hotuba ya kanisa (Mathayo 18)

Hotuba hii inalenga, namna ya kuchukuliana sisi kwa sisi (Kanisa), tuliomwamini Yesu katika eneo la kujishusha na kunyenyekeana, kutokwazana, kutokupuuziana, lakini pia kuwa tayari kuwatafuta wale waliopotea na kuwarudisha kundini, ni muhimu sana, akatoa mfano wa mtu aliyeacha kondoo wake tisini na tisa, na kwenda kumtafuta Yule mmoja aliyepotea. Na sisi yatupaswa tuwe na moyo huo wa kichungaji.

Vilevile kusameheana sisi kwa sisi hata saba mara sabini akatoa mfano wa Yule mtu aliyesamehewa talanta elfu kumi, lakini yeye hakuwa tayari kumsamehe aliyemdai dinari mia, pia alifundisha njia nzuri ya kuonyana kingazi kufatana na utaratibu kwa kikanisa.

Hivyo usomapo hotuba hii, utafahamu namna ambavyo Bwana anataka sisi tuishi kama ndugu tuwapo pamoja kama kanisa lake.

5) Hotuba ya siku za mwisho (Mathayo 24)

Hii ni hotuba inayohusu, matukio yote ya siku za mwisho wa dunia, na kurudi kwa Yesu kutakavyokuwa, anaeleza kwa urefu dalili zake, mabadiliko ya kimwenendo ya watu, yatakavyokuwa, majanga ya asili, na vita vitakavyofuata baadaye, anatoa tahadhari ya manabii wa uongo, unyakuo wa kanisa, dhiki kuu na mapigo ya Mungu, Na mwisho anatoa angalizo ni nini tunapaswa tufanye. Kwamba “Tukeshe”, kwasababu hatujui siku wala saa.

Hotuba hii ni vizuri ukaisoma kwa urefu, na kuelewa kwa undani, kwasababu nyakati tulizopo sasa, tupo katika “mwisho wa siku za mwisho.” Dalili nyingi zilizotabiriwa zilishatimia. Jiulize umejiandaaje kwa yaliyo mbele yetu?

Hivyo kwa hitimisho ni kuwa, ufahamupo Mahubiri hayo (Hotuba), utapata uelewa wa undani kimaudhui ndani ya kitabu cha Mathayo, Jifunze kusoma sana, na kurudia rudia, hotuba hizi, kulikuwa na sababu kwanini Bwana atoe habari zake kwa urefu, kwasababu ndio “Fundisho” la mwamini. Zingatia hayo na Bwana akubariki.

Tutakuwa na uchambuzi wa vitabu vingine..

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 2

UFALME WA MUNGU HAUPATIKANI KIRAHISI.

NENO LA MUNGU KATIKA UTIMILIFU WOTE.

ANGUKO LA UFALME WA SHETANI:

Rudi Nyumbani

Print this post

NI MAJIRA YAPI YA NEEMA WEWE UPO?

Kuna wakati wa kukokotwa-kokotwa, lakini kuna majira ya  kuachwa ufanye maamuzi mwenyewe, na usipofanya unakufa. Mtu aliye mchanga kiroho, ni rahisi Mungu kuchukuliana naye katika mambo yasiyofaa kutokana na uchanga wake kwa siku zile za awali, lakini haiwezi kuwa hivyo siku zote, kwa jinsi siku zinavyokwenda, kusukumwa sukumwa hakutakuwepo, ni kuwa makini sana!.

Ukitafakari habari ya Mke wa Lutu, unaweza kupata picha halisi jambo hili lilivyo, yeye alidhani ataendelea kuvutwa-vutwa tu nyakati zote, lakini walipofikishwa mahali Fulani, nje kidogo ya mji wameshaijua njia, waliambiwa wajiponye wenyewe nafsi zao, lakini yeye akageuka nyuma, na wakati ule ule akawa jiwe la chumvi.

Mwanzo 19:15 Hata alfajiri ndipo malaika wakamhimiza Lutu, wakisema, Ondoka, mtwae mkeo na binti zako wawili waliopo hapa, usipotee katika maovu ya mji huu. 

16 AKAKAWIA-KAWIA; nao wale watu wakamshika mkono, na mkono wa mkewe, na mkono wa binti zake wawili, KWA JINSI BWANA ALIVYOMHURUMIA, wakamtoa wakamweka nje ya mji. 

17 Ikawa walipomtoa nje, mmoja alisema, JIPONYE NAFSI YAKO USITAZAME NYUMA, wala usisimame katika hilo bonde po pote; ujiponye mlimani, usije ukapotea.

Hatari tuliyonayo sisi tuliopo katika siku hizi za mwisho, katika kanisa hili la Laodikia (Ufunuo 3:14-21), ni kwamba tunafahamu mambo mengi, na tumeshaona mifano mingi kwenye maandiko na kwenye historia, lakini geuko la dhati ndani ya wengi halipo, tukifikiri  tutalinganishwa na wale watu wa zamani. Neema kwako wewe haifanyi kazi katika kukokotwa tena, bali katika kukimbia. Ilifika wakati Yesu hakuwaambia tena wanafunzi wake “nifuate”, aliwaambia na “ninyi mnataka kuondoka?”

Halikadhali, kama umeshaokoka, jichunge sana, dhambi usiifanye rafiki kwako, ukidhani kila kosa tu utakalolifanya upo msamaha, acha hayo mawazo, unajitafutia kuwa mke wa lutu. Neno la Mungu linasema;

Waebrania 6:4  Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu,

5  na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo,

6  wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri.

7  Maana nchi inayoinywa mvua inayoinyeshea mara kwa mara, na kuzaa mboga zenye manufaa kwa hao ambao kwa ajili yao yalimwa, hushiriki baraka zitokazo kwa Mungu; 8  bali ikitoa miiba na magugu hukataliwa na kuwa karibu na laana; ambayo mwisho wake ni kuteketezwa.

Ni kusimama imara, sio tena kumbelezewa injili, sio tena kukumbushwa-kumbushwa wajibu wako wewe kama mkristo, na kuambiwa kaombe, nenda ibadani, mtafute Mungu, acha anasa, soma biblia. Ni wakati wa kujitambua kuwa sasa umeshatolewa nje ya mji, changamka, zama ndani ya Kristo. Acha kuwa vuguvugu utatapikwa, zama hizi ni zama za uovu. Wokovu wa mawazo mawili sio sasa, neema hiyo haipo kwetu mimi na wewe siku hizi za mwisho. Injili ya maneno laini, isikupumbaze, fanya Imara uteule wako na wito wako.

Ufunuo 22:10  Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia.

11  Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa

12  Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.

Kimbia, usiangalie nyuma.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Je! “majira na sheria” mpinga-kristo atakayokuja kubalisha ni kupindua siku ya sabato na kuwa jumapili?

Nini tofauti ya Majira na Wakati?

UMEJIANDAAJE KWA NYAKATI ZA KUWA PEKE YAKO?

WAKATI ULIOKUBALIKA NALIKUSIKIA

Rudi Nyumbani

Print this post

JE! UNATAKA UITWE MSOMI NA MUNGU?

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo, Karibu katika kuyatafakari maneno ya uzima.

Sulemani, mtoto wa Daudi, katika kitabu chake cha mhubiri, kilichojawa na utafiti wa hali ya juu wa mambo mengi ya kimaisha yamuhusuyo mwanadamu, Tunaona mwishoni kabisa mwa utafiti wake alihitimisha kwa maneno haya;

Mhubiri 12:11 “Tena, zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo; HAKUNA MWISHO WO WOTE WA KUTUNGA VITABU VINGI; NA KUSOMA SANA HUUCHOSHA MWILI. 

13 Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.

12 Tena, zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo; hakuna mwisho wo wote wa kutunga vitabu vingi; na kusoma sana huuchosha mwili. 

13 Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu”.

Sulemani alikuwa ni mtafiti sana, na kama kusoma na kutunga vitabu, basi alitunga vingi sana, na katika vyote (viwe Vya ki-Mungu na visivyo wa ki-Mungu ) alijaribu kutafuta siri, na mwongozo sahihi wa mwanadamu. Lakini tunaona akapata jawabu, ambalo ni rahisi sana kwa wote. Na jawabu lenyewe ni hili “kumcha Mungu na kuzishika amri zake”.

Akasema unaweza ukakesha kusoma vitabu vingi sana katika huu ulimwengu, na matokeo ya kusoma sana, ni kudhoofika, Na bado usipate ukweli mwingine zaidi ya ule ule “kumcha Mungu na kuzishika amri zake”. Ndio maana akahitimisha kwamba Mtu akizingatia sana hilo, laweza kuzidi usomaji mwingi tuuona hapa duniani.

Sasa kumcha Mungu na kuzishika amri zake maana yake ni nini?

Kumbuka biblia nzima inazungumzia habari za Yesu Kristo mwokozi wetu. Hivyo hapo ni sawa na kusema “Kumcha Yesu na kuzishika amri zake”. Hiyo Ni zaidi ya kuwa na maarifa ya vitabu milioni moja, au elimu za shahada elfu,. Ikiwa na maana yule mtu aliyemwamini Yesu, kisha akawa anaishi kwa kulifuata Neno lake, na kuitimiza amri yake kuu, ambayo alisema ni UPENDO. Huyo ni zaidi ya Msomi yoyote aliyewahi kutokea duniani. Au mtunzi yoyote mwenye hekima aliyewahi kuandika vitabu vingi. Ni mtu aliyemaliza kusoma vitabu vyote.

Yohana 13:34  Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo.

35  Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.

Hivyo, usisumbukie maarifa  mengi, ukadhani kuwa ndio utamwelewa Mungu, sumbukia Kristo moyoni mwako, sumbukia upendo wa agape moyoni mwako. Kwasababu huko kote utakapokwenda kutakurudisha hapo hapo, ndicho alichokigundua sulemani katika usomaji wake mwingi, hakuna jipya ndani yake Ni kujisumbua tu, ndio maana biblia inasema, yapo mambo mengi aliyoyafanya Yesu na kama yangeandikwa basi vitabu vyote visingetosha duniani.

Yohana 21:25  Kuna na mambo mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa.

Umeona? Vitabu visingetosha kuandika mambo yote ya Yesu, kwasababu maudhui yake ndio yaleyale, tunayoyasoma katika maneno machache ya kwenye biblia. Ambayo ni wokovu na Upendo wa Mungu. Tukiyatimiza hayo ni sawa na kusoma vitabu vyote duniani.

Hivyo mimi na wewe tuanze kuweka juhudu, kimatendo, kutendea kazi Neno lake, zaidi ya kuhangaika kutafuta maarifa mengi. Kwasababu anasema mwenyewe chanzo cha maarifa ni kumcha yeye, na sio chanzo cha kumcha yeye ni maarifa.

Kumbuka pia asemapo kusoma kwingi huuchosha mwili, hamaanishi uwe mjinga usiwe msomaji kabisa hapana, Lakini anakupa shabaha ni wapi uweke juhudi zako nyingi ili ufanikiwe kuwa na Maarifa ya kweli ya kisomi, Usije ukawa unaufuata upepo.

Tumia nguvu nyingi kuyatendea kazi yale yaliyopo kwenye biblia tu, zaidi ya mihangaiko mingi huku na kule, na elimu nyingi za kidunia.  Utaitwa Msomi na Mungu.

Bwana akubariki.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

JINSI YA KUSOMA BIBLIA.

Uchaji ni nini kama tunavyosoma katika 1Timotheo 2:10?

NI NANI ANAYEUFUNGA MLANGO WA MAARIFA?

Rudi Nyumbani

Print this post

FAHAMU KURUDI KWA YESU KUKO KWA NAMNA NGAPI?

Wengi, tumeshasikia kuwa Yesu atarudi, lakini mpaka mtu anasema atarudi, maana yake ni kuwa alishawahi kuja hapo nyuma. Na kama tunavyojua Bwana wetu Yesu Kristo alikuja mara moja tu, miaka karibu elfu mbili iliyopita, akaishi, akafa,akazikwa, akafufuka, akapaa mbinguni. Lakini wakati wote alipokuwa hapa duniani aliwaahidi wanafunzi wake kuwa atarudi tena.

Hivyo somo hili, ni muhimu kufahamu,  namna ambazo Yesu alisema atarudi, ili usikose maarifa, kwasababu wengi hapa wanakosa shabaha katika kutambua kauli za Yesu. Naomba Soma kwa utulivu somo hili mpaka mwisho.

Sasa kuhusu kurudi kwake duniani, alizungumza katika nyakati tofuati tofauti kurudi kwa namna mbili.

  1. Namna ya kwanza, ni kama Roho
  2. Namna ya pili ni kama Mwizi

Tuangalie kwa undani, namna hizi mbili. Husasani tutailenga hiyo ya pili.

Je! ni kwa namna gani, alirudi kama Roho,Aliwaambia hivi mitume wake;

Yohana 14:18  “Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu. 19  Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona. Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai.

20  Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu”.

Soma pia, katika Yohana 16:16, amerudia maneno hayo hayo,

Unaona? Mitume walidhani hawatamwona tena, lakini siku ile aliyopaa mbinguni,siku kumi baadaye, biblia inasema walikuwa wamekusanyika wote mahali pamoja, akawajilia Roho Mtakatifu akawakalia wote, wakajazwa Roho Mtakatifu. Na kama tunavyojua tangu huo wakati na kuendelea, kila mmoja alijua anaye Yesu moyoni mwake, hakuna mtu aliyeuliza Yesu yupo wapi.

Uyatima uliondoka kabisa, kabisa, ndipo wakatambua maana ya yale maneno. Hivyo tumeshaona kurudi kwake kwa kwanza duniani, kulikuja kwa namna hiyo ya Roho Mtakatifu, na mpaka sasa Kristo yupo ndani ya mioyo ya waliomwamini, na kupokea Roho Mtakatifu.

Lakini pia katika maneno yake mengine, alisema atarudi kama mwizi.

Soma,

Mathayo 24:43  Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.

44  Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.

Unaona tena?, Hajasema, atarudi kama askari, au mfanya biashara, bali kama mwizi. Sasa ni vema tujue sifa za mwizi, ni zipi kibiblia, ndipo tuelewe jinsi kurudi kwake kwa namna hiyo kutakavyokuwa.

Ukisoma Yohana 10:10  Yesu anasema hivi;  Mwivi haji ila AIBE na KUCHINJA na KUHARIBU; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele”.

Kumbe mwizi hasaa, anayezungumziwa ni mfano wa jambazi, na sio wale wadokozi, ni wale wanaobeba silaha, ili kuharibu na kuua wanaowaona, wachukue mali yao waondoke.

Na Yesu ndivyo atakavyokuja katika siku za mwisho hizi, atatimiza sifa hizo zote tatu.

1.) Jambo la kwanza Atakuja saa tusiyodhani, Kisha ATAIBA kitu chake cha thamani duniani. Ni hicho si kingine zaidi ya watakatifu wake. Hapo ndio suala la unyakuo linapoibukia.

Mathayo 24:40  Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; 41  wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.

2) Lakini pamoja na hilo, kuja kwake kutaambatana na KUCHINJA.

Maana yake ni kwamba, kama unyakuo utakupita, dunia itakuwa inajiandaa kuingia katika siku ile ya mapigo ya ghadhabu ya Mungu, ambayo mwisho wake utaishia na Kristo kuonekana katika umbile la kibinadamu kabisa, kuwaua mataifa yote ambayo yatakusanyika kupigana naye katika ile vita kuu ya Harmagedoni.

Ufunuo 19:11  Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita.

12  Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe.

13  Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu.

14  Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi.

15  NA UPANGA MKALI hutoka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi.

16  Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANAWA MABWANA.

Huu ni wakati ambao Yesu, atauangamiza  ulimwengu, mfano wa mwizi, asiyekuwa na huruma. Usitamani uwepo wakati huo ndugu, ni majuto vilio na kusaga meno.

3) Lakini mwisho kabisa, ATAHARIBU.

Tunafahamu kuwa mwizi, huvunja, mahali ili aingie, huvuruga kila kitu anachokiona, vivyo hivyo na hii dunia itafumuliwa yote, mifumo yote itaangushwa, itafinyangwa upya, yote hayo yatatokea katika siku hiyo hiyo ya Bwana, ambayo itaharibu kila kitu.

2Petro 3:10  Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea. 11  Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa, 12  mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka?

Soma pia,(Ufunuo 16:17-21), kuongeza maarifa..

Hivyo ndugu, wakati huu wa Yesu kurudi kama mwizi umekaribia sana, ambao utaanza  Kwanza kwa tukio la unyakuo. Bwana anatutaka sisi tukeshe(rohoni), asitukute tumelala. Ili Siku hiyo isitujilie ghafla, tukabaki hapa duniani.

1Wathesalonike 5:1  Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.

2  Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.

3  Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.

4  Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi.

5  Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza.

6  Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.

7  Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku. 8  Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu.

Bwana atupe macho ya kuona haya.

Je! Umempokea Yesu maishani mwako, Je! Ameziondoa dhambi zako? Kama jibu ni la, unasubiri nini? Hujui kesho kama utakuwepo, hujui kama leo atarudi. Hivyo tubu sasa, mwamini Yeye upate ondoleo la dhambi zako, kisha utapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Ikiwa utapenda kupokea wokovu basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii bure. Bwana akubariki.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

USILALE USINGIZI WAKATI WA KUMNGOJEA BWANA.

KAMA MWIZI USIKU WA MANANE.

Kuna tofauti gani kati ya “Mwivi” na “Mwizi”?

Fahamu Namna ya Kuomba.

Rudi Nyumbani

Print this post

Kuapiza ni nini? (Mathayo 5:21-22)

Mathayo 5:21  Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu. 22  Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto.

JIBU: Katika vifungu hivi tunaona Bwana Yesu anatoa mtazamo mpya kuhusiana na dhambi ya uuaji. Hapo mwanzo ilidhaniwa kuwa pale mtu anapochukua hatua ya kumchinja ndugu yake, au kumpiga mpaka kufa kama alivyofanya Kaini, ndio umehitimu kuwa muuaji. Lakini Bwana Yesu anasema..

Kitendo  tu cha kumwonea hasira ndugu yako, kumfyolea, na kumwapiza, tayari ni kosa la uuaji.

Sasa alikuwa na maana gani kwa maneno hayo matatu. “Hasira, kufyolea na kuapiza?”

Hasira kwa ndugu, huzaa mambo kama kinyongo, uchungu, na wivu. Kwahiyo kama mtu akiwa na mambo kama hayo  kwa ndugu yake, mbele ya Kristo amestahili kuhukumiwa.

Lakini pia akimfyolea. Kumfyolea ni kumwita mwenzako mjinga wewe, au mpumbavu wewe. Ukilenga mtu asiye na akili, Kwa urefu wa tafsiri hii fungua hapa>> RACA Hilo nao ni kosa lililostahili kuketishwa kwenye mabaraza ya wazee, utoe hesabu.

Lakini mbaya zaidi kumwapiza. Hichi ni kitendo cha kumtamkia kabisa maneno ya  laana. Kana kwamba ni mtu mwovu sana aliyepindukia. Kwamfano kumwita ndugu yako mwana-haramu wewe, au kumwita ‘shoga wewe’, kumwita msenge(neno lenye maana mtu anayeshiriki uovu kinyume na jinsia yake), kumwita pepo, kafiri wewe, n.k. maneno ambayo hayawezi kutamkika, ni sawa na tusi kwa mwenzako. Huko ndio kuapiza.

Adhabu yake Kristo anaifananisha na kutupwa katika jehanamu ya moto.

Hivyo hatupaswi kudhani kuwa, kuua ni mpaka tumwage damu, lakini twaweza kufanya hivyo tokea moyoni mwetu hadi vinywani mwetu, kabla hata hatujafikia kwenye kitendo chenyewe.

Tujazwe Roho Mtakatifu, tuwezi kuzishinda tabia hizi mbaya za mwili.

Katika agano la kale ilikuwa sio tu kumpiga mzazi wako, ilikupasa kifo (Kutoka 21:15), lakini pia kumwapiza huku, adhabu yake ilikuwa ni moja tu na hilo kosa la kwanza yaani kifo.

Kutoka 21:17 “Yeye amwapizaye baba yake au mama yake, sharti atauawa”

Shalom.

Je! Umeokoka? Fahamu kuwa usipomwamini Kristo, na kupokea msamaha wake wa dhambi, hauna uzima wa milele ndani yako. Kwasababu kamwe hutakaa umpendeze Mungu kwa nguvu zako au matendo yako mwenyewe. Na sababu ya Yesu kufa msalabani kwa ajili yako kukusaidia, kupokea msamaha wa dhambi, lakini pia nguvu ya kushinda mambo mabaya kwa Roho wake Mtakatifu tuliopewa. Ikiwa upo tayari kumpokea Yesu akuokoe leo, basi fungua hapa kwa mwongozo wa sala hiyo ya wokovu, Bwana akubariki >>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Amen

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Bwana alimaanisha nini kusema “atazamaye mwanamke kwa kumtamani” amezini naye?

Je ni sahihi kumwita mtu “Mkuu”?

SIKU YA HASIRA YA BWANA.

UFANYE MOYO WA MUNGU UWAELEKEE WATU WAKE.

Rudi Nyumbani

Print this post

Fahamu maana ya Isaya 24:16-18 Kukonda kwangu!

SWALI: Nini Maana ya Isaya  24:16-18, inapomzungumzia mwenye haki, na anaposema Kukonda kwangu!

Isaya 24:16 Toka pande za mwisho wa dunia tumesikia nyimbo, Atukuzwe mwenye haki. Ndipo niliposema, Kukonda kwangu! Kukonda kwangu! Ole wangu! Watenda hila wametenda hila, naam, watendao hila wametenda hila sana. 

17 Hofu, na shimo, na mtego, vi juu yako, Ee mwenye kukaa duniani. 

18 Itakuwa kila akimbiaye sauti ya hofu ataanguka katika shimo; na kila apandaye na kutoka shimoni atanaswa na mtego; kwa maana madirisha yaliyo juu yamewekwa wazi, na misingi ya dunia inatikisika


JIBU: Vifungu hivyo vinazungumzia unabii wa Masihi (Yesu Kristo) mwokozi wetu.

Katika mstari wa 16, nabii Isaya anaonyeshwa maono, ya nyimbo za “mwenye haki” ambaye si mwingine zaidi ya Kristo, Kwamba atukuzwe. Jambo ambalo ni la furaha, Kristo kuja duniani, ni tendo ambalo lilishangaliwa sio tu na malaika (Luka 2:8-14), lakini pia na wanadamu (Yohana 12:12-13).

Lakini tunaona katika sentensi inayofuata nabii Isaya, anaonyesha masikitiko yake, kwa kusema Kukonda kwangu! Kukonda kwangu!  Ole wangu, watenda hila wametenda hila.  Akifunua kimifano hali ya taabu na huzuni inayompelekea hata kupoteza afya kwasababu ya mienendo ya watu waovu baada ya pale. Yaani badala wampokee mwokozi, wengi walimpinga na kumkataa, wakamsulubisha, na kuukata wokovu, ulioletwa na huyo mwenye haki.

Hivyo katika vifungu vinavyofuata 17-18, Anaeleza hukumu itakayowapata waliopo duniani, kwa kosa la kumkataa masihi, akilenga hasaa siku ile kuu ya Bwana, siku ya mwisho ya ghadhabu ya Mungu ambayo hii dunia itaharibiwa kabisa pamoja na watu waovu. Ambapo kwa urefu wake, inaelezwa pia katika vifungu vinavyofuata.

Unabii ambao ni kweli kabisa, unapompinga Kristo leo, aliye mwenye haki, aliyekuja kukuondolea dhambi zako, huwezi kuikwepa jehanamu ya moto, kwasababu matendo yako pekee hayawezi kukufanya mkamilifu, vilevile katika siku za mwisho ikiwa utakuwepo duniani, huwezi kuyakwepa mapigo ya Mungu juu yako.

Hivyo mpendwa ni heri ukampokea Yesu leo, akusamehe dhambi zako. Jina lako liandikwe kwenye kitabu cha uzima. Mwisho umekaribia sana, Jiulize ukifa leo katika hali ya dhambi utaenda kuwa mgeni wa nani huko ng’ambo ufikapo?

Ikiwa upo tayari kuupokea wokovu leo, upate msamaha wa dhambi zako basi fungua hapa kwa mwongozo huo >>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Dunia inalewa-lewa kama mlevi, nayo inawaya-waya kama machela.

Nini maana ya Mithali 19:21Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la Bwana ndilo litakalosimama.

“Nami nikiinuliwa juu ya nchi,NITAWAVUTA WOTE KWANGU”(Yohana12:32).

Rudi Nyumbani

Print this post