AGANO LA MOYO LENYE NGUVU

AGANO LA MOYO LENYE NGUVU

Amri za kwanza Mungu aliziandika juu ya mawe aliyoyachonga yeye mwenyewe, lakini mawe yale ambayo juu yake amri 10 yalivunjwa vunjwa na Musa wakati ule ule aliposhuka kutoka mlimani…

Kutoka 31: 18 “Hapo Bwana alipokuwa amekwisha zungumza na Musa katika mlima wa Sinai, akampa hizo mbao mbili za ushuhuda, mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa chanda cha Mungu”

Baadaye Mungu akamwambia Musa achonge, mbao nyingine mbili za mawe mfano wa zile za kwanza zilizochongwa na Mungu mwenyewe..Na Musa alipochonga aliwapa wana wa Israeli…

Kutoka 34:1 “Kisha Bwana akamwambia Musa, Chonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza; nami nitaandika juu ya mbao hizo maneno hayo yaliyokuwa juu ya mbao za kwanza, hizo ulizozivunja”.

Mbao hizi za pili nazo hazikudumu muda mrefu, kwamaana alipokuja Mfalme Nebukadreza alivunja sanduku na kuzipoteza kabisa,.na kukawa hakuna tena sanduku la ushuhuda ambalo ndani yake mna mbao hizo za mawe zilizobeba Amri za Mungu.

Lakini baada ya miaka Mingi kupita Bwana Mungu akarudia tena kuziandika amri hizo kwa mara nyingine ya mwisho, lakini safari hii si katika mwamba aliouchonga yeye kwa vidole vyake, wala si katika mwamba uliochongwa na Musa, BALI KATIKA MOYO WA MTU.

Yeremia 31:31 “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. 

32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana. 

33 Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; NITATIA SHERIA YANGU NDANI YAO, NA KATIKA MIOYO YAO NITAIANDIKA; NAMI NITAKUWA MUNGU WAO, NAO WATAKUWA WATU WANGU. 

34 Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena”.

Umeona? Kumbe agano jipya linahusu Moyo!.. Maana yake hatuhitaji tena kwenda Yerusalemu kuzisikia amri, wala sharia wala maagizo ya Mungu, bali tunapomwamini Yesu zile sharia zinaandikwa ndani yetu na kidole cha Mungu mwenyewe.

Na matokeo ya sharia, na amri za Mungu kuandikwa ndani ya mioyo yetu, maana yake muda wote zitakuwa zinabubujika na hivyo hakuna haja ya mtu kukufundisha kuzishika amri, zenyewe tu zitakuwa zinabubujika ndani yako.. kama maandiko yanavyosema hapo katika mstari wa 34…. “Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana”.

Hiyo ndio sababu kwanini watu waliompokea Yesu kikweli kweli na kujazwa na Roho wake Mtakatifu, haihitaji kuwaambia wala kuwakazania kuwa ulevi ni dhambi, au uvaaji mbaya ni dhambi.. Tayari sheria ipo ndani yao, hata pasipo kuambiwa na mchungaji,… ndani ya mioyo tayari kuna mahubiri yaliyoandikwa na kidole cha Mungu mwenyewe yanayowaambia kuwa si sawa kufanya baadhi ya mambo. Hayo mahubiri haihitaji wasafiri mbali kwenda kuyatafuta, tayari yanakuwa yameandikwa ndani yao, haihitaji kuwakumbusha kusali, tayari hayo mahubiri yapo ndani yao, haihitaji kuwakumbusha kwenda ibadani, tayari hayo maagizo Bwana kayaandika ndani yao, hivyo daima yanabubujika.

Kumbukumbu 30:11 “Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali.

 12 Si mbinguni, hata useme, Ni nani atakayetupandia mbinguni akatuletee, aje atuambie tusikie, tupate kuyafanya? 

13 Wala si ng’ambo ya pili ya bahari, hata useme, Ni nani atakayetuvukia bahari, akatuletee, aje atuambie, tusikie, tupate kuyafanya? 

14 Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na MOYO WAKO, upate kulifanya”

Lakini maandiko hayo hayawezi kuandikwa ndani ya moyo wa mtu, kama mtu huyo hajafungua moyo wake kwa kumwamini Yesu na kumkiri kwa kinywa, vile vile kwa kutubu dhambi kwa kumaanisha kuziacha, pamoja na kubatizwa, kwa maana maandiko yanasema hivyo..

Warumi 10:6  “Bali ile haki ipatikanayo kwa imani yanena hivi, Usiseme moyoni mwako, Ni nani atakayepanda kwenda mbinguni? (Yaani, ni kumleta Kristo chini),

7  au, Ni nani atakayeshuka kwenda kuzimuni? (Yaani, ni kumleta Kristo juu, kutoka kwa wafu.)

8  Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo.

9  Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.

10  Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu”.

Je sheria za Mungu zimeandikwa ndani yako??

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mada Nyinginezo:

JE! UNAMPENDA BWANA?

Agano ni nini? na kuna aina ngapi za maagano?

Amri zilizo ndogo alizozizungumzia Yesu ni zipi?

TAFUTA UZIMA WA MILELE NA SI UZIMA TU!.

Mti wa Mshita ni mti wa namna gani?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Leave a Reply