Je agano la kale litatoweka kabisa kulingana na Wabrania 8:13?

Je agano la kale litatoweka kabisa kulingana na Wabrania 8:13?

Jibu: Tusome,

Waebrania 8:13 “Kwa kule kusema, Agano jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kianzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka”.

Neno “kuukuu” maana yake ni “kitu kilichochakaa/ kilichoisha muda wake”.. Hivyo hapo biblia inaposema kuwa Agano la kwanza amelifanya kuwa kuukuu tafsiri yake rahisi ni kwamba “Agano la kwanza yaani lile la kale amelifanya kuwa chakavu (lililoisha muda wake)/ lisilofaa tena”.

Lakini swali ni je!.. kupitia mstari huo inamaanisha kuwa Agano la kale litapotea kabisa na halitatumika?…kiasi kwamba halifai tena wala halitatumika?

Jibu ni la! Bwana Yesu alisema mwenyewe kuwa “hakuna yodi moja wala nukta moja ya torati itakayoondoka (soma Mathayo 5:18)”… Na Zaidi sana alisema hakuja kuitangua torati bali kuitimiliza.

Mathayo 5:17 “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.

18  Kwa maana, amin, nawaambia ,Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka ,hata yote yatimie”.

Sasa swali linarudi pale pale kama hivyo ndivyo kwamba Bwana YESU hakuja kuitangua torati bali kuitimiliza, na kwamba agano la kale bado litaendelea kuwepo, ni kwanini hapo katika Waebrania 8:13 biblia iseme kuwa litatoweka kabisa?. Je! Biblia inajichanganya??

Jibu ni La! biblia haijichanganyi bali tafakari zetu ndizo zinazojichanganya!.

Ili tuelewe vizuri tutafakari mfano ufuatao.

Kampuni moja limetoa aina Fulani la gari, na aina hiyo ya gari ikatumika kwa miaka kadhaa, lakini baada ya miaka 10 ikatoa toleo lingine jipya la aina ile ile ya gari, na hivyo kampuni hilo likaacha kuzalisha lile toleo la kwanza lililo dhaifu na kujikita katika uzalishaji wa toleo jipya.

Sasa ni wazi kuwa kwa jinsi miaka inavyozidi kwenda lile toleo la kwanza litaenda kupotea kabisa na kubaki hili la pili… kwa lugha nyepesi tunaweza kusema kuwa… “Kampuni lile limelifanya toleo la kwanza kuwa kuu, na hivyo lipo karibuni kutoweka kabisa”.

Lakini kwa kutoa toleo jipya haimaanishi kuwa limelipinga lile la kwanza, kwamba badala ya kuzalisha magari sasa linazalisha treni. Hapana! Bali kinyume chake limeliimarisha lile la kwanza, ikiwa na maana kuwa kama tairi za toleo la kwanza zilikuwa dhaifu, basi toleo la pili limeziongezea uimara, lakini gari ni lile lile, vile vile  kama mwonekano wa toleo la kwanza ulikuwa si mzuri basi toleo la pili limeongeza uzuri wa kimwonekano lakini gari ni lile lile.

Na ndivyo katika habari ya agano jipya na lile la kale, Hakuna kilichoondolewa, na kuletwa kingine kipya, bali ni kile kile kilichokuwepo kimeimarishwa Zaidi, kuwa bora Zaidi, kuwa imara Zaidi, kuwa chenye uwezo Zaidi n.k

Kwamfano biblia inasema katika mojawapo wa amri katika agano la kale kuwa “usizini” ikaishia hapo… Sasa hii amri ilikuwa ni dhaifu, kwasababu inasema usizini tu!, mtu anaweza asizini kweli lakini moyoni mwake akalipuka tamaa..

Lakini sasa Bwana YESU aliye mjumbe wa agano jipya anakuja kuitimiliza amri hiyo kuwa “mtu amtazamaye mwanamke kwa kumtamani amekwisha kuzini naye nafsini mwake”. Hata kabla ya kwenda kufanya kile kitendo.

Mathayo 5:27  “Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini;

28  lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake”

Na vile vile katika amri ya “kuua” ni hivyo hivyo…(soma Mathayo 5:21-22).

Kwahiyo kwa lugha nyepesi ni kwamba Agano la pili ni toleo jipya la Agano la kwanza. Lakini mambo ni yale yale.

Sasa ni swali lingine.. Ni wakati gani ambapo agano la kale lilianza kuwa kuu kuu?

Jibu: Ni wakati wa kuja kwa Bwana Yesu kwa mara ya kwanza.

Kipindi Bwana Yesu alipokuja, yeye ndiye wa mwanzilishi wa agano jipya, na kuanzia huo wakati ndio agano la kale katika maarifa yake machanga lilipoanza kuisha muda wake, na mpaka leo hatulitumii tena, limetoweka! Na nguvu katika damu ya Yesu ndani ya agano jipya inatawala.

Ndio maana maarifa machanga ya agano la kale, mfano matumizi ya damu za wanyama kama sadaka za kafara zimebaki kutumiwa na watumishi wa shetani, na katika ukristo Damu ya Yesu ndio utimilifu wa Torati za kafara. Na yeyote anayetumia kafara za wanyama leo hii, awe anajiita mtumishi wa Mungu au mtu yeyote yule anafanya ibada za miungu.

Kwahiyo leo hii katika ukristo hatuna matambiko, wala kafara za wanyama, wala utakaso kupitia damu za wanyama, wala hatuishi kwa kujizuia kuua lakini mioyoni tuna hasira, au tamaa.. bali tunaishi kwa Roho mtakatifu na tunamuabudu Mungu katika roho na kweli.

Bwana atubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

MJUMBE WA AGANO.

Je! waliokufa kabla ya Bwana Yesu wataokolewaje?

LISHIKILIE SANA LILE AGIZO LA KWANZA.

Tofauti kati ya ufalme wa mbinguni na ufalme wa Mungu ni ipi?

Kiti cha Rehema kilikuwaje? (Kutoka 40:20)

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments