MADHARA YA KIBURI KATIKA MAISHA YA MTU.

MADHARA YA KIBURI KATIKA MAISHA YA MTU.

Kiburi ni hali ya moyo wa mtu kuinuka kutokana na kitu fulani alichonacho, au alichokipata au atakachokipata ambacho kinamtofautisha au kitamtofautisha yeye na mwingine.

Hali hii inamfanya mtu anakuwa na majivuno, dharau na jeuri na asiyetii na hata kukosa staha.

Mtu huyu anakuwa ni mgumu kushaurika, na wakati wote yeye ndio anajiona yupo sahihi  na wengine wote wana kasoro.

Vifuatavyo ni vitu vichache ambavyo vinatengeneza kiburi ndani ya mtu.

1.MALI

Hiki ni kitu cha kwanza ambacho kinatengeneza kiburi ndani ya mtu, na kiburi chenyewe ni “kiburi cha uzima” tunachokisoma katika 1Yohana 2:16.

Hapa mtu anakuwa anaamini anao uzima au maisha kupitia vile alivyonavyo.. Hivyo hahitaji kuambiwa kingine chochote ambacho kitampa yeye uzima, tayari yeye anakuwa anaamini mali alizonazo ndizo jawabu la mambo yote..hivyo hata ukimpelekea Neno la Mungu ambalo ndilo uzima hawezi kukusikiliza…

Na kiburi hiki pia kwa sehemu kipo kwa watu wasio na mali, wanaozisaka wakiamini kuwa watakapozipata zintawapa majibu yote…na hawa ndio wale ukiwapelekea Neno la Mungu wanadharau na kukejeli na kuulizia pesa.

Lakini Bwana YESU alisema kuwa uzima wa mtu haupo katika wingi wa vitu mtu alivyonavyo..(Luka 12:15).

2. ELIMU

Maarifa hususani ya kidunia ni mlango wa pili wa kuzalisha kiburi ndani ya mtu.

Hapa ni pale mtu kapata elimu ambayo ni ya juu kuliko wengi..moyo wake unanyanyuka na kuona wengine wote hawawezi kumzidi akili au uwezo wa kutafakari..

Hivyo anapoletewa Neno la Mungu basi anaanza kumpima yule aliyemletea na anapogundua kuwa ana elimu ndogo ya kidunia kuliko yake, basi hamsikilizi akiamini kuwa atakuwa na upambanuzi hafifu…pasipo kujua kuwa elimu ya mbinguni haipatikani katika shule za wanadamu..kwani hata Mitume wa Bwana Yesu hawakusoma isipokuwa Mathayo tu..lakini leo mafunuo yao tunayasoma na kutusaidia.

3. KIPAWA/KARAMA

Kipawa/kipaji/Karama mtu alichonacho ni mlango wa tatu wa kuzalisha kiburi ndani ya mtu.

Hapa ni pale mtu anapotambua kuwa anao uwezo pengine wa kuimba kuliko wengine, anauwezo wa kufundisha kuliko wengine, ana uwezo wa kutenda jambo fulani kuliko wengine, na badala atumie uwezo huo kujaza pale palipopunguka, kinyume chake anautumia uwezo huo kujisifia au kujionyesha yeye ni bora na hivyo hata kusikiliza wengine au kushawishwa na wengine inakuwa ni ngumu.

4. CHEO/NAFASI.

Cheo au nafasi ni mlango wa nne wa kiburi kuzalika ndani ya mtu..

Hapa ni pale mtu anapopata nafasi fulani katika kanisa, au jamii au kazi…na kuona wote walio chini yake hawawezi kumwongezea chochote.

5. MWONEKANO

Huu ni mlango wa tano ambao unatengeneza kiburi ndani ya mtu..

Hapa ni pale mtu inatokea kujiona anavutia kimwonekano kuliko wengine, na kuamini kuwa yeye ni mzuri/mrembo zaidi ya wote na hakuna wa kumzidi..

Na kiburi hiki kinazalika pale anapopokea maoni ya kusifiwa na mtu mmoja au wawili.. Mtu kama huyu anapotokea mtu mwingine na kutaka kuzungumza naye inakuwa ni ngumu kumsikiliza kwasababu alijiona kama atachafuliwa mwonekano wake.

Sasa yafuatayo ni madhara ya kiburi juu ya mtu kibiblia.

1.Kiburi kinaondoa Neema ya Mungu.

Petro 5:5 “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema”.

Neema ya Mungu inapokuwa juu ya mtu inamwongezea kibali kwake Mungu na kwa wanadamu…

Mtu mwenye neema ya Mungu tele juu yake, inakuwa ni vyepesi kwake kushinda dhambi tofauti na yule ambaye amepungukiwa neema, vike vile inakuwa vyepesi kwake kufanya jambo likafanikiwa.

2. Kiburi kinamletea mtu Aibu.

Mithali 11:2 “Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu…”

Watu wengi wenye kiburi wanaishia kuabika, kutokana na majivuno yao na dharau zao hivyo mwisho wake huwa hawapati vile wanavyovitafuta na hivyo wanakuja kuaibika baadaye.

3. Kiburi kinaharibu Nyumba

Mzazi mmoja au wote wanapokuwa na kiburi wanaiharibu familia yao wenyewe…

Mithali 15:25 “BWANA ataing’oa nyumba ya mwenye kiburi..”

4. Kiburi kinamshusha mtu chini (kimaisha).

Wote wenye kiburi Mungu anawashusha chini..

Mithali 29:23 “Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa”.

5. Kiburi kitamshusha mtu kuzimu.

Wote wenye kiburi hawataurithi uzima wa milele.

Isaya 2:12 “Kwa maana kutakuwa siku ya BWANA wa majeshi juu ya watu wote wenye kiburi na majivuno, na juu ya yote yaliyoinuka; nayo yatashushwa chini……..

17 Na majivuno ya mwanadamu yatainamishwa, na kiburi cha watu kitashushwa; naye BWANA, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo”

Tabia nyingine ya mtu wenye kiburi pia ni mashindano na ubishi

Mithali 21:24 “Mwenye kiburi na kutakabari, jina lake ni mbishi; Hutenda mambo majivuno ya kiburi chake”.

Mithali 13:10 “Kiburi huleta mashindano tu…”

Jihadhari na kiburi..Na tunajihadhari nacho kwanza kwa kuokoka kisha kujazwa Roho Mtakatifu katika maisha yetu na kujitahidi kwa bidii kukaa mbali na mazingira yote yanayochochea kiburi.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Kiburi cha Uzima ni nini? (1Yohana 2:16)

MUNGU HUWAPINGA WENYE KIBURI.

Unyenyekevu ni nini?

Babeli ni nchi gani kwasasa?

DHAMBI ILIYOMKOSESHA SHETANI:

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments