JIBU: Kwanza ni muhimu kufahamu nini maana ya watoto wa kwenye chupa…ikitokea mama anakuwa ana mayai lakini anapata shida kushika mimba huwa kuna uwezekano wa kuyatoa mayai yake kutoka kwenye uzazi na kuyaweka kwenye kifaa maalum kinachoitwa test tube au kwa kiswahili chupa, sasa wakishaliweka hilo yai la mwanamke mule huwa wanachukua mbegu za mwanamume na kuziweka kule kitaalamu ili kurahisisha lile yai kurutubishwa kirahisi…na baada ya lile yai kurutubishwa ndani ya ile chupa wanalichukua lile yai na kulirudisha kwenye tumbo la yule mama na kuendelea na hatua nyingine za ukuaji wa yule mtoto kwenye tumbo la mama yake…hiyo ndio maana ya mtoto wa kwenye chupa, sio kwamba yule mtoto anawekwa kwenye chupa maisha yake yote hapana….ni yai tu ndio linalorutubishiwa kule na kurudishwa mahali husika…
kwahiyo hakuna mazingira yoyote nje na tumbo la mama mtoto anaweza kukua..wanadamu hawajafikia huo uwezo. Tumbo la mama ndio sehemu pekee mtoto anaweza kukua mpaka kufikia hatua ya kuzaliwa.Sasa tukirudi kwenye swali je! ni dhambi yai kurutubishiwa kwenye chombo hicho maalumu nje na tumbo la mama??J
ibu ni kwamba Mungu anaangalia nia ya mtu kufanya vile ni ipi, wengi wanaofanya hivyo unakuta wana matatizo ya kutokushika mimba, kwahiyo njia rahisi wanayoshauriwa na madaktari ni kutumia hiyo njia, hivyo sio dhambi kwasababu nia yao ni kutafuta mtoto sio kuua mtoto. Na hatua hiyo ya kurutubisha yai kwenye chupa ni hatua ya awali kabisa hata mtoto hajaanza kutengenezwa. Ingekuwa kufanya hivyo ni dhambi basi pia kuzaa kwa operation ingekuwa ni dhambi kwasababu sio njia ya asili Mungu aliyoiumba kwa kuzalia watoto. Kwahiyo inategemea na sababu ya mtu kufanya hivyo ni nini?, kama mtu anafanya kwa nia nyingine tofauti na hiyo basi ni dhambi, Lakini ingekuwa ni vizuri zaidi kumtegemea Mungu kuliko madaktari yaani kumwamini Mungu kuliko kutafuta njia mbadala, lakini pia hatuna imani zinazofanana…wako wenye imani kuwa Mungu atawapa watoto pasipo njia hizo na wapo wasio na imani hiyo…Lakini mtu akitumia hiyo njia hafanyi dhambi endapo tu atakuwa na nia njema.
Warumi 14:5…”Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe.
Ukiwa na swali, lolote unaweza ukatutumia, kwa neema za Bwana tutakujibu na kukutumia kwa njia ile iliyo rahisi kwako (inbox, e-mail, au whatsapp)Weka jina lako, na swali lako”.
Ubarikiwe!
Mada Nyinginezo:
JE! NI HALALI KWA MTU WA MUNGU KUTUMIA NJIA ZA UZAZI WA MPANGO,IKIWAMO MIPIRA?
JE! MUNGU ANAUPENDELEO KWA WANAUME ZAIDI YA WANAWAKE?
VIGEZO VYA KUWA KARIBU NA YESU KRISTO KATIKA ULIMWENGU UJAO.
MAJARIBU MATATU YA YESU KRISTO
JIBU: Waebrania 6:1-3 Inasema..
“1 Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu, 2 na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele. 3 Na hayo tutafanya Mungu akitujalia.”
Ndio Bwana anatuonyesha kwamba ukristo ni safari isiyoishia tu pale mtu anapotubu na kubatizwa na kumwamini Mungu, bali ni jambo endelevu siku baada ya siku tunakua, na ndio maana mtume Paulo anasema hapo TUKAZE MWENDO ili tuufikilie huo utimilifu. Hatupaswi kila siku tu tukae kwenye mafundisho yanayohusu ubatizo sahihi, au kutubu au kumwamini Mungu, au ziwa la moto, hayo ni mafundisho ya chini sana, kwamba pindi tu pale mtu alipompa Bwana maisha yake alipaswa ayatambue.
Na hivyo anakuwa na wajibu wa kusonga mbele kujifunza mambo mengine ya muhimu zaidi. Lakini inasikitisha kwamba utakuta mtu anadai yeye ni mkristo wa muda mrefu lakini bado suala la ubatizo sahihi linampiga chenga, mwingine haamini kabisa mambo hayo, mwingine hata ubatizo anaona hauna umuhimu kwake, anaamua kuendelea kubaki hivyo hivyo tu kwa muda mrefu, angali akijua kabisa biblia inafundisha kuwa pale tu mtu anapoamini , bila kupoteza muda anapaswa akabatizwe, kuukamilisha wokovu wake, lakini bado kwake anaona ni jambo linaloweza kusubiri tu, halina umuhimu sana .(Matendo 8:35-38) .
Sasa kama mambo hayo machanga yanakuwa bado ni mitihani kwa watu unategemea vipi Mungu aachilie neema kwa watumishi wake kufundisha mambo mengine ya ndani zaidi yatakayomfanya mtu akomae kiroho?. Ikiwa mtu haweza kuhesabu moja mpaka kumi, ya nini kufundishwa milinganyo?. Hivyo yatubadilishe mienendo yetu kwanza, ili Bwana aachilie neema ya kutufundisha mambo mengine ya ndani yahusuyo ufalme na na siri zimuhusuzo Bwana wetu YESU KRISTO.
Vinginevyo tukiendelea kumzimisha Roho ndani yetu kwa kutokutaka kutii maagizo madogo, tutatii vipi yale makubwa, tutaendelea tu kubaki katika hali ile ile ya uchanga kwa muda mrefu bila mabadiliko yoyote, hatutastahili kupata chakula kigumu cha kutufanya tukue. Kama Mtume Paulo alivyosema kwa Waebrania..
Waebrania 5: 11 “..Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia.12 Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu.13 Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga.14 Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya”
Ubarikiwe sana.
JIBU: Biblia haikatazi mtumishi yeyote wa Mungu kutambuliwa kwa karama aliyo nayo. Kwamfano kuitwa mchungaji, au mwinjilisti au mtume, au mwalimu au nabii au askofu n,k. Hakuna mahali ilipokataza, Lakini kuongeza Neno hapo juu yake mfano “mkuu” au “kiongozi ” “mighty” “chief” “lead” “great” n.k. hiyo ni roho ya kujiinua na ni roho ya mpinga-kristo yenyewe. Kwani vyeo hivyo vinamuhusu Bwana wetu YESU KRISTO mwenyewe.. Yeye ndiye mchungaji mkuu biblia inasema hivyo..yeye ndiye mtume mkuu, yeye ndiye nabii mkuu, Yeye ndiye Bwana wa mabwana, na yeye ndiye Mfalme wa wafalme.Na ndio maana utaona hakuna Mtume yeyote wa Kristo alijiita kuwa yeye ni mtume mkuu, bali cheo hicho walikitambua kuwa ni cha Kristo mwenyewe.
Waebrania 3:1 “Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini sana MTUME NA KUHANI MKUU wa maungamo yetu, Yesu, aliyekuwa mwaminifu kwake yeye aliyemweka, kama Musa naye alivyokuwa, katika nyumba yote ya Mungu.”
Waebrania 3:20 “Basi, Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu MCHUNGAJI MKUU wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu,”
Unaona? Hivyo hao watu wote wanaojivika hivyo vyeo vya juu zaidi ya walivyopewa, utatambua kuwa dhima yao ni kuvuta watu kwao, wawafuate wao na si Kristo, na ndio maana utaona hawaoni hata haya kujivuka vyeo vya juu kama hivyo. Lakini biblia inasema ajikwazaye atashushwa..Watu wa namna hiyo Bwana mwenyewe atawashusha, kwasababu yeye kasema Utukufu wake hatagawana na mwingine yeyote.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
MANABII WALISEMA “NENO LA MUNGU LIKANIJIA” ..MAANA YA HILI NENO NI NINI?
Jina la Bwana YESU litukuzwe daima. Karibu tujifunze Neno la Mungu, leo kwa neema za Bwana tutajifunza juu ya njia sahihi ya kufunga.
Zipo aina nyingi za kufunga lakini kwa vyovyote vile, hatufungi ili Mungu atusikie au atujibu maombi yetu, Mungu hasubiri kwanza tuteseke ndio atusikie hapana kwani alishaweka wazi katika Neno lake, kuwa yeye anajua tunachohitaji kabla hata hatujamwomba (Mathayo 6:8)…Lakini pamoja na hayo Kufunga kunasaidia kuongeza uwezekano wa wewe kupata majibu ya maombi yako au kupata unachokitafuta kwa haraka tofuati na yule asiyefunga. Ni sawa tu na mwanafunzi anayesomea maktaba na Yule anayesomea nyumbani, anayesomea maktaba anaongeza uwezekano mkubwa wa kufaulu mitihani kuliko Yule anayesomea nyumbani, kwasababu kule maktaba kunakuwa na utulivu mkubwa na mazingira mazuri ya kujisomea kuliko nyumbani..Lakini hiyo haimfanyi afaulu mtihani moja kwa moja Yule wa nyumbani anaweza kufanya vizuri kushinda hata yeye..Lakini itampasa awe mtu wa kujitambua sana.
Vivyo hivyo na katika kufunga, Mtu mwenye desturi ya kuomba kwa kufunga anajijengea daraja zuri la yeye kuwasiliana na Mungu kuliko Yule apelekaye dua zake kwa Mungu bila kufunga, Kwasababu Kufunga kunampa utulivu Fulani wa Roho tofauti na mtu asiyefunga.
Na hiyo yote ni Kutokana na kutokuwa na Mungu katika mwili, au kutokumwona Mungu katika mwili ndio maana inatupelekea tumtafute Mungu kwa umakini zaidi kuliko kama tungekuwa tunamwona kwa macho…Mitume walipokuwa na Bwana duniani hakukuwa na sababu ya kufunga, ufunge ya nini wakati unayemtafuta upo naye hapo? Mpaka watu wengine wakashangaa inakuwaje hawa ni mitume wa Bwana lakini hawafungi, Ndipo Bwana alikawaambia wanachokifanya hawajakosea kwasababu mimi nipo, Siku zitakuja nitakapoondoka ndipo watakapofunga kama wengine…
Marko 2:18 “Nao wanafunzi wake Yohana na Mafarisayo walikuwa wakifunga; basi walikuja, wakamwambia, Kwani wanafunzi wa Yohana na wanafunzi wa Mafarisayo hufunga, bali wanafunzi wako hawafungi?
19 Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu bwana-arusi yupo pamoja nao? Muda wote walipo na bwana-arusi pamoja nao hawawezi kufunga.
20 Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana-arusi, ndipo watakapofunga siku ile.”
Hivyo kitendo cha kufunga hakikwepeki sasa kwa mkristo yeyote. Na zipo aina nyingi za kufunga, lakini aina iliyozoeleka ni ile ya kuacha kula chakula. Lakini mfungo huu unafanywa kimakosa na wengi kwasababu ya kutokufahamu ni kwanini mtu anaacha kula..Na ndio hapo mtu mmoja atafunga vizuri kweli hata wiki tatu au mwezi au siku arobaini, lakini anafanya kama desturi za dini nyingine wanavyofanya, ukiangalia huku nyuma utamwona anaendelea na maisha yake ya kidunia anadhani kusikia kule njaa ndo Mungu anampa thawabu,. Hajui kuwa Mungu hamjibu mtu kwa mateso,(Maombolezo 3:31-35) sasa hapo mtu wa namna hiyo kaamua tu kujitesa bure..Hakuna chochote atakachokipata kutoka kwa Mungu.
Au unakuta mwingine anafunga kwa lengo la kumuomba Mungu mambo ambayo sio sawa na mapenzi yake, mwingine atamwomba Mungu ampe mali, lakini ndani ya moyo wake anawaza aitumie kwa anasa, mwingine atamwomba Mungu ampe hiki au kile, lakini nia yake moyoni ni kutumia kwa mambo maovu.. mtu wa namna hiyo pia asitazamie kupata kitu.
Isaya 58:3 “Husema, Mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu.
4 Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu.
5 Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana?
6 Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?
7 Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe?
8 Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde.
9 Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu;
10 na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri.”
Unaona? Dhumuni la msingi kabisa la kujizuia kutokula mtu anapaswa afahamu ni kuyaleta mapenzi ya mwili chini na kuruhusu mapenzi ya Mungu yaje juu, ile njaa inakukumbusha kwenda mbele za Mungu kwa unyenyekevu mwingi , sikuzote mtu mwenye njaa anakuwa katika uhitaji sana kuliko mtu aliye shiba, hivyo mtu wa namna hiyo anapokwenda mbele za Mungu kumaanisha kwake kunakuwa kwa kiwango cha juu zaidi kuliko mtu aliyeridhika, hata maombi yake yanakuwa marefu sana, jaribu hata kwako utaligundua hilo..Na hiyo ndio faida kubwa ya kutokula wakati wa maombi. Hivyo inapelekea maombi yako kuwa na nguvu zaidi mbele za Mungu kuliko wengine.
Vile vile kuna kufunga ambako sio kwa kula, bali kwa kujizuia na mambo mengine yanayoweza kukusonga usiisikie sauti ya Mungu. Kufunga kwa namna hii kumekuwa kwa kawaida kwa watumishi wengi wa Mungu, Nabii Elisha ilimpasa atumie muda mwingi kujitenga na mazingira ya watu ili kudumisha joto la uhusiano wake na Mungu. Sio kwamba kuna shida kujihusisha na mambo ya kawaida ya kila siku, hapana lakini ni utaratibu wa Mungu kuzungumza katika sauti ya utulivu, na kama ni sauti ya utulivu hivyo naye huwa anahitaji mazingira tulivu ya kumwelewa.
Ufunuo wowote Mungu anaompa mwanadamu, hampi akiwa katika mazingira ya usumbufu wa akili, Usijidanganye kuwa Mungu atakupa ufunuo wowote katika hali ya masumbufu, kama utaisoma biblia na huku unasikiliza miziki ya kidunia, au huku una chat, au huku unafanya mambo mengine, Ni heri uifunge uje usome baadaye usiku peke yako…. inahitaji utulivu wa fikra na mawazo..Na hapo ndipo inakupasa ufunge baadhi ya vitu unavyovifanya, au ulivyozoea kuvifanya..Na kwa jinsi unavyovifunga kwa muda mrefu zaidi ndivyo unavyoongezeka uwezekano wa Mungu kusema na wewe kwa haraka na kwa mara nyingi zaidi.
Kufunga ni kuna faida kwasababu yeye mwenyewe anasema wote wafanyao hivyo huwapa thawabu kama hawatafanya kinafki na kwa nia mbaya..(Mathayo 6:16)
Ni ahadi yake kukulipa, Funga tu kwa kumaanisha kumsogelea Mungu zaidi, utapata zaidi ya kile ulichomwomba. Kuna mtu aliuliza swali je! Maandiko yanasema tunapaswa tufunge kuanzia saa ngapi hadi saa ngapi na ni kwa siku ngapi?..Jibu ni kuwa Biblia haijatoa masharti yoyote juu ya muda wa kufunga au siku za kufunga..Imezoeleka siku 3, siku 21 na siku 40 kwasababu ndio siku ambazo zimeonekana zikifungwa na wengi..Lakini hiyo haimaanishi kuwa nawe ufunge muda huo, ni vile Roho atakavyokuongoza na kulingana na aina ya dua uipelekayo kwa Mungu, unaweza ukafunga, siku moja, au wiki, au mwezi, au mwaka, na Mungu akaridhia, vile vile unaweza ukafunga saa 6 kwa siku, saa 12, au siku tatu bila kula, au siku 40 bila kula , ni vile tu Mungu atakavyokupa neema..Lakini vyovyote vile kufunga ni muhimu kwa kila mkristo. Na kuna manufaa na thawabu nyingi.
Ubarikiwe sana.
Maran atha!
Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
JIBU: Ukisoma kuanzia hiyo mistari wa kwanza wa kitabu cha Warumi Mlango wa 10, Utaona kuwa Mtume Paulo alikuwa anazungumza habari za juu ya Wayahudi ambao wanaamini katika kuhesabiwa haki kwa matendo ya sheria na wala sio kwa Imani. Sasa Mtume Paulo alichokuwa anataka kuonyesha ni kwamba..Torati Musa aliyopewa na Mungu, imezungumza habari zote mbili yaani habari ya kuishi kwa sheria kwamba Mtu akiitenda sheria zilizoandikwa katika mbao zile ataishi katika hizo..Yaani Mtu akifanya maagizo yote ya torati basi atafanikiwa katika maisha yake.. Na pia torati hiyo hiyo mahali pengine pia imezungumzia kuhusu haki ipatikanayo kwa njia ya Imani kwamba..
Sheria za Mungu zikiandikwa ndani ya moyo wa mtu basi naye pia atabarikiwa zaidi..Kwasababu maana halisi ya agano jipya ni kuwa zile zile sheria za Mungu zinakuwa zinaandikwa ndani ya Moyo wa Mtu. Sasa ukisoma Kitabu cha kumbukumbu utaona Mungu anaizungumzia hiyo Mtume Paulo aliyoinukuu.
Kumbukumbu 30: 11 “Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali.
12 Si mbinguni, hata useme, Ni nani atakayetupandia mbinguni akatuletee, aje atuambie tusikie, tupate kuyafanya?
13 Wala si ng’ambo ya pili ya bahari, hata useme, Ni nani atakayetuvukia bahari, akatuletee, aje atuambie, tusikie, tupate kuyafanya?
14 Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya.
15 Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya”
Unaona Haki ipatikanayo kwa njia ya Imani kwamba sheria za Mungu zitakuwa karibu sana na mtu mahali alipo, hazipo mbinguni kwamba Bwana Yesu aende akatuchukulie atuletee katika gari la moto, au hazipo kuzimu kwamba Bwana Yesu azifuate atuletee katika mbao kama Musa alivyozileta katika mbao kwa wana wa Israeli ili wazishike.. Hapana sheria zake ataziandika ndani yetu (ndani ya mioyo yetu)..zipo karibu sana na sisi, hakuna haja ya kwenda milimani kuzitafuta kama alivyofanya Musa, wala hakuna haja ya kusubiria mtu atoke mbinguni au kuzimu kutufundisha…yeye Bwana ataziandika mioyoni mwetu kutufundisha mwenyewe..
Hiyo ndiyo maana ya huo mstari.. “Usiseme moyoni mwako,Ni nani atakayepanda kwenda Mbinguni? (yaani ni kumleta Kristo chini), “au,Ni nani Atakayeshuka kwenda Kuzimu? (yaani, ni kumleta Kristo juu,kutoka kwa wafu.) Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo” Mtume Paulo alielezea vizuri zaidi juu ya agano hilo jipya katika kitabu cha
Waebrania 8:8 “…Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, Nami nitawatimizia nyumba a Israeli na nyumba ya Yuda agano jipya;
9 Halitakuwa kama agano lile nililoagana na baba zao, Katika siku ile nilipowashika mikono yao niwatoe katika nchi ya Misri. Kwa sababu hawakudumu katika agano langu, Mimi nami sikuwajali asema Bwana.
10 Maana hili ndilo agano nitakaloagana na nyumba ya Israeli Baada ya siku zile, asema Bwana; NITAWAPA SHERIA ZANGU KATIKA NIA ZAO, NA KATIKA MIOYO YAO NITAZIANDIKA; Nami nitakuwa Mungu kwao, Nao watakuwa watu wangu.
11 Nao hawatafundishana kila mtu na jirani yake, Na kila mtu na ndugu yake, akisema, Mjue Bwana; Kwa maana wote watanijua, Tangu mdogo wao hata mkubwa wao.
12 Kwa sababu nitawasamehe maovu yao, Na dhambi zao sitazikumbuka tena”
Ubarikiwe!
Mada Nyinginezo:
AMEFANYIKA BORA KUPITA MALAIKA!
MADHARA YA DHAMBI YA UASHERATI.
Shalom, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, maandiko yanasema,
Mhubiri 10:10 “Iwapo chuma hakipati, wala mtu hakinoi; Ndipo hana budi kutumia nguvu zaidi. Walakini yafaa kutumia hekima, na kufanikiwa”.
Katika tafsiri nyingine hilo Neno Chuma limetafsiriwa kama shoka, ikiwa na maana kuwa kama shoka ni butu au halinolewi mara kwa mara basi itampasa mtu kutumia nguvu zaidi katika kukata vitu au kuchonga, au kuchanja kama anakata nyama itampasa atumie nguvu zaidi kuikata nyama ile, kama anakata mti basi itampasa atumie jitihada ya ziada yenye kuchosha kuudondosha mti kwasababu Shoka ni butu haliwezi kupenya kwa haraka ndani ya shina..Tofauti na kama kifaa hicho kingekuwa ni kikali, angetumia nguvu chache tu na matokeo kuwa makubwa ndani ya muda mfupi…
Ni kama tu kisu au kiwembe kikiwa ni kakali basi ukipitisha hata kwenye karatasi ni mara moja tu limegawanyika, lakini kama ni butu basi utakipeleka mbele na nyuma, na utachukua muda, na bado halitachanika vizuri kama lile lililochanwa na kiwembe kikali..
Lakini Mhubiri anaendelea kwa kusema, “walakini yafaa kutumia hekima, na kufanikiwa”,.. Ikiwa na maana usipoweza kutumia hekima, kuamua maisha yako kwa kukifanya kisu chako kuwa kikali basi mambo yako, licha tu ya kuwa magumu lakini pia utatumia nguvu nyingi kuyafikia…
Duniani Vipo visu vingi tofauti tofauti na mashoka tofuati tofauti na kila mtu analo lake, ambalo kwa namna moja au nyingine linamsaidia kufanya mambo yake kuwa mepesi, wengine ni elimu, wengine ni ujuzi, wengine ni fedha n.k..Lakini hasara moja ya vifaa hivyo vyote sio vya kudumu, huwa vinakuwa butu kwa jinsi muda unavyokwenda na kwa jinsi vinavyotumika…. Mtu akiviacha vinachakaa na pia isitoshe havitumiki kila mahali…huwezi kutumia elimu kutibu kifo, vile vile huwezi tumia pesa kununua furaha, au upendo au amani..
Ni kifaa kimoja tu ambacho Mtu mwenye akili na Hekima anaweza kukitumia kwa matumizi yote na kukata kila kitu pasipo kutumia nguvu, na bado kutokupungua ubora wake na makali yake…Nacho ni Neno la Mungu..
Waebrania 4:12 “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
13 Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu.”
Mtu akiwa na Neno la Mungu peke yake, hiyo ni salaha tosha, ya kurahisisha mambo yako..hili haliwi butu kama vile mengine, linao uwezo sio tu wa kukata kwa ukali zaidi ya upanga wowote, bali pia linaweza kuchoma hata kuzigawanya nafsi na roho, yaani linaingia ndani ya moyo wa mwanadamu na kugawanyisha kila kitu na kutambua mawazo yake, kitu ambacho pesa haiwezi kufanyi, elimu ya dunia hii haiwezi kufanya, ujuzi wowote ule wa mwanadamu hauwezi kufanya..
Ndio maana mtu yeyote aliyejaa Neno la Mungu ndani yake, hakuna jambo lolote linaloweza kumlemea hata liwe gumu kiasi gani kwasababu anafahamu vizuri silaha aliyonayo inaubora kiasi gani..
Mhubiri anatushauri NI HERI KUTUMIA HEKIMA NA KUFANIKIWA, tunapaswa tujue ni kifaa gani kitakachotufaa katika maisha yetu, katika mapori yanayotuzunguza mbele yetu ambayo yanapaswa yafyekwe kweli kweli, kifaa ambacho tunaweza kukabiliana na adui yetu ibilisi na kummaliza haraka sana bila kutumia nguvu nyingi… silaha hiyo si nyingine zaidi ya Neno la Mungu.
Waefeso 6: 17 “Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;”
Tunapoliishi Neno la Mungu, maisha yetu hatutayaona ni magumu, hatutasumbuka kama ulimwengu unavyosumbuka, Kwani ni Mungu mwenyewe ndiye atakayekuwa anatupigania,,Lakini tunapoliweka Neno la Mungu kando, tunapolidharau na kuchagua mambo mengine, au kuyaona mambo mengine ni ya muhimu zaidi ya Neno lake, tuwe na uhakika kuwa safari yetu itaishia ukingoni…Ni kutumia kifaa butu, kuufyeka msitu…Mambo yatakuwa magumu tu, huo ndio ukweli, Nira iliyo nyepesi ipo kwa Bwana Yesu tu, pengine kote ni Nzito na mateso yasiyoelezeka..(Mathayo 11:28)
Ndugu/Kaka Ikiwa hujayakabidhi maisha yako kwa BWANA Mlango wa Neema upo wazi, usisubiri baadaye au kesho, muda umekwenda sana kama unyakuo hautakukuta moja ya hizi siku, hujui baadaye yako itakuwa vipi, waliokufa leo asubuhi sio kwamba walikuwa waovu zaidi yako wewe, au walikuwa wameshajiandaa kwa safari ya kwenda huko ng’ambo, hapana lakini kifo kiliwakuta kwa ghafla tu, na ndivyo kitakavyotukuta wote walio haki na wasio haki…Hivyo fanya uamuzi wa busara wakati huu kwa kutubu dhambi zako kama hujatubu na kumgeukia Bwana sasa hivi.. kumgeukia Bwana Yesu sio kuwa vuguvugu, ni kitendo cha kumaanisha kabisa….Kisha utafute mahali wanapobatiza ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi kwa Jina la YESU KRISTO, kama pia bado hujafanya hivyo..Upate ondoleo la dhambi zako, kulingana na (Matendo 2:38) ili Bwana akupe kipawa cha Roho wake Mtakatifu ambaye ndio muhuri wetu, Mungu anaotutia mpaka ile siku wa ukombozi wetu (Waefeso 4:30).
Bwana azidi kukubariki.
Maran atha!
Maji yanawakilisha uhai, mahali ambapo hapana maji hapana uhai hiyo inajulikana na watu wote….Sayari zilizopo huko juu hazina maji, na ndio moja wapo ya sababu inazozifanya zisiwe na uhai…Hivyo hata hii dunia tunayoishi iliumbwa kutoka katika maji.
2 Petro 3: 5 “Maana hufumba macho yao wasione neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu;
6 kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia”.
Mwanzo 1: 1 “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. 2 Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji”.
Kwahiyo sehemu yoyote isiyo na maji ni makazi ya kifo…Kadhalika katika roho, yapo maji ya rohoni, ambayo hayo mtu yeyote asiyekuwa nayo, moyo wake unakuwa ni nchi kavu, au nchi kame, makao ya kifo… Na hivyo Roho Mtakatifu hawezi kushuka mahali palipo pakame, yeye anashuka mahali penye maji, kama alivyotua wakati wa kuitengeneza upya dunia ya kwanza, alitua juu ya uso wa vilindi vya maji, ndipo akaanza uumbaji….Maji na Roho vinakwenda pamoja, (1 Yohana 5:9
“Kisha wako watatu washuhudiao duniani], Roho, na maji, na damu; na watatu hawa hupatana kwa habari moja.) ndio maana kuna umuhimu sana wa kubatizwa ubatizo wa maji mengi na si wa kunyunyiziwa ndipo Roho aingie ndani ya mtu, kwasababu dunia ya kwanza biblia inasema Roho Mtakatifu hakutua juu ya chemchemi, au juu ya unyevunyevu bali juu ya uso wa vilindi, ikiwa namaana kuwa ni dunia yote ilikuwa imejaa maji sio sehemu baadhi tu! hapana Bali yote..ndipo uumbaji ukaanza.
Mtu aliyempa Kristo Maisha yake kwa kudhamiria kabisa kuacha dhambi, na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi, na kwa jina la Yesu Kristo, hapo mtu huyo ni sawa na anaujaza moyo wake na maji ya uzima..Moyo wake unakuwa umejaa maji mpaka juu kabisa, vilindi vya maji ya uhai vinakuwa juu yake, na hivyo tayari Roho Mtakatifu kushuka juu yake na kuanza uumbaji, anakuwa amezaliwa mara ya pili na kuwa kiumbe kipya. Roho Mtakatifu anaanza kusema na iwe Nuru juu yake, na inakuwa hivyo, Roho Mtakatifu anaanza kutenga maji na maji,na kutengeneza ndani yake mito, chemichemi, na vipindi vya mvua, na kuchipusha kile ki-kijani ndani yake n.k
Bwana Yesu alisema katika
Yohana 7: 38 “Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake.
39 Na neno hilo alilisema katika habari ya Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa”.
Sasa tumeshaona ni namna gani Roho ya mtu aliyezaliwa mara ya pili mbele za Mungu inaonekana kama ni mahali penye maji, penye uhai na mahali ambapo ni makazi ya Roho Mtakatifu, na tumeshaona kuwa Ili Roho Mtakatifu akae ndani ya mtu ni lazima ubatizo sahihi wa kimaandiko wa maji mengi uhusike..Kama Ilivyokuwa katika uumbaji.
Vivyo hivyo mtu yeyote ambaye hajamwamini Yesu Kristo, wala hajabatizwa inavyopaswa wala hajapokea Roho Mtakatifu, moyoni mwake ni nchi kavu..Na hakuna namna yoyote ile ambayo Roho Mtakatifu atatua juu yake…Na kama Roho Mtakatifu hatatua juu yake basi ni Dhahiri kuna roho nyingine zitatua juu yake…Na hizo si zaidi ya roho chafu za Mapepo…Roho za Mapepo ndizo zinazotafuta sehemu kavu isiyo na maji na kushuka juu yake..Tusome..
Mathayo 12:43 “Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika, asipate.
44 Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa.
45 Mara huenda, akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya”.
Unaona hapo?..Biblia inasema anapitia sehemu isiyo na maji, na hiyo si nyingine Zaidi ya mtu ambaye hajamwamini Kristo, na hajabatizwa na kupokea Roho Mtakatifu.Kitu kimoja watu wengi wasichokijua ni kwamba shetani sasa hayupo kuzimu…wala haungui moto sasahivi…shetani yupo hapa hapa duniani na baadhi ya mapepo yake, yapo mapepo baadhi biblia imesema kuwa ndio yapo kuzimu sasa kwenye vifungo, lakini sio yote! (2 Petro 2:4) Idadi kubwa ya mapepo yapo huru ulimwenguni, yakisubiri siku ya mwisho ifike yakusanywe yote pamoja na shetani yakatupwe katika lile ziwa la moto.
Haya yaliyopo huru sasa hayatamani kwa namna yoyote kwenda huko kuzimu(au kwa lugha nyingine shimoni), kwasababu yanajua mateso yaliyopo kule, ndio maana yalimsihi sana Bwana wakati ule yasipelekwe shimoni (soma Luka 8:30-32).
Na kitu kingine kisichojulikana na wengi ni kuwa, mtu yeyote ambaye hajampa Kristo Maisha yake, anayo mapepo ndani yake, anaweza akawa anayo machache au mengi, na yanatofautiana ubaya, yapo yaliyo mabaya sana na yapo ya wastani, yapo ambayo madhara yake ni ngumu kuonekana kwa wazi na yapo ambayo madhara yake yanaonekana waziwazi, lakini yote katika yote mtu ambaye hajampa Kristo Maisha yake, mwili wake ni makao ya roho chafu…aidha anajua au hajui..Na wengi wenye mapepo hawajijui kama wanayo, Mpaka siku watakapobadilika ndio watakapojijua kuwa hawakuwa sawa hapo kwanza.
Sasa mtu anayempa Kristo Maisha yake leo na kukusudia kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu mapepo yanamtoka, na kumbuka mapepo yakimtoka mtu sio lazima yalipuke! Hapana! Kufikiri hivyo ni kufikiri kichanga! Mapepo mengi yanawatoka watu pasipo hata kulipuka wala kuonesha mabadiliko yoyote ya mwili, baada ya kipindi Fulani tu mtu ndio atajiona amekuwa tofuati kuliko alivyokuwa hapo kwanza. Kwahiyo baada ya mapepo haya kutoka ndani ya mtu hayaendi kuzimu wala hayaendi jangwani, yanakwenda kutafuta mahali ambapo hapana maji, na huko si kwingine Zaidi ya mtu ambaye hajampa Kristo Maisha yake au kwa Wanyama, kwasababu Wanyama hawana Roho Mtakatifu, kipawa hicho hawajaahidiwa wao…Lakini yanapendelea Zaidi watu kuliko ya Wanyama…Kwahiyo mtu huyo kila siku anakuwa anaongeza mapepo juu ya mapepo ndani yake pasipo kujijua, ndio maana mtu ambaye hajampa Kristo Maisha yake, hali yake ya kiroho kila siku inazidi kuwa mbaya…Kwanini? Kwasababu kila siku anaongoza idadi ya mapepo ndani yake?
Unaweza kutengeneza picha yule mtu Bwana Yesu aliyemwombea alikuwa ana mapepo wangapi? Biblia inasema ni jeshi! Sasa hebu fikiri nguruwe pale walikuwa 2,000 na kila nguruwe tuseme kaingiwa na mapepo mawili tu! Kwa hesabu hizo jumla ya mapepo yaliyokuwa ndani ni wazi kuwa ni Zaidi ya mapepo 4,000 ndani ya mtu mmoja!.. na kila pepo linatabia yake..
Hivyo ndugu ambaye hujampa Kristo Maisha yako au ambaye mguu mmoja leo huko mwingine kule…hayo ndio madhara yatakayokupata endapo hutaamua kufanya maamuzi thabiti sasa…Kama hali yako itazidi kuwa mbaya kila kukicha, shetani yupo na anafanya kazi sasa…Mkabidhi Yesu Kristo Maisha yako ukabatizwe kama hujafanya hivyo, ili akupe na Roho wake Mtakatifu ili vijito vya maji ya uzima vianze kububujika ndani yako. Na ufanikiwe katika roho yako, na mwili wako usiwe makazi ya roho chafu za shetani. Nguvu za shetani sasa zinafanya kazi sana, kuliko kipindi cha nyuma, na hiyo yote biblia inatumbia ni kwasababu anajua kuwa muda wake umebakia mchache, na ndio maana utaona leo hii matendo mengi maovu ya ajabu ajabu yanatokea ulimwenguni, vitu ambavyo huwezi ukadhani kama mwanadamu anaweza kuvifanya..Hivyo fanya bidii uingie katika ulinzi wa Damu ya Yesu Kristo kwa kutubu na kumwamini Yeye.
Bwana akubariki sana.
Mada Zinazoendana:
JE! NI SAHIHI MTU KUBATIZWA KWENYE MAJI YA KISIMANI?
MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO.
JIBU: Ikiwa Bwana alituagiza tupendane sisi kwa sisi hata tufikie hatua ya kuweza kutoa uhai wetu kwa ajili ya wengine wapone kama yeye alivyofanya kwetu sisi, Sasa! damu itakuwa ni kitu gani kwetu?. Tumeambiwa tusipende kwa neno au kwa ulimi tu bali kwa tendo. Biblia inatuambia
1Yohana 3:16 “Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu.
17 Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?
18 Watoto wadogo, TUSIPENDE KWA NENO, wala kwa ulimi, BALI KWA TENDO NA KWELI.”
Ni sawa na kumwona ndugu yako amepungukiwa damu na, hivyo asiposaidiwa atakwenda kufa muda si mrefu, na wewe angali unao uwezo huo wa kumsaidia na hautaki unasema sitoi damu yangu ni dhambi, hivyo nakuombea tu,kisha Mungu akupumzishe salama, je! hapo utakuwa umeonyesha upendo gani kwa ndugu yako huyo?. Huoni kama utakuwa umependa kwa Neno na wala si kwa tendo?. Lakini wapo watu wanafanya hivyo kama biashara kwa kisingizio cha kuwa wanasaidia watu, wanatoa damu zao, wanatoa figo zao, si kwa lengo la kumsaidia ndugu yake, bali kwa lengo la kufanya biashara. Hiyo ni dhambi mbele za Mungu na wanaofanya hivyo siku zinakuja watuvuna walichokipanda.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
NI RAHISI KWA NGAMIA KUPENYA KATIKA TUNDU LA SINDANO, JE! NI SINDANO IPI HIYO INAYOZUNGUMZIWA?
JE! NI HALALI KUTOA CHETI KWA WAKRISTO WANAOOANA?
NIFANYE NINI ILI NIIKWEPE HUKUMU.
AMIN! NAWAAMBIA KIZAZI HIKI HAKITAPITA
SIKU YA BWANA INAYOTISHA YAJA!
Tukisoma kitabu cha Mithali sura ya 30 tunamwona mtu mmoja aliyeitwa Aguri bin Yake akiandika mithali ambazo ni mahusia aliyompa mtu mmoja anayeitwa Ithieli. Kati ya mambo mengi aliyokutana nayo katika maisha yake kuna manne yaliyomshangaza sana nayo ni haya tunayoyasoma katika mstari wa 18,
Mithali 30:18 “Kuna mambo matatu yaliyo ya ajabu kwangu, Naam, kuna manne nisiyoyafahamu.19 Mwendo wa tai katika hewa; Na mwendo wa nyoka juu ya mwamba; Mwendo wa merikebu katikati ya bahari; Na mwendo wa mtu pamoja na msichana.
Ukiisoma hii mistari kwa juu juu utaona unaweza usione jambo lolote la kushangaza, lakini ukiitafakari kwa undani utagundua kweli alivyoviona vinamshangao mkubwa sana katika mienendo yao. Hapo amevitaja vitu vine, Kwanza ni TAI, pili NYOKA, tatu MERIKEBU, na nne MTU pamoja na Mwanamke..
Aguri alitafakari kutembea kwao kukamshangaza sana, kwa mfano alimtazama Tai jinsi anavyoweza kwenda kwa kasi hewani, akaona japokuwa amepewa miguu lakini haitegemei miguu yake katika mwendo wake, leo hii hakuna mnyama yoyote wala ndege yeyote mwenye mwendo wa kasi kama Tai,Vile vile akamtazama Mnyama nyoka, ambaye nawe pia unamfahamu jinsi alivyo hana miguu, lakini nyoka kama koboko anakimbia karibia mara 2 zaidi ya mwendo ya wanadamu wengi..Hivyo Aguri akaona kumbe hata miguu sio nyenzo pekee ya kuamua mwendo wa kiumbe hai, kwamba bila hicho mambo hayawezi kwenda..
Akachunguza tena, Merikebu bahari akaona haina magurudumu kama vifaa vingine vya usafiri mfano ma gari, baiskeli, treni au pikipiki lakini inauwezo wa tembea tena kwa kasi tu..hata ingepewa matairi bado yasingeweza kumsaidia katika mwendo kasi wake, kama tu vile miguu isivyomsaidia Tai kutembea kwa kasi, na kama vile miguu isivyotumika kwa nyoka kukimbia kwa kasi, jongoo anayefanana na nyoka mwenye miguu mingi kuliko nyoka na kuliko Wanyama wengi lakini bado hawezi kukimbia..
Hivyo Aguri akamalizia kuchunguza na mwendo wa mwingine ambao ulimshangaza naamini zaidi ya yote nayo ni ni mwendo wa Mtu pamoja na msichana, hapo ukisoma katika tafsiri nyingi inaeleza kwa undani zaidi inasema jinsi mtu na msichana wanavyopendana, au mwenendo wao katika upendo.
Mara nyingi nimekutana na watu wakikosoa ndoa za wengine, labda utaona mmoja anasema mbona kulikuwa na wanawake wazuri kuliko Yule kwanini amemwoa yule bibi-kizee?, mwengine atasema kwanza alishakuwa na watoto huko nyuma ni kitu gani kilichomfanya ampendee, mwingine anatasema alikuwa ni kahaba maarufu anayejulikana mtaa mzima, imekuwaje huyu jamaa kampenda?, mwingine atasema Yule mwanaume hana mwelekeo, hana pesa Yule mwanamke kampendea nini?..Mwingine atakuwa kweli anayopesa lakini mwanamke /mwanamume Yule hakumpenda kwa ajili ya mali zake, Hayo ni maswali ambayo yapo kila mahali, Uliyempenda wewe mwingine atajiuliza ulimpendea nini?
Hilo ndio jambo linaloshangaza, kati ya wawili wapendanao. Kile kinachodhaniwa kuwa kingekuwa chanzo cha wao kuwa pamoja kinagundulika kuwa sio.
Na ndivyo ilivyo Kristo na kanisa lake..Kristo ndio Mume wa kanisa, ametuoa sisi tulio kanisa lake..
2 Wakoritho 11:2 “Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi.”
Yeye hakutazama kuwa sisi tulikuwa ni wachafu kiasi gani, au tulikuwa hatustahili kiasi gani?, Aliacha enzi yake na utajiri wake wote, na mamlaka yake, kuja duniani kutukomboa sisi, mambo ambayo hata malaika hawana majibu nayo, kwanini alitupenda… akatoa uhai wake kwa ajili yetu sisi tusiostahili..Ukatazama ni kitu gani kizuri alichokiona kwetu, huwezi kukiona, ukitazama ni faida gani basi ataipata kutoka kwetu huwezi kuiona, ametupenda tu kwasababu ametupenda…Huo ni mwendo wa ajabu sana.
Vivyo hivyo na Kanisa lake halisi linarudisha upendo wa namna hiyo hiyo kwake. Japo sasa hatumwoni kwa macho lakini tunampenda, wengi watajiuliza mbona huyo Yesu mnayemtumika hamumwoni? Jibu ni kwamba Upendo tulio nao kwake hautegemei macho kujidhihirisha, ni zaidi ya macho, na hata kama tutamwona kwa macho bado hatutategemea macho yetu kumpenda yeye..Kuna kitu ndani yetu kinachotufanya tutamani kuwa naye siku zote, hakielezeki kwa namna ya kibinadamu.
1Petro 1:8 “Naye mwampenda, ijapokuwa hamkumwona; ambaye ijapokuwa hamwoni sasa, mnamwamini; na kufurahi sana, kwa furaha isiyoneneka, yenye utukufu,”
Vile vile hatumpendi Bwana Yesu kwasababu ya utajiri wake,.Upendo wetu kwake ni zaidi ya hapo..
Hivyo wewe ndugu ambaye bado upo nje ya Kristo umeshajua ni kwasababu gani unaona ni ngumu kumtumikia Mungu usiyemwona au usiyetembea naye? ni kwasababu hujaingizwa bado kwenye pendo lake., Siku ukiingizwa hutahitaji macho ili kutembea naye, hutahitaji akupe kwanza kitu Fulani ndipo umpende..Kwani atajidhihirisha kwako kwa namna ya ajabu ambayo hata macho hayafikii hicho kilele.
Unasubiri nini? Yeye anasema “Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini.(Zaburi 34:8)”…
Mkaribishe sasa maishani mwako aanze kutembea na wewe mwendo ambao hata watu wa nje watashangaa unawezaje kuwa naye katika hali zote, utafanyika kuwa Bibiarusi na utaingia kwenye pendo ambalo litakusangaza hata wewe ambalo hutatamani hata utoke.
Warumi 8: 38 “ Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu”.
Ufunuo 22: 17 “Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure.”
Ubarikiwe.Tafadhali “Share” na kwa wengine..
Mada Nyinginezo:
AYUBU 28 : HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?
MSTARI HUU UNA MAANA GANI? “YUKO MWENYE HAKI APOTEAYE KATIKA HAKI YAKE”?
WALIOITWA NI WENGI, ILA WATEULE NI WACHACHE.
JIBU: Kwanza tunapaswa kufahamu kuwa si mapenzi ya Mungu sisi tupitie shida yeyote ile.Lakini zipo shida na dhiki ambazo Mungu huwa anaziruhusu ziwapate wale wateule wake kwa kutimiza kusudi Fulani, aidha kwa kuwafundisha, au kwa kuonyesha utukufu wake, au kwa kuwaonya, lakini mwisho wa siku shida hizi huwa zinaishia na mwisho mwema, na ndio maana mtume Paulo alisema mahali fulani katika
2Wakorintho 12:9 “ Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.10 Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.
Kadhalika zipo shida ambazo zinatokana wanadamu wenyewe, au tunaweza kusema zinasababishwa na wanadamu wenyewe na hizo hazipo ndani ya uwezo wa Mungu kuzizua bali kwa mwanadamu mwenyewe unajua ni kwasababu gani? Jaribu kuwazia mfano huu. Kama vile sisi wanadamu wenyewe kwa wenyewe hatupendi kuchaguliwa baadhi ya mambo kwamfano kijana anapofikia hatua ya kuoa au kuolewa, mzazi mwenye busara hatoweza kwenda kumlazimisha mtoto wake aoe mke amtakaye yeye hata kama msichana huyo atakuwa ni mzuri kiasi gani, au atakuwa na maadili kiasi gani, suala la maamuzi ni la mtu binafsi. Hivyo kitu pekee atakachoweza kufanya kama mzazi mwenye busara ni kumshauri tu, na kumpa mapendekezo mema lakini si kumlazimisha, hata kama anajua huyo mke mtoto wake aliyekwenda kumchagua atakuja kumletea madhara makubwa kiasi gani mbeleni, bado hana uwezo wa kumlazimisha asimwoe.
Na ndivyo ilivyo kwa Mungu wetu, mara zote anaona madhara yanayokuja mbele yetu, na ni kweli anatamani kuyazuia, lakini jambo analoweza kulifanya yeye kama Mungu wetu, ni kututahadharisha, au kutuonyesha jinsi mwisho wake utakavyokuwa, ili tusipotee au tusidondoke kwenye madhara. Sasa suala la kuamua kuendea au kutokuiendea njia hiyo ni la mtu binafsi. Ikiwa mtu atakubali mashauri ya Mungu basi, Mungu atamwepushia mabaya yale lakini ikiwa hatakubali basi Mungu atamwacha aangamie, hata kama Mungu atakuwa na uwezo mkubwa kiasi gani wa kumwepusha, bado hatoweza kufanya hicho kitu.
Kwasababu Mungu katuumbia sisi ndani yetu uwezo wa kuchagua.Ikiwa mtu ni mzinzi, na huku Mungu alishamwonya kuwa wazinzi hawataurithi ufalme wa mbinguni, na mtu huyo bado anaendelea katika njia zake mbovu, Hapo Mungu hawezi kumzuia japo anajua kabisa njia yake mwisho wa siku ataishia kifo, halafu aende kwenye ziwa la moto. Alimwonya shetani, hata kabla hajawa shetani, lakini hakumlazimisha asihasi, japo alijua kuwa ataasi na mwisho wa siku kuishia motoni,Mungu alimwonya lakini hakutaka kusimama katika kweli kama malaika wengine watakatifu walivyokuwa. Na ndivyo ilivyo hata kwetu,Mungu katuwekea maamuzi yetu binafsi. Kukubali au kukataa. Hakuna kulazimishwa.
Ubarikiwe
Mada zinazoendana:
JE! MUNGU ANASABABISHA AJALI, KWAMFANO AJALI YA KIVUKO CHA MV NYERERE KUZAMA?
ALIYE MKUU KATIKA UFALME WA MBINGUNI.
MAJARIBU MATATU YA YESU KRISTO
JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?