Category Archive Home

UFUNUO:Mlango wa 6-( Maelezo ya Muhuri saba)

Tukisoma kitabu cha ufunuo sura ya tano, tunaona Mungu akiwa ameketi kwenye kiti chake cha enzi akiwa na kitabu katika mkono wake wa kuume, kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kikiwa kimetiwa mihuri saba. Na tunasoma hapakuonekana mtu yeyote mbinguni wala duniani aliyestahili kukifungua hicho kitabu wala kukitazama, kwani Ni kitabu kilichobeba siri zote za ukombozi wa mwanadamu,kuanzia mwanzo wa mambo yote hadi mwisho wake, jambo lililomfanya hata Yohana alie machozi kwa kuwa hapakuona mtu yeyote aliyestahili kukifungua wala kukitazama. Lakini  mmoja  tu aliyeonekana amestahili kukifungua hicho kitabu, naye ni BWANA wetu YESU KRISTO haleluya!. (soma ufunuo sura ya tano yote.) utaona habari hiyo.

Kisha nikaona napo Mwana kondoo alipofungua moja ya zile muhuri saba, nikasikia mmoja wa wale wenye uhai wanne akisema, kama kwa sauti ya ngurumo, Njoo! nikaona na tazama, farasi mweupe na yeye aliyempanda ana uta, akapewa taji, naye akatoka, ali akishinda tena apate kushinda.

Lakini tukiendelea ile  sura ya 6 tunaona Bwana Yesu akivunja mihuri ya kile kitabu. Kumbuka kile kitabu sio kama hivi vitabu tunavyoviona leo, bali ni vitabu vya kuzunguka (scroll), na mihuri yake ni kama vifungo, tazama picha chini..

Na kila muhuri ulipofunguliwa ulikuwa unaambatana na tukio fulani, moja baada ya lingine, mpaka mihuri yote 7 imalizike ndipo kitabu kifunguliwe. Ni vema kama hujafahamu bado juu ya NYAKATI 7 ZA KANISA (ufunuo 2&3), ukasome kwasababu mihuri hii inaendana sana na zile nyakati saba za kanisa. kama utahitaji fuatilia link hii


MUHURI WA KWANZA:

Ufunuo 6:1-2, “Kisha nikaona napo Mwana kondoo alipofungua moja ya zile muhuri saba, nikasikia mmoja wa wale wenye uhai wanne akisema, kama kwa sauti ya ngurumo, Njoo! nikaona na tazama, farasi mweupe na yeye aliyempanda ana uta, akapewa taji, naye akatoka, ali akishinda tena apate kushinda.”

Tunaona hapo kuna wale wenye uhai wanne na wale farasi wanne.Wale wenye uhai wanne walioonyeshwa katika sura hii, wanaashiria nguvu ya Mungu iliyoachiwa kwa watu wake, kupambana na uovu na njama za yule adui.Mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba, na wa pili alikuwa mfano wa ndama na wa tatu kama mwanadamu, na wanne kama tai arukaye.(Ufunuo 4:6-8). Vivyo hivyo na kwa wale farasi: farasi wa kwanza alikuwa ni mweupe, wa pili mwekundu, watatu ni mweusi na wanne ni wa rangi ya kijivujivu. Embu tuangalie ufunuo wa mambo haya kwa ufupi.

 Na alipoifungua muhuri ya pili, nikamsikia yule mwenye uhai wa pili akisema Njoo!. akatoka farasi mwingine, mwekundu sana, na yeye aliyeimpanda alipewa kuiondoa amani katika nchi, ili watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa.

Kwahiyo muhuri wa kwanza ulipofunguliwa, yule mwenye uhai wa kwanza aliposema njoo! akatoka farasi mweupe, na aliyempanda juu yake ana uta (upinde wa mshale). Huyo farasi mweupe na aliyempanda  ni roho ya mpinga Kristo ikianza kutembea katika kanisa la Mungu kwenye kanisa la kwanza Kabisa (EFESO) ,Lilidumu kwa kipindi cha kati ya AD 53- AD 170.

Mtume Paulo akiwa kama mjumbe wa kanisa hilo alisema hivi..2thesalonike 2:3 ” Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yeyote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu: akafunuliwa yule mwana wa kuasi, mwana wa uharibifu.” kwahiyo hapo tunaona kuwa mwisho wa yote usingefika kabla ya ule uharibifu( ukengeufu) kuja kwanza na kuingia katika kanisa. Na huo ukengeufu ndio ulipoanza na huyo farasi mweupe, kumbuka rangi nyeupe inaashiria usafi hivyo shetani alikuwa anajigeuza kama malaika wa nurukatikati ya kanisa lakini kwa ndani alikuwa ni mbwa mwitu mkali.(2 Wakoritho 11:13-15)

Hii roho ya shetani ilianza kuingia katika kanisa la kwanza baada ya mitume kuondoka hapa Paulo anasema matendo 20:29 ” najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao.” 1Yohana 2:18 aliongezea kusema ” watoto ni wakati wa mwisho na kama vile mlivyosikia ya kwamba mpinga kristo yuaja, hata sasa wapinga kristo wengi wamekwisha kuwapo. kwasababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho. Walitoka kwetu lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wakwetu wangalikaa pamoja nasi.Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu.”

Kwa hiyo hapa tunaona mitume walilionya kanisa lililokuwa kipindi kile juu ya mafundisho ya uwongo ambayo hayakuhubiriwa na mitume. Hivyo yule farasi mweupe ni roho ya mpinga kristo ikitembea katika kanisa la kwanza, na alionekana mweupe na aliyempanda ameshika uta (upinde) lakini hana mshale, kuashiria kutokuwa na madhara yoyote (yaani kuhusisha mauaji ya watakatifu) . roho hii ilanza kuingia kama mafundisho ya uwongo lakini Mungu aliachia Roho ya kuishinda iliyofananishwa na yule mwenye uhai wa kwanza ambaye ni mfano wa SIMBA aliyesema Njoo!. Tabia ya simba ni mnyama asiyeogopa, mwenye ujasiri hivyo wakristo wa kipindi kile waliweza kuishinda ile roho ya mpinga kristo kwa ujasiri wa neno la Mungu.


Kumbuka Nyakati hii ya mpanda farasi wa kwanza ilidumu kati ya kipindi cha 53AD-170AD. katika kanisa la kwanza ambalo ni Efeso.

Kristo alitoa pia angalizo kwa kanisa hili tunasoma katika kitabu cha ufunuo 2:2″ nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio ukawaona kuwa ni waongo……lakini unalo neno hili, ya kwamba wayachukia matendo ya wanikolai ambayo na mimi nayachukia.”.

MUHURI WA PILI:


Ufunuo 6:3-4 ” Na alipoifungua muhuri ya pili, nikamsikia yule mwenye uhai wa pili akisema Njoo!. akatoka farasi mwingine, mwekundu sana, na yeye aliyeimpanda alipewa kuiondoa amani katika nchi, ili watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa.”

Hapa katika muhuri huu tunaona shetani (roho ya mpinga kristo), baada ya kuona kwamba ameshindwa kuwazuia wakristo wa kweli kumwabudu Mungu katika Roho na kweli wakisimamia neno wakiongozwa na ile nguvu ya Mungu kwa mfano wa simba ambayo ndiyo ile Roho ya Mungu aliyoiachia kwa watu wake kumshinda shetani,

Hivyo shetani akaamua  kubadilisha mbinu zake za kuwashambulia wakristo, kwa kubadilika kutoka farasi mweupe kwenda kuwa farasi MWEKUNDU, na tunaona aliyempanda ni yule yule aliyekuwa anamwendesha yule farasi wa kwanza. Tunasoma kuwa alipewa mamlaka ya kuiondoa amani na upanga mkubwa mkononi mwake, kuashiria kuleta dhiki za mauaji kwa wale watu wanaomwamini Mungu na kuzishika amri zake, Kumbuka shetani huwa hafanyi vita na watu wote bali na watakatifu wa Mungu wanaolishika NENO lake.

Hii roho ya uovu(mpinga kristo) ilianza kama mafundisho yasiyohusisha mauaji, (ndiyo yale matendo ya wanikolai), baada ya kudumu muda mrefu yakatengeneza DINI, Na hii dini kumbuka ilianzia Roma kwasababu wakati ule RUMI ndio ilikuwa inatawala dunia, Wakati huo kulitokea makundi mawili, kundi lilishikilia mafundisho ya mitume tu! na lile lilichukua mafundisho yaliyochanganyikana na uongo. Ikapelekea kutokea mizozano kati ya haya makundi mawili, hivyo Rumi wakaunda dini moja chini ya mtawala(costantine), inayoitwa UNIVERSAL(CATHOLIC) CHURCH (AD 315), yaani DINI YA ULIMWENGU MZIMA. Hapo ndipo upagani wa kirumi ulipochanganyikana na Ukristo. Na ilipitishwa sheria yoyote atakayeonekana anaenda kinyume na DINI hiyo sheria ilikuwa ni moja tu! KIFO!!

Katika utawala wa Roma, Historia inaonyesha kuanzia mwaka 354 AD hadi kufikia kipindi cha matengenezo ya kanisa utawala wa Rumi chini ya kanisa katoliki ulifanikiwa kuwauwa wakristo zaidi ya milioni 68, kwa dhumuni la kuimarisha itikadi za dini yao. kwa mtu yeyote kuwa na imani nyingine nje ya dini ya kikatoliki adhabu ilikuwa ni kifo. Wakristo na wayahudi wengi waliuawa kwa kusimamia imani yao. damu nyingi za watakatifu zilimwagika.

Huu ndio ule upanga wa yule FARASI MWEKUNDU, alikuwa na kazi moja kuondoa amani katikati ya watakatifu. Na wakati huu wa farasi mwekundu ulitembea katika makanisa mawili yaani SMIRNA na PERGAMO. kati ya mwaka 170 AD -606 AD.

lakini pamoja na hayo Mungu alijua namna gani ya kuwashindia watueule wake hivyo aliachia Roho ya kuweza kuikabili hiyo nguvu ya mpinga kristo nayo ni nguvu iliyofananishwa na NDAMA (yaani YULE MWENYE UHAI WA PILI aliyesema njoo!), Ndama ni mnyenyekevu sana yupo tayari kwenda kuchinjwa na siku zote anaandaliwa kwa ajili ya kutolewa sadaka, hivyo wakristo wengi kwa kutaka wenyewe walijitoa maisha yao kwenda kuuawa kwa ajili ya imani yao bila kuogopa kwani Mungu ndiye aliyeachia hiyo Roho ya WEPESI juu yao, Kama vile tu BWANA wetu alivyokuwa mnyenyekevu akatii mpaka mauti ya msalaba, walichinjwa, walisulibiwa, waliliwa na simba, waliburutwa lakini kwa jinsi walivyozidi kuwauwa ndivyo walivyozidi kujitoa nafsi zao ziwe dhabihu .

 na alipoifungua muhuri ya tatu,nikamsikia yule wa tatu mwenye uhai akisema, Njoo! nikaona, na tazama, FARASI  MWEUSI, na yeye aliyempanda ana mizani mkononi mwake. Nikasikia kama sauti katikati ya hao wenye uhai wa nne, ikisema, kibaba cha ngano kwa nusu rupia, na vibaba vitatu vya shayiri kwa nusu rupia, wala usiyadhuru mafuta wala divai."

warumi 8:36 ” …..kwa ajili yako tunauwa mchana kutwa, tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa” kipindi cha huyu farasi mwekundu kilidumu mpaka mwishoni mwa kanisa la pili.


MUHURI WA TATU:

Ufunuo 6:5 “na alipoifungua muhuri ya tatu,nikamsikia yule wa tatu mwenye uhai akisema, Njoo! nikaona, na tazama, FARASI  MWEUSI, na yeye aliyempanda ana mizani mkononi mwake. Nikasikia kama sauti katikati ya hao wenye uhai wa nne, ikisema, kibaba cha ngano kwa nusu rupia, na vibaba vitatu vya shayiri kwa nusu rupia, wala usiyadhuru mafuta wala divai.”

Sasa baada ya shetani kuona anawaua wakristo na bado wanaendelea kukubali kwenda kuuawa kwa kuishikilia imani yao iliyoanzishwa na mitume na si vinginevyo wakipinga mafundisho ya dini ya uongo(yaani ya kikatoliki), akaamua kubadili mbinu ya kulivamia kanisa la Mungu kwa namna nyingine kwa kubadilisha rangi kutoka kuwa farasi mwekundu kwenda kuwa farasi mweusi.

Hichi ni kipindi kinachojulikana na wanahistoria wengi kama kipindi cha giza (dark age) kilidumu kwa zaidi ya miaka 1000 kuanzia karne ya 5 mpaka karne ya 16. Ni kipindi ambacho utawala wa kipapa chini ya dini ya kikatoliki ,ulianza kuuza kile wanachokiita neno la Mungu kwamfano mtu akitaka kuoa au kuolewa ni lazima atoe fedha, ibada za kuwaombea wafu (ambazo ni kinyume na neno la Mungu) ni lazima utozwe pesa, kushiriki meza ya Bwana ni lazima utozwe pesa, ukitaka kusamehewa dhambi unapaswa kutoa pesa, ukitaka kuombewa kama unaumwa ni lazima utoe pesa n.k ndio maana tunasoma yule mpanda farasi alikuwa amebeba mizani mkononi mwake hii inamaanisha kuwa ukitaka kitu lazima utoe kitu.

Kwa njia hii kanisa katoliki likiongozwa na utawala wa kipapa lilijikusanyia UTAJIRI MKUBWA SANA USIO WA KAWAIDA, sio ajabu hata leo hii tunaona jinsi taifa la Vatican lilivyo na utajiri mkubwa na halifanyi biashara yoyote ya kuliingizia kipato, linadhamini pesa za kujenga maseminari, na mashule, pamoja na miradi mingi mikubwa duniani kote inayogharimu mabilioni ya dola na bado halifanyi biashara yoyote. Utajiri huu ulianza katika kile kipindi mpanda farasi mweusi. Kwa kuwa hii dini ya uongo ilikuwa imeshaenea duniani kote, NURU ya Mungu ilififia sana, ikasababisha GIZA nene kulikumba dunia kwasababu hakuna mafundisho ya kweli yanayohubiriwa tena. Uchawi na ushirikina vilienea sana wakati huo.

Lakini pamoja na hayo Mungu aliachilia nguvu ya kulishinda hilo giza kwa watu wake wachache waliokuwa wanashikilia mafundisho ya mitume,na ile sauti iliyosikika ikisema usiyadhuru mafuta wala divai. Mafuta yanaashiria Roho Mtakatifu na divai inaashiria ufunuo wa neno la Mungu, hivyo basi lile kundi dogo la Mungu lililopitia kwenye hichi kipindi kirefu cha giza Bwana aliachia Roho ya ufunuo juu yao kwa mfano wa USO WA MWANADAMU ikiashiria hekima ya kibinadamu, ndipo kuanzia huo wakati Mungu akaanza kuwanyanyua wana-matengenezo kuirejesha ile Nuru ya Mungu iliyokuwa inakaribia kutoweka.

Hivyo basi Katika hichi kipindi cha giza hadi kwenye matengenezo ya kanisa, Mungu alinyanyua watu kama Martin Luther na fundisho la (mwenye haki wangu ataishi kwa imani) ambapo hapo mwanzo ilikuwa hairuhusiwi mtu yeyote kufundisha au kusoma biblia isipokuwa kwa viongozi tu wa kanisa katoliki!.hivyo Mungu aliendelea kunyanyua na wengine wengi kama, Zwingli, Calvin, Knox,Bucer, John Wesley na ujumbe wa (Pasipo utakatifu hakuna yoyote atakayemwona Mungu) n.k .Kwa ajili ya matengenezo ya kanisa na kulirejesha katika yale mafundisho ya mitume ya mwanzo ambayo shetani alijaribu kuyafukia.

Wakati huu wa FARASI MWEUSI, ulidumu katika makanisa matatu, yaani ; THIATIRA, SARDI, na FILADELFIA. Kuanzia mwaka AD 606-1520 AD.. ndipo ukaja wakati wa matengenezo ya kanisa.

MUHURI WA NNE:

Ufunuo 6:7-8 “Na alipoifungua muhuri ya nne, nikasikia sauti ya yule mwenye uhai wa nne akisema, Njoo! nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu na yeye aliyempanda jina lake ni mauti, na kuzimu ikafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, na kwa hayawani wa nchi.”

Tunaona hapa yule MPANDA FARASI ambaye ndiye mpinga Kristo alipoanza kubadilika kutoka kwenye farasi mweupe akaenda kwenye farasi mwekundu, akaenda tena kuwa farasi mweusi na sasa kwa FARASI WA KIJIVUJIVU. Rangi ya kijivujivu inaashiria mchanganyiko wa rangi zote tatu yaani nyeupe, nyekundu na nyeusi. ambayo pia inaashiria udanganyifu na mauti.

Hii ni roho ya mpinga kristo inayotembea leo hii katika kanisa  la mwisho la saba, (LAODIKIA), farasi huyu amechanganyikana na anazo tabia zote tatu za wale farasi wa kwanza. Ameitwa kuzimu na mauti inafuatana naye kwasababu katika  kipindi cha mwisho anaonyesha rangi zake zote na kujifunua yeye ni nani kwa kuwaua watu na kuwapeleka kuzimu kwa namna mbili:

1) KWA KUWAUWA WATU KIROHO kwa  mafundisho yake ya uongo, akiyaleta makanisa yote na dini zote pamoja (WORLD COUNCIL OF CHURCHES) Kwa ulaghai wake kama ilivyotabiriwa katika kitabu cha Daniel ili kuunda ile chapa ya mnyama, ambapo hakuna mtu atakayeweza kuuza wala kununua pasipo hiyo.

2) Na namna ya pili ni kwa kuwaua wakristo wote aidha kwa wazi au kwa siri wale wanaoenda kinyume na yeye, zaidi sana atakuja kuonyesha rangi yake katika kile kipindi cha ile dhiki kuu.

Kumbuka hazina yote ya dunia ipo Roma hii inaonyesha yule farasi mweusi anatembea katika utawala wa dini ya katoliki. Na tabia zote za wale farasi wa kwanza amezibeba huyu wa kijivujivu. unaweza ukaona tunaishi katika kipindi cha hatari kiasi gani.

Lakini pamoja na hayo Mungu ameachia nguvu ya kupambana na roho hii ya mpinga kristo nayo imefananishwa na yule MWENYE UHAI WA NNE, (Aliyefananishwa na TAI). Tai ana uwezo wa kuona vitu vya mbali sana na Bwana aliwafananisha manabii wake na Tai, hivyo basi katika kanisa hili la Laodikia ambalo ndio la mwisho Bwana ameachia Roho ya kinabii kuweza kuzitambua hila za yule adui, na kuturudishwa katika imani ya mababa(yaani mitume wa Kristo) na nguvu Mungu aliyoiachia ni ROHO YA UFUNUO ya kumtambua Mpinga Kristo na chapa yake na ujumbe wa kutoka kwake na kutokushiriki mafundisho yake ya uongo..

Na alipoifungua muhuri ya nne, nikasikia sauti ya yule mwenye uhai wa nne akisema, Njoo! nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu na yeye aliyempanda jina lake ni mauti, na kuzimu ikafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, na kwa hayawani wa nchi."

 

Ufunuo 18:4 Inasema “…tokeni kwake, enyi watu wangu msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.” Ikiwa wewe ni mkristo na hauna ndani yako Roho ya ufunuo ya kuona mbali kama Tai huwezi kamwe kumshinda shetani, utaangukia kumezwa na yule mnyama kwa mafundisho yake ya uwongo na unajua ni jambo gani linaambatana naye,

biblia inasema ni MAUTI NA KUZIMU, hakuna namna yoyote utakayoweza kumshinda shetani kama upo kwenye mifumo ya madhehebu na DINI ya uongo. umekwisha pokea chapa ya mnyama pasipo wewe kujijua, Kama hauna Roho Mtakatifu mwombe Mungu akupe na Roho ya ufunuo ya kulielewa neno lake.Amen!


Na huu wakati wa FARASI WA KIJIVUJIVU ulianza, mwaka 1906- Hadi mwisho wa dunia utakapofika pale utawala wa mpinga-kristo utakapohukumiwa na YESU KRISTO, BWANA WA MABWANA, na MFALME WA WAFALME.


MUHURI WA TANO:

Ufunuo 6:9-11 “Na alipoifungua muhuri ya tano, nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao. Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi? Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vilevile kama wao.”

Hapa tunaona hakuna mwenye uhai yeyote akitangaza kufunguliwa kwa muhuri huu, hivyo hatuoni kanisa la mataifa likihusishwa wala mpanda farasi yoyote habari yao imeshakwisha.. lakini ulipofunguliwa muhuri wa tano zilionekana roho nyingi chini ya madhabahu zikimlilia Mungu. Sasa hizi ni roho za wayahudi waliouawa kipindi cha utawala wa kimabavu wa Adolf Hitler (Holocaust), watu hawa waliuliwa kwa sababu moja tu kuwa wao ni kwasababu wayahudi na si kingine!, historia inasema Hitler aliwaua wayahudi zaidi ya milioni 6 katika kipindi cha vita ya pili ya dunia.

Tunafahamu licha ya kwamba wayahudi wengi hawamwini YESU kuwa ni MASIA wao lakini bado ni watu wa Mungu na shetani anawachukia, kwasababu wanashika NENO la ushuhuda wao waliopewa na Mungu, (ambayo ni TORATI). Kwahiyo hapa tunaona kuwa hawa walikufa kwa ushuhuda wao, na sio ushuhuda wa Yesu Kristo, na pia hawa wanamwomba Mungu alipize kisasi juu ya maadui zao, kwani kulingana na torati kulipiza kisasi ni desturi ya wayahudi.

Na alipoifungua muhuri ya tano, nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao. Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi? Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vilevile kama wao."

(Haya ni mateso ya wayahudi chini ya utawala wa dikteta Adolf Hitler)

kwamfano tunaona kuna maandiko yanayosema jino kwa jino, jicho kwa jicho,n.K ,Hivyo hatuwezi tukashangaa kwanini hapa walikuwa wanamwomba Mungu alipize kisasi juu ya maadui zao, lakini hiyo siyo desturi ya wakristo. Wakristo hawalaani wala hawaombi kisasi, bali wao husema baba uwasemehe, tunaona mfano wa Bwana wetu Yesu Kristo na Stefano walivyofanya.Hivyo hizi roho zinazozungumziwa hapa ni wayahudi na sio wakristo.

Na pia tunaona walipewa nguo ndefu nyeupe, hizi zinaashiria kupewa neema ya wokovu kwa ushuhuda wao wenyewe walioushikilia, kwa lile agano Mungu alilomuahidia Ibrahimu na uzao wake,hawa ni wale wayahudi waliokuwa waaminifu na dini yao ya kiyahudi wakiishikilia torati kikamilifu hata kufa , wakaambiwa tena wangojee kwa kipindi kifupi mpaka idadi ya wajoli wao itimie ambao watakufa kama wao.hii inamaanisha katika kipindi cha ile DHIKI KUU  ambayo mpinga kristo atawaua wayahudi wengi na kulivunja lile agano atakalofanya na wayahudi ambalo limezungumziwa katika kitabu cha Danieli sura ile ya tisa.


MUHURI WA SITA:

Ufunuo 6:12 “Nami nikaona, alipoifungua muhuri ya sita, palikuwa na tetemeko kuu la nchi; jua likawa jeusi kama gunia la singa, mwezi wote ukawa kama damu,

13 na nyota zikaanguka juu ya nchi kama vile mtini upukutishavyo mapooza yake, utikiswapo na upepo mwingi.

14 Mbingu zikaondolewa kama ukurasa ulivyokunjwa, na kila mlima na kisiwa kikahamishwa kutoka mahali pake.

15 Na wafalme wa dunia, na wakuu, na majemadari, na matajiri, na wenye nguvu, na kila mtumwa, na mwungwana, wakajificha katika pango na chini ya miamba ya milima,

16 wakiiambia milima na miamba, Tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na hasira ya Mwana-Kondoo.

17 Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani awezaye kusimama?”

Hapa tunaona muhuri huu ulipofunguliwa dunia nzima iliathirika na ndiyo ile siku kuu ya kuogofya ya Bwana kama Yesu Kristo alivyoizungumzia katika katika mathayo 24:29-30 ” Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika; ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi”. Hii siku ya Bwana itakuja mwishoni mwa miaka mitatu na nusu baada ya kumalizika ile dhiki kuu.

Siku hii ya Bwana itadumu kwa kipindi cha siku 75 ikianzia kwa kumimina ghadhabu ya Mungu katika dunia, ambayo itahusisha vita vya harmagedoni (ufunuo 19-21, zekaria 14:1-4, 12).ndani ya siku hizi 75 kutakuwa pia na kufufuliwa kwa watakatifu waliouawa katika kipindi cha dhiki kuu (ufunuo 11:18, 20:4), itamalizia na hukumu ya mataifa (mathayo 25:31-46) kabla ya kuingia katika matengenezo ya utawala wa miaka 1000 wa Bwana Yesu Kristo (mathayo 19:28).

hizi siku 75 zinapatikana kutoka katika zile siku 1335 zilizozungumziwa katika kitabu cha daniel 12:12. siku hizi 1335 ukitoa siku 1260 (au miezi 42) ambayo mpinga kristo atatawala baada ya kuikomesha sadaka ya kuteketezwa ya daima daniel 9:24-27″……Naye atafanya agano thabiti na watu wengi kwa muda wa juma moja; na kwa nusu ya juma hiyo ataikomesha sadaka na dhabihu; na mahali pake litasimama chukizo la uharibifu; na hivyo, hata ukomo, na ghadhabu iliyokusudiwa imemwagwa juu yake mwenye kuharibu.”


MUHURI WA SABA:


Ufunuo 8:1 “Hata alipoifungua muhuri ya saba, kukawa kimya mbinguni kama muda wa nusu saa. “

Mstari wa pili unaelezea juu ya wale malaika waliojiweka tayari kupiga baragumu ambayo ni habari nyingine isiyohusiana na muhuri wa saba, Huu ukimya mbinguni unaashiria kuna jambo linakwenda kutokea ambalo ndilo tunaloliona katika ufunuo sura ya kumi.

Kumbuka kulingana na mtiririko wa matukio yatakayotokea siku za mwisho, ni dhahiri kuwa Muhuri wa Saba utatimia kabla ya Muhuri wa sita kutimia.

katika sura ya kumi.

Ufunuo 10:1 “Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto.

2 Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, nao wa kushoto juu ya nchi.

3 Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao.

4 Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike”

Malaika huyu anayeonekana hapa si mwingine bali ni Bwana Yesu Kristo akiwa ameshika kile KITABU KIDOGO. kumbuka kitabu hichi ndio hicho kilichokuwa kumefungwa na mihuri 7, Na ndani ya muhuri huu wa saba ambao bado haujafunuliwa kwetu kwa sasa lakini utakapokuja kufunuliwa na upo mbioni kufunuliwa, UTAMPA BIBI ARUSI WA KRISTO IMANI YA KWENDA KWENYE UNYAKUO (ambapo ukisoma utaona siri hii imejificha katika zile ngurumo saba Yohana alizoambiwa asiziandike Ufunuo 10:4). Na muhuri huu wa saba utatimia kabla ya muhuri wa sita kutimia, kwasababu muhuri wa sita unaelezea siku kuu ya Bwana ambayo ni mwisho wa mambo yote.

kulingana na 1thesalonike 4:16-17 “Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele”.

Kuja kwa Bwana kutafuata hatua tatu, ya kwanza ni Bwana atakuja na mwaliko (shout) na ya pili ni sauti ya Malaika Mkuu na ya tatu ni parapanda ya Mungu.

Hatua ya kwanza: ya mwaliko ndiyo tuliyopo sasa hivi iliyoletwa na Mjumbe wa kanisa la saba (William Branham) yenye ujumbe wa kutuandaa sisi kumpokea Kristo na kuturudisha katika ukristo wa biblia.

Mathayo 25:6 “Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki” Mjumbe wa kanisa la saba alikuja kututangazia ujio wa Bwana Yesu Kristo ambao ni wakati wa sisi kuzitengeneza taa zetu na kuwa tayari kumlaki Bwana Yesu mawinguni.

Hatua ya pili: ni sauti ya Malaika mkuu. na ndiye tunayemwona katika ufunuo 10 na si mwingine zaidi ya Yesu Kristo, na ujumbe wake utakuwa kwa yule bibi arusi aliyekwisha kujiweka tayari kumlaki, bikira safi ambaye taa yake inawakaa, huyu ni mkristo aliyebatizwa na Roho Mtakatifu aliyejitenga na uasherati wa yule kahaba (dini ya katoliki na madhehebu yote) yasiyofanya neno la Mungu kuwa mwongozo wao na kushikilia mafundisho ya wanadamu na ibada za kipagani. Huyu bibi arusi atakuwa bikira ndiye pekee atakayeisikia sauti ya malaika mkuu ambayo itahubiriwa na zile ngurumo saba tunazoziona katika kitabu cha ufunuo 10:3-4 Yohana alizoambiwa asiziandike lakini mwingine yoyote asiye bikira safi hatoweza kuisikia sauti ya hizo ngurumo saba.

NGURUMO SABA zitakuwa ni Sauti saba(watu,au huduma,) ambazo Mungu atazinyanyua katika kipindi hichi cha mwisho na kuleta uamsho mkuu duniani kote, ambazo kupitia hizi sauti saba tutapata imani itakayotuwezesha sisi kwenda katika unyakuo. Na hizi ngurumo saba zipo karibuni kutoa sauti zake..je? umejiweka tayari? unaye Roho Mtakatifu? kumbuka watakaoweza kuupokea ujumbe wa ngurumo saba ni bibi arusi tu mwenye Roho wa kristo. Na wakati huo ukifika kutakuwa hakuna muda tena, ni wakati wa wewe kutengeneza mambo yako sasa vizuri kwa Bwana.


Hatua ya tatu
: na ya mwisho ni parapanda ya Mungu. katika kipindi hichi kila mmoja wetu aliye mkristo ataisikia sauti ya Mungu ikimwita na gafla tutaona mabadiliko ya miili yetu na kuchukuliwa juu mbinguni kwa Bwana milele na milele haleluya!.

Kwahiyo kwa kuelewa Ufunuo wa MIHURI SABA, utaweza kufahamu kalenda ya Mungu na wakati unaoishi kwamba tunaishi katika siku za mwisho..


Mungu akubariki.!

Print this post

UFUNUO: Mlango wa 5

Shalom! Karibu katika mwendelezo mfupi wa uchambuzi wa kitabu cha ufunuo, kwa neema za Mungu tulishatazama sura zilizotangulia tukaona ile sehemu ya kwanza ya maono Yohana aliyoonyeshwa katika sura ya kwanza, ilihusu sana sana ujumbe wa yale makanisa saba ambayo tunayasoma katika ile sura ya 3 na ya 4, hivyo kama haujafahamu bado ufunuo wa yale makanisa 7 katika wakati wetu tunaoishi sasa, ni vema ukapitia kwanza kule, ili tuende pamoja katika sura hii.

Katika hii sura ya tano, tunaona Yohana akionyeshwa mfululizo wa maono mengine tofauti na yale ya kwanza ambayo alionyeshwa katika sura ile ya kwanza, sehemu hii ya pili ya maono haya yalianzia katika ile sura ya nne, yakaendelea mpaka sura ya 5, ambapo tunaona Yohana alichukuliwa juu mbinguni na kuonyeshwa kiti cha enzi cha Mungu katika roho, na wale wazee 24 wakiwa wamekizunguka kiti cha enzi, na wale wenye uhai 4, kadhalika na zile Taa saba za moto ambazo ndio Roho 7 za Mungu, na mbele ya kiti cha enzi kulikuwa pia na bahari ya kioo kama bilauri ikifunua weupe na usafi wa watakatifu, na bahari ikifunua wingi wa watakatifu, tutakuja kuona vizuri katika ile sura ya 15 inaonekana bahari nyingine ya kioo isipokuwa hiyo imechanganyikana na moto, ikifunua watakatifu waliosafishwa kwa moto katika dhiki kuu,.

Tukirudi kwenye sura ya tano, tunaona mkazo umewekwa kwa yule aliyeketi katika kiti cha enzi, na kile alichokuwa amekishika katika mkono wake wa kuume..Tusome hapo.

Ufunuo 5: 1 “Kisha nikaona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba”.

Kumbuka hapo biblia inasema “yeye” ikimaanisha ni mmoja ambaye alishazungumziwa katika sura ya 4:2, ameshika KITABU kilichoandikwa NDANI na NYUMA. Na huyu si mwingine zaidi ya Elohim katika ofisi yake ya ubaba, ambaye yeye kabla ya kuumba ulimwengu vitu vyote vilikuwa ndani yake, yeye ndiye mjenzi wa vitu vyote vilivyokuwepo na vitakavyokuwepo, asiyekuwa na mwanzo wala asiyekuwa na mwisho, na kama yeye ndiye aliyebuni maisha na dunia na wanadamu, na malaika na viumbe vyote kama ni hivyo basi ni dhahiri kuwa yeye ndiye mwenye siri na misingi ya vitu vyote. Kuanzia mwanzo wao mpaka mwisho wao, Na hakuna yeyote atakayeweza kuvumbua jambo lolote kwa uweza wake au nguvu zake mwenyewe isipokuwa kwanza kafunuliwa na Mungu (Elohimu).

Kama vile tunafahamu leo hii mtu akibudi chombo chake labda tusema ni gari, siku akitaka kwenda kumpa mtu mwingine labda kumuuzia au kumrithisha hawezi kumpa hivi hivi tu bila kuambatanisha na mwongozo (MANUAL) fulani, ili kumsaidia yule anayepokea kuweza kukifahamu na kukitumia chombo hicho kwa ufasaha zaidi sawa sawa na jinsi kilivyokusudiwa kiwe. Kwa kupitia mwongozo ule atafahamu uwezo wa usafiri wa chombo chake, atafahamu wakati unaopaswa kukifanyia marekebisho, atafahamu aina ya nishati itakachotumia, atafahamu tahadhari za kuchukua wakati wa matumizi ili kisimletee madhara yoyote kwake bali faida n.k..

Vivyo hivyo na Mungu (Elohimu) kama muumbaji wa kila kitu alipoiumba dunia kwa hekima zake nyingi, na kuamua kumpa mwanadamu hakumpa pasipo mwongozo, wa jinsi ya kuindesha hii dunia na kuitunza ili iweze kumuhifadhi mtu milele asipatikane na madhara yoyote na aishi kwa amani na furaha siku zote alizowekewa mbele yake, Hivyo huu mwongozo (MANUAL) alianza kupewa mtu wa kwanza Adamu pale Edeni, Mungu alianza taratibu taratifu kumpa maarifa na kanuni za kuishi na kuitawala dunia milele.

Lakini tunaona Adamu mwanzoni kabisa mwa maagizo yale aliharibu mpango mzima, kwa kutokutii na kufuata yale aliyoambiwa ikapelekea ule mwongozo kutokuwa na maana tena mbele yake (ukafichwa) kwasababu mambo yote ameshayaharibu tangu mwanzo.

Kwamfano wewe unalo gari lako, umelibuni kwa utashi mwingi, na umekusudia kumrithisha mwanao liwe lake moja kwa moja, lakini wakati unaanza tu kumwonyesha gari kwa nje, matairi, vioo, milango, site mirrors n.k. yeye unashangaa tayari kashafungua mlango na kupiga ufunguo kasha kukanyaga mafuta na kuanza kuondoka,kumbuka na hapo hajawahi kuendesha gari hata siku moja, ni mara yake ya kwanza, ila amesikia tu! Ukishawasha gari weka “D” kisha kanyaga mafuta gari litaenda..wewe unadhani ni jambo gani litatokea hapo kwa mtu kama huyo? Ni dhahiri kuwa atasababisha ajali?? Na mwisho wake ni mauti??. Hicho Ndicho kilichomtokea Adamu, pale Bwana alipomwonyesha kuwa hii dunia ni urithi wake, hakusubiria ule mwongozo ambao alikuwa anapewa taratibu taratibu, siku baada ya siku na Baba yake…yeye alikimbilia moja kwa moja kusikiliza mwongozo bandia wa Shetani, wa jinsi ya kuiendesha hii dunia kama Mungu anavyoiendesha, Biblia inasema..

Mwanzo 3:4 “Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa,
5 kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya”.

Unaona hapo ni kweli ulikuwa ni mpango wa Mungu Adamu kufahamu mema na mabaya, lakini ilikuwa sio kwa wakati ule, bali Mungu alikusudia kumpa mwongozo kidogo kidogo, lakini yeye kwa maneno machache tu ya shetani alidhana kuwa angeweza kuiendesha dunia kama Mungu, matokeo yake maarifa yale yalimsababishia KIFO. Hivyo Mungu asingeweza kuendelea kumpa mwongozo ule mtu ambaye yupo katika hali ya mauti. Kuanzia hapo Mungu AKAUFUNGA ule mwongozo kwa MIHURI asiweze mtu yeyote kuifungua mpaka atakapoonekana anayestahili.

Kwahiyo Huu mwongozo ni kitabu cha MAARIFA ya Mungu juu ya mwanadamu na urithi aliopewa, kimebeba siri zote za uumbaji wa ulimwengu, misingi yake ilipo, namna ya kuifanya idumu milele, namna ya kuifanya iwe na amani,furaha, namna ya kuifanya mwanadamu asiishi kwa taabu, shida, maumivu, kero, adha n.k..kimebeba siri zote zinazohusiana na sayari na magimba mengine huko angani, na mambo mengine mengi sana ambayo hata sasa hivi hatuyajui..Hayo yote yapo ndani ya hicho kitabu na ndio hicho tunakuja kukiona tena katika Ufunuo sura ya 5 kimeshikwa na yeye (ELOHIMU) mwenyewe katika kiti chake cha enzi kikiwa kimefungwa kwa mihuri saba huku kikiwa kimeandikwa NDANI na NYUMA.

Tukiendelea kusoma.

Ufunuo 5: 2 “Nikaona malaika mwenye nguvu akihubiri kwa sauti kuu, N’nani astahiliye kukifungua kitabu, na kuzivunja muhuri zake?

3 Wala hapakuwa na mtu mbinguni, wala juu ya nchi, wala chini ya nchi, aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama.

4 Nami nikalia sana kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama.

5 Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba.

6 Nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote.

7 Akaja, akakitwaa kile kitabu katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi”.

Unaona hapo? Hakuonekana mtu aliyestahili kukifungua hicho kitabu wala kukitazama, mara baada ya Adamu kuasi tu,tangu huo wakati hakuonekana mtu yeyote aliyestahili, na sio tu kikifungua bali hata kukitazama,! Hivyo Yohana alivyoona alilia sana, kuona kuwa dunia itaendelea kubaki vile vile katika hali yake ya ubovu, kama ilivyokuwa zamani, majanga, magonjwa, vifo, dhiki, taabu, shida, vitaendelea kuwepo, dunia itaendelea kuyumba yumba kama mlevi hivyo hivyo mpaka itakapofikia uharibifu wake.

Jaribu kifikiria hata ingekuwa ni wewe katika hali kama ile kuona hata malaika wa mbinguni hakuna aliyeonekana amestahili,..hakika ungevunjika moyo sana na kulia, ungeona hakuna tumaini tena, maisha hayana maana tena, …Lakini ashukuriwe Mungu wa mbingu na nchi, kwani alionekana MMOJA aliyestahili kukifungua kile kitabu na kuvunja mihuri yake naye si mwingine zaidi ya Simba wa Yuda, Bwana wa Mabwana, Mfalme wa Wafalme, YESU KRISTO Bwana wetu, sifa na utukufu vina yeye milele na milele Amina..yeye pekee ndiye aliyestahili kukitwaa kile kitabu, hivyo basi tumaini la marejesho lipo! Limeinuka tena! Haleluya!!.

Na ndio maana ilimpasa aje duniani kwanza ajaribiwe kama sisi tulivyojaribiwa, aishi kama sisi tulivyoishi, bila kutenda dhambi yoyote, afe msalabani bila shutumu lolote kisha aongezee kuwakomboa wanadamu kwa damu yake, ili siku ile asiwe peke yake bali pamoja na ndugu zake (yaani mimi na wewe) na ndipo apande mbinguni akajionyeshe mbele za Mungu kuwa amestahili yeye kukitwaa hicho kitabu na kuvunja mihuri yake..Lakini kama asingeyapitia hayo yote kuishi na kufa kwa ajili yetu, kadhalika yeye naye asingestahili hata kikutazama kile kitabu.Lakini alishinda ili sisi nasi tushinde pamoja naye, Utukufu na heshima anastahili yeye peke yake milele na milele amina.

Lakini kumbuka pia usisahau jambo hili Yesu Kristo ni Elohimu mwenyewe katika mwili,( soma 1Timetheo 3:16) na ndio maana utaona pale katikati ya kile kiti cha enzi anatoka mwanakondoo, ambaye ni Yesu Kristo, Ni Elohimu Yule Yule akijidhihirisha katika ofisi ya mwana (Ufunuo 5:6), Na ndio maana tukiendelea, kusoma tunaona viumbe vyote mbinguni na duniani vyote vinatambua kwamba amestahili yeye pekee kukifungua kile kitabu..

Ufunuo 5:8-14“8 Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za Mwana-Kondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu.

9 Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa,
10 ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.

11 Nikaona nikasikia sauti ya malaika wengi pande zote za kile kiti cha enzi, na za wale wenye uhai, na za wale wazee, na hesabu yao ilikuwa elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu,

12 wakisema kwa sauti kuu, Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka.

13 Na kila kiumbe kilichoko mbinguni na juu ya nchi na chini ya nchi ya juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake, nalivisikia, vikisema, Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-Kondoo, hata milele na milele.

14 Na wale wenye uhai wanne wakasema, Amina. Na wale wazee wakaanguka, wakasujudu.”

Kumbuka Bwana Yesu alivyokuwa duniani, hakufahamu mambo yote, na ndio maana alisema siku ile hakuna mtu aijuaye, hata mwana bali Baba, lakini alipopaa juu mbinguni, alipewa funguo zote, ikiwemo funguo za mauti na kuzimu, pamoja na mamlaka yote ya mbinguni na duniani, na ukuu, na ufalme,kuteka vipawa na URITHI wote, n.k. mambo haya yote yalikuwa ndani ya kile kitabu cha mwongozo kilichokuwa katika mkono wa Mungu mwenyezi.

Hivyo alipopaa mbinguni ndipo alipokwenda kutwaa kile KITABU, na hapa Yohana anaonyeshwa katika maono siku aliyopokea Kitabu kile, Kumbuka kitabu kile kimeandikwa NDANI na NYUMA,. Ikimaanisha kuna mambo ya nje na ya ndani,..Ya nje! Ndio hayo tutakayoyajua tukiwa hapa duniani, bali ya ndani tutayafahamu vizuri tukifika mbinguni..ndio siku hiyo tutafahamu vizuri maana ya yale maneno Bwana aliyotuambia

Yohana 14: 1 Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.

2 Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.

3 Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.

4 Nami niendako mwaijua njia.”
Makao yanayozungumziwa hapo ni miili yetu ya utukufu, urithi wetu wa milele unaokuja.

Ndani ya kile kitabu kumeandikwa urithi wote umuhusuo mwanadamu na mambo anayopaswa kuyafanya ili dunia iwe katika hali ambayo Mungu aliikusudia tangu mwanzo, kuna siri nyingi na maarifa mengi Mungu ameyasitiri ambayo sehemu ya hayo yatakuja kufunuliwa kwa Bibi-arusi wa Kristo pekee! Tukiwa hapa hapa duniani itakuwa ni karibia sana na nyakati kufungwa (karibia na unyakuo), ndio zile ngurumo saba, ambazo hazijarekodiwa mahali popote katika biblia, hizo zitampa Bibi-arusi imani ya kunyakuliwa, na sehemu iliyobaki ya ndani ya kitabu hicho tutaijua tukifika mbinguni mara baada ya kubadilishwa miili yetu,

Kumbuka mbinguni tutaenda kwa kitambo tu! Urithi wetu ni hapa DUNIANI, Mungu ndio aliotupa,.Tutaenda mbinguni kisha tutarudi, na ndio maana maandiko yanasema Kristo atarudi tena, moja ya kusudi la sisi kwenda mbinguni, si tu kufunuliwa uzuri wa kule bali pia kufunuliwa siri za urithi wetu tuliopewa na BABA na mikakati ya kuiunda tena kulingana na ule mwongozo ambao Bwana Yesu aliutwaa katika mkono wa ELOHIMU. Na baada ya hayo Kristo atashuka na watakatifu wake kutoka mbinguni, kuisafisha dunia.(urithi tulioahidiwa na baba)

Ndugu yale mambo yote ambayo tulikuwa hatuna majibu nayo, kwanini hivi?..kwanini vile?..ingekuwa hivi..ingekuwa vile..n.k…yote haya tutapata majibu yake siku ile tukifika mbinguni. Na ndio maana ukisoma Ufunuo 20:5-7, utaona kuna utawala wa MIAKA 1000 wa Bwana wetu Yesu Kristo unazungumziwa pale..Sasa hii miaka 1000 itakuwa ni miaka ya matengenezo kwa hekima ya ki-Mungu, kuirejesha dunia katika viwango vya ule urithi unaopaswa uwe, kuanzia hali iliyokuwepo pale Edeni na kuendelea..bahari itaondolewa, uovu utadhibitiwa, majangwa yatabadilishwa na kuwa kama Edeni, wanyama watarejeshwa katika hali yao ya asili, samba atakula majani kama ngo’ombe hawatadhuriana n.k dunia itajaa Amani (soma Isaya 65:17-25 na Isaya 11:1-9) Na baada ya ile miaka 1000 kuisha ya Kristo kuijenga dunia pamoja na watakatifu wake, kwa wakati huo dunia sasa itakuwa tayari kustahimili UMILELE. Wakati huo wale waovu wote watahukumiwa katika kiti cheupe cha enzi cha Mungu, pamoja na shetani na malaika zake kwa pamoja watatupwa katika lile ziwa la moto.

Huko katika UMILELE kusikokuwa na muda, ni kuishi tu, kuishi tu, kusikokuwa na mwisho, raha isiyokuwa na kifani, kila siku kutakuwa na uvumbuzi wa mambo mapya kumuhusu Mungu, itatuchukua umilele kumaliza kumjua Mungu, kila siku tutamwona Mungu ni mpya kwetu,hakutakuwa na dhambi tena wala waovu, wala machozi wala magonjwa,wala uchungu, wala shida,wala njaa wala mateso..Ni raha isiyokuwa na kifani..Na siku hiyo ndipo tutakapojua maana ya mstari huu.

Isaya 55: 8 “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana.

9 Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu”. Na Maana ya mstari huu Yeremia 29: 11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho”.

Tutampenda Mungu kwa viwango vingine, tutakapojua kuwa hakuumba kitu kinyonge wala kidhaifu bali kikamilifu ni sisi wenyewe ndio tuliojiharibu.

Ufunuo 21: 1 “Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena.

2 Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe.

3 Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.

4 Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.

5 Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli.

6 Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure.

7 YEYE ASHINDAYE ATAYARITHI HAYA, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.

8 Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”.

Tukiyajua hayo ndugu na mambo mazuri ambayo Mungu ametuandalia, hatutataka tupoteze URITHI huu ambao Mungu ametuandalia kwa mambo ya kitambo tu yapitayo,.Itakufaidia nini leo hii upate kila kitu, uwe wa kisasa kuliko watu wote, uwe wa kidunia kuliko watu wote, uwe maarufu kuliko watu wote halafu siku ile unakuwa hauna sehemu katika ule urithi wa watakatifu, Kama sasa hivi unaona uchungu kukosa utajiri tu wa kitambo itakuaje kule utakapoona unakosa URITHI NA UTAJIRI wa milele usioisha, hapo ndipo kutakuwa na majuto yasiyokuwa na mwisho, uchungu hautakuwa sana kwasababu unakwenda kuteketea katika ziwa la moto, uchungu utakuja utakapoona wenzako ndio wanaanza kuona maana ya maisha kwa kurithi yote hayo na wewe huna kitu haupo.

Bwana anasema Zaburi 147:4-5 “[Yeye] Huihesabu idadi ya nyota, Huzipa zote majina.
5 Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu, Akili zake hazina mpaka”.

Kila nyota ya mbinguni inayo jina, ikimaanisha kuwa zimepewa uhai, hazijawekwa kama urembo tu! Na kuna mabilioni ya nyota mbinguni na kumbuka kila nyota ina mfumo wake wa sayari, hivyo kuna mabilioni na mabilioni ya sayari na magimba angani ambayo hayo yote yana makusudi yake, ambayo yatapata kazi huko mbeleni (kwenye umilele), huo wote ni urithi wa watoto wa Mungu, Unaweza kuona ni jinsi gani itatuchukua umilele kummaliza Mungu na utajiri mkuu ulioko huko mbeleni.

Kwanini usitamani uwepo huko? Mpe Kristo leo maisha yako ayakomboe, ukabatizwe na umaanishe kabisa kumuishia Kristo naye ameahidi atakupa uwezo wa kushinda dhambi, na kuwa pamoja nawe siku zote.

Ubarikiwe

Katika sura ya sita tutaona hatua za awali kabisa wa kile kitabu kufunuliwa kimeshaanza, na sasa hivi tupo katika hatua ya mwisho ya kufunuliwa kwa muhuri wa saba, na siku yoyote utafunuliwa,

Tafadhali share kwa wengine ujumbe huu na Mungu atakubariki.Kwa Mwendelezo >>> Ufunuo: Mlango wa 6

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.


Mada Zinazoendana:

ACHENI MJUE YA KUWA MIMI NI MUNGU.

UNYAKUO.


Rudi Nyumbani

Print this post

UFUNUO: Mlango wa 4

Shalom! Karibu tujifunze Neno la Mungu, leo tukiendelea na ile sura ya 4, tulishakwisha kuona katika sura zilizotangulia jinsi Mungu alivyotembea katika yale makanisa 7 yaliyokuwa Asia ndogo, yaliyowakilisha makanisa 7 katika nyakati saba tofauti tofauti kuanzia wakati wa Pentekoste hadi wakati wa kurudi kwa Bwana wetu Yesu Kristo mara ya pili, na tuliona pia sisi tunaishi katika kanisa la mwisho, linalojulikana kama Laodikia, na kwamba baada ya hili hakutakuwa na kanisa lingine la nane, kadhalika pia kila kanisa lilikuwa na mjumbe wake, na kanisa hili la mwisho mjumbe wake alikuwa ni Ndugu.William Branham ndiye Mungu aliyemnyanyua kubeba ujumbe wa nuru ya wakati huu wa mwisho. Hivyo ukiwa haujapitia sura zilizotangulia ni vizuri ukazipitia kwanza , ili tuende pamoja.

Sasa katika sura hii ya nne tunasoma..“1 Baada ya hayo naliona, na tazama, mlango ukafunguka mbinguni, na sauti ile ya kwanza niliyoisikia kama sauti ya baragumu ikinena nami, ikisema, Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo”.

Hapa tunaona Mtume Yohana ambaye anamwakilisha bibi-arusi wa Kristo (Kanisa), akisikia sauti ambayo ndio ile iliyokuwa inazungumza naye hapo kwanza kutoka mbinguni, na sauti hiyo sio ya mwingine zaidi ya sauti ya Bwana wetu YESU, ikimwambia “Panda hata huku nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo “. Unaona hapo kabla Yohana hajajua lolote mlango ulimfungukia kwanza mbinguni, ikimaanisha kuwa hakuna mtu yeyote atakayeweza kupokea ufunuo wowote ule wa Roho kama mlango wa mbinguni haujamfungukia,.Kanisa/mtu ni lazima awe wa rohoni kwanza ndipo liweze kuelewa mambo ya mbinguni, vinginevyo halitaweza kuyaona yaliyo juu likitegemea mifumo au mapokeo ya kibinadamu peke yake.

Na tunasoma pia ile sauti ikamwambia “Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi KUWAKO BAADA YA HAYO”. Ikiwa na maana kuwa, yale maono aliyoonyeshwa kwanza, kama tulivyotangulia kusoma huko nyuma, Yohana alivyomwona YESU KRISTO katika ule mwonekano mwingine, mwenye uso kama jua, macho kama miale ya moto, miguu kama ya shaba n.k. alimwona akitembea katika vile vinara saba, pamoja na nyota saba katika mkono wake, n.k. haya yote yalifunga sehemu ya kwanza ya maono…Na sasa hapa anafungua sehemu ya pili ya maono mengine ambayo yatakuwa pia ni msingi wa mambo mengine tutakayokuja kuyaona huko mbeleni yahusuyo mihuri saba, kama tu vile yale maono ya kwanza yalivyokuwa msingi wa kufahamu tabia za makanisa saba. Na ndio maana hapo anasema ” Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo. “..Hivyo ni muhimu kuyazingatia haya maono pia kwasababu tusipoyaelewa hapa mwanzoni basi sehemu zinazofuata za kitabu cha Ufunuo zitakuwa ni ngumu kuelewa,..

Tuliona kila kitu Yohana alichoonyeshwa katika lile ono la kwanza linalohusu mwili, tabia na mwonekano wa Kristo (Ufunuo 1) vilikuwa na maana kubwa katika yale makanisa 7 yaliyofuata (Ufunuo 2&3), Kwamfano ile miguu ya shaba ilikuwa na sehemu yake katika ujumbe wa kanisa husika, kadhalika na yale macho kama mwali wa moto, na ule upanga utokao kinywani mwake, na vile vinara saba na zile nyota saba zilizokuwa mkononi mwake n.k. yote haya tuliona jinsi yalivyokuwa na mahusiano makubwa sana katika kuelezea nyakati saba za kanisa..Vivyo hivyo na hapa pia katika hii sehemu ya pili ya maono, ambayo Yohana aliitwa juu kuonyeshwa mambo mengine tofauti na aliyoyaona hapo kwanza..Tusome;

Ufunuo 4:2 “Na mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti;

3 na yeye aliyeketi alionekana mithili ya jiwe la yaspi na akiki, na upinde wa mvua ulikizunguka kile kiti cha enzi, ukionekana mithili ya zumaridi.

4 Na viti ishirini na vinne vilikizunguka kile kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na wanne, wameketi, wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu.

5 Na katika kile kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. Na taa saba za moto zilikiwaka mbele ya kile kiti cha enzi, ndizo Roho saba za Mungu.

6 Na mbele ya kile kiti cha enzi kulikuwa na mfano wa bahari ya kioo, kama bilauri; na katikati ya kile kiti cha enzi, na pande zote za kile kiti, walikuwako wenye uhai wanne, wamejaa macho mbele na nyuma.

7 Na huyo mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa mwanadamu; na mwenye uhai wa nne alikuwa mfano wa tai arukaye.

8 Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja.

9 Na hao wenye uhai wanne wanapompa yeye aketiye juu ya kiti cha enzi utukufu, na heshima, na shukrani, yeye aliye hai hata milele na milele,

10 ndipo hao wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi, nao humsujudia yeye aliye hai hata milele na milele, nao huzitupa taji zao mbele ya kile kiti cha enzi, wakisema,

11 Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa”.

Mstari wa pili unasema..Na mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti;

3 na yeye aliyeketi alionekana mithili ya jiwe la yaspi na akiki, na upinde wa mvua ulikizunguka kile kiti cha enzi, ukionekana mithili ya zumaridi”.

Hapa Yohana anaonyeshwa kiti cha Enzi na “MMOJA” Kumbuka sio watatu, ameketi katika Kiti hicho, na anaonekana pia mithili ya jiwe la yaspi na akiki,. Sasa kumbuka mawe haya kwa wakati wa agano la kale yalikuwa ni mawe yenye uzuri wa kipekee na ya thamani kubwa sana,yalitumiwa na makuhani katika kifuko cha kifuani (Kutoka 28:15), ni mawe 12 yaliyotumika kama Urimu na thimimu na mojawapo ya hayo mawe ndio Yaspi na akiki, Hivyo hapo mawe hayo yanafunua UZURI wa Mungu, na thamani ya Uzuri wake kwetu sisi wanadamu pia Yohana aliona kile kiti kimezungukwa na upinde wa mvua ikifunua rehema na neema za Mungu pamoja na uthabiti wa maagano yake, Kumbuka baada ya Gharika Mungu kwa rehema zake aliuweka ule upinde wa mvua kama Ishara ya kughahiri hasira yake itakapokuja kutokana na maovu ya watu.

Tukiendelea tunaona pia, Yohana alionyeshwa wazee 24 wamekizunguka kile kiti cha Enzi, wamevikwa mavazi meupe na juu ya vichwa vyao walikuwa na mataji ya dhahabu, pamoja na taa 7 mbele ya kile kiti cha enzi ambazo ndio Roho 7 za Mungu, Kadhalika pia alionyeshwa wale wenye uhai wanne wamekizungu kiti cha enzi wote kwa pamoja wakimpa Mungu utukufu

Kwahiyo Mungu alikuwa anamuonyesha Yohana, mahali kiti chake cha enzi kilipo,kwamba ni lazima kiwe kimezungukwa na wale wazee 24, pili kiwe kimezungukwa pia na wale wenye uhai wanne Na tatu kiwe na Taa saba mbele yake…Hapo kiti cha enzi cha Mungu kimekamilika..hakuonyeshwa kama kimezungukwa na miji au makasri na magorofa ya dhahabu hapana.

Sasa huyu aliyeketi katika kiti cha enzi ni nani?

Kwa maelezo yake marefu tutakuja kumuona vizuri katika sura inayofuata ya tano.

Lakini sasa tuwatazame wale wazee 24 ni akina nani?.

Kwanza ni vizuri kufahamu mbinguni hakuna wazee 24, walioketi kando kando ya Mungu hapana, kumbuka yale ni maono, na wale wazee 24 ni ROHO 24 za Mungu zinazotengeneza ufalme wake katikati ya wanadamu, na ndio maana zimechukua taswira ya mwanadamu. Sasa hizo roho 24 ziliachiwa ulimwenguni kulitengeneza taifa la Mungu katikati ya wanadamu,.Na tunafahamu kuwa ufalme wa Mungu (KANISA) umeundwa na mataifa mawili,nayo ni Wayahudi na Wakristo.

Hivyo mwanzo kabisa Bwana alipoanza kuunda ufalme wake alianza na taifa la mwilini (yaani Israeli), na tunajua taifa la Israeli limegawanyika katika makabila 12, Mungu aliruhusu hivyo makusudi ili kulitengeneza taifa lake. Hivyo Bwana aliachia hizi roho 12 za kwanza kukaa juu ya kila kabisa ili kulijenga taifa la Israeli ambalo ni sehemu moja ya ufalme wake. Ndipo hizi roho zikaanzia kwa wana 12 wa Yakobo na kuendelea.

Lakini baadaye Mungu alipokusudia kuunda sehemu ya pili ya ufalme wake, ndipo akawajia watu wa mataifa (sisi), hivyo kama tu alivyoanza na misingi 12 katika taifa la Israeli kadhalika na huku pia alianza na misingi 12, kujenga sehemu ya pili ya ufalme wake, hivyo akaachia Roho nyingine 12 zilizokuja kukaa juu ya wale mitume 12 wa Bwana Yesu. 

Wefeso 2: 20 ” Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni”.

Ile injili tuliyoipokea sisi kwa mikono ya mitume wa Bwana ndio imekuwa chachu mpaka leo hii ukristo umeenea duniani kote, Hizo ndio zile Roho 12 nyingine zilizoifanya hiyo kazi, kwahiyo kwa ujumla watakatifu wote wa agano la kale na wa agano jipya ndio wanaokizunguka kiti cha enzi cha Mungu katika roho, ndio wale wazee 24…Na ndio maana utaona wamevikwa mavazi meupe kuashiria usafi na weupe wa watakatifu na mataji kuashiria mamlaka ya kifalme kwa ushindi waupatao kutoka kwa yule adui.

Kadhalika na wale wenye uhai wanne, ni Roho nne za Mungu zinazowakilishwa na tabia za wale wanyama wanne. Utaona pia walikuwa wamejaa macho mbele na nyuma, ikiashiria kuwa wapo kwa kazi ya ulinzi, wanaona vitu vitakavyokuja kabla hata havijawasili, wanaona mambo yaliyopita na yanayokuja.

Kwamfano mwenye uhai wa kwanza alionekana akiwa na mfano wa simba, inamaanisha kuwa ni Roho ya Mungu iliyokuwa ikililinda (Kanisa la Mungu), kwa wakati husikia ikijifunua kama tabia ya Simba. Tunajua simba siku zote sio mwoga, ni jasiri, hivyo tutakuja kuona huko mbeleni ni wakati gani hii Roho ilijidhihirisha hivyo katikati ya watu wa Mungu.Kadhalika na yule mwenye uso kama wa ndama, na yule mwenye uso mfano wa Tai arukaye n.k. wote hawa wanabeba tabia fulani inayoendana na maumbile yao..hizi roho zimechukua mfano wa malaika zina mabawa na kupaa tofauti na wale wazee 24, zenyewe zilikuja kwa mfano wa wanadamu,..

Kadhalika tunaona pia Taa saba za moto mbele ya kile kiti cha enzi. Hizo ni roho saba za Mungu, ambazo tulishakwisha kuziona zenyewe kwenye sura zilizotangulia zikitembea katika yale makanisa saba ya Mungu.

Kwahiyo kwa ujumla katikati ya vitu hivyo vyote ndipo kiti cha enzi cha Mungu kilipo, yaani ndani ya kanisa lake (Israeli na Mataifa), linaloongozwa na hizo Roho saba, na Roho za wenye uhai wanne, Hivyo ni muhimu kufahamu ni roho gani inayoliongoza kanisa ulilopo sasa, kadhalika na ni Roho ya mwenye uhai yupi aliye juu yako na juu ya wakati wa kanisa ulilopo vinginevyo hutaweza kukiona kiti cha enzi cha Mungu au kumshinda shetani kwa namna yoyote ile katika wakati huu unaoishi.

Kumbuka shetani naye anacho kiti chake cha enzi, na chenyewe pia kimezungukwa na roho chafu nne, ndio wale wapanda farasi wanne ambao tutakuja kuwaona katika sura ya 6, na anazo roho nyingine chafu saba, ndizo zilizokuwa zinatembea pia katika makanisa saba ya Mungu kulichafua kanisa la Mungu na kupoteza watu Ndio zile Bwana Yesu alizozizungumzia katika..

Mathayo 12: 43 ” Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika, asipate.

44 Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa.

45 Mara huenda, akachukua pamoja naye PEPO WENGINE SABA walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa KIZAZI HIKI kilicho kibaya. “

Unaona hapo katika ile siku ya Pentekoste Bwana alilijenga tena kanisa kwa kulitakasa kwa Roho wake, kwa wakati ule Kanisa lilikuwa kamilifu lakini mitume wa kweli walipoondoka,mitume wa uongo wakanyanyuka kuunda misingi ya kanisa lingine la uongo na kuanza kuchanganya kweli ya Mungu na mafundisho ya kibinadamu, hivyo ikapelekea ile roho (pepo) ambalo Bwana Yesu alilitoa pale Kalvari kurudi tena katika kanisa la Mungu kwa taswira mbaya zaidi, lilirudi katika mwishoni wa kanisa la kwanza, kadhalika na katika kanisa la pili likaongezeka lingine la pili, na katika kanisa la tatu, na la nne, mpaka kanisa la saba, mapepo yote saba maovu yakalivaa kanisa, na ndio maana hali ya kanisa hili la Laodikia ni mbaya kuliko makanisa yote yaliyotangulia…Lakini siku zote mbegu halisi haiwezi changanyikana na ya uharibifu Bwana alishalianza kuwatenga watu wake na kanisa hilo la uharibifu tangu zamani.

Hivyo ni muhimu kufahamu pia kiti cha enzi cha shetani kilipo, kwasababu yeye naye anachokiti chake cha enzi Soma Ufunuo 2: 13 ” Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; ….” Unaona hapo?

Ikiwa na maana kuwa hata yeye naye analo kanisa lake aliloliunda ndipo aketipo yeye. Na kanisa hilo ni Kanisa Katoliki. Hilo ndilo linaloongozwa na (mapepo) yale saba maovu, na wale wapanda farasi wanne, ambao kwa ujumla roho hizi zilishughulika sana kupambana na uzao wa Mungu na kuuharibu kama tutakavyokuja kuona katika sura ya sita.

Kama vile Mungu alivyotwaa mwili na kuishi katikati yetu na kufanyika mfalme wa kanisa la Mungu, kadhalika shetani naye amemtia mtu mafuta akae badala yake katika kiti chake cha enzi, na si mwingine zaidi ya mpinga-kristo (PAPA atakayekuja) aliye kichwa cha kanisa hilo la uongo.

Hivyo ndugu jiulize je! umeketi katika kiti cha enzi cha Mungu au cha shetani??..Kama unadai umeketi katika kiti cha enzi cha Mungu, na bado haupo katika misingi ya mafundisho ya mitume 12(BIBLIA), na haufahamu kanisa unaloishi!, na hauifahamu Roho inayoliongoza kanisa lako? basi ni dhahiri kabisa kwamba unaketi katika kiti cha enzi cha shetani pasipo hata wewe kujijua, kwasababu ile roho ya uhai yenye macho mbele na nyuma ambayo ingepaswa ikuongoze haipo juu yako ambayo ingekupa wewe uhai na macho ya kuweza kuona mambo ya mbele na ya nyuma na kukuwezesha wewe kuzijua fumbo za shetani imeondoka. Na pia kumbuka viti vyote vya enzi (cha MUNGU na cha shetani) vinaundwa hapa hapa duniani..Hivyo jitathimini maisha yako. je! umeoshwa kwa damu ya YESU KRISTO na kujazwa Roho Mtakatifu? Huyo tu ndiye atakayekuongoza katika kweli yote na sio dini au dhehebu. Mkumbuke muumba wako siku za ujana wako kabla haijakaribia miaka utakayosema sina furaha katika hiyo (Mhubiri 12).

Ubarikiwe. Kwa Mwendelezo >>> Ufunuo: Mlango wa 5

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.


Mada Zinazoendana..

SEHEMU ISIYO NA MAJI.

MKUU WA GIZA.


Rudi Nyumbani

Print this post

UFUNUO: Mlango wa 3 part 3

Sehemu ya tatu:

Jina kuu la Bwana wetu YESU KRISTO litukuzwe. Karibu katika mwendelezo wa uchambuzi wa kitabu cha Ufunuo, Leo tukimalizia sehemu ya mwisho ya sura hii ya tatu. Ambapo tutaona kanisa lile la LAODIKIA. Tulishatazama makanisa mengine 6 yaliyotangulia pamoja na wajumbe wao, na jumbe walizopewa kutoka kwa Bwana.Kama haujayapitia unaweza ukayapitia kwanza ili tuende pamoja katika kanisa hili la mwisho, Tunasoma…

Ufunuo 3: 14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu”.

Kama tulivyotangulia kujifunza tunaona ule utambulisho wa kwanza Bwana anaoutoa kwa kanisa, huwa una uhusiano mkubwa sana na ujumbe wenyewe wa kanisa husika. Hapa Bwana anasema ” yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu “. Na hasemi “yeye aliye na ule ufunguo wa Daudi, au yeye mwenye uso ung’aao kama jua. au yeye aliyekuwa amekufa kisha akawa hai” kama alivyokuwa anasema katika makanisa yaliyotangulia, hapana bali anasema “anenaye yeye aliye Amina, SHAHIDI MWAMINIFU na wa Kweli”. Ikiashiria kuwa katika kanisa hili anatazamia kuona UAMINIFU, kama aliokuwa nao yeye tangu mwanzo wa kuumba kwa Mungu.

Kwa ufupi kanisa hili la Laodikia lilianza kati ya kipindi cha mwaka 1906 WK na litaisha na siku ya ujio wa Bwana mara ya pili (yaani Unyakuo). Na mjumbe wa kanisa hili ni WILLIAM BRANHAM. Na tafsiri ya neno LAODIKIA ni “HAKI ZA WATU”. Katika Asia ndogo ambapo haya makanisa 7 yalikuwepo, Mji wa Laodikia ndio uliokuwa umeendelea kuliko miji mingine, kama efeso, smirna, pergamo n.k. Ni mji uliokuwa tajiri kuliko yote, ulikuwa upo juu kibiashara na kiuchumi na kiusomi, hivyo ikapelekea na watakatifu waliokuwa katika mji huo kuwa na hadhi ya kitofauti na watakatifu waliokuwa katika miji mingine. Na ndio maana hatushangai kwanini Bwana Yesu kutoa ujumbe ufuatao;

“15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi”.

Unaona hapo? kutokana na mafanikio makubwa yaliyokuwepo katika ya hao watu, Ikawafanya watakatifu waridhike na kupoa sana kiroho pasipo hata wao kujitambua. Watu wa mji ule (wasiomjua Mungu) wakaanza kuweka mambo kwenye mizani, kila kitu nusu kwa nusu, kama tafsiri ya jina lake lilivyo “HAKI ZA WATU” Mambo kama haki sawa, yakazaliwa wanaume kwa wanawake,

Sasa hii roho ya haki sawa nayo ikapenyeza mpaka kwenye kanisa la Mungu.. Kwamba kwa Mungu kuna haki sawa, nusu kwa nusu, Mungu kidogo na Ulimwengu kidogo, Unasali kidogo unafanya anasa kidogo, unakuwa mtakatifu leo kesho unaendelea na mambo mengine, unatenda mema leo, baadaye unakula rushwa, leo unakuwa wa rohoni kesho wa mwilini, hivyo hivyo leo moto kesho baridi (Yaani vuguvugu). Na kibaya kibaya zaidi kutokana na utajiri wake wa nje waliokuwa nao kanisa hili lilikuwa Laodikia, shetani akalipiga UPOFU mkubwa juu yake, likawa halijitambui tena kama linakwenda mbali na ukweli. Jaribu kutengeneza picha upo uchi, na hujitambui kama upo hivyo..Hiyo ni hatari kubwa sana.

Kwa kuwa Bwana anaona mbele alilifanya kanisa hilo kuwa unabii wa watu wa nyakati fulani itakayokuja miaka mingi huko mbele nao sio wengine zaidi ya sisi watu wa kizazi hichi tunachoishi leo ambacho kilianza tangu kipindi cha miaka ya 1906, Hivyo ndugu ni muhimu sana kufahamu kuwa tunaishi katika kanisa linalofanana na lile la Laodikia.

Kama vile mji ule ulivyokuwa tajiri kuliko miji mingine yote sita, kadhalika na dunia ya sasa tunayoishi ndio dunia iliyoendelea na iliyotajirika kuliko nyakati nyingine zote zilitangulia, kiuchumi, kiteknolojia na kielimu n.k.. Kiasi kwamba dunia leo hii ni kama kijiji, utandawazi umefikia viwango vya juu sana. Sayansi imefika hatua ya kwamba mwanadamu anaweza akaenda mwezini, mambo mengi sana yamevumbuliwa kuanzia karne ya 20, yaani kuanzia mwaka 1901 na kuendelea uvumbuzi wa mambo mengi ulitokea tukianza kueleza moja moja hatutamaliza. Mambo ambayo hayakuonekana katika karne zote zilizotangulia. Hii ni kuonyesha kwamba dunia ya sasa tunayoishi inafanana kabisa na mji ule wa LAODIKIA.

Kadhalika “haki za binadamu”, agenda za haki sawa kati ya wanawake na wanaume zilizuka katika karne hii hii ya 20, kwamba chochote mwanaume anachoweza kufanya hata mwanamke anaweza akafanya, hata mavazi mwanaume anayovaa hata mwanamke pia anaweza akayavaa, haki za watu kuoa mtu anayemtaka aidha mwanaume kwa mwanaume, au mwanamke kwa mwanamke haina shida n.k. mambo ambayo hayakuonekana katika karne zote za nyuma zilizotangulia.

Hivyo hiyo roho iliyokaa katika ulimwengu ikajiambukiza tena katika kanisa la KRISTO kama ilivyokuwa kwa wakati wa Laodikia. Kwa kuwa tunaishi katika kipindi cha mafanikio makubwa ya kielimu, kiuchumi na kiteknolojia, watakatifu wa wakati huu wakaanza kuendana pia na watu wa ulimwengu huu, na wao pia wakaanza kuiga mambo ya ulimwengu na kuyaleta katika kanisa la Mungu.

Kutokana na kwamba kuwa na utajiri wa vitu vingine vya nje, kama makanisa makubwa, vitendea kazi vya kisasa vya ibada kama vyombo vya muziki, vipaza sauti vikubwa vya kuwafikia watu wengi mambo ambayo hayakuwepo katika makanisa ya nyuma, vitu kama televisheni, radio na internet vimekuwa nyenzo rahisi za kuwafikia watu, kadhalika vyombo vya kisasa vya usafiri kama ndege, magari n.k. tofuati na hapo zamani watakatifu walikuwa wakitumia miguu, na punda kwenda kuhubiri injili, Ikawasababishia shabaha yao ihame kutoka katika mambo ya rohoni zaidi na kuhamia kwenye mambo ya mwilini. n.k. watakatifu wakaanza kujiona kwa vitu walivyonavyo Mungu anapendezwa nao,

Hivyo nguvu ile ile inayoiendesha dunia, ndio hiyo hiyo inayoiendesha kanisa, mambo yale yaliyotukuka katika dunia ndiyo yanayotukuka ndani ya kanisa la leo, Badala utakatifu utukuzwe ndani ya kanisa, inatukuzwa elimu, kwamba kipimo cha kuwa mchungaji au umekubaliwa na Mungu ni kiwango cha elimu na sio utakatifu, kadhalika utajiri wa Fedha imetukuzwa zaidi kuliko utajiri wa Rohoni, kiasi kwamba kipimo cha mtu kubarikiwa na Mungu sio kukua kiroho hapana bali kuwa na fedha nyingi..Injili inayoweza kumfaa mtu kwasasa ni injili ya mafanikio na sio injili ya toba.

Kadhalika vyeo vilivyotukuka duniani vinavyotumika kuongozea ustaarabu wa kidunia vimepewa heshima kubwa zaidi kanisani kuliko vyeo Mungu alivyovikusudia viwepo kwa uongozo wa kanisa. Kiasi kwamba ili uonekane umekubaliwa na Mungu ni lazima Uwe Raisi wa dhehebu fulani, M/kiti, Katibu/ Papa/ Mkurugenzi, Dokta, Profesa n.k. na sio Karama fulani ya rohoni kama unjilisti, uchungaji, ualimu, mitume na manabii, au karama nyingine za Roho kama miujiza,lugha, unabii uponyaji n.k. zimewekwa nyuma na hazina nafasi yoyote katika kanisa la sasa.

Dunia tunayoishi leo hii ni ya “HAKI ZA KIBINADAMU”, kadhalika na kanisa nalo limechukua hizo tabia, kwamba hata mavazi anayovaa mwanaume hata mwanamke wa kikristo anaweza kuyavaa, kwamba karama za uongozi ambazo Mungu aliziweka kwa wanaume tu, kulingana na (1Timotheo 2:12) kama vile uchungaji, ualimu na utume, hata mwanamke anaweza akazifanya; Imefikia hatua kwamba ndoa za jinsia moja zinazofungishwa na watu wa ulimwengu zinafungishwa pia Kanisani..Na bado watu hao wanajiita wakristo na kibaya zaidi shetani amewapiga upofu hawajijui kwamba wapo uchi, vipofu, maskini, na wanyonge….Ni uvuguvugu wa hali ya juu sana. Kristo ametupwa nje.

Kumbuka katika kila nyakati kulikuwa na mjumbe wa kanisa hilo ambalo Mungu alimnyanyua kutoa nuru ya wakati huo, Tuliona katika kanisa la Tano Bwana alimnyanyua Martin Luther na wengine kama wakina Calvin na Zingwli, kadhalika katika nyakati ya sita Bwana alimnyanyua John Wesley na wenzake. Vivyo hivyo na katika hili kanisa la mwisho Bwana alimnyanyua mjumbe wake WILLIAM BRANHAM na ujumbe wa kuwarudisha watu katika NENO na watoke katika hali ya uvuguvugu iliyopo sasa katikati ya madhehebu na kutoka katika mifumo ya yule mwanamke kahaba (Kanisa Katoliki) na pia Bwana alimpa ujumbe wa kutangaza kuja kwa pili kwa Kristo.

William Branham ni nani?.

William Branham alizaliwa huko Kentucky, Marekani mwaka 1909alizaliwa katika familia ya kimaskini sana, baba yake alikuwa ni mtengenezaji wa pombe, hivyo aliishi katika mazingira ya kushawishika na ulevi, alipofikisha umri wa miaka 7 anasema siku moja wakati anatoka kuteka maji kisimani alisikia sauti juu ya mti ikimwambia, “Usikae unywe pombe, wala kuvuta sigara,kwani kuna kazi ya yeye kufanya utakapokuwa mtu mzima”, aliogopa sana lakini maneno hayo aliyaweka moyoni, kwani aliogopa kuwaeleza watu maono aliyokuwa anayaona kwasababu wengi miongoni mwa wachungaji walikuwa wakimwambia hayo ni maono kutoka kwa shetani, lakini ilifika kipindi akampa Kristo maisha yake, na kukata shauri kumtumikia Mungu, ndipo Bwana akaanza kumtumia kwa namna ya kipekee, Siku moja wakati anabatiza umati mkubwa wa watu katika mto mmoja huko Marekani unaitwa Ohio, alipokuwa anambatiza mtu kama wa 17, nyota kubwa ilishuka juu yake akiwa pale mtoni, watu wote wakaishuhudia na ndipo akasikia sauti ikimwambia “Kama vile Yohana mbatizaji alivyotumwa kutangaza kuja kwa kwanza kwa Kristo, vivyo hivyo ujumbe wako utatangaza kuja kwa pili kwa Kristo”. Habari ya tukio hilo ilisambaa sana na kuchapishwa katika magezeti na vyombo vya habari vya Marekani.

Na alipofikisha umri wa miaka 37, siku moja alipokuwa anasali usiku malaika wa Bwana alimjia na miongoni mwa maneno aliyoambiwa ni; “Kama akiwa mwaminifu atakapoomba hakuna kitachoweza kusimama mbele yake hata kansa, aliambiwa pia atawaombea wafalme na ujumbe wake utafika duniani kote,” . Hivyo kuanzia huo wakati Ishara na miujiza ya kupita kawaida viliambatana naye, mambo ambayo hapo nyuma yalikuwa hayaonekani, karama za upambanuzi wa roho ziliambata naye siku zote za huduma yake, siku moja wakati anahubiri Mungu kutaka kuithibitisha huduma yake NGUZO YA MOTO ambayo ilikuwa ikimfuata tangu kuzaliwa kwake, ilitokea hadharani na kukaa juu yake, mamia ya watu waliokuwa pale waliiona, na ikapigwa picha, hiyo ilikuwa ni mwaka 1950, Picha hiyo upesi ilipelekwa kwa George J. Lacy, Mchunguzi Mweledi wa Hati Zinazoshukiwa wa F.B.I. ya Marekani, ambaye aliihakiki picha hiyo kwa maoni yake ya kitaalamu. Hati rasmi iliyotolewa na Bw. Lacy kuhakiki kuwa ile ilikuwa ni picha ya kwanza ya kimiujiza iliyothibitishwa kisayansi. Hii ilikuwa ni mapema zaidi kabla ya kompyuta na kamera za tarakimu, wala haingeweza kuelezewa kwa njia zozote zinazojulikana na sayansi, mbali na kwamba kulikuwa na Nuru halisi juu ya kichwa cha William Branham. Leo hii picha hiyo hiyo inaweza kuonekana kwenye Maktaba ya Bunge la Marekani, katika makao makuu ya taifa, Washington DC. (Tazama picha chini).

Kwahiyo historia ya maisha na huduma ya William Branham ni ndefu kidogo hatuwezi kuielezea yote hapa ila kama utahitaji utaipata mwisho wa ukurasa huu.

Hivyo ishara zote na miujiza Mungu aliyomjalia William Branham viliambata na ujumbe, Na ujumbe wenyewe ulikuwa ni Kuwarudisha watu kwenye misingi ya Neno la Mungu, Kuwarejesha watu katika Imani ya kanisa la mwanzo, na kwamba watu wa Mungu watoke katika mifumo ya dini na madhehebu ambayo Mungu ameikataa, na kujiandaa kwa kuja kwa pili kwa Kristo, Kadhalika Bwana aliwanyanyua na wengine kama ORAL ROBERT, TL OSBORN, na BILL GRANHAM na wengine baadhi. Wote hawa ni ili kuangaza nuru ya Mungu katika kanisa la mwisho tunaloishi sasa. Hivyo uamsho wa Roho ulikuwa ni mkubwa sana katikati ya karne ya ishirini, tofuati na tunavyoona sasa hivi, kuzuka kwa wimbi kubwa la manabii wa uongo na waalimu wa uongo, na miujiza bandia kama tunavyoona sasa.

Sasa turudi katika kanisa hili la LAODIKIA Bwana anasema;

“15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi”.

Unaona hapo, kanisa tunaloishi ni vuguvugu, kwa wingi wa vitu tulivyonavyo tumejikinai, Na Bwana anasema atatupika kama tusipotubu.. Bwana anasema..

“18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.

19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.

20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami”.

Ujumbe huo unajieleza wenyewe kwamba ni wakati wa kurudi na kufahamu ujumbe wako wa saa wa nyakati unayoishi.. unaweza ukajiona ni moto kumbe ni baridi kwasababu umeshindwa kufahamu ni nyakati gani unaishi. na ujumbe wa wakati huu ni kurudi kwenye misingi ya NENO LA MUNGU ambayo tumeiacha ili tuwe moto na sio vuguvugu, tuache kuchanganya neno la Mungu mapokeo ya kidini, tuache kuchanganya Neno la Mungu na mambo ya ulimwengu huu kama kanisa la Laodikia lilivyokuwa (Kwani ni sawa na kufanya uasherati wa kiroho)..Leo hii unafanya ibada, kesho upo disco, jumapili unavaa vizuri, jumatatu unavaa vimini, leo unakuwa mwaminifu kesho unakula rushwa, leo unazungumza ukweli kesho unadanganya na kutukana, n.k.huko ndio kuwa vuguvugu, au KUTOKUWA MWAMINIFU na Kristo katika kanisa hili anataka kuona UAMINIFU kama yeye alivyojitambulisha hapo mwanzo kuwa YEYE NI MWAMINIFU TANGU MWANZO.

Na Bwana anamalizia kwa kusema..

“21 Yeye ashindaye, nitampa KUKETI PAMOJA NAMI KATIKA KITI CHANGU CHA ENZI, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.

22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”.

Unaona hapo? Kanisa hili ndilo lililopewa thawabu kubwa kuliko makanisa yote yaliyotangulia, kwamba kwa yeye atakayeshinda kwa kuwa mwaminifu kama yeye alivyokuwa atapewa nafasi ya kuketi pamoja naye katika kiti chake cha Enzi” Je! hupendi thawabu kama hiyo?..Wote tunaipenda hivyo tukizijua thawabu hizi njema Mungu alizotuandalia huko, tutaishi maisha ya kujilinda sana asije mwovu akalitwaa taji letu katika nyakati hizi za hatari.. Kumbuka pia hakutakuwa na kanisa linguine zaidi ya hili. Hatua iliyobaki ni unyakuo tu.

Ubarikiwe sana.

Huu ndio mwisho wa ujumbe Bwana alioutoa kwa yale makanisa saba. Kwa neema za Mungu tutazidi kuzitazama sura zinazoendelea. Kwa Mwendelezo >>>Ufunuo: Mlango wa 4

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.


Mada Zinazoendana:

Print this post

UFUNUO: Mlango wa 3 part 2

Sehemu ya pili:

Bwana wetu YESU KRISTO atukuzwe. Karibu katika kujifunza kitabu cha Ufunuo, leo tukiendelea na ile sehemu ya pili ya sura hii ambapo tutajifunza juu ya kanisa la sita linalojulikana kama FILADELFIA. Tulishayatazama makanisa matano ya kwanza na tukaona kila moja ujumbe wake, thawabu zake pamoja na wajumbe au Malaika zake. Hivyo kama bado hujazipita ni vema ukazianza hizo kwanza kisha tuendelee kwa pamoja na kanisa hili la sita.

Tunasoma…

Ufunuo 3: 7 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye”.

Kama tulivyokuwa tunajifunza katika sura zilizopita kuwa ule utambulisho wa kwanza wa Bwana kabla hajatoa ujumbe unakuwa na mahusiano makubwa sana na ujumbe wenyewe wa kanisa husika..Kwamfano hapa anaanza kwa kusema ” Haya ndiyo anenayo yeye aliye MTAKATIFU, aliye wa kweli, aliye na UFUNGUO WA DAUDI, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye”.

Unaona hapo anasema yeye “aliye mtakatifu” hajasema “yeye aliye na hizo Roho saba” kama alivyofanya katika kanisa lililopita la Sardi, au “yeye aliye na huo upanga mkali utokao kinywani mwake kama alivyosema katika kanisa la tatu” hapana! Bali hapa anasema “yeye aliye mtakatifu na mwenye UFUNGUO wa Daudi”. Ikiashiria kuwa “Anategemea kuona UTAKATIFU kama yeye alivyo katika hilo kanisa”..Kadhalika na ufunguo pia alionao inaamaanisha “Anakwenda kufungua au kufunga kitu fulani katika hilo kanisa”. Hivyo tutakuja kuona hizo funguo za Daudi alizonazo ni zipi?..

Kwa ufupi kanisa hili la FILADELFIA lilianza mwaka 1750WK na kuisha mwaka 1906WK. Lilidumu kwa kipindi cha miaka 156, na Mjumbe/Malaika wa kanisa hili aliitwa JOHN WESLEY. Na tafsiri ya neno Filadelfia ni “UPENDO WA NDUGU”..Hivyo hili ni kanisa lililoonyesha utofauti mkubwa na makanisa mengine yote. Baada ya ule uamsho wa Luther wa kuwahubiria watu watoke katika ule mfumo wa yule mwanamke Yezebeli (Kanisa Katoliki). Bwana alimnyanyua tena Mjumbe wake mwingine mwaminifu, John Wesley na nuru ya ziada kwamba pamoja na “kuhesabiwa haki kwa imani kwa Mungu”, mtu anapaswa aongezee juu yake “UTAKATIFU

1Petro 1: 15 “bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;

16 kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. “

Na tena inasema… Waebrania 12: 14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo UTAKATIFU, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao”

Mambo ambayo Kanisa la Sardi halikuonekana wala mjumbe wa kanisa lile Martin Luther hakulifundisha sana, yeye alitilia mkazo sana kuhusu kuhesabiwa haki kwa imani”. Hivyo mjumbe wa hili kanisa la FILADELFIA John Wesley alianza kuhubiri UTAKATIFU kwa nguvu, na kwamba usafi katikati ya maisha ya waumini ni jambo la muhimu sana.

Wesley alizaliwa huko Epworth, nchini Uingereza mwaka 1703 na alipokuwa chuoni Oxford ndipo Bwana alipoanza kubadilisha maisha yake, yeye na kaka yake aliyeitwa Charles waliunda kikundi pamoja na wengine kinachosimamia itikadi ya “Kuishi maisha kama ya Kristo aliyoishi”, kuliko maisha ya kidini, walianza kwenda kuwatembelea wagonjwa mahospitalini, na wafungwa, na kuwahurumia maskini, n.k na kujifanya wao wenyewe kuwa vielelezo(njia ya kufuata) hivyo wakajiundia uongozi wa kiroho wakauita “(METHOD yaani NJIA”)..na kuanzia huo wakati wakaitwa WAMETHODISTI. Baada ya hapo Wesley na wenzake Bwana aliwagusa kwa namna ya kipekee, wakaona umuhimu wa kwenda kufanya kazi ya umishionari duniani kote. Hapo ndipo injili ikaanza kupelekwa duniani kote kwa nguvu, kasi na kwa bidii hata zile sehemu ambazo zilikuwa ngumu kufikiwa kama Afrika zikafikiwa na nuru ya neno la Mungu, ndio wakati wamishionari wengi wakaanza kufika sehemu za Afrika,Asia na Marekani ya kusini.

Wesley alikuwa ni mtu aliyeimarika kiroho sana, anasema hakumbuki kama alishawahi kupunngua nguvu rohoni hata kwa robo saa tangu siku aliyozaliwa. Alisema hakuwahi kulala zaidi ya masaa 6 siku zote za huduma yake, kila siku alikuwa akiamka saa 11 alfajiri, na kwenda kuhubiri zaidi ya mara nne kwa siku, ili kwamba kwa mwaka afikishe kwa wastani wa mafundisho 800. Alikuwa akisafiri maelfu ya maili kwa farasi kwenda kuhubiri. Kwa mwaka inakadiriwa alikuwa anasafiri zaidi ya maili 4,500 kwenda kuhubiri.

Tukiendelea na mistari inayofuata…

Ufunuo 3:8 “Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu”.

Bwana anasema amewapa mlango uliofunguliwa mbele yao.? Sasa huu mlango ni upi?.

Kumbuka hapo awali BWANA alijitaja kama “yeye aliye na ufunguo wa Daudi“. Na ni kwanini aseme funguo za Daudi na asiseme funguo za Musa, au Ibrahimu?. Ni kwa nini Daudi?. Hii inatupa picha halisi kuwa upo ufunguo ambao alikuwa nao Daudi na Bwana naye akawa nao. Hivyo ni vizuri tukaufahamu huu ufunguo kwanza ni nini ili tupate msingi mzuri wa huko tunapoelekea?..

Kumbuka Baada wa Wana wa Israeli kutoka Misri na kuingia katika nchi yao ya ahadi, watu wote baada ya kuiona ile nchi ni nzuri walitawanyika na kila mtu kwenda kukaa sehemu yake, walijenga na kupanda na kufanikiwa wakamsahau Mungu, Wao walifanikiwa lakini Mungu katikati hao hakuwa na nafasi yoyote, wao walikaa kwenye makasri lakini Mungu alikaa kwenye mahema ya giza. Na iliendelea hivyo kwa kipindi kirefu cha zaidi ya mamia ya miaka, na hakukuwa na mtu yeyote kutia moyo wake ufahamu kuona kwamba kwanini sanduku la Mungu linakaa kwenye mahewa yenye giza leo huku kesho kule, Mungu mkamilifu anayetujali hapaswi kukosa sehemu ya kukaa, Ndipo Daudi siku moja akatia moyo wake ufahamu na kusema nimtengenezee Mungu wangu mahali pa kukaa, haiwezekani yeye akae kwenye jumba la kifahari wakati, Bwana Mungu wake hajamjengea nyumba, ndipo Daudi kwa bidii akaiteka ngome ya Sayuni (YERUSALEMU), Kisha akakusudia kuanzia huo wakati amjenge Mungu wake nyumba ( yaani HEKALU). Na ndipo Mungu akamwambia Daudi.

2 Samweli 7: 2 “Mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia.

3 Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana Bwana yu pamoja nawe.

4 Ikawa usiku uo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema,

5 Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, Bwana asema hivi, JE! WEWE UTANIJENGEA NYUMBA, NIKAE NDANI?

6 Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani.

7 Mahali mwote nilimo kwenda na wana wa Israeli wote, JE! NIMESEMA NENO LOLOTE NA MTU YO YOTE WA WAAMUZI WA ISRAELI, NILIYEMWAGIZA KUWALISHA WATU WANGU ISRAELI, NIKISEMA, MBONA HAMKUNIJENGEA NYUMBA YA MIEREZI?

8 Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, Bwana wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli;

9 nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani.

10 Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza;”

Unaona hapo sababu kubwa iliyomfanya hata Bwana Yesu kuitwa mwana wa Daudi, ni tabia aliyoionyesha Daudi ya kumuundia Mungu wake mji wa kukaa pamoja na Hekalu la kuweka Jina lake, katika ya makuhani, kati ya wafalme, kati ya waamuzi, kati ya manabii, ni Daudi pekee ndiye aliyeliona jambo hilo?. Na Mungu alikaa kimya makusudi aone ni nani atakayekuwa na akili ya kufanya hivyo. Na akaonekana Daudi peke yake. Na huo ndio UFUNGUO Daudi aliokuwa nao KUFUNGUA ukimya wa Mungu.

Kadhalika na Bwana wetu Yesu Kristo aliposema “yeye mwenye Ufunguo wa Daudi” alimaanisha na yeye pia anaunda Yerusalemu yake na Hekalu kwa Mungu wake. Isipokuwa yeye YERUSALEMU yake ni ya rohoni sio ya mwilini,na hekalu kwa Mungu wake ni la rohoni sio la mwilini. Daudi hasaa asingeweza kabisa kumwandalia Mungu mji utakayomfanya ashuke yeye mwenyewe na kukaa katikati ya watu lakini Bwana Yesu anaandaa mji utakaoleta makao ya Mungu katikati ya watu..na huu “MJI” anaoundaa ni watakatifu wake. Tukisoma…

1 Wakorintho 3: 16 ” Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?

17 Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, AMBALO NDILO NINYI “.

Tutakuja kuona vizuri juu ya mji mtakatifu wa Mungu (Yerusalemu mpya) ni nini, tutakapofika katika Ufunuo sura ya 21.

Hivyo alipoliambia hili kanisa la Filadelfia “Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako”, Alimaanisha kuwa ni mlango wa kuujenga mji wake pamoja naye. Hivyo wale watu walipoanza kwenda huku na huko kufanya umishionari wa kuwaleta watu wengi (Ikiwemo) wapagani kwa Kristo, ndio ulikuwa mlango uliofunguliwa mbele yao. JOHN WESLEY na mamisionari wengine waliifanya kazi hiyo duniani kote, kipindi hicho pia ndio biblia kusambazwe duniani kote, hakuna nchi ambayo haikufikiwa na nuru ya Neno.

Tukiendelea ..

“9 Tazama, nakupa walio wa sinagogi la Shetani, wasemao kwamba ni Wayahudi, nao sio, bali wasema uongo. Tazama, nitawafanya waje kusujudu mbele ya miguu yako, na kujua ya kuwa nimekupenda.

10 Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi”.

Sinagogi la shetani halikuanzia tu kwenye hili kanisa la sita, bali lilikuwepo pia katika makanisa ya nyuma, lilitajawa pia katika kanisa la pili (Ufunuo 2:9), Hili ni kanisa la uongo ambalo walikuwepo watu waliojifanya kama kanisa la kweli la Mungu na kuiga mambo yaliyokuwa yanafanywa na watakatifu lakini ndani yao walikuwa ni mbwa-mwitu wakali, wanaliharibu kundi, ni tabia ya shetani popote palipo na nuru ya kweli ya Mungu, atanyanyuka na kupanda magugu yake katikati yao. Lakini katika hili kanisa kwa kuwa walilishika Neno la subira ya Mungu kwa uaminifu wote, Mungu akayadhoofisha hayo makundi mengine ya uongo shetani aliyoyanyanyua katikati yao na kumtukuza sana bibi-arusi wake zaidi yao.

Bwana anaendelea na kusema…

“10 Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi.

11 Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako”.

Unaona hapo Kanisa hili liliahidiwa pia kulindwa kutoka katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwenguni wote (Na hii saa ya kuharibiwa itakuwa ni kipindi cha dhiki kuu), Ikiwa na maana kuwa dhiki hii kuu ingepaswa itokee tangu wakati wa hili kanisa la Filadelfia lakini kwasababu ya Subira na uaminifu wao, Bwana akawaepusha, hivyo itatokea katika kanisa linalofuata la mwisho la Laodikia. Na kama anavyosema saa hiyo itakuwa ni ya “kuwajaribu hao wakaao juu ya nchi”, ina maana kuwa ulimwengu mzima utapitia jaribu moja zito la “aidha kupokea chapa ya mnyama uishi au kuikataa ufe” litakuwa ni jaribu kubwa sana kwa wale watakaoachwa kwenye unyakuo. Ndugu Unaona wakati tunaoishi?, ni hatari kubwa sana ipo mbele yetu kama tusipokuwa waangalifu?.

Na anazidi kusema 11 Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako”.

Hapa anasema “naja upesi” ikiwa na maana kuwa “hakawii” biblia inasema waebrania 10: 37 “Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, YEYE AJAYE ATAKUJA, WALA HATAKAWIA”.

Na pia anasema “shika sana ulicho nacho” ikiwa na maana kuwa, kile ulichokipokea ukiihifadhi, kwa kuwa “mtakatifu” na kujiepusha na “mafundisho yadanganyayo” asije “MTU”, akatwa taji yako, kumbuka ni “mtu” na sio “malaika” ikifunua kuwa mataji tunapewa hapa hapa duniani, mbinguni tukifika ni kuvikwa tu. Na tukiwa hapa duniani kuna mtu anaweza akatwaa mataji yetu, SASA huyu “MTU” atafutaye kutwaa mataji yetu (au THAWABU) zetu ni nani??

2 Wathesalonike 2: 3 ” MTU awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule “MTU WA KUASI”, mwana wa uharibifu;

4 yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.

5 Je! Hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi naliwaambieni hayo? “

Unaona hapo huyu MTU anayezungumziwa hapo ni mpakwa mafuta wa shetani (yaani MPINGA-KRISTO ndani ya cheo cha UPAPA), na mifumo yake yote,na mitume wote wa uongo wajigeuzao kuwa mitume wa Kristo, ambao kwa kipindi hichi cha siku za mwisho wamezagaa kila mahali, wasiofundisha toba na msamaha wa dhambi wala wasiofundisha ujio wa Bwana bali mungu wao ni tumbo..Mtume aliwataja katika…

Wafilipi 3: 17 Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi.

18 Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, KUWA NI ADUI ZA MSALABA WA KRISTO;

19 mwisho wao ni uharibifu, MUNGU WAO NI TUMBO, utukufu wao u katika fedheha yao, WANIAO MAMBO YA DUNIANI.

20 Kwa maana sisi, WENYEJI WETU UKO MBINGUNI; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo;

21 atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake.

Na mwisho kabisa Bwana anamalizia kwa kusema…..

” 12 Yeye ashindaye, nitamfanya kuwa NGUZO katika HEKALU LA MUNGU WANGU, wala hatatoka humo tena kabisa, nami nitaandika juu yake jina la Mungu wangu, na jina la mji wa Mungu wangu, huo Yerusalemu mpya, ushukao kutoka mbinguni kwa Mungu wangu, na jina langu mwenyewe, lile jipya.

13 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. “

Bwana aliwaahidia watu wa kanisa hili la Filadelfia, wale ambao waliokuwa watakatifu, na kujiepusha na mafundisho ya uongo na kujitoa kwa bidii yote kupeleka injili huku na kule duniani kote, na kuusimamisha mji wa Bwana Yerusalemu yake ya rohoni, na hekalu ndani yake, kama Daudi alivyoadhimia kumjengea Bwana nyumba, hata BWANA kuuchagua Yerusalemu kuwa makao yake makuu, na mji wake mtakatifu, kadhalika hawa wa Filadelfia Bwana aliwaahidia kuwafanya kama nguzo, katika ule mji uliotukuka Yerusalemu mpya ambao tutakuja kuuona habari zake katika sura ile ya 21..

Tukiyajua hayo, ni wakati wa kuzifanya taa zetu ziwe zinawaka, kwa kumuamini, Bwana Yesu Kristo, na kutubu, na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa na kwa JINA LA YESU na kupokea Roho Mtakatifu, na kuishi maisha yanayolingana na wokovu,(yaani maisha matakatifu), na zaidi ya yote kuipeleka habari njema kwa watu wote ulimwenguni kote, na kujihadhari “mtu” asije akayatwaa mataji yetu.

Ubarikiwe na Bwana Yesu, aliyetoa maisha yake kuwa dhabihu hai, kwa Mungu kwa ajili yetu.

Tafadhali “share” kwa wengine ujumbe huu na Mungu atakubariki. Kwa Mwendelezo >>> Ufunuo: Mlango wa 3 Part 3

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.


Mada Zinazoendana:

WEWE NI HEKALU LA MUNGU.

MPINGA-KRISTO


Rudi Nyumbani

Print this post

UFUNUO: Mlango wa 3 part 1

Sehemu ya kwanza.

Bwana na mwokozi wetu YESU KRISTO atukuzwe daima. Karibu katika mwendelezo wa uchambuzi wa kitabu cha Ufunuo, Leo tukiliangalia lile kanisa la TANO kati ya yale makanisa SABA, na Ujumbe aliopewa Mtume Yohana ayapelekee. Kanisa hili linaitwa SARDI. Tunasoma.

Ufunuo 3:1 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa”.

Kumbuka hapa Bwana anajitambulisha kama “yeye mwenye hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba”. Katika kanisa hili hakujitambulisha kama “yeye mwenye macho kama mwali wa moto au yeye mwenye huo upanga mkali utokao kinywani mwake n.k.” bali alijitambulisha kama yeye mwenye hizo Roho saba, akifunua asili yake ya ndani, Sasa Hizi Roho saba, sio kwamba Mungu anazo Roho 7 na kila moja inajitegemea kivyake hapana, bali ni Roho ile ile moja isipokuwa inatenda kazi katika nyakati tofauti tofauti saba. Mfano tuna siku 7 katika juma, na kila siku tunaona jua likichomoza na kuzama, sasa hatuwezi tukasema kwa wiki tuna ma-jua 7, hapana tunafahamu kuwa jua ni lile lile moja isipokuwa limetenda kazi katika siku saba tofauti, na ndivyo ilivyo kwa Roho wa Mungu. Kwanza ni vizuri kufahamu Mungu ni Roho, na ni mmoja, na Roho yake ni moja, kadhalika na nafsi yake ni moja. Kwahiyo hapo ni ile ile Roho moja ikitenda kazi katika nyakati tofauti tofauti saba za Kanisa.

Kwahiyo kwanini Bwana alijitambulisha kama yeye mwenye Roho 7, ni kwasababu “Roho ndiyo inayotia uzima”. Na ndio iliyokuwa inatia UZIMA kwa makanisa yote 7 kuanzia la kwanza mpaka la mwisho. Ikiwa na maana kuwa kanisa hilo la SMIRNA lilihusiana na kupungukiwa na Roho wa Mungu. Hivyo kama tunavyofahamu mtu akikosa Roho wa Mungu ni sawa na kakosa uzima,na Kinachobakia ni kifo. Wakati fulani Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake katika

Yohana 6: 63 “ROHO NDIYO ITIAYO UZIMA, mwili haufai kitu; MANENO HAYO NILIYOWAAMBIA NI ROHO, TENA NI UZIMA”.

Unaona hapo anasema ni Roho tena ni uzima. Hivyo kanisa hili limehusiana na kuacha maneno ya Bwana ambayo ndio Roho yenyewe itiayo uzima kwao. Na ndio maana Bwana anasema anayajua matendo yao ya kwamba “wana jina lililohai lakini WAMEKUFA”.

Tulichunguze kidogo hili kanisa la SARDI; Tafsiri ya neno SARDI ni “WALE WALIOTOROKA”..Na kanisa hili lilianza mwaka 1520WK na kuisha mwaka 1750WK, Kanisa hili halikudumu kwa muda mrefu sana kama Kanisa lililopita la Thiatira ambalo lenyewe lilidumu kwa muda wa zaidi ya miaka 900. Kipindi hichi cha kanisa hili kinajulikana maarufu kama “wakati wa matengenezo ya kanisa”, Ni wakati ambao lile giza ambalo lilikuwa limetanda duniani kutoka katika nyakati za kanisa la nne lilianza kumezwa na Nuru ya kweli ya Mungu kidogo kidogo baada ya kanisa kuharibiwa kwa muda mrefu na mafundisho ya dini ya uongo (Katoliki).

Hivyo Mungu akaanza kunyanyua watumishi wake waaminifu ambao waliyashika yale maneno ya Bwana aliyosema katika lile kanisa la Nne lililotangulia kwamba “wanamridhia yule mwanamke YEZEBELI”. Hivyo hawa baada ya kuzijua fumbo za shetani na kwamba makao yake makuu yapo katika dini ya uongo inayofanana sana na ukristo (Katoliki), hawakumridhia kama watu wa kanisa la nne walivyofanya.. Hivyo wakaanza kunyanyuka na kwenda kinyume na kuyapinga mafundisho yake kwa kuhubiri UKWELI WA NENO kwa watu wote pasipo kumwogopa. Ndipo tunakuja kuona Mungu akamnyanyua mtu kama “MARTIN LUTHER”, Ambaye yeye ndiye aliyekuwa mjumbe/Malaika wa kanisa hilo (SARDI), na wengine pia kama wakina Calvin, Zwingli, na wengineo..Wote hawa kwa pamoja hawakumridhia yule mwanamke YEZEBELI. Na kama vile tafsiri ya jina la Kanisa hili lilivyo (Sardi=wale waliotoroka), hivyo hawa wakristo wa nyakati hii walifanikiwa kutoroka kwa sehemu kutoka kwa yule mwanamke Yezebeli.

Tunaona Martin Luther ambaye mwanzoni alikuwa ni kasisi wa kikatoliki, baada ya kuona njia ya kanisa Katoliki haiendani na kweli ya Mungu, aligeuka na kuyapinga mafundisho ya kanisa hilo, siku moja katika safari yake ya kuutafuta ukweli, alisikia sauti ikimwambia..“Mwenye haki ataishi kwa Imani” (Warumi 1:17). Hivyo baada ya kupokea ufunuo huo akaanza kuyakataa mafundisho yote ya “wanikolai” ya “Balaamu” na ya “Yezebeli” kwamba mtu hatapitia kwa kuhani fulani au Padre fulani au Papa ili amfikie Mungu, Bali kwa IMANI kwa Mungu kila mtu atamfikia yeye na kumpendeza..kwamba mtu anasamehewa dhambi zake kwa IMANI kwa Mungu, na sio kwa kupitia mwanadamu yoyote, kadhalika na uponyaji na mahitaji na mambo mengine yote…

Hivyo kuanzia huo wakati Martin Luther alizidi kupinga kwa Nguvu mifumo ya kanisa Katoliki siku moja aliandika HAYA 95 zinazopinga mfumo wa kipapa na kuzigongelea kwenye mlango wa ngome ya kanisa kubwa la kiKatoliki lililokuwepo huko wittenberg Ujerumani mwaka 1517. Na ndipo uprotestant ulipoanzia ikasababisha uamsho mkubwa wa roho, watu wengi wakaanza kutoka kwenye hiyo dini ya uongo kwa kupitia injili za hawa wana matengenezo.

Biblia zikaanza kutafsiriwa jambo ambalo hapo kwanza zilikuwa zinasomwa tu na makuhani wa kikatoliki, Hivyo ndivyo nuru ya kweli ilivyoanza kurejeshwa kidogo kidogo.

Lakini ilifikia wakati miaka kadhaa baada ya wale wajumbe kuondoka, watu wakaanza kujisahau, na kuanza kujiundia dini badala ya kuuendeleza uamsho wa Kweli ya Mungu, badala ya kuendelea kujitakasa kutoka katika yale mafundisho ya uongo zaidi na zaidi wakajiundia ngome, nao pia wakaanza kujiita Walutheran, wacalvism, wabrownist, wamennonite n.k. watu wakaanza kujivunia wanadamu na dini, badala ya kujivunia Kristo hivyo ikawafanya wasahau kabisa ule msingi wa uprotestant ambao haukuwa na lengo la kuanzisha dini nyingine bali ulikuwa na lengo la kuwatoa katika uongo wa yule mwanamke Yezebeli (Katoliki) na kuwarejesha watu kwenye NENO LA MUNGU.

Jambo ambalo Mtume Paulo alilikemea pia kwa nguvu katika…

1wakorintho 1: 11 “Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu.

12 Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu kusema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo.

13 Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo? “

Hivyo mbele za Mungu hawa watu wa Sardi ambao mwanzoni walianza vizuri kwa nje walionekana kama wapo hai, lakini kwa ndani walikuwa WAMEKUFA kwasababu Roho ya uhai, na UZIMA haikuwa tena ndani yao, ya kuwafanya waweze kuuendeleza ule UAMSHO walioanzana nao hapo mwanzo.

Tukiendelea kusoma tunaona…

“2 Uwe mwenye kukesha, ukayaimarishe mambo yaliyosalia, yanayotaka kufa. Maana sikuona matendo yako kuwa yametimilika mbele za Mungu wangu.

3 Basi kumbuka jinsi ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia; yashike hayo na kutubu. Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako”.

Unaona hapo waliambiwa wakeshe, na wayaimarishe mambo yaliyoyasalia, (yaani kumalizia kuondoa mafundisho yote ya Yezebeli ndani ya Kanisa), na kwamba wasipofanya hivyo (yaani kukesha) atakuja kwao kama mwivi na wala hawatajua hiyo saa atakayokuja.

Swali ni saa gani hiyo anayoizungumzia atalijilia hilo kanisa? Angali wakati wa hilo kanisa ulishapita na unyakuo haujatokea?

Ni muhimu kufahamu kwamba kila kanisa Bwana alikuwa na wakati wake wa kulijilia kanisa hilo, na kujiliwa huko kulikuwa ni UAMSHO fulani wa kipekee ambao ni mahususi kwa kuwavusha watu katika hatua nyingine ya kiimani inayofuata na huo Uamsho huwa unakuja karibu na mwishoni kabisa mwa nyakati wa kanisa husika..Hivyo kwa kanisa la kwanza baada ya kuacha upendo wao wa Kwanza Bwana aliwajilia kwa kupitia uamsho wa Irenio mjumbe wa kanisa la pili hivyo kwa ile jamii iliyoweza kumtii Kristo kwa ujumbe wa wakati waliokuwa nao(Wa mtume Paulo) waliweza kuchukuliana na ujumbe wa nyakati iliyofuata..Hivyo kwao Bwana anakuwa amewajilia lakini sio kama mwivi kwasababu Roho wa Mungu hajazimishwa ndani yao, lakini wale waliokataa, kwao inakuwa kama mwivi ndio unakuta watu wanaishia kuupinga ule ujumbe wa kuwaua, Na kuishia kuchukuliwa na mafundisho ya shetani.

Kadhalika na kwa nyakati ya pili, kujiliwa kwao kulikuwa ni mwishoni kabisa mwa nyakati, jamii ya watu waliodumu na mafundisho ya Irenio (Mjumbe wa kanisa la pili) waliweza kuchukuliana na uamsho wa mjumbe anayefuata..Vivyo hivyo na kwa kwani la nne, la tano.

Sasa katika hili la tano saa ya kujiliwa kwao ilikuwa ni wakati wa uamsho wa kanisa lililofuata ambalo Bwana alimtumia Mjumbe wa Kanisa lile JOHN WESLEY kuja na ujumbe wa UTAKASO KWA DAMU YA YESU, na utakatifu Hivyo kwa wale wachache ambao waliruhusu Roho wa Mungu awatoe kutoka hatua moja hadi nyingine ya IMANI, na kukaa mbali na mifumo ya yule kahaba Yezebeli walipewa neema ya kuuamini na kuupokea ujumbe wa John Wesley na huko ndiko kulikokuwa kujiliwa kwao. Lakini wale wengine waliokuwa wanaonekana wapo hai lakini wamekufa kwa kujiundia “majina” na kutengeneza madhehebu, Bwana alipokuja na uamsho wa Roho wa Wesley hawakujua chochote Sasa hiyo ndiyo kujiliwa kama mwivi, walibaki na dini zao na madhehebu yao.wakawa hawataki kufahamu jambo lingine la ziada ya ulutheri, ucalvinism, umennonite n.k. wakati lile kundi dogo ambalo lilikuwa tayari kwenda na Roho wa Mungu lilipokea uvuvio mpya wa Roho. Kwamba kuhesabiwa haki kwa Imani peke yake hakutoshi bali pia na Utakatifu ambao hakuna mtu atakayemwona Mungu asipokua nao (Waebrania 12:14)

Kadhalika na kwa kanisa la sita Filadelfia vile vile Bwana alilijia na wale waliokuwa wanadumu katika mafundisho ya mjumbe wa kanisa la sita John Wesley ilipofika wakati kujiliwa waliweza kupewa neema ya kuonja Uamsho uliofuata lakini wale ambao waliridhika na kuchukulia ujumbe wa Wesley kama dini, walibakia katika madhehebu yao wakajifungia katika Umethodisti na wakati wa Pentekoste ya Bwana ulipokuja mwaka 1906 huko Asuza Marekani, hawakujua chochote, wengine waliishia kupinga na kusema hicho kitu ni cha shetani na wengine hawakuelewa ni kitu gani.. Kwamba kuhesabiwa haki kwa imani pamoja na utakaso havitoshi bali pia Ubatizo wa Roho Mtakatifu ndio ukamilifu wa mambo yote. (Waefeso 4:30) kwamba huo ndio muhuri wa Mungu.

Vivyo hivyo na kwa kanisa la mwisho tunaloishi linaloitwa Laodikia, wale wote watakaoupokea ujumbe wa mjumbe wa kanisa hili WILLIAM BRANHAM wakidumu katika kujitenga na mafundisho ya yule kahaba mkuu YEZEBELI na kuruhusu Roho ya Mungu ya uhai ifanye kazi ndani yao, Na kukua kutoka hatua moja kwenda nyingine kila siku, Sasa hawa Bwana atakapokuja watajua kwasababu Roho wa Mungu anatenda kazi ndani yao, na taa zao zinawaka, lakini wale wengine hawatajua chochote, wataishia aidha kupinga, au kutokuelewa juu ya huo uamsho wa mwisho unaokuja. na kwa vile hakuna nyakati nyingine zaidi ya saba..Umsho huo utakuwa ni kwa ajili ya unyakuo wa kanisa. Na zile ngurumo 7 kwenye ufunuo 10 (zilizobeba siri ambazo hazijaandikwa mahali popote ), hizo ndizo zitakazoleta uamsho wa mwisho zitakazomvusha bibi-arusi wa Kristo kutoka katika nyakati ya saba, na kuingia katika umilele. Na ndio maana Bwana alisema…

Marko 13: 33 “Angalieni, kesheni, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo.

34 Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe.

35 Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jimbi, au asubuhi;

36 asije akawasili ghafula akawakuta mmelala.

37 Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni”.

Na utaona maneno haya haya aliliambia hili kanisa la SARDI…

Ufunuo 3: 3 “Basi kumbuka jinsi ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia; yashike hayo na kutubu. Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako”. …

Lakini pamoja na hayo walikuwepo wachache katika kanisa hilo, walioweza kuenenda kwa uongozo wa Roho na kujitenga na yule mnyama hao ndio Bwana aliowaambia wataenda naye katika uvuvio wa Roho utakaokuja wa John Wesley.

“4 Lakini unayo majina machache katika Sardi, watu wasioyatia mavazi yao uchafu. Nao watakwenda pamoja nami hali wamevaa mavazi meupe, kwa kuwa wamestahili.

5 Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake.

6 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”.

Anasema yeye ashindaye jina lake halitafutwa katika kitabu cha uzima, na zaidi ya yote yale mavazi meupe yanawakilisha usafi wa hali ya juu, ‘heri wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu (Mathayo 5:8) inasema hivyo”..Hivyo kundi hili katika umilele unaokuja watakuwa na nafasi ya karibu sana na Mungu kuliko watu wengine.

Hivyo ndugu Ujumbe huo pia unatuhusu hata sisi watu wa kizazi hichi tunachoishi, wa kanisa hili la mwisho la laodikia. Je! unakesha? na taa yako inawaka? je! Roho wa Mungu bado yupo hai ndani yako?. au una jina lililo hai lakini ndani yako umekufa?..Kumbuka huu ni wakati wa jioni, ondoka katika madhehebu na vifungo vya dini kama umeupokea ujumbe wa wakati wako halafu unaugeuza kuwa kama dini au dhehebu huu ni wakati wa kugeuka. Hivi karibuni Bwana ataenda kuachilia uvuvio wa mwisho nao utakuwa ni wa kipindi kifupi sana, utakaompa bibi arusi imani ya kwenda kwenye unyakuo.

Luka 12: 35 “Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka;

36 nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara”.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali share ujumbe huu kwa wengine na Mungu atakubariki. Kwa Mwendelezo >>> Ufunuo: Mlango wa 3 Part 2

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.


Mada Zinazoendana:

YEZEBELI NI NANI?

KAMA MWIZI USIKU WA MANANE

HATUA ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA KUTUONGOZA

NINI MAANA YA KUTOKA KATIKA MADHEHEBU?


Rudi Nyumbani.

Print this post

UFUNUO: Mlango wa 2 part 4

Sehemu ya nne.

Shalom! mwana wa Mungu, karibu tujifunze Neno la Mungu, leo tukiwa katika mwendelezo wa kitabu cha Ufunuo. Hii ni sehemu ya nne, inayozungumzia juu ya lile kanisa la nne kati ya yale saba aliyoyachagua Bwana (Ufunuo 1:11), linaloitwa THIATIRA. Katika sura hii ya pili tulishayaona makanisa matatu ya mwanzo, tukaona ni jinsi gani yalivyokuwa yanaenenda na tabia zake kulingana na nyakati hayo makanisa yaliyopitia. Na leo tutamalizia sehemu ya mwisho ya sura hii ya pili, ambayo tutaliona kanisa hili la Thiatira na ujumbe wake waliopewa kutoka kwa BWANA.

Ufunuo 2:18 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika; Haya ndiyo anenayo Mwana wa Mungu, yeye aliye na macho yake kama MWALI WA MOTO, na miguu yake mfano wa shaba iliyosuguliwa sana”.

Hapa tunaona Bwana ananza na utambulisho kama yeye azungumzaye ni “yule mwenye macho kama mwali wa moto, na miguu yenye mfano wa shaba iliyosuguliwa sana”..Kama tulivyojifunza kila utambulisho unaotangulia kabla ya ujumbe,huwa una mahusiano makubwa sana na ujumbe wenyewe wa kanisa husika. Mfano tuliona katika lile kanisa lililopita alijifunua kama “yeye aliye na huo upanga mkali ukatao kuwili utokao katika kinywa chake”, na tunajua upanga unaashiria vita, na tulipokuja kusoma tuliona alikuja kufanya vita na wale wote ambao hawakutubia matendo yao maovu ndani ya kanisa. Kadhalika na hapa Bwana anakuja kama mwenye macho kama mwali wa moto na miguu iliyosuguliwa, mfano wa shaba. Tunajua kuwa macho kazi yake ni kuona. Na kama yanatoka moto inamaana kuwa anachokiona kinastahili moto. Hivyo hapa katika hili kanisa vile vile anakuja kwa hukumu kwa kile anachokiona. Swali ni kitu gani alichokiona ambacho kinastahili hukumu?..Tutakuja kukiona mbeleni.

Tukiendelea kusoma..

“19 Nayajua matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza”.

Kwa historia fupi kanisa la Thiatira lilianza mwaka 606WK hadi mwaka 1520WK, na mjumbe wake aliitwa KOLUMBA, Ni kanisa lililodumu kwa kipindi kirefu kuliko makanisa yote saba, takribani miaka 914. Kipindi hichi kinajulikana kama kipindi cha giza ni wakati ambao nuru ya NENO la Mungu lilikuwa imefifia sana kutokana na mafundisho ya kipagani kuongezeka na mambo mengine kama uchawi, na umaskini vilikuwa vimekithiri sana duniani. Lakini kulikuwa pia na kuna kundi dogo la wateule wa Mungu ambao walikusudia kutokujitia madoa na mambo maovu, walidumu katika Imani yao pasipo kujali mateso waliyoyapitia, walidumu katika upendo, na uvumilivu wa hali ya juu, na wenye bidii katika kujisafisha kila siku, wakihama kutoka utukufu hata utukufu na zaidi ya yote walikuwa na bidii sana ya kumtumikia Mungu(huduma), wakihubiri huku na kule mpaka kufikia Bwana kuwaambia matendo yao ya mwisho yamezidi yale ya kwanza, (je na sisi tunaweza tukafika hatua ya kuambiwa hivyo?)

Lakini pamoja na kwamba watu wa kanisa hilo ni watu waliokuwa na bidii nyingi na upendo na uvumilivu na subira lakini Bwana alikuwa na Neno moja juu yao ambalo ndilo lililomfanya aonekane mbele zao kama “mwenye macho kama mwali wa moto”…Unaona hapo na sisi tunaweza tukawa tunafanya mema na bidii lakini Bwana bado akawa na Neno juu yetu..tusome..

“20 Lakini nina neno juu yako, ya kwamba WAMRIDHIA YULE MWANAMKE YEZEBELI, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu.

21 Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake.

22 Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake;

23 nami nitawaua watoto wake kwa mauti. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake”.

Tunaona pamoja na kwamba kanisa hili lilitenda mema mengi kiasi cha kusifiwa lakini kilionekana kikwazo ndani yao na hicho si kingine zaidi ya yule MWANAMKE YEZEBELI kama tunavyomsoma.

YEZEBELI NI NANI?

Yezebeli tunamwona katika agano la kale alikuwa ni mke wa mfalme Ahabu wa Israeli. Kumbuka mwanamke huyu hakuwa binti wa kiyahudi, bali Ahabu alimtoa katika mataifa ya kipagani,(huko Lebanoni) ingekuwa heri kama angebadilishwa imani yake na kuwa myahudi kama ilivyokuwa kwa Ruthu, lakini haikuwa hivyo kwake, yeye alitoka huko nchi za mataifa ya kipagani, akiwa na dini yake, ya kuabudu miungu mingi pamoja na Baali, na kibaya zaidi hakuja peke yake, bali alikuja na manabii wake wengi wa kumsaidia kufukiza uvumba kwa miungu yake akiwa Israeli hivyo akawa kikwazo kikubwa kwa Israeli kwasababu hakufanya hizo ibada za sanamu peke yake bali pia aliwafundisha na kuwalazimisha watu wote hata wale waliokataa kuiabudu miungu yake kufanya hivyo (1Wafalme 19).

Hivyo Bwana alilifananisha hili kanisa la Thiatira na Israeli kipindi cha Mfalme Ahabu. Kumbuka tafsiri ya neno THIATIRA ni “MWANAMKE ANAYETAWALA”..Hivyo kama Israeli kwa wakati ule kulikuwa na mwanamke anayetawala Yezebeli, Kadhalika na katika kanisa hilo yupo mwanamke anayetawala mwenye tabia zinazofananishwa na za Yezebeli. Na huyu si mwingine zaidi ya “KANISA KATOLIKI”., mwanamke huyu huyu tunamwona pia katika ile sura ya 17, ambayo tutakuja kuzisoma kwa undani habari zake hapo baadaye, ..

Ufunuo 17: 3 “Akanichukua katika Roho hata jangwani, nikaona MWANAMKE, ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, mwenye kujaa majina ya makufuru, mwenye vichwa saba na pembe kumi.

4 Na mwanamke yule alikuwa amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake.

5 Na katika kipaji cha uso wake alikuwa na jina limeandikwa, la siri, BABELI MKUU, MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI.

6 Nikamwona yule mwanamke amelewa kwa damu ya watakatifu, na kwa damu ya mashahidi wa Yesu. Nami nilipomwona nikastaajabu ajabu kuu. “

 

Sasa kumbuka kwenye lile kanisa la kwanza, shetani alianza kujipenyeza kama “matendo ya wanikolai”, na katika kanisa la tatu na kuendelea akakomaa yale matendo yakabadilika na kuwa “mafundisho” ..Tunaona pia roho ile ile iliyokuwa kwa wanikolai ndio hiyo hiyo ilitenda kazi kwa Balaamu katika kanisa la tatu, na ndiyo hiyo hiyo inatenda kazi ndani ya Yezebeli katika Kanisa hili la Nne. Konstantini alisimama kama Balaamu, na Kanisa Katoliki linasimama kama mwanamke Yezebeli. Nao wote hawa ukiangalia kazi yao ilikuwa ni moja ni kuwakosesha watu wa Mungu wazini na kula vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu. Hivyo Kanisa katoliki liliwakosesha watakatifu wa wakati ule wamkosee Mungu kwa kufanya uasherati wa kiroho. Na uasherati wenyewe ni upi?. Ni dhahiri kuwa waliyapokea mafundisho mengine ambayo hawakukabidhiwa na Mungu tangu awali kupitia mitume wake watakatifu kwa kulichanganya Neno la Mungu na desturi za kipagani, kwamfano ibada za sanamu, kuomba kwa wafu, ibada za miungu mitatu, sala za mapokeo ya kipagani, ubatizo wa vichanga n.k.

Hivyo pamoja na kwamba walikuwa ni watakatifu, wanajitahidi kufanya mambo mema, na kutenda kazi ya Mungu kwa bidii lakini bado Mungu alikuwa anaona kasoro ndani yao, kwamba WAMEMRIDHIA yule mwanamke Yezebeli. Maana ya “kuridhia” ni kuvumilia / kukubaliana /kuchukuliana naye..Hivyo wale watakatifu wa kipindi hicho waliopewa macho ya kumtambua kwa kupitia Mjumbe wa Mungu aliyemteua kwa wakati huo (KOLUMBA) walimridhia yule mwanamke na kuchukuliana na mafundisho yake. Hivyo Bwana akawaonya watubu na kwamba wasipotubu atawaua kwa mauti na makanisa yote ndipo yatakapojua ya kuwa Bwana anachunguza viuno(fahamu za watu) na mioyo ya watu wote, kwamba yale macho yake yaonayo mpaka sirini na hakuna jambo lolote linalositirika kwake!

Kanisa Katoliki nalo Bwana alilipa muda wa kutubu, lakini halikutaka kutubu, kama tulivyoona hapo juu, hata hivyo

(Yeremia 51: 9 ilishatabiri habari zake na kusema ..“Tungependa kuuponya Babeli, Lakini haukuponyeka; Mwacheni, nasi twendeni zetu, Kila mtu hata nchi yake mwenyewe; Maana hukumu yake inafika hata mbinguni, Nayo imeinuliwa kufikilia mawinguni. “

Na ndio maana Bwana Yesu alisema ..” 21 Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake.

22 Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake;

23 nami nitawaua watoto wake kwa mauti. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake. “

Kumbuka Yezebeli alikuwa anao watoto, na mmoja wapo aliitwa “ATHALIA” (2Wafalme 9). Huyu naye alienda kuolewa na Mfalme wa Yuda na mambo yale aliyoyafanya mama yake aliyafanya na yeye vilevile na mabaya kuliko hayo. Aliutwaa ufalme kwa nguvu,na kutawala Israeli kwa muda wa miaka 7 jambo ambalo lilikuwa ni machukizo makubwa kwa Israeli taifa la Mungu kutawaliwa na mwanamke. Alidiriki pia kuuangamiza uzao wa Daudi kwa kuwaua wazao wote wa kifalme lakini mpango wake haukufanikiwa. Na zaidi ya yote aliwakosesha watu wa Yuda kama mama yake alivyowakosesha watu wa Israeli kwa kuabudu miungu migeni.

Hivyo kama Yezebeli alivyokuwa na binti anayefanana na yeye kitabia kadhalika Kanisa Katoliki (Yezebeli wa rohoni), amezaa mabinti wanaofanana na yeye kitabia na ndio maana anajulikana kama mama wa makahaba, na mabinti zake ni madhehebu yote yanayofanana na yeye. Na watu wanaoshikamana nayo Bwana atakuja kuwaua kwa mauti ( katika lile Ziwa la moto.)

Tukiendelea kusoma mistari inayofuata….

“24 Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wo wote wasio na mafundisho hayo, wasiozijua FUMBO ZA SHETANI, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine.

25 Ila mlicho nacho kishikeni sana, hata nitakapokuja”.

Unaona hapo? Bwana anasema kuna watu wasiojua “FUMBO ZA SHETANI” na walikuwa katikati ya kundi la Mungu..Hivyo shetani naye anazo fumbo zake, nazo zinahitaji hekima kuzitambua. Ikiwa na maana kuwa anajua namna ya kumdanganya mtu kulingana na jinsi anavyoenenda, ukiwa ni mwovu atakudanganya kwa njia ya uovu, na ukiwa mtakatifu atakuja kwa kivuli cha utakatifu. na ndio maana biblia inasema yule mwanamke jina lake limeandikwa kwa SIRI, kumbuka sio kwa wazi bali kwa siri, BABELI MKUU MAMA WA MAKAHABA, NA MACHUKIZO YA NCHI.. Hapo ndipo kiti cha enzi cha shetani kilipo..Yeye pamoja na watumishi wake wanajigeuza kuwa kama malaika na watumishi wa nuru. Hivyo ni kujichunguza na kujihakiki kila siku je! tupo kwenye NENO? hiyo ndiyo njia pekee ya kulifumbua fumbo la shetani na kumshinda. Lakini tukipuuzia mambo kama hayo yatatukuta kama hayo ya kanisa la Thiatira Bwana atatuua kwa mauti.

Unakumbuka watu wa kanisa hili waliambiwa matendo yao mema yamezidi hata yale ya kwanza, walijitahidi sana kuwa wakamilifu lakini walikosa kuzitambua mbinu za shetani, Kadhalika na sisi wa kanisa la mwisho tulilopo, Yule mwanamke YEZEBELI na MABINTI zake wapo, na wanazidi kuwakosesha watu na kuwapeleka mamilioni ya watu kuzimu (hususani wakristo), Kwahiyo kiini cha ujumbe ambao Bwana alikuwa anataka kuwaambia ni kwamba katika ukamilifu na utakatifu wao waongezee tu kumtoa yule mwanamke kahaha na uzinzi wake katikati yao kwa kutokuridhia mafundisho yake, na sisi vivyo hivyo katika bidii yetu yote tuliyonayo kwa Mungu katika upendo subira, uvumilivu, huduma tumalizie kwa kujitenga na yule kahaba Babeli mkuu (Katoliki) pamoja na mabinti zake wote (madhehebu).

Ufunuo 18:4 “Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, ENYI WATU WANGU, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.

5 Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake”.

Kwahiyo wote walioshinda katika kanisa hilo kwa kujitenga na yule mwanamke Yezebeli na kudumu katika Neno Bwana aliwaahidia thawabu..

” 26 Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa,

27 naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyanzi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea kwa Baba yangu.

28 Nami nitampa ile nyota ya asubuhi.

29 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. “

Thawabu hizi ni katika ulimwengu unaokuja, Bwana atakapokuwa MFALME WA WAFALME, ni dhahiri kuwa atatwaa wafalme wachache chini yake ili yeye awe Mfalme wa Wafalme na ndio watakaokuwa watu wa kanisa hili, hawa ndio watakaopewa mamlaka juu ya mataifa, na hiyo fimbo ya chuma itakuwa ni kutoa amri na kutekelezwa. Na ile nyota ya asubuhi ina maana kuwa utukufu wao utakuwa ni wa kipekee tofauti na wengine, kumbuka nyota ya asubuhi ndio nyota pekee yenye kuangaza hata wakati wa mchana, wakati nyingine nguvu zao za kung’aa zinakuwa ni usiku tu. Hivyo kule katika mbingu mpya na nchi mpya watang’aa milele na milele pamoja na Bwana Yesu. Hivyo ndugu kwanini ukose mambo hayo yote mazuri?..Tafuta kwanza ukamilifu (UTAKATIFU) mpe Bwana maisha yako leo, kisha malizia kwa kujitenga na yule mwanamke kahaba, na mabinti zake kwa kudumu katika NENO LA MUNGU TU!.na sio katika mapokeo na dini.

Ubarikiwe sana.

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.

Print this post

UFUNUO: Mlango wa 2 part 3

Sehemu ya tatu.

BWANA wetu YESU KRISTO apewe sifa. Karibu katika kujifunza Neno la Mungu, leo tukiendelea na sehemu ya tatu, ya sura hii ya pili, ambapo tulishatangulia kuona lile Kanisa la Efeso na Smirna, pamoja na wajumbe na ujumbe wao kutoka kwa Bwana. Na hapa tutaona kwa ufupi kanisa lingine la tatu linaloitwa PERGAMO. Tunasoma

KANISA LA PERGAMO.

Ufunuo 2: 12 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na huo upanga mkali, wenye makali kuwili”.

Kama tulivyotangulia kujifunza tunaona hapa Bwana anaanza kwa kujitambulisha kama “yeye aliye na huo upanga mkali,wenye makali kuwili”. Tulishaona katika makanisa yaliyopita,kwamba ule utambulisho wa kwanza Bwana anaoanzana nao, una uhusiano mkubwa na ujumbe wa kanisa husika..Sasa hapa anaposema “yeye mwenye upanga mkali”, haimaanishi jambo jema sana kwa kanisa hilo, kama alivyojitambulisha katika kanisa la Smirna aliposema “yeye aliyekuwa amekufa kisha akawa hai” kuonyesha kwamba kuna tumaini baada ya kifo,.Lakini hapa ni tofauti, anaanza kwa kutamka upanga na upanga siku zote unaashiria vita, na tena anasema unatoka katika kinywa chake ikiwa na maana kuwa ataenda kufanya vita kwa kinywa chake, (Ambalo ndio Neno lake). Na pia kumbuka hapa hazungumzi na watu wa mataifa (yaani wasio wakristo na wasiomjua Mungu) hapana bali anazungumza na wakristo, na hao ndio atakaofanya nao vita kwa huo upanga utokao katika kinywa chake.. Lakini ni kwanini afanye nao vita?, tutakuja kuona hapo mbeleni sababu zenyewe:

Tukiendelea kusoma..:

” 13 Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu, hata katika siku za Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo Shetani. “

Neno “Pergamo” tafsiri yake ni “NDOA”. Na Historia inaonyesha kanisa hili lilianzia mwaka 312WK na liliisha mwaka 606WK. Lakini hapa tunaona Bwana anawaambia watakatifu wa wakati huo kwamba anafahamu kuwa mahali walipokaa ndipo penye kiti cha Enzi cha shetani, (mahali penyewe tutapaona mbeleni) na pia ameona kuwa wamelishika sana jina lake wala hawakuikana imani, licha ya kwamba shetani alikuwa anawaua wakristo wengi, tangu kanisa lililotangulia nyuma hadi huo wakati waliokuwepo wakristo wengi waliuawa, hata katika siku za Antipa, ambaye alikuwa pia ni shahidi mwamifu wa Bwana aliyeishindania Imani mpaka kufa bila kuikana.Hawa wote hawakutikisika kwa lolote pamoja na dhiki hizo zote.

Lakini Bwana anaendelea kusema;

 ” 14 Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini.

Baada ya shetani kuona kuwa watu bado wapo radhi kutoa hata maisha yao kwa ajili ya IMANI yao, akaona kwa njia ya vitisho na dhiki haina nguvu tena kuwatoa watu kwa Mungu, ndipo akabadilisha mbinu, na kuhamia kwenye njia ya udanganyifu, Na ndio maana hapo tunaona Bwana anasema ” unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu ” Swali ni je! haya mafundisho ya Balaamu ni yapi?.

Habari za Balaamu tunazipata katika agano la kale kitabu cha Hesabu 22. Tunasoma kuwa wakati wana wa Israeli wakiwa jangwani katika safari yao ya kuelekea nchi ya ahadi walikutana na wana wa Moabu njiani, na walipotaka kukatiza katika nchi yao mfalme wao aliyeitwa Balaki aliwazuia. Na zaidi ya yote akaenda kumwajiri Balaamu nabii wa uongo ili awalaani wana wa Israeli (Kuwaloga) wasifanikiwe katika safari yao. Hivyo Bwana alimzuia Balaamu mara tatu asiwalaani, na kinyume chake akawabariki. Lakini haikuishia hapo Balaamu yule nabii wa uongo kwa kupenda fedha ya udhalimu, kutoka kwa mfalme Balaki alitafuta njia mbadala ya kuwakosesha wana wa Israeli. Ndipo akamshauri Balaki afanye karamu na kuwaalika wanaume wa Israeli ili wafanye uzinzi na wanawake wa kimoabu na kutoa sadaka kwa miungu yao, ili iwe ukwazo kwao kwa Mungu wa Israeli na Mungu awaadhibu. Hivyo njama yake kweli ilifanikiwa, na hasira ya Mungu ikawaka juu ya Israeli, nao wakaadhibiwa kwa kosa lile. Hivyo tunaona hapo Balaamu ndiye aliyekuwa chanzo cha kuwakosesha Israeli.

Vivyo hivyo katika hili kanisa la Pergamo, Kumbuka kwa wakati ule Rumi ndiyo iliyokuwa inatawala dunia, na utawala ule ulikuwa ni utawala wa kipagani, Lakini ilifika wakati mtawala wa Rumi aliyeitwa KONSTANTINI alipokuwa anataka kwenda kupigana vitani dhidi ya maadui zake, aliota ndoto na akaona angani ya msalaba, Hivyo alipoenda vitani akaweka nembo ya msalaba katika mavazi yake ya kivita akiamini kuwa yale ni maono kutoka kwa Mungu, na aliposhinda ile vita akasema Mungu wa wakristo amemsaidia hivyo kuanzia huo wakati akataka kuifanya dini ya kikristo kuwa ya dini ya taifa, hivyo akaanza kufanya jitihada za kuunganisha pamoja warumi na wakristo hivyo akachukua desturi za dini za kipagani za Rumi(za kuabudu miungu mingi) na ukristo akavileta pamoja ili awapate wote. Kwa lugha nyepesi alichofanya Konstantini ni KUOANISHA ukristo na upagani..Na ndio maana tafsiri ya neno Pergamo ni NDOA.

Kwahiyo alichofanya mwaka 325WK ni kuitisha baraza kubwa la maaskofu, na viongozi wote wa Kikristo mahali panapoitwa NIKEA. Ambapo zaidi ya viongozi wa kidini 1,500 walihudhuria kuzungumzia suala hilo. Na ndipo wote wakafikia muafaka wa kuundwa Dini moja ya ulimwengu mzima (Kanisa Katoliki). Kumbuka tafsiri ya Neno Katoliki ni “ulimwengu wote” hivyo kanisa Katoliki maana yake ni “Kanisa la ulimwengu wote”.. Sasa kuanzia hapo ule ukristo ambao ulikuwa haujachanganyikana na mafundisho yoyote ya uongo, ukafa na kuzaliwa ukristo mpya bandia ambao umechukuliwa na desturi za kipagani za Rumi mfano wa kuabudu miungu mingi, na ndio hapo vitu kama ubatizo wa vichanga ukazaliwa, ubatizo wa kunyinyuziwa ukaundwa, ibada za sanamu,kusali rozari na za kuomba kwa watakatifu waliokufa zamani mambo ambayo huwezi kuyaona katika maandiko matakatifu au kufanywa na mitume wa zamani,pamoja na ibada za miungu mitatu, Ambazo utazikuta kwenye desturi za kirumi.

Sasa kumbuka huyu Konstantini ndio mfano wa Balaamu Bwana Yesu aliyemzungumzia kuwa anawakosesha watu wake (Kumbuka roho ile ile ya shetani iliyokuwa ndani ya Balaamu ndiyo hiyohiyo iliyokuwa ndani ya Konstantini). Kama vile Balaamu alivyotia ukwazo kwa wana wa Israeli wale vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu na kuzini vivyo hivyo Konstantini alianza kuwakosesha watu wa Mungu (wakristo) kwa kuwatoa katika mstari wa ukristo wa kweli wa mitume, na kuwaingiza katika dini ya kipagani aliyoianzisha yeye (Ukatoliki). Na kuwafanya wafanye uzinzi wa kiroho na kuamsha ghadhabu ya Mungu katikati yao.

Bwana Yesu aliendelea na kusema…

“15 Vivyo hivyo wewe nawe unao watu wayashikao mafundisho ya Wanikolai vile vile”

Kumbuka pia hawa wanikolai tuliwaona tokea Kanisa la kwanza la Efeso, isipokuwa kule walikuwa wanaonyesha matendo tu lakini hapa katika kanisa hili wamehama kutoka katika matendo na kuwa katika “Mafundisho” ikifunua kuwa ni kitu kilichotia mizizi sana, kimeundiwa kanuni na sheria za kufuatwa. Kumbuka tena tafsiri ya neno NIKOLAI ni “kuteka madhabahu”. Hivyo wanikolai ni watekaji madhabahu, watu wanaochukua nafasi ya madhabahuni ambayo ingepaswa iwe ya Roho Mtakatifu mwenyewe na kuifanya yao. Mfano vyeo vya upapa, ukadinali, upandre viongozi wakuu, n.k.kujengwa kwa madaraja yanayomtofautisha mkristo mmoja na mwingine mbele za Mungu. Kwamba ilikuwa huwezi kumfikia Mungu au kumwomba Mungu bila kupitia kwanza katika ngazi za juu yako.Ilikuwa ili kusamehewa dhambi ilimpasa mtu apitie kwa pandre wake amwombee, yeye mwenyewe hawezi kufanya hivyo. Hivyo uhusiano binafsi wa mtu na Mungu uliuliwa, ukaundwa uhusiano wa mtu na mtu kwa niaba ya Mungu..(Huo ndio unikolai), uongozi wa Karama za rohoni ukafa, ukanyanyuka uongozi wa kibinadamu kanisani… Na mafundisho haya yalipokomaa na kuhasiliwa na hiyo dini ya ulimwengu mzima (Kikatoliki) ndipo ukatokea UPAPA (ambao Unasimama kama mwakilishi wa Mwana wa Mungu duniani)..Hii ndiyo ngazi ya juu kabisa ya hii roho ya unikolai.

Lakini Bwana anamaliza na kusema…

” 16 Basi tubu; na usipotubu, naja kwako upesi, nami nitafanya vita juu yao kwa huo upanga wa kinywa changu.

17 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea. “

Unaona kama vile wana wa Israeli walivyouliwa kwa upanga siku ile watu elfu 24, kwa kosa tu la Balaamu.. Vivyo hivyo Bwana aliwaonya na hao wakristo wa hilo kanisa la Pergamo kwamba watubu na wajiupushe na mafundisho ya Konstantini yaliyofananishwa na Balaamu (yaani dini iliyoundwa ya kikatoliki), inayowapelekea kufanya uasherati wa kiroho, na ibada za sanamu. Lakini walikuwepo watu ambao hawakutubu kipindi hicho wakachukuliana na hiyo dini ya uongo ya Konstantini, Bwana aliwaua hao wote kwa upanga utokao katika kinywa chake, Hao wote walikufa kiroho, na kabla ya kuangamizwa nafsi zao Bwana aliwanyanyulia mjumbe kwanza na kuwahubiria mambo hayo na kuwarudisha katika njia ya kweli ya mitume kwa udhihirisho wa kipekee kutoka kwa Bwana, na mjumbe huyo ni MARTINI ndiye aliyekuwa (Malaika/Mjumbe) wa hilo kanisa.

Kwahiyo wale wote walioupokea ujumbe wake,na kujitenga na uasi huo Mungu aliwalinda mpaka mwisho kama tunavyosoma..’

“17 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea”.

Hivyo wote walioshinda, Bwana alizidi kuwaongozea ufunuo wa ziada wa kuzijua siri zake, na kumtambua shetani na hila zake (Ndiyo ile mana iliyofichwa). Kumbuka ni mana iliyofichwa ikimaanisha kuwa sio watu wote wataiona isipokuwa bibi-arusi tu aliyejitenga na mifumo yote ya yule kahaba mkuu (Katoliki). Huyo tu ndiye atakayepokea hicho chakula cha kipekee kitokacho mbinguni. Kadhalika alisema pia yeye ashindaye atapewa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea..Sasa thawabu hii watapewa katika ule ulimwengu unaokuja..

Ni mfano wa zawadi na ndio maana anasema juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea. Kuashiria kwamba siku atakapolipokea ndipo atakapojua thamani ya alichopewa na watu wengine wataiona baadaye.. Sasa kumbuka anaposema kupewa jina, haimanishi kubadilishiwa jina, au kupewa jina lenye mvuto mzuri hapana, tunaweza tukajifunza kwa maisha tu ya kawaida unaweza ukapita mahali fulani ukasikia mtu fulani ana jina mahali pale.. Haimaanishi kuwa jina lake ni zuri au ni la kipekee sana hapana moja kwa moja utajua huyo mtu anayo nguvu fulani labda ya kifedha au kimamlaka, au ki-sifa ndiyo iliyompa jina hilo..Na ndivyo itakavyokuwa huko katika utawala wa milele unaokuja.. Kuna watu watakuwa na majina mazito na makubwa kutokana na uaminifu wao waliokuwa nao hapa duniani, na kuna watu pia watakuwa na majina madogo. Biblia inatuambia hata Bwana mwenyewe atakuja na Jina jipya, siku hiyo ndiyo kila mtu atamfahamu kwa mapana yeye ni nani na biblia ilikuwa inamaanisha nini ilipokuwa inasema kuwa yeye ni BWANA WA MABWANA na MFALME WA WAFALME. HALELUYA!!.

Kwahiyo ndugu yangu hata sasa haya mafundisho ya Balaamu yapo ndani ya Kanisa na yapo katika kiwango cha juu sana kuliko hata kile cha kipindi kile, roho ya mafundisho ya kipagani imejichanganya katikati ya watu wa Mungu. Hivyo toka huko. Bwana leo hii anaachilia mana yake iliyositirika kwa wachache waliotayari kutii, lakini wakati utafikia tusipotubu na kuyaacha mafundisho ya uongo na kuyakimbia.. Bwana atakuja kufanya vita nasi kwa Neno lake kwa kupitia vivywa vya watumishi wake. Na ukishafikia hiyo hatua, kutakuwa hakuna nafasi ya pili, hapo ni kuingojea ile siku ya Bwana inayowaka kama moto na kutupwa katika lile ziwa la moto. Hivyo huu ni wakati wa kutengeneza mambo yako sawa ili hayo yote yasikupate kabla ya mlango wa neema kufungwa.

Ubarikiwe.

1.Ufunuo: Mlango wa 2 Part 4

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.

Nyumbani

Print this post

UFUNUO Mlango wa 2: Sehemu ya pili.

Sehemu ya pili.

Libarikiwe jina la mwokozi wetu YESU KRISTO milele na milele AMINA!. Karibu katika kujifunza kitabu cha Ufunuo. Leo tukiendelea katika ile sehemu ya pili ya mlango huu. Kama tulivyotangulia kuona katika sehemu ya kwanza juu ya kanisa la Kwanza (EFESO) na ujumbe wake kutoka kwa Bwana..Kwamba watu wa kanisa lile waliuacha ule upendo waliokuwa nao hapo mwanzo, na jinsi Bwana alivyowaonya watubu na kwamba wasipotubu Bwana atakuja kukiondoa kile kinara chao cha taa. Lakini tukiendelea na Kanisa la Pili linaloitwa SMIRNA tunasoma;

KANISA LA SMIRNA.

Ufunuo 2:8 ” Na kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna andika; Haya ndiyo aneneyo yeye aliye wa kwanza na wa mwisho, aliyekuwa amekufa, kisha akawa hai”.

Hapa tunaona Bwana anaanza kwa utambulisho kwamba “yeye ni wa kwanza na wa mwisho, aliyekuwa amekufa, kisha akawa hai”. Kumbuka Kama tulivyotangulia kujifunza utambulisho wa awali wa Bwana unakuwa na uhusiano mkubwa sana na kanisa husika kabla hata ya ujumbe wenyewe kutolewa. Mfano hapa Bwana anaposema aliyekuwa amekufa kisha akawa hai, kama alivyotangulia kujitambulisha hivyo hivyo katika ile sura ya kwanza (Ufunuo 1:18), Hii ikifunua kuwa kuna mapito ya mateso na dhiki nyingi mpaka kupelekea KIFO lakini pia kuna matumaini ya kufufuka baada ya kifo kama Bwana alivyopitia. Na ndio maana hapa hakujitambulisha kama yeye mwenye ule upanga mkali utokao kinywani mwake(maana upanga unawakilisha vita na hapa hajaja kufanya vita), au mwenye uso kama unaong’aa kama jua n.k bali ni “yeye aliyekuwa amekufa kisha akawa hai”

Tukiendelea kusoma;

Ufunuo 2: 9 “Naijua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani.

10 Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima”.

Kumbuka neno “SMIRNA” tafsiri yake ni “(MANE MANE ILIYOSAGWA au CHUNGU)”. Hivyo kama jina lilivyo ndivyo kanisa lilivyokuwa, Hili kanisa lilipitia uchungu mwingi na mateso kutokana na IMANI yao. Kanisa hili lilianza mwaka 170WK na kuisha mwaka 312WK. Katikati ya hichi kipindi maelfu ya wakristo waliuliwa kwa kuingizwa magerezani, wengine walitupwa kwenye matundu ya simba, wengine waliburutwa,wanawake walikatwa matiti na kuachwa damu zichuruzike mpaka kufa, wengine walichomwa moto, wengine walisulibiwa n.k. Hivyo historia inarekodi walipitia dhiki nyingi sana kama vile tu Bwana alivyopitia akiwa hapa duniani. Na Bwana aliwaambia pia kuwa anajua UMASKINI wao, na dhiki yao lakini ni matajiri.

Ni kweli watakatifu wa wakati huo wa kanisa la Smirna walikuwa ni maskini, lakini mbele za Mungu walikuwa ni matajiri..Kama vile Bwana alivyokuwa duniani maskini lakini mbele za BABA alikuwa ni tajiri kuliko watu wote duniani. 2Wakorintho 8: 9 “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake”. Vivyo hivyo na hawa watu wa hili kanisa hawakupenda maisha yao hata kufa kwa ajili ya BWANA. Walichekwa na kudharauliwa na kuonekana kama watu wasiostahili kuishi katikati ya jamii za watu wengine (Waebrania 11:38).

Na kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna andika; Haya ndiyo aneneyo yeye aliye wa kwanza na wa mwisho, aliyekuwa amekufa, kisha akawa hai

Tunaona pia Bwana aliwaambia ” huyo Ibilisi atawatupa baadhi yao gerezani ili wajaribiwe nao watakuwa na dhiki siku kumi “. Tunaona jambo hilo lilikuja kutimia katika utawala wa Rumi chini ya kiongozi mkatili aitwaye Diocletian ndani ya miaka 10 aliwaua maelfu ya wakristo katika magereza kuanzia mwaka 300WK hadi 310WK. (Hizo ndio zile siku 10 zilizozungumziwa na Bwana). Pamoja na hayo BWANA aliwaambia ” wawe waaminifu hata kufa, naye atawapa taji ya uzima. “..Haya ni maneno ya faraja kutoka kwa BWANA mwenyewe kwa watu wa kipindi kile ambapo Bwana alitumia kinywa cha IRENIO kama mjumbe wa kanisa hilo kuwafariji watakatifu na kuwarudisha kwenye Neno akiyapinga yale mafundisho ya Wanikolai ambayo tuliyoyaona katika lile kanisa la kwanza, na hapa Bwana anawaita sinagogi la shetani, wanajifanya kuwa watu wa Imani kumbe sio.

Kadhalika walikuwepo pia watu wengine waliokuwa waaminifu kama wakina Polycarp ambao Mungu aliwatumia pia kunyanyua imani za watu na kuwafariji kwa kufa vifo vya kishujaa kama Bwana.Waliishindania imani kwa nguvu zote katika kanisa hilo la Smirna.

Bwana alimalizia na kusema “11 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. “. Hivyo Japo Bwana aliruhusu WAFE (wapate mauti ya kwanza ya mwili). Lakini aliwaahidia wale watakaoshinda kuwa hawatapatikana na mauti ya pili (Kifo cha Roho). Kumbuka mauti ya kwanza ni hii roho ya mtu kutenganishwa na mwili hivyo mwili unakuwa umekufa lakini roho ya yule mtu bado inaendelea kuishi. Sasa mauti ya pili ni roho inakufa kabisa kama vile mwili unavyokufa. Na hii inauliwa katika lile ziwa la moto tu. Na kama vile mauti ya kwanza inavyokuwa na uchungu, si zaidi sana mauti ya roho? itakuwa na uchungu mara nyingi zaidi.

Watu wa kanisa hilo walizingatia lile Neno Bwana alilosema katika Mathayo 10: 28 ” Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum”.

Unaona hapo, watu hawa japokuwa walikuwa ni maskini sana, watu wenye dhiki nyingi sana, mpaka kufikia wakati Bwana anawaambia “kifo kinakuja mbele” lakini hawakuikana IMANI, Walizidi kuishikilia imani mpaka kufa. Je! na sisi tunaweza tukawa kama hawa?. Jiulize leo hii unapopitia tabu kidogo, aidha magonjwa, au dhiki fulani unajitenga na Imani..Ujawezaje kupokea taji ya uzima . Na kuepuka madhara ya mauti ya pili? siku ile Bwana atakapokuja? .

Huu ni wakati wa kujihakiki na kujiweka sawa, ili wakati wa kujaribiwa utakapofika tuweze kuwa imara, kama Bwana wetu YESU KRISTO aliyapitia hayo, na watakatifu wake wa kanisa la mwanzo, kadhalika sisi nasi siku yatakapotujia hayo yatupasa tuyashinde kama Bwana.

Ubarikiwe.

Tafadhali share ujumbe huu kwa wengine na Mungu atakubariki. Kwa Mwendelezo >>> Ufunuo: Mlango wa 2 Part 3

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.


Mada Zinazoendana:

JE! UKRISTO UNAMPA MTU DHAMANA YA KUWA TAJIRI?

NJIA YA ‘UTAJIRI MKUU’ KWA KIJANA NI IPI?

“HERI WALIO MASKINI WA ROHO” JE HATUNA RUHUSA YA KUWA MATAJIRI WA ROHO?

Rudi Nyumbani

Print this post

UFUNUO Mlango wa 2: Sehemu ya kwanza.

(Sehemu ya kwanza)

Jina kuu la BWANA wetu YESU KRISTO litukuzwe milele yote. Karibu katika mwendelezo wa uchambuzi wa kitabu cha Ufunuo, Leo tutaitazama ile sura ya pili. Kama tulivyotangulia kusoma katika ile sura ya kwanza, Tuliona Yohana akionyeshwa Sura na umbo la YESU KRISTO , na wasifa wake ambao alionyeshwa kwa lugha ya picha,(Kumbuka Bwana Yesu kiuhalisia hana muonekano kama ule), jinsi alivyokuwa anaonekana na nywele nyeupe kama sufu, macho ya moto, miguu ya shaba, upanga unaotoka kinywani mwake, mwenye sauti kama maji mengi, aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu n.k. hizo zote zilisimama kama viashiria (Nembo) vya tabia yake, ambayo kila moja ina nafasi yake katika hichi kitabu cha Ufunuo na ndio maana zilitangulizwa kuelezwa mwanzoni kabisa mwa kitabu hichi.

Hivyo katika sura ile ya kwanza mwishoni tuliona jinsi Yohana anaambiwa ayaandike yale aliyoyaona na ayapeleke kwa yale makanisa saba. 

Ufunuo 1: 19 Basi, uyaandike mambo hayo uliyoyaona, nayo yaliyopo, na yale yatakayokuwa baada ya hayo.

20 Siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume, na ya vile vinara saba vya dhahabu. Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba; na vile vinara saba ni makanisa saba.”

Ni muhimu kufahamu Barua hizi Yohana alizopewa hazikuyahusu tu yale makanisa 7 yaliyokuwa Asia ndogo kwa wakati ule, bali pia na kwa makanisa yatakayokuja huko mbeleni na ndio maana hapa anaambiwa ayaandike mambo hayo YALIYOPO na YATAKAYOKUJA baada ya hayo. Ikiwa na maana kuwa yale yaliyoko ndio yale makanisa 7 yaliyokuwa Asia katika wakati wa Yohana, na yale yatakayokuja ni Makanisa 7 tuliopo sisi baada ya Yohana kuondoka. Kwahiyo Tunaposoma leo hii kitabu cha ufunuo tunajua kuwa yale makanisa 7 yaliyokuwa katika kipindi cha Yohana yameshapita. Na tangu kipindi cha Bwana YESU kuondoka hadi sasa ni takribani miaka 2,000 na kanisa la Kristo limekuwa likipita katika vipindi tofauti tofauti saba ndani ya huo muda wa miaka 2000, vijulikanavyo kama NYAKATI SABA ZA KANISA.

Sasa tukirudi katika sura ya pili. Tunaona Bwana Yesu akianza kutoa ujumbe kwa kanisa moja baada ya lingine, Kuanzia kanisa la Efeso mpaka Laodikia ambalo ndio la mwisho. Tunasoma;

KANISA LA EFESO:

Ufunuo 2:1 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu”.

Awali ya yote tunaona Bwana Yesu anajitambulisha hapa kama “yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu na aliyeshika zile nyota saba”. Kumbuka hapa hajajitambulisha yeye kama yeye mwenye macho ya moto au uso ung’aao kama jua. Lakini alisema yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu ikiwa na maana kuwa uelekeo wake wote utakuwa katika kuchunguza kinara cha hilo kanisa na yale makanisa mengine. Kumbuka kinara ni taa iliyokuwa inawekwa katika nyumba ya Mungu (Hekaluni) Kwa ajili ya kutia Nuru kule ndani (Patakatifu) ili shughuli za kikuhani ziende sawasawa (Kutoka 27:20), na kilikuwa hakizimwi muda wote, sharti ni lazima kimulike daima usiku na mchana pasipo kuzimwa. Vivyo hivyo hapa Bwana alipoanza kwa kujitambulisha hivyo alikuwa anatazamia nuru isiyozimika ndani ya hilo kanisa husika (nyumba yake) ambalo analitolea habari zake hapo chini.

Siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume, na ya vile vinara saba vya dhahabu. Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba; na vile vinara saba ni makanisa saba.

(katika nyumba ya Bwana kinara cha taa kilikuwa na mirija/matawi saba, na kilikuwa kinatia nuru nyumba ya Mungu daima)

Na NURU hii ni ipi Bwana aliyokuwa aliitazamia kuiona inaangaza?. Biblia inatuambia

1Yohana 2: 8 Tena nawaandikia amri mpya, neno lililo kweli ndani yake na ndani yenu; kwa kuwa giza linapita na ile nuru ya kweli imekwisha kung’aa.

9 Yeye asemaye kwamba yumo NURUNI, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa.

10 Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo.

11 Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.

Na pia tukisoma 1Wakorintho 13 inasema Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote, Upendo haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli n;k. Hivyo kwa ujumla NURU ni UPENDO. Ambao huo unaanza kwanza kwa KUMPENDA BWANA MUNGU WAKO kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote,na kwa nguvu zako zote, (Kwa kuzishika na kuzifuata amri zake) na pia kumpenda jirani yako kama nafsi yako. Kwa kuzingatia hayo mawili KINARA CHAKO kitakuwa kinatoa Nuru ya kutosha.

Sasa tukirudi katika Kanisa lile la EFESO, tunaona Bwana aliendelea kulitolea habari zake na kusema:

Ufunuo 2:2-5 “Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo;

3 tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka.

Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza.

Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.

6 Lakini unalo neno hili, kwamba wayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo na mimi nayachukia.”

Kwanza kabisa maana ya neno EFESO ni “Kuacha mema yaondoke”. Hivyo hili kanisa kama jina lake lilivyo mwanzoni lilianza kuenenda katika Nuru ya Neno ambao ni UPENDO wa kiungu, lilikuwa japokuwa linapitia majaribu mengi liliendelea kumpenda Mungu, lilivumilia mabaya,Hii tunaona katika utawala wa Rumi chini ya kiongozi mkatili Nero, aliyewaua wakristo wengi wakati ule kwa kuwasingizia kuwa wameuchoma mji na hali sio wao. Kanisa hili pia mwanzoni lilijiweka katika utakatifu wa hali ya juu, liliwapima manabii wa uongo na kugundua kuwa sio, kwa muda mrefu sana. Walikuwa na uwezo pia wa kuyagundua matendo ya WANIKOLAI na kuyapinga katikati ya Kanisa. Kumbuka neno “Nikolai” tafsiri yake ni “Kuteka madhabahu” Hivyo kulikuwa na tabia zilizokuwa zimeanza kujitokeza katikati ya baadhi ya makanisa, watu(wasio wa Mungu) walianza kijipachikia vyeo vilivyoua uongozi wa Roho Mtakatifu. kwamfano watu badala ya kwenda kumuomba Mungu msamaha, walianza kuwafuata wanadamu wenzao wawaombee au wawaondolee dhambi zao kwa niaba ya Mungu, Badala karama za roho ziongoze kanisa, vyeo vya kibinadamu vikaanza kuongoza kanisa n.k. Huku ndiko kuteka madhabahu na hayo ndiyo yaliyokuwa matendo ya Wanikolai, ambayo kanisa la Kristo la kweli lilichukizwa nayo na Bwana vilevile.

Lakini Kanisa hili la Efeso lilifikia kipindi ule upendo waliokuwa nao hapo kwanza ukaanza kupoa (wakaanza kuacha mema yaondoke katikati yao kama vile Jina la kanisa lao lilivyo), uvumilifu kwa ajili Imani, utakatifu na subira vikaanza kupoa, zamani walikuwa wanawajaribu manabii wa uongo na kuwaondoa katikati yao lakini sasa hawafanyi hivyo tena.. Na ndio maana Bwana hapa anatokea na kuanza kukichunguza kinara chao na kuwaambia NURU yao imeanza kufifia na kukaribia kuzima Ukiendelea kusoma utaona Bwana anawaambia watubu 

” 5 Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye MATENDO YA KWANZA. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.”

Kama tulivyoona Pale mwanzoni katika ile sura ya kwanza juu ya ule mwonekano wake, jinsi alivyoonekana akipita katikati ya vile vinara vya taa, ikiwa na maana kuwa anapeleleza na kufanya masahihisho, kinara kilichofifia na kukaribia kuzima anakiondoa na kile kinachozidi kuwaka anakiongezea nuru, kwasababu biblia inasema “mwenye nacho ataongezewa asiye nacho hata kile kidogo alicho nacho atanyang’anywa” Hivyo kama wasingeimarisha matendo yao, hata ile nuru waliyokuwa nayo kidogo ingeondolewa kwao. Na ile taabu yao ya mwanzo waliyoisumbukia ingekuwa ni sawa na bure.

Sasa kanisa hili la Efeso lenye tabia hizi lilianza kati ya kipindi cha 53WK hadi mwaka 170WK. Na Malaika wa kanisa hilo alikuwa ni Mtume Paulo. Kumbuka Neno “malaika” tafsiri yake ni “mjumbe”  hivyo wapo wajumbe wa kimbinguni(ndio malaika wa rohoni) na wapo wajumbe wa duniani. Hawa wanaotajwa katikati ya haya makanisa saba ni wajumbe wa kiduniani (yaani wanadamu). Kwahiyo malaika wa Kanisa hili la Efeso alikuwa ni Mtume Paulo. Kwasababu yeye ndiye mtume aliyepewa neema ya kupeleka Injili kwa mataifa. Na mafunuo mengi aliyopewa yalikuwa ni msingi katika makanisa ya wakati ule, na hata sasa.

Kadhalika na sisi tuliopo katika Kanisa la mwisho (Laodikia) ambalo tutakuja kusoma habari zake hapo baadaye na sisi pia tunaonywa tusipotubu kinara chetu kitaondolewa.. Kumbuka BWANA pale anaonekana akipita katikati ya vile vinara saba na sio “Kinara kimoja“. Hivyo anavichunguza vyote kuanzia cha kwanza mpaka cha mwisho. Na kama asipoiona ile nuru aliyoikusudia iwepo katika kinara chetu vile vile kitaondolewa.. Na tunafahamu madhara ya Nuru kuondolewa, anamaanisha giza linaachiliwa liingie ndani yako.

Ndugu Mwanzoni ulipoanza kuamini ulikuwa mtakatifu lakini sasa hivi utakatifu wako umepoa, ulikuwa unasali, ulikuwa unavaa vizuri, ulikuwa na huruma kwa ndugu, ulikuwa na upendo, ulikuwa na uvumilivu juu ya imani yako hata kama watu wanaokuzunguka wanakudhihaki, ulikuwa huwezi kuabudu sanamu au kuchukuliana na mafundisho ya uongo lakini sasahivi unayapokea mafundisho ya uongo na kuyafurahia, Injili zisizokufanya utazama ufalme wa mbingu ndio unazozipenda, huwezi tena kusali, kujisitiri huwezi tena, hukutazamii tena kuja kwa Bwana umechoka na kuishiwa nguvu. Hizo ni dalili za Kinara chako kuzima..Jitahidi kabla hakijaondolewa. Maana siku kitakapoondolewa ndugu hali yako ya mwisho itakuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Ule upendo uliokuwa nao kwanza wa Mungu unaondoka kabisa ndani yako, unafanana tena na watu wasiomjua Mungu, au unakua kama vile mtu ambaye hajawahi kumjua Mungu kabisa.

Hivyo tujitahidi na sisi TAA zetu ziwe zinawaka katika hizi siku za kumalizia kwasababu Bwana hivi karibuni anarudi.. yeye mwenyewe alisema; katika Luka 12: 35 Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na TAA ZENU ZIWE ZINAWAKA; 36 nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara.”

Ubarikiwe sana.

Endelea hapo chini sehemu ya pili ya sura hii ya pili ya kitabu cha Ufunuo,.ambapo tutakuja kuona ujumbe wa kanisa la pili (SMIRNA).

Tafadhali “Share” kwa wengine ujumbe huu na Mungu atakubariki.

1.Ufunuo: Mlango wa 2: Sehemu ya 2

Nyumbani

Print this post