Category Archive Home

Biblia inakataza kuapa kabisa, lakini kwanini watu wanaapa mahakamani na katika vifungo vya ndoa?

JIBU: Ni vizuri kuelewa aina ya viapo mbalimbali vinavyozungumziwa katika biblia, ili usichanganyikiwe unapokutana na baadhi ya vifungu vinavyoonyesha wengine wakiapa lakini Biblia haiwahesabii kosa lolote kwa mfano pale mtume Paulo aliposema.

2Wakorintho 1: 23 “Lakini mimi NAMWITA MUNGU AWE SHAHIDI JUU YA ROHO YANGU, ya kwamba, kwa kuwahurumia sijafika Korintho”.

Warumi 1:9 “Kwa maana Mungu, nimwabuduye kwaroho yangu katika Injili ya Mwana wake, NI SHAHIDI wangu jinsi niwatajavyo pasipo kukoma”,

Hivyo kwa maelezo mafupi Vipo viapo vya aina mbili..aina ya kwanza ni viapo vya uaminifu, mfano wa hivi ni maagano au nadhiri.. Kwamfano Nadhiri ni kiapo, kinachomfunga mtu kwa Mungu wake kwamba unakuta mtu anamwambia Mungu ukinitendea hivi nitakutendea hivi, au sitafanya kitu fulani kwa wakati fulani mpaka nimalize kutimiza kusudi fulani..Hivi vyote mbele za Mungu ni viapo, na mtu anafungwa katika hivyo mpaka avitimize, asipovitoa kwake mtu huyo inakuwa ni dhambi.  

Hali kadhalika na pale wenzi wawili wanapofunga ndoa mbele za Mungu sawasawa na maagizo yake, moja kwa moja wanaingia katika viapo kwamba hakuna chochote kitakachowatenganisha mpaka kifo kitakapowakuta..Sasa iwe wamekiri hadharani au hawajakiri hadharani, wakishaingia kwenye ndoa tu, tayari maandiko yameshawafunga.   Hali kadhalika na mahakamani au katika mikataba ya kidunia: Ili mtu kujiridhisha na wewe uaminifu wako, huwa unaapishwa, kwamba unalolisema ni kweli, na kwamba utafanya sawasawa na mkataba au makubaliano mliyoingia..

Sasa viapo kama hivyo vyote haviji kwa lengo la kujihesabia haki, au kujiona wewe uko sawa mbele za mtu, au kujifanya wewe ni mkamilifu hapana bali ni vya kuthibitishwa tu.   Lakini sasa vipo viapo ambavyo vinakuja nje ya utaratibu wa Mungu, kwa mfano mtu pale anaposema HAKI YA MUNGU vile!!, au naapa juu ya kaburi la babu yangu, au naapa kwa kichwa changu, au naapa juu ya kiti cha enzi cha Mungu, n.k…

Unaona Vyote hivi ni viapo vinavyokuja kwa shinikizo fulani, au vinavyotokana na kiburi fulani, na mara nyingi viapo vya namna hii vinatoka katika kinywa cha mtu kwa makosa ya kushutumiwa, na si vinginevyo, hivyo watu wa namna hii mara nyingi hata bila kufikira anatoa maneno makuu kama hayo yaliyovuka mipaka, maneno ambayo hawezi hata kuyasimamia, kwamfano anaposema ninaapa kwa kichwa changu, utadhani kama yeye anajua hata hicho kichwa kiliundwaje undwaje, au mwingine anasema ninapa mbele ya kiti cha enzi cha Mungu utadhani yeye na Mungu ni mtu na mdogo wake, na hivyo ana uwezo sawa au unaokaribiana na Mungu n.k.  

Viapo vya namna hii ndivyo Mungu kavikataa kwasababu vinatoka moja kwa moja kwa yule mwovu, Mungu hapendi watu wanaojikweza na wenye viburi..Hivyo mtu akijikuta katika hali kama hiyo ya kushutumiwa hapo maneno yake ndio yanapaswa yawe Ndio ndio, au Siyo siyo.. Basi,   Lakini ikiwa ni kama vitu kama nadhiri, au maagano,au mapatano ya ndoa, au mikataba, au mahakamani..Hayo hayaji kutokana na kushutumiwa au kiburi bali yanakuja kwa lengo la kujiridhisha, kukiri uaminifu wako tu, na si zaidi ya hapo, na hiyo huwa mtu hafikii hatua ya kujikweza au kujihesabia haki, au kujihalalishia mamlaka ya kutendewa alichosema kama imethibitika kuwa hajasimamia alichosema.

Ubarikiwe.


Mada Nyinginezo:

NADHIRI.

KWANINI AWE NI PUNDA NA MWANA-PUNDA?

BWANA ALIMAANISHA NINI KUSEMA JIKANE MWENYEWE?

KUNA HUKUMU ZA AINA NGAPI?

JE! ADAMU ALIWASALIANA NA MUNGU KWA LUGHA IPI PALE BUSTANINI?

LULU YA THAMANI.


 

Rudi Nyumbani:

Print this post

Tamaa yako itakuwa kwa mumeo.Ni tamaa ipi ya Hawa?

SWALI: Ndugu zangu baada ya yule mwanamke Hawa kuvuka mpaka wa maagazo ya Bwana na kula lile tunda alilokatazwa asile:Baada ya Pale tunaona Bwana akimuadhibu kwa adhabu tofauti-tofauti mojawapo ni kuzidishiwa uchungu wa kuzaa. Nataka kufahamu hii adhabu nyingine hapa anaambiwa [TAMAA YAKO ITAKUWA KWA MUMEO.Mwanzo3:16]-Ni tamaa Ipi hiyo Bwana Mungu aliyozungumzia hapo ndugu zangu?


JIBU: Kumbuka jambo la kwanza shetani alilolidadisi kwa mwanamke kwa muda mrefu na kuliona ndani yake ni TAMAA. Tamaa ya kuwa fulani, tamaa ya kuwa juu, tamaa ya kuwa juu ya vitu vyote, tamaa ya kutawala, tamaa ya kudiriki hata kutaka kuwa kama Mungu mwenyewe aliyemuumba..Na ndio maana nyoka alipokuja kumdanganya mwanamke hakumwambia maneno mengine yeyote labda utakuwa mzuri, au utapendwa zaidi au vinginevyo lakini badala yake alimwambia pindi utakapokula tunda utafumbuliwa macho na KUWA KAMA MUNGU!..

 Unaona? “Kuwa kama Mungu”.

Jambo hilo lilimfurahisha sana, pengine labda kwa kujiona yeye aliumbwa wa mwisho zaidi ya viumbe vingine vyote, halafu leo hii anasikia habari za kuwa kama Mungu lilimpa faraja sana..Lakini jambo hilo halikuwa ndani ya Adamu wakati wowote, japo yeye ndiye aliyeumbwa wa kwanza hakuwahi kutamani kuwa kitu fulani zaidi ya pale alipo, hakuwahi kuwa na tamaa ya kuwa juu ya kila kitu japo Mungu alimtawaza juu ya vyote, wala hakuwahi kumtawala mwanamke japo alitoka katika ubavu wake,. Sasa mwanamke alipoasi tu, mambo yakageuka, Ndipo Mungu akamlaani na kumwambia “tamaa yako itakuwa kwa mumeo”..

Hiyo tamaa ya kutaka kuwa juu, hiyo tamaa ya kutaka kuwa kichwa, ya kutaka kutawala sasa imehamishwa na kupelekwa kwa mumeo na matokeo yake, yeye ndiye atakayekutawala. Na ndio maana hayo mambo tunayaona sasa..wanaume wanatawala nyumba zao kwa nguvu, wanataka kujionyesha kuwa wao ni vichwa kati ya wake zao,wanawatiisha wanawake chini, wanataka waonekane kuwa wao ni watawala tu, wao wapo juu tu na wanawake wapo chini. jambo ambalo kiuhalisia halikupaswa kuonyeshwa kwa mwanaume yeyote yule, japo yeye ndiye aliyeumbwa wa kwanza. Umeona hiyo ndiyo laana iliyomkumba mwanamke.. na ndio maana mpaka leo jambo hilo ni Mwiba kwao, hususani kwa wanaume ambao hawajampa Bwana maisha yao, Lakini pia kumbuka Laana sio maagizo..Hatujaagizwa kuwatawala wanawake kwa mabavu katika maandiko.

 Tunanapokuwa wakristo na kumpa Bwana maisha yetu, tunabadilika kutoka katika laana hiyo, na badala yake tunakuwa sio wa kuwaonyesha mabavu yetu kwa wanawake badala yake tunatumia mamlaka yetu KUWAPENDA na kuwajali na kuwatunza kama vile Kristo alivyoonyesha kielelezo kwa kanisa.. mwanaume anapaswa ampende mke wake, kwa Upendo wote…Lakini hilo haliwapi wanaume mamlaka ya kuwatawala wanawake kwa namna isiyopasa bali tuwapende na tusionyeshe tabia kama hizo katika ndoa zetu. 

Waefeso 5:25 “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake;

26 ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno;

27 apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.

28 Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.

29 Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa.

30 Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake”. 

Unaona?. Kristo hatupigi sisi, Kristo hatutesi sisi, Kristo haonyeshi tabia ya kutokutujali sisi, au kutokutupenda sisi..Vivyo hivyo na wanaume wanaomcha Mungu wanapaswa waonyeshe tabia hizo hizo kwa wake zao.. Na wanawake pia wafahamu wasipojinyenyekeza na kujishusha na badala yake kutaka wao wawe vichwa katika nyumba, hawatawaki kuwatii waume zao, wafahamu kuwa laana hiyo haikwepeki juu yao..Watatawaliwa tu kwa mabavu, wapende au wasipende!!.

Ndio maana ya hilo neno Tamaa yako itakuwa kwa mumeo

Ubarikiwe.


Mada nyinginezo:

UZAO WA NYOKA.

MTI WA UZIMA NA MTI WA MAARIFA.

MUNGU WANGU,MBONA UMENIACHA?.

SI SHETANI BALI NI WEWE. (CHAGUA MEMA)

DHAMBI ZINAZOTANGULIA NA ZINAZOFUATA.

MAVAZI YA NDANI NA YA NJE.

UKWELI UNAOPOTOSHA.


Rudi Nyumbani:

Print this post

Je! mtu anaweza kutamka Neno zuri au baya kwa akili zake na likaja kutokea ikiwa si Mungu?

SWALI: Bibi yangu amenihadithia kuna Kaka yake mmoja alimuoa mke na akawa anamtesa na baadaye huyo kaka akaja kumkataa huyo mke baada ya kuzaa naye,Yule mke alipokuwa anarudi kwao Arusha alisema huyo Mume wake ataoa wake 1-12,kisha huyo wa 12 atakuwa kama fisi ammalize.Sasa baba huyo anaendelea kuoa leo mke huyu kesho yule kwasasa wameshafika takribani wake 6..Anaendelea..Swali je! Maneno yale ya yule mwanamke yanasimamiwa na Mungu au na Shetani?.


JIBU: Mtu yoyote akizungumza Neno kwa imani ni lazima litokee, uwezo huo Mungu amemuumbia mwanadamu ndani yake..Mwanadamu anaweza akaumba jambo lolote katika kinywa chake na likaenda kutokea kama lilivyo ikiwa atalifanya kwa imani.   Lakini Imani imegawanyika katika sehemu kuu tatu,..  

1.Imani inayotokana na Mungu, hii inakuja kwa kumwamini Mungu, na Neno lake, kwa mfano mtu anaweza kuamrisha ugonjwa utoke kwa Jina la Yesu, na ugonjwa huo ukatii, anaweza akatamka uzima kwa maiti na maiti ile ikarudia uhai,.Sasa imani ya namna hii ni ile imani ya Ki-Mungu na hii haina mipaka.  

2.Pili kuna imani inayotokana na shetani. Hii ni imani ile ambayo mtu anaweza akawa ni mchawi, au mshirikina au ana pepo fulani, kwa hiyo akizungumza Neno kwa imani, zile nguvu zilizopo ndani yake zinachanganyika na nguvu za giza kuhakikisha kuwa lile jambo linakwenda kutimia..kwa lugha ya sasa ndio unaweza ukasema mtu kalogwa au kafanyiwa jambo fulani la kichawi.  

3.Na tatu kuna imani ya mtu binafsi..hiyo haitokani na shetani wala Mungu..bali inatokana na nia ya mtu mwenyewe..kwamfano unapounyanyua mkono wako juu, hiyo ni roho yako unaunyanyua huo mkono kwa Imani, mkono wako lazima utii na kunyanyuka juu, vinginevyo usingenyanyuka kama maagizo yasingetoka rohoni, unapotaka kupaa mpaka mawingu, mpaka mwezini, ni jambo ambalo haliwezekani kwa namna ya kawaida, japo sasa mwanadamu hana mabawa lakini aliposema ninataka kufika kule juu, alifika kwa imani yake..sio Mungu wala shetani anayefanya hivyo ni wewe(roho yako)..Sasa kwa namna hiyo hiyo pia roho ya mtu inaweza ikazungumza jambo na likatimia vilevile, kama Mungu hataingilia kati..(Mathayo 17:20)   Mara nyingi Baraka za wazazi au laana za wazazi, huwa zinatokana na aina hii ya tatu ya imani, utakuta mzazi hamjui Mungu kabisa, wana hana habari yoyote na Mungu, lakini anaweza akambariki mtoto na mtoto anapata zile Baraka, au akamlaani na laana ile ikamfikia.

Kwahiyo kwa suala kama la huyo mwanamke kama sio Mkristo au kama hatumii nguvu za giza, basi inawezekana kaumizwa na tukio hilo sana na akaamua kuzungumza Neno lile la laana kwa Imani, na kama ni kama Mungu hatoliingilia kati basi ni lazima litimie.   Hivyo tuwe makini na sisi katika vinywa vyote, na ndio maana biblia inatushauri wakai wote tubariki wala tusilaani, maana hatujui maneno yetu tunayotoa yatakwenda kumuathiri yule kwa kiwango gani.(Warumi 12:14)

Ubarikiwe.


Mada Nyinginezo:

NJIA KUU YA KUINGIA KATIKA ULE MJI.

WATU WASIOJIZUIA.

KISASI NI JUU YA BWANA.

CHACHU YA MAFARISAYO NA CHACHU YA HERODE.

MAVAZI YAPASAYO.

DAMU YA ZAKARI BIN BARAKIA.

KWA MUNGU ASIYEJULIKANA.



Rudi Nyumbani:

Print this post

Je, kama hauna ubatizo sahihi hauwezi kuwa na Roho Mtakatifu?

JIBU: Utendaji kazi wa Roho Mtakatifu ni kama ufuatavyo, Mungu anapomchagua mtu aliye dhambini, huwa anamtumia Roho wake mtakatifu kumvuta mtu yule ndio hapo mtu huyo anaanza kusikia kuhukumiwa dhambi zake moyoni, na hatimaye anafikia toba, sasa huyo ni Roho Mtakatifu siku hizo zote anakuwa anamvuta mtu yule, anakuwa anatembea na yule mtu kama rafiki yake wa pembeni, lakini bado hajaingia ndani yake, ni kama mwanamume anapokuwa katika hatua za awali za kumchumbia mwanamke, anakuwa anaweza kuwa karibu naye, kumpa zawadi chache chache, kuzungumza naye maneno mazuri, kumwonyesha vitu vyake n.k, hayo yote mwanamume anayafanya ili tu kumvuta yule mwanamke, lakini bado yule mwanamke sio mali yake mpaka siku atakayoamua kumkubalia na kufunga naye ndoa, ndipo siku hiyo atakuwa milki halali ya yule mwanamume.

 Na Roho Mtakatifu ndio hivyo hivyo, katika hatua za awali, Roho Mtakatifu anaweza akazungumza na mtu, wakati mwingine akampa hata maono,kumfanikisha katika mambo yake n,k lakini akawa bado hajaingia ndani yake, yote hayo Roho Mtakatifu anayafanya ili kuzidi kumshawishi kuielekea njia sahihi ya wokovu……Na kama mtu yule bado atakuwa hajachukua hatua ya kumkaribisha ndani ya moyo wake kwa kutubu kabisa kwa kumaanisha kuacha dhambi zake na kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi, ataendelea kumshiwishi ndani yake mpaka siku atakapokubali.. 

Sasa siku yule mtu yule atakapoamua kubatizwa katika ubatizo sahihi, siku ile ile yule Roho Mtakatifu ambaye alikuwa anatembea naye anaingia ndani yake na kuwa milki halali ya Roho Mtakatifu mwenyewe, wanakuwa ni kama wamefunga ndoa na Roho Mtakatifu, kwasababu ubatizo ndio kibali cha Roho Mtakatifu kuingia ndani ya mtu, ni ishara ya dhambi za mtu kuondolewa kwa damu ya Yesu, na ni muhimu sana na ndio maana Bwana aliyaagiza, sasa baada ya hapo ndipo Roho Mtakatifu anakuja kufanya makao ndani ya yule mtu. Biblia inasema Roho Mtakatifu ndio Muhuri wa Mungu, kama unavyojua barua yoyote isiyokuwa na muhuri halisi hiyo ni batili. Roho Mtakatifu ni kama Pete ya ndoa kwa wanandoa. 

Waefeso 4: 30 “Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi”.

2Wakorintho 1: 22 “..naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu”. 

Na akishaingia ndani ya yule mtu anaanza kupitishwa madarasa mengine ya kiroho zaidi, na huyo mtu shetani hawezi kumpata tena kwasababu ni kama kashakatiwa leseni mbinguni kuwa milki halali ya Roho mtakatifu, Na pia maandiko yanasema katika ….Warumi 8:9 “……Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.”…kwa lugha nyepesi mtu yoyote ambaye hajafunga ndoa na Roho Mtakatifu kwa njia ya UBATIZO SAHIHI huyo sio wake, haijalishi Roho Mtakatifu anamwonyesha maono, anazungumza naye n.k bado huyo sio wake. 

Mwingine atasema mbona wapo ambao wamebatizwa huo ubatizo sahihi lakini bado ni waovu? je! wewe unamkosoa Bwana wako aliyekupa hayo maagizo kwamba alichokisema hakina umuhimu sana katika kazi ya ukombozi?..Mbona husemi hivyo kwa mitume waliobatizwa kwa njia hiyo?.. Nakushauri usiwaangalie wanadamu kama ni kipimo cha wokovu wako, hujui mtu huyo aliuendea ubatizo kwa kidini tu, au kuwaridhisha wanadamu, au kwa faida zake mwenyewe..Lakini fahamu kuwa Ubatizo sahihi wafaa sana kwa wokovu wako mwenyewe. 

Ubarikiwe.


Mada nyinginezo:

JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?

HATUA ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA KUTUONGOZA.

NITAIFAHAMU VIPI KARAMA YANGU?

NINI MAANA YA KUTOKA KATIKA MADHEHEBU?

ROHO ZILIZO CHINI YA MADHABAHU:

MKATAE SHETANI NA MAWAZO YAKE YA KIBINADAMU.

SIKU YA TAABU YA YAKOBO.


 

Rudi Nyumbani:

Print this post

Je! Mungu anaupendeleo kwa wanaume zaidi ya wanawake?

JIBU: Ndivyo inavyodhaniwa na wengi, hususani linaposomwa lile andiko lisemalo

1Timotheo 2:13 “Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye.”

Maneno hayo yanathibitisha kuwa Adamu ndiye aliyepewa kipaumbele cha kwanza kuliko mwanamke..   Lakini ifahamike kuwa Mungu ni Mungu wa utaratibu. Tunapotaka wote tufanane, wote tuje kwa wakati mmoja, na wote tuwe na mamlaka yanayofanana, basi maisha yangekuwa hayana maana. Hivyo Ili Mungu kutimiza kusudi lake, na kuweka mambo yote katika utaratibu ilimpasa aweke ngazi lakini hilo halimaanishi kuwa mmoja ni bora zaidi ya mwingine..Kwasababu kama tukichukulia kigezo cha kuumbwa kwa mwanaume kwanza zaidi ya mwanamke ndio tiketi..

Kumbuka pia wanyama na mimea yote iliumbwa kwanza kabla hata ya Adamu kuumbwa..Sasa hapo tuseme wanyama wamepewa upendeleo mkubwa zaidi ya sisi?.   Jibu ni hapana, lakini tatizo kubwa linakuja pale wanaume wanapotaka kuwa kama wanawake na wanawake wanapotaka kuwa kama wanaume, katika utendaji kazi wao Mungu aliowawekea, hususani pale katika suala la UONGOZI katika kanisa, na nyumbani. Biblia inasema je! MAUMBILE NAYO HAYATUFUNDISHI?(1Wakorintho 11:14).

Tujifunze katika maumbile ya kila mmoja, jinsi alivyoumbwa, ili tupate kulijua kusudi la Mungu katikati yetu, jaribu kufikiria suala la uleleaji wa mtoto, baba hata aweze kufanya shughuli zote za ndani namna gani, hata aonyeshe upendo kwa mtoto mkuu dizaini gani bado hataweza kumtolea mtoto chakula mwilini mwake.   Hiyo shughuli nzito na jukumu la kipekee namna hiyo ameumbiwa mwanamke tu (mama). Shughuli nzito ya kumlea akiwa kijusi tumboni, mpaka kiumbe kipya duniani na changamoto zake zote, wakati mwingine hata wengine kupoteza maisha yao kwa changamoto hizo, ni mama peke yake ndiyo aliyeumbiwa, mwanaume hata awe shujaa kiasi gani,..akijaribu kufanya hivyo atakuwa anapoteza muda wake…..hawezi kufanya hivyo hata atamanije!!….Kadhalika kazi ya ulinzi, uangalizi wa nyumba, kazi za kutumia nguvu nyingi, mwanamke hata akijitahidi vipi kwenda kubeba viroba vya michanga atakuwa anajiumiza tu mwenyewe.

Shughuli hizo na taabu hizo Mungu kamuumbia mwanaume. Japo zipo zinazofanywa na wote hilo lipo wazi, lakini tatizo linakuja ni pale kila jambo, ambalo mwanaume ametawazwa na Mungu kulifanya mwanamke naye anataka kulifanya..asilimia 50 kwa 50..Na hilo ndio limekuwa tatizo kubwa.Ambao ni mpango mkamilifu wa shetani, mwanaume anavaa suruali mwanamke naye anataka kuvaa suruali, mwanaume anavaa kaptura mwanamke naye anataka kuvaa kaptura, mwanaume ananyoa nyewe zake, mwanamke naye ananyoa kipara afanane na mwanaume.   Kwa mfano tukirudi kwenye kanisa:

Biblia inasema

1Wakorintho 14.34 “Wanawake na wanyamaze katika kanisa, maana hawana ruhusa kunena bali watii, kama vile inenavyo torati nayo..”Na pia inasema 1Timetheo 2: 12 “Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu”.  

Utakuta Baadhi yao wanaona kama Mungu kawaweka nyuma katika kazi yake, na hivyo wanaamua kuyahalifu kwa makusudi maagizo ya Mungu na kwenda kufundisha makanisani, na kuwatawala waume zao. Wakidhani kuwa ndio wanajenga, kumbe hawajui kuwa wanabomoa. Hekima ya Mungu ni kubwa zaidi ya mwanadamu, akisema hivi anamaanisha hivyo, yeye anajua ni jinsi gani mwanaume atatenda vizuri katika eneo hilo zaidi ya mwanamke na ndio maana akasema hivyo..  

Lakini kwa anayemwona Mungu hapo kakosea kuweka ngazi, na mamlaka katika kazi yake mwenyewe aliyoibuni duniani biblia ipo wazi yanasema hivi:

1Wakorintho 14: 37 “Mtu akijiona kuwa ni nabii au mtu wa rohoni, na ayatambue hayo ninayowaandikia, ya kwamba ni maagizo ya Bwana. 38 LAKINI MTU AKIWA MJINGA, NA AWE MJINGA”.  

Baki katika nafasi uliyoitiwa, Biblia haina mfumo dume hapana bali ina utaratifu. Na utaratibu huo ni Mungu mwenyewe ndio kauweka kulingana na jinsia.  

Ubarikiwe.


Mada Nyinginezo:

NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA

RABONI!

MARIAMU

UZAO WAKO UTAMILIKI MALANGO YA KUZIMU;

NJIA KUU YA KUINGIA KATIKA ULE MJI.

UTAWALA WA MIAKA 1000.

UNYAKUO.


 

Rudi Nyumbani:

Print this post

Mimi ni askari magereza, na nimeamuriwa kumnyonga mfungwa aliyekuwa mwalifu kwa kosa la uuaji. Je! kufanya hivyo ninatenda dhambi?.

JIBU: Tunapaswa tufahamu vizuri utumishi wa Mungu jinsi ulivyogawanyika ili tusikose maarifa tukidhani ya kuwa Mungu anatenda kazi sehemu moja tu kanisa, mahali pengine hayupo, wala hajihusishi na mambo hayo. Tukisoma biblia tunaona Mungu anao watumishi wa aina mbili: 1) Watumishi wa ufalme wa mbinguni: 2) Watumishi wa kidunia:

 Watumishi wa ufalme wa mbinguni: Ni wale wote wanaofanya kazi zihusuzo ufalme wa mbinguni tu, kuhakikisha habari njema zinawafikia watu wengi kwa njia ya injili, kulichunga kundi la Mungu wakati wote, kulihudumia kwa kila namna kupitia karama za Roho ambazo Mungu aliziachia katika kanisa..Na mfano wa watumishi hawa tunawajua ni wachungaji, waalimu, mitume, manabii, na wainjilisti, mashemasi, karama za maombezi, lugha, uponyaji, Neno la Hekima, Maarifa n.k..

 Lakini Mfano wa watumishi wa kidunia, ni wale ambao wameamuriwa na Mungu kutimiza kusudi lake maalumu hapa duniani. Na mfano wa hao ni Serikali na taasisi zake zote zilizo chini yake..

Na Wengine mfano, ni mashirika mengine yote yasiyo ya Umma, yanayohusika na kutoa huduma za kijamii kwa watu. Hawa wote wanatimiza kusudi maalumu la Mungu lakini sio kusudi kamilifu lile ambalo alilitaka kila mmoja alifikie. Hivyo Mungu huwa anatumia vyombo hivi vyote viwili kwa aidha kubariki, au kijilipizia kisasi, kwa walio waovu na walio wema. Sasa kama imetokea Mfano mtu anayo kiu ya kuijua haki, anapenda kutafuta kujua masuala ya Mungu kwa bidii hata kama yeye sio mkristo..Jambo Mungu analofanya ni kumsaidia kwa kumpelekea huyu mtu mtumishi wake wa ufalme wa mbinguni ili amfikishie huduma hiyo aliyokuwa anaihitaji mahali pale alipo.

Mfano tunamwona Kornelio katika biblia, yeye hakuwahi hata siku moja kumfahamu YESU, lakini kwa jinsi alivyokuwa anabidii katika kumtafuta Mungu na kutenda haki na kutoa sadaka nyingi, basi Petro alitumwa kwake kwenda kumshuhudia habari njema za YESU KRISTO (Matendo 10), Mfano wa mwingine kama huo tunaona kwa yule Mkushi aliyetoka Afrika kwenda kuhiji Yerusalemu, lakini alipokuwa njiana anarudi nchini kwake huku anasoma torati mahali palipoandikwa habari za YESU lakini katika fumbo. Mungu aliona kiu yake hivyo kutokana na bidii yake kwa Mungu ya kutaka kujua, basi Mungu akamtumia Mtumishi wake Filipo aende kumwelezea habari zile kwa ufasaha zaidi. 

Vivyo hivyo mtoto wa Mungu anapomwomba Mungu ampe riziki za dunia, hawezi kwenda kumtafutia kazi kanisani kwasababu makanisa sio taasisi za kutengeneza fedha, au sio sehemu za biashara, Bwana Mungu atakachokifanya ni kuhakikisha anamtafutia nafasi nzuri katika taasisi Fulani husika, labda wizara Fulani ambapo pengine atamweka chini ya ma-manager Fulani wa serikali..ambao watamwajiri na kumpatia mshahara mzuri..sasa hao ma-manager ni watumishi wa Mungu kwa Yule mtoto wa Mungu anayetafuta riziki za kidunia.

 Vivyo hivyo mtoto wa Mungu anapohitaji, maji safi au umeme mzuri, Bwana Mungu hawezi kumpelekea mchungaji au nabii kumpatia huduma hiyo, atampelekea watumishi wake wengine wanaohusika na mambo hayo kama tanesco na Idara ya Maji, watahakikisha wanamfikishia maji na umeme mpaka chumbani kwake anapolala. 

Hali Kadhalika pale mtu anapokuwa mwovu, anapotenda mabaya, anapomfanyia Mungu makosa kwa makusudi wapo vile vile watumishi Mungu aliowaandaa kwa ajili ya shughuli kama hizo ili kujilipizia kisasi kwake, na mojawapo wa hao watumishi wa Mungu ndio hivyo vyombo vya dola, mtu anapoua, unapoiba, unapobaka, unapokula rushwa,. Asidhani kuwa Mungu atasema naye kwa upole kama asemavyo naye kanisani, Na ndio hapo anakamatwa na kutiwa gerezani na wakati mwingine kuhukumiwa kunyongwa kama atakuwa anastahili adhabu hiyo,. Sasa Kwa namna ya kawaida unaweza kusema ni hawa watu wamemtendea hivyo, lakini kiuhalisia sio wao bali ni Mungu ndiye aliyemlipiza kisasa kwa makosa yake mwenyewe. Na ndio maana biblia inasema:

Warumi 13:1 “Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu.

2 Hivyo amwasiye MWENYE MAMLAKA HUSHINDANA NA AGIZO LA MUNGU; NAO WASHINDANAO WATAJIPATIA HUKUMU.

3 Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake;

4 kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu kwako kwa ajili ya mema. LAKINI UFANYAPO MABAYA, OGOPA; kwa maana hauchukui upanga bure; kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, amlipizaye kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu.

5 Kwa hiyo ni lazima kutii, si kwa sababu ya ile ghadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri.

6 Kwa sababu hiyo tena mwalipa kodi; kwa kuwa wao ni wahudumu wa Mungu, wakidumu katika kazi iyo hiyo”.

Unaona hapo? Sasa tukirudi kwenye swali lililoulizwa linalosema: Mimi ni askari magereza, na nimeamuriwa kumnyonga mfungwa aliyekuwa mwalifu kwa kosa la uuaji. Je! kufanya hivyo ninatenda dhambi?. Jibu ni kuwa “hutendi dhambi” .

Kwani wewe umeamuriwa kutimiza wajibu wako, kwa kosa ambalo lilishaonekana limefanywa na mtu mwenyewe, mpaka kufikia hapo ni Mungu mwenyewe ameruhusu. kwasababu maagizo hayo hayajatoka kwako bali yametoka juu, lakini hutahesabiwa thawabu katika hilo mfano wa wale wanaomtumikia Mungu kwa habari ya kuokoa roho za watu na sio kuangamiza,..Na ndio maana ni vema pia kujua pale unapokuwa mkristo, ufahamu kazi unayotaka kuifanya ujue na majukumu yake yatakavyokuwa, Sio kila kazi itampa mkristo amani kuifanya, japo hata afanyapo hatahesabiwa makosa.

Uamuzi ni wako binafsi. Hivyo kabla hujaamua kujiingiza kwenye utumishi wowote piga kwanza faida zake na hasara zake. Je! Utumishi uufanyao ni ule utimizao mapenzi makamilifu ya Mungu au ni ule wa kisasi cha Mungu, kabla hujawa mwanajeshi jitafakari mara mbili mbili, kabla hujawa polisi jitafakari mara mbili mbili na daktari vivyo hivyo na kazi nyingine zote.

Ubarikiwe.


Mada Nyinginezo:

MAWE YALIYOKWISHA KUCHONGWA MACHIMBONI.

MNARA WA BABELI

WAFALME WATOKAO MAWIO YA JUA.

KUCHEZA KARATA NI SAHIHI KWA MTU ALIYE MKRITO?

KIFAA BORA CHA MATUMIZI.

WALIO NA HEKIMA NDIO WATAKAOELEWA.


 

Rudi Nyumbani:

Print this post

Je! Kufanya masturbation (Punyeto) ni dhambi?

Punyeto ni dhambi?..Na je! Kuoa ni suluhisho la kuzuia tamaa kama biblia inavyosema katika 1 Wakorintho 7:9?.


JIBU: Bwana Yesu alisema amtazamaye mwanamke kwa kumtamani amekwisha kuzini naye nafsini mwake. Sentensi hiyo inaonyesha kuwa dhambi haianzii nje ya mwili bali inaanzia moyoni, hivyo zinaa pia inaanzia moyoni, ikishafanyika moyoni ndipo inatoka nje, kwahiyo chochote kinachofanyika mwilini ni matokeo ya kitu kilichofanyika tayari rohoni, hivyo uasherati, masturbation (punyeto), utazamaji wa pornography hayo yote ni matokeo ya uasherati ambao tayari yalishafanyika ndani ya moyo wa mtu.  

Ndio masturbation ni dhambi. Na suluhisho pekee la kuikwepa hiyo dhambi ni kumkabidhisha Bwana Yesu maisha yako ki-kweli kweli, na kudhamiria kuanza maisha mapya katika Kristo, na kuamua KUACHA!! Wengi wanatafuta kuombewa waache kutazama pornography au kufanya masturbation lakini hawajadhamiria kuamua kuacha hivyo vitu,..wanasubiria miujiza ishuke wajikute wameacha na huku bado mioyo yao inaelekea kwenye zinaa…Nataka nikuambie ndugu yangu unayemtafuta Mungu,Hakuna maombi yoyote ya kuondoa hicho kitu ndani ya mtu, ili hivyo vitu viondoke ni kuamua kwanza kuchukua uamuzi wa kuacha hayo mambo ndipo Bwana anakuongezea UWEZO wa kushinda hayo mambo,. Kumbuka na Biblia inasema waasherati wote sehemu yao ni katika ziwa la moto.   Na pia kuhusu kuoa biblia imeweka wazi katika kitabu cha

1 Wakorintho7 :1 “Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke.2 Lakini kwa sababu ya ZINAA kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe”.

Ukisoma kwa makini huo mstari wa 2 anasema kwasababu ya ZINAA kila mtu mwanamume awe na mke wake mwenyewe…sio kwasababu ya KUEPUKA TAMAA…bali kwasababu ya ZINAA…na zinaa maana yake ni kufanya mapenzi nje ya ndoa au kabla ya ndoa, Hii ikiwa na maana kuwa, kuwa na mke hakumzuii mtu kulipuka tamaa…kama tabia ya mtu ni kutamani! Hiyo tabia hataiacha hata akioa au akiolewa..pengine ataepuka zinaa tu baada ya kuoa/kuolewa kwasababu atakuwa na mke/mume wake ndani!…. Lakini tama ya kutazama wanawake wengine itakuwa palepale kama atakuwa hajabadilishwa.  

Kwahiyo suluhisho pekee la kuzuia tamaa kwa aliyeoa au asiyeoa, ni kumkabidhi Kristo maisha kwanza, na kukusudia kuacha dhambi, (kumbuka Mungu hawezi kumsaidia mtu ambaye hajakusudia kwa dhati kuacha kile kitu kibaya anachokifanya)..mtu akishakusudia kuacha kwa vitendo tabia ya kutamani, kujitenga na vichochezi vyote vya uasherati, muvi zenye vimelea vya ngono ndani yake, pornography, matusi, maneno ya mizaha yasiyokuwa na maana, ndipo Roho Mtakatifu anakuja juu yake na kumsaidia na hivyo anajikuta vile vitu havimsumbui tena maishani mwake. Tofauti na yule anayetamani tu kuacha lakini haonyeshi jitihada yoyote ya kutaka hivyo vitu viondoke ndani yake.  

Ubarikiwe!


 

Mada Nyinginezo:

JE! KUSHIRIKI AU KUJIHUSISHA KWENYE MICHEZO NI DHAMBI?

JE! KUBET NI DHAMBI?

JE! ULEVI NI DHAMBI?.

NIFANYE NINI ILI NIIKWEPE HUKUMU.

MADHARA YA DHAMBI YA UASHERATI.

NITASHINDAJE HALI YA KUUMIZWA NA MANENO YA WATU!


Rudi Nyumbani:

Print this post

Mti wa MLOZI alioonyeshwa nabii Yeremia 1:12 tafsiri yake ni nini?

JIBU: Ubarikiwe ndugu…Mlozi ni mti fulani, unaositawi sana sana huko mashariki ya kati (Lebanoni, Israeli, Palestina n.k.).Jina lake kwa kiyahudi unaitwa “SHAKEI” na tafsiri yake ni KUTAZAMA/KUANGALIA...Kwahiyo Yeremia kuonyeshwa pale Mti wa Mlozi ni lugha tu ya picha anayoonyesha kwamba Bwana ANATAZAMA, na je! anatazama nini?..Anatazama NENO lake ili alitimize alilolinena juu ya Israeli..na ndio maana ukisoma hapo anasema..

Yeremia 1: 11 Tena neno la Bwana likanijia, kusema, Yeremia, waona nini? Nikasema, Naona ufito wa mlozi. 12 Ndipo Bwana akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize…

Kumbuka pia Mungu huwa anatazama Neno lake ili alitimize kwa namna zote, Hivyo kama ni jema, ni lazima alitimize, na kama ni baya juu ya watu wake ni lazima alitimize pia!.Kote kote. Lakini tunaona Israeli walikuwa waasi kwa Mungu tangu zamani, ukisoma katika habari za wafalme utaona jambo hilo, jinsi walivyokuwa wanamuasi Mungu mpaka akawaapia kuwa wataenda utumwani tena Babeli, kwa vinywa vya manabii wake waliotangulia kabla ya Yeremia mfano Isaya n.k. Na ndio maana hapo Yeremia anaonyeshwa kama UFITO(FIMBO) tu, ya mlozi, Ikimaanisha kuwa Mungu analitazama NENO lake, na kulitimiza juu yao kama ADHABU na sio BARAKA...

kwasababu FIMBO ni kwaajili ya kuadhibu siku zote tunajua hilo. Hivyo Ukizidi kuendelea mistari inayofuata ndio utaona mabaya yote Mungu aliyoyanena juu ya yao yalikuja kutimia ikiwemo kuchukuliwa utamwani Babeli.

ubarikiwe


Mada Nyinginezo:

FIMBO YA HARUNI!

UFUNUO: MLANGO WA 1

SANDUKU LA AGANO LILIKUWA LINAWAKILISHA NINI KATIKA AGANO JIPYA?

NI RAHISI KWA NGAMIA KUPENYA KATIKA TUNDU LA SINDANO, JE! NI SINDANO IPI HIYO INAYOZUNGUMZIWA?

SWALI LA KUJIULIZA!

RACA

AMIN! NAWAAMBIA KIZAZI HIKI HAKITAPITA

USIPIGE MATEKE MCHOKOO!


Rudi Nyumbani:

Print this post

Tofauti kati ya Myunani, Farisayo na Sadukayo ni ipi?

JIBU: Mafarisayo na Msadukayo chimbuko lao ni moja dini zao zimeegemea katika Torati ya Musa, wote hawaamini maagizo mengine nje ya torati isipokuwa tofauti inakuja katika kuamini kiama cha wafu.. Mafarisayo wanaamini kuwa kuna kiama cha wafu (yaani maisha baada ya kufa, wanaamini yote yaliyoandikwa katika torati hata tumaini ya kuja kwa Masihi duniani) lakini masadukayo hawaamini kama kuna kufufuliwa kwa wafu, wanaamini kuwa mtu akishakufa, amekufa hakuna chochote baada ya hapo, wala hakuna malaika wala ulimwengu wa roho wala mbingu. 

Ukisoma Mathayo 22:24-34 utaona Bwana Yesu akiwajibu hao mafarisayo kuhusu mitazamao wao hafifu ya maandiko Na kuwaambia kuwa Mungu asingesema yeye ni Mungu wa Ibrahimu, na Isaya na Yakobo kama watu hao ni wafu sasa. Kwasababu siku zote Mungu si Mungu wa wao bali wa wanaoishi..Hivyo Neno hilo linathibitisha kuwa kiama kipo. Ukisoma tena Matendo 23 Utaona Mtume Paulo akiyagonganisha madhehebu hayo mawili.

Matendo 23: 6 “Paulo alipotambua ya kuwa sehemu moja ni Masadukayo, na sehemu ya pili ni Mafarisayo, akapaza sauti yake katika ile baraza, Ndugu zangu, mimi ni Farisayo mwana wa Farisayo; mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu.

7 Alipokwisha kunena hayo palikuwa na mashindano baina ya Mafarisayo na Masadukayo, mkutano ukafarakana.

8 Kwa maana Masadukayo husema ya kwamba hakuna kiyama wala malaika wala roho; bali Mafarisayo hukiri yote.

9 Pakawa na makelele mengi. Waandishi wengine wa upande wa Mafarisayo wakasimama, wakateta, wakisema, Hatuoni uovu wo wote katika mtu huyu; bali ikiwa roho au malaika amesemanaye, ni nini?

10 Ugomvi mkubwa ulipotokea, yule jemadari akachelea Paulo asije akararuliwa nao, akaamuruaskari washuke na kumwondoa kwa nguvu mikononi mwao, na kumleta ndani ya ngome.”

Hivyo kwa maandiko hayo utapata kuelewa tofauti ya watu hawa ipo wapi.. MYUNANI: Sio dini au imani, bali ni watu wa taifa la uyunani, kwasasa ni Ugiriki.Hivyo katika agano jipya mahali popote anapotajwa myunani, linalenga watu wa aina mbili, aina ya kwanza ni aidha wayahudi wanaotokea katika nchi za wayunani, na hivyo wanajulikana kama wayunani lakini kiasili ni wayahudi, kwa mfano wale watu waliotaka kumwona Bwana zamani zile ni wayahudi lakini sio wa kuzaliwa Israeli. tunasoma:.

 Yohana 12:20 “Palikuwa na WAYUNANI kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu.

21 Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya,wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu “

Unaona? Kadhalika pia wale watu waliokuwa Yerusalemu siku ile ya Pentekoste, (Matendo 2) wakishangaa matendo makuu ya Mungu, biblia inasema walikuwa Warparthi na Wamedi na Waelami,n.k. wote hawa hawakuwa watu wa mataifa mengine (yaani watu wasio wayahudi) hapana bali walikuwa ni Wayahudi waliotoka katika hayo mataifa yaliyotajwa hapo,Na aina ya pili: ni Wayunani ambao asili yao ni Uyunani kabisa, watu wa mataifa. Mfano tunaweza kumwona mwanamke huyu aliyezungumziwa hapa ni myunani lakini hana uyahudi wowote ndani yake:

 Marko 7:24 “Akaondoka huko, akaenda zake hata mipaka ya Tiro na Sidoni. Akaingia katika nyumba,akataka isijulikane na mtu; lakini hakuweza kusitirika.

25 Ila mara mwanamke, ambaye binti yake yuna pepo mchafu, alisikia habari zake,akajaakamwangukia miguuni pake.

26 Na yule mwanamke ni Myunani, kabila yake ni Msirofoinike. Akamwomba amtoe pepo katikabinti yake.

27 Akamwambia, Waache watoto washibe kwanza; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto,na kuwatupia mbwa

28 Naye akajibu, akamwambia, Naam, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hulamakombo ya watoto.

29 Akamwambia, Kwa sababu ya neno hilo, enenda zako, pepo amemtoka binti yako.

30 Akaenda zake nyumbani kwake, akamkuta yule kijana amelazwa kitandani, na yule pepo amekwisha kumtoka.”

 Kadhalika tunaona watenda kazi wa Mungu wengine kama Tito, mwanafunzi wa Paulo (Wagalatia 2:3).

Na Timotheo (Matendo 16:1) hawa wote biblia inawataja kama ni Wayunani, na sio wayahudi. 

Ubarikiwe sana.


Mada Nyinginezo:

MATOWASHI NI WAKINA NANI?

WANA WA MAJOKA.

NIFANYAJE ILI NIJUE KUWA UAMUZI NINAOKWENDA KUCHAGUA KUFANYA NI MAPENZI YA MUNGU?

USIWE SABABU YA WATU KUMKUFURU MUNGU.

MUNGU WANGU,MBONA UMENIACHA?

MASHEHE NI WAKINA NANI?


 

Rudi Nyumbani:

Print this post

Je!Mungu anaweza kuleta majibu kupitia nguvu za giza maana nashindwa Kuelewa ninaposoma habari za Mfalme Sauli kupata majibu kwa mwanamke mchawi?

JIBU:Shalom!. Ni vizuri tuifahamu sifa ya Mungu, ili tusiishie tu kumchukulia yeye yupo mbinguni kaketi kwenye kiti cha Enzi, mahali pengine popote palipo pachafu hawezi kuingia wala kukanyaga, wala kujua kinachoendelea huko.

Zaburi 139:7 “Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? 8 Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko. 9 Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari; 10 Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume utanishika. 11 Kama nikisema, Hakika giza litanifunika, Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku; 12 Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana; Giza na mwanga kwako ni sawasawa.”

Na ndio maana ukisoma ule mstari ule mstari wa 6 juu yake kidogo unasema hivi.. “Maarifa hayo ni ya ajabu, yanishinda mimi, Hayadirikiki, siwezi kuyafikia.” Hii Ikiwa na maana kuwa uweza wa Mungu hautambulikani, na njia zake hazitafutikani hata tukijaribu kumtafakari Mungu vipi, hatuwezi kumpima kwa akili zetu hizi za kibinadamu kwa jinsi alivyoenea kila mahali.   Hiyo Inatuthibitishia kuwa Mungu pekee ndiye anayeweza kuwepo kila mahali, na ndio pekee mwenye funguo za makao ya viumbe vyote ulimwenguni,..hakuna mwingine yeyote mwenye uwezo huo.Kama tunavyofahamu..

Zipo falme Kuu tatu zinazotembea katika duara lote la uumbaji wa Mungu, Ufalme wa kwanza ni ufalme wa Mungu mwenyewe ambao huo upo katika ulimwengu wa roho, na ufalme wa pili ni ufalme wa giza nao pia upo katika ulimwengu wa roho, na ufalme ya tatu ni ufalme ya wanadamu ambao ndio huu tunaouona katika mwili na ndio huu tunaoishi mimi mimi na wewe.   Na falme hizi zote kila mmoja inayo utendaji kazi wake wenyewe, na nguvu zake, na mamlaka yake yenyewe, na kama zilivyojipanga ile Falme ya kwanza ndiyo yenye nguvu zaidi mbali na nyingine zote ndiyo ya Mungu wetu, kisha hapo chini unafuata ufalme wa giza ambao ndio shetani anaumiliki, na wa mwisho ndio huu wa kwetu sisi wanadamu.   Sasa Yule mwenye nguvu zaidi ndiye mwenye uwezo wa kuingia na kutoka kwenye ufalme wa chini yake.

Kwa mfano ufalme wa mbinguni ambao ndio wa Mungu wetu, unaouwezo wa kuamua lolote juu hizi falme mbili za chini, unaouwezo wa kuzitumia au kuziamurisha lolote la kufanya, zinaweza kutumiwa pia kutimiza kusudi Fulani la Mungu kwa muda kwa kipindi fulani. Vivyo hivyo na ufalme wa pili ambao ni wa giza unao nguvu wa kuumurisha ufalme wa chini yake (yaani sisi tunaouishi), kamwe mwanadamu hata afanyaje hawezi kuushinda ufalme wa ibilisi kama hana Mungu, atatawaliwa tu na falme hizo mbili, na ndio maana shetani naye alikuwa na ujasiri wa kujigamba mbele ya Yesu na kumwambia hivi vyote ni vyangu nami humpa yeyote nimtakaye na huku sisi tunajua kuwa dunia na vyote viijazavyo ni mali ya Mungu. Unadhani shetani alikuwa anajisifia bure?, hapana kwasababu ufalme wake ni kweli una nguvu zaidi ya ufalme wa wanadamu..

Hivyo alikuwa na haki ya kusema vile. Hali kadhalika ule ufalme ulio dhaifu hauwezi kuelewa mambo yanayoendelea katika ufalme ulio juu yake wenye nguvu hata uwe na bidii kiasi gani.   Hivyo ufalme wa ibilisi hauwezi kujua lolote linaloendelea katika ufalme wa Mungu, hata atafute kiasi gani hawezi kujua chochote.   Sasa Tukirudi kwenye swali lililoulizwa Je!Mungu anaweza kuleta majibu kupitia nguvu za giza maana nashindwa Kuelewa ninaposoma habari za mfalme Sauli .kupata majibu kwa mwanamke .mwenye pepo.nisaidie hapo.   Jibu ni Ndio Mungu anaoweza kuleta majibu sio tu kupitia ufalme wa giza, bali pia kupitia ufalme wa kibinadamu, Kwasababu yeye yupo mahali popote,.kama hapo juu anavyosema

Zaburi 139:8 “Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.9 Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari; 10 Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume utanishika. ”  

Lakini yeye kuwa uwezo huo wa kupitisha ujumbe wake kupitia falme hizo zote mbili haimaanishi kuwa unampendeza au umemfikia Mungu kinyume chake ni hukumu inafuata…Pia hiyo haimaanishi kuwa mtu anapokwenda kwa mganga kumtafuta Mungu atamwona, kumbuka wote wanaokwenda kwa waganga hawana lengo la kumtafuta Mungu, hakuna hata mmoja, huwa wanakwenda kutafuta njia za kutatuliwa matatizo yao na wala sio kumtafuta Mungu,kama wangekuwa na lengo la kumtafuta Mungu wasingedhubutu kutumia njia hizo ambazo wanajua kabisa Mungu amezikataa. Hata Sauli mwenyewe hakwenda kumtafuta Mungu kule kwa mganga,bali samweli amsaidie kutatua ufumbuzi wa shida iliyo mbele yake..  

Na ndio huko huko Mungu wakati mwingine anatokea kuzungumza na watu, na ikishafika hatua kama hiyo basi ujue kuwa kinachofuata ni hukumu tu kwa kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu.   Hata wachawi wenyewe huwa wanakutana na sauti ya Mungu huko huko katika shughuli zao zikiwaonya matendo yao, lakini hawawezi kusema siri hizo wanazo wao wenyewe, wale ambao wanakuja kuokolewa ukiwauliza watakuthibitishia hilo kwamba kuna wakati Fulani ambao Mungu alishawahi kuwaonya.  

Sio tu Sauli alikwenda kwa waganga..Yupo ambaye alikuwa ni mchawi kabisa biblia inamtaja naye ni Balaamu, nabii wa uongo, huyu naye Mungu alikuwa anazungumza naye akimwonya asiwalaani Israeli, lakini yeye hakusikia sauti ile ya Mungu akatia ukwazo kwa wana wa Israeli, Mungu baadaye akaja kumuua.   Hivyo huo uwezo Mungu anao,lakini sio njia Mungu anayoitumia kuleta majibu ya maombi wa watu. Njia yoyote nje ya Yesu Kristo, yaani njia ya sanamu, njia ya uganga, njia ya sayansi, hakuna hata moja yenyewe uwezo wa kufikisha maombi kwa Mungu, wala usijaribu kufanya hivyo utaangukia hukumu, isiyoponyeka. japo Mungu anaweza kuzitumia hizo kuleta majibu kwa watu tena majibu yaambatanayo na hukumu wala sio jambo jema.

Ubarikiwe.


Mada Nyinginezo:

JINSI WATU WANAVYOZAMA KATIKA USHIRIKINA NA UCHAWI.

JE! NI KWELI KUNA VIUMBE VINAVYOISHI SAYARI NYINGINE (ALIENS)?

BWANA YESU ALIMAANISHA NINI ALIPOSEMA; MAFARISAYO HUPANUA HIRIZI ZAO, NA KUONGEZA MATAMVUA YAO?

HATARI YA KUTOKUITAFAKARI BIBLIA VIZURI?

EPUKA KUTOA UDHURU.

MSTARI HUU UNA MAANA GANI? “TUPA CHAKULA CHAKO USONI PA MAJI; MAANA UTAKIONA BAADA YA SIKU NYINGI”. (MHUBIRI 11:1)


Rudi Nyumbani:

Print this post