Category Archive Home

MWAMUZI WA KWELI:

Shalom mtu wa Mungu, ni siku nyingine tumepewa neema ya kuishi, Hivyo karibu kwa pamoja tushiriki kujifunza maneno ya uzima, ambayo ndio msingi hasaa wa sisi kuwa hapa duniani.

Tukisoma biblia tunaona jinsi Mungu alivyowanyanyua waamuzi wengi tofauti tofauti kwa udhihirisho tofauti tofauti katika vipindi vya awali kabisa baada ya wana wa Israeli kutoka katika nchi ya Misri,Na Mungu aliwanyanyua kwa lengo lile lile moja la kuwarejesha watoto wake katika njia sahihi, kuwarejesha mahali ambapo walipaswa wawepo.Hivyo kitu alichokifanya Mungu kwa wakati ule ni kumtia “mafuta ya kipekee” mtu mmoja ili aende kushughulika ipasavyo na yule adui yao mtekeaji, na mwisho wa siku wanapata ukombozi wao kuwa yule mtu Mungu aliyemtia mafuta..

Kwa mfano tunaweza kumwona Musa, Mafuta yaliyokuwa juu ya Musa ni ISHARA NA MIUJIZA na yale MAPIGO. Hivyo kwa kupitia huduma hiyo aliweza kukishusha kiburi cha Farao na Misri nzima na hivyo wakaweza kuwaacha wana wa Israeli waende katika nchi yao Mungu aliyokusudia wafike ili wakamtumikie Mungu. Lakini japo ishara zile kubwa zilionekana kwa mkono wa Musa bado watu wale hawakupata ukombozi mkamilifu ambao ungewafanya wawe huru kabisa kabisa mbali na maadui zao wote.

Tunaona pia wakati mwingine Mungu aliwanyanyanyulia mwamuzi mwingine baada ya kutumikishwa na maadui zao kwa muda mrefu kutokana na dhambi zao wenyewe ndipo Mungu akawaletea Gidioni kwa Roho(Mafuta) ya ushujaa ili kuwaamua kwa upanga,(Waamuzi 6)..Ni kweli mwisho wa siku walipata ukombozi, lakini ukombozi ule ulikuwa ni wa kitambo tu, baada ya muda kidogo watu walirejea katika dhambi zao za kumwasi Mungu.

Hali kadhalika tunaona wakati mwingine Mungu alimtia mafuta Samsoni katika upako wa “Nguvu za kibinadamu”…Hivyo kwa nguvu zile za kimwili aliweza kuwashida wafilisti mpaka kuwafanya wawaache huru kabisa wana wa Israeli. Lakini ukombozi ule ulidumu kwa muda tu, haukuweza kutoa ulinzi wa kudumu kwa wana wa Israeli,kwa wakati ujao.Ndivyo ilivyokuwa siku zote waamuzi zaidi ya waamuzi 12 walipita juu ya Israeli.

Hali kadhalika wakati ulipofika walipohitaji kiongozi, Mungu aliwanyanyulia mtu mwenye Hekima atakayeweza kuwaamua katika mambo yote. Na hivyo akatokea Sulemani, wakamfurahia kwa muda lakini alipokengeuka kwa muda nchi ilitetereka kwa kasi sana, na kusababisha watu kurejea katika hali zao za zamani.

Vivyo hivyo tunaona kwa manabii kama Samweli, Eliya, Elisha, Samweli, Yehu, Yohana mbatizaji ambaye Yesu alisema watu waliifurahia nuru yake kwa kitambo tu (Yohana 5:35) na baadaye ikazima..wote hao Mungu aliwatia mafuta kwa namna tofauti tofauti ili kuwaokoa au kuwarejesha wana wa Israeli katika mstari waliopaswa wawe, lakini hakukuwa na hata mmoja aliyefanikiwa kuleta ukombozi mkamilifu wa kudumu kwa watoto wa Mungu, licha ya kuwa walikuwa hodari na mashujaa.

Lakini tunasoma katika biblia wakati ulipofika wa Mungu kumleta KRISTO duniani, hakuja na kauli mbiu ya mapanga au nguvu za misuli kama Samsoni, hapana badala yake alikuja kutumbua JIPU ambalo lilikuwa limekaa kwa muda mrefu kwa SIRI tangu zamani ambalo ndio lilokuwa linawafanya watoto wa Mungu wajione ni wananafuu kwa kipindi kifupi tu pale wanapookolewa na waamuzi lakini kumbe ugonjwa bado upo ndani yao, na ndio maana mwisho wa siku wanaishi kurudia kumuudhi Mungu..

Waamuzi wote waliotangulia walikuwa wanatoa tu dawa za kutuliza maumivu (Pain-killer), lakini YESU alipokuja kuutibu ugonjwa wote,kutoa mpaka mzizi wa mwisho na kisiki, wala hakikusalia chochote si hata kovu la alama.

Na ugonjwa huo si mwingine zaidi ya DHAMBI ambayo chimbuko lake ni SHETANI.

Na ndio maana ukisoma agano la kale utaona Shetani akitajwa mara chache sana, utaona shetani akijidhihirisha mara chache sana, tofauti na ilivyo katika agano jipya…Hivyo BWANA alivyokuja ilikuwa ni kwa lengo la kumweka huru mwana yoyote wa Mungu, tena kuwa huru kweli kweli, na sio nusu nusu kesho utumwa unajirudia… na ndio maana baada yake yeye hakuna mkombozi mwingine yeyote anayehubiriwa, hata hapa hatumuhubiri mtu mwingine zaidi ya YESU yule aliyesulibiwa miaka 2000 iliyopita na aliyeandikwa kwenye biblia takatifu kwamba yeye ndiye anayeweza Kumwokoa mtu na kumfanya kuwa huru kweli kweli, hana mshirika na yeye ndiye mwanzo na mwisho, hakuna mwingine.

Yeye mwenyewe anasema.. Yohana 8:36 “Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli”.

YESU anakomesha dhambi kwa mtu yeyote anayemwamini, kumbuka dhambi ndio chimbuko la kila kitu; dhambi, ndio chimbuko la magonjwa, ndio chimbuko la mateso, ndio chimbuko la tabu, ndio chimbuko la kuteswa na mapepo, ndio chimbuko la kukosa raha, na kukata tamaa ya kuishi ndio chimbuko la masumbufu ya kila namna unayoyofahamu wewe huku duniani, ndio chimbuko la mauaji na vitendo vyote viovu vinavyoendelea huku duniani…n.k.

Dhambi ndio “control tower” ya shetani, ndio dira yake hiyo kukumaliza wewe na mimi..Wana wa Israeli walikuwa wanapata ukombozi wa miili yao kutoka kwa maadui zao, lakini hawakujua kuwa bado hajawekwa huru kweli kweli kwani yao dhambi bado zilikuwa zinawatawala, na shetani ametulia kimya asiwafunulie siri hiyo..na ndio maana baadaye waliendelea kurudi katika mateso yao ya siku zote, lakini mtu anayemwamini YESU KRISTO leo hii, hatarejea tena katika mateso yake ya kwanza.

Kumbuka wale waamuzi walipoondoka habari zao ziliishia pale pale lakini YESU wakati alipokuwa duniani alitujali na kutuombea kwa Baba tulindwe na yule mwovu, halikadhalika na alipopaa juu kwa Baba amesimama mpaka sasa kama kuhani mkuu akituombea kwa Mungu..Hivyo unaweza kuona hapo mtu aliye ndani ya Kristo kweli kweli sio wale mguu mmoja nje mwingine ndani hapana bali yule aliyekusudia kutembea na Kristo anayo faida nyingi kiasi gani!…Shetani anafahamu kabisa mtu wa namna hiyo hawezi kumpata tena milele, kwasababu mwamuzi wake, mkombozi wake anasimama mbele yake daima masaa 24, kumuamua na kumlinda.

Leo hii watu watashangaa inawezekanikaje mtu kuishi bila kuzini, mtu kuishi bila kutazama pornography, kuishi bila pombe, kuishi bila sigara, kuishi bila kuongoa matusi, inawezekanikaje mtu kuishi maisha ya furaha wakati huna pesa, inawezekanikaje unapitia shida zote hizo lakini bado tumaini lako lote lipo kwa Kristo, inawezekanikaje katika kizazi hiki cha Sodoma na Gomora, kutokuvaa suruali kwa mwanamke, na kuweka mawigi na ma-lipstick na marangi usoni, wala kupaka uwanja kama Yezebeli, inawezekanikaje unadumu katika imani bila kutetereka…

Hawajui kuwa nguvu hizo si zake bali ni za yule mwamuzi wake YESU KRISTO aliyemchagua maishani mwake, laiti zingekuwa ni zake asingekuwa vile alivyo leo…..

Maneno ya YESU yana nguvu ndugu, hilo tunalithibitisha kwa maombi yake aliyomwomba Baba akiwa hapa hapa duniani akisema..

Yohana 17: 9 “Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako;

10 na wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao.

11 Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, KWA JINA LAKO ULILONIPA UWALINDE HAWA, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo.

12 Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie.

13 Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao.

14 Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyowa ulimwengu.

15 Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; BALI UWALINDE NA YULE MWOVU.

16 Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.

17 Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli”.

Unaona hapo?, YESU aliwaombea wale waliomwini kuwa Baba awalinde na yule mwovu,na si watu wote..Sasa kama Kristo amekataa kukuombea mtu mwingine akikuombea ina faida gani?? ni sawa na bure tu!….hivyo mtu yeyote anayemwamini Kristo sasa kwa kumaanisha kabisa kumfuata na kujikana nafsi yake kama mitume na sio kwa maneno tu , hapo hapo bila kupoteza muda Neno hilo linakuwa linaanza kufanya kazi ndani yake, na ndio hapo anajikuta anao uwezo wa kuvishinda vishawishi vyote vya shetani vile ambavyo hapo mwanzo alikuwa hawezi kuvishinda kwasababu nguvu za shetani zinakuwa hazijakaa juu yake kumtawala.

Vile vile, hiyo haiishii hapo tu bali mtu huyo hata akihitaji lolote kutoka kwa Mungu, mwamuzi wake wakati wote yupo kumtetea huko juu mbinguni..Ni faida juu ya faida.

Warumi 8:33 “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki.

34 Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; TENA NDIYE ANAYETUOMBEA”.

Sasa kama Mungu hapokei mashtaka yako…mtu mwingine akikushtaki yadhuru nini?

Unaona Faida zote hizo ni kwa mtu yule aliyemwamini Kristo,lakini ikiwa upo nje ya wokovu, au upo vuguvugu leo huku kesho kule, usijidanganye fahamu kuwa hutakaa uishinde dhambi milele, itaendelea kukusumbua na huku shetani akiichochoa zaidi na zaidi, utaendelea tu kutazama pornography, kufanya mustarbation na kuwa mzinzi, na kuvaa mavazi machafu ya kikahaba na kwako mambo hayo yataendelea kuwa magumu kuyaacha hata kama utatamani kuyaacha hutaweza kwasababu Kristo hajakamilika ndani yako..Na mwisho utakufa katika hali hiyo hiyo ya dhambi na kujikuta kuzimu. Kwasababu biblia hiyo hiyo inasema mshahara wa dhambi ni MAUTI!

Ni maombi yangu sote tutamtazama huyu MWAMUZI mkuu, aponyaye roho zetu na miili yetu kuanzia sasa, kwake kuna raha, kwake kuna amani, kwake kuna tumaini, kwake kuna utulivu…

Kwa kumalizia yatafakari maneno yake haya..

Mathayo 11: 28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; NANYI MTAPATA RAHA NAFSINI MWENU;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.

Ubarikiwe sana. Tafadhali “SHARE” na wengine.


Mada Nyinginezo:

https://wingulamashahidi.org/ikabodi-maana-yake-ni-nini/

ADAM NA EVA.

NINI MAANA YA SISI KUWA WATOTO WA MUNGU?

Watoto wa Ibrahimu/Wana wa Ibrahimu walikuwa ni wangapi?

JE KUVAA PETE NI DHAMBI?

Rudi Nyumbani:

Print this post

KWA MUNGU ASIYEJULIKANA.

Tunasoma katika Matendo 17 Mtume Paulo, alipofika Athene mji mkuu wa Ukigiriki, mji ambao ulikuwa umejaa wasomi wengi ambao hata sasa historia ya dunia inarekodi sehemu kubwa ya Elimu na Sayansi tuliyonayo leo hii chimbuko lake lilikuwa ni huko Ugiriki, Wanafalsafa maarufu ambao wanafahamika kwa akili zao na hekima zao nyingi walizowahi kuzionyesha duniani mfano Aristotle, Xenophon, Plato,Pythagoras,Socrates,Plotemy, n.k. wote hao Walitokea huko huko Ugiriki, hivyo tangu zamani hawa watu walijulikana kama ni watafiti wakubwa (Great thinkers), na wagunduzi wa vitu vingi, na hivyo hawakuwa watu wa kubabaishwa tu na habari zinazovuma au maneno ya kutungwa yasiyoweza kuthibitishwa uhalisia wake yanayokuja katika jamii zao…

Na ndio hapa tunaona Mtume Paulo anaingia Athene sasa baada ya kuzunguka mataifa mengi na nchi nyingi kuhubiri, nchi hii kwake ilikuwa ni ya tofauti kidogo Kama Biblia inavyotuleza watu hawa wa Athene walikuwa hawana muda wa kufanya mambo mengine yoyote isipokuwa kutoa habari tu na kusikiliza juu ya taarifa mpya zinazowafikia (Soma Matendo 17:21), hii inaonyesha ni jinsi gani walivyokuwa wamejikita katika masuala ya utafiti na usomi ili kujua nini maana ya mambo yote na uhalisia wake zaidi ya kuganda katika mambo yale yale wanayoyaona kila siku..

Hivyo mtume Paulo alipoingia katika mji ule alianza kuupeleleza ili aone ni mambo gani yanayoendelea kule, lakini alipokuwa akizunguka huko na kule alikutana na madhahabu kubwa sana, iliyoandikwa maneno haya KWA MUNGU ASIYEJULIKANA..Hilo likateka sana fikra zake kupelekea kutaka kufahamu ni kwanini waandike vile, ni kwanini watengeneze madhabahu kwa Mungu wasiyemjua,

Kumbuka kama tulivyoona hapo mwanzo Wagiriki hawakuwa kama watu wa mataifa mengine mfano wa warumi au wamedi, hapana hawa ni watu waliokuwa wanafikiria sana, na wadadisi na wachunguzi wa kina wa mambo yote, hivyo kuandika vile sio kwamba walijisikia tu kuandika au walibuni wazo hilo kisha watengeneze madhabahu ya Mungu asiyejulikana kisha waabudu juu yake, hapana badala yake, ni kweli walitazama mambo yote,na kutathimini kwa kina na kwa utaratibu wakagundua kuwa katikati ya vitu vyote vilivyopo duniani na vinavyoabudiwa hakuna hata kimoja kinachoweza kuleta ufasaha wa mambo yao yote, isipokuwa kwa Mungu asiyejulikana asifanya vikao na wanadamu. hii ikiwa na maana japo kulikuwa na miungu mingi ugiriki watu wanayoiabudu wakati ule, lakini hakuna hata mmoja aliyefikia viwango vya kustahili kupokea Ibada zote za kiungu kwa kazi zake zote zinazoonekana ulimwenguni kote..

Walijua kabisa kipo kitu kingine zaidi ya wao wanavyoweza kukifikiri au kikitafsiri kiitwacho Mungu au vinginevyo, kinachoendesha shughuli zote za ulimwenguni, na wanadamu na kitu hicho hawawezi kuwasiliana nacho kwa njia za kawaida kwasababu ni kikuu sana, zaidi ya upeo wa kufikiri wa wanadamu, ni cha elimu ya juu sana, hakijulikani kama kipo mbali na sisi au karibu na sisi, ni kwamba tu hakina ushirika na wanadamu, wala hakielezeki, wala hakifananishwi, njia zake hazieleweki hali kadhalika hazichunguziki na makao yake hayafahamiki, na hivyo wakaona ili kufanya habari zake kuwa fupi basi wakaweka madhabahu yake mahali pa juu sana kuliko madhabahu nyingine zote na kuanza kumwabudu hivyo hivyo tu pasipo maarifa yoyote kumuhusu yeye..Ila walichokuwa wanajua ni kwamba ni kwa Mungu huyo anayeishi na ni mkuu kuliko vitu vyote.

Matendo 17:22 “Paulo akasimama katikati ya Areopago, akasema, Enyi watu wa Athene, katika mambo yote naona ya kuwa ninyi ni watu wa kutafakari sana mambo ya dini.

23 Kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua.

24 Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono;

25 wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote.

26 Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao;

27 ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu.

28 Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wenu, mtunga mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazao wake.

29 Basi, kwa kuwa sisi tu wazao wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu.

30 Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu.

31 Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu.

32 Basi waliposikia habari za ufufuo wa wafu wengine walifanya dhihaka; wengine wakasema, Tutakusikiliza tena katika habari hiyo.

33 Basi hivi Paulo akaondoka akawaacha.

34 Baadhi ya watu wakashikamana naye, wakaamini; katika hao alikuwamo Dionisio, Mwareopago, na mwanamke mmoja jina lake Damari, na watu wengine pamoja na hao”.

Kama tunavyosoma tunaona mtume Paulo alifika na kuanza moja kwa moja kuwafunulia kwa utaratibu habari za Mungu huyo ambaye wanamwabudu pasipo wao kumjua, Mungu asiyejulikana. Na hivyo waliposikia habari za jambo hilo jipya masikioni mwao wengi wao walikaa chini na kumsikiliza.

Ndugu, hao watu walikuwa wapo sahihi kabisa kuenenda katika hali hiyo ni kweli kumwelewa ni kazi sana,au tunaweza kusema haiwezekani kabisa kumwelewa yeye au kumjua yeye kama hatutajua njia fasaha ya kumwendea…

Mambo hayo hayo ya Athene yanajirudia hata leo hii, Wanasayansi sio kwamba hawaamini kuwa hakuna nguvu ya kimiujiza (Supreme being) inayouongoza huu ulimwengu hapana wanaamini kabisa isipokuwa wao wanamtambua kwa jina lingine (nature) na hiyo inawafanya wasiamwamini kabisa Mungu tunayemwamini sisi, hawaamini kama huyo (nature) ambaye sisi tunamwita Mungu anaweza akawa dhaifu namna hiyo etu ajishughulishe na wanadamu na kutazama dhambi zao ili awaadhibu, angali yeye tunamfahamu anayo mambo makubwa sana yasiyokuwa na mwisho huko angani na ulimwengui kote yasiyoweza kuelezeka kwa fikra za kibinadamu iweje leo, eti udhaifu wa mtu umuudhi, huyo sio Mungu…Unaona? Ndivyo wanavyowaza na kuamini.

Mwanasayansi mmoja maarufu wa kizazi chetu ajulikanaye kama ALBERT EINSTEIN,ambaye dunia sasa inamwona kama mtu wa karne kwa mapinduzi yake makubwa aliyoyaleta katika ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia, yeye anasema hivi …..

“Mimi naamini katika Mungu, lakini sio katika Mungu huyu watu wanaomwita wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo ambaye yeye msingi wake ni kujishughulisha na vitu vidhaifu vya wanadamu, kama dhambi, na kuadhibu watu, huyu hawezi akawa ni Mungu ninayemfahamu: anaendelea kusema: mimi anasema naamini katika Mungu ambaye ni mkuu zaidi ya upeo wa kibinadamu muumba wa UNIVERSE, ambaye akili za kibinadamu hazijitoshelezi kumwelezea tabia zake”.. Yaani kwa ufupi anaamini kwa Mungu asiyeweza kufikiwa.

Unaona? Hali kadhalika jambo kama hilo tunaliona kwa ndugu zetu waislamu, wanasema Mungu tunayemwabudu ni Mungu mkuu sana (Allah), hajazaa, wala hajazaliwa, wala hana mtoto, wala hana USHIRIKA na mwanadamu yeyote wala kiumbe chochote, si mwanaume, wala si mwanamke, na hivyo mtu yeyote anayemwita Mungu baba, au mfalme wake anatenda dhambi kubwa sana ya kumshusha Mungu hadhi ya kumfananisha na Mwanadamu ambayo ni sawa na dhambi ya kukufuru…

Sasa hawa wote sio kwamba wanakosea kuamini hivyo, hapana, walichokiona kuhusu Mungu ni kweli kabisa, na ndivyo Mungu alivyo katika uhalisia wake, lakini kumbuka jambo hilo ndio kama lile lile lililowakuta watu wa Athene wao walitengeneza madhahaba na kumwabudu Mungu ndani yake lakini madhahabahu hiyo ilikuwa na jina la “KWA MUNGU ASIYEJULIKANA.”

Unaona? Walimwabudu Mungu asiyejulikana, walimwabudu Mungu wasiyemjua, Sasa madhara yanayokuja kujitokeza kwa watu wa namna hiyo ni kwamba maisha yao yote wataishia kutokumwelewa muumba wao kabisa mpaka kufa kwao, pia hawatakaa wanufaike na chochote kutoka kwa muumba wao, Na mwisho wa siku wanaishi akutokumwelewa hata pale Mungu atakapotaka kusema nao hawatamwelewa na hivyo kupotea kabisa katika dira ya Mungu. angalia kwa makini utaona, watu na namna hiyo wanaishia kumwogopa, na kuwa na wasiwasi, na kumwendea kwa hofu zisizokuwa na maana yoyote, kwasababu wametaka kumwona yeye katika uhalisia wa ukuu wake lakini sio katika njia ambayo amewapangia wanadamu wote wamwone yeye.

Ndugu yangu Mungu kumleta Yesu Kristo duniani kulikuwa na manufaa sana, kwangu mimi na kwako wewe, ni kutufanya sisi tumwelewe yeye vizuri katika utimilifu wote, biblia inasema “Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili.”(Wakolosai 2:9), Unaona pale ambapo tulikwama pasipo kumwelewa Mungu sasa tunamwelewa kwa kupitia mwana wake YESU KRISTO.

Na ndicho Paulo alichokifanya mara moja kwa wale watu wa Athene, Aliwahubiria Kristo, Mwana wa Mungu, ambaye kwa huyo sisi tunahama moja kwa moja kutoka kuwa viumbe tu vya kawaida vya mwenyezi Mungu, na kufanyika kuwa WANA WA MUNGU aliye hai kama yeye alivyokuwa.. Na kwa kumwamini yeye basi tunakuwa na uwezo wa kumwelewa Mungu na mapenzi yake katika maisha yetu kwa urahisi kabisa, tunakuwa na uwezo wa kusimama mbele ya madhabahu ya Mungu mbinguni na kuzungumza naye bila kutaabika kama wengine walivyo sasa hivi…

Na ndio maana alisema… (Yohana 14.6…”Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.)..Na pia alisema… Aliyeniona mimi amemwona Baba;….Hatuwezi kumjua Mungu kwa njia yoyote ile isipokuwa kwa kupitia mwana wake YESU KRISTO. Huo ni ukweli ndugu wala usihangaike pengine”

Waebrania 1:1”Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi,

2 mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.

3 Yeye kwa kuwa ni mng’ao wautukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;

4 amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao”.

Tuchulie Mfano ulio hai ni sawa na leo hii unataka kuwasiliana na mimi bila kutegemea hicho kioo kilichopachikwa mbele ya simu yako, ni kweli kabisa Simu sio hicho kioo ambacho unakipangusa,na kuandika namba juu yake, …Simu ni ni kitu kingine cha ndani kilichojawa na Commands tofauti tofauti ili kufanya kifaa hicho kiweze kutumika kwa mawasiliano, sasa ikiwa utaondoa hicho kioo cha juu na ukataka kuwasiliana nami, basi jiandae kukukutana huko nambo ambayo hujayazoea maneno huko kama Galllery, au Contacts, au SMS, usitazamie utayakuta huko wala kidole hakitahitajika huko kufanya mawasiliano yaende.., ni wazi kuwa utakutana na vitu kama chips, cards,modems,processors,circuit board, na vinginevyo ambavyo hata kwa lugha ya Kiswahili havina tafsiri, ambavyo wewe kwa akili yako ya kawaida hutaelewa chochote isipokuwa yule mtaalamu wa hivyo vitu, yeye pekee ndiye anayeweza kupiga simu pasipo kioo kile, kwa vifaa na ujuzi alionao ..

Lakini sasa kwanini kile kioo kimewekwa, ni kwa faida yako wewe usiyejua hayo mambo magumu yaliyopo ndani ya hiyo simu, ili kufanya simu ionekane kuwa na maana kwako ndio hapo ukawekewa hicho kioo kizuri kwa nje chenye mpangilio mzuri wa mafile, kazi yako wewe ni kubofya tu au kupangusa, na moja kwa moja taarifa zako zinapelekwa ndani ya simu, na hivyo simu inafahamu kuwa ulimaanisha nini, na saa hiyo hiyo simu inapigwa kwenye minara kuungwa na mimi mahali nilipo kuwasiliana na wewe, Unaona hapo? jambo ambalo lingepaswa lifanywe na wataalamu wa hali ya juu, kuamrisha hizo code za simu lakini sasa linafanywa na wewe kirahisi tu kupitia kidole chako juu ya kile kioo.

Hivyo hivyo YESU ndiye kioo chetu kwa Mungu, ili tuweze kunufaika na Muumba wetu aliye mkuu sana, asiyechunguzika njia zake, asiyeelezeka kwa namna ya kibinadamu, asiyekuwa na mwanzo, aliye mwanadamu hatuna budi kumtumia yeye kama kirahisi chetu vinginevyo hatutakaa tumjue Mungu kwa kumchunguza.. Kwa kumwamini yeye na maneno yake,na sasa yale mambo yote ambayo tunayaona ni magumu kwetu, kumfikia Mungu wetu basi yanafanyika kuwa marahisi kabisa, embu fikiria kwa kuiamini tu damu ya Yesu unakuwa na nafasi ya moja kwa moja kusimama mbele za Muumba wa mbingu na nchi na kupata rehema ya kujibiwa maombi yako mambo ambayo watu wa agano la kale waliyatafuta kwa kafara nyingi lakini wasiweze kabisa kufikia hatua ya kuondolewa dhambi zao, au kusimama mbele ya madhabahu ya Mungu mbinguni…Unadhani hilo ni jambo dogo au rahisi, ukiwa nje ya Kristo hilo haliwezekani kabisa ndugu na ndio maana utaona hao wengine wanateseka huko nje, ni haki yao,kuwa hivyo japo wanamuheshimu Mungu kwa hofu lakini upendeleo huo hawataweza kuupata mpaka watakapoingia ndani ya KRISTO..

Wanamwamini Mungu lakini sio katika maarifa, wanamfahamu kuwa ni muweza wa yote lakini uweza wake hauna matunda yoyote ndani ya maisha yao, magonjwa yao hayaponywi, hawawezi kufunguliwa katika vifungo vya giza, hawawezi kupata faraha ya kudumu na amani ambayo ni YESU KRISTO tu pekee ndio anayeitoa, hawana uzima wa milele ndani yao, hawawezi kumwomba chochote kwasababu yeye huwa hajishughulishi na mambo ya wanadamu…Hana mshirika, ..Kwasababu hanawa ushirika naye kama wanavyosema…kwao ni Mungu asiyejulikana! Na asiyefanya vikao na wanadamu,..Lakini kwetu tuliomwamini Kristo Yesu, Mungu anafanya vikao na sisi, na anakuwa ni Mungu tunayemfahamu, tunakuwa ni watu wa Milki ya Mungu, ukuhani wa kifalme, uzao mteule haleluya!!

Hivyo ndugu yangu, ikiwa bado upo nje ya Kristo, wakati ndio huu, wewe mkristo-jina, wewe ni mwislamu, wewe ni asiye-na-dini mkabidhi leo maisha yako, utubu dhambi zako kabisa kwa kumaanisha kuziacha, kisha fanya hima ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na uwe ni kwa jina la YESU KRISTO, hapo ndipo utakapopokea uwezo wa kuwa mwana wa Mungu, na kuhesabiwa kuwa mtu wa kimbunguni kwasababu Roho wa Mungu atashuka ndani yako kuanzia huo wakati , kukusaidia wewe kumkaribia Mungu..na kumwelewa Mungu, Kwasababu atayatwaa yaliyo ya Kristo na kukupasha wewe habari.

Wakolosai 1:15 “naye (KRISTO) ni mfano wa Mungu asiyeonekana , mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.

Lakini ikiwa utaendelea kubakia nje ya wokovu ufahamu kuwa hutakaa umfikie Mungu, wala kumjua wala maombi yako hayatakaa yamfikie yeye kama mwana, utakufa katika dhambi, utakufa katika kukosa maarifa ya kumjua Mungu hiyo haijalishi unaonyesha heshima nyingi kwake kiasi gani, utafanana na wale watu wa ATHENE wanamwabudu Mungu wasiyemjua.. na mwisho wake utaishia katika lile ziwa la Moto.Wakati ndio huu, fanya bidii uje kwa Kristo. Na Bwana atakusaidia.

Tafadhali “shiriki ” neema hii kwa wengine, ili nao waponywe na Neno la Mungu, na Bwana atakubariki.

Maran Atha. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

INJILI KULINGANA NA TEKNOLOJIA

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

MWANA WA MUNGU.


Rudi Nyumbani

Print this post

KANUNI RAHISI YA KUFANIKIWA.

Tujifunze siri mojawapo iliyopelekea habari za Bwana wetu Yesu Kristo kuenea kwa mafanikio makubwa sana ndani ya kipindi kifupi. Tunaweza kudhani kujisifia kwetu mbele za watu, au kuonyesha wema wetu mbele ya macho ya watu wengi kutatusaidia kuongeza umaarufu wetu, Utamwona mtu mfano ametoa msaada kidogo tu, au kamsaidia mtu kwa kitu kidogo,atatangaza kila mahali, na watu wote watajua kuwa yeye ndiye aliyefanya lile jambo.

Lakini embu tuangalie mbinu Yesu aliyoitumia. Nasi tupate kitu hapo kitakachotusaidia katika huduma zetu , na shughuli zetu tuzifanyazo kila siku, na mambo mengine yote.

Marko 1:40 “Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa.

41 Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika.

42 Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika.

43 AKAMKATAZA KWA NGUVU, akamwondoa mara,

44 akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao.

45 LAKINI AKATOKA, AKAANZA KUHUBIRI MANENO MENGI, NA KULITANGAZA LILE NENO, HATA YESU ASIWEZE TENA KUINGIA MJINI KWA WAZI; bali alikuwako nje mahali pasipokuwana watu, wakamwendea kutoka kila mahali”.

Unaona, sio kwenye habari hiyo tu peke yake alimzuia yule mtu asimtangaze, lakini kila mahali alipofanya miujiza yake alitumia kanuni hiyo hiyo, sio kana kwamba hakutaka UTUKUFU au habari zake zisienee kila mahali hapana! badala yake alifahamu kuwa “kumbe kumzuia mtu asikutangaze ndio kumruhusu atangaze”..

Marko 7:34 “akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka. Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri. AKAWAONYA WASIMWAMBIE MTU; LAKINI KADIRI YA ALIVYOZIDI KUWAAGIZA, NDIVYO WALIVYOZIDI KUTANGAZA HABARI; wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme”

Tukitaka sifa zetu zienee katika nyanja yoyote ile maishani iwe ni katika Utumishi, au shughuli zetu, au chochote kile tukifanyacho, tuhakikishe tunatoa kilicho bora kwanza, kisha tukae kimya, tusijikweze, tukatae kutukuzwa tukuzwa na watu, Kwa kufanya hivyo ndio tutasifiwa, yule yule aliyekipokea ndiye atakayekisambaza kwa nguvu kuliko hata wewe unavyodhani..Hiyo ndio ilikuwa kanuni ya Bwana..alisema “ajikwezaye atashushwa na ajishushaye atakwezwa”…Kwahiyo yeye mwenyewe alijishusha ili akwezwe.

Hali kadhalika mara nyingine Tunamwomba Mungu jambo kubwa, na huku tunatazamia jibu kubwa kutoka kwake. Tunamwomba Mungu atupe labda tuchukue mfano wa Gari, tunamwomba atupe gari, lakini kwa bahati mbaya haliji gari inakuja baiskeli tunaweza tukasema sio Mungu lakini tusipojifunza kanuni za Mungu kibiblia tunaweza tukakosa shabaha ya kupokea majibu yetu.

Embu mtafakari Eliya jinsi alivyofanya alimwomba Mungu mvua kubwa ya kutosha itakayoinyeshea nchi kame ya Israeli iliyokaa zaidi ya miaka 3 bila kupata hata tone moja la maji, lakini alipoomba kwa nguvu nyingi na kwa bidii mara 7 huku akitazamia kuona wingu zito jeusi, likitokea mashariki, lakini badala yake kilizuka kiwingu kidogo kama mkono wa mtoto mchanga. Lakini Kwa imani yeye alipoona vile hakushtuka kusema kuwa Mungu hajanisikia, kiwingu kile sio cha mvua, bali kijiupepo tu kimeuvumisha, badala yake alipokea vile vile katika udogo ule kwa Imani, na kuondoka mahali pale, lakini biblia inasema ghafla wingu zito likatanda juu ya nchi,na mvua kubwa sana ikanyesha.

Usidharau udogo wa majibu utokao Kwa Bwana juu yako, “usiidharau siku ya mambo madogo”…Ulimwomba nyumba kwa muda mrefu lakini umejikuta unapata pikipiki kwa sasa, usiseme Mungu hajakusikia pokea hiyo kwa Imani na kwa shukrani ukijua kuwa Mungu alishakusikia ulichomwomba na ghafla hiyo pikipiki moja itazaa nyumba 5 kwa muda mfupi sana usioutazamia…

Lakini pia usisahau, duniani sisi ni wapitaji tu! Hatujaitiwa kupata majumba, wala magari, wala mashamba…hayo ni ya muda tu! Pindi tukiwapo hapa duniani na yote yanapita…lakini tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya kama maandiko yanavyosema (2 Petro 3:13), mbinguni ndio kwetu, Hivyo Kila siku ni wajibu wetu, kutazama usalama wa roho zetu zaidi ya vitu vyetu tunavyomiliki. Kwasababu Biblia inasema 

“ Uzima wa Mtu haupo katika wingi wa vitu tulivyonavyo Luka 12:15” na tena inasema “itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake Marko 8:36”

Bwana akubariki sana. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

NJIA YA ‘UTAJIRI MKUU’ KWA KIJANA.

BEI YA UFALME WA MBINGUNI:

Print this post

MADHAIFU:

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe.

Mambo mengi yanayoendelea katika ulimwengu wa mwili ni ufunuo wa mambo yanayoendelea katika ulimwengu wa roho..Uhusiano wa Baba na mtoto..ni ufunuo wa Uhusiano wa Baba yetu wa mbinguni na sisi watoto wake tuliopo hapa duniani…Kama Baba mzazi asivyoweza kumdharau mwanawe hata kama afanye jambo la kitoto kiasi gani ndivyo Baba yetu wa mbinguni asivyoweza kutudharau sisi watoto wake katika uchanga wetu. Na watoto wa Mungu ni wapi? Watoto wa Mungu ni wale waliomwamini Mwanawe mpendwa Yesu Kristo, hao ndio watoto wa Mungu…

Yohana 1: 11 “Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika WATOTO WA MUNGU, NDIO WALE WALIAMINIO JINA LAKE”

Kauli hiyo Ikiwa na maana kuwa kama mtu hajampokea bado Yesu Kristo bado hajapewa huo uwezo wa kufanyika kuwa mtoto wa Mungu, Hivyo sio mtoto wa Mungu bali anakuwa kama mtu tu au kiumbe cha Mwenyezi Mungu.

Upo usemi unasema “mtoto hakui kwa mzazi wake”…Na ndivyo ilivyo kwa Baba yetu wa mbinguni..sisi ni watoto wake na tutabaki kuwa watoto wake tu milele…na Mungu hana wajukuu (wote sisi ni watoto wake).

Wapo watu wanapitia vita vya kiakili sana wanapokwenda kumwomba Mungu, kwasababu wanajiangalia ni jinsi gani wana madhaifu mengi, wanajiona hawajui kupangilia maneno wanaposali, wanakosa mtiririko mzuri wa maneno, Ningependa nikuambie kuwa Baba yetu haangalii wingi wa maneno au mpangilio mzuri wa Maneno tulionao mbele zake, bali anaiangalia nia yetu ya ndani, tamaa yenu au kusudi letu la ndani…kwasababu yeye mwenyewe alishasema anajua haja za mioyo yetu hata kabla ya sisi kwenda kumwomba. (Mathayo 6:8).

Mzazi anao uwezo wa kujua kuwa mwanawe anahitaji chakula na maji…kabla hata huyo mtoto hajajua kuzungumza wala kujua nini maana ya chakula wala maji..kwasababu upeo wake ni mkubwa zaidi ya huyo mtoto, ameishi muda mrefu na hivyo anafahamu mambo yote mtoto anapaswa ayapate hata kama hatazungumza..Ndivyo ilivyo kwa Baba wa mbinguni. Na pia Mungu hana kinyongo wala hatukinai. Madhaifu yetu hayamfanyi Baba yetu wa mbinguni atuchukie..kama tu madhaifu ya vichanga vyetu hayatufanyi tuwachukie…zaidi sana ndio tunawapenda, na kuwatengenezea njia kila siku ya wao kukua ili baadaye waachane na hayo madhahifu, hilo lipo wazi hakuna mzazi katika hali ya kawaida anamchukia mtoto wake mchanga..tena zaidi ya yote ndio anampenda zaidi.

Mathayo 7:11 “Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?”

Lakini tatizo kubwa linakuja ni wengi kutokuelewa tofauti kati ya MADHAIFU na DHAMBI. Mungu hachukizwi na madhaifu yetu lakini anachukizwa na dhambi…Kwasababu madhaifu ni kitu kinachotokana na uchanga au kukosa ufahamu, lakini dhambi ni kitu kingine…Wengi wanabadili dhambi kuwa madhaifu…Labda utasikia mtu ni mwasherati halafu atakwambia ni udhaifu wangu tu!, mtu anatukana halafu anakuambia ni udhaifu wetu wanadamu tumeumbiwa hayo kwahiyo Baba anaelewa, mtu ni mwizi au mlevi halafu anasema huo ni udhaifu wake..Ndugu huo sio udhaifu unaozungumziwa katika maandiko Hizo ni Dhambi na zinamchukiza Mungu, ambazo mshahara wake ni mauti. Hebu wewe mwenyewe tafakari mtoto wako akiwa mwizi au mtukanaji unaweza kwenda mbele za watu na kuwaambia walimwengu kuwa mwanangu anaudhaifu wa utukanaji au uzinzi?..kuna mtu atakuelewa kweli..Ni wazi kuwa watu wote watakuambia umfunze mwanao aache hizo tabia.

LAKINI NINI MAANA YA UDHAIFU?.

Udhaifu ni kitu mtu anakifanya kisivyopaswa, kwa kutokujua..lakini endapo akijua usahihi wa jambo hilo basi anajirekebisha mara…Kwamfano mtu aliyempa Kristo maisha yake kwa mara ya kwanza (Yaani kasikia injili na kuchomwa moyoni na kumwamini kuwa Yesu Kristo ni Kweli) anaweza kuwa na madhaifu mengi…anaweza akawa bado anatabia Fulani za kiulimwengu ambazo anakuwa anazionyesha..tabia za ubishi ubishi, wakati mwingine ugomvi, tabia za kupenda baadhi ya vitu vya kiulimwengu, vijitabia vya kutokujali n.k na hiyo yote ni kwasababu bado hajasikia mahali popote na wala hajasoma maandiko na kuelewa kuwa mambo hayo mtu aliyempa Bwana maisha yake hapaswi kuyafanya…Na inapotokea anausikia ukweli kuwa mambo hayo sio sahihi aliyokuwa anayafanya, haraka sana anakuwa ni mwepesi kugeuka…

Sasa mtu wa namna hiyo Mbele za Baba wa mbinguni alikuwa anaonekana kama ni mtoto tu! Mwenye madhaifu ambayo baadaye atakapokuja kujua ukweli atabadilika. Na hata angekufa katika ile hali ya madhaifu bado angeokoka kwasababu alikuwa anafanya mambo ambayo alikuwa hajui kama ni makosa…Na alikuwa hafanyi vile kwa makusudi…bali ni kwasababu alikuwa hajui! Ni sawa na mtoto wako mchanga anapojisaidia kwenye nguo zake za ndani..huwezi kumpiga au kumwadhibu kwa kosa lile au anapochukua kikombe na kukirusha kule? utamwekea kinyongo?…kwasababu unajua amefanya vile kwa uchanga wake wa akili…endapo angekuwa mtu mzima asingefanya vile. Na Baba wa mbinguni ni zaidi ya hayo, yeye anaangalia kwa jicho la ndani zaidi kuliko hata sisi tunavyoona.

Lakini sasa endapo mtu kashaujua ukweli kuwa uasherati ni dhambi, uzinzi ni dhambi, ulevi ni dhambi, rushwa ni dhambi, wizi ni dhambi, utazamaji pornography na utoaji mimba ni dhambi, ufanyaji masturbation ni dhambi,uvaaji mbovu ni dhambi..halafu bado anaendelea kufanya hivyo kwa makusudi, pengine kaujua kwa kusoma maandiko au kuhubiriwa….huyo mtu mbele za Mungu sio mdhaifu bali ni muasi na atahukumiwa..

Biblia inatuonya sana kuhusu dhambi za makusudi…ni hatari sana hizo…

Waebrania 10:26 “Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, HAIBAKI TENA DHABIHU KWA AJILI YA DHAMBI;

27 bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao.

28 Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu.

29 Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?”

Shetani amedanganya wengi kuwa uasherati ni madhaifu yetu sisi wanadamu, kwahiyo mtu anakwenda kufanya uzinzi akiamini moyoni mwake kuwa Bwana anaelewa, …akiamini kuwa huo ni udhaifu Mungu aliomwekea kila mwanadamu ndani yake..usidanganyike ndugu yangu hiyo ni tiketi ya kwenda kuzimu moja kwa moja…shetani anakushawishi kukuambia ufanyaji wa masturbation ni udhaifu, usidanganyike ndugu, huo ni muhuri wa kukupeleka kuzimu..Shetani anakushawishi kuamini kuwa utukanaji, chuki, kutokusamehe na vinyongo ni udhaifu na huku unajua kabisa ndani ya moyo wako mambo hayo ni machukizo mbele za Mungu..usidanganyike ndugu yangu mambo hayo ni njia panda ya Jehanamu ya moto..

Na moja ya dhambi kubwa inayowapeleka watu wengi kuzimu ni UASHERATI na nyingine ni KUTOKUSAMEHE…Uasherati ndio inayoshika namba moja na kutokusamehe inafuata hapo nyuma…Watu wengi wanakimbilia kuomba toba wasamehewe dhambi zao, lakini maandiko yanasema…

Mathayo 6: 14 “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, WALA BABA YENU HATAWASAMEHE NINYI MAKOSA YENU,”..

Na unafikiri madhara ya kutokusamehewa na Bwana dhambi zako ni nini??..Ni ZIWA LA MOTO!!!..Kwahiyo ndugu kutokusamehe sio udhaifu bali ni dhambi..Kwaufupi jambo lolote unalolifanya huku unajua kabisa sio sahihi kimaandiko, jambo hilo ni dhambi.

Ni matumaini yangu kuwa utakuwa umeongeza kitu juu ya vile unavyovijua, na Kama hujampa Bwana maisha yako, mlango upo wazi leo, fanya hivyo leo kabla nyakati za hatari hazijafika..

Bwana akubariki sana. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?:

VITA VYA KIFIKRA BAADA YA KUZALIWA MARA YA PILI

KITABU CHA UKUMBUSHO


Rudi Nyumbani

Print this post

RABONI!

Shalom mpendwa, karibu tujifunze Maneno ya Uzima.

Kama tukifakari kwa ukaribu matukio yaliyokuwa yanatokea baada ya Bwana wetu Yesu kufufuka, tutaona siri nyingi sana zimejificha ndani yake, kwamfano embu leo tuitazame siku ile ya kwanza kabisa ya Juma (Jumapili alfajiri), ambayo Mariamu Magdalene aliamka mapema sana kuliko hata watu wengine wote na kwenda kaburini kwa Yesu kutazama, Kwanza mpaka hapo hii inatuonyesha ni kwa jinsi gani huyu mama alikuwa anaupendo wa kipekee kwa Bwana zaidi hata ya watu wengine wote , lakini tunasoma alipofika tu makaburini kwa bahati nzuri au mbaya, alikuta tayari Kristo ameshamtangulia kufufuka, alichokiona ni jiwe tu la kabuni likiwa limeviringishwa pembeni na hakuna mtu ndani yake, wala chochote maeneo hayo, hivyo kwa hofu kubwa na kwa kuogopa akarudi haraka kwenda kuwaita mitume waje kulithibitisha hilo, ndipo tunaona Petro na mwanafunzi mmoja wakaondoka kwa kasi nyumbani pale, kuelekea makaburini,na walipofika kule ni kweli hawakuona mtu wala kitu chochote isipokuwa vitambaa vya sanda tu vimezongwa zongwa pembeni, hiyo iliwasikitisha sana lakini wakawa hawana namna isipokuwa kurudi tu nyumbani kuendelea kuomboleza…

Yohana 20:6 “Basi akaja na Simoni Petro, akaingia ndani ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala,

7 na ile leso iliyokuwako kichwani pake; haikulala pamoja na vitambaa, bali imezongwa-zongwa mbali mahali pa peke yake.

8 Basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza wa kufika kaburini, akaona na kuamini.

9 Kwa maana HAWAJALIFAHAMU BADO ANDIKO, YA KWAMBA IMEMPASA KUFUFUKA.”

Japo mitume ndio waliokwenda kuitwa lakini hawakuweza kudumu kwa muda mrefu pale makaburini kuangalia mwisho wake utakuwa vipi, badala yake wao moja kwa moja walirudi nyumbani, Lakini Mariamu aliendelea kubaki pale makaburini akijiuliza kwa uchungu moyoni mwake ni nini kinachoendelea mahali hapa na ni nani aliyeyafanya haya yote! Kwanini haya yote yampate Bwana?..Lakini wakati alivyokuwa anazidi kulia pale pembezoni mwa kaburi la Bwana, alirusha macho yake kwa mbali na ndani ya kaburi aliona malaika wawili wameketi mmoja kichwani na mwingine miguuni pa Yesu alipokuwa amelazwa, mahali pale pale wakina Petro walipokuwa wanapaangalia kwa makini wakizipapasa zile Leso,..Kumbe hakawajua mahali pale pale walikuwa wameketi malaika wa Bwana wakiwatazama tayari wakisubiria tu muda wa kusema nao, Lakini kwa kukosa kwao kuwa na subira waliondoka kwa huzuni, na ndio sasa tunamwona Mariamu akiwaona, na kuwauliza…

Yohana 20:12 “Akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe, wameketi, mmoja kichwani na mmoja miguuni, hapo ulipolazwa mwili wake Yesu.

13 Nao wakamwambia, Mama, unalilia nini? Akawaambia, Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka”.

Hiyo habari hapo inatufundisha nini?..Tusiwe wepesi kuondoka uweponi mwa Bwana, Pale ambapo tunaona hakuna tegemeo kwa Mungu, tumaini lote la mwisho limepotea, kumbe hapo hapo ndipo Mungu kaketi ili kutuhudumia..Tusiwe wepesi kuondoka uweponi mwa Bwana.

Lakini tukirudi kwa Mariamu hilo peke yake halikutosha kumpa yeye majibu ya maswali yake, japo aliwaona malaika wa Bwana yeye alizidi kuendelea kulia tu, na muda kidogo mahali alipokuwa amekaa akasikia kama mtu anatembea maeneo ya karibu na pale alipokuwepo wala Mariamu hakuwa na muda wa kumtazama wala kumsemesha kwani alidhani atakuwa ni MTUNZA BUSTANI tu, hivyo Yule mtu akamfuata na kumwambia maneno haya:

Yohana 20:15 “Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa.

16 Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, RABONI! (Yaani, MWALIMU WANGU).

17 Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.

18 Mariamu Magdalene akaenda, akawapasha wanafunzi habari ya kwamba, Nimemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia hayo”.

Unaona hapo dakika za mwisho kabisa Mariamu anakuja kumwona na kumtambua Bwana Yesu, Lakini swali la kujiuliza hapo, ambalo hasaa ndio kiini cha somo letu la leo ni kwanini Bwana alimwambia “USINISHIKE; KWA MAANA SIJAPAA KWENDA KWA BABA”?

Sasa kama ukichunguza hapo, utaona Mariamu alipomwona Bwana, huyu mwandishi wa kitabu hichi cha Yohana Mtakatifu, hakunukuu maneno yale Mariamu aliyozungumza kwa kumuita Yesu Bwana au mwana wa Mungu au jina lingine lolote, wala hakutumia neno la moja kwa moja la mwalimu, badala yake aliandika kwa lugha ya kiebrania RABONI, ikiwa na maana MWALIMU WANGU..Sasa Uandishi huo haukuandikwa ili kutufundisha sisi maneno ya kiebrania, hapana kuna sababu kubwa kwanini hakuwenda moja kwa moja kuandika “mwalimu wangu” bali alianza na neno RABONI!, Hiyo ilikuwa ni kuweka msisitizo wa uzito wa kauli hiyo aliyoitoa Mariamu kwa BWANA…

Na ndio maana baada ya Maneno hayo kutoka kinywani mwa Mariamu tunaona Bwana akamwambia sasa USINISHIKE; KWA MAANA SIJAPAA KWENDA KWA BABA”?…Sasa hilo ni Neno usinishike, haimaanishi kuwa usinishike mwili wangu hapana bali Bwana alimaanisha kuwa.

“kwa kauli yako hiyo, ya kunifahamu mimi kama Raboni/mwalimu wako, usinijue mimi hivyo kwasasa, mpaka nitakapopaa kwenda kwa Baba…”

Na sio kwamba alimaanisha usinishike mwili wangu, kama wengi wanavyodhani,..Ikumbukwe kuwa kulikuwa na wakati mwingine walikuja kukutana naye yeye pamoja na Mariamu yule wa pili, na wote wakamshika miguu na kumsujudia (Mathayo 28:9). Sasa kama ingekuwa ni kumshika mwili asingeruhusu kitendo hicho kifanyike tena mahali hapo.

Hivyo Bwana alikuwa anamaana gani kusema vile?. Kumbe Japo walimwona YESU kama ni MWALIMU wao, lakini kiukweli walikuwa bado hawajamwelewa, na ndivyo Yesu alivyowaona….Lakini watakuja kumwelewa vizuri atakapopaa kwenda kwa Baba yake…Kwasababu kama wangekuwa wamemwelewa tangu zamani wasingekuwa wanapoteza muda kwenda kulia makaburini, badala yake saa ile ile wangepaswa wafurahie ushindi ambao wameupata kwa kufufuka kwake, kama alivyotabiriwa lakini wao kinyume chake walikuwa wanawaza habari za kuibiwa kwa mwili wake..Ni wazi kuwa walikuwa bado hawajamwelewa kama Mwalimu wao.

LAKINI NI KWANINI BWANA APAE KWANZA?

Jibu lipo wazi ndio hili kama tunavyosoma katika..

 Yohana 16:7 “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo MSAIDIZI hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.

8 Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.

9 Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi;”

Umeona hapo? Kupaa kwa Bwana ni kwa ajili yetu sisi tupate msaidizi, ambaye kama tungemkosa huyo basi tungebaki katika mafumbo mengi ya kutomwelewa Kristo kama RABONI wetu, hata kama tungejifanya kumwita mwalimu kiasi gani,kama hatuna Roho mtakatifu haiwezekana kumwelewa Kristo. hata kama Kristo atatembea na sisi na kulala na kula na kunywa na sisi kila siku kama alivyofanya kwa mitume, kama tutakosa Roho Mtakatifu hatutakaa kamwe tumwelewe yeye..Huo ndio ukweli!

Na ndio maana Bwana Yesu aliweka wazi kabisa katika..

Yohana 16:13 “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.”

Na ndivyo tunavyokuja kuona kwenye maandiko mara baada ya Kristo kuondoka Roho alipoachiliwa kwa wale wote waliotaka kumpokea siku ya Pentekoste, kuanzia huo wakati na kuendelea, tunaona jinsi mitume walivyomwelewa Kristo kwa namna ya kipekee hata zaidi ya ule wakati walipokuwa naye duniani..Tunaona jinsi gani walivyokuja kumwelewa sana KRISTO kama RABONI!, MWALIMU WAO MKUU, kwa Yule Roho tu Mtakatifu aliyeachiwa ndani yao……Unaona umuhimu wa kuwa na ROHO MTAKATIFU ndugu?

Vivyo hivyo na hata leo, haijalishi unampenda Bwana Yesu kiasi gani, haijalishi wewe ni mfuasi wa Yesu kiasi gani, haijalishi utajiita ni mwanafunzi wa Yesu kiasi gani, haijalishi utaona maono kiasi gani, haijalishi Yesu atakutokea mara ngapi, na kula na wewe na kutembea na wewe..KAMA hauna ROHO MTAKATIFU, basi fahamu kuwa bado upo mbali sana na KRISTO, kama vile Mashariki ilivyo mbali na Magharibi.

Kumbuka pia Roho Mtakatifu sio kunena kwa Lugha, ni zaidi ya hivyo vitu..Unaweza ukanena kwa Lugha na bado Roho wa Mungu akawa mbali na wewe vile vile…Uthibitisho wa kuwa na Roho Mtakatifu ni Matunda ya Roho katika tunavyoyasoma katika biblia Wagalatia 5:22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”..yaani kwa ufupi “UTAKATIFU”….Kunena kwa lugha, maono, miujiza,uponyaji hivyo vyote ni vipawa vya Roho na sio matunda ya Roho…Na vipawa hivi havifanani kwa watu wote, kila mtu kapewa cha kwake, kwa jinsi roho alivyomjalia…Kwahiyo mtu anaweza akajazwa Roho na asinene kwa lugha bali akaonyesha karama nyingine labda uponyaji, imani au unabii, Neno la Maarifa n.k…

Kwahiyo uthibitisho pekee wa kujitambua kama unaye Roho Mtakatifu au la! ni UTAKATIFU ulionao..ambao ni upole, uvumilivu, huruma, fadhili,furaha, mwenye kiasi, mwaminifu n.k…Na sio kunena kwa lugha…Vipawa vya Roho ni uthibitisho namba mbili…lakini uthibitisho namba moja ni Utakatifu.

Biblia inasema..

Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”.

Hivyo na wewe ndugu, hata sasa Roho wa Mungu anataka kuja juu yako maana ahadi hii ni ya kwako pia, na anataka akufanye uwe mwanafunzi wa YESU KRISTO kweli kweli ili afanyike kuwa RABONI! Kwako Katika maarifa yote..Unachopaswa kufanya ni kutubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kabisa kuziacha hapo ulipo, Unakusudia kuacha ulevi kama ulikuwa mlevi, unakusudia kuacha uasherati kama ulikuwa mwasherati, unakusudia kuacha usengenyaji kama ulikuwa msengenyaji, unakusudia kuacha utazamaji wa picha chafu mitandaoni kama ulikuwa unafanya hivyo n.k kisha hatua inayofuata ni kwenda kutafuta mahali wabatizwapo ubatizo sahihi wa kimaandiko, yaani ule wa kuzamishwa katika maji mengi na uwe ni kwa JINA LA YESU KRISTO na si vinginevyo, Kumbuka hayo ni maagizo Bwana aliyoyatoa kwa ajili ya ondoleo la dhambi zetu, na ikiwa hayo yote umemaanisha kuyafanya kwa kumaanisha kabisa kuanza kuishi maisha mapya matakatifu ya kumwishia Mungu, basi fahamu kuwa kuanzia huo wakati na kuendelea Roho wa Mungu atakuja juu yako kukufanya kuwa mwanafunzi wa KRISTO. Na kukupa uwezo wa kumwelewa mwana wa Mungu kwa mapana yake yote na marefu yake,..

Mafundisho hayo sio wote wanapewa isipokuwa wale tu waliopokea Roho wa Mungu.

Hivyo ni maombi yangu kuwa utachukua uamuzi huo leo. Na Bwana akubariki sana. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

BADO KITAMBO KIDOGO HAMNIONI

JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOKUJA JUU YA MTU.

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?


Rudi Nyumbani

Print this post

MWILI NA DAMU YA YESU KRISTO.

Shalom, karibu katika kujifunza Neno la Mungu, ambapo leo tutajifunza juu ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu…kama maandiko yanavyotuambia.. “tumfahamu sana mwana wa Mungu hata kufikia cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo Waefeso 4:13”. Yaani kwa lugha rahisi ni kwamba “tunapaswa tumfahamu na kumwelewa Yesu Kristo mpaka kufikia kile kiwango ambacho yeye anataka sisi tumfahamu”…Ndio jukumu pekee tulilopewa hapa duniani, Ili kwamba tusipelekwe na kuchukuliwa na kila aina ya upepo wa elimu zilizozagaa za kidini.

Kwahiyo kuna umuhimu sana wa kumwelewa Yesu Kristo, ni dhahiri kuwa usipomwelewa mtu fulani, huwezi kutembea naye, wala huwezi kuishi naye…hata mazungumzo yenu mnaweza msielewane au mkapishana. Kila mmoja asielewe nia ya mwenzake ni ipi hiyo ni kwasababu hamfahamiani. Na kwa Yesu Kristo ndio hivyo hivyo tusipomwelewa vizuri tutapishana naye tu kwa kila kitu.

Kuna maneno mengi ambayo Bwana Yesu aliyaongea ambayo pasipo Roho kumjalia mtu kuyaelewa, kamwe hatayaelewa na mwisho wa siku ataishia kutafsiri kwa akili tu.

Kwamfano kuna mahali Bwana Yesu alimwita Herode Mbweha.

Luka 13: 32 “Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika”.

Kwa sentensi hiyo ni rahisi kusema Bwana kamtusi Herode, Nimewahi kukutana na watu wanasema Bwana alimtusi Herode, na hivyo Mungu gani anatukana.

Kadhalika kuna mahali Bwana alisema..

Luka 14.25 “Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia,

26 Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu”.

Kwa maneno hayo, pasipo msaada wa Roho, unaweza ukasema Bwana anahalalisha chuki kwa wazazi na ndugu.

Sentensi nyingine tena ya Bwana yenye utata mkubwa ni pale aliposema maneno haya…

Yohana 6:52 “Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi MWILI wake ili tuule?

53 Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.

54 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.

55 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.

56 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake.”

Kwa maneno hayo, hata wewe unaweza ukasema Bwana anahalalisha unywaji wa damu..na ulaji wa nyama ya mtu.

Na yapo maneno mengine mengi sana, katika maandiko ambayo pasipo msaada wa Roho-Mtakatifu ni rahisi kutafsiri kivingine..

Lakini hebu tuzichambue baadhi ya hizi sentensi kwa ufupi kisha tujifunze kitu..

Pale Bwana alipomwita Herode Mbweha..hakumaanisha kumtusi kwamba Herode ni Mbweha..kama sisi wanadamu tunavyotukanana na kuvunjiana heshima…Hapana Bwana alimwita Herode Mbweha kufunua tabia yake ya ndani..tabia yake ya ndani ya kurarua na kuwinda vitu vidogo vidogo aliifananisha na Mbweha, kwasababu Mbweha ndio anatabia hizo…Kwahiyo alikuwa anaangalia tabia ya rohoni ya Herode na kuifananisha na aina Fulani ya mnyama…Ndio maana yeye Bwana mwenyewe pia alijifananisha na Mwana-kondoo na sio tu yeye alijifananisha na mwana-kondoo bali hata Yohana Mbatizaji alimwita Bwana Yesu “mwana-kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu”…Yohana alimwita Bwana kondoo kwa kuiona tabia ya Bwana ya Upole kama kondoo na ya unyenyekevu….sasa kama Bwana alimtukana Herode na yeye mwenyewe atakuwa anajifanyaje?..maana kama ni matusi basi ni heri uitwe Mbweha kuliko kondoo..wafugaji wanawaelewa kondoo walivyo..Nimewahi kukutana na mfugaji mmoja akaniambia mtu anitukane matusi yote duniani, lakini asiniite mimi kondoo…kwao ni kama tusi kubwa sana.

Tukirudi kwenye mfano wa pili Bwana alisema… “mtu akija kwangu naye hamchukii Baba yake na Mama yake hawezi kuwa mwanafunzi wangu”..Na sentensi hii pia ni sentensi yenye utata sana..lakini Hebu tafakari…Inawezekanaje Bwana Yesu aseme sehemu moja, “wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi”…halafu na hapa ajisahihishe tena aseme “mtu akija kwangu ahakikishe amemchukia Baba yake na Mama yake”..unaona hiyo inawezekana kweli??..Ni dhahiri kuwa haiwezekani kwasababu Bwana Yesu hawezi kusema hapa hivi na baadaye ageuke aseme vile…kwasababu yeye sio kigeugeu..Kwahiyo hapo Bwana alikuwa haizungumzii chuki ya kuwachukua wazazi au ndugu, hapana bali chuki inayozungumziwa hapo ni chuki ya mapenzi ya wazazi..mfano mzazi mapenzi yake ni wewe usimfuate Bwana, hayo mapenzi unapaswa uyachukie…mzazi mapenzi yake ni wewe kuwa mlevi na mtu wa kidunia vuguvugu, mapenzi yake ni wewe uwe mganga, au mvaaji kama wanawake wa kidunia, hayo mapenzi ndio ya kuyakataa, na kuyafuata mapenzi ya Mungu, na kwa kuyakataa ndio kuyachukia kwenyewe huko.

Lakini sio kwenda kumtukana mzazi, au kumchukia kabisa na kukataa kuongea naye na kumwekea uadui…hapana hiyo sio maana yake..Tunapaswa tuwapende wazazi na kuwaombea…lakini kuna mipaka ya uhusiano wetu na Mungu, wasiyopaswa wao kuyaiingilia.

Na tukimalizia na huo mfano wa Mwisho Bwana aliousema Mtu asipoula mwili wangu na damu yangu hana uzima ndani yake hapa ndipo kiini cha somo letu kilipo…Hapo Bwana hakuhalalisha tukamshike na kumchinja na kuila nyama yake na kuinywa damu yake kama wachawi wanavyofanya..

Hapana bali alimaanisha kuula mwili wake katika roho na kuinywa damu yake katika roho kama yeye alivyosema…

Kwasababu katika roho tunakula na kunywa kama tunavyokula na kunywa katika mwili.. Na hivyo kumla Bwana Yesu Kristo ni KUYASIKIA MANEO YAKE NA KUYAAMINI NA TAFAKARI MANENO YAKE, NA KUYAISHI..na maana ya kuinywa damu yake ni KUTAFAKARI UWEZO ULIOPO KATIKA DAMU YAKE NA KUUTUMIA.. Hiyo ndiyo maana ya kuula mwili wa Yesu na kuinywa damu yake…Na kwa nje tunashiriki kama ishara tu! Ambayo ndio ule MKATE na DIVAI. Ambao ni ishara tu ya nje kuelezea mlo unaoendelea rohoni.

Sasa hata leo wapo watu wanaokula nyama ya Bwana Yesu na kuinywa damu yake, hao ndio wale watu wanaojifunza Neno lake na kulitafakari usiku na mchana na kuishi katika hilo na kuna watu wanakula nyama za watu wengine na kuna wengine wanakula nyama za miili yao wenyewe..Kama tulivyotangulia kusema…nyama ya mwili wa Bwana Yesu ni MANENO YAKE, kadhalika nyama za watu wengine ni Maneno ya hao watu…Na nyama za mtu binafsi ni maneno yake mwenyewe.

Kuna kipindi mwanzoni mwanzoni tu wakati nimempa Bwana maisha yangu..kuna vitu nilikuwa navitafakari halafu navipatia majibu mwenyewe pasipo kutumia mrejesho wa Biblia..Ilikuwa hivyo tu, na nilikuwa nayaamini majibu yangu zaidi kuliko kitu kingine..Na kwasababu nilikuwa bado ni mchanga kiroho, nilikuwa sielewi hata namna ya kuisikia sauti ya Mungu, wala kuithibitisha..Kwahiyo ilikuwa nikisoma mstari mmoja kwenye maandiko nilikuwa nauchukua huo na kuutafakari kwa jinsi niuelewavyo na kisha kuupatia tafsiri..

Siku moja usiku nilisoma mstari mmoja katika kitabu cha Mwanzo, na kuupatia tafsiri mwenyewe na kuiamini hiyo tafsiri nikaenda kulala…Usiku nikaota ndoto nimekaa kwenye kiti halafu miguu yangu ipo kwenye sufuria inayotokota maji….sasa wakati ile miguu yangu inachemka kule majini nilikuwa sisikii maumivu hata kidogo, na maji yale yalikuwa yamechemka mpaka miguu imekuwa meupe, na kuna mtu nilikuwa kama naongea naye mbele yangu ninayemfahamu…wakati tunaongea nikajikuta kama kuna sahani imeletwa mbele yangu yenye nyama..nikawa nakula zile nyama…na nikataka kama kumkaribisha Yule mtu niliyekuwa naongea naye..kabla hajaanza tu na yeye kuila ile nyama.. nikaangalia chini..nikaja kugundua kuwa zile nyama nilizokuwa ninazila zilikuwa zinatoka kwenye miguu yangu mwenyewe hiyo iliyokuwa inachemka hapo chini..na nilikuwa nimeshaanza kuila nakaribia kuimaliza..nikaacha!. Na ghafla nikashtuka usingizini…Nikawa natafakari maana ya ndoto hiyo nikiwa pale pale kitandani, Niliogopa sana.

Wakati naitafakari hiyo ndoto Nikasikia kama maelezo Fulani yamekuja kichwani yanayosema “nisizifuate akili zangu bali niliangalie Neno la Mungu”…Saa hiyo hiyo nikapata tafsiri ya ile ndoto nikikumbuka na mistari niliyokuwa nasoma jana usiku ambayo nilijitengenezea tafsiri yake mwenyewe…Kuwa ile nyama niliyokuwa naila ni nyama ya mwili wangu mwenyewe..Na kama unavyojua mtu ukijikata mguu na kuula, na ukajikata mkono nakuula maana yake, ni unajimaliza mwenyewe na mwishowe utakufa…Kwahiyo siku hiyo ndio nikaelewa madhara ya kuyafuata na kuyaamini maneno yangu mwenyewe ambayo hayana mrejesho wa kutosha kwenye maandiko…mwishoni yataniletea mauti ya kiroho. Nikamshukuru Mungu kwa kunionyesha hilo, Kwahiyo nikabadilika kuanzia siku hiyo na kuanza kuisoma biblia kwa undani sana…kitabu kwa kitabu, sura kwa sura, Kabla ya ufunuo wowote kuuamini ni lazima niuhakiki kwenye maandiko kwa nguvu zote, na niwe na mistari ya kutosha kuisimamia Roho Mtakatifu akiwa ni msaidizi wangu wa pembeni..Na nikaja kuelewa kuwa nilikuwa najipoteza mwenyewe, kwa kujiaminisha mwenyewe na mitazamo yangu..Nikaja kugundua nilivyokuwa nawaza ni tofauti kabisa na Maneno ya Mungu..ingawa katika kile kipindi nilikuwa najiona nipo sawa..

Kwahiyo ndugu Maneno ya Yesu Kristo ndio maneno ya Uzima, yanayotupa afya mwilini mwetu. Tunapoula mwili wake (Maneno yake) na Damu yake ipasavyo ndivyo tunavyojiongezea afya katika roho zetu, na tusipoula mwili wake na damu yake ndivyo tunavyojidhoofisha wenyewe kwasababu yeye mwenyewe anasema… “AMIN, AMIN, NAWAAMBIENI, MSIPOULA MWILI WAKE MWANA WA ADAMU NA KUINYWA DAMU YAKE, HAMNA UZIMA NDANI YENU”…Na zaidi ya yote unapotegemea maneno yako mwenyewe ndivyo unavyojimaliza mwenyewe na mwishowe utakufa…

Ifuatayo ni mifano michache tu ya mtu anayekula nyama ya mwili wake mwenyewe.(mawazo yake).

1) Imani ya kuamini kuwa Mungu hawezi kuiteketeza dunia na watu wote hawa..ndugu hiyo ni unajilisha nyama ya mwili wako mwenyewe.

2) Imani ya kuwa utakwenda mbinguni kwa kutenda mema tu pasipo kumwamini Bwana Yesu Kristo.

3) Imani ya kuwa ubatizo ni ubatizo tu, uwe wa maji mengi au machache haujalishi.

4) Imani ya kuwa siku moja Mungu atamsamehe shetani.

5) Imani ya kuwa hakuna Mungu wala shetani.

6) Imani ya kuwa Mungu haangalii mavazi yangu wala mwonekano wangu bali anaangalia roho yangu peke yake.

7) Imani ya kuwa Yesu Kristo harudi leo wala kesho, 

8) Imani ya kuwa hakunaga Jehanum ya moto mtu akifa amekufa tu.

9) Imani ya kuwa Biblia ni kitabu kilichotungwa na wanadamu. N.K

10) Imani ya kujiona wewe huna dhambi nyingi sana kustahili kuzimu kama yule.

Na unapotegemea maneno ya watu wengine ambao Hawamhubiri Kristo katika utimilifu wa Neno lake, ndivyo unavyokula nyama zao zilizotengenezwa kuzimu…Na mwisho wa siku unazizoelea hata unapoletewa chakula cha kweli cha uzima (yaani maneno ya Yesu Kristo) hutaki tena kusikia..Kwasababu umenenepeshwa kwa nyama hizo.

Na ifuatayo ni baadhi tu ya mifano ya Nyama zinazotengenezwa kuzimu watu wanazolishwa pasipo wao kujijua.

1) Ibada za Sanamu, hizo ni nyama kutoka kwa Yule adui…haihitaji mtu awe mchawi ndio ale nyama hiyo..Ibada hizo tu tayari ni uchawi.

2) Mafundisho ya kwenda toharani ni nyama za Yule adui. Watu wanalishwa mchana na usiku.

3) Ubatizo wa vichanga ni nyama za Yule adui.

4) Mafundisho ya ndoa za Mitara (mwanamume mmoja wake wengi).

5) Mafundisho yasiyolenga utakatifu wala Toba, badala yake yanalenga tu mafanikio na elimu za kichawi…Ni nyama za Yule adui. N.k.

Kwahiyo ndugu yangu kama umeshalishwa NYAMA zozote za aina hiyo, zieupuke sasa, na kama hujampa Yesu Kristo maisha yako, Nakushauri ufanye hivyo leo, kabla wakati wa hatari haujafika..Na yeye anakupenda na hataki upotee ndio maana anakuhitaji leo utubu, akupe uzima wa Milele. Akupa chakula chake cha uzima bure. Akupe mwili wake na damu yake halisi…Na sio nyama za mashetani.

Hivyo unachopaswa kufanya ni KUTUBU KWANZA KWA KUDHAMIRIA KUACHA DHAMBI Zako zote. Unadhamiria kuacha uasherati, uwongo, ulevi, rushwa, pornography, wizi, uvaaji mbaya, utukanaji, utoaji mimba, anasa na mambo yote uliyokuwa unayafanya yasiyompendeza Mungu, Na baada ya kufanya hivyo nenda ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kimaandiko wa kuzamishwa mwili wako wote kwenye maji na kwa jina la YESU KRISTO kulingana na (Matendo 2:38, 8:16, 10:48, na 19:5,) ili upate ondoleo la dhambi zako..Na kisha Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi na kukuongoza katika kuijua kweli yote ya kimaandiko..

Usikubali kulishwa nyama za watu wengine watakaokuambia utaokoka siku ile tu pasipo Yesu Kristo, au wanaokuambia kwamba ubatizo sio wa muhimu..Wala usikubali kula nyama za mwili wako mwenyewe zinazosema hakuna Mungu, wala hakuna jehanum,wala Yesu Kristo harudi..

Badala yake uule mwili wa Yesu Kristo unaosema… “Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa Luka 16:16” na unaosema

“ Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu upamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.

13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho”…..

Ufunuo 22:16 “Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi.

17 Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure”.

Bwana akubariki sana. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

MEZA YA BWANA, NA KUTAWADHANA MIGUU

MANA ILIYOSHUSHWA KUTOKA MBINGUNI.

CHAKULA CHA ROHONI.

HADITHI ZA KIZEE.


Rudi Nyumbani

Print this post

HADITHI ZA KIZEE.

Mtume Paulo anamwambia Timotheo “Bali hadithi za kizee, ZISIZOKUWA ZA DINI, uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa.”( 1Timotheo 4.7).

Hizi hadhithi za kizee ni zipi? (kwa kiingereza zinaitwa old wives’ tales). Ni Misemo na hadithi zilizotungwa na watu wa zamani, ambazo kwa kuzitazama kwa nje zinaonekana kama zina ukweli fulani ndani yake, lakini kimsingi hazina uhalisia wowote, ni hadithi za uongo. Karibu kila jamii zipo na naamini hata wewe ulishakutana nazo.

Kwa mfano embu jaribu kutafakari maneno haya ambayo pengine ulishawahi kuyasikia.

* Ukiwa unakojoa hakikisha unatema mate chini, vinginevyo mama yako atavimba matiti.

* Mtoto mchanga akiangalia kioo haoti meno,.

* Mtu akikuruka hutorefuka.

* Mtoto wa kike akikaa katikati ya mlango, hatoolewa

* Ukipita makaburini, ukanyoosha kidole chako kuelekea kule, king’ate mpaka kiume vinginevyo mama/baba yako atakufa.

* Binti akipika huku aimba, ataolewa mbali.

* Mwanaume asilie kwenye sufuria la sivyo siku ya ndoa yake mvua nzito itanyesha.

* Ukimuona albino usipojitemea mate kifuani mwako, basi wewe nawe utazaa albino. n.k N.K. zipo nyingi.

Sasa mambo haya, yameaminika kwa wengi, mpaka imefikia hatua licha tu ya kubakia kwenye jamii ya watu wasiomini (yaani watu wasio wakristo), sasa imefikia mpaka kwa watu wanaomfahamu Mungu, waliookoka . Siku moja nilisikia mtu mmoja anayejiita mtumishi wa Mungu kwenye Whatasapp, anaitwa Apostle Vincent Mkalla(samahani kwa kulitaja jina) akitoa ujumbe ambao umesambaa sana mitandaoni na unajulikana na wengi, katika ujumbe huo, alitoa habari ya mti mmoja ujulikanao kama mti MWAMVULI, akisema mti huu, ukiwa umepandwa nyumbani, basi fahamu kuwa utaleta mabalaa makubwa katika hiyo nyumba, anasema kwanza kabisa ukichunguza utaona kuwa baba ya nyumba hiyo lazima afe, pili, unaleta hali ngumu za kiuchumi katika familia, tatu unaleta magonjwa, na pia unasababisha familia kutawanyika, familia kuwa na madeni, pia watu wa nyumba hiyo wanajikuta wanapitia katika hali ya kulaumiwa pasipo kujua chanzo ni nini n.k.…na mambo mengine aliyoyasema pale kuhusiana na mti..

 

Lakini kilichonisikitisha zaidi wakati huo nilipokuwa ninasikiliza nilikuwa na mama mmoja, ambaye naye alikuwa anausikiliza kwa makini sana, kwa hofu akiamini kinachozungumzwa pengine ni kweli, na siku chache mbeleni nilikwenda nyumbani kwao, ambapo mti huo wenye kivuli ulikuwa umepandwa uwani, nikakutwa umekatwa, hali kadhalika niliporudi nyumbani kwetu kwa mama, nikakutwa umekatwa,maana hata nyumbani upo, na sehemu nyingine nyingi.. Kwa hofu kwamba madhara yatokanayo na mti huo waliosikia kutoka kwa mtumishi huyo wa Mungu yasiwakute.

Kaka/Dada hizi ni nyakati za mwisho na biblia inasema..

1 Timotheo4 : 1-2”Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wenginewatajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;

2 kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;

Hizi ndizo siku hizo za mwisho, Na hizi ndio HADITHI ZA KIZEE ZISIZO ZA DINI Mtume Paulo anamwonya Timotheo ajiupushe nazo, ni mafundisho ya mashetani, hadithi ambazo zinafanya watu wapoteze shabaha ya kuujua uweza wa Mungu bila wao kujua wakidhani kuwa vitu vya asili vinaweza kuathiri hatma zao na sio mambo ya rohoni. Na hilo ndio linalowafanya wengi mpaka kufikia hatua ya kuabudu sanamu, kwasababu imani yao kidogo kidogo ilianza kuhamishwa kutoka kwa Mungu, na kuanza kuangalia mambo ya mwilini kama suluhisho la mambo yao na matatizo yao. Mwisho wa siku hata mtu akiwambiwa kaoteshe mkaratusi katikati ya shamba lako utapata hela atakwenda na kufanya hivyo kwasababu siku nyingi tayari alishahamishwa Imani yake kutoka katika Neno la Mungu na kuingizwa katika “Maashera” (ibada za masanamu), na pasipo yeye kufahamu hajui kuwa anamwabudu shetani mwenyewe..

Dada yangu tena sikumoja ananiambia ukiona mjusi au mende, kwenye nyumba hiyo ni ishara mbaya, ya kutokufanikiwa kiuchumi.

Siku nyingine nikakuta Ua moja ambalo sikujua maana yake, mpaka siku moja mama yangu mdogo ambaye amesema ameokoka aliponiambia ua lile, ni la Baraka linaeleza hali ya kiuchumi ya nyumba hiyo,likistawi basi uchumi unastawi, likisinyaa basi uchumi ni mdogo..Niliposikia vile nilisikitika sana rohoni.

Kumbukumbu 16:21 “Usipande mti uwao wote kuwa Ashera kwako kando ya madhabahu utakayofanya ya Bwana, Mungu wako”.

Sasa Yapo mambo mengi hatuwezi kuyasema yote hapa, yanafundishwa na baadhi ya watu wanaojiita ni watumishi wa Mungu na yanazidi kukithiri, na kusambaa, naamini hata na wewe ulishakutana yao.

Ndugu nataka nikuambie ukweli wa kibiblia hakuna ubaya wowote katika miti, ikiwa imepandwa kwa nia njema, hakuna ubaya wowote wa vyakula vya aina Fulani, ikiwa navyo vimepokelewa kwa shukrani kama biblia inavyosema, vyote vinatoka kwa Mungu, na vimeumbwa na Mungu..Kusema mti Fulani unasababisha kifo cha baba wa nyumba, jiulize ni nyumba ngapi duniani zimefiwa na wazazi wao,

Unaposema miti inasababisha hali mbaya kiuchumi ni familia ngapi duniani zinapitia matatizo ya kiuchumi?. Ndugu yangu, chanzo cha matatizo yote ni DHAMBI, na kutokumjua Kristo na uweza wake, lakini badala yake, wanafundisha chanzo cha mafarakano na magombano katika familia ni MITI, tangu lini mti ukimfarakanisha mtu na mtu?..Na mtu huyo anajiita ni mtumishi wa Mungu, na bado tena mkristo anamwamini mtu wa namna hiyo kisa tu katumia vipengele fulani vya maandiko kutibitisha uongo wake, na wengi wanamwamini, hujui kuwa hata shetani alitumia maandiko kuuthibitisha uongo wake kwa Yesu kule jangwani.

Hofu zimewakubwa watu wengi mpaka sasa, kila kitu wanachotokea hata kujikwaa kidogo tu anasema kalogwa, akipishana na paka, kuna mtu kamwendea kwa mganga, akipishana na mbwa mweusi usiku basi ni mchawi, sasa mbwa wa kweli atakuwa ni yupi? Kama kila mbwa ni mchawi, bundi wa kweli aliyeumbwa na Mungu atakuwa ni yupi kama wote ni wachawi, paka wa kweli aliye mweusi ambaye aliumbwa na Mungu atakuwa ni yupi kama kila paka mweusi ni mchawi,?…utasikia mwingine anakuambia jicho likicheza kidogo tu anasema kuna mtu anamsema, akipiga chafya kuna watu wanamtakia mabaya, huyo ni mkristo anazungumza maneno hayo. ..HADITHI ZA KIZEE zisizo na dini…

2 Timotheo 4.3 “Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti;

4 nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.

5 Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako.”

Timotheo kama mwalimu alionywa ajiuepushe na injili za namna hiyo, hali kadhalika azikatae, azikemee zisifundishwe katika kanisa la Mungu, na sisi leo tunazikemea na tunazikataa zisifundishwe kwa watu..Leo watu wengi wanafahamu zaidi habari za uchawi na ushirikina kuliko hata kumjua Mungu, shuhuda zilizojaa kwenye kichwa vya watu ni uchawi tu, kana kwamba huo ndio msingi wa kuwa mtu wa rohoni. Na hiyo inapelekea watu kuwa WAOGA kwa shetani, kwasababu mioyo yao imejazwa shuhuda za shetani zaidi kuliko Mungu, Mtu anaogopa hata kusalimia, au kumsaidia mtu asiyemjua kwa hofu tu ya uchawi, lakini haogopi maneno ya Mungu yanayomkataza yeye kwenda kutenda dhambi za makusudi. Na siku zinavyozidi kwenda hofu hii inazidi kuongezeka katikati ya watu..(hususani wanaojiita wakristo).

Hivyo hata ukiwaeleza nguvu zilizokatika Neno la Mungu, haziwasaidii sana, kwasababu mioyo yao haijajazwa na Neno la Mungu bali Neno la Shetani. Kwasababu biblia inasema Hazina yako iliyo ndipo utakapokuwepo na moyo wako. Na hivyo kila elimu inayokuja inawachukua..leo hata wakiambiwa wasipange mchicha kwenye nyumba zao zinawaletea umaskini watafanya hivyo, kesho wakiambiwa wasitumie mafuta ya nazi ya roho za majini watatatii, kesho kutwa wakiambiwa wakate kidole gumba kinawaletea mikosi na wakithibitishiwa na maandiko mawili matatu, watafuata..kwasababu ndani yao kumjua Mungu hakupo..Biblia inasema Tumjue sana Mungu ili tuwe na AMANI sio tumjue sana shetani ndio tuwe na Amani…Elimu ya shetani haileti amani bali hofu.

Mtu akija kukuambia leo, kuna bundi nimemwona batini kwako jana usiku, na ni mchawi…kitakachofuata hapo ni hofu, na wala si kitu kingine, utaanza kuiogopa hata nyumba yako unayoishi…

Lakini leo hii utakaposikia elimu iliyopo katika uweza wa Mungu…Kwamba Kristo alitwaa madhaifu yetu na yeye anatupenda kiasi cha kutuhurumia, na tena anatuambia tuutafute kwanza ufalme wake na haki yake, Hakuna hata unywele wetu mmoja utakaopotea, na zaidi ya yote anatuambia sisi tuliomwamini kuwa Baba yetu wa mbinguni anatujali sisi kuliko baba zetu wa kimwili..Mambo hayo ukiyajua yanakupa amani na furaha katika wokovu…na hayakufanyi kuwa mateka zaidi yanakufanya kuwa huru, elimu ya mashetani ndio inayokufanya kuwa mateka, na matunda ya roho ya shetani ndio haya..uwoga, hofu, mashaka, kukosa raha, uchungu, wasiwasi,visasi, wivu, hasira, chuki n.k mambo haya yote yanazalishwa na roho za mashetani kupitia elimu zake. Na shetani ndio anataka mambo hayo yawepo ndani ya mtu, ili apate nafasi ya kumkandamiza kimawazo na kiakili, Lakini Roho Mtakatifu ndani ya mtu, hayupo hivyo na wala matunda yake hayapo hivyo ….matunda ya Roho wa Mungu ndio haya..

Wagalatia 5: 22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”.

Hizi ni nyakati za hatari ndugu yangu, mafundisho kama hayo yatazidi kuongezeka, hayataishia kwenye miti, wanyama, na vyakula, yataendelea mpaka kwenye mwili wako, na maumbile yako..Hivyo usipokuwa makini kwa kutaka kukaa chini na kujifunza zaidi uweza wa Mungu katika Neno lake, KUMJUA SANA MWANA WA MUNGU (Waefeso 4:13)…badala yake unapenda kutafuta njia za mwilini kutatua matatizo yako nataka nikuambie ukweli wote, shetani atakutesa sana, utakosa raha ya kuishi hata kama unajiita umeokoka… na mwisho wa siku utachukuliwa na wimbi hilo na manabii, na waalimu wa uongo, ambao hao Injili ya kweli ya Kristo ipo mbali nao.

Sina muda wa kutosha ningekupa mifano kadha wa kadhaa ya hawa watumishi wa shetani ambao mimi binafsi nimewahi kukutana nao..ambao wengine wanatumia mifupa, na nywele, na biblia kuchukua watu mateka na sana sana wanawake kwasababu wao ndio sana sana wanahangaika huku na kule kutafuta mambo ya rohoni…Watumishi hawa ni ngumu sana kuwagundua kwasababu shetani kawanoa vya kutosha kama hujui maandiko wanakuchukua…na target yao kubwa ni wanawake…

1 Timetho 3:5 “…wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.

6 Kwa maana katika hao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu, na kuchukua mateka wanawake wajinga wenye mizigo ya dhambi, waliochukuliwa na tamaa za namna nyingi;

7 wakijifunza siku zote, ila wasiweze kabisa kuufikia ujuzi wa kweli.

8 Na kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani”.

2 Petro 1.16 “Maana hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake”.

Kristo alipokuwa duniani hakutuelekeza katika miti, wala vyakula, wala wanyama, wala hakutuhubiria habari za washirikina na wachawi, badala yake alitumia muda mwingi kutufundisha jinsi ya kuwa na mahusiano ya karibu na Baba yetu wa mbinguni kama yeye alivyokuwa kwa baba yake..Na hilo ndio jambo la muhimu kwasababu ukishajua nafasi yako kwa Mungu wako basi hayo mambo mengine hayatakusumbua, hutakuwa na hofu, ya kifo, au matatizo, au shida, au chochote kile kwasababu baba yako atakuwa pamoja na wewe wakati wowote kukusaidia…hutakimbilia kwenda kuisingizia miti, na paka, na mbwa, na bundi, na mijusi, na popo, na fisi, kwa hali unayoipitia…Badala yake Mungu ndiye atakayekuwa jibu lako wakati wote.

Hivi unajua kwamba wapagani wasiomjua Mungu, hawakuanza hivi hivi kuabudu miti na mawe?..unalijua hilo?..walianza kidogo kidogo kufikiri tatizo Fulani linasababishwa na miti Fulani au mawe Fulani, na walipoisafisha ile miti na yale mawe waliona kama matatizo yameondoka lakini walipoona kuwa kuna mengine ni sugu..waliona njia pekee ni kwenda kwa unyenyekevu chini ya hiyo miti..kuiomba kwa upole na utaratibu iwaondolee hayo matatizo na endapo hayo matatizo yataondoka basi wanaahidi kuifanyia jambo Fulani labda kuipa heshima Fulani..na kwasababu ni shetani yupo nyuma ya ule mti..anaondoa lile tatizo lao kwa muda na wale wanadhani ni mti umesikia maombi yao, hivyo wanaugeuza ule mti kuwa mungu wao..na shetani anatuma maroho yake kuwaingia wale watu wakati mwingine wanaanza kuota ndoto zinazoutukuza ule mti au wengine wanaona vitu vya ajabu kwenye ule mti n.k..lengo ni kutoa umakini wao kumhusu Mungu wa Mbinguni na kuwaleta kuamini miti na mawe kama miungu…Na haishii hapo akishajua watu wameuamini ule mti kupita kiasi..anawapa mpaka nafasi ya wao kuomba maombi yao au kupeleka mahitaji yao kwenye ule mti na akawafanyia…

Sasa roho hiyo hiyo ndio inayoingia kwa kasi katika kanisa katika siku hizi za mwisho, wengi wanaingizwa kwenye ibada za sanamu pasipo wao kujijua, shetani anahamisha umakini wa watu kumhusu Mungu wa Kweli wa Mbinguni na kuwatengenezea watu miungu ya kuiabudu, miti, mawe, sanamu n.k

Warumi 8: 35 “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?……..

38 Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,

39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu”.

Ni matumaini yangu kuwa umepata kitu na utazidi kuchukua tahadhari juu ya hizi HADITHI ZA KIZEE, na kuanza kumtazama Mungu ili njia zetu ziwe zimenyooka siku zote.Na tuwe na Amani.

Ubarikiwe. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

MAFUNDISHO YA MASHETANI

SI SHETANI BALI NI WEWE. (CHAGUA MEMA)

CHANZO CHA MAMBO

JINSI WATU WANAVYOZAMA KATIKA USHIRIKINA NA UCHAWI.


Rudi Nyumbani

Print this post

UFUFUO WA UZIMA NA WA HUKUMU.

Shalom, Mtu wa Mungu karibu tujifunze Injili, uweza wa Mungu uuletao wokovu, leo tutajifunza kwa ufupi juu ya NGUVU YA UFUFUO ILIYOPO NDANI YA YESU KRISTO. Katika kitabu cha Yohana tunasoma maneno yafuatayo aliyoyazungumza Bwana Yesu.

Yohana 5: 25 “Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja,na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai.

26 Maana kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake.

27 NAYE AKAMPA AMRI YA KUFANYA HUKUMU KWA SABABU NI MWANA WA ADAMU.

28 Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini WATAISIKIA SAUTI YAKE.

29 Nao watatoka; wale waliofanya MEMA KWA UFUFUO WA UZIMA, na wale WALIOTENDA MABAYA KWA UFUFUO WA HUKUMU”.

Katika mistari hiyo Biblia inasema Mwana kapewa amri na Baba ya kufanya hukumu na tena amepewa uwezo wa kufufua wafu kama vile Baba alivyo na uwezo wa kufufua wafu, tunayasoma hayo juu kidogo katika Yohana 5: 21 “Maana kama Baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, vivyo hivyo na MWANA AWAHUISHA WALE AWATAKAO”.

Kama wengi wetu tunavyofahamu kuwa kuna ufufuo utakaokuja baada ya maisha haya kuisha ambapo wale wote waliotenda haki watafufuliwa na kuurithi uzima wa milele, na wale wote waliotenda mabaya watafufuliwa kwaajili ya hukumu, na kila mmoja atahukumiwa kulingana na matendo yake na wale waovu watatupwa katika lile ziwa la moto, lenye moto usiozimika, waangamie milele.

Sasa jambo la kujiuliza hapa ni kwanini, Bwana Yesu awafufue wale waovu na kisha awahukumu na awatupe katika ziwa la moto…kwanini asingewaacha huko huko mautini, awahukumu huko huko na kuwatupa kwenye lile ziwa la moto wakiwa huko huko mautini, kuna umuhimu gani au haja gani ya wao kufufuliwa na tena wakati kuzimu wataenda tu??.

Kuna siri nzito sana hapo. Lakini kwa ufupi ni kwamba, siku ile ya hukumu watu wote waovu watavaa miili yao waliyokuwa nayo hapa duniani..yenye damu na mifupa na macho na moyo, na kusimama mbele za Bwana, na kisha kuongea naye ana kwa ana, kutoa hesabu kwa kila jambo na kila uovu waliokuwa wanaufanya, mbele ya kiti cha Hukumu…Jambo hilo halitafanyika mtu akiwa katika roho, hapana bali litafanyika mubashara kabisa katika mwili kama tulivyo hapa duniani…Na katika ziwa la moto mtu hatatupwa katika roho, bali atatupwa akiwa na mwili wake wa damu na nyama, na utaungua kule na ukiisha ndipo roho itaendelea nayo kuteseka milele kwenye huo moto milele.

Kwahiyo leo hatutaingia sana huko, lakini napenda tujifunze Nguvu ya ufufuo.

Ukiutafakari kwa makini mstari huo utakuja kugundua kuwa Kumbe Ufufuo sio tija. Kwasababu watu wote watafufuliwa, waovu na wema..kinachojalisha ni sababu ya kufufuliwa kwako. Kama mtu alikuwa mcha Mungu basi ufufuo kwake utakuwa wa maana, lakini kama alikuwa mwovu basi ufufuo kwake utakuwa ni laana.

Na ufufuo maana yake, ni “kukirudishia tena uhai au maisha kitu kile kilichokuwa kimekufa”..hiyo ndio maana ya ufufuo.

Sasa kuna ufufuo wa roho ambao unaendelea sasahivi, ambapo watu wote WANAISIKIA SAUTI YA MWANA WA ADAMU, na wanafufuka kutoka kwa wafu katika roho…Na sauti ya mwana wa Adamu ni Habari njema inayohubiriwa duniani kote leo, habari za msalaba na wokovu uliopo katika Kristo Yesu, sasa wapo ambao wanafufuka kwaajili ya uzima wa milele na wapo ambao wanafufuka kwaajili ya hukumu.

Wako ambao pindi tu wanapoisikia injili macho yao yanafumbuliwa (wanafufuka katika roho), hii inatokea pale ambapo wanachomwa dhamiri zao ndani ya mioyo yao, na kujijua kuwa njia zao sio sawa, hivyo kwa moyo mnyoofu wanaitii injili na kuokoka kikamilifu,wanaacha njia zao mbaya za kale, na kuzaliwa mara ya pili wakati huo huo na kuwa viumbe vipya.

Na wapo pia ambao wanapoisikia tu injili macho yao yanafunguka (wanafufuka) na kujua kabisa ndani ya mioyo yao Neno la Mungu ni kweli, na Roho Mtakatifu anawashuhudia kabisa kuwa Njia ya wokovu ni hii, na njia wanayoiendea wao sio sawa…Roho anawafufua katika roho zao, lakini kwasababu wanapenda giza kulika Nuru wanaikataa ile njia ya kweli,..na kwa makusudi, hawataki kugeuka na kutubu, wanaendelea na njia zao mbaya, hawa ndio wanaofufuliwa sasa kwa ajili ya hukumu. Wanayafumba macho yao kwa makusudi ingawa wamepewa neema ya kuona..Wanafahamu kabisa hata wakifa sasa hivi wanastahili Jeahanum ya Moto, lakini bado hawataki kutubu. Hawa wamefufuliwa kwa ajili ya Hukumu.

Kwahiyo ndugu unayesoma ujumbe huu, usifurahie tu Roho wa Mungu anapokushuhudia ndani yako kuwa KRISTO ndiye njia ya kweli na uzima, huo ni ufufuo tu! Ambao hata waovu wanapewa…hata waovu katika nyakati hizi za mwisho wanapewa neema hiyo mioyoni mwao kujua kuwa Kristo ni njia ya kweli na uzima, na kwamba hakuna uzima wowote nje yake yeye.. Hiyo ni neema ya ufufuo ambayo watu wote wanapewa waovu na wema..Lakini swali ni je! Unafufuliwa kwa sababu gani?.

Kama unaisikia injili kila siku inayokuambia ulevi, uasherati, utukanaji, rushwa,uvaaji mbaya ni dhambi, mustarbation, usagaji, na pornography…na ndani ya moyo wako unajua kabisa ni kweli ni dhambi kufanya mambo hayo..fahamu tu! Ufufuo uliopewa ni wa hukumu na sio wa uzima wa milele, haijalishi unayajua maandiko kiasi gani, au umezungumza na malaika kiasi gani,au umemwelewa Kristo kiasi gani, au umeponywa na Yesu kiasi gani,

Mtume Paulo kwa uwezo wa Roho aliandika habari za watu hawa wafanyao dhambi kwa makusudi huku wakijua kabisa wanayoyatenda sio sawa…Wameisikia injili (wakapata ufufuo katika roho zao)..lakini ufufuo wao ukawa ni wa mauti.

Warumi 1: 18 “Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu.

19 Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, KWA MAANA MUNGU ALIWADHIHIRISHIA.

20 Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; HATA WASIWE NA UDHURU

21 kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza.

22 Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika;

23 wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo.

24 Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao.

25 Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina.

26 Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili;

27 wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.

28 Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.

29 Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya,

30 wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao,

31 wasio na ufahamu, wenye kuvunjamaagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema;

32 ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao”.

Unaona Biblia inasema..”kwa maana walipomjua Mungu hawakumtukuza” na inasema “Mungu aliwadhihirishia ndani yao”..ikiwa na maana kuwa watu hawa, nuru ya haki iliwazukia ndani yao, au kwa lugha nyepesi tunaweza kusema ufufuo ulipita ndani ya roho zao, wakaiona kweli na kuiamini lakini walipoiamini hawakuifuata!..Hilo ndio jambo la kuogopesha, mtu anauona ukweli lakini haufuati…Nimewahi kuona madaktari bingwa ambao wanajua elimu yote ya biolojia ya ini na figo, na ni washauri wazuri wa kushauri watu wasitumie pombe na sigara kwani ni hatari kwa afya zao, lakini wao ndio watumiaji wakubwa wa mambo hayo, na wanakufa kwa magonjwa hayo hayo…Na ukiwauliza kwanini wanafanya hivyo na hali wanajua kwa kina na mapana madhara ya hivyo vitu katika mwili, zaidi hata ya watu wengine wanavyojua…wanakujibu basi tu! Nimeamua na nimependa kufanya hivyo, na atazidi kukuambia yupo tayari kufa na wala haogopi.

Sasa watu wa namna hii pia wapo katika Kanisa la Kristo, wanajua kabisa uzinzi ni dhambi, kwamba waasherati wote sehemu yao ni katika lile ziwa la moto, na wengine wamepewa maono na ndoto za jehanamu wameonyeshwa mahali wanawake wanaovaa vimini na suruali walipo lakini hao hao utawakuta wanaendelea kufanya hivyo bila uoga wowote. Ni kwasababu gani wanafanya hivyo? Ni kwasababu wapo katika ufufuo wa hukumu. Mpaka unaweza ukasema kwanini Mungu awafunulie mioyo yao waiamini injili halafu na bado wasiifuate si ni bora asingewapa kabisa neema hiyo..kuliko kuwapa halafu wasiifuate?..Jibu ni rahisi… “kila mtu lazima aisikie sauti ya mwana wa Adamu na kutoka kaburini aliko”.

Kadhalika pia usifurahie kwasababu kazi yako iliyokuwa imekufa ikafufuliwa tena, kwasababu huo unaweza ukawa ni ufufuo wa mauti kwako, furahia kazi yako kufufuka kwa ajili ya ufufuo wa uzima..

Unapokwenda kuombewa kazi yako au afya yako na kupona, na kisha maisha yako hayageuki hata kidogo, zaidi ya yote ndio unakuwa mbaya kuliko ulivyokuwa hapo kwanza, hujisikii vibaya kuendelea na uasherati wako, wala kiburi chako, nataka nikuambie hiyo ni dalili moja wapo ya kazi yako kufufuliwa kwa ajili ya hukumu yako mwenyewe,..hiyo kazi yako yako itakuwa kitanzi kwako cha kukuua na hatimaye kukupeleka katika ziwa la moto…Biblia inasema “…Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza Mithali 1:32”.

Kwahiyo furahia pale kazi yako inapofufuka na kustawi na inazidi kukufanya kuwa mtakatifu na mkamilifu mbele za Mungu, mali zako zinapoongezeka ndipo na kiwango chako cha usafi kinavyozidi kupaa..hapo kazi yako itakuwa imefufuliwa kwa ufufuo wa uzima. Haitakupeleka jehanamu.

Bwana akubariki sana, kama hujampa Yesu Kristo maisha yako…usikawie kawie, kama amezungumza nawe moyoni mwako zaidi ya mara moja na kukushuhudia kuwa njia unayoiendea sio sawa, na wewe mwenyewe umehakikisha jambo hilo moyoni mwako, usijaribu kwenda kutatufa visababu vya kujihalalishia njia zako. Mtii leo, yeye anawakubali wakosaji, na anasamehe dhambi, akikusamehe amekusamehe kweli kweli hana visababu sababu vidogo vidogo vya kukushitaki tena au kukulaumu..Unakuwa mpya kabisa mbele zako.

Waefeso 5.14 “Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza.”

kwahiyo Hapo ulipo tubu, dhamiria kuacha dhambi zote ulizokuwa unazifanya nyuma, Fufuka sasa katika ufufuo wa Uzima katika jina La Yesu, na sio ufufuo wa Mauti, mfanye Bwana kuwa tumaini lako kuanzia leo na kuendelea.. Na baada ya kutubu katafute ubatizo kwani ni wa umuhimu sana kukamilisha wokovu wako na ni maagizo ya Bwana mwenyewe aliyoyatoa kwamba ni lazima kila mtu aliyempokea yeye akabatizwe, na ubatizo sahihi ni wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kulingana na Matendo 2:38, na Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi na kukuongoza katika kuijua kweli yote ya maandiko.

Bwana akubariki. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

UFUFUO WA UZIMA NA WA HUKUMU

UTALIPWA KATIKA UFUFUO WA WENYE HAKI

KUNA UFUFUO WA AINA NGAPI?

WALE WATAKATIFU WALIOFUFUKA NA BWANA YESU WALIKUWA WAPI KABLA YA KUFUFUKA KWAO?

NIFANYE NINI ILI NIIKWEPE HUKUMU


Rudi Nyumbani

Print this post

MADARAKA YA WAKATI MKAMILIFU.

Shalom mtu wa Mungu, ni kwa rehema za Bwana tumeiona siku ya leo, hivyo hatuna budi kumshukuru sote pamoja kwa mema anayotutendea na pia kushiriki katika kujifunza maagizo yake kila iitwapo leo. Hivyo nakukaribisha tutafakari kwa ufupi juu ya haya “madaraka ya wakati mkamilifu” yanayozungumiwa kwenye maandiko, tutayaona ni yapi, na yatakuja wakati gani?.

Biblia inasema.

Waefeso 1:9 “akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo.

10 Yaani, KULETA MADARAKA YA WAKATI MKAMILIFU atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu VYA MBINGUNI na vitu VYA DUNIANI pia. Naam, katika yeye huyo;

11 na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake.”

Sasa Kama ukisoma huo mstari wa 10 kwenye tafsiri nyingine za biblia kwa lugha iliyo nyepesi unaweza kusomeka hivi,

“Wakati mkamilifu utakapofika, basi vitu vyote ya mbinguni na duniani vitajumuishwa pamoja kwa yeye huyo..Au wakati uliokusudiwa (wa Mwisho) basi mambo yote ya mbinguni na ya duniani yataletwa pamoja katika yeye huyo (KRISTO YESU)..”

Ndugu tukimjua Kristo, na ukuu wake na uweza wake, basi hatutaishi maisha ya kutokujali tu, tukiwa hapa duniani, hatutauchukulia ukristo wetu kama kitambulisho cha dini tu kama wengine wanavyofanya badala yake tutaishi kwa mitume wa zamani walivyoishi,..Leo Tunaishi maisha ya uvuguvugu na machafu kila siku na huku bado tunajiita ni wakristo, ni kwasababu tumekosa ufunuo wa kumjua Yesu Kristo ni nani katika maisha yetu, tumekosa shabaha ya kufahamu ni mambo gani na gani yalimfanya Yesu kuja duniani, tunadhani alikuja kufa tu msalabani halafu basi, na sasa ameketi mkono wa kuume wa Mungu mbinguni akisubiria kurudi tena kuja kunyakua watu wake….Hatujui mengine zaidi ya hayo.

Hiyo ndio sababu inayotufanya tunaishi maisha ya kuukinai wokovu, tunaposoma habari za watu ambao walijitoa maisha yao, watu ambao hawakupenda maisha yao hata kufa kwa ajili ya Bwana, tukisoma habari ya Ibrahimu ambaye japo Mungu alimpa kila kitu lakini aliishi kama mpitaji hapa duniani kukaa kwenye mahema, akiutazamia mji wenye misingi (YERUSALEMU MPYA),sio hii ya sasa inayoharibika,(Waebrania 11:8)…watu ambao Mungu aliwapa kila kitu lakini hawakupumbazwa na vitu walivyopewa, macho yao wakati wote yalielekea juu, mfano wa Ibrahimu na Ayubu…Sio kana kwamba walikuwa hawajipendi hapana bali waliona mbele, walipokea ufunuo wa mambo yanakuja na hivyo wakaanza kujijengea misingi mizuri kuanzia hapa duniani ili wakifika kule, iwe heri kwao. Lakini sisi tunaona wokovu ni kama kitu-baki, ni kitu tu cha ziada, na sio kila kitu katika maisha yetu.

Hatujui kuwa Kristo sasa yupo katika hatua za mwisho kabisa za kutimiliza mambo yake yote, na yeye mwenyewe hakutuficha siku anakwenda kwa Baba alisema, “ninakwenda kuwaandalia makao”,

Sasa ni vizuri kufahamu kuwa Kristo alipokuwepo duniani alikuja kufanya upatanisho wa kitu vikuu vitatu.

1) UPATANISHO KATI YA SISI KWA SISI

2) UPATANISHO KATI YA SISI NA MUNGU

3) UPATANISHO KATI YA MBINGU NA DUNIA.

Kristo alikuja kutupatanisha sisi kwa sisi, kumbuka hapo mwanzo wayahudi (yaani Waisraeli) walikuwa hawachangamani na mataifa kabisa, Israeli limekuwa likijulikana ni Taifa teule la Mungu, Mungu alilolibariki kupitia Ibrahimu. Ilikuwa hakuna namna yoyote ile sisi watu wa mataifa tungeweza kumfikia Mungu, lakini kwa kupitia Bwana Yesu, sisi ambao tumezaliwa mara ya pili ni mamoja sawa na wayahudi, mbele za Mungu hakuna aliye juu ya mwenzake, bali wote tunakubaliwa sawa kwa kupitia damu ya Kristo. Hiyo ni nafasi kubwa sana ya upendeleo..Jaribu kufikiria taabu walizozipata wengine kwa muda mrefu sisi tunakuja kuzila kiuwepesi namna hiyo. Ni neema kubwa sana. Jambo hilo unaweza kulipata katika kitabu cha Waefeso..

Waefeso 2: 11 “Kwa ajili ya hayo kumbukeni ya kwamba zamani ninyi, mlio watu wa Mataifa kwa jinsi ya mwili, mnaoitwa Wasiotahiriwa na wale wanaoitwa Waliotahiriwa, yaani, tohara ya mwilini iliyofanyika kwa mikono;

12 kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani.

13 Lakini sasa, KATIKA KRISTO YESU, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo.

14 Kwa maana yeye ndiye amani yetu, ALIYETUFANYA SISI SOTE TULIOKUWA WAWILI KUWA MMOJA; AKAKIBOMOA KIAMBAZA CHA KATI KILICHOTUTENGA.

15 Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani.

16 AKAWAPATANISHA WOTE WAWILI NA MUNGU KATIKA MWILI MMOJA, KWA NJIA YA MSALABA, AKIISHA KUUFISHA ULE UADUI KWA HUO MSALABA.

17 Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu.

18 Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja.

19 Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu”.

Hali kadhalika Kwa kumwamini tu Yesu na uweza katika damu yake, basi moja kwa moja tunakuwa tumepatanishwa na Mungu na hivyo tunakuwa na uwezo wa kupakaribia patakatifu pa patakatifu mahali Mungu alipo juu sana, na kuzungumza naye uso kwa uso katika roho, na kupokea rehema itokayo kwake. mambo ambayo hapo mwanzoni hayakuwepo, ilikuwa ni kuhani mkuu tu, alipelekea maombi yake katika maskani iliyofanywa na wanadamu huku chini mfano wa ile ya mbinguni, kisha Kerubi wa Mungu pale chini ndiye aliyekuwa anayachukua hayo maombi na kuyasogeza mbele ya kiti cha enzi cha Mungu huko juu mbinguni, lakini sasa kwa kupitia damu ya Yesu, sisi wenyewe tuingia moja kwa moja mbinguni kwa damu ya Yesu, na kupeleka haja zetu na majibu ya maombi yetu, sawa tu na makerubi na malaika wa Mungu walio mbinguni, sisi na wao hatuna tofauti yoyote, mbele za Mungu tukiwa ndani ya Kristo ni kitu kimoja.

2 Wakorintho 5: 17 “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.

18 Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, ALIYETUPATANISHA SISI NA NAFSI YAKE KWA KRISTO, NAYE ALITUPA HUDUMA YA UPATANISHO;

19 yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho”.

Na Jambo lingine la mwisho Kristo aliloleta NI KUIJUMUISHA MBINGU NA NCHI KUWA KITU KIMOJA..vitu vya mbinguni na vitu vya dunia, Sasa Hakuna yoyote ambaye angeweza kufanya jambo hili, inahitaji nguvu ya ajabu inayovuka viwango vya fikra za kibinadamu, inahitaji iwe muumba kufanya shughuli hii..

Wakolosai .1:9 “Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae;

20 na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; KWA YEYE, IKIWA NI VITU VILIVYO JUU YA NCHI, AU VILIVYO MBINGUNI”.

Sasa jambo hilo ndilo linalokuja kutokea katika WAKATI MKAMILIFU ULIOKUSUDIWA, Yesu aliposema naenda kuwaandalia makao, ili nilipo mimi na nyinyi muwepo, na makao hayo yamegawanyika katika sehemu tatu, ya kwanza ni makao ya roho zetu ambayo hata sasa sisi tuliopokea Roho Mtakatifu tupo ndani yake,

Waefeso 2: 6 “Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu;

Na makao ya pili ni MIILI MIPYA ambayo tutaipokea tukifika mbinguni miili isiyoharibika, na makao ya tatu ndio hiyo NCHI MPYA NA MBINGU MPYA…Ambayo hiyo sasa itashuka kutoka mbinguni na kutua hapa duniani…Itashuka Hapa hapa duniani hatutaishi mbinguni milele, makao yetu yatakuwa ni hapa maandiko yanasema hivyo.

Na ndio hapo hilo neno linalosema “atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia.” Ndipo litakapotimia,

Ndugu yangu Kristo anayo nafasi kubwa sana maishani mwetu, kwanza kati yetu sisi wanadamu, pili kati yetu sisi na Mungu na tatu kati ya makao yetu ya sasa na ya yale ya baadaye..Embu jaribu kufikiria, ikiwa leo hii hutaweza kuzishiriki Baraka za Ibrahimu tu ambazo Mungu alimwahidia yeye na uzao wake (Wayahudi) kuwa watakuja kuirithi nchi, japo kweli walikuwa vile lakini bado hawakuweza kumkaribia Mungu, sasa wewe ambaye sasa ni mtu wa mataifa na bado huna habari na Kristo siku ile utaonekania wapi?..Itawezekanikaje kumfikia Mungu, au utamshawishi vipi Mungu hata akusikie maombi yako sasa wewe ambaye unasua sua katika mawazo mawili.

Hujapatanishwa, na Wayahudi, hujapatanishwa na Mungu, bado hujapatanishwa na hayo makao mapya yanayokuja huko mbeleni, unatagemea vipi, Mbingu utaiona ndugu?. Matumaini yako ni nini?, tegemeo lako lipo kwa nani?…

Muda umekaribia wa madaraka ya wakati mkamilifu kuanza, Kristo kuvileta vitu vyote pamoja, chini ya mikono ya MUNGU..lakini wale wote wanaopinga, biblia inasema kitakachosalia kwao ni kuangamizwa milele.

Yesu yupo mlangoni ndugu yangu, fanya uamuzi sasa, wakati ndio huu, pokea kuponi yako sasa ya kuwa na uhakika wa maisha baada ya kufa, ulimwengu huu unaousumbukia unakuahidia nini miaka yako 100 mbeleni kama sio ukomo wa mauti?.

Kwanini usikubali NEEMA HII YA UPATANISHO inayokuja kwako bure, ingekuwa ni wanadamu ungejaza fomu ngapi ili ukubaliwe tu uwe raia wa taifa fulani?, ungejaza fomu ngapi ili ukubaliwe kuwa mrithi wa taifa fulani?, ungejaza form ngapi ili ufikie tu kigezo cha kumfika raisi wa taifa fulani?. Lakini kwa Mungu haipo hivyo, vyote hivyo ni bure, na vinapatikana hata hapo ulipo sasa hivi.

Chukua maamuzi sasa, kabla ya mlango wa neema kufungwa. Unachopaswa kufanya hapo ulipo ni kutubu kabisa dhambi zako kwa kukusudia kuziacha,..unakusudia kuacha ulevi, anasa, wizi, uasherati uongo, uvaaji usio na maadili, na kila aina ya uchafu, Kisha hatua inayofuata ni kwenda kubatizwa, hakikisha unabatizwa katika ubatizo ulio sahihi wa kimaandiko, yaani ni ule wa kuzamishwa katika maji mengi, na kwa jina la YESU KRISTO, (zingatie hilo uwe ni kwa jina la YESU) sawasawa na maandiko (Matendo 2:38, 8:16, 10:48, 19:5), ili upate ondoleo la dhambi zako. Na baada ya hapo Mungu mwenyewe atakupa kipawa cha Roho Mtakatifu, atakayekusaidia kushinda dhambi na kukuongoza katika kuijua kweli yote ya maandiko Yohana 16:13.

Na kuanzia hapo utakuwa na nafasi ya kuwa mshirika wa mambo yote ya kimbinguni Mungu aliokusudia kuwafunulia watoto wake.

1Wakorintho 2:9 “lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.”

Ni maombi yangu utafanya hivyo sasa.

Tafadhali “SHIRIKI” ujumbe huu na wengine.Bwana akubariki sana. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada zinazoendana..


DAMU YA YESU INANENAJE MEMA KULIKO YA HABILI?

MWILI NA DAMU YA YESU KRISTO.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1


Rudi Nyumbani

Print this post

LULU YA THAMANI.

Shalom, Mtu wa Mungu karibu tujifunze Neno la Mungu, ambapo leo kwa Neema za Bwana tutajifunza kwa sehemu juu ya ufunuo uliopo katika ufalme wa Mbinguni. Biblia inasema katika..

Mathayo 13.45 “Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta LULU NZURI;

46 naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua”.

Mfano huu ulitolewa na Bwana Yesu Kristo, alipokuwa anawafundisha makutano maana ya ufalme wa Mbinguni..Kama ukichunguza kwa makini utagundua kuwa Bwana Yesu alikuwa anapenda kutumia mifano ya kidunia hii kuifananisha na ufalme wa mbinguni Ikiwa na maana kuwa mambo mengi au shughuli nyingi za ulimwengu huu zimebeba kwa sehemu Fulani siri za ufalme wa Mbinguni ndani yake..Katika shughuli za haki au za uovu ndani yake kuna hekima za Kimungu..ndio maana utaona mahali pengine Bwana anatoa mfano wa Mpanzi aliyekwenda kupanda mbegu zake shambani…na mahali pengine Bwana Yesu anatoa mfano wa mwizi (kwamba atakuja kama mwivi usiku wa manane)…ikiwa na maana kuwa hata katika WIZI kuna hekima ya kiMungu ndani yake…ingawa kwa kusema hivyo sio kwamba anahalalisha wizi, sehemu nyingine anatoa mfano wa yule kadhi dhalimu..ikiwa na maana kuwa hata katika udhalimu pia ipo hekima ya Mungu ndani yake..nk

Lakini leo tutajifunza juu ya huu mfano wa Mfanyabiashara aliyekuwa akitafuta lulu ya thamani na alipoiona alikwenda kuuza kila alicho nacho ili kuinunua.

Sasa LULU ni nini?.

Lulu ni madini fulani ya thamani sana..ambayo hayachimbwi kutoka ardhini kama madini mengine yachimbwavyo bali asili yake ni baharini…Madini haya yanatengenezwa ndani ya mwili wa samaki, wanaojulikana kama “Oyster”…na samaki hawa sio kama samaki wa kawaida tunaowajua wenye mapezi na mikia na macho, hapana bali jamii ya hawa samaki hawana mapezi wala macho, wala mikia na wala hawaogelei ogelei kama viumbe wengine wa majini, bali wapo kama kokwa la embe hivi lililokauka na wanakaa katika sakafu ya bahari chini kabisa, hawaruki ruki huko na huko, wakati wote wanakuwa wametulia tu chini ya habari, …Hivyo ni ngumu kuwaona kwani unaweza ukapita ukadhani ni mawe tu yamelala kumbe ni samaki.

Sasa hayo madini yanayoitwa LULU yanaanza kujitengeneza kama chembe ndogo ya mchanga, tumboni mwa hao samaki, na kwa kadiri muda unavyozidi kuendelea..yanaongezeka ukubwa kidogo kidogo na hata kufikia ukubwa wa kama hizi gololi wanazochezea watoto wadogo..kwa jinsi inavyokuwa kubwa ndivyo thamani yake inavyozidi kuongezeka. Watu wanaokwenda kuyatafuta madini hayo baharini wanatumia gharama nyingi na muda mwingi na hatari nyingi..kwasababu inawagharimu waende mbali kwenye vilindi vya maji na wazame chini mpaka kwenye sakafu ya bahari na kuanza kuangalia angali huku na huko kama mtoto anayetafuta hela aliyoiangusha njiani..inawaachua hata siku nzima kukaa chini maji, hana hiyo inaweza kwenda kwa miezi kadhaa, Na kwa tabu nyingi wakibahatika kuwapata hao samaki wanawachukua na kwenda kuwapasua na kutoa hayo madini..

Sasa kutokana na madini hayo kuwa adimu na kuwa mazuri kupita kiasi, thamani yake nayo inakuwa kubwa zaidi…lulu moja ya ukubwa wa juu, thamani yake inaweza ikafika mpaka sh.milioni 250 za kitanzania. Hiyo ni moja tu!

Sasa tukirudi kwenye huo mfano Bwana Yesu alioutoa unaosema…ufalme wa Mungu umefanana na mfanya biashara aliyeona LULU ya thamani akaenda kuuza kila kitu alicho nacho ili kuinunua, alikuwa na maana kuwa, huyu mfanya biashara, alikwenda mahali akakuta LULU inauzwa kwa thamani ya chini…tuchukue mfano hiyo lulu yenye thamani ya sh.milioni 250 akaikuta inauzwa sh.milioni 100. Na alipoiona kwasababu yeye anaijua thamani yake halisi, na hana hela ya kutosha akatumia akili ya kwenda kuuza vyote alivyo navyo kama ni mashamba, kama ni nyumba kama ni mifugo yake, vyovyote vile…ili kwamba apate hela ya kutosha, akainunue hiyo lulu inayouzwa kwa bei ya chini..

Sasa kumbuka Bwana Yesu anamwita huyu mtu mfanyabiasha, na unajua mtu akiwa mfanyabiashara yupo kimaslahi zaidi, uyo kwaajili ya kupata faida.

Hivyo yeye kuuza kila kitu ili akainunue ni alijua siku atakapokwenda kuiuza kwa thamani yake halisi atapata faida kubwa na hivyo atakwenda tena kununua mashamba mazuri kuliko hata yale aliyouza, atakwenda kununua tena mifugo mingine mingi, atakwenda kujenga tena nyuma yenye thamani kama ile ya kwanza na bado atabakiwa na faida yake juu..

Kwahiyo huyu mfanyabiashara hakuwa mjinga, kwamba auze kila kitu halafu akae na lulu ndani kama urembo…hapana kumbuka yeye ni mfanya-biashara, aliinunua ili akaiuze.

Ndugu yangu Bwana Yesu Kristo ndio hiyo LULU YA THAMANI, Anapatikana BURE lakini HAPATIKANI KIRAHISI. Kama tu Lulu Baharini inavyopatikana bure lakini si kirahisi, kadhalika na Bwana Yesu, ndio maana alisema katika Luka 14.33 “Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, HAWEZI KUWA MWANAFUNZI WANGU”.

Unapousikia ujumbe huu, mimi ninayekuhubiria ni kama mfanya biashara ninayekuletea YESU KRISTO kwa bei ya chini..na wewe unayesikia ni kama mfanya-biashara mwenye kutafuta lulu hii ya thamani, hivyo unachopaswa kufanya ni kwenda kuuza kila ulicho nacho..ili upate pesa ya kutosha kumnunua huyu Yesu Kristo moyoni mwako, na kisha nenda kamwuze nawe kwa wengine ndipo utaona faida. Na gharama za kumnunua ndio hizo…”kuuza kila kitu cha ulimwengu huu unachokishikilia sasa kinachokufanya uwe mbali na Mungu wako” kuacha kila kitu kiovu, kukubali kuacha kila aina ya dhambi maishani mwako, kukubali kuingia gharama ya kuacha anasa, na mambo ya kiulimwengu, kukubali kuacha uasherati na uzinzi, kukubali kuacha utumiaji mbaya wa mitandao, kuchat mambo yasiyofaa mitandaoni, kukubali kuacha ulevi, na utazamaji wa pornography, kukubali kuacha kuvaa nguo fupi na zinazobana na suruali na vimini, kukubali kuacha kampani mbaya za watu wenye mizaha, na matusi, kukusudia kuuza muda wako wote kwa Mungu, kukusudia kumgeukia Mungu kwa moyo wako wote, na kwa akili zako zote, na kubeba msalaba wako na kuelekea Kalvari. Ndugu yangu wa thamani mtu asikudanganye kuwa utampa Bwana Yesu nje ya njia hiyo…yeye mwenyewe alisema katika..

Luka 14.25 “Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia,

26 Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

27 Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu”

Maneno haya ni magumu, lakini ndio ukweli wa mambo…ukitaka kwenda kununua lulu ya thamani Yule anayekuuzia atakwambia usipofikia kiwango Fulani cha fedha, huwezi kuipata..sio kwamba anataka kukuumiza hapana bali huo ndio ukweli wa mambo kwamba kitu unachokitafuta ni cha thamani ya juu, hivyo anaweza kukushauri uende ukauze hata shamba au nyumba ili upate fedha ya kutosha ya kuinunua..lakini kama usipotaka basi ni sawa uamuzi ni wakwako.

Hivyo ndugu unayesoma ujumbe huu ambaye hujampa Bwana Yesu maisha yako, au upo mguu mmoja nje, mguu mmoja ndani na unataka kuwa na maisha mazuri ya hapa duniani na huko mbinguni, unataka kupata faida hapa duniani na mbinguni, basi fahamu kuwa NJIA YA MSALABA haikwepeki. Ni lazima ujikane nafsi tu! Ni lazima uache KILA KITU CHA ULIMWENGU HUU, Ni lazima umgeuke yeye kikweli kweli, hakuna njia ya mkato..wengi wanapenda kufarijiwa kwamba kwa Bwana Yesu ni mteremko tu! Usidanganyike..Kristo ni LULU YA THAMANI. Kama alitoka mbinguni mahali penye utukufu atakuwaje wa bei rahisi huyo??..hebu chukua muda mtafakari huyu MFALME WA WAFALME!!.

Kwahiyo Bwana Yesu anatupenda na ataka tupate faida ndio maana, alitupa mfano huo wa mfanyabiashara, anataka na sisi tuwe wafanya biashara werevu tunaotafuta faida na si hasara, anataka tuingie gharama kupoteza vitu vidogo vya muda vya kitambo visivyo na maana ili tupate vitu vikubwa vya muda mrefu vyenye faida..huoni kama hiyo ni fursa nzuri kwetu??..Ndio ni fursa nzuri sana na ya faraja…ndio maana wanafunzi walipopata mashaka ya kupoteza mambo yao yote kwa ajili ya Kristo, yeye mwenyewe aliwapa faraja akawaambia watapata mara 100 hapa duniani na katika ulimwengu ujao uzima wa milele.. Tunayasoma hayo katika…

Marko 10:28 “Petro akaanza kumwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe.

29 Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili,

30 ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; NA KATIKA ULIMWENGU UJAO UZIMA WA MILELE”.

Hivyo Kama hujampa Bwana Yesu maisha yako, ni wakati wako sasa wa kufanya hivyo, unachopaswa kufanya ni kutubu kwa kumaanisha na kudhamiria kuziacha dhambi zako zote, na kumaanisha kutokuzifanya tena, (UNAZIACHA KABISA) Kama ulikuwa mlevi, unaacha ulevi, kama ulikuwa unatanga tanga kwa uasherati, unauacha uasherati, kama ulikuwa unavaa vibaya unaacha, na kisha baada ya kufanya hivyo nenda katafute ubatizo sahihi popote pale kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako, kulingana na matendo 2:38 na ubatizo sahihi ni wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO, baada ya kufanya hivyo Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi na kukuongoza katika kuijua kweli yote ya Biblia.Na hapo utakuwa umezaliwa mara ya pili.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu na wengine na Bwana akubariki. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

BEI YA UFALME WA MBINGUNI:

UFALME WA MUNGU HAUPATIKANI KIRAHISI

JIKANE NAFSI MTEULE WA MUNGU

SHETANI ANATOLEA WAPI FEDHA, ANGALI TUNAJUA FEDHA NA DHAHABU NI MALI YA BWANA?


Rudi Nyumbani

Print this post