Shalom! Karibu tujifunze Neno la Mungu,leo tutajifunza siri mojawapo ya kipekee iliyolala katika kitabu cha cha Ruthu. Kitabu hichi ni chepesi kukisoma, kwasababu ni kitabu kinachoelezea historia ya maisha ya watu zaidi kuliko unabii, hivyo nakushauri mahali ulipo chukua biblia yake ukipitie kwanza binafsi,kisha tuendelee ni kitabu chenye sura 4 fupi zinazoeleweka, hivyo ni vema ukafanya hivyo ili tuende pamoja.
Kitabu hichi kinaanzana na habari ya mtu anayeitwa Elimeleki, ambaye huyu alikuwa akiishi Israeli zamani kipindi cha Waamuzi, na biblia inatuambia siku njaa ilipokuja katika mji ule, Elimeleki alifunga safari kwenda nchi ya jirani kuishi huko yeye pamoja na mke wake aliyeitwa Naomi pamoja na wana wake wawili wa kiume..Lakini baada ya Muda kidogo mambo yalibadilika Elimeleki alikufa na kumwacha mke wake akiwa mjane na watoto wake wawili katika nchi ya ugenini..
Na Baadaye kidogo watoto wake wote wawili walibahatika kupata wake wazuri tu, lakini kwa bahati mbaya, nao pia walifariki wakiwa bado hawajapata watoto na wale wanawake, Hivyo yule mwanamke mjane Naomi hakufanikiwa kuambulia chochote, si mume, si watoto, wala si wajukuu, na hapa sasa ameshakuwa mzee sana hawezi kubeba mimba tena, hata angesema azae asingeweza tena kwani muda umeshakwenda amekaa ugenini zaidi ya miaka 10, hata hana wa kumsaidia tena, nguvu zake zimeisha kilichobakia ni kurudi tu katika nchi yake Israeli kwenda kumalizia siku zake za kuishi.
Kabla hatujaendelea mbele Embu jiulize, zamani zile za kipindi cha waamuzi kulikuwa na watu wengi mashujaa tu kama tunavyokisoma, kulikuwa na wajane wengi tu, kulikuwa na watu wengi wema tu, Hivyo habari zao zingeweza kuandikwa kama mojawapo ya kumbukumbuku nzuri kama funzo kwa ajili ya vizazi vya mbeleni, lakini ni kwanini habari za watu wengine hazijaandikwa isipokuwa za huyu mtu mmoja tu Elimeleki na familia yake ndizo zimenakiliwa hapa, na kuwekwa kama vitabu vitakatifu?..
Njia za Mungu sio njia zetu, Naomi hakufahamu kuwa japo maisha yake yalionekena kuwa ni ya bahati mbaya mbele za watu, maisha ya kusahauliwa, mtu ambaye sasa hana kumbukumbu tena, ambaye aliyekuwa amefanikiwa sana lakini sasa si kitu, hana mume,wala watoto,wala wajukuu, wala mali, wala chochote kile..hakujua kuwa kumbe Mungu alikuwa anaandika kwa kupitia maisha yake ufunuo mzito ambao ndio huo unakuja kutusaidia hata sisi watu ambao hatukustahili kupata neema za kumjua Kristo. Kwahiyo wakati mwingine maisha ya mtu yanaweza kubeba ufunuo Fulani wa Roho.
Lakini tukiendelea kusoma habari tunaona Naomi sasa anakusudia kurudi katika nchi yake mpweke,mwenye uchungu mwingi, na hapa tunaona anawaambia wale wakwe zake, ambao mwanzoni walikuwa wameolewa na watoto wake wawili kwamba kila mmoja sasa awe na amani kurudi kwa jamaa zake wakaolewe na kufanikiwa na kuishi maisha ya furaha siku zote za maisha yao.
Lakini tunaona wale wanawake wawili mwanzoni wote walikataa kumwacha Naomi peke yake, Lakini hilo halikumfanya Naomi aache kuwasihi wasifuatane naye, kwani hakutaka mtu yeyote abebe wake wowote kwa kulazimishwa, hivyo aliwabariki na kuwaomba warudi kwa jamaa zao wenyewe, lakini kama tunavyosoma habari, moyo wa Ruthu ulikuwa thabiti kuliko wa Orpa, Yeye Orpa baadaye alikubali kurudi kwa jamaa zake lakini Ruthu hakutaka kinyume chake alikuwa tayari kuambatana na Naomi popote aendapo kwa gharama zozote, alikubali kuchukuliana na gharama zote.
Tunasoma:
Ruthu 1: 11 “Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, mrejee; kwani kufuatana na mimi? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu?
12 Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume;
13 je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa Bwana umetoka juu yangu.
14 Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthuu akaambatana naye.
15 Naye akasema, Tazama, shemeji yako amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji yako.
16 Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu;
17 Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; Bwana anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami.
18 Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye”.
Sasa ukiendelea kusoma habari huko mbeleni utaona Ruthu alikubali kuondoka na Naomi katika umaskini wao, Ruthu asijue anapoelekea, asijue wakifika watapokelewa na nini, Ruthu akimtazama mwanamke yule kashakuwa mzee, na yeye bado ni binti kijana, ambaye anao uwezo wa kwenda kuolewa tena, ameacha vijana wazuri wenye mali katika nchi yake mwenyewe, pengine mabinti wenzake wanamkebehi wakimwambia hivi wewe umelogwa na kale kabibi?
Kwani katakupa nini? mwangalie mwenzako Orpa, aliona mbele kuwa huko hakuna tena uelekeo wa maisha, zaidi ni kuzeeshwa tu akili za wazee na kuwahudumia tu, na mwisho wa siku kuwa kama mjakazi wao..Isitoshe anakwenda mahali asipopajua, wala hajawahi kuwafahamu watu wa huko, pengine walimwambia Unakwenda kupotea tu huko na mwisho wa siku utajuta..Wewe bado binti mdogo hata bado hujazaa, unakwenda wapi?
Lakini Ruthu hakujali kuipoteza nafsi yake kuwa ni kitu cha maana sana, kuliko kujitenga na mama wa mume wake marehemu, hivyo aliendelea kufuatana naye tu katika taabu zote kama alivyoapa.
Kumbuka ni sheria iliyokuwa imetolewa na Mungu katika Israeli, kwamba mtu yeyote aliye myahudi asioe mwanamke ambaye si myahudi, kadhalika ni mwiko pia kwa mwanamke wa Kiyahudi kuolewa na mtu wa mataifa, Lakini hapa tunaona Naomi akirudi katika nchi yake mwenyewe akiwa amemwambulia mtu mmoja tu..
Pengine wale ndugu zake waliokuwa wamebaki Israeli walitazamia Elimeleki pamoja na Naomi watarudi na mali nyingi, kondoo, mbuzi, ngamia pamoja wa watoto wao na wajukuu wengi, na wajakazi wengi. Lakini hapa anaonekana Naomi peke yake, na binti mmoja wa kimataifa, na tena kibaya zaidi ni heri angekuwa kijakazi wake, lakini kumbe ni mke wa mtoto wake, jambo ambalo ni machukizo makubwa kwa Israeli.
Lakini kwa jinsi Ruthu tabia yake ilivyokuwa njema, na ya kupendeza watu wote, na kwa ukarimu wake wote aliomfanyia Naomi bibi yake,basi habari zake zikasikika katikati ya jamaa za Naomi. Na siku moja alipokuwa anakwenda kuokota masazo ya nafaka kwenye mashamba ya watu matajiri, aliingia katika shamba la mtu mmoja mkuu sana wa mji huo jina lake Boazi, ndipo Boazi akamwona na kuulizia habari zake, na kuambiwa kuwa huyu ni binti wa Naomi.
Wakati huo huo Boazi na Elimeleki mumewe Naomi walikuwa ni mtu na kaka yake. Hivyo ukiendelea kusoma habari hiyo mpaka mwisho kwa kuwa sasa hatuna nafasi ya kueleza habari yote, utaona kuwa mwisho wa siku Ruthu ambaye ni mwanamke wa kimataifa anakuja kuolewa na Boazi mtu mkuu wa Uzao wa kifalme, na ndiye kwa kupitia huyu Mfalme Daudi alitokea. Daudi ni kitukuu cha RUTHU.
Sasa kama tunavyojua mambo yote yanayotokea katika agano la kale ni kivuli cha mambo yanayoendelea katika agano jipya, habari yote ya Naomi na Ruthu, ni habari ya Kristo na bibi-arusi wake ambayo Mungu alikuwa anaichora kwa kupitia maisha ya hawa watu.
Kumbuka YESU Kristo alishuka kutoka mbinguni na utajiri mkubwa, kama Mfalme, aliyeacha enzi na mamlaka juu mbinguni, alikuja kwa watu wake Wayahudi, na hivyo alikaa nao, alikula nao,mfano tu wa Naomi jinsi alivyotoka Israeli na mumewe na watoto wake, na mali zao nyingi na kukaa katika nchi ya ugenini Moabu.
Lakini haikuwa vile kwa Naomi kama alivyotarajia, Mungu alimpiga na kumwacha pasipo kitu chochote na kubakia yeye tu alivyo. Picha kamili ya Bwana wetu Yesu kristo jinsi alivyopitia, ilimpasa yeye awe mfalme kwa wakati ule aliokuja ulimwenguni kwa mara ya kwanza lakini Mungu hakufanya hivyo kwa wakati ule, kinyume chake, alikataliwa, watu walimwona kuwa si kitu, walimtupa, walimtemea mate, walimpiga mijeledi, walizipiga kura nguo zake, walimsulibisha jaribu kufikiria mtu ambaye angepaswa awe mfalme lakini sasa anakuwa kituko kitu cha kuchekesha hana lolote tena..
Biblia inasema hivi juu yake:
“2 Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.
3 ALIDHARAULIWA NA KUKATALIWA NA WATU; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; NA KAMA MTU AMBAYE WATU HUMFICHA NYUSO ZAO, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.
4 Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.(Isaya 53)”….
8 Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; NA MAISHA YAKE NI NANI ATAKAYEISIMULIA? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.
9 Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.
10 Lakini Bwana aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi, Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake;
11 Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki Atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao.
12 Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu, Naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari; Kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa, Akahesabiwa pamoja na hao wakosao. Walakini alichukua dhambi za watu wengi, Na kuwaombea wakosaji…
Unaona biblia inasema maisha yake Bwana Yesu ni nani awezaye uyasimulia?..Jinsi yalivyoonekana kuwa ya ajabu mbele za watu waliomwona kama vile maisha ya Naomi. Lakini kumbe Mungu alifanyia vile Naomi kwa makusudi ili ampate RUTHU haleluya..
Angalia ni upendo mkuu namna gani huo, kumgharimu Mungu kwenda kuyaharibu maisha na raha ya mwingine, kwa ajili ya mtu mmoja asiyestahili kupata lolote asiyekuwepo hata katika mzao wa kiyahudi huko mbali katika nchi za wachawi na waabudu masanamu…Kwani hakukuwa na wanawake wazuri Israeli, wenye kumcha Mungu wakati ule, walikuwepo, lakini kwa jinsi Rehema za Mungu zilivyokuwa nyingi, alikwenda kumtafutia Boazi mke mwema katika nchi za mataifa mabovu, tena kwa kuyaharibu kwanza maisha ya Naomi kwa kunyang’anya kila kitu pamoja na watoto wake ili tu Ruthu apate mlango wa kumwendea BOAZI.
Ndugu yangu, mimi na wewe hatukustahili kuitwa bibi-arusi wa Kristo hata kidogo..Wayahudi walistahili heshima hiyo, kwani wao ndio waliochanguliwa na Mungu tangu awali, Lakini Mungu alituhurumia sisi zaidi, na kuja kutuchagua kututoa sisi katikati ya mataifa, Na zaidi ya yote hakuja kututwaa pasipo gharama, hapana bali alimtoa mwanawe wa pekee ambaye ndiye kama Naomi wetu, kuja kuteseka kupoteza kila kitu alichokuwa nacho, kupigwa, kutemewa mate kudharauliwa, kwa ajili yetu, na mwisho wa siku kufa, na kufufuka na alipofufuka alitaka sasa kurudi kwa Baba yake juu mbinguni, katika makao yake aliyotoka huko kama vile Naomi alivyotaka kurudi kwa watu wa jamaa zake.
Lakini sasa tendo la sisi kumfuata Kristo lipo mikononi mwetu, na si mikononi mwake,..Je! tutaamua kuanza naye safari ya kwenda kwa BOAZI wetu mbinguni? Au tutataka kuwa kama Orpa, kuona kuwa Naomi hana faida yoyote kwetu, Yesu Kristo hana chochote cha kutugawia, tukimfuata tutaendelea kuwa maskini, tukimfuata tutakuwa washamba, tukimfuata kampani zetu za Disco na vilabuni zitatuacha, tukimfuata vimini vyetu tutavitupa, tukimfuata, tutaonekana vibibi,. tukimfuata tutakwenda kupotea moja kwa moja na kuwa vichaa..
Ndugu fahamu kuwa huu wakati ambao Bwana ameshakulipia gharama zote, hatakuja tena kukulazimisha, bali kinyume chake atakupa uhuru wa kuchagua, je! utakuwa tayari kujitwika msalaba wako kumfuata kama Ruthu au kuendelea kubaki katika dunia kama Orpa. Ukitaka kubaki kama Orpa ni sawa lakini kumbuka BOAZI yupo Israeli anamsubiria yule aliyetayari kumtii NAOMI, na maagizo yake yote.
Hivyo huu ni wakati wako wa kupiga gharama, mambo ambayo Wayahudi wameyakosa japo walikuwa wanayatazamia tangu zamani yamepewa wewe, mfano tu wa wale wajakazi wa Boazi waliokuwa wanafanya kazi shambani mwake miaka yote, hata mmoja hakuna aliyekuja kuolewa na Boazi isipokuwa mgeni wa mbali wa Ruthu. Ni kwasababu gani?..Ni kwasababu NAOMI ndiye aliyekuwa na SIRI ya jinsi ya kumwingia BOAZI na siri hiyo alipewa Ruthu peke yako.
Na ndio maana Bwana alimaanisha kuwaambia makutana maneno haya..
Luka 9:23 “Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.
24 Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha.
25 Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?”.
Na alisema “Mimi ndimi njia na kweli na Uzima mtu hafiki kwa Baba ila kwa njia yake yeye”
Je! leo hii utachukua uamuzi wa kumfata Kristo? kama vile Ruthu alivyojitoa kikamilifu mpaka kuwa tayari kuacha vyote alivyonavyo kwa ajili ya mkwe wake?.
Hizi ni siku za mwisho Tubu ukabatizwe, moja ya hizi siku bibi-arusi wa Kristo atanyakuliwa kwenda kwenye karamu iliyoandaliwa huko juu ya Mungu mwenyewe, watakaofika huko ndugu si kila mtu anayejiita ni mkristo halafu maisha yake yanaonyesha kabisa hajachukua msalaba wake kumfauta Kristo, mguu mmoja upo nje, mwingine ndani, watakaokwenda kwenye unyakuo ni wachache sana, ni kikundi kidogo sana mfano wa Ruthu pekee yake, wale walioamua kumfuata Kristo kikweli kweli pasipo kuangalia mbele wala nyuma, Nawe usiwe ni mmojawapo wa watakaokosa karamu hiyo. Ni heri upoteze kila kitu sasa kuliko kuikosa karamu ya mwana-kondoo.
Ubarikiwe sana
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
USITAFUTE FAIDA YAKO MWENYEWE BALI YA WENGINE.
VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 13 (Kitabu cha Hosea).
VIACHENI VYOTE VIKUE HATA WAKATI WA MAVUNO.
Nimekuwa kama mwari nyuni wa jangwani,
JE MGOGORO WA URUSI NA UKRAINE,UMETABIRIWA KIBIBLIA?
About the author