Inadhaniwa na wengi ili kwamba mtu asemehewe dhambi zake na Mungu ni lazima aongozwe sala Fulani ijulikanayo kama sala ya Toba, na kwamba mtu asipoongozwa sala hiyo basi huwezi kusamehewa dhambi zake, Na hiyo imewafanya watu wengi hata wale wasio wakristo kusema wameokoka, kisa tu huko nyuma walishawahi kuongozwa Sala ya Toba. Lakini biblia inatufundisha nini juu ya toba halisi inayopelekea kusamehewa dhambi?. Embu tufuatilie kwa pamoja tukio hili alilokutana nalo Bwana wetu Yesu na mwitikio wake jinsi ulivyokuwa, kuna jambo la Fulani nataka ulione pengine hata na wewe hujawahi kulijua japo ni habari tunayoisoma kila siku, Tusome:
Luka 7:37 “Na tazama, mwanamke mmoja wa mji ule, aliyekuwa mwenye dhambi, alipopata habari ya kuwa ameketi chakulani katika nyumba ya yule Farisayo, alileta chupa ya marimari yenye marhamu.
38 Akasimama nyuma karibu na miguu yake, akilia, akaanza kumdondoshea miguu machozi yake, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake, akiibusu-busu miguu yake na kuipaka yale marhamu.
39 Basi, yule Farisayo aliyemwalika alipoona vile, alisema moyoni mwake, Mtu huyu kama angekuwa nabii, angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi.
40 Yesu akajibu akamwambia, Simoni, nina neno nitakalo kukuambia. Akasema, Mwalimu, nena.
41 Akasema, Mtu mmoja mkopeshaji alikuwa na wadeni wawili; mmoja amwia dinari mia tano, na wa pili hamsini.
42 Nao walipokuwa hawana cha kumlipa, aliwasamehe wote wawili. Katika hao wawili ni yupi atakayempenda zaidi?
43 Simoni akajibu akasema, Nadhani ni yule ambaye alimsamehe nyingi. Akamwambia, Umeamua haki.
44 Akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, Wamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyu amenidondoshea machozi miguu yangu, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake.
45 Wewe hukunibusu; lakini huyu tangu nilipoingia hakuacha kunibusu sana miguu yangu.
46 Hukunipaka kichwa changu mafuta; bali huyu amenipaka miguu yangu marhamu.
47 Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo.
48 Kisha alimwambia mwanamke, UMESAMEHEWA DHAMBI ZAKO.
49 Ndipo wale walioketi chakulani pamoja naye walianza kusema mioyoni mwao, Ni nani huyu hata asamehe dhambi?”.
Utaona pia sehemu nyingi ambazo Bwana Yesu anatamka hili Neno “UMESAMEHEWA DHAMBI ZAKO.” Watu wanachukizwa na kumwona kama ni mkufuruji, kujiamulia kumtolea mtu tu hukumu kana kwamba yeye ni Mungu, utasoma hilo pia katika (Marko 2:112) pale alipomwona Yule mtu aliyepooza na kumwambia umesamehewa dhambi zako, watu walikasirika sana na kusema huyu anakufuru..Lakini hawakuona kitu ambacho Kristo alikuwa anakiona, wao walidhani anajiamulia tu kutamka maneno yale kwa kila mtu, hata kwa Yule ambaye hana mpango na Mungu kumwambia “Umesamehewa dhambi” hapana Bali Kristo alikuwa anaona ndani kabisa kwenye vyumba vya ndani vya mioyo ya watu wale
Alikuwa anaona mioyo ya Toba, mioyo inayojutia dhambi zao, mioyo inayosema laiti Mungu angenisikia akanisamehe wingi wa dhambi zangu hizi, nitamtumikia milele, mioyo inayosema sitakaa nirudie tena dhambi hizi natuja ni kwanini nilijihusisha katika dhambi hizi,..Ndicho Bwana Yesu alichokiona ndani ya yule mwanamke na Yule mtu aliyepooza..Sasa japo kwa nje! Hawakuzungumza na Bwana lolote, lakini ndani walikuwa wanamlilia Bwana.. Na pale pale utaona Yesu anawatamkia hadharani “UMESAMEHEWA DHAMBI ZAKO”, Sasa wale watu ambao hawajui chochote na huku wakimwona yule kahaba asemi chochote, na kumsikia Bwana Yesu anazungumza maneno kama yale wanasema anakufuru. Na kumbuka Bwana hakusema “nimekusamehe dhambi” hapana! Bali alisema “umesamehewa” ikiwa na maana kuwa alikuwa ni kama anatoa taarifa ya kitu ambacho kimefanyika tayari huko mbinguni…ni sawa na wewe umwambie mtu Fulani “umesamehewa riba” hiyo haimaanishi ni wewe ndio umemsamehe, bali wewe unasimama kama mwakilishi wa kitu ambacho kimefanyika sehemu nyingine. Na ndio Mamlaka Kristo aliyokuwa nayo ya kusamehe dhambi duniani. Alikuwa hafanyi chochote isipokuwa ameona kwanza kwa Baba yake.
Yohana 5: 19 “Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile”.
Lakini endapo Bwana angemwona yule mwanamke amekuja na marhamu na kulia chini ya miguu yake, na kuanza kumpangusa miguu yake kwa machozi yake, na ndani ya moyo wake hana moyo wa Toba, ni Dhahiri kuwa asingemwambia yale maneno, labda angemwambia maneno mengine ya kumjenga lakini sio kumwambia amesamehewa dhambi zake.
Ndugu Mungu hategemei Sala 100 za toba unazoongozwa kila siku, hategemei unafungua kinywa chako kumkiri yeye mbele zake mara ngapi na kulia kwa kupaza sauti ya kuomba msamaha mara ngapi..Ikiwa ndani yako hakuna moyo wa kudhamiria kabisa kugeuka moja wa moja kuacha dhambi na kumfuata Kristo,..Toba yako ni batili.
Mtu mmoja anaweza akawa ni muuaji, jambazi na gaidi lakini siku moja akajutia makosa yake na kusema kuanzia leo Mungu wangu ninakugeukia na haya mambo siyataki tena, na akayaacha kweli akaanza kumtafuta Mungu, lakini wewe unayekwenda kila siku madhahabuni pa Mungu na kulia daima na kumwambia Mungu nisamehe, unaongozwa kila siku sala ya Toba lakini bado huku nyuma unazini kisiri siri, unatazama picha chafu za ngono kisirisiri, unakunywa pombe kisirisiri unajiita ni mshirika wa siku nyingi kanisani nataka nikuambie ukweli ni kwamba Mungu “HAKUWAHI KUKUSAMEHE DHAMBI ZAKO”.
Bwana anaisamehe mioyo ya Toba, sio midomo ya toba.
Hivyo hatupaswi kujidanganya kwa namna yoyote ile. Toba ya kweli haipo midomoni bali moyoni, Iwe ni kwa sala au sio kwa sala kinachojalisha ni kugeuka kwa dhati ndani ya moyo, na kujutia kile kitu na kusema sifanyi tena kwa vitendo..Je! wewe umegeuka? kama bado basi wakati ndio huu, fanya uamuzi wa busara usio na majuto, mguekie yeye ili upokee msamaha halisi na wa kweli kutoka Mbinguni kwa Mungu Baba..
Ubarikiwe sana.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada zinazoendana:
SAMEHE KUTOKA NDANI YA MOYO WAKO.
JIBU: Tukisoma Yohana 10:16 Inasema…
“Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja”.
Katika Mstari huo tunaona imeweka wazi kabisa kuwa Mchungaji ni Bwana Yesu mwenyewe…na Bila shaka kondoo ni watu wake…..Na kama kondoo ni watu wake ni Dhahiri kuwa ni lazima Mahali wanapoishi ndipo patakuwa zizi lao. Sasa katika Biblia Nchi ya Israeli inafananishwa na zizi la Mungu, ikiwa na maana kuwa wayahudi ni kondoo wa Mungu waliopo katika zizi linaloitwa Israeli. Tunalithibitisha hilo katika..
Ezekieli 34:13 “Nami nitawatoa katika watu wa mataifa, na kuwakusanya katika nchi zote, nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe; nami nitawalisha juu ya milima ya Israeli, kando ya mifereji ya maji; na katika mahali pote pa nchi panapokaliwa na watu.
14 Nami nitawalisha malisho mema, pa juu ya milima ya mahali PALIPOINUKA PA ISRAELI LITAKUWA ZIZI LAO; huko watalala katika zizi jema; nao watakula malisho mema, juu ya milima ya Israeli.
15 Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo zangu, nami nitawalaza, asema Bwana MUNGU”.
Vivyo hivyo kinyume chake, watu wote ambao si wa Israeli ndio wapo zizi lingine ambalo Bwana alilolizungumzia pale, Yaani sisi watu wa Mataifa ndio Bwana aliokuwa ana maanisha kondoo wa Zizi lingine, ambao nasi pia ulifika wakati, tuliingizwa na kuwa miongoni mwa kondoo wake Bwana, kwasababu injili ilianza kwanza kwa wayahudi ndipo ikaja kwetu…..na kwa kupitia msalaba sisi pamoja na wayahudi wote tumekuwa kundi moja, na Bwana wetu amekuwa ni mmoja (Yesu Kristo).
Waefeso 2:11 “Kwa ajili ya hayo kumbukeni ya kwamba zamani ninyi, mlio watu wa Mataifa kwa jinsi ya mwili, mnaoitwa Wasiotahiriwa na wale wanaoitwa Waliotahiriwa, yaani, tohara ya mwilini iliyofanyika kwa mikono;
12 kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani.
13 Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo.
14 Kwa maana yeye ndiye amani yetu, ALIYETUFANYA SISI SOTE TULIOKUWA WAWILI KUWA MMOJA; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga”
Unaona hapo? Alitufanya sisi wawili (yaani sisi watu wa mataifa na wayahudi) kuwa mmoja…yaani kwa kundi moja.
Wagalatia 3:27 “Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo.
28 Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu”.
Je! Na wewe ni miongoni mwa kondoo wake?..Umeingizwa ndani ya kundi la Kristo, Kumbuka hatufanyiki kondoo wa Kristo kwa kujiunga na Kanisa bali kwa kutubu na kubatizwa na kupokea Roho? Na kuishi Maisha matakatifu?.
Ubarikiwe.
Mada zinazoendana:
MAMBO YATAKAYOTOKEA ISRAELI SIKU ZA HIVI KARIBUNI.
AMIN! NAWAAMBIA KIZAZI HIKI HAKITAPITA!
JE! MABALASI BWANA YESU ALIYOYATUMIA KUGEUZIA MAJI KUWA DIVAI, YALITUMIKA TU KWA KAZI HIYO?
Kufanya kitendo cha ndoa na mtu ambaye hamjaoana, ni kwenda kinyume na maagizo ya Mungu, kuwa na boyfriend au girlfriend na kujihusisha na vitendo vya kukutana kimwili kuna madhara makubwa sana kiroho.
Dhara la kwanza: Wote mnakuwa mwili mmoja.
Biblia inasema katika…
1 Wakorintho 6:16 “Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja. 17 Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye”.
Ili kuelewa juu ya kuwa mwili mmoja, hebu tutafakari ni kwa namna gani, kanisa ni mwili mmoja na Kristo, ndipo tuelewe ni madhara ya kuwa mwili mmoja na kahaba.
Maandiko yanasema..katika
Warumi 12:5 “ Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake.”
Hii ina maana kuwa watu wote waliomwamini Kristo na kubatizwa na kupokea Roho, hao wanafanyika kuwa viungo vya Kristo, yaani mwili wa Kristo, wanakuwa mwili mmoja na Kristo.
Sasa ni faida gani mtu anazipata anapokuwa mwili mmoja na Kristo?..Ni wazi kuwa Baraka zote Kristo alizokabidhiwa na Baba zinakuwa juu ya huyo mtu…
Waefeso 1:20 “..aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho;
21 juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia;
22 akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo
23 ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote”
Umeona Kristo aliwekwa juu sana kwaajili ya kanisa, ndio maana popote atakapokuwepo Kristo na sisi tupo naye, baraka zote alizobarikiwa Bwana Yesu na sisi tumebarikiwa nazo, enzi yote aliyopewa Bwana Yesu na sisi tumepewa, kwasababu sisi ni mwili wake, yeye ni kichwa. Ndio maana biblia inasema hakuna awezaye kutushitaki,
Warumi 8:31 “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?
32 Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?
33 Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki.
34 Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea”.
Baraka zote hizo ni kutokana na kwamba tumeunganishwa kuwa mwili mmoja na Kristo. Lakini kinyume chake endapo Kristo angekuwa amelaaniwa nasi pia tungekuwa sehemu ya laana yake. Lakini Kristo hakulaaniwa bali alibarikiwa ndio maana nasi pia tumebarikiwa.Sasa kinyume chake mtu ambaye ni Kahaba, moja kwa moja anakuwa anaishi chini ya Laana ya Mungu, mtu huyu anapokwenda kukutana na mtu mwingine ambaye si kahaba kama yeye, na akalala naye, katika ulimwengu wa roho anafanyika mwili mmoja naye…Hivyo anashiriki laana zake zote kwa Yule mtu mwingine, Matatizo yake yote anakuwa anashiriki na yule aliyekutana naye kimwili, hapo ndio chanzo cha matatizo ya watu wengi yanapoanzia.
Unakuta mtu alikuwa ni mzuri tu na hana matatizo yoyote, lakini anapokwenda kulala na mtu mwingine ghafla hali yake inabadilika, hajui tatizo ni nini, kumbe katika ulimwengu wa roho, anashiriki matatizo yote, na laana zote, na mikosi yote ya yule mwenzake aliyoibeba….Mbele za Mungu wote wanaonekana ni mwili mmoja…Kama yule mtu alikuwa ni adui wa Mungu, pengine ni muuaji, au ni mshirikina, au mchawi, au mtu wa kudhihaki injili…na wewe unakwenda kulala naye…Hapo mbele za Mungu wote ni washirikina, wote ni wachawi, na wauaji…haijalishi hujawahi kuua, wala kwenda kwa waganga…kitendo tu! cha wewe kukutana kimwili na mtu mwenye matendo hayo, tayari mbele za Mungu wewe nawe ni mshirika.
Kama tu Ukimwi unaweza kumwingia mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa kitendo hicho, kwanini matatizo ya rohoni mtu usiambukizwe!..Watu hawaelewi kuwa kuna magonjwa ya rohoni ambayo nayo pia yanaambukizwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kwa vitendo kama hivyo.
Na kahaba sio tu mtu anayejiuza kule barabarani akitafuta fedha, la! Kahaba ni mtu yeyote ambaye yupo tayari kufanya kitendo cha kukutana kimwili kwa malipo au hata pasipo malipo..Kinachohuzunisha ni kwamba siku hizi kitendo hicho hata hakifanyiki kwa malipo, tofauti na zamani…kwahiyo makahaba wa siku hizi ni wabaya Zaidi kuliko wa zamani, mtu yeyote aliye na boyfriend au girlfriend na anaishi naye na hawajaoana, huyo ni kahaba! Haijalishi wana mpango wa kuoana huko mbeleni! Kitendo tu cha kukutana na mtu huyo kabla ya ndoa tayari huo ni uasherati!.
Unataka laana hizo zote zisikupate?..Jiepushe na uasherati!..utasema haiwezekani kujiepusha nao?..wapo mamilioni ya watu wanaoshinda uasherati! Na hawaishi Maisha ya zinaa hata kidogo! Shetani asikudanganye kwamba hakuna mtu anayeweza kushinda uasherati huo ni uongo!Dhara la Mwisho na Kubwa la uasherati ni ZIWA LA MOTO!Biblia inasema wazinzi wote sehemu yao ni katika lile ziwa la moto..
Ufunuo 21:8 “… Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”.
Wagalatia 5: 19 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi …….kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu”.
1Wakoritho 6:9 “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,”
Hatima ya wote wanaofanya uasherati au uzinzi kwa siri, ni ziwa la moto.Ikiwa leo unaishi na mwanamume au mwanamke ambaye hamjafunga ndoa! Mwache haraka sana kama unataka kwenda mbinguni, au mwambie mkafunge ndoa …Ikiwa unaishi na mtu unayemwita girlfriend au boyfriend nataka nikuambie mpo chini ya laana, na endapo mkifa ghafla ni moja kwa moja kwenye ziwa la moto, hiyo ni kulingana na maandiko. Kaa mwenyewe mpaka wakati utakapofika wa wewe kuoa au kuolewa, kama uliweza utotoni kwanini usiweze ukubwani!! Epuka injili za shetani zilizozagaa huko zikikuambia ni ngumu kuishi bila hayo mambo, hizo zote zina lengo la kukupeleka kuzimu.
Bwana akubariki sana, kama hujampa Bwana Yesu Maisha yako, ni vyema ukafanya hivyo kabla siku zako hazijaisha za kuishi hapa ulimwenguni..kabla haijakaribia miaka utakaposema sina furaha katika hiyo (Mhubiri 12).
Maran atha!.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii 0789001312Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group
Mada zinazoendana:
“MOTO HUFA KWA KUKOSA KUNI’’..NA NDIVYO ILIVYO KWA UASHERATI
Nini Tofauti kati ya uzinzi na uasherati ?
Danieli 12:8 “Nami nikasikia, lakini sikuelewa; ndipo nikasema, Ee Bwana wangu, mwisho wa mambo haya utakuwaje?
9 Akasema, Enenda zako, Danieli; maana maneno haya yamefungwa, na kutiwa muhuri, hata wakati wa mwisho.
10 Wengi watajitakasa, na kujifanya weupe, na kusafika; bali wabaya watatenda mabaya; wala hataelewa mtu mbaya awaye yote; bali wao walio na hekima ndio watakaoelewa.”
Licha ya Danieli kuonyeshwa maono mengi sana yahusuyo siku zake na siku za mwisho ukisoma sura zote za nyuma utaona hayo lakini bado mwishoni kabisa utaona Danieli anamuuliza Bwana “mwisho wa mambo haya utakuwaje?”….Alitamani kuona jinsi mwisho utakavyomalizikia…Ni jambo ambalo sio mitume tu wa Bwana walitamani kufahamu ukisoma (Mathayo 24), bali pia hata sisi wa leo tunatamani kujua mwisho wa mambo yote utakuwaje… Lakini Mungu hakumfunulia Danieli kwasababu moja tu, na sababu yenyewe ni kuwa Danieli hakuwa anaishi katika siku za mwisho, Na ndio maana Maneno yale yalifungwa hadi wakati wa siku hizo zitakapofika.
Lakini kwa bahati mbaya Danieli anaambiwa pia watakaofahamu sio wote…na kama sio wote basi lile Neno la ghafla na kama mwivi usiku wa manane litawakumba watu wengi sana, na watu hao Danieli anaambiwa ni wale waovu na watenda mabaya ndio wakati huo ukifika hawatelewa chochote, lakini wenye hekima Danieli anaambiwa watajua na kuelewa hivyo siku hiyo haitawajilia kwa ghafla kama mwivi. Watu wengi wanadhani siku ile watu watajiliwa kama mwivi usiku, ndugu nataka nikuambie hilo halitakuwa kwa watakatifu ukisoma.
1Thesalonike 5:1 inasema “Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.
2 Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.
3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.
4 BALI NINYI, NDUGU, HAMMO GIZANI, HATA SIKU ILE IWAPATE KAMA MWIVI. 5 Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza.
6 Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.
7 Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku.
8 Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu”.
Unaona biblia inatuambia sisi wana wa Nuru, wenye hekima hatupo gizani, hadi siku ile itujie kama mwivi..Ndugu hizi ni nyakati ambazo Mungu hamlazimishi mtu kuchagua njia yoyote ya kuiendea katika maisha yake, Ukiwa upo nje ya wokovu, au unasuasua mguu mmoja ndani au mguu mmoja nje, fahamu kuwa utatapikwa kulingana na maandiko (Ufunuo 3:16) na Bwana atakuwa hana mpango na wewe…Na kama hana mpango na wewe basi usitazamie kuwa utafahamu chochote kinachoendelea sasa hivi, au kitakachotokea mbeleni juu ya mpango wake wa wokovu wa siku hizi za mwisho..
Na wala hutakaa ufahamu ni kwa kiasi gani tunaishi katika majira ya kumalizia..siku ile utakapoona mambo yamebadilika tu ghafla, Ukiona kuwa dunia haina miaka mingine mitatu na nusu ya kuishi mbeleni, ndipo utakapolia kilio cha kusaga meno.. siku hizo utabakia kusema mbona sikutazamia kama ingekuwa haraka hivi, mbona sasahivi ni wakati wa amani na utulivu dunia ipo kwenye ustaarabu mzuri kuliko hata kipindi cha vita ya kwanza ya dunia imekuwaje dunia inakwenda kuisha kiajabu ajabu tu..sasa wakati unafikiria hivyo wenzako wakati huo watakuwa wanang’aa kama jua mbinguni wewe umebaki hapa unangojea mauti.
Ndugu hatua za UNYAKUO zimeshaanza kama hulijui hilo, tafuta kulijua hilo au ikiwa utataka kufahamu tutumie ujumbe inbox nikutumie somo linalohusu unyakuo uone ni jinsi gani tunaishi katika nyakati za hatari.
Huu sio muda tena wa kutanga tanga na ulimwengu, huu sio muda tena wa kulala usingizi wa kiroho bali ni kumtafuta Bwana kwa bidii ili na sisi atuingize katika mpango wake wa wokovu aliokusudia kwetu, kama wenye hekima wengine.
Hivyo Ikiwa bado hujafanya uamuzi sahihi yaani hujatubu dhambi zako fanya hivyo sasa kwa kumaanisha kisha tafuta mahali ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwenye maji mengi na kwa Jina la YESU KRISTO, Upate ondoleo la dhambi zako (Matendo 2:38) na Bwana atakupa Roho Mtakatifu kukuongoza katika kweli yote siku hizi za mwisho. Au kama unalishaamini na unasuasua rudi upande wa Bwana kwa moyo wote, kabla hazijakaribia siku utakazosema sina furaha katika hizo (Mhubiri 12). Huu ni wakati wajioni giza linakaribia kuingia ulimwenguni kote, utafika wakati watu wataitamani Nuru wataikosa.
Bwana akubariki sana,
Mwana-kondoo amechinjwa kwa ajili yetu.
Maran atha!
Mada zinazoendana:
AMIN NAWAAMBIA KIZAZI HIKI HAKITAPITA
Shalom, Karibu tujifunze Biblia,
Huu ni mwendelezo wa uchambuzi wa vitabu vya Biblia leo tutasogea mbele kitabu kimoja kinachofuata cha Ezra.Katika vitabu vilivyotangulia vya Wafalme na Mambo ya Nyakati, tuliona ni kwa jinsi gani, Mungu alishughulika na Taifa la Israeli kupitia Wafalme wake, na Tumeona ni jinsi gani wafalme hao ambao walitaka wawatawale jinsi walivyokuwa mwiba kwao, mpaka kuwasababishia waingie katika matatizo mazito..
Tunamwona kwamfano Mfalme Sulemani japokuwa alikuwa ni mpakwa Mafuta wa Bwana lakini aliwatumikisha Israeli vikali sana, (1 Wafalme 12:4 ) jambo ambalo halikuwa mpango wa Mungu tangu mwanzo, tunalisoma hilo katika 1Samweli 8:11-18 na Pia ndiye aliyesababisha Taifa la Israeli kugawanyika sehemu mbili (Upande wa kaskazini na upande wa kusini), jambo ambalo pia halikuwa mpango kamili wa Mungu watu wake wagawanyike.
Na wafalme wengine wote waliofuata wa Israeli na Yuda kama Mfalme Yeroboamu, Mfalme Ahabu na Mfalme Manase waliwakosesha waisraeli sana, na kuwafanya watu waabudu sanamu na miungu migeni…Kwamfano Mfalme Manase hakuishia tu kuabudu sanamu bali pia aliitengeneza madhabahu ya mungu mgeni ndani ya lile Hekalu la Sulemani na kuiabudu huko,(2 Wafalme 21) na pia alimtoa sadaka ya kuteketezwa mwanawe, na alikuwa anafanya uchawi na uganga pamoja na kutazama bao na kujihusisha na wachawi na wapunga pepo. Huyo ni Mfalme anafanya mambo hayo yote, akafanya dhambi kuliko hata mataifa wasio mjua Mungu wa kweli.
Kwasababu hiyo basi Mungu akaghadhibika sana kuahidi kuwa watakwenda utumwani. Na wakati ulipofika walichukuliwa utumwani, ambapo mataifa 10 yalichukuliwa utumwani Ashuru na Yuda wakachukuliwa Babeli, na huko wakakaa miaka 70 sawasawa na unabii Mungu aliompa Nabii Yeremia. Na baada ya miaka hiyo sabini kuisha Mungu alitabiri kuwa watatoka. Sasa kama hujapitia uchambuzi wa vitabu hivi kwa ufupi ni vyema ukapitia ili tuende pamoja.
Sasa Ni mambo gani yalikuwa yanaendelea walipokuwa huko Babeli?..Tutakuja kuona tutakapofika katika kitabu cha Danieli na Ezekieli…Lakini kitabu hichi cha EZRA kinaruka mpaka wakati wana wa Israeli wanatoka Babeli…Kwa mpangilio mzuri kingepaswa kianze kwanza kitabu cha Danieli ndipo kifuate cha Ezra lakini biblia haijaviweka vitabu katika mfululizo huo.Kitabu cha Ezra kimeandikwa na Ezra mwenyewe.
EZRA NI NANI?
Biblia inasema Ezra alikuwa ni mwandishi mwepesi katika sheria ya Musa.
Ezra 7: 6 “.. huyo Ezra akakwea kutoka Babeli; naye alikuwa MWANDISHI MWEPESI KATIKA SHERIA YA MUSA, aliyokuwa ameitoa Bwana, Mungu wa Israeli; naye mfalme akamjalia matakwa yake yote, kama mkono wa Bwana, Mungu wake, ulivyokuwa pamoja naye”
Maana ya mwandishi mwepesi ni mtu ambaye YUPO TAYARI kufanya jambo, yaani mwepesi katika kufanya jambo fulani, sio mzito..Ndio maana hapo biblia imemtaja Ezra kama Mwandishi mwepesi.
Kadhalika Mwandishi katika desturi za wayahudi alikuwa ni mtu anayefanya kazi kama za sasahivi za uwakili, alikuwa ni mtu anayeijua sheria ya Musa vizuri na hivyo ni rahisi kufahamu kipengele fulani cha sheria kinasema hivi au vile…Katika Agano jipya utaona Bwana Yesu amewataja waandishi sehemu kadha wa kadha..soma (Mathayo 17:10, Mathayo 20:18, Mathayo 21:15, Mathayo 23:2 n.k).
Pamoja na kwamba walikuwa na kazi ya kuhukumu kwa kupitia vipande vya sheria na kufundisha watu, lakini pia walikuwa na kazi nyingine wanayoifanya ya kunakili torati…Kumbuka zamani hizo hakukuwa na mashine za photocopy kama tulizonazo leo…Hivyo Nakala zote zilikuwa zinatengenezwa kwa kunakiliwa tena mahali pengine…
Kwahiyo kazi ilikuwepo kubwa ya kutengeneza nakala nyingi kila siku, waandishi hawa walikuwa wanaandika usiku na mchana, Katika kunakili walikuwa na vigezo vyao vya kufuata, kwanza mwandishi lazima ayatamke maneno Dhahiri ndipo ayaandike, na pia wakati wa kuandika anapokutana na jina la Mungu takatifu YEHOVA alikuwa anasimama kwanza ananawa mwili wote na kuisafisha kalamu yake ndipo aliandike. Na nakala ikishakamilika, itahakikiwa kwa siku 30 kabla ya kuruhusiwa itumike, na endapo zitaonekana kurasa mbili au tatu zitahitaji marekebisho basi nakala nzima inaachwa, kazi inaanza upya. Na kila aya na kila Neno lilikuwa linahesabiwa kuhakikisha na kitabu halisi. Kulikuwa na sheria nyingine nyingi tu katika uandishi…
Hivyo kazi ya uandishi ilikuwa inaheshimiwa sana katika Israeli, na huyu Ezra alikuwa mmoja wao wa hao waandishi, lakini biblia inamtaja alikuwa ni mwandishi mwepesi, yaani alikuwa anaifanya kazi yake kwa kupenda pasipo kusukumwa, na katika ufasaha, tofauti na wengine, Ndiye aliyekiandika kitabu cha Mambo ya nyakati tulichotangulia kukipitia…
Na katika kitabu hichi Roho ya Bwana ilimjia na kuanza kuandika hatua kwa hatua jinsi wana wa Israeli walivyotoka Babeli na kurudi Israeli, kuanzia Kundi la kwanza lililotoka Babeli na kurudi Nchi ya Ahadi mara baada tu ya Mfalme Koreshi kutoa amri ya uhuru wao. Na Kundi hilo ndio tunalolisoma katika Ezra Mlango wa 2.
Naye pia Ezra alikuwa ni miongoni mwa waliotoka Babeli na kurudi nchi ya Ahadi lakini yeye alikuwa katika lile kundi la pili ambalo tunalisoma katika mlango wa 7. Wakati Ezra anarudi kulikuwa tayari kuna lile kundi la kwanza lililotangulia miaka kadhaa nyuma, hivyo kuna mambo ambayo walikuwa wameyasahau yahusuyo sheria za Mungu, na kadhalika hata nyumba ya Mungu ambayo walikuwa wanaijenga upya ilisimama… hivyo Ezra alikusudia moyoni mwake atakaporudi awafundishe na kuwakumbusha wana wa Israeli sheria zote za Mungu wa Israeli na nini torati ya Musa inasema, na Bwana alimsaidia kupata kibali mbele ya Mfalme wa Uajemi, na kusapitiwa kwa kila kitu alichokihitaji ili tu akawafundishe sheria za Mungu.
Ezra 7: 6 “huyo Ezra akakwea kutoka Babeli; naye alikuwa mwandishi mwepesi katika sheria ya Musa, aliyokuwa ameitoa Bwana, Mungu wa Israeli; naye mfalme akamjalia matakwa yake yote, kama mkono wa Bwana, Mungu wake, ulivyokuwa pamoja naye.
7 Nao wakakwea baadhi ya wana wa Israeli, na wa makuhani, na wa Walawi, na waimbaji, na mabawabu, na Wanethini, ili kwenda Yerusalemu, katika mwaka wa saba wa mfalme Artashasta.
8 Naye Ezra akafika Yerusalemu mwezi wa tano katika mwaka wa saba wa huyo mfalme.
9 Maana alianza kukwea kutoka Babeli siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, naye akafika Yerusalemu siku ya kwanza ya mwezi wa tano, kama mkono mwema wa Mungu wake ulivyokuwa pamoja naye.
10 Kwa maana huyo Ezra alikuwa ameuelekeza moyo wake kuitafuta sheria ya Bwana, na kuitenda, na kufundisha maagizo na hukumu katika Israeli”.
Utaona mbeleni baada ya Ezra kuingia nchi ya Ahadi, alikuta kasoro nyingi watu tayari walikuwa wameshaanza kufanya machukizo ya kuoa wanawake wageni, kama alivyofanya Sulemani jambo lililosababisha Israeli kugawanyika, na Ezra kama Mwandishi aliijua vizuri Torati hivyo akawaonya na kuwasaidia Wana wa Israeli na kuwarejesha tena kwa Mungu wao.
Na kwa ushujaa wote huo Mungu alimuheshimu, hakuwa Nabii, hakuwa anaona maono, hakuwa mtu mkubwa sana, lakini kwa Moyo wake wa kuwasaidia ndugu zake na kuwarejesha kwenye Torati Mungu alimheshimu, mpaka leo hii tunazisoma habari zake. Hiyo yote ni kwasababu alikuwa msaada kwa wengine kama jina lake lilivyo EZRA Maana yake MSAADA. Hivyo ni vizuri ukakipita kitabu hichi mwenyewe utapata vitu vingi vipya usivyokuwa unavijua hapo kwanza.
Bwana akubariki. Usikose mwendelezo wa vitabu vinavyofuata.
Kwa maombezi/ Ushauri/ Ratiba za Ibada/Maswali/ Whatsapp/ Piga namba hizi: +255693036618/ +255789001312
Mada Nyinginezo:
MUNGU NDIYE ANAYEISHAWISHI MIOYO.
NYAKATI SABA ZA KANISA NA WAJUMBE WAKE.
Shalom, mtu wa Mungu karibu tujifunze maneno ya Mungu, ambayo ndio kweli pekee inayoweza kumfungua mtu moja kwa moja bila kubakisha chembe zozote za vifungo nyuma..
Leo kwa neema za Bwana tutamtazama mtu anayeitwa Nehemia, Jina lake limekuwa kubwa kutokana na kuwa tunakiona kitabu chake kikiwa miongoni mwa vitabu vitakatifu (BIBLIA), Lakini Nehemia kama tunavyomsoma hakuwa mtu wa maana sana tukizungumza kwa ngazi za kibiblia, hakuwa nabii, wala hakuzaliwa katika familia za kikuhani, Nehemia alikuwa ni mnyweshaji wa mfalme, mhudumu aliyekuwa anayepanga vinywaji mezani pa mfalme.
Lakini leo hii tunaisoma bidii yake, na sio tu kuisoma bali pia tunaiona sehemu ya kazi yake kwa macho yetu, Ukienda pale Yerusalemu utakutana na watu wengi ikiwemo wayahudi na watu wa mataifa mbalimbali wakisimama mbele ya kipande cha ukuta, na kuomba dua zao mbele za Mungu usiku na mchana..Sasa ukuta ule ulijengwa na Nehemia miaka karibia 2500 iliyopita, na mpaka sasa upo.
Nehemia hakuwa mtu wa kuona maono, lakini ni mtu aliyejitoa kwa ajili ya kazi ya Mungu zaidi hata ya manabii na watu wengine..Wakati mwingine aliifanya kazi ya Mungu akidhani kama Mungu vile hayupo karibu naye mpaka akawa anafikia hatua ya kusema Unikumbuke Ee Mungu wangu kwa mema yote niliyowafanyia watu hawa (Nehemia 5:19, 13:14, 13:22)..
Leo hii sisi ndio tunaojua ni jinsi gani Mungu amemkumbuka..Kumbukumbu lake linasomwa vizazi baada ya vizazi,
Hivyo hatutaenda sana kwa undani kuutazama ujenzi aliofanya lakini tutajifunza kitu kimoja kwake ambacho kitatufaa sisi hata katika mambo yetu ya kawaida tunayoyapitia kila siku..Ukisoma pale utaona mwanzoni kabisa Nehemia alipokuwa anafanya kazi yake ya kuhudumu mezani pa mfalme, baadhi ya ndugu zake walimletea taarifa kuwa Yerusalemu umebomolewa, na kuta zake zimetoketezwa na moto, hivyo hilo lilimuhuzunisha sana na kumfanya alie na kuomboleza kwa muda mrefu, mbele za Mungu na kufunga..
Ukichunguza pale utagundua Nehemia alikuwa katika hali ya uzuni na maombolezo kwa muda wa miezi minne, akimwomba Mungu ampe kibali kutoka kwa mfalme kwenda kuikarabati nyumba ya Mungu iliyokuwa Yerusalemu na mji, lakini cha ajabu ambacho ninataka ukione hapa, ni kuwa wakati wote huo Nehemia akiwa katika maombolezo, mfalme hakugundua kitu chochote kinachoendelea ndani ya Nehemia..Mpaka wakati ambapo Nehemia ameacha sasa kuhuzunika, anacheka, anamuhudumia mfalme, ndipo mfalme akaona kitu cha tofauti katika uso wa Nehemia..
Nehemia 2:1 “Ikawa katika mwezi wa Nisani, mwaka wa ishirini wa mfalme Artashasta, na divai imewekwa mbele yake, nikaishika ile divai, nikampa mfalme. NAMI MPAKA SASA SIKUWA NA HUZUNI MBELE YA MFALME WAKATI WO WOTE.
2 Basi mfalme akaniambia, Mbona umesikitika uso wako, nawe huna ugonjwa? Nini hii, isipokuwa ni huzuni ya moyo? Ndipo nikaogopa sana.
3 Nikamwambia mfalme, Mfalme na aishi milele; kwani uso wangu usiwe na huzuni, iwapo mji, ulio mahali pa makaburi ya baba zangu, unakaa ukiwa, na malango yake yameteketezwa kwa moto?
4 Ndipo mfalme akaniambia, Una haja gani unayotaka kuniomba? Basi nikamwomba Mungu wa mbinguni.
5 Nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na ikiwa mimi, mtumishi wako, nimepata kibali machoni pako, tafadhali unipeleke mpaka Yuda, niuendee mji wa makaburi ya baba zangu, nipate kuujenga.”
Unaona? Ukiangalia utaona kile kitendo cha yeye kutokuonyesha dalili yoyote ya nje kuwa yupo katika maombolezo halafu mtu anamwambia yupo katika maombolezo ndicho kilichomwogopesha Nehemia, pengine alijiuliza kwanini wakati wote wa nyuma nikiwa katika huzuni inayoonekana mfalme hakugundua chochote iweje iwe leo?.Mungu tangu zamani huwa hategemei hisia za mtu kumsaidia kuleta majibu ya maombi yake..
Mungu hataki wakati mmoja tumlilie yeye, na wakati huo huo tumlilie mwanadamu, au wakati mmoja tumwonyeshe yeye hisia Fulani na wakati huo huo tumwonyeshe mwanadamu hisia hizo hizo, kwamfano unaweza ukawa unapitia shida Fulani, au unataka upandishe ngazi fulani kazini, au unamdai mtu na unafahamu kabisa mtu Fulani anaweza kukusaidia, na wewe ukafanya uamuzi wa busara kwenda kumwomba Mungu kwa kufunga, sasa ukianza kujionyesha tena kwa Yule mtu unashida Fulani, kwa vitendo Fulani Fulani ili akuone, nataka nikuambie Mungu atasubiri kwanza uache vitimbwi hivyo ndipo akusaidie,..Lakini ukitulia na kuishi kwa njia ya kuonyesha kama haupitii shida yoyote au huna haja ya chochote lakini ndani unapitia,..bali huku nyuma ni Mungu tu ndio unayemlilia kila siku, nataka nikuambie utauvuta muujiza wako haraka kuliko unavyodhani.
Na ndio maana Bwana Yesu alisema,
Mathayo 6.16 “Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao.
17 Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso;
18 ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi”.
Unaona? Mungu hapendi mambo yetu ya siri mtu mwingine ayajue, Embu jaribu kufikiria kama Nehemia angeonwa na mfalme wakati wa kuonesha huzuni zake mbele ya watu, ni wazi kuwa angedhani ni kwasababu ya kulia kwake ndio maana kaonewa huruma na mfalme, lakini siku alipobadilisha uso wake, ndipo alipomshangaa Mungu.
Na sisi tutumie kanuni hii ya Mungu ili tufanikiwe..Bwana akubariki sana.
Ikiwa bado maisha yako bado yapo mbali na wokovu, mlango wa neema bado upo wazi kwa ajili yako, nakushauri uingie sasa nawe uanze kuufurahia uzuri wa Mungu..Wewe mwenyewe unaona dunia inavyochosha, hakuna haya ya kueleza ulitazamia ingekupa amani moyoni mwako, lakini hiyo amani mpaka sasa huioni, Nataka nikuambie ni mmoja tu ndiye aliyeahidi kutoa AMANI ya kweli ambayo ulimwengu hautoi naye ni Yesu mwenyewe huipati kwa mwingine yeyote..
Yohana 14:27 “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.”
Maran atha!
Mada zinazoendana:
UWEZA WA MUNGU UNAONEKANA WAPI?
Moja ya dhambi kuu inayopeleka wengi kuzimu ni kutokusamehe…Bwana alisema, msipowasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni naye hatawasamehe ninyi makosa yenu (Mathayo 6:15). Ikiwa na maana kuwa, unaweza ukaomba toba kuanzia asubuhi mpaka jioni, lakini ikawa ni bure mbele za Mungu endapo ukiwa ndani ya moyo wako hujamsamehe mtu Fulani aliyekukosea.
Maadamu tupo hapa duniani, hatutaachwa kukosewa, kila siku tutaudhiwa, tutakasirishwa, tutaumizwa n.k lakini hatuna budi kusamehe kutoka moyoni, huo ndio mtihani wetu.Kama hujamsamehe mtu aliyekutukana kipindi Fulani nyuma, fahamu kuwa Bwana hajakusamehe tusi ulilomtukana mtu Fulani huko nyuma, aidha kwa mdogo au kwa moyo. Kama hujamsamehe mtu aliyekuudhi huko nyuma fahamu kuwa Mungu hajakusamehe maudhi yako uliyomwudhi mtu mwingine huko nyuma…
Kama hujamsamehe mtu aliyekusengenya fahamu kuwa na wewe hujasamehewa dhambi uliyowahi kumsengenya mtu mwingine, na makosa mengine yote, kama hujamsamehe aliyekutendea tambua na ya kwako pia hayajasamehewa, hali kadhalika kama ulimsamehe mtu na baadaye ukarudia tena kuukumbuka uovu wake na kumwekea kinyongo, Mungu naye ataukumbuka uovu wako uliowahi kumfanyia mtu Fulani huko nyuma, na hivyo toba zako zote ulizowahi kuzifanya zikawa ni bure.…Maandiko yanasema hivyo (Mathayo 18:23-35).
Kadhalika biblia imetuonya juu ya kisasi. Kisasi ni kitendo cha kumrudishia uovu mtu aliye kutendea uovu. Mafundisho yoyote yanayohusiana na kumlipizia mtu kisasi ni mafundisho ya uongo, yanayopalilia roho ya kutokusamehe, na yanalenga kuwapeleka watu jehanamu. Hubiri lolote linalokufanya utoke na hasira dhidi ya adui yako, limetengenezwa na roho ya Adui, Hubiri lolote linalokuachia hamu kubwa ya mtu Fulani anayekuchukia, au aliyekuudhi, kufa, au kuteseka, au kupigwa ni hubiri la shetani…Hubiri lolote linalokuacha katika hali ya kumpania mtu Fulani aliyekudharau ni fundisho lililotengenezwa na yule adui shetani..Biblia inasema…
Mithali 20:22 “Usiseme, Mimi nitalipa mabaya; Mngojee Bwana, naye atakuokoa”.
Waebrania 10:30 “Maana twamjua yeye aliyesema, Kupatiliza kisasi ni juu yangu, mimi nitalipa. Na tena, Bwana atawahukumu watu wake. 31 Ni jambo la kutisha kuanguka katika mikono ya Mungu aliye hai”
Warumi 12:19 “Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana. 20 Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake. 21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema”
Roho wa Kristo anatupigania kwa namna isiyoweza kuonekana kwa macho, ukiona kuna mtu anakuchukia jua ni sehemu ndogo sana ya roho ya shetani inayojidhihirisha juu yako…, laiti ungefunuliwa macho katika ulimwengu wa roho uone ni maroho gani yanakuwinda usiku na mchana, na jinsi gani Mungu amekuepusha nayo, usingeona kama ndugu yako kukuchukia au kukusengenye ni Adui…Laiti ungeona ni kwa jinsi gani hata usiku wa leo ulikuwa umepaniwa maangamizi, na Mungu kaepusha huo mpango wa mapepo..usingeona mtu aliyekutukana kama ni Adui.
Hivyo leo hii kama ulikuwa una mpango wa kumlipizia mtu Fulani mabaya, uzike huo mpango leo na utaona Mungu atakavyokupa mema, utapata amani ambayo hujawahi kuipata na utaona mzigo Fulani mzito umeondoka ndani yako, huo mzigo utakaoona umeondoka ndio mzigo wa dhambi zako na wewe Mungu kaziondoa, tenga muda kumbuka ni wangapi hujawasamehe kwa moyo, ukishawapata tamka kuanzia leo umewasamehe, utaona kuna mzigo Fulani umeutua ndani ya moyo wako, hiyo hali ni konesha kuwa na wewe Kristo katua mzigo wako chini.
Bwana atusaidie katika jambo hili, tuweze kuishi Maisha ya msamaha na ya kujiepusha na visasi.
Bwana akubariki.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada zinazoendana:
SAMEHE KUTOKA NDANI YA MOYO WAKO.
Swali ambalo ni wajibu wetu sote kulijua ni juu ya Roho saba za Mungu, kwamba zenyewe ni nini na zinatendaje kazi. Na pia ni muhimu kufahamu juu ya makanisa saba
JIBU: Tukisoma mandiko yanatuambia kuwa Mungu ni mmoja, agano la kale linatuthibitishia hilo, (Kumb 6:4), vile vile agano jipya linatuthibitishia hilo, tukisoma katika (Marko 12:29) pale Bwana Yesu alipofuatwa na Yule mwandishi na kuulizwa ni amri ipi iliyo ya kwanza alijibu..
“….Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; 30 nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.”
Hivyo maagano yote mawili yanathibitisha kuwa Mungu ni mmoja, lakini sasa kwanini tunamwona YESU kama Mungu, kwanini tunamwona Roho kama Mungu, tena tukiendelea kusoma tunaziona kuna Roho nyingine saba za Mungu, swali ni je! hawa wote wametokea wapi, ikiwa Mungu ni mmoja?.Hili ni moja ya swali lililoleta migawanyiko mikubwa sana sio tu katika ukristo, bali hata kwa wale wasioamini limewafanya wazidi kwenda mbali zaidi kwa kushindwa kuelewa utendaji kazi wa Mungu.
Tukiweza kujua kuwa kitu kinachoitwa Dhambi na kutengwa mbali na uso wa Mungu ndicho chanzo kilichopelekea tumwone Mungu katika taswira nyingi tofauti tofauti, tukilifahamu hilo basi hatutashindwa kumwelewa Mungu katika nafasi yake ya Uungu.. Na ameamua kufanya hivyo makusudi kwa lengo la kuturejesha sisi asingefanya hivyo leo hii tungekuwa makapi sisi. Laiti kama tusingeanguka katika dhambi, tungemwona Mungu na kuzungmza na Mungu kama yeye tu tusingejua kitu kingine cha ziada kumuhusu yeye, tabia zake zilivyo.
Kwamfano kulikuwa hakuna sababu ya Mungu kuutafuta mwili na kuiweka Roho yake mwenyewe ndani yake aje asulubiwe ili atupatanishe sisi na yeye kama tusingepotea katika dhambi, vile vile kulikuwa hakuna haja ya Roho Mtakatifu kuwa msaidizi wetu kama tungekuwa tunazungumza na Mungu uso kwa uso kama ilivyokuwa pale Edeni Adamu alipokuwa anazungumza na Mungu..
Ni sawa tu ni kifaa kinachoitwa simu, kama sio suala la umbali kati ya mtu mmoja na mwingine, simu isingehitajika katika jamii, kusingekuwa na haja ya wewe kuisikia sauti yangu kwenye kifaa kinachoitwa simu..Lakini je! Fikiria pia siku ile uliposikia mimi ninazungumza ndani ya kifaa kile, je ulisema nimegawanyika?, na kuwa wawili, kwamba mimi unayeniona tukizungumza uso kwa uso ni tofauti na Yule unayenisikia kwenye kifaa-simu? Ukweli ni kuwa utasema ni kifaa tu lakini mimi ni Yule Yule..Na ndivyo ilivyokuwa kwa Bwana Yesu kuja kwake duniani, ..yule ni Mungu yule yule kauvaa mwili lakini sio MUNGU wa pili katika UUNGU, kama wengi wanavyodhani…YESU na Mungu BABA, sio Mtu na Mtu mwenzake, Ni Mungu yule Yule mmoja isipokuwa amekuja kwetu katika vazi lingine.
Kwa maelezo marefu ya kufahamu kwanini Yesu alikuja duniani, tutumie ujumbe inbox tukutumie somo lake..
Vivyo hivyo na Roho wake Mtakatifu, Yule sio Nafsi ya Tatu katika uungu bali ni ofisi ya tatu ya Mungu Yule Yule mmoja katika hatua zake za kuturejesha sisi katika mstari wake wa ukamilifu..Kama tusingekuwa katika hali ya dhambi na kumsahau Mungu, basi hakukuwa na haja ya sisi kupewa msaidizi, lakini Mungu aliona ajitoe sehemu ya nafsi yake iliyo moja aje kwetu kama Roho Mtakatifu ili atukumbushe yale yote Bwana Yesu aliyotuagiza.(Yohana 14:26).
Vile vile Roho Mtakatifu alipoachiwa pale Pentekoste, hakuachiwa kwa mtu mmoja mmoja tu peke yake kama wengi wanavyodhani, bali aliachiwa pia na kwa kanisa kwa ujumla..Hivyo kulikuwa na makanisa tofauti tofauti kulingana na wakati na majira..Sasa Roho huyu huyu aliyetenda pia kazi tofauti tofauti kulingana na kanisa husika..Ndio yale makanisa saba tunayoyasoma katika kitabu cha ufunuo sura ya 2&3, ..
Ufunuo 1:4 Yohana, kwa yale makanisa saba yaliyoko Asia; Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwake yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja; na zitokazo kwa roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi;
Sasa biblia inaposema Roho saba za Mungu nadhani utakuwa umeelewa kuwa hakuna tena Roho nyingine 7 zilizo mbele za Mungu, bali ni Roho Yule Yule mmoja akitenda kazi katika yale makanisa saba, Biblia inasema pia ndio macho 7 ya Mungu (Ufunuo 5:6), Na Taa 7 za moto (Ufunuo 4:5).
Kwa maelezo marefu juu ya nyakati saba za Kanisa,pia tutumie ujumbe inbox tukutumie somo lake..
Hivyo hizo zote ni hatua za Mungu za utendaji kazi lakini ni yeye Yule Yule, Mungu mmoja, hajagawanyika..
Lakini Swali lingine mtu anaweza kuuliza je! Tunafanya makosa kumwabudu YESU au Roho Mtakatifu? Jibu ni hapana, unapomwabudu Bwana YESU umemwabudu Mungu Yule Yule mmoja, Unapomwabudu Roho Umemwabudu Mungu Yule Yule mmoja, ni ofisi tu imebadilika, lakini Mungu ni Yule Yule umwabuduye..
Hivyo YESU ni Mungu mwenyewe katika mwili (1Timotheo 3:16), Roho Mtakatifu ni Mungu mwenyewe katika roho, vile vile zile Roho 7 za Mungu ndio Yule Yule Roho mmoja na ndio Mungu mwenyewe YEHOVA muumba wa mbingu na nchi, Hana mwanzo wala hana mwisho, ALFA NA OMEGA. Haleluya!
Je unampenda kwa moyo wako wote? Jibu unalo.
Ubarikiwe.Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Washirikishe na wengine habari hizi
Mada zinazoendana:
KWANINI YESU KRISTO ALIKUJA DUNIANI?
JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?
ACHENI MJUE YA KUWA MIMI NI MUNGU.
MUNGU KUSEMA NA WEWE PEKEE, HAITOSHI KUKUPA USHINDI.
SWALI: Huyu AZAZELI ni nani? Kwa sababu ukisoma maandiko naye aikuwa anapewa kafara? (Walawi 16:8).
JIBU: Neno Azazeli linaonekana likitajwa mara moja tu katika kitabu cha Mambo ya Walawi sura ya 16, Azazeli sio mtu au kuhani bali ni mbuzi aliyetengwa kwa ajili ya upatanisho wa dhambi za Wana wa Israeli ndiye aliyejulikana kwa jina hilo, ambaye yeye hakuwa anachinjwa kwa ajili ya dhambi kama mbuzi wengine hapana bali yeye alikuwa anachukuliwa akiwa hai mpaka jangwani na kutelekezwa huko.
Maagizo hayo Mungu aliwapa wana wa Israeli, wayafanye katika siku ile kuu ya Upatanisho ambayo ilikuwa inafanyika mara moja tu kwa mwaka, tarehe 10 mwezi wa 7 wa kalenda ya Kiyahudi, wakati huo ndio ule Kuhani Mkuu anakwenda kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi za wayahudi wote siku hiyo kila mtu alipaswa asifanye kazi yoyote, bali unatulia nyumbani kwake ukiitesa nafsi yake kwa dhambi zake.
Sasa katika siku hii Kuhani Mkuu kwanza anawajibika kufanya upatanisho kwanza kwa ajili ya nafsi yake yeye mwenyewe na ya watu wake (wa nyumbani kwake), kisha ndio aende kufanya upatanisho wa dhambi za watu wengine, vinginevyo atakufa. Sasa katika kufanya upatanisho wa wana wa Israeli aliagizwa atwae mbuzi wawili kutoka katika mkusanyiko wa Wayahudi kwa sadaka ya dhambi na kondoo mmoja mume kwa sadaka ya kuteketezwa (Walawi 16:5), baada ya hapo kuhani mkuu anasimama mbele ya hema na kupiga kura kati ya wale mbuzi wawili.
Walawi 16:7 “Kisha atawatwaa wale mbuzi wawili na kuwaweka mbele za Bwana mlangoni pa hema ya kukutania.
8 Na Haruni atapiga kura juu ya wale mbuzi wawili; kura moja kwa ajili ya Bwana; na kura ya pili kwa ajili ya Azazeli.”
Akishamaliza mmoja anachukuliwa kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa kwa dhambi za watu wote,
kisha damu yake inachukuliwa na kwenda kunyunyizwa katika hema ya kukutania na madhabahu, na yule wa pili hauliwi bali kuhani mkuu anamchukua na kuweka mikono yake yote miwili juu ya pembe za Yule mbuzi ambaye ndio anaitwa Azazeli kisha kuhani anaungama makosa yote na dhambi zote za wana wa Waisraeli walizozifanya juu ya mbuzi Yule,..baada ya hapo mbuzi huyo anakabidhiwa kwa mtu mmojawapo kisha anapelekwa jangwani mbali kabisa na makazi ya watu na kutelekezwa huko. Ndipo ouvu wa Israeli unafunikwa.
Walawi 16:21 “Na Haruni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha yule mbuzi aliye hai, na kuungama juu yake uovu wote wa wana wa Israeli, na makosa yao, naam, dhambi zao zote; naye ataziweka juu ya kichwa chake yule mbuzi, kisha atampeleka aende jangwani kwa mkono wa mtu aliye tayari.22 Na yule mbuzi atachukua juu yake uovu wao wote, mpaka nchi isiyo watu; naye atamwacha mbuzi jangwani.”
Ni picha kamili tunayoiona katika agano jipya, Kristo akiwa kama Azazeli wetu alichukua dhambi zetu na mashutumu yetu yote, akasulibiwa nje ya mji, alihesabiwa kuwa si Kitu kwa ajili yetu.. Na kwa kupitia yeye dhambi zetu zinaondolewa moja kwa moja, tofauti na mbuzi Yule ambaye ikifika mwakani anapaswa atolewe mwingine…Ni raha kiasi gani ukikombolewa na Kristo,.Ukisamehewa dhambi zako, umesamehewa milele. Haleluya.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
KUFUKIZA UVUMBA NDIO KUFANYAJE?
SIKUKUU 7 ZA KIYAHUDI ZINAFUNUA NINI KWETU?
SANDUKU LA AGANO LILIKUWA LINAWAKILISHA NINI KATIKA AGANO JIPYA?
NAOMBA KUJUA WATAKAOENDA MBINGUNI JE! NI WENGI AU WACHACHE?
JIBU: Ndoto ni mfululizo wa picha na mawazo na hisia zinazokuja wakati mtu amelala, Na hizo zinakuja pasipo hiyari ya mtu, kwamba mtu hapangi au haamui ni nini cha kuota! zinakuwa zinajitengeneza zenyewe tu!..Na ndoto zinaweza kuathiriwa na shughuli zetu tunazozifanya kila siku au mazingira yanayotuzunguka au yaliyokuwa yanatuzunguka kipindi kifupi nyuma (Mhubiri 5:3, Isaya 29:8),
Na kuna ndoto zinatokana na shetani na nyingine zinazotokana na Mungu (Mwanzo 28:12, 37:5-10).
Na Maono hayana tofauti sana na ndoto, Maono ni mawazo ya picha na hisia yanayokuja wakati mtu akiwa hajalala…Na haya vile vile hayaji kama atakavyo mtu, wala mtu haamui ni aina gani ya maono ayaone wala huwezi kuyavuta kama mtu anavyovuta usingizi…. anajikuta tu ghafla anaona kitu ambacho sio cha kawaida au cha kawaida, au unakuta anaona tukio Fulani kama vile anaota, na anaporudi anajikuta alikuwa hajalala, pengine alikuwa anatembea au amesimama au alikuwa anaongea na mtu na analikumbuka lile tukio aliloliona kwenye hilo ono.
Na maono yapo yanayotokana na shughuli nyingi, hususani watu ambao wana msongo mkubwa wa mawazo na walioathirika na matumizi ya madawa makali, kadhalika yapo yanayoletwa na shetani haya yanawatokea wengi ambao ni wachawi au wenye roho za mapepo..na yapo yanayoletwa na Mungu.
Tofauti na inavyoaminiwa na wengi kuwa ni lazima kila mtu aliyezaliwa mara ya pili aone maono ya kiMungu, ukweli ni kwamba sio lazima kila mtu aone maono, mtu anaweza akazaliwa mara ya pili na hadi anakufa akawa hajawahi kuona ono hata moja na akaenda mbinguni..Kwasababu suala la kuona maono au kutabiri hivyo ni vipawa vya Roho Mtakatifu, na anapanga nani ampe na nani asimpe, ambaye hajapewa basi atakuwa amepewa kipawa kingine cha kipekee tofauti na hicho, na aliyepewa atakuwa amenyimwa vipawa vingine vya Roho. Haiwezekani watu wote wafanane au wawe na karama zinazofanana na haiwezekani mtu mmoja akawa na karama zote yeye peke yake (1 Wakorintho 12:29-31).
Jambo la muhimu ni kuzaliwa mara ya pili na kuwa kiumbe kipya,(Wagalatia 6:15) na kuishi kulingana na Neno, kuona maono au kutabiri au kufundisha hivyo sio vipimo vya utakatifu au tiketi za kwenda mbinguni (Mathayo 7:22).
Bwana akubariki.
Kwa mawasiliano/mafundisho zaidi kwa njia ya whatsapp, tutumie ujumbe kwenye
namba hizi: +255789001312/ +255693036618
Mana zinazoendana:
NITAJUAJE KAMA NDOTO NI YA MUNGU AU YA SHETANI?
FUATILIA NDOTO HII, UTAJIFUZA KITU.
VIUNO VYENU VIWE VIMEFUNGWA NA TAA ZENU ZIWE ZINAWAKA.
TUSIPOUTHAMINI WOKOVU TUTAPATAJE KUPONA?
NI TAMAA IPI HIYO HAWA ALIAMBIWA ITAKUWA KWA MUMEWE?
JE! ASKARI MAGEREZA AKIAMURIWA KUMNYONGA MTU ANATENDA DHAMBI?