MUONEKANO MPYA WA YESU BAADA YA KUFUFUKA.

MUONEKANO MPYA WA YESU BAADA YA KUFUFUKA.

Muonekano mpya wa yesu baada ya kufufuka, unabeba somo gani?


Bwana Yesu alipokuwa bado anaishi duniani, ilikuwa ni rahisi kumtambua, kwani kwa sura yake tu watu waliweza kumtambua kuwa huyu ndiye. Lakini mara baada ya kufufuka kwake, mambo yalikuwa tofauti kabisa, haikuwezekana kumtambua tena Bwana Yesu kwa sura yake..Ilihitaji kipimo kingine tofauti..

Hilo tunalithibitisha sehemu kadha wa kadha, wengine walipomwona walidhani ni mtunza bustani makaburini, wengine walidhani ni mpita njia tu, na wengine walidhani ni mzee Fulani tu anapunga upepo beach..Na kama wangekikosa hicho kipimo kingine ndani yao cha kumtambua Yesu basi wasingekaa wamjue daima haijalishi huko nyuma waliishi naye na kutembea naye na kulala naye muda mrefu kiasi gani..kamwe wasingemjua.

Kwamfano embu tumwangalie Mariamu Magdalene, yeye ile siku ya kwanza ya juma, siku Yesu aliyofufuka, ndio aliyekuwa wa kwanza kufika pale makaburini, lakini alipomkosa Bwana, akidhania kuwa ameibiwa, alikwenda kuwaambia mitume, nao walipokwenda hawakukuta mtu kaburini.. wakaamua kuondoka zao, Sasa wakati Mariamu akiwa pale kaburini analia, kulikuwa na mtu yupo pale muda mrefu tu, anazunguka zunguka, pengine wakina Petro walimwona wakadhani ni watu wale wasio na shughuli wanaozunguka makaburini, lakini Mariamu alipokaa pale muda kidogo akiwa analia, ndipo Huyu mtu ambaye alimwona kama mtunza bustani akamfuata na kumuuliza unatafuta nini?.

Mariam akasema: ikiwa ni wewe ndio umemuiba Bwana wangu niambie..Kumbe hakujua anayezungumza naye ni YESU mwenyewe..Ndipo Yesu akalitaja jina lake Mariamu!..Na alipolitaja tu, Hapo hapo Mariamu akaitambua sauti ile, ni ile sauti yake yenye uweza, sauti ile ile iliyomwita Lazaro atoke makaburini kipindi kile kule nyuma, sasa imemwingia na yeye mpaka kwenye vilindi vya moyo wake ikampa uhakika kuwa huyu ndiye BWANA….Haikujalisha sauti ilikuwa ni ya mtu mwingine,inayofanana na mtu wa taifa lingine, lakini uweza tu wa ile sauti ulimpa uhakika kwamba huyu ndiye Bwana..(Soma..Yohana 20:1-18).

Lakini kama Mariamu asingekuwa na ushuhuda huo huko nyuma, basi ingekuwa ni rahisi kumpoteza Yesu..

Vivyo hivyo wale watu wawili ambao walikuwa wanakwenda katika kile Kijiji cha Emau, nao pia walipokuwa wanatembea njiani, Yesu alikutana nao isipokuwa katika sura nyingine..Na akaanza kuzungumza nao habari za kutabiriwa kwake, kuja kwake, na kufufuka kwake..Wale watu waliposikia tu yale maneno, jinsi yalivyokuwa yenye nguvu kwa namna ile ile waliyokuwa wanamsikia Bwana akifundisha makutano akiwa bado hai, hawakumuacha aondoke hivi hivi, wakamkaribisha nyumbani kwao, ndipo baada tu ya kuumega mkate na kuwapa, wakafumbuliwa macho wakatambua kuwa alikuwa ni YESU. Na saa hiyo hiyo akatoweka mbele ya macho yao.(Luka 24:13-33)..Lakini kama wasingetilia maanani uweza uliokuwa unatoka ndani ya maneno yale..wasingekaa wamtambue Kristo.

Mwisho kabisa Petro na wenzake, walipokuwa wanakwenda kuvua samaki, baada ya kuhangaika usiku kucha hawajapata kitu..Asubuhi yake kwa mbali walimwona mtu kama mzee akiwa pwani, mwenye sura wasioijua, mtu yule akawauliza wanangu mmepata kitoweo, wakasema hapana Bwana, akawaambia, tupeni jarife upande wa pili, wakidhani ni mzee tu wa kawaida anawashauri, wajaribu bahati yako, ..Na walipotupa tu jarife, wakapata samaki wengine..Mwanafunzi mmoja alipoiona ile ishara, akatambua kuwa hii ni ishara ile ile aliyotufanyia Bwana kipindi kile akiwa hapa duniani..Ndipo Yule mwanafunzi akamwambia Petro aliyetupa maagizo haya ni Bwana Yesu..Petro kusikia hivyo muda huo huo akapiga makasia kumfuata Pwani..

Biblia inatuambia walipomwona Bwana japo aliwatokea katika sura nyingine tofuati kabisa..Lakini hakuna hata mmojawao aliyetaka uthibitisho kama yeye ni Bwana kweli au la, Wote walipata uhakika ule, kwa ule uweza wake mkuu , na yale maneno aliyokuwa anazungumza nao akiwa pale ufukweni..(Yohana 21:1-25)..Lakini kama wasingeyaona matendo makuu kama yale Bwana aliyowahi kuwafanyia huko nyuma, kamwe wasingejua hata kama yule ni YESU. Wangedhani ni mzee Fulani tu amewapa dili la kazi.

Hivyo ndivyo Kristo alivyochagua kujidhihirisha kwa watu baada ya kufufuka kwake..Mpaka ikawafanya hata wengine wamtilie shaka..Hao ndio wale ambao walioukosa ushuhuda wake ndani yao..ndio wale waliokuwa wanalitazama umbo la Yesu, lakini hawayatafakari matendo yake, na ishara zake.

Mathayo 28:16 “Na wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda Galilaya mpaka mlima ule aliowaagiza Yesu. 17 Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi yao waliona shaka”.

Sasa kwa mabadiliko hayo, mitume kuanzia huo wakati wakatoa akili zao kabisa katika kuitegemea sura ya YESU, kama kipimo cha kumtambua Kristo mpaka kuutegemea ushuhuda wa YESU Maishani mwao.

Hivyo sura ya Yesu ikawa haina umuhimu tena kwao..Na ndio maana utaona Mitume mahali popote hawakuwahi kujisifia umbile la Yesu au Sura yake, au sauti yake..Bali ule Ushuhuda wa YESU uliokuwa ndani yao, ndio uliowafanya wamjue na kumtambua Yesu.

Vivyo hivyo leo hii KRISTO yupo kila mahali, lakini kama umeukosa ule ushuhuda wake ndani yako, utamwona tu kama mtunza bustani, utamwona tu kama mpita njia, utamwona tu kama mzee Fulani..

Ndio maana kuna umuhimu sisi tunaojiita wakristo, kujifunza biblia sana..kwasababu wakati utafika Kristo atajidhihirisha kwako, lakini hutamtambua kwasababu huujui ule ushuhuda wake alipokuwa hapa duniani ulivyokuwa.

Kwamfano Injili ya Kristo inapohubiriwa kwako, na unaona kabisa imekuja kwa ukali, na uzito, na kwa nguvu, labda inakutaka wewe ufanye jambo Fulani.. Sasa kwa kuwa wewe huna ushuhuda wa Yesu ndani yako, unaokushuhudia hata katika maandiko kuwa kulikuwa na watu wawili wa Emau, ambao neno la Kristo liliwajia kwa uzito kama huo, wakachukua hatua ya kusikiliza mpaka mwisho..Wewe unapuuzia, Unadhani ni mlokole Fulani anahubiri, au mchungaji tu Fulani, au kijana tu Fulani anauhibiri..kumbe hujui unampuuzia Kristo mwenyewe.

Na wakati huo huo unakesha kuomba kwamba Bwana akutokee, unataka akutokee vipi? Unataka umwone kavaa mavazi meupe, mwenye nywele ndefu, ndio umtambue?. Hilo wazo na ufute. YESU ameshafufuka, haji kwetu kwa muonekano ule tena.

Huu ni wakati wa kumjua yeye kwa ushuhuda wake.Hapo ndipo tutakapomwona akitembea katika Maisha yetu kila siku. Na hiyo inakuja pale tu Neno la Kristo linapokaa kwa wingi ndani yetu.

Vingenevyo tutamtilia shaka tu sikuzote, hata akitokea kwa sura ipi, kama wale wengine walivyomtilia shaka kule Galilaya, na wewe utamtilia shaka hivyo hivyo.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye boksi la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

TULICHUNGUZE UMBO LA YESU NA MWENENDO WAKE.

USIISHIE KUTAZAMA JUU, ENDELEA MBELE.

TUWATAFAKARI NZIGE WA JANGWANI.

WAZAZI WA YOHANA NA YAKOBO.

LOLOTE ATAKALOWAAMBIA FANYENI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Daniel shotoli
Daniel shotoli
11 months ago

Nahitaji kuwa natumiwa masomo haya kwenye Email yangu yq shotolidanieljacob@gmail.com