Udhaifu shetani anaoupenda kwa mtu ni kufikiri fikiri…Tabia ya kufikiri fikiri inasababisha kupoteza ujasiri, na hata Imani…Kwamfano ukitaka kwenda kukutana na mtu, ukianza kutumia muda mrefu kufikiri fikiri itakuwaje utakapokutana naye …ni rahisi sana kuingiwa na woga na hata kupoteza shabaha ya kile ulichokuwa unakwenda kukifanya au kukisema.
Na katika Imani, kuna vitu vichache vidogo vidogo ambavyo ni vya kuvizingatia vinginevyo utajikuta unakosa ujasiri na utulivu kila mahali na kushindwa kumtumikia Mungu. Roho Mtakatifu anafanya kazi katika utulivu.
Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi maneno haya…
Mathayo 10:16 “Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua. 17 Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; 18 nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. 19 Lakini hapo watakapowapeleka, MSIFIKIRI-FIKIRI JINSI MTAKAVYOSEMA; maana mtapewa saa ile mtakayosema”.
Mathayo 10:16 “Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.
17 Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga;
18 nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa.
19 Lakini hapo watakapowapeleka, MSIFIKIRI-FIKIRI JINSI MTAKAVYOSEMA; maana mtapewa saa ile mtakayosema”.
Hapo Bwana alizungumzia katika eneo la kusimamishwa mbele za washitaki…kwamba hatupaswi kuogopa na kuanza kufikiri namna ya kujitetea au namna ya kujibu…badala yake TUTULIE!! Roho Mtakatifu afanye kazi yake…kwani wakati huo huo ukifika atatupa kinywa cha hekima ambacho kitategua mitego yao yote…
Hali kadhalika wakati wa kuhubiri ni hivyo hivyo..Unapotumwa na Roho Mtakatifu kwenda kusimama na kuhubiri…sio wakati wa kuanza kufikiri fikiri utakwenda kusema nini, nitawezaje kuhubiri muda wote huo uliopangwa, nitawezaje kupangilia maneno, nitawezaje kuombea, nitaaanzaje anzaje kuelezea mstari huu na ule. Ukishaanza kuruhusu hayo mawazo basi jua ni rahisi sana kumzuia Roho asitiririke vizuri ndani yako…
Unachopaswa kufanya baada ya kuliandaa somo, kwamba kuna ufunuo Roho Mtakatifu kakupa, kupitia katika roho yako mwenyewe au kupitia mtumishi wake…na hivyo unasikia kuongozwa kwenda kuwashirikisha wengine…moja kwa moja andaa mistari michache ambayo inashikilia somo lako..baada ya hapo muda uliobakia endelea kuombea mambo mengine…na subiri huo muda ufikie…na utakapofika anza kuzungumza…wakati unazungumza Roho Mtakatifu ataungana na wewe na utajikuta unatiririka kwa namna ambayo hata wewe mwenyewe utajishangaa.
Lakini ukianza kuogopa..na kufikiri fikiri…yule mchungaji anajua kuliko mimi, itakuwaje nikihubiri mbele zake, fulani anajua biblia kuliko mimi itakuwaje…nikikosea itakuwaje, nikiishiwa na maneno katikati itakuwaje…nitaweza kweli kumaliza lisaa lizima nikihubiri?..na sauti yangu hii ya kigugumizi itakuwaje?..nianze na mstari gani nimalize na mstari gani?
Usiwaze yote hayo…wala usiruhusu hivyo vikao vya maswali kuzunguka kichwani kwako…Roho Mtakatifu atakupa kinywa cha hekima saa ile ile utakayokuwa unahubiri. Na baada ya kuhubiri tu utajiona umerudia hali yako ya kawaida…Na kujishangaa umemalizaje lisaa haraka hivyo, umewezaje kupangilia maneno hivyo na si kawaida yako, utashangaa na lile Neno linawageuza watu, na wengine kufunguliwa na kuponywa…ukiona hivyo jua ni Roho Mtakatifu alikuwa kazini…wewe ulitumika tu kama chombo.
Sasa nguvu hiyo ya Roho Mtakatifu huwa inajaa na kupungua ndani ya mtu…lakini haiondoki ndani ya mtu…Mtu anapokuwa katika hali ya shughuli zake za kawaida au amelala inakuwa inapungua…lakini likitokea tu jambo! Huwa inashuka ndani ya mtu kwa nguvu…kwamfano mtu anaposimama kuhubiri, huwa inashuka ndani yake…hapo ndio mtu anajikuta anapata ujasiri wa kipekee, yale mambo aliyokuwa hawezi kuzungumza au kuyafanya anajikuta uwezo fulani umemwingia ghafla wa kuyafanya…au mtu wa Mungu anaposimamishwa mbele ya washtaki mahakamani au penginepo na hajui la kusema…ghafla anashangaa amepata hekima ya kujibu. Nk.
Ndio maana Bwana alisema “tusifikiri fikiri” maana yake ni kwamba upo wakati ambao utajiona huwezi wala hustahili kufanya kitu fulani, ni wakati wa kujiona mdhaifu…wakati huo sio wakati wa kufadhaika, kwasababu yupo Roho Mtakatifu atakayeshuka kukutia nguvu..Kama Mtume Paulo alivyosema kwa uweza wa Roho mahali fulani…
2Wakorintho 12:9 “Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana UWEZA WANGU HUTIMILIKA KATIKA UDHAIFU. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu”
Kama ni msomaji wa biblia utakuwa unazijua Habari za Samsoni…Mtu huyu si wakati wote alikuwa na nguvu..na wala biblia haisemi kwamba alikuwa ni mtu mkubwa kuliko wote, au kama Goliathi…alikuwa ni mtu wa kawaida tu…pengine hata alikuwa na misuli ya wastani tu, kama ya wanaume wengine ndio maana ilikuwa ni ngumu watu kujua asili ya nguvu zake ni nini?..kwasababu alionekana kama wengine tu..Sasa kilichokuwa kinatokea kwa Samsoni ni kwamba lilipokuwa linatokea jambo fulani ndipo zile nguvu zilimshukia…Sio wakati wote alikuwa nazo…wakati mwingine wowote alikuwa kama watu wa kawaida mwenye nguvu za wastani…Ila linapotokea jambo aidha maadui wamemzunguka ndipo zile nguvu za Roho Mtakatifu zinamshukia na kumpa uwezo wa ajabu wa kuwaangamiza…na baada ya hapo zile nguvu zinapungua na kurudia kuwa mtu wa kawaida…Mpaka tena wakati mwingine wa tukio..(Kasome habari za Samsoni kwa makini utaligundua hilo).
Sio yeye tu…hata baadhi ya wafalme na Waamuzi katika biblia…Kwamfano Mfalme Sauli, wakati kulipotokea vita katika Israeli na watu wanakosa ujasiri wa vita…ndipo Roho wa Mungu alikuwa anamshukia kwa nguvu na kumpa ujasiri wa ajabu wa kwenda vitani…ambao ulikuwa unawashangaza wengi.
Hivyo kuanzia leo usifikiri fikiri wakati wa kwenda kuifanya kazi ya Mungu kama ulikuwa una tabia hiyo..na sio tu kazi ya Mungu bali hata kazi yoyote ile..maadamu umempa Kristo Maisha yako na umezikabidhisha njia zako kwake..Kwasababu huko unakokwenda yeye atakuwa na wewe, kukupa kinywa, kukupa hekima, kukupa akili, kukupa ufahamu, kukupa uwezo, kukupigania, kukuongoza…Usijipime hapo ulipo akili uliyo nayo, utaishia kupaniki na kuishiwa nguvu, usijipime hekima hapo ulipo sasa…subiri mpaka utakapofika huko ndipo utaona Mkono wa Mungu…na utajua kuwa Mungu yupo na pasipo yeye wewe huwezi kufanya lolote…Hivyo endelea mbele usiangalie kushoto wala kulia..
Kutoka 14:14 “Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya. 15 Bwana akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele”
Kutoka 14:14 “Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.
15 Bwana akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele”
Bwana atubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
KWARESMA IPO KIMAANDIKO?
KUWA WEWE.
JE KUHUDUMU KWA NYIMBO ZA INJILI KUKOJE?
USIWE NA HOFU, USHUKAPO CHINI.
YEZEBELI ALIKUWA NANI
Rudi Nyumbani:
Print this post
Namshukuru Mungu kwa somo hili nimetiwa nguvu sana na kuamua kuendelea mbele nyuma mwiko.
Amen hongera sana, BWANA YESU akusaidie katika hilo..