SWALI: ‘Siku ya uovu’ inayozungumziwa katika Waefeso 6:13 Ni ipi? Waefeso 6:13 “Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.
JIBU: Ikiwa umedumu katika wokovu kwa muda mrefu utaelewa, si wakati wote mambo yatakwenda sawa kama unavyotaka wewe,
Bwana Yesu aliweka wazi kabisa juu ya suala hilo..akasema..
Mathayo 18:7 “Ole ni wa ulimwengu kwa sababu ya mambo ya kukosesha! Maana hayana budi kuja mambo ya kukosesha…
Unaona anasema, hayana budi kuja..Hiyo haijalishi wewe ni mtakatifu au la!. Si wakati wote shetani atakuwa anakuangalia ukiufurahia wokovu wako kwa kwa amani na utulivu, kuna wakati atapanga mashambulizi ya kukuangamiza, au kukufanya utetereke kwenye imani, au ya kukuudhi, kipindi hicho ukikipitia basi ujue hiyo ndio “siku ya uovu” inayozungumziwa hapo.
Kwahiyo kama siku hiyo ikikukuta halafu ulikuwa hujajiweka tayari, ni ngumu sana kumshinda shetani, ni rahisi kupoa au kuurudia ulimwengu kabisa, katika eneo lolote ulilopo hata katika utumishi wako, anaweza kukuletea vitisho visivyo vya kawaida, anaweza kukuletea majaribu, anaweza kukuletea magonjwa, anaweza kukuletea mashahidi wa uongo, anaweza kukubambikizia hata kesi, anaweza kukujia kwa njia yoyote ile, lengo ni kukuangusha, yalimkuta Yusufu, yalimkuta Danieli, yalimkuta Ayubu, yakamkuta Bwana wetu Yesu Kristo, yakawakuta mitume, mimi na wewe ni nani yasitukute?. Hivyo usipojua namna ya kukabiliana na mitego hiyo inapokuja kwa ghafla, utaanguka mara moja.
Na ndio maana mtume Paulo anatoa suluhisho baada ya mstari huo, anasema;
Waefeso 6:13 “Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama 14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, 15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; 16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. 17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; 18 kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote”
Waefeso 6:13 “Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama
14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,
15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;
16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.
17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;
18 kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote”
Umeona, vigezo vimeshatolewa hapo juu, ili kumshinda shetani wakati wote, kusema tu umeokoka haitoshi, na huku hujijengei desturi ya kuwa mwombaji wa mara kwa mara, husomi Neno, huifanyi kazi ya Bwana kwa jinsi Mungu alivyokupa karama, Ukiwa ni mkristo wa dizani hiyo ni ngumu kustahimili vishindo vya adui siku ya uovu ikifika, maana ni lazima ije.
Ni sawa na mtu anayejisifia nyumba yake kubwa ya kisasa yenye mali nyingi za thamani, lakini ndani amekosa vifaa vya uokozi kama vile zima moto, au waya wa Earth. Anaweza kuifurahia kweli nyumba yake nzuri kaijenga na kuipamba kwa muda mrefu, lakini siku janga kama la moto litakapotokea kwa ghafla na kuteketeza mali zake zote, pamoja na nyumba yake yote, au umeme unapozidi ndani ya nyumba au radi itakapopiga nyumba, ndipo atakapojua kuwa alikosa vifaa muhimu sana ndani ya nyumba yake.
Vivyo hivyo, tukitaka na sisi tuwe wakristo tuliokamilika, ni lazima tuzingatie vigezo tajwa vyote hapo juu. Tuyafanye maombi kuwa sehemu ya maisha yetu kama tahadhari, Neno la Kristo likae kwa wingi ndani yetu kutuongezea imani, na tutumie karama zetu kuwapelekea na wengine habari njema.
Bwana atutie nguvu.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
MWANANCHI WA UFALME WA MBINGUNI
MAPAMBANO DHIDI YA SHETANI.
WALIO NA HEKIMA NDIO WATAKAOELEWA.
KUOTA UPO KANISANI.
FAIDA ZA MAOMBI.
Rudi Nyumbani:
Print this post