UPO UMUHIMU MKUBWA WA KUMTOLEA BWANA!

UPO UMUHIMU MKUBWA WA KUMTOLEA BWANA!

Jina la Mwokozi wetu, Yesu libarikiwe..
Karibu tujifunze biblia, leo tutajifunza jambo dogo, linalohusiana na faida za kumtolea Bwana.

Moja ya mambo ambayo shetani kayakoroga sana katika Ukristo na nje ya ukristo, ni suala la utoaji.

Shetani hataki watu wanaomjua Mungu wawe watoaji na hata wale wasiomjua Mungu wawe watoaji.

Kwasababu anajua hata mtu asiyemjua Kristo akiwa mtoaji, basi atapata thawabu kwa hicho…kwahiyo atajitahidi kumpandikizia mtu roho ya kutokutoa kwa gharama zozote, hata akisikia jambo lolote linalohusiana na kutoa asisikilize, na hata achukie kabisa.

Lakini nataka nikuambie.. Chochote unachokitoa aidha kwa Bwana au kwa mtu , kina thamani kubwa sana kwake yule unayekipokea…Kama ni Kristo au kama ni mwanadamu mwenzako.

Sijui kama umewahi kupitia mazingira fulani ambayo upo katika hali ya kuhitaji sana, halafu anatokea mtu anakusaidia, au anakukopesha…kuna furaha fulani unaipata isiyokuwa ya kawaida.

Sasa wengi wetu tunafikiri ni sisi tu waanadamu ndio tunapitia hayo mazingira ya kupungukiwa na kuhitaji msaada..Lakini leo nataka nikuambie ya kwamba futa hayo mawazo… Hata Kristo naye ambaye ni Mungu, anapitia hayo mazingira kila siku, na anatafuta watu wa kumsaidia, Ingawa yeye ana kila kitu..

Kikawaida ukiwa na mtoto au watoto wanaokupenda na wewe unawapenda, halafu uwaone wanapitia shida..ni wazi kuwa wewe ndio utateseka zaidi na kupitia shida zaidi..kwasababu kwanza ni damu yako, na vile vile wapo moyoni mwako..

Na Kristo naye ni hivyo hivyo, wale wote ambao wapo katika agano la damu yake, na wapo moyoni mwake, na yeye yupo mioyoni mwao..wanapopitia matatizo ni yeye ndiye anayekuwa katika shida..zaidi hata ya yule anayepitia shida.

Kwahiyo hata Kristo naye anapitia shida hata sasa, ndivyo maandiko yanavyosema..

Mathayo 25:41 “Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake;

42 kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe;

43 nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama.

44 Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie?

45 Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi.

46 Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa mmilele”.

Umeona?

Na “Wadogo” wanaozungumziwa hapo sio wale watu wanaosimama njiani na kuomba, ambao wengi wao ni watu wakidunia na walevi, watukanaji, na hata wengine wanamtukana Kristo hadharani..

Bali “wadogo”, Kristo anawaozungumzia hapo ni wale ambao “Ndani yao yupo Kristo wa kweli”… Lakini wapo katika mahitaji pengine kutokana na kuishikilia imani yao, wapo vifungoni pengine kutokana na kuhubiri injili, hawana chakula, mavazi n.k kutokana na mambo ya kiimani wanayoyafanya. Hao ndio ambao ukiwasaidia unakuwa umemsaidia Kristo mwenyewe…Kwasababu Kristo yupo ndani yao.

Sasa kuna aina ya mahubiri, yameenea sana leo, kwamba watu wote waliompokea Kristo, hawapitii kabisa kipindi cha kuwa na mahitaji.. Nataka nikuambie hiyo injili si ya ukweli..watu waliookoka watapitia vipindi vyote, vya kupungukiwa na vya kuongezekewa, watapitia vipindi vya magonjwa, watapitia vipindi vya vifungo, na dhiki kwasababu bado wapo ulimwenguni..Lakini hiyo haimaanishi kuwa hawatapitia pia vipindi vya raha, watavipitia lakini pia vya dhiki watakutana navyo.

Sasa katika wakati kama huo, ambao unaona watu wa Mungu wapo katika hali ya kuhitaji, huo ndio wakati wa kujizombea baraka..kwasababu ukiwasaidia hao, umemsaidia Kristo mwenyewe..Mungu anaruhusu watu wake wawe hivyo, sio kwamba hawezi kuwatajirisha ghafla la!..bali anawafanya hivyo, ili watu wengine wapate nafasi ya kubarikiwa kwa kuwasaidia.

Kwahiyo ndugu usikwepe hata kidogo kumtolea Bwana kwasababu kuna thawabu kubwa, Bwana Yesu mwenyewe alisema maneno haya…

Marko 9:41 “Kwa kuwa ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake”.

Na hilo sio jukumu la kundi fulani tu la watu, kwamba ni watu fulani wenye uwezo ndio wanapaswa wamtolee Bwana..Au kwamba ni washirika na waumini tu, hapana!..bali ni la watu wote, walio wahudumu na wasio wahudumu…Watumishi na wasio watumishi. Wote hatuna budi kumtolea Bwana kwa namna hiyo, kama tunataka kubarikiwa.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

DALILI ZIPI ZITAMTAMBULISHA MTU KUWA AMEFANYIKA KIUMBE KIPYA?

Zile Rangi saba za Upinde wa Mvua zinawakilisha nini?

Roho, Nafsi, na Mwili vina utofauti gani?

Katika (Mathayo 25:8 na Marko 16:8) Wale wanawake walitangaza kufufuka kwa Bwana au walikaa kimya?

MKARIBIE BWANA ZAIDI ILI UFANYIKE NGUZO.

HEKIMA YA KIMUNGU, INAINGIAJE MIOYONI MWETU?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments