Kwanini kabla ya Kristo, miaka ilikuwa inahesabiwa kwa kurudi nyuma?

Kwanini kabla ya Kristo, miaka ilikuwa inahesabiwa kwa kurudi nyuma?

Nyakati zote kabla na hata baada ya Kristo miaka inahesabiwa kwa kwenda mbele, hakuna wakati wowote au kipindi chochote miaka ilihesabiwa kwa kurudi nyuma.

Litakuwa ni jambo lisilo la kiakili kama miaka itahesabiwa kwa kurudi nyuma..yaani kwa mfano leo ni mwaka 2021 halafu mwakani iwe mwaka 2020 badala ya 2022.

Sasa kama ni hivyo tunaweza kujiuliza ni kwanini, miaka ya nyuma inaonekana kama inahesabika kwa kurudi nyuma?.

Ili tuelewe vizuri hilo hebu tujifunze katika huu mfano mdogo.

Tuseme mwaka 2019 kulitokea janga kubwa la dunia la Korona lililobadilisha mfumo mzima wa maisha ya walimwengu.

Na kisha mtu mmoja akataka kurejea  tukio fulani lililotokea mwaka2015 ambapo kulitokea janga la kimbunga,na akasema.. “miaka 4 kabla ya Korona kuzuka duniani, kulitokea kimbunga kikubwa kikaharibu miundo mbinu”.

Na mwingine labda akataka kurejea tukio lililotokea mwaka 1978, wakati Tanganyika inapigana na Idd Amini wa Uganda, badala ya kusema mwaka 1978 kulitokea vita, akasema miaka 41, kabla ya janga la korona (41Kk) kulitokea vita kati ya Tanganyika na Uganda, vilivyogharimu uhai wa watu wengi.

Vile vile mtu mwingine labda akataka kurejea vita vya pili vya dunia vilivyotokea mwaka 1945, hivyo badala ya kutaja huo mwaka 1945 akasema, miaka 74 kabla ya Korona,(74kk) ilitokea vita kubwa sana ya dunia iliyogharimu maisha ya watu wengi..

Tuseme na mwingine akataka kurejeatukio la ajali lililotokea mwaka 2021, hivyo badala ya kusema mwaka 2021 kulitokea ajali mbaya sana, akasema miaka miwili baada ya Korona kuzuka duniani(2Bk), kulitokea ajali mbaya sana. N.k hiyo ni mifano tu.

Sasa kwa kusema hivyo haimaanishi, kwamba kuanzia mwaka huo wa 2019 janga la Korona lilipotokea kushuka chini, miaka ilikuwa inahesabiwa kwa kurudi nyuma.

La! Miaka ilikuwa inahesabiwa kwa kupanda, lakini kwasababu kulitokea tukio kubwa na maarufu mwaka 2019 ikabidi kalenda ibadilike, matukio yote ya nyuma yatajwe kwa kurejea tukio fulani kubwa lililowahi kutokea.

Kadhalika Kuzaliwa kwa MKUU WA UZIMA, NA MWANZILISHI WA MAMBO YOTE, YESU KRISTO. Ni lazima dunia itetemeke, tarehe haziwezi kubaki vile vile, majira hayawezi kubaki vile vile, kadhalika na kuzimu haiwezi kubaki vile vile. Ni lazima mabadiliko makubwa yaambatane na kuzaliwa kwake, kwasababu kitu alichokileta ulimwenguni ni kikubwa, Damu yake iliyomwagika pale Kalvari, imeleta mageuzi makubwa katika ulimwengu wa mwili na roho.

Maandiko yanasema..Kristo alikuja kuutangaza MWAKA WA BWANA uliokubaliwa (Isaya 61:1-2). Hivyo haiwezekani “aje autangaze mwaka wa Bwana” halafu tarehe zibaki vile vile. Ni lazima tu matukio yote ya kabla au baada yarejee kuzaliwa kwake.

Isaya 61:1 “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu BWANA amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema….

2 Kutangaza mwaka wa BWANA uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao”.

Bwana Yesu amekuwa Jiwe kuu la pembeni, Jiwe la kurejea..Korona imetikisa dunia lakini bado haijaweza kubadilisha majira, wapo wanadamu waliokuwa maarufu lakini hawajabadili majira, wamekuja na kupita, ni mkuu wa Uzima (Yesu), pekee yake ndiye ambaye mpaka leo, alama yake ipo katika kila mwanzo wa barua, mwanzo wa siku, na miezi na Miaka. Kuonesha kwamba yupo hai mpaka sasa hivi, na hakuna aliyemzidi,  leo hii hakuna mahali utakwenda usilisikie jina la Yesu likitajwa.

Na kama jinsi yeye alivyokuwa nguzo ya kurejewa, atabaki kuwa hivyo hivyo milele.

Je! Umemwamini leo?.. Umetubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha?, umebatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu upate ondoleo la dhambi zako?. Kama bado ni vyema ukafanya hivyo leo, maadamu mlango wa neema upo wazi, siku utakapofungwa kutakuwa hakuna nafasi tena ya kutubu.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

TABIA YA WAZI INAYOWATOFAUTISHA MANABII WA UONGO NA WALE WA UKWELI.

BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?

Jiepushe na tamaa ya Mali/kupenda fedha.

USITAZAME NYUMA!

SI MAPEPO YOTE NI YA KULIPUKA.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments