USIPUNGUZE KUTUMBUIZA!

USIPUNGUZE KUTUMBUIZA!

Unaweza kujiuliza je! Sisi tumeitiwa kutumbiza?.. Jibu ni Ndio! sisi tumeitiwa kutumbuiza lakini si kwenye majukwaa ya dansi au anasa. Bali mbele za Malaika na wanadamu kupitia Maisha yetu ya usafi na utakatifu!.

1Wakorintho 4:9 “Maana nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume mwisho, kama watu waliohukumiwa wauawe; kwa sababu TUMEKUWA TAMASHA KWA DUNIA; kwa malaika na wanadamu”.

Maana yake Maisha yetu ni kama tamthilia inayotazamwa!, ambayo baada ya kuisha itatolewa hukumu kama ni nzuri au mbaya!.

Kutumbuiza ni kitendo cha kuonesha ujuzi wako na kipaji chako mbele ya watu wanaokuzunguka kwa lengo la kupata fedha!,

Wanaoimba na kucheza dansi kwenye majukwaa wanatumbuiza!, wanaoruka sarakasi kwenye majukwaa  huku wanaimba wanakuwa wanatumbuiza, wanaocheza na nyoka mbele za umati wanakuwa wanatumbuiza! N.k

Leo napenda tuangalie kibiblia hii namna ya kutumbuiza kwa kutumia nyoka.

Kipindi cha Nyuma kidogo!, na hata sasa katika nchi baadhi, kuna mchezo wa kutafuta nyoka wenye sumu kali (kama Kobra), na kisha kujifunza kuwapumbaza kwa nyimbo na sauti za filimbi, na kwenda nao kufanya maonyesho kwenye matamasha kwa lengo la kupata fedha!, Watu walipowaona watu hao wanauwezo wa kusimama mbele ya Nyoka  wenye sumu bila kudhuriwa, waliburudika na kuwapa fedha nyingi kuliko hata wale waliokuwa wanaruka sarakasi au kuimba tu peke yake!, kwasababu ni jambo ambalo lilikuwa si la kawaida!.

Lakini pamja na hayo ulikuwa ni mchezo wa hatari sana, kwani endapo ikitokea ajali yule Nyoka akamwuma yule Mtumbuizaji, basi mchezo ndio umeishia pale pale na hakuna fedha yoyote atakayopata huyo mtumbuizaji!, Hivyo ilihitaji umakini mkubwa..

Sulemani kwa hekima alisema..

Mhubiri 10:11 “NYOKA AKIUMA ASIJATUMBUIZWA, BASI HAKUNA FAIDA YA MTUMBUIZI”.

Hii ni hekima ya kidunia tu ambayo Sulemani aliitoa kwa kutazama Maisha ya watumbuizaji!. Lakini hakuisema tu hiyo hekima kutufurahisha!, la!, bali hekima hiyo ina funzo kubwa sana kwetu wakristo ndio maana ipo kwenye biblia!, ingekuwa haina funzo lolote isingewekwa kwenye biblia.

Na sisi wakristo ni watumbuizaji!, Na Nyoka ni adui yetu shetani!..ambaye anasimama kutupinga siku zote!, akitafuta kutudhuru siku zote katika Maisha yetu ya hapa duniani, Na mbingu inatutazama tutaumalizaje mchezo wetu!, jinsi gani tutampumbaza shetani mpaka mwisho, ili tupokee Tuzo bora!.

Endapo tukisimama mpaka mwisho wa muda wetu bila kuangushwa na shetani aliyeko mbele yetu basi tutapokea tuzo kubwa sana mbinguni, lakini tukiumwa na shetani kama maandiko yasemavyo hapo juu.. “Nyoka akiuma asijatumbuizwa, Basi hakuna faida ya mtumbuizi”.

Hatuna faida yeyote tutakayoipata endapo tukiruhusu shetani atuangushe.

Sasa tunampumbazaje shetani?

Zamani hawa watu waliokuwa wanawapumbaza nyoka!, walitumia sauti za filimbi, walikuwa wanazipuliza filimbi zile kwa ustadi, na walikuwa hawapotezi umakini katika hilo, walijua kwa kupoteza umakini kidogo tu!, wale nyoka akili zao zinawarudia na kuwadhuru!..Sasa zile filimbi hazikuwa zinawaburudisha wale nyoka hata washindwe kuwauma..la!, bali zilikuwa zinawachanganya!..zinawafanya wale nyoka, wakose sababu ya kuwauma!..kwani nyoka ili amuume mtu, ni lazima apate shabaha ya utulivu katika akili yake, sasa zile sauti za filimbi zilikuwa zinawakosesha shabaha, hivyo wanakuwa wanababaika na kusubiri wakati zitakapotulia..

Sasa wakati zile sauti zinawapumbaza wale nyoka, wakati huo huo zinawafurahisha watazamaji..

Na sisi wakristo ili shetani ashindwe juu ya Maisha yetu!, hatuna budi muda wote tupulize filimbi zetu za kiroho, huku tukimkabili adui yetu shetani. Na wakati filimbi hizo zinampumbaza shetani na majeshi yake, wakati huo huo zitakuwa zinaifurahisha mbingu.

Sasa Filimbi hizo za kiroho ni zipi?

Zifuatazo ni filimbi za kiroho.

1/Utakatifu

3/Maombi

4/Kusoma Neno

2/Ushuhudiaji

Tukizipuliza filimbi hizi Nne!, basi shetani atakuwa hana nguvu zozote kwetu, atakuwa kama ZUZU!, mpaka tunamaliza safari yetu hapa duniani!.

Na faida kubwa ya kumfanya shetani zuzu hapa duniani ni Thawabu kubwa kule mbinguni, na heshima kubwa!..kwasababu yeye aliyekuwa anajiona ni kitu!, amekuwa takataka mbele yetu!.

Bwana atusaidie tusiyapunguze mambo hayo..Maana tukipunguza utakatifu, Maombi, Kusoma Neno, na Ushuhudiaji basi tunamrejeshea shetani shabaha yake!, na akituangusha basi anguko letu linakuwa kubwa na hatutakuwa na thawabu yoyote baada ya Maisha haya.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote.

NJIA YA KUPATA WOKOVU.

Wale Nyoka wa Moto jangwani, walikuwa ni wa namna gani?

TUMEPEWA AMRI YA KUKANYAGA NGE NA NYOKA.

KUOTA NYOKA.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments